Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Bungoma Diocese Mock Exams 2021/2022

Share via Whatsapp

 Instructions to candidates

  • Jibu maswali yote
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa Lugha ya Kiswahiliekee
  1. Ufahamu (Alama 15)
    Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuata


    Wahenga walisema kutoa ni moyo usambe ni utajiri. Iwapo wangefufuka leo hii wangeongezea kuwa ujasiri ni moyo usiseme ni umri. Kauli hii kama ile ya kwanza imesheheni ujumbe muhimu. Katika jamii nyingi, mtoto haruhusiwi kukaa au kuzungumza mbele ya watu wazima. Akiwa wa kike ndiyo basi. Ni ajabu basi kwa mtoto wa kike kutoka jamii yenye imani kali za jadi zinazomdunisha mwanamke kuweza kupata tuzo yenye staha ya juu zaidi.

    Malala Yousafzai alishinda Tuzo ya Nobel mwaka 2014 akiwa na umri wa miaka 17. Aliyeshinda naye tuzo hii adhimu ni Kailash Satyarthi. Kigoli huyu alituzwa tunu hii kwa kupigania haki za wasichana kupata Elimu nchini Pakistan. Harakati hizi hakuzianza juzi. Mwaka 2012 alipigwa risasi na mijibaba ya ugaidi ya kundi Fulani linaloegemea mrengo wa siasa kali kwa ‘hatia’ za kuwatetea mabanati. Inasemekana alishambuliwa alipokuwa akisafiri kwenye basi la shule. Kilichochochea mashambulizi ni tuhuma kuwa alikuwa ameanzisha jukwaa kwenye mtandao wa Shirika la Utangazaji la BBC alilokuwa akichangia maandishi alipokuwa na umri wa miaka 11. Maandishi yake yalikuwa na ujumbe wa kupinga juhudi za makundi Fulani kuwanyima wanawake Elimu.

    Haikuwezekana hata baada ya kupona kurudi Pakistani. Alihamia Uingereza alipofadhiliwa na wahisani. Licha ya kuwa aliishi ugenini na bila aila yake mwana huyu hakupoteza makali ya ari yake ya kuendelea kutetea maslahi ya kielimu ya wenzake wa kike.

    Yeye ndiye mwenye umri wa chini zaidi katika historia kupata tuzo hili. Baadhi ya wale walioshinda Nobel katika umri mkubwa ni Desmond Tutu, Nelson Mandela na Wangari Maathai. Kila mmoja wao alitambuliwa kwa sababu mahususi zinazohusu jitihada za kuboresha maisha ya wanajamii.

    Njia nyingine kuu aliyoitumai Malala ni hotuba. Mwaka 2013 alihutubia Kongamano la Vijana la Umoja wa Mataifa katika hafla iliyoandaliwa kwa heshima yake. Aliwashangaza wengi kwa ufasaha na uweza wake wa kutongoa hoja. Kila mtu aliguswa na dhati ya kauli zake. Katibu Mkuu hakuwa na jingine ila kulipa kongamano hilo jina Malala. Mtoto huyu wa kimaskini alipewa taathima ambayo watu wachache sana wamepata kutunukiwa. Hii ni heshima inayotengewa marais na wafalme. Na wanapoipata huruhusiwa kuhutubia kwa dakika tano tu.

    Mwaka 2014, viongozi wenye sifa za ubabe wa kuwabinya wapinzani wao lakini wameshindwa kuwaokoa wanyonge walipokuwa wakilaza damu, yeye alisafiri hadi Naijeria kudai kuachiliwa kwa wasichana 200 waliotekwa nyara na kundi haramu.

    Katika hotuba iliyojaa hisia ambazo huhusishwa tu na akina mama wenye uzazi mkubwa aliyoitoa Naijeria , aliwaasa watoto wenzake wasimruhusu mtu yeyote awaambie kuwa wao ni wanyonge au hawana uwezo. Aliwanasihi kuwa wao sio wadhaifu kuliko wavulana na wasijione wanyonge kuliko watoto wa kitajiri wala wale wanaotoka nchi zenye uwezo mkubwa . Alihitimiza kuwa wao ndio watakaoijenga jamii na kuwa wana uwezo wa kuyaendesha mambo.

    Mshindi wa tuzo hii yenye thamani ya dola za kimarekani milioni moja ameitabaruku kwa watoto wenzake ulimwenguni. Bila shaka mwanzilishi wa tuzo ya Nobel ameguswa na tendo la mtoto huyu huko kuzimuni. Kama kumbukizi tunu hii hutolewa wakati wa kuadhimisha kifo cha Mwanaviwanda wa Kiswidi aliyeasisi tuzo hii kufuatana na wosia wake mwaka 1895. Kama Alfred Noble mwenyewe, kwake Malala, ngwenje au darahimu si muhimu . Lililo muhimu ni ukombozi wa watoto na hasa wa kike kielimu. Malala bado anavaa mtandio wake huku akidhihirisha adabu na unyenyekevu wa kupigiwa mfano.
    Maswali
    1. Eleza mtazamo wa jamii ya Malala kuhusu watoto wa kike. (alam.2)
    2. Unafikiri Malala alistahili kutuzwa Tuzo ya Nobel? Toa sababu tatu. (alama.3)
    3. Ni njia zipi alizozitumia Malala kutetea haki ya watoto wa kike kupata Elimu? (alama 3)
    4. Malala anawapa ushauri upi watoto wenzake? (alama. 1)
    5. Kwa nini inasemekana kuwa Tuzo ya Nobel ina staha ya juu zaidi? (alama.2)
    6. Andika kichwa kifaacho kwa kifungu hiki. (alama.2)
    7. Eleza maana za maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika taarifa: (alama. 3)
      1. Tunu
      2. Wahisani
      3. Ubabe
  2. UFUPISHO
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

    Ukame ni tukio hatari la kimaumbile. Athari zake hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine. Kwa sababu hiyo, si rahisi kuielewa dhana ya ukame; kwa hakika si rasihi kuifafanua dhana hii. Katika eneo la Bali, kwa mfano, isiponyesha kwa muda wa siku sita wenyeji huchukulia hali hiyo kuwa ukame japo kiasi hicho cha mvua ni kikubwa mno ikilinganishwa na Libya ambayo hupata kiasi kidogo cha chini ya milimita 180 ya mvua kwa mwaka.

    Katika hali ya kawaida ukame hutokana na kipindi kirefu cha uhaba wa mvua hasa katika mzima au zaidi. Uhaba huu wa mvua huweza kusababisha uhaba wa maji kwa shughuli, kundi au sekta Fulani. Shughuli za binadamu huweza kufanya hali ya ukame mbaya zaidi.Shughuli hizo ni pamoja na kilimo, unyunyiziaji maji na ukataji wa miti.

    Ni vigumu kubaini wakati mahususi ambao ukame huanza kwa kipindi hicho cha ukosefu wa mvua huwa cha mfululizo, na eneo huendelea kupata mvua iliyopungua kwa miezi au hata miaka. Mimea hukauka na wanyama hufa kutokana na ukosefu wa maji. Ukame basi huwa hatari kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine kwa kuwa huweza kusababisha njaa na kuyafanya maeneo kuwa majangwa.

    Mbali na ukosefu wa mvua, ukame pia husababishwa na kiangazi. Kiangazi huongeza kiwango cha joto. Joto hilo hufanya maji yaliyohifadhiwa kuwa mvuke haraka, hivyo kiwango chake kupungua. Hali ya el ninyo pia husababisha ukame katika baadhi ya maeneo ambayo huwa hayana mvua. Upepo huivutia mvua mahali panaponyesha na kuliacha kame eneo ambalo halina mvua ya aina hii. Hata katika maeneo yenye mvua ya el ninyo , kiangazi kikali huifuata na hivyo kusababisha ukame. Hali hii huitwa la nina. Mambo yanayotokana na mabadiliko ya hali ya anga ulimwenguni pia yanaweza kuchangia ya ukame. Ongezeko la joto duniani linafanya hali ya ukame kuwa mbaya zaidi.

    Ukame una mdhara chungu nzima kwa binadamu. Madhara hayo huweza kuwa ya kiuchumi, kimazingira, kimazingira au hata kijamii. Ukame husababisha kupungua kwa mimea na mavuno. Huweza pia kutokea dhoruba za mchanga. Dhoruba hizi hutokea palipo na jangwa. Ukosefu wa maji ya kunyunyizia mimea husababisha njaa na magonjwa kama vile utapiamlo yanayotokana na ukosefu wa lishe bora. Makazi ya wanyama wanchi kavu na wale wa majini pia huathiriwa vibaya. Hali kadhalika, ukame husababisha uhamaji. Hii inamaanisha kuwa jamii huweza kutoka katika makazi asilia na wakati mwingine huweza hata kuwa wakimbizi.

    Ukame husababisha ukosefu mkubwa wa maji. Ukosefu huu huwa na athari hasi kwa maendeleo ya viwanda kwa kuwa vingi huhitaji kiasi kikubwa cha maji. Juu ya hayo, maji huhitajika katika kuzalisha umeme. Umeme una matumizi mengi katika viwanda, nyumbani, afisini na hata hospitalini. Ukosefu wa umeme basi huwa ni tatizo kuu.

    Aidha, ukame husababisha madhara mengi, binadamu wanaweza kujikinga kutokana na uhaba wa rasilimali za asili kama vile chakula na maji. Pia mioto mikubwa huweza kuenea haraka wakati wa ukame na hivyo kusababisha vifo vya binadamu na wanyama na uharibifu wa rasilimali nyingine.

    Ingawa ukame husababisha madhara mengi, binadamu wanaweza kujikinga kutokana nao kwa kupunguza makali ya ukame. Jambo la kwanza wanaloweza kufanya binadamu ni kuhifadhi maji. Maji ya mvua yanafaa kuhifadhiwa katika mabwawa na mapipa. Haya yanaweza kutumiwa wakati wa ukame hasa katika kukuza mimea. Mkakati mwingine ni kutumia mbinu za kupunguza chumvi na kemikali nyingine zilizomo kwenye maji ya bahari ili yaweze kutumika katika unyunyiziaji wa mimea. Hili litapunguza tatizo la ukosefu wa chakula. Pia ni muhimu kufanya utafiti kuhusu hali ya anga ili kupanga na kuweka mikakati ifaayo kukabiliana na hali hiyo.

    Ni muhimu kuwa na mipangilio mizuri ya matumizi ya ardhi. Mathalani upanzi wa mimea itakayozuia mmomonyoko wa udogo, kubadili aina ya mimea inayokuzwa sehemu fulani pamoja na upanzi wa mimea isiohitaji mvua nyingi katika kame ni hatua mwafaka. Aidha, ni vizuri kupunguza matumizi ya maji hasa katika mazingira ya nyumbani kwa mfano tunapofua na kuosha. Njia nyingine ya kukabiliana na tatizo hili ni kusafisha maji yaliyotumiwa ili kuyatumia tena.
    1. Kwa maneno 50, eleza visababishi vya ukame kwa mujibu wa taarifa  (alama. 4; 1 ya mtiririko)
    2. Fupisha ujumbe wa aya ya tano hadi saba kwa maneno 70. (alama. 6; 1 mtiririko )
    3. Eleza masuala ambayo mwandishi ameibua katika aya mbili za mwisho kwa maneno 60. (alama 5; 1 ya mtiririko)
  3. SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA ALAMA 40
    1. Andika maneno yenye miundo ifuatayo . (alama.2
      1. Kipasuo ghuna cha midomoni, irabu ya chini, kati, kipasuo sighuna cha ufizi, irabu ya juu mbele.
      2. Nazali ya ufizi, kipasuo ghuna cha kaakaa laini, irabu ya juu, nyuma, irabu ya nyuma wastani.
    2. Bainisha silabi zinazowekwa shadda katika maneno yafuatayo (Alama. 1)
      1. Waliotusifia
      2. Sherehekea
    3. Andika sentensi ifuata katika wingi. (Alama.2)
      Wayo wa mguu wangu wa kulia umeungua
    4. Geuza sentensi ifuatayo katika hali ya udogo. (alama. 1)
      Njia hii yetu inapitiwa na mtu mnene
    5. Tunga sentensi moja yenye kivumishi cha pekee kinachoonyesha idadi jumla. (alama.1
    6. Andika upya sentensi zifuatazo kulingana na maagizMaafisa hao walipewa uhamisho. 
      1. Maafisa wengine hawakupewa uhamisho
        (unganisha kuunda sentensi ambatano) (alama.2)
      2. Hadithi hiyo ilitungwa vizuri ikawavutia wengi
        ( badilisha vitenzi vilivyopigiwa mstari kuwa nomino) (alama.2)
      3. Tunda halitaoshwa vyema. Tunda halitalika .
        (unganisha kuwa sentensi moja kwa kutumia ‘po’) (alama.2)
      4. Kengewa alitoa ahadi .Wengi waliiamini ahadi hiyo. (unganisha kuwa sentensi moja inayoanza kwa . Ahadi….) (alama .2)
    7. Tunga sentensi ya masharti inayoonyesha kwamba kitendo kilifanikiwa kutokana na kufanikiwa kwa kingine. (alama. 2)
    8. Tunga sentensi yenye kishazi kirejeshi ambacho ni kielezi. (alama.2)
    9. Ainisha maneno ya liyopigwa mstari katika sentensi ifuatayo. (alama. 3)
      Mwenyewe hakuwa amekupa ruhusa kuitumia
    10. Akifisha sentensi ifuatayo.
      Kiwango cha umasikini katika kaunti ya homabay kinasikitisha sana itabidi sote wakatizi wa hapa tujizatiti ili tutimize malengo ya millennia seneta mteule alituhimiza
    11. Andika maneno yenye mofimu zifuatazo. (alama. 2)
      1. Umoja (ngeli ya u-i), mzizi, kiisho
      2. Kikanushi, kiambishi ngeli (ki-vi, Umoja)
        Mzizi, kauli tendeka, kiisho
    12. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao. (alama. 2)
      KN (N+RH) + KT (T+RE)
    13. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya kukanusha . (alama. 2)
      Ngoma hizo zilihifadhiwa ili ziuzwe mjini.
    14. Andika sentensi ifuatao katika wakati uliopita hali ya mazoea. (alama.2)
      Ekapolon atawashauri wanafunzi kuhusu umuhimu wa kufanya bidii
    15. Andika sentensi ifuatayo katika kauli ya kutendesha kwa kuzingatia maneno yaliyopigiwa mstari   (Alama. 2)
      Alimfanya mtoto anywe uji ukamfanya ashibe.
    16. Tunga sentensi ukitumia mzizi, ingineo kumaanisha “mbali na”. (Alama. 1)
    17. Hewala ni kwa kukubaliana na jambo, ……………………… .ni kwa kutoka kitu kinusurike, na…………….ni kwa aliyefanya vyema katika jambo. (alama.1)
    18. Zito ni kwa jepesi, ……………………..ni kwa choyo na, ……………………ni kwa kali. (alama.2)
    19. Andika visawe vya kauli zilizopigiwa mstari.
      Atyang alikumbwa na matatizo mengi lakini hakukata tama.
  4. ISIMU JAMII. (Alama.10)
    Eleza sababu tano zinazowafunga watu kufanya makosa ya kisarufi katika mazungumzo.


MARKING SCHEME

  1. UFAHAMU
    1. Watoto wakike hawastahili kwenda shuleni. Bali wapate mafunzo ya kupika kulea watoto na kutunza waume zao nyumbani (2)
    2. Ndiyo (3)
      • Kupigania suala lililokuwa mwiko katika jamii yake.
      • Kuhatarisha maisha yake
      • Ujasiri wa kubeba jukumu la watu wazima
      • Uweza wa kiakili na kinafsia.
    3.  
      • kuchangia maandishi ya hoja kwenye blogi (3)
      • Kutoa hotuba
      • Kuwa kielelezo bora kwa kwenda shuleni
    4. wasijione wanyonge au kujidharau maana wao ndio wanaotumainiwa kujenga jamii ya baadae (1)
    5. Hutolewa kwa watu wachache wenye mchango mkubwa uliothiri jamii pana kwa njia change na wanateuliwa baada ya mchujo mkali . (2)
    6. Mtoto Bomba (1)
      Elimu kwa mtoto msichana
    7.  
      1. Tuzo (3)
      2. Wasamaria wema
      3. Mabavu/ nguvu
  2. Ufupisho  
    1.  (3 zozote, 1 mtiririko) 
      • Uhaba wa mvua
      • Shughuli za binadamu kama vile kilimo, onyunyiziaji maji na ukataji miti.
      • Kiangazi
      • Hali ya el ninyo
      • Mabadiliko ya hali ya anga
    2. (5 zozote, 1 mtiririko)
      • Madhara ya ukame ni nyngi, kwa mfano.
      • Madhara ya kiuchumi , kimazingira na hata jamii.
      • Kupungua kwa mimea na mavuno .
      • Dhoruba ya mchanga
      • Njaa na magonjwa
      • Kuathiriwa vibaya kwa makaazi ya wanyama wa nchi kavu na majini.
      • Uhamaji
      • Ukosefu wa maji
      • Ukosefu wa maji
      • Ukosefu wa umeme
      • Uhasama kwa jamii
      • Mioto
    3. Ili kupunguza makali ya ukame, binadamu anafaa (4 zozote 1, mtiririko)
      1. Kuhifadhi maji
      2. Kutumia mbinu za kupunguza chumvi na kemikali zingine zilizomo kwenye maji bahari
      3. Kufanya utafiti kuhusu hali ya anga ili kupanga mikakati iffayo kukabiliana na hali hiyo.
      4. Kuwa na mpangilio mzuri wa matumizi ya ardhi.
      5. Upanzi wa mimea inayozuia mmomonyoko wa udongo.
      6. Kubadili aina ya mimea inayokuzwa sehemu Fulani.
      7. Upanzi wa mimea isiohitaji mvua Nyingi katika maneo kame.
      8. Kupunguza matumizi ya maji hasa nyumbani
      9. Kusafisha maji yaliyotumiwa
  3. Lugha
    1.  
      1. Bati (2x1)
      2. Nguo
    2.  
      1. Waliotusisia ( 1x½ )
      2. sherehekea
    3. Nyayo za miguu yetu ya kulia zimeungua 2/0
    4. Kijia hiki chetu kinapitiwa na jitu nene 1/0
    5. Chakula chote kimeliwa 1/0
    6.  
      1. Maafisa hao walipewa uhamisha lakini wengine hawakupewa 2/0
      2. Ilitungwa – tungo 2x1
        Ikawavutia - mvuto
      3. Tunda lisipooshwa vyema halitalika 2/0
      4. Ahadi iliyotolewa na kengewa iliaminiwa na wengi 2/0
    7. Hali ya ‘nge’ na ‘ngeli’ 2/0
      Ningeimba vizuri, ningepata tuzo hilo
      Ningelisoma kwa bidii, ningelipita mtihani.
    8. Mgeni aliwasili tulipokuwa tunafagia njia/ tukifagia njia 2/0
    9. Mwenyewe – kiwakilishi 3x1
      Hakuwa - kitenzi
      Amekupa - kitenzi kikuu
    10. “Kiwango cha umasikini katika Kaunti ya Homabay kinasikitisha sana; itabidi sote wakazi wa hapa tujizatiti ili tutimize malengo yetu ya Milenia,” Seneta mteule alituhimiza. 6x ½
    11.  
      1. Ukate/ulete/ ubebe/ mkononi/ mguuni/mtini mchezo 2x1
      2. halikiki , hakiandikiki
    12. Vitabu vilivyo kabatini kimeandikwa vizuri 4x ½
          N               RH               T               RE
    13. Ngoma hizo hazikuhifadhiwa ili zisiuzwe mjini. 2/0
    14. Ekapolon alikuwa anawashauri/ akiwashauri vijana kuhusu umuhimu wa michezo 2/0
    15. Alimnywesha mtoto uji ili umshibishe 2/0
    16. Nilitee kiti kinginecho 1/0
    17. Hamadi, 1x ½
      Heko/ hongera/ pongezi/kongole
    18. Karimu 2x1
      Butu/pole/tamu
    19. Kabiliwa/ tingwa/ patwa 2x1
      Hakufa moyo
  4. ISIMU JAMII (5x2 mwanafunzi atoe mifano)
    1. Athari ya lugha ya kwanza – ulefu/urefu.
    2. Hali ya kiakili ya msemaji – mgonjwa au mlevi hudondosha sauti
    3. Kuhamasisha mafunzo na lugha moja hadi nyingine – katoto/kitoto
    4. Kutodhibiti mfumo na ngeli katika lugha – ng’ombe hii/ng’ombe huyu.
    5. Kujumuisha kanuni za lugha- mnyambuliko wa vitenzi – soma – somanya.
    6. Kasi ya uzungumzaji huathiri usanifu wa lugha.
    7. Makosa ya kimakusudi – ili kuburudisha au kuchekesha.
    8. Kosa la kutoelewa maana ya neno kimatumizi au umilisi wa maneno.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Bungoma Diocese Mock Exams 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest