Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kigumo Mocks 2021 Exams

Share via Whatsapp

Maagizo

  1. Andika jina lako na nambari yako ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
  2. Tia sahihi yako kisha uandike tarehe ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
  3. Jibu maswali manne pekee.
  4. Swali la kwanza ni la lazima.
  5. Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani: Riwaya, Hadithi Fupi, Kigogo na Fasihi Simulizi.
  6. Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  7. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  8. Majibu yote sharti yaandikwe kwenye nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali.
  9. Karatasi hii ina kurasa 5 zilizopigwa chapa.
  10. Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.


MASWALI

SEHEMU A : USHAIRI

  1. Lazima
    Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

    Afrika
    Bara uliyetukuka na kusifika,
    Unayevumbika asili yetu,
    Bara uliyekumbwa na vimbunga,
    Vimbunga vya kila aina,
    Tangu zama za utumwa hadi za leo,
    Bara usiyekata tamaa,
    Bara usiyejua kukimwa,
    Bara usiyejua kinyongo.

    Ardhi yako imejaa hazina kochokocho,
    Batini yako imefunika nemsi na utajiri,
    Unagombaniwa,
    Unapong’ang’aniwa,
    Utajiri unaokugeuza kinyang’anyiro,
    Kinyang’anyiro cha kushindaniwa.

    Uso wako umeenea machozi tele,
    Machozi ya kilio cha wanao,
    Wanaopigana vita kila uchao bila kujua kwani,
    Kilio cha wanao wanaokufa njaa penye wingi wa mali,
    Kilio cha waliao wakitamani kuiona haki, usawa na ukweli,
    Wengine wanakukatia tamaa, sikati,
    Wengine wanakulaani, silaani,
    Wengine hawana matumaini, ninayo.

    Najua iko siku,
    Utasimama kama mlima kwa kujishasha,
    Utanguruma kama simba mwenye kutisha,
    Siku hiyo watajua Afrika bado haijawa.
    1. Eleza dhamira ya shairi hili.(alama 2)
    2. “Shairi hili ni la kutamausha.” Thibitisha kwa mifano tano.(alama 5)
    3. Fafanua umuhimu wa aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili.(alama 2)
    4. Eleza mitindo inayojitokeza katika shairi hili. (alama 4)
    5. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 1)
    6. Andika ubeti wa pili katika lugha nathari (alama 4)
    7. Eleza toni la shairi hili. (alama 2)

SEHEMU B: RIWAYA
Assumpta K. Matei: Chozi la Heri
Jibu swali la 2 au 3

  1.                            
    1. “Tathmini nafasi ya wimbo wa Shamsi katika kuijenga riwaya ya “Chozi la Heri.”(alama 10)
    2. “Nilitaka kuhizika kwa kutamani kufa lakini nikauambia moyo wangu kwamba nimekufa japo sijafa.”
      Kwa kurejelea hoja kumi kutoka kwenye riwaya hii, thibitisha kwamba mzungumzaji wa maneno haya anastahili kutamani kufa. (alama 10)
  2. “Niliichukia jaala iliyonipa mama anayejali masilahi yake tu, nilichukia nguvu ya maumbile iliyoniweka kwenye jinsia ya kike ...”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.(alama 4)
    2. Andika toni ya kauli hii.(alama 2)
    3. Kwa kurejelea maisha ya mzungumzaji, bainisha vichocheo sita vya kauli iliyopigiwa mstari. (alama 6)
    4. Fafanua umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya katika kuijenga riwaya hii.(alama 8)

SEHEMU YA C:HADITHIFUPI
TUMBO LISILOSHIBA NA HADITH INYINGINE(ALIFACHOKOCHO NA DUMU KAYANDA)

Jibu swali la 4 au 5
TUMBO LISILOSHIBA (S.AMOHAMMED)

  1.                    
    1. Hakuna aliyeweza kukitegua kitendawili chenyewe lakini…’
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama4)
      2. Tambua mitindo uliyotumiwa katika dondoo hili. (alama2)
      3. Fafanua chanzo na hatima ya kitendawili kinachorejelewa katika dondoo hili.(alama 6)
      4. Eleza wasifu wa warejelewa katika dondoo hili. (alama4)
    2.  Huku ukirejerea hadithi ya Tulipokutana tena eleza namna unyanyashaji umeshughulikiwa(alama 4)
  2.              
    1. Bainisha masharti ya kisasa yanayoongoza ndoa ya kisasa kwa mujibu wa hadithi ya “Masharti ya Kisasa.” (alama 10)
    2. Kwa kurejelea “Shibe Inatumaliza”, bainisha mchango wa raia katika kuizorotesha jamii yao. (alama 10)

SEHEMU D: TAMTHILIA
Pauline Kea: Kigogo

Jibu swali la 6 au 7

  1. “Na hii Runinga ya Mzalendo nayo haina maisha Sagamoyo. Kitabakia kituo kimoja tu!”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Fafanua umuhimu wa anayeambiwa maneno haya.(alama 4)
    3. Kando na kizingiti kinachojitokeza katika dondoo hili, bainisha vizingiti vingine kumi na viwili walivyokumbana navyo Wanasagamoyo katika kupambana na udhalimu jimboni.(alama 12)
  2. “Ukitaka kuwafurusha ndege,katamti”
    1. Weka dondoo hili katika muktadha wake (alama4)
    2. Onyesha mbinu nyingine zinazotumiwa na wahusika hawa kutimiza malengo yao. (alama16)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

  1.                      
    1. Soma maelezo yafuatayo kisha ujibu maswali.
      Zamani, jamii mbalimbali ziliwasiliana kwa njia ya ngoma kutangaza kifo, kusherehekea mavuno mazuri na kadhalika.
      1. Fasihi hii ya kuwasiliana na ngoma inaitwaje? (alama 1)
      2. Fasihi hii ilikuwa na dhima gani katika jamii? (alama 4)
    2. Bainisha majukumu matano ya nyimbo katika maigizo.(alama 5)
    3. Umepewa jukumu la kukusanya data ukitumia hojaji.
      1. Eleza manufaa matano ya kutumia mbinu hii. (alama 5)
      2. Eleza changamoto tano za kutumia mbinu hii. (alama 5)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA 

  1. USHAIRI
    1. Kusifu bara la Afrika/Kueleza kuhusu shida za bara la Afrika/ Kueleza kuhusu kilio cha Waafrika. 1 x 2 = 2
    2. Shairi hili ni la kutamausha:
      1. Waafrika wanalia/wana kilio/wana machozi tele.
      2. Vita - watu wanapigana vita.
      3. Njaa - Waafrika wanakufa njaa licha ya kuwa na mali.
      4. Hakuna haki, usawa na ukweli barani Afrika.
      5. Bara la Afrika limekatiwa tamaa na baadhi ya watu.
      6. Laana - kulaaniwa kwa bara la Afrika. 5 x 1 = 5
    3. Aina za urudiaji:
      1. Urudiaji wa sauti - unagombaniwa, unapong’ang’aniwa, utajiri (ubeti 2) Umuhimu: Kujenga ridhimu/kulipa shairi mwonjo/mdundo wa kimuziki/kuleta urari wa vina.
      2. Urudiaji wa silabi - kujishasha, kutisha (ubeti 4)
        Umuhimu: Kujenga ridhimu/kulipa shairi muonjo/mdundo wa kimuziki/kuleta urari wa vina.
      3. Urudiaji wa neno - vimbunga/bara/kilio Umuhimu: Kusisitiza ujumbe wa nafsineni.
      4. Usambamba:
        Kilio cha wanao wanaokufa Kilio cha waliao wakitamani
        Umuhimu: Kuchimuza toni ya shairi – huzuni
        Kutaja na mfano - alama 1/2; umuhimu - alama ½
        Za kwanza 2x1
    4. Mitindo
      1. Uhaishaji/tashihisi/uhuishi - Bara usiyekata tamaa
      2. Kinaya - Kilio cha wanao wanaokufa njaa penye wingi wa mali
      3. Tashibihi - Utanguruma kama simba/Utasimama kama mlima
      4. Taswira - Utasimama kama mlima kwa kujishasha
      5. Takriri - vimbunga/bara/kilio
      6. Jazanda - vimbunga ni jazanda ya dhiki zinazolikumba bara la Afrika zozote 4 x 1= 4
    5. Mwafrika/Mtu wa asili ya Afrika - Bara unayevumbika asili yetu 1 x 1 = 1
    6. Ardhi yako ina hazina tele. Ndani mwako mna sifa nzuri na ukwasi. Unapiganiwa kutokana na ukwasi wako. Umekuwa kitu cha kushindaniwa/ kupiganiwa. 2 x 1= 2
    7. Toni:
      1. Toni ya kusifu - Bara uliyetukuka na kusifika/Unayevumbika asili yetu
      2. Toni ya huzuni - Uso wako umeenea machozi tele.
      3. Toni ya matumaini - Najua iko siku utasimama kama mlima kwa kujishasha
        1 x 2 = 2
  2. Riwaya
    1. Umuhimu wa wimbo wa Shamsi:
      1. Kukashifu Shamsi kwa kutumia mbinu hasi kutatua shida ambayo alisababishiwa na watu. Shamsi anasema kuwa pombe imekuwa dawa mujarabu ya kuuguzia banguzi alilosababishiwa na mahasidi.
      2. Kuonyesha madhara ya ulevi. Shamsi anaitwa ‘Bwana Dengelua’ kwa sababu ya tabia yake ya ulevi.
      3. Kukashifu unyanyasaji wa wanyonge. Bwana Mabavu anaipoka aila ya Shamsi ardhi yao akitumia hatimiliki bandia na kuwaacha wakiwa maskwota.
      4. Kuendeleza maudhui ya ufisadi. Bwana Mabavu anawapoka akina Shamsi ardhi yao akitumia hatimiliki bandia.
      5. Kuwakashifu wanyonge kwa kuchangia kukandamizwa kwao. Akina Shamsi wanapokwa ardhi yao na Bwana Mabavu lakini wanajikunyata kwa woga badala ya kujitetea. Wanaishia kuwa vibarua katika shamba lililokuwa lao.
      6. Kukuza maudhui ya uwajibikaji. Baba Shamsi anajibidiisha kufanya kazi ili kupata hela za kulipa karo ya Shamsi.
      7. Kuonyesha jukumu la elimu katika jamii. Shamsi anasema kuwa alisoma chuoni kwa lengo la kuja kumvua baba yake ufukara.
      8. Kuendeleza maudhui ya umaskini. Aila ya Shamsi ni maskini. Shamsi anasoma kwa lengo la kuja kuivua umaskini unaoigubika.
      9. Kukashifu ubaguzi na unasaba. Shamsi akitafuta kazi, hapati. Wanaoajiri wanatoa kazi hizo kwa ndugu zao na kuwaacha wasomi kama Shamsi wakitaabika bila ajira.
      10. Kukashifu ukiukaji wa haki za wafanyakazi:
        • Shamsi na wafanyakazi wengine wanalipwa ujira duni.
        • Wafanyakazi kama Shamsi wanapoomba nyongeza ya mshahara wananyimwa kwa madai kwamba wao ni vibarua wasiokuwa na maarifa ya kazi.
        • Wafanyakazi wasomi kama Shamsi hawapandishwi vyeo kama wanataaluma wengine.
        • Wafanyakazi kama Shamsi wanafanyia kazi kwenye mazingira duni. Anafanyia kazi katika banda.
        • Wafanyakazi kama Shamsi wananyimwa haki ya kugoma na kuandamana ili kutetea maslahi yao. Kampuni inamfuta kazi pamoja na wafanyakazi wengine kwa madai kuwa wanawazia kugoma, hivyo kuifilisi kampuni.
        • Kufutwa kazi. Shamsi na wafanyakazi wengine wanafutwa kazi kwa madai kuwa wanawazia kugoma hivyo kuifilisi kampuni.
      11. Kuchimuza athari za ukosefu wa chakula. Baba Shamsi anakufa kutokana na kula mizizi mwitu yenye vijasumu kwa kukosa chakula.
      12. Kukashifu ukosefu wa uwajibikaji wa viongozi. Hakuna hospitali kijijini mwa Shamsi. Hata kwenye hospitali ya walalahoi jijini haina dawa, hivyo kuchangia kifo cha Baba Shamsi.
      13. Kukuza maudhui ya utabaka. Kuna hospitali za maskini na za matajiri. Shamsi anasema kwamba hospitali za walalahoi jijini hazikuwa na dawa.
      14. Unaendeleza ukoloni mamboleo. Mabavu anaendeleza tabia ya kikoloni ya unyakuzi wa ardhi kwa kuipoka aila ya Shamsi ardhi na kuiacha ikiwa skwota.
      15. Kukashifu matumizi mabaya ya vileo. Inambidi mkewe Shamsi anayeitwa Bi. Halua kumfuta Shamsi siku ya kulipwa ujira ili ajitwalie sehemu yake kabla ya Shamsi kuutumia ujira wote kwenye ulevi. Zozote 10 x 1 = 10
    2. uk. 30. Kaizari anastahili kutamani kufa kwa sababu ya dhiki zilizomkumba:
      1. Kubakwa kwa wanawe. Mabarobaro watano wanawabaka watoto wake, Lime na Mwanaheri.
      2. Kukatwa kwa mke. Vijana watano wanamkata mkewe Subira kwa sime.
      3. Dhiki za kisaikolojia. Anashuhudia wanawe Lime na Mwanaheri wakibakwa, hivyo kubaki na dhiki za kisaikolojia.
      4. Kutoroka nyumbani. Anatoroka nyumbani baada ya wanawe kubakwa na mkewe kukatwa bila kujua aendako.
      5. Kushuhudia watu wakichomwa. Akitoroka ghasia za baada ya uchaguzi, anashuhudia barabarani mabasi mazima yakichomwa pamoja na shehena zayo, hivyo kuathirika kimawazo.
      6. Gari kuisha petroli. Gari alilokuwa akisafiria akitoroka ghasia za baada ya uchaguzi liliishiwa mafuta, hivyo kumlazimu kuingia msituni.
      7. Kulala njaa. Siku ya kwanza katika Msitu wa Mamba, yeye na aila yake walilala njaa kutokana na ule ugeni wa kutojua hata kuliko na matunda mwitu.
      8. Baridi. Akiishi katika Msitu wa Mamba, aliathiriwa na baridi na umande wa asubuhi hadi yeye na wakimbizi wenzake wakaamua kujenga vibanda.
      9. Kuishi kwenye kibanda.Akiwa mkimbizi, analala kwenye kibanda kilichoezekwa kwa nyasi na kukandikwa kwa udongo.
      10. Ukosefu wa maji safi. Akiwa mkimbizi anakosa maji safi ya kunywa.
      11. Magonjwa. Akiwa mkimbizi, homa ya matumbo inazuka baada ya wakimbizi kunywa maji machafu ya Mto wa Mamba. Baadhi yao wanakufa.
      12. Kupigania chakula. Akiwa kambini anapigania uji na aliyekuwa na waziri wa fedha.
      13. Ukosefu wa misala. Yeye na wakimbizi wenzake wanakosa misala kambini na kuanza kutumia vyoo vya kupeperusha hali inayozua ugonjwa wa kipindupindu.
      14. Kuishi katika mazingira machafu. Wakimbizi wanayachafua mazingira kwa kutumia vyoo vya kupeperusha kutokana na kutokuwepo wa misala.
      15. Ukosefu wa chakula. Yeye na wakimbizi wenzake wanakosa chakula. Wanasaidiwa na misikiti na makanisa.
      16. Kunyeshewa kwa wanawe. Akiwa mkimbizi, wanawe Lime na Mwanaheri wananyeshewa kwa kukosa hata tambara duni la kuwafunika. Za kwanza 10 x 1 = 1
  3. Uk. 149
    1. muktadha
      1. Maneno ya Pete mawazoni mwake.
      2. Anayaelekeza kwa Selume na Meko.
      3. Yu katika kituo cha afya cha Mwanzo Mpya.
      4. Ni baada ya kulazwa katika kituo cha afya cha Mwanzo Mpya kisha akakumbuka madhila aliyokumbana nayo kwenye ndoa yake na Fungo baada ya kuozwa na mama yake kwa lazima. 4 x 1 = 4.
    2. Toni ya uchungu - Pete ana uchungu kwa kuwa mwanamke kutokana na shida anazokumbana nazo kwa sababu ya jinsia yake. 1 x 2 = 2.
    3. Vichocheo;
      1. Kumkatiziwa masomo - Wazazi wake wanamkatizia masomo akiwa darasa la saba kwa kumwoza kwa Fungo kwa lazima ili wapate pesa za kuelimisha nduguze wa kiume.
      2. Kuozwa kwa lazima - Mama yake anamwoza kwa lazima akiwa darasa la saba, hivyo kumkatizia masomo yake.
      3. Kubaguliwa - Wazazi wake wanamwoza kwa Fungo akiwa darasa ka saba ili wapate pesa za kuwaelimisha nduguze (Pete) wa kiume, hivyo kumkatizia masomo.
      4. Kukataliwa - Baba yake anamkataa kuwa yeye si mwanawe kwa sababu ya kutokuwa na mshabaha naye.
      5. Kukosa sodo - akiwa mwezini alitumia tambara la blanketi na kanzu kuukuu kwa kukosa sodo za kutumia.
      6. Kudanganywa - Nyangumi anamhadaa kuwa wajaribishe maisha kisha wafunge ndoa baada ya miezi mitatu ila anamfurusha baada ya mkewe kumrudia.
      7. Kunyanyaswa kimapenzi - akiwa mlevi kwenye baa, anabakwa na kupachikwa mimba. Za kwanza 6 x 1 = 6
    4. Umuhimu wa Pete:
      1. Kukuza maudhui ya umaskini - anatumia kanzu kuukuu kwa kukosa sodo.
      2. Kielelezo cha watu wanaotumia mbinu hasi kutatua shida zao. Anakunywa dawa ya kuulia panya ili kujiangamiza kwa kuchoshwa na dhiki za maisha.
      3. Kielelezo cha dhiki za wafanyakazi. Akifanya kazi kwa Patel analipwa mshahara duni - sh. 200 kwa siku.
      4. Kukuza sifa za wahusika wengine kama vile ubaguzi wa wazazi wake. Wazazi wake wanamwoza akiwa darasa la saba, wanamwoza ili kupata pesa za kuelimisha nduguze wa kiume watano.
      5. Anaonyesha madhara ya tohara ya wasichana. Anaozwa kwa lazima kwa maana katika jamii yake inaaminiwa kuwa msichana akiisha kupashwa tohara ataipaka familia tope ikiwa ataendelea kuozea kwao bila mume.
      6. Kukuza maudhui ya mabadiliko. Baada ya kunywa dawa za kuulia panya na maisha yao kuokolewa, anaamua kutoishi maisha ya kujidhalilisha.
      7. Kuonyesha vizingiti vinavyoikumba elimu ya mtoto wa kike. Anaachishwa shule akiwa darasa la saba na kuozwa kwa Fungo.
      8. Anaonyesha madhara ya matumizi mabaya ya vileo. Akiuza pombe, anaanza kulewa na kuishia kubakwa.
      9. Anatumiwa kukashifu unyanyasaji wa kimapenzi. Anabakwa akiwa amelewa kwenye baa.
      10. Kielelezo cha wanawake wanaokiuka haki za watoto. Anameza vidonge ili aavya mimba aliyopachikwa na Nyangumi.
      11. Anaonyesha changamoto zinazokumba ndoa ya wanawake wengi. Mke mwenza wa pili anamwonea wivu baada ya kuolewa na Fungo. zozote 8 x 1 = 8
  4. Tumbo lisiloshiba 
    1. uk. 47
      1.                                                
        1. Hii ni kauli ya mwandishi
        2. anarejelea tukio la ulafi wa Jitu
        3. mahali ni katika mkahawa mshenzi wa Mzee Mago
        4. watu wamepigwa na butwaa kwa tendo la ulafi wa Jitu.4x1=4
      2.                    
        1. nahau-kukiangua kitendawili
        2. jazanda -neno`kitendawili’kurejelea jambo Fulani lililofichika
        3. mdokezo- chenyewe lakini..(zozote 2x1)
      3.                
        •  Chanzo
          1. Kuwepo kwa uvumi na nong`ono kuhusu uwezekano wa kunyakuliwa ardhi ya Wanamadongoporomoka.
          2. Mzee Mago kuwahamasisha raia kuhusu haja ya kutetea kazi zao.
          3. Mikutano ya kuandaa mikakati ya kutetea haki zaWanamadongoporomoko inayofanyika katika mkahawa.
          4. Jitu kuwasili mkahawa mshenzi na kuzua taharuki
          5. Jitu kuamrisha kuhudumiwa na kula chakula chote kilichoandaliwa.
          6. Watu kupigwa na butwaa kwa ulafi wa jitu na kuwazia tendo hili (zozote 3x1)
        • Hatima
          1. Jitu kuahidi kurudi keshoye kula maradufu ya siku hiyo.
          2. Hatimaye jitu kufika na mabuldoza
          3. Askari wa baraza kuandamana na jitu
          4. Jeshi la polisi kuwalinda askari wa baraza
          5. watu kupigwa virungu bila hatia
          6. Vibanda kubomolewa
          7. Watu kujenga upya`vibanda mshezi’zaidi ya hapo awali
            (Hoja zozote 3x1)
      4. Wasifu wa warejelewa katika dondoo hili.
        1. Wazalendo halisi;wanaendeleza harakati za kupigania haki zao za kumilikina kukomboa ardhi yao.
        2. Wenye bidi:hawasiti/hawakomi kuandaa mikakati ya kupigania haki zao. mfano:mikutano yao.
        3. Wenye umoja na ushirikiano:wanashirikiana kwa kukutana na kupanga utetezi wa haki zao.
        4. Wakakamavu/jasiri:wanakaidi hatua ya Jitu na kuikomboa ardhi yao
          (zozote 4x1)
    2.                      
      1. Bogoa anatenganishwa na jamaa wake anapopelekwa kuishi na Bi Sinai
      2. Bogoa kufanyishwa kazi nyingi na ngumu na Bi Sinai-kuna nazi ,kupara na kutoa matumbo ya samaki nk
      3. Kuamshwa mapema kuliko wengine ili kuchoma mandazi ya kuuza shule.
      4. Bogoa kunyimwa elimu ya shule na Bi Sinai .
      5. kunyimwa haki ya lishe bora kwani analazimika kula makoko na makombo yaliyobaki.
      6. Bogoa kuchomwa viganja vya mkono kwa moto anapounguza mandazi aliyokuwa akichoma.
        ( Zozote 4x1)
  5.                          
    1. Masharti yanayoongoza ndoa ya kisasa:
      1. Wanandoa wote kufanya kazi - Dadi na Kidawa walifanya kazi; Kidawa - umetroni na Dadi - kuchuuza samaki.
      2. Mume kumsaidia mke kazi za nyumbani - Masharti ya kisasa yalimlazimu Dadi kumsaidia mkewe Kidawa kazi za nyumbani.
      3. Kupanga uzazi - Kidawa na Dadi wanapanga kuwa na mtoto mmoja katika uzazi wa kisasa.
      4. Wanandoa kuwa waaminifu - Dadi anakereka anapomwona mkewe Kidawa akiamkiana na kuzungumza na wanaume kwa kudhani kwamba anayavunja masharti ya ndoa yao.
      5. Mwanamke kutoa mitihani kwa wanaume - Kabla Kidawa achague mume wa kumwoa, aliwapa wengine waliomtaka mtihani kisha akamchagua Dadi aliyefaulu mtihani huo.
      6. Mwanamume kufanya wajibu wa kisasa. Kidawa anamwambia Dadi kabla amwoe kwamba akitaka kumwoa lazima afanye wajibu wa kisasa kwa yeye atakayekuwa mkewe wa kisasa.
      7. Mwanamke kutafuta mume mwenye mapenzi ya kisasa. Kabla wafunge ndoa, Kidawa anamwambia Dadi kwamba yeye ni mwanamke wa kisasa anayemtafuta mwanamume mwenye mapenzi ya kisasa.
      8. Mwanake kuamua wakati wa kuposwa. Wakati wa kuposwa ulipofika, Kidawa alimwagiza Dadi kuenda kwao kumposa.
      9. Masharti yanayoongoza ndoa kutiwa saini. Kidawa anamtilisha Dadi saini masharti ya kisasa ambayo yangeongoza ndoa yao.
      10. Mwanamke kujipodoa - Kidawa alijipodoa ili kumhakikishia mumewe Dadi kwamba yeye ni mwanamke mrembo wa kisasa ili asije akatamani wanawake wengine.
      11. Mume kuthibitisha ikiwa mwanamke ameremebeka. Kila wakati baada ya kujipodoa, Kidawa alienda na kusimama kwa Dadi na kumuuliiza iwapo alipendeza au la.
      12. Mwanamke kuwa na uhuru wa kuvaa. Japo buibui hufunika kifua, buibui ya Kidawa haikufunika kifua. Hili lilimkera Dadi ila hakuwa na la kufanya.
      13. Mwanamke kugharimia mahitaji yake. Kidawa alijinunulia viatu na kanzu. n.k.
        (Zozote 10 x 1 = 10)
    2. Raia walivyovunja jamii:
      1. Mambo analifilisi taifa lake kwa kupokea mshahara bila kufanya kazi - uk. 37
      2. Katika taifa la Mambo kinachoangaliwa zaidi ni kwenda kazini wala si kufanya kazi. Jambo hili linapalilia uzembe miongoni mwa wafanyakazi - uk. 37
      3. Raia kama Mambo wanatumia dini kuficha uovu wao. Mambo analipora taifa kisha anajiliwaza kwa aya takatifu kuwa Allah humpa amtakaye bila kiwango maalumu ilhali ameiba - uk. 37
      4. Wafanyakazi wananyanyaswa kwa maana wao wanafanya kazi kisha wasiofanya kazi kama Mzee Mambo wanapokea mshahara - uk/ 37
      5. Mambo anatumia runinga ya taifa kupeperusha sherehe ya kibinafsi iliyofanyika nyumbani kwake ilhali runinga hii inafaa kupeperusha masuala ya kitaifa - uk. 38
      6. Mambo anatumia magari ya serikali vibaya. Anayatumia katika kusomba jamaa zake na mapambo kwenye sherehe iliyofanyika nyumbani kwake - uk. 38 - 39
      7. Rais anaruhusu gari la ikulu kutumika vibaya. Analiruhusu kutumika katika kusomba chakula kuelekea nyumbani mwa Mambo badala ya kumbeba rais
      8. Badala ya kuwa kazini, Sasa na Mbura wanaibia serikali saa za kufanya kazi kwa kuenda kuhudhuria sherehe nyumbani mwa Mambo - uk. 39
      9. Wanakumbatia vyakula vya kigeni kama mchele wa basmati vilivyo na madhara na kupuuza vyakula vya kienyeji kama mchele wa Mbeya vyenye manufaa katika miili yao.
      10. Mambo anaendeleza ufisadi ila hajali. Analifilisi taifa kisha anacheza nyimbo zenye ujumbe wa ‘sijali lawama’ kwenye sherehe yake ishara kwamba hajali kulifilisi taifa lake - 43
      11. Mzee Mambo anaifilisi serikali kwa kugharimia sherehe ya inayofanyika nyumbani kwake. Serikali inagharimia malipo ya walioifanikisha sherehe hiyo kama vile DJ
      12. DJ anazorotesha uchumi wa taifa lake kwa kupora pesa kutoka kwenye bohari kuu ya dawa za serikali na kufungua duka lake la dawa - uk. 43
      13. DJ analihini taifa lake ushuru kwa kutolipia huduma za maji, umeme na matibabu kama wananchi wengine - uk. 43
      14. Serikali inawadhulumu wanyonge kwa kuwalazimisha kulipia huduma za maji, umeme na matibabu huku matajiri kama DJ wakizipata huduma hizi bila malipo
        (Zozote 10x1)
  6. Tamthilia
    Uk. 37
    1. Muktadha
      1. Maneno ya Majoka.
      2. Anamwambia Kenga.
      3. Wamo ofisini mwa Majoka.
      4. Ni baada ya ya Runinga ya Mzalendo kuonyesha maandamano ya wachuuzi wakipinga kufungwa kwa soko kisha Majoka akaamua kuifunga. 4 x 1 = 4
    2. Umuhimu wa Kenga
      1. Kielelezo cha watu wanaopata kazi kwa sababu ya mahusiano yao na walio mamlakani - anateuliwa na Majoka kuwa mshauri mkuu wa Majoka kwa sababu ni binamuye - uk. 9
      2. Kuendeleza maudhui ya ukiukaji wa haki za binadamu - anamuua Jabali
      3. Kujenga maudhui ya ufisadi - anakubali kugawiwa ardhi ya soko la Chapakazi iliyokuwa imenyakuliwa na Majoka - uk. 69
      4. Ametumiwa kubainisha taasubi ya kiume ya Majoka. Majoka anamwita ovyo kwa kuisikiliza hotuba ya mwanamke (Tunu).
      5. Kuendeleza maudhui ya mabadiliko - raia wanapoandamana kumtoa Majoka mamlakani, anaacha mrengo wa Majoka na kuungana nao - uk. 91 4 x 1 = 4
    3. Vizingiti:
      1. Majoka anawafurusha wafadhili wa Tunu kwa sababu ya Tunu kuwahutubia waadishi wa habari na kumkashifu kwa kufunga soko na kufuja pesa za kusafisha soko.
      2. Tunu anapoongoza maandamano ya kupinga kufungwa kwa soko, Majoka anawatuma wahuni wanaomvamia na kumjeruhi.
      3. Jabali anaunda chama cha upinzani cha Mwenge ili kuleta upinzani wa kisiasa dhidi ya Majoka na kuboresha uongozi, Majoka anamuua.
      4. Majoka anapogundua kwamba Tunu na Sudi wanashirikiana katika kuupinga udhalimu wake wa kufunga soko, anawatuma wahuni kwa Tunu kusambaratisha umoja wao; wanampiga na kumwambia kwamba ni Sudi na Ashua wanaoiwinda roho yake ilhali ni Majoka; anataka kuuvunja ushirikiano wao katika kuupinga udhalimu wake.
      5. Baadhi ya raia kama Ngurumo wanasifu udhalimu wa Majoka wakati wengine kama Tunu wanaukashifu. Tunu anataka soko lifunguliwe ilhali Ngurumo anasema kuwa tangu soko lifungwe, Sagamoyo pamekuwa pazuri zaidi.
      6. Tunu anawaalika raia katika mkutano wa kupinga kufungwa kwa soko na Majoka lakini raia kumi wanamsaliti kwa kuamua kuhudhuria mkutano wa Majoka.
      7. Badala ya wafanyabiashara kama Boza na Kombe kuungana na Tunu katika kumlazimisha Majoka kufungua soko, wao wanahamia ulevini soko linapofungwa ilhali ni wao waliolitegemea katika kupata riziki.
      8. Watetezi wa haki kama Tunu wanadhalilishwa wanapowazindua wanyonge. Anapoenda Mangweni na kuwaambia walevi kujiokoa kutokana na pombe kwa maana iliua na kupofusha, walevi wanamwimbia wimbo wa kukashifu hali yake ya kuchelewa kuolewa.
      9. Raia kama Hashima, badala ya kuungana na akina Tunu katika harakati za kuhakikisha kuwa soko limefunguliwa, yeye anapanga kutoroka Sagamoyo, hivyo kupalilia udhalimu zaidi. Haya yanabainika kwenye wimbo wake.
      10. Vijana watano waliondamana kupinga kupandishwa kwa chakula kwenye kioski cha kampuni ya Majoka wanauliwa.
      11. Raia asilimia sitini inataka kumchagua Tunu kuwa kiongozi wao kama njia ya kupambana na udhalimu wa Majoka lakini wanakutana na kizingiti cha Majoka kutaka kumrithisha mwanawe Ngao Junior uongozi, hivyo kuwahini nafasi ya kumchagua wanayemtaka.
      12. Kufutwa kazi. Kingi anapokataa kuwaua waandamanaji alivyotaka Majoka; Majoka anampiga kalamu.
      13. Vitisho - Kingi anapotaka kuwaua waandamanaji, Majoka anaanza kumtisha kuwa angevunjwavunjwa na chatu. Za kwanza 12x1
      14. Sudi anapokataa kumchongea Majoka kinyago kama njia ya kuupinga udhalimu wake, Majoka anamfunga mkewe Ashua ili kumlazimisha kukichonga. n.k.
        12 x 1 = 12
  7.                
    1. (Dondoo)
      Mnenaji: Kenga
      Mnenewa Majoka
      Mahali Ofisini mwa majoka
      Mada(kuhusu)Jinsi/mbinu za kuwazima
      Wapinzani na hasa kiongozi wao ambaye ni tunu aliyeongoza maandamano
      (4x1=4)
    2. Mbinu nyingine walizotumia
      1. Mauaji–wapinzani kama jabali waliuawa
      2. Vishawishi/tuzo–AshuanaTunu walikuwa wanapewa ajira ili kushawishika wakakataa
      3. Kutumia vikaragosi kama Kenga(mshauri mkuu,askari nk)
      4. Kutoa ajira kwa misingi ya mapendeleo
        Km Asiya na mradi wa keki Kenga alikuwa binamu wa Majoka
      5. Mikopo kutoka nje fedha ambazo zinafujwa kwa manufaa ya Majoka na wenzake kama vile Kenga zinatumiwa kupata uungwaji mkono
      6. Polisi–polisi wanatumika kuwatawanya waandamaji
      7. Uchochezi–wapinzani wanatupiwa vijikaratasi vya kuwataka wahame.
      8. Hofu–Hashima anaishi kwa hofu
        Hii inawafanya watu kuwa wanyenyekevu na kumuabudu majoka
      9. Ukiritimba–lengo la majoka ni kuwa na Chama Kimoja cha kisiasa,kituo
        Cha runinga na kampuni kutajwa kwa jina lake tu.
      10. Vyombo vya habari kituo;sauti ya mashujaa kinaendeleza shughuli zao
      11. Majoka anatumia redio kutangaza kufungwa kwa soko,watu kuchezewa
        Nyimbo za uzalendo bandia.
      12. Kuidhinisha shughuli haramu–upikaji wa pombe,ukataji wa miti
      13. Unasaba uongozi wa kurithishwa kifamilia.
      14. Matumizi ya msimbo–Majoka na Kenga wanatumia lugha ya kitamathali/msimbo wanaofahamu wao tu.Km‘Kuvunja miguu’‘kuvunjwa vunjwa na chatu’kupangiwa safari(kuuawa)
      15. Kuficha siri–chopi anapashindwa kumuua Tunu kwa njama wanapanga kumuua ilikufanikisha kadhia hiyo.
      16. Propaganda km.Eti Jabali alifariki katika ajali wavamizi wa Tunu wanasema Ashua na Sudi ndio walikuwa wakiwinda roho yake
      17. Jela–ilitumiwa kulipiza kisasi na kuwatisha wazalendokm Ashua (zozote 16x1)
  8. FASIHI SIMULIZI
    1. Kifungu
      1. ngomezi 1 x 1 = 1
      2. Dhima:
        • Iliiwezesha jamii kuwasilisha ujumbe kwa njia isiyoeleweka na jamii nyingine, hivyo kudumisha siri fulani.
        • Ngomezi ya kisasa hutahadharisha umma kuhusu kutendeka kwa jambo la dharura kama vile moto, vita, n.k.
        • Ni kitambulisho cha jamii. Kwa mfano, kila jamii ina aina zake za ngoma na mtindo wake wa midundo.
        • Ilidumisha utamaduni wa jamii kwa kuipitisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
        • Ilikuza uzalendo kwa kuwasababasha wanajamii kuionea fahari jamii yao.
        • Hukuza ubunifu – wanajamii walibuni mitindo mipya ya kuwasilisha jumbe kwa njia ambayo adui hangeelewa maana yake.
        • Ilidumisha umoja wa jamii – matumizi ya ngoma kuwasiliana yaliwafanya wanajamii kujihisi kuwa kitu kimoja. ( Zozote 4x1)
    2. Majukumu ya nyimbo katika maigizo:
      1. Hufanya maigizo kuburudisha zaidi.
      2. Husisitiza wazo kuu (dhamira) ambalo waigizaji wanadhamiria kukuza katika uigizaji wao.
      3. Ni kitulizo/kipumuo kwa hadhira katika maigizo yenye matukio ya kitanzia.
      4. Husaidia kuondoa ukinaifu/uchovu unaotokana na kuutumia mtindo wa aina moja kwa kipindi kirefu. Ubadilishaji wa mtindo wa uwasilishaji huifanya hadhira kuufurahia uigizaji zaidi.
      5. Husisitiza baadhi ya maudhui/migogoro katika maigizo.
      6. Huweza kutumiwa kufupisha baadhi ya matukio maigizoni; hivyo kupunguza uigizaji kwa maana mawazo makuu yatakuwa yamejumuishwa katika wimbo.
      7. Ni njia ya mwigizaji ya kuihusisha hadhira. Anaweza kuitaka kushiriki katika uimbaji.
      8. Huchochea hisia ambazo mwigizaji anaazimia kuzipitisha kwa hadhira yake kama vile furaha au huzuni.
      9. Hutumiwa kusawiri sifa za baadhi ya wahusika katika maigizo.
      10. Husaidia kurefusha maigizo.
      11. Kuwazindua wasikilizaji ambao huenda wakawa wamelala au kusinzia wakati maigizo yanaendelea. ( Za kwanza 5 x 1 = 5)
    3. Hojaji
      1. Manufaa ya hojaji
        • Ina gharama ya chini zaidi ikilinganishwa na njia nyinginezo.
        • Mtafiti anaweza kufikia idadi kubwa ya watoaji habari kwa kipindi kifupi kwa maaan hojaji zinaweza zikatumiwa watu hao kwa njia kama vile posta.
        • Inaweza kutumiwa katika mahojiano kama mwongozo. Mhoji anaweza kuitumia katika mahojiano kufidia udhaifu wa mhojiwa.
        • Humpa mhojiwa muda wa kuwazia maswali na kuyafanyia uchunguzi kabla ya kuyajibu.
        • Hazina athari za mtafiti kwa sababu aghalabu zinapojazwa mtafiti hayupo. Mhojiwa hujaza habari za kweli bila kushinikiwa kuchukua mtazamo fulani kutokana na kuwepo kwa mtafiti.
        • Zinaweza kubadilishwa kulingana na kiwango cha wajazaji/wahojiwa.
          (Za kwanza 5 x 1 )
      2. Changamoto za hojaji
        • Maswali yenye utata husababisha fasiri mbalimbali ambazo hufanya matokeo yasitegemeke.
        • Huenda wengine wasikamilishe kujaza hojaji, hivyo kumhini mtafiti habari anazotaka.
        • Hojaji ikiwa ndefu sana huenda baadhi ya watu wakakataa kuijaza.
        • Hojaji wazi huwa ngumu sana kwa mtafiti kuchanganua data. Uchanganuzi huchukua muda mrefu.
        • Huenda wahojiwa wasijaze mambo ya kweli. Si rahisi kwa mtafiti kuthibitisha iwapo habari zilizojazwa ni za kweli.
        • Wahojiwa wanawenza kuchelewa kutuma hojaji zao, hasa hojaji zilizotumwa kwa posta.
        • Zinaweza kujazwa tu na watu waliosoma, hivyo kuwatenga wengine ambao labda wangetoa habari za kutegemeka.
        • Kwa vile mtafiti hakabiliani na mhojiwa ana kwa ana, hawezi kupata sifa za uwasilishaji wa vipera vya fasihi simulizi kama vile toni na kidatu.
          (Za kwanza 5 x 1)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Kigumo Mocks 2021 Exams.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest