Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mokasa II Mock Examination 2021/2022

Share via Whatsapp

KISWAHILI
Karatasi ya 3
FASIHI

Maagizo:

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobakia, yaani: Tamthilia, Riwaya, Hadithi fupi, na Ushairi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.


Maswali

SEHEMU YA A: FASIHI SIMULIZI

  1. Lazima
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Ndimi Chesirwo, kijana barubaru,
    Ndume na gwiji, la ukoo mtukufu,
    Najivunia umahiri, kusakata kandanda.

    Tazama umbo langu, guu mithili ya jokovu,
    Kifua cha miraba, weusi wa kijungu,
    Wenzangu wanienzi, na hata kuduwaa.

    Misuli ni tinginya,
    Kijijini nasifika,
    Wazee kunienzi,
    Mabinti kunikabidhi.

    Maswali
    1. Tambua utungo huu na uthibitishe jibu lako. (alama 2)
    2. Kwa kurejelea hoja zozote nane, jadili sifa za utungo uliotambua katika (a) (alama 8)
    3.          
      1. Eleza maana ya maghani. (alama 1)
      2. Taja na ueleze tofauti za aina mbili za maghani. (alama 4)
    4. Eleza jinsi jamii ya kisasa inavyojaribu kuendeleza fasihi simulizi. (alama 5)

SEHEMU YA B: RIWAYA
Assumpta Matei: Chozi la Heri
Jibu swali la 2 au la 3

  1. Watu wengi huko mashambani hutegemea mashamba, mvua haijakubali kunyesha kwa muda. Wengi wa wanaofanya kazi za ajira, hufanya kazi za kijungu jiko.
    1. Bainisha muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Bainisha mbinu nne za kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)
    3. Eleza nafasi ya msemaji katika kuendeleza maudhui riwayani. (alama 12)
  2.          
    1. Inasikitisha kwamba badala ya kuiongoza jahazi letu wameligongesha mwamba bila kujua. Eleza jinsi warejelewa katika riwaya nzima walivyogongesha mwamba jahazi lao. (alama 14)
    2. Neno jahazi limetumika kitamathali. Onyesha jinsi tamathali hiyo ilivyotumika riwayani. (alama 6)

SEHEMU YA C: USHAIRI
Jibu swali la 4 au la 5

  1. Soma shairi hili kisha ujibu maswali:

    Wanaume ni Wanyama

    Nakumbuka vyema sana, sisahau siku ile
    Nilipoitwa na nina, akanipa ya kivyele
    Mwanangu u msichana, nakuasa usikile
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Kuwa umevunja ungo, ni hali ya maumbile
    Bora uwapo na bongo, anasa uzikimbile,
    Ukijitia maringo, utatungwa mimba mbele
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Ngawa waje na manoti, “Nakupenda” wakwambile
    Wakuvalie makoti, usiwaachie mbele
    Hata wapige magoti, wambile mna kelele
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Ngono ni tendo la suna, Amina sikimbile
    Wala miguu halina, kwamba lingekukimbile
    Muhimu kwako Amina, kwanza uthamini shule
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Kuzurura mitaani, si tabia njema ile
    Unapotoka nyumbani, fululiza hadi shule
    Si kwenda vichochoroni, kuwaona kina wale
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Uwe mwana msikizi, yano uyazingatile
    Mengine kuhusu penzi, mwanangu taonywa shule
    Kama mameyo mzazi, nimekuonya kimbile
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama

    Wakaja kina Hamadi, mwana wa Mzee Sule
    Kwangu wakapiga hodi, hata mkuu wa shule
    Ila nikajitahidi, kukwepa mitego ile
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Na kuna Karisa, mwanafunzi kule shule
    Akawa hunipapasa, name pia vilevile
    Mwishowe itakupasa, tugawe tunda tulile
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Nani akachovya uto, wa asali tamu vile
    Na kisha aape kuto, kula asali milele
    Kuwa mjamzito, wamenifukuza shule
    Si waone vile, wanaume ni wanyama.
    Karisa yu vilevile, angali ywaenda shule
    Na mie kitumbo mbele, ninajikuna upele
    Yameshatumia yale, niloonywa siku ile
    Si watu waone vile, wanaume ni wanyama.

    Maswali:
    1. Hili ni shairi la aina gani? Toa sababu. (alama 2)
    2. Eleza dhamira ya shairi hili. (alama 2)
    3. Bainsha mambo manne ambayo nafsineni anatoa kama ushauri kwa nafsinenewa. (alama 4)
    4. Huku ukitoa mifano, bainisha vipengele vitatu vya kimtindo ambapo mshairi ametumia kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu. (alama 3)
    5. Tambua uhuru wa kishairi uliotumiwa kwa kurejelea mifano mitatu. (alama 3)
    6. Andika ubeti wa sita kwa lugha nathari. (alama 4)
    7. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)

  2. Soma shairi hili kisha ujibu maswali:

    Nikiwa na njaa na matambara mwilini
    Nimehudumika kama hayawani
    Kupigwa na kutukanwa
    Kimya kama kupita kwa shetani
    Nafasi ya kupumzika hakuna
    Ya kulala hakuna
    Ya kuwaza hakuna
    Basi kwani hili kufanyika
    Ni kosa gani lilotendeka
    Liloniletea adhabu hii isomalizika?

    Ewe mwewe urukaye juu angani
    Wajua lililomo mwangu moyoni
    Niambie pale mipunga inapopepea
    Ikatema miale ya jua
    Mamangu bado angali amesimama akinisubiri?
    Je, nadhari hujitokeza usoni
    Ikielekea huku kizuizini?

    Mpenzi mama, nitarudi nyumbani
    Nitarudi hata kama ni kifoni
    Hata kama maiti yangu imekatikakatika
    Vipande elfu, elfu kumi
    Nitarudi nyumbani
    Nikipenya kwenye ukuta huu
    Nikipitia mwingine kama shetani
    Nitarudi mpenzi mama...
    Hata kama kifoni.

    Maswali
    1. Lipe shairi hili kichwa mwafaka (alama 1)
    2. Tambua nafsineni katika shairi hili (alama 1)
    3. Eleza toni katika shairi hili (alama 1)
    4. Taja mambo manne ambayo mshairi analalamikia (alama 4)
    5. Fafanua dhamira katika shairi hili (alama 2)
    6. Thibitisha kuwa hili ni shairi huru (alama 4)
    7. Taja na ufafanue sifa mbili za mshairi (alama 2)
    8. Fafanua mbinu tatu za kimtindo zilizotumika katika ubeti wa tatu. (alama 3)
    9. Eleza maana ya maneno yafuatoyo kama yalivyotumiwa katika shiari hili (alama 2)
      1. Hayawani
      2. Nadhari

SEHEMU YA D: TAMTHILIA
P. Kea: Kigogo
Jibu swali la 6 au la 7

  1. Huwezi kuyang’amua kwa kuwa umeyafumbia macho. Hujaibambua ngozi yako ya zamani.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Eleza mbinu za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 4)
    3. Kwa kurejelea tamthilia nzima, thibitisha kuwa mzungumziwa hajaibambua ngozi yake ya zamani. (alama 12)
  2.       
    1. Asasi ya ndoa imo hatarini katika jamii ya kisasa. Tetea kauli kwa mifano kumi katika tamthilia. (alama 10)
    2. Eleza umuhimu wa Babu katika Tamthilia ya Kigogo. (alama 10)

SEHEMU YA E: HADITHI FUPI
A. Chokocho na D. Kayanda:Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine
Jibu swali la 8 au la 9

  1.        
    1. A. Chokocho: “Masharti ya Kisasa”
      “Mwanzoni bila ya shaka, mambo hayakufikia kiasi hicho. Pale alipokuwa kufa na kupona akimtafuta Kiadawa, alipokuwa kiguu na njia akimwinda kama kunguru mwerevu, moyoni mwake alidhani anafuata nyuki apate kula asali. Ajabu lakini, kwa nini misumari ya nyuki inamuuma sasa ila si wakti ule wa tama ya ushindi ilipokuwa mbali, mbingu na ardhi?”
      1. Bainisha vipengele vine vya kimtindo vilivyotumiwa kwenye dondoo. (alama 4)
      2. Onyesha jinsi mrejelewa alivyokuwa ameumwa na misumari ya nyuki. (alama 6)
    2. A. Chokocho: “Tulipokutana Tena”
      “Mimi pia nilifurikwa na machozi lakini sikuyafuta. Nilibaki kushangazwa tu kusikia ukweli wenye makali yaliyochinja bila huruma”.
      Eleza kilichowaliza warejelewa katika dondoo hili. (alama 10)
  2. A. Abdulla Ali: “Ndoto ya Mashaka”
    Kwa nini matajiri wanazidi kutajirika na fukara wanazidi kufukarika na kudidimia?
    1. Bainisha muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Fafanua umuhimu wa msemaji. (alama 3)
    3. Eleza maudhui yanayojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
    4. Bainisha tamathali moja iliyotumika katika dondoo. (alama 1)
    5. Ufukara ni kikwazo kikubwa katika maisha ya wananchi wa kawaida. Huku ukitoa hoja kumi, tetea ukweli wa kauli hii ukirejelea hadithi ya Ndoto ya Mashaka. (alama 10)


Mwongozo wa Kusahihisha

  1. Lazima
    1. Tambua utungo huu na udhibitishe jawabu lako. (Alama 2)
      • Majigambo/vivugo- mwandishi anajisifu kwa umahiri wake binafsi.
        Kutaja alama 1 kudhibitisha alama 1

    2. Kwa kurejelea hoja zozote nane, jadili sifa za utungo uliotambua kwenye swali la (a). (alama 8)

      Sifa za majigambo
      • Hutungwa na kuganwa na muhusika mwenyewe.
      • Hutungwa kwa usanii mkubwa. Anayejigamba hutumia mitindo tofauti au ishara.
      • Mwenye kujigamba - hujitungia kivugo kufuatia tukio lililowah kuitokea maishani mwake.
      • Mara nyingi majigambo hutungwa na kuganwa na wanaume.
      • Husheheni matumizi ya chuku.
      • Hutolewa kwa nafsi ya kwanza.
      • Anayejigamba huweza kubeba baadhi ya vifaa vyake vya kazi au vinavyoonyesha jambo analojisifia.
      • Majigambo yanaweza kutungwa papo kwa hapo.
      • Anayejigamba huweza kutaja usuli wake wa kinasaba. Anaweza kusifu ukoo wake
      • Anayejigamba huwa mlumbi.
      • Maudhui makuu katika majigambo huwa ushujaa.
        (Akikosa (a) , atuzwe 0 katika (b) – Z a kwanza 8 x 1 = 8 athibitishe dai)
    3.                
      1. Maghani ni nini? (Alama 1)
        • Maghani ni ushairi ambao hutolewa kwa kalima badala ya kuimbwa. 1 x 1 = 01

      2. Taja na ueleze tofauti za aina mbili za maghani unazojua. (Alama 4)
        • maghani ya kawaida- tungo za mashairi yenye hubeba masuala ya kawaida; mfano, njaa, mapenzi, elimu nk.
        • Maghani simulizi: mashiri ya kihadithi ambayo husimulia sifa za mtu ,mnyama, kitu, historia au tukio fulani.
        • Kutaja – alama 2, kutofautisha 2/0

    4. Eleza jinsi jamii ya kisasa inavyojaribu kuendeleza fasihi simulizi. (Alama 5)
      1. Tamasha za kimziki. Wanafunzi hukariri, hugana na kuimba mashairi katika tamasha za muziki
      2. Sherehe za harusi, jando, mazishi na matambiko bado zinaendelezwa na jamii ya sasa.
      3. Utungaji na utegaji wa vitendawili kupitia redio na runinga.
      4. Michezo ya kuigiza katika runinga na redio.
      5. Tamasha za drama hihifadhi utanzu wa maigizo,mazungumzo na ushairi simulizi.
      6. Sarakasi za wasanii huhifadhi kipera cha vichekesho.
      7. Ngoma za kienyeji huchezwa kwenye hafla kama vile harusi au mikutano ya kisiasa.
      8. Wapo watafiti ambao huandika na kuhifadhi rekodi za vipera vya fasihi simulizi.
      9. Utambaji wa hadithi hutambwa na jamii nyingi za kisasa hasa sehemu za mashambani. ( Zozote 5 x 1 = 05)

  2. Watu wengi huko mashambani hutegemea mashamba, mvua haijakubali kunyesha kwa muda. Wengi wa wanaofanya kazi za ajira, hufanya kazi za kijungu jiko.
    1. Bainisha muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      1. Msemaji ni Tila.
      2. Msemewa ni Ridhaa
      3. Walikuwa nyumbani.
      4. Ridhaa alikuwa akiwazia mazungumzo baina yake na Tila. Tila alikuwa akirejelea hali ngumu ya maisha iliyowakumba wafanyakazi huko mashambani.
        4 x 1 = 4

    2. Bainisha mbinu nne za kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)
      1. Tashihisi mvua haijakubali kunyesha kwa muda.
      2. Takriri/uradidi – kazi
      3. Mbinu rejeshi/kisengere nyuma/ mbinu ya kioo – Ridhaa anakumbuka mazungumzo kati yake na Tila.
      4. Msemo – kazi ya kijungu jiko. 4 x 1 = 4

    3. Eleza nafasi ya msemaji katika kuendeleza maudhui riwayani. (alama 12)
      1. Kupitia kwake, mwandishi anaonyesha umuhimu wa elimu. Tila anayarejelea mafunzo waliopewa shuleni kuhusu masuala ya uongozi, uchumi na usawa wa kijinsia.
      2. Anabainisha maudhui ya mabadiliko. Tila anasema kuwa walifundishwa jinsi mifumo ya uzalishaji mali imebadilika kutoka ujima hadi utandawazi.
      3. Anaendeleza maudhui ya uongozi. Tila anaeleza kuwa, utawala huteuliwa maksudi kuendeleza mfumo uliopo wa kiuchumi.
      4. Anabainisha maudhui ya siasa. Tila anaeleza mabadiliko ya kisiasa ilivyokumba jamii yao na wapiga kura kuwazia kumchagua Mwekevu. Kura ya maoni ilionyesha Mwekevu akiongoza kwa asilimia sitini.
      5. Kubainisha nafasi ya mwanamke katika jamii. Tila anasema kuwa, mwalimu wao alisema kwamba, uwajibikaji wa mtu haufai kupimwa kwa misingi ya kijinsia.
      6. Anadokeza maono ya wapiganiaji wa uhuru. Anadai kuwa, lengo la wapiganiaji uhuru lilikuwa kuondoa umaskini, ujinga na magonjwa katika jamii.
      7. Anabainisha umaskini uliopo katika jamii. Tila anasema kuwa, mara nyingi alikuwa amemwona Ridhaa akijishika tama kulalamikia asilimia kubwa ya raia ambao hawakumudu gharama ya matibabu ya kimsingi.
      8. Anaonyesha kuwa vifo vya vingi vya watoto husababishwa na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa lishe bora.
      9. Ajira duni- watu wengi wanaofanya kazi za ajira mashambani hufanya kazi za kijungu jiko.
      10. Ukoloni mamboleo – Tila anadai kuwa, uchimbaji wa madini unafadhiliwa na wafadhili wa kigeni hivyo faida inayopatikana inaishia kwenye mifuko ya wageni hao. Anaonyesha kuwa mashamba mengi yanamilikiwa na wakoloni huku wenyeji wakiwa maskwota hata baada ya uhuru.
      11. Kuendeleza maudhu ya haki – alizoea kuwambia babake kuwa alitaka kuwa jaji wa mahakama kuu ili kusuluhisha kesi ambazo zilikuwa zimeselelea mahakami kwa miongo miwili au zaidi bila kusikizwa.
      12. Ufisadi – anadokeza kuwa, faili za kesi mahakamani ‘hupotea’ hivyo kuchelewesha uamuzi wa kesi.
      13. Ametumiwa kuonyesha maudhui ya utegemezi – Kwa mujibu wa Tila, wenyeji hawana mashamba wanategemea wageni kwa vyakula na ajira. Zozote 12 x 1 = 12

  3.                 
    1. Inasikitisha kwamba badala ya kuiongoza jahazi letu wameligongesha mwamba bila kujua. Eleza jinsi warejelewa katika riwaya nzima walivyogongesha mwamba jahazi lao. (alama 14)
      1. Wanashiriki ubakaji – kundi la mabarobaro watano linawabaka Lime na Mwanaheri baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka.
      2. Wanashirikishwa katika ulanguzi wa dawa za kulevya. Dick anatumiwa na Buda katika biashara ya kulangua dawa za kulevya.
      3. Kuwateka nyara watoto – Sauna anashiriki katika utekaji nyara wa watoto. Anawateka nyara Dick na Mwaliko.
      4. Kuwadanganya wapiga kura vikongwe. ‘Hitman’ anadai kuwa vijana wanashiriki katika njama za kifisadi za wanasiasa kuwadanganya maajuza kuwachagua viongozi fulani.
      5. Vijana wanawapiga na kuumiza raia - Subira anajeruhiwa na vijana waliomvamia wakati wa mizozo ya baada ya uchaguzi.
      6. Kushiriki katika maandamano yanayosababisha vifo vya baadhi yao. Baadhi ya vijana wanaoandamana wanauawa na polisi kwa kupigwa risasi.
      7. Vijana wanasababisha matatizo ya kisaikolojia kwa raia. Kaizari anavunjika moyo baada ya kuona kundi la vijana likitendea unyama binti zake.
      8. Vijana kunywa pombe haramu. Baadhi ya vijana wanatumia vileo kwa sababu familia zao zimesambaratika. Kipanga anajiingiza katika unywaji baada ya aliyemdhani kuwa babake kumkana.
      9. Kuendeleza ukeketaji/ tohara kwa wasichana. Tuama anajificha kwenda kupashwa tohara licha ya pingamizi kutoka kwa babake, Mzeee Maarifa.
      10. Kuharibu mali - Vijana wanaoandama, kama yule aliye na shati lililoandikwa ‘Hitman’ anaonekana akirushia bomu la petrol magari.
      11. Wanashiriki mauaji – vijana kama yule mwenye shati lililoandikwa ‘Hitman’ wanashiriki katika mauaji ya raia kwa kuwarushia bomu ya petroli.
      12. Kuwanunua wapiga kura. Kijana mwenye shati lililoaandikwa ‘Hitman’ anasema kuwa, vijana wananunuliwa kwa vihela vidogo ili kuwapigia kura viongozi fulani.
      13. Kupuuza ushauri wa wazazi. Tindi anashiriki burudani ya densi na vinywaji wakati wa sherehe ya kukumbuka siku ya kuzaliwa kwa usiku wote hivyo kutorejea nyumbani mapema kama alivyoshauriwa na mamake.
      14. Kuapata mimba za mapema wangali shuleni. Zohali anashiriki mapenzi shule hali inayosababisha kupachikwa mimba akiwa kidato cha pili.
      15. Kujaribu kuavya mimba. Pete anajaribu kuavya mimba mara nne bila mafanikio. Alipopata mimba ya tatu anajaribu kujiua pamoja na kijusi tumboni mwake kwa kunywa sumu ya panya.
      16. Vijana wanashiriki ulaghai -Sauna anashiriki biashara ya kuwauzia watu maji ya mito wakiambiwa kuwa ni ‘mineral water’.
        Zozote 14 x 1 = 14

    2. Neno jahazi limetumika kitamathali. Onyesha jinsi tamathali hiyo ilivyotumika riwayani. (Lazima mtahiniwa atolee mfano kwenye riwaya baada ya kutoa ufafanuzi. Alama ni 1/0) (alama 6)
      1. Ni sitiari/jazanda
      2. Majabali ya maisha (uk.3) – kauli hii ni jazanda inayorejelea matatizo yanayoweza kumkumba mtu maishani. Kwa mfano, (atolee mfano)
      3. Ukoo ambao umezaa majoka ya midimu. Majoka ya midimu inarejelea Waombwe kwa sababu ya tabia yao ya kuwa wachoyo.
      4. Mtoto wa miaka hamsini asiyesota wala kupiga dede ni jazanda ya nchi zinazoendelea ambazo licha ya kupata uhuru wa bendera hawajajistawisha kiuchumi, kijamii na kisiasa. Halikadhalika, kutopiga dede inadhihirisha kuwa nchi hizi bado zinategemea nchi nyinginezo zilizoendelea ili kujistawisha.
      5. Itakuwa kukivika kichwa cha kuku kilemba (uk.18). Kauli hii inamaanisha kuwa mwanamke hawezi jukumu la kuongoza wanajamii.
      6. Kumbe machozi yenyewe ni ya mamba! (uk.22). Jazanda hii inarejelea unafiki wa viongozi wanaojifanya kuwajali vijana kumbe lengo lao ni kupata kura tu.
      7. Tulikuwa kuni kwenye uchaga (uk.25). Hii imetumiwa kumaanisha kuwa akina Kaizari wangefuata safu hiyo ya kuvamiwa na wengine wao kuuawa.
      8. Mara hii kama wapiga kura tumeamua kujaribu mbinu mpya za kilimo (uk.40). Mbinu mpya za kilimo ni kuchaguliwa kwa mwanamke (Mwekevu). Hii ni kwa sababu jamii ya Wahafidhina imekuwa ikiwachagua wanaume kama viongozi wao.
      9. Haya matumizi ya visagalima yameanza kupitwa na wakati (uk.40). Matumizi ya visagalima ni jazanda ya kuchaguliwa kwa watu kutokana na misingi yao ya kijinsia hasa kuwa, mwanamume.
      10. …atakayeweza kulielekeza jahazi hili letu kwenye visiwa vya hazina (uk.40) ‘Jahazi’ inarejelea nchi ya Wahafidhina na ‘visiwa vya hazina’ ni ufanisi wa kiuchumi.
      11. Hili ni wingu la kupita na bila shaka wingu la kupita halipaswi kumtia mkulima matumaini (uk.45). Wingu la kupita linarejelea uongozi wa Mwekevu, ambao kwa mujibu wa mpinzani wake haungedumu.
      12. Baada ya muda, lori lilivamiwa na nzige ambao hawakuwa na hadhari (uk.55). Nzige ni watu waliong’ang’ania mafuta kwenye lori lililobingirika.
      13. Ziliangukia masikio ya fisi (uk.55). Wanaochota mafuta wanarejelewa kama fisi kutokana na tamaa waliyokuwa nayo.
      14. Wanasema wajuao kuwa msitu ni mpya, ila nyani ni wale wale (uk.92). Msitu mpya unarejelea uongozi na nyani ni viongozi ambao hawajabadilika kihulka.
      15. Kwamba ndiye aliyewafanya majirani zetukutuchomea boma ili watuondolee gugu ambalo liliutia najisi utambulisho wetu (uk.94). Gugu limetumiwa kurejelea Subira mamake Mwanaheri kwa kuwa alitoka katika jamii tofauti na mumewe.
      16. Mwanangu jua langu li karibu kuchwa (uk.110). Jua imetumika kurejelea maisha ya Ridhaa. Hivyo, kuchwa kwa jua ni kufikia mwisho wa maisha yake.
        Zozote 6 x 1 = 6

  4.           
    1. Hili ni shairi la aina gani? Toa sababu. (alama 2)
      1. Ni tarbia (alama 1)
      2. Lina mishororo minne katika kila ubeti (alama 1)

    2. Eleza dhamira ya shairi hili. (alama 2)
      1. Kuwafunua macho vijana hasa wasichana kuhusu hatari zilizopo katika ujana
      2. Linalenga kuwatahadharisha wasichana dhidi ya hadaa kutoka kwa wanaume.(1x1=02)

    3. Bainsha mambo manne ambayo nafsineni anatoa kama ushauri kwa nafsinenewa.(alama 4)
      1. Akimbie anasa
      2. Asijitie maringo
      3. Asitungwe mimba
      4. Wanaume wakimwambia wanampenda awakimbie
      5. Asishiriki ngono
      6. Asizurure mtaani
      7. Akitoka nyumbani afululize
      8. Asitembee vichochoroni
      9. Ajiepushe na wanaume, ni mnyama (Za kwanza 4 x 1 = 4)

    4. Huku ukitoa mifano, bainisha vipengele vitatu vya kimtindo ambapo mshairi ametumia kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu. (alama 3)
      1. Jazanda/istiari – wanaume ni wanyama (afafanue)
      2. Balagha – nani akachovya uto, wa asali tamu vile
      3. Takriri - si watu waona vile, wanaume ni wanyama
      4. Nahau –umevunja ungo – umekomaa (Za kwanza 3 x 1 = 3)

    5. Tambua uhuru wa kishairi uliotumiwa kwa kurejelea mifano mitatu. (alama 3)
      1. Inkisari
        1. ngawa – ingawa
        2. Taonywa – utaonywa
        3. Mameyo – mama yako

      2. Tabdila –
        1. ukimbile – ukimbie
        2. Usikile – usikie
        3. Uzingatile – uzingatie

      3. Kubananga sarufi /kufinyanga sarufi/ miundo ngeu ya kisintaksia
        1. Ngoma ni tendo la suna, Amina sikimbilie – Amina sikimbilie ngono ni tendo la suna
        2. Kuzurura mitaani, si tabia njema ile – ile tabia ya kuzurura mitaani si njema
          (Za kwanza 3 x 1 = 3)

    6. Andika ubeti wa sita kwa lugha nathari. (alama 4)
      1. Uwe mwana anayesikia/ msikivu wa kuzingatia
      2. Mambo kuhusu mapenzi utaonywa shuleni
      3. Kama mama yako mzazi ninakuonya kimbele
      4. Ajihadhari na wanaume kwa sababu ni wanyama (Zozote 4 x 1 = 4)

    7. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)
      1. Mama yake mshauriwa kwa mfano, mamayo mzazi, nakuonya ukimbile

  5.                
    1. Lipe shairi hili kichwa mwafaka (alama 1)
      1. Mama nitarudi
      2. Nitarudi
      3. Kizuizini alama 1 (asizidishe maneno sita)

    2. Tambua nafsineni katika shairi hili (alama 1)
      1. Nafsineni ni aliye kizuizini. Anauliza iwapo mamake angali anasimama na kusubiri akitazama kule kizuizini aliko nafsineni (atambue na athibitishe alama 1/0)

    3. Eleza toni katika shairi hili (alama 1)
      1. Toni ya masikitiko / uchungu wa moyoni/huzuni kwa mfano, anasikitikia hali yake ya kuvaa matambara, njaa, kufanyiswha kazi tele
      2. Toni ya matumaini kwa mfano, mshairi ana matumaini kwamba siku moja atatoka kizuizini (atambue na athibitishe alama 1/0)

    4. Taja mambo manne ambayo mshairi analalamikia (alama 4)
      1. Kuachwa njaa
      2. Kufungwa
      3. Kufukuzwa
      4. Kutopewa nafasi ya kupumzika, kulala na kuwaza
      5. Kuvaa matambara
      6. Kufanyizwa kazi kama mnyama (Zozote 4 x 1 = 4)

    5. Fafanua dhamira katika shairi hili (alama 2)
      1. Mshairi anadhamiria kulalamikia/kukashifu namna anatumiwa vibaya kizuizini
      2. Mshairi anakashifu madhila na mateso ambayo wafungwa hutendewa
      3. Kumpa mamake matumaini kwamba atatoka kizuizini siku moja (Zozote 2 x 1 = 2)

    6. Thibitisha kuwa hili ni shairi huru (alama 4)
      1. Kuna matumizi ya mistari mishata
      2. Idadi ya mishororo inabadilikabadilika kutoka ubeti mmoja hadi nyingine
      3. Silabi za mwisho katika kila mshororo zinatofautiana
      4. Idadi ya mizani katika kila mshororo inatofautiana (Zozote 4 x 1 = 4)

    7. Taja na ufafanue sifa mbili za mshairi (alama 2)
      1. Ni mwenye kulalamika kwa mfano, analalamikia hali yake ya kuwa na njaa, kupigwa
      2. Mwenye matumaini kwa mfano, anatumai kuwa siku moja atatoka kizuizini
      3. Mwenye mapenzi kwa mfano, anampenda mamake na kumwita mama mpenzi
        (Zozote 2 x 2 = 4) kila sifa itolewe mfano - atuzwe 2/0

    8. Fafanua mbinu tatu za kimtindo zilizotumika katika ubeti wa tatu. (alama 3)
      1. Takriri kwa mfano, neno nitarudi limerudiwarudiwa
      2. Mdokezo kwa mfano, nitarudi mama mpenzi
      3. Tashibihi kwa mfano, kupitia mwingine kama shetani
      4. Balagha kwa mfano, Ni kosa gani lilotendeka - Liloniletea adhabu hii isomalizika? (Za kwanza 3 x 1 = 3)

    9. Eleza maana ya maneno yafuatoyo kama yalivyotumiwa katika shiari hili (alama 2)
      1. Hayawani - mnyama
      2. Nadhari - fikira
        (Za kwanza 2 x 1 = 1)
  6. Huwezi kuyang’amua kwa kuwa umeyafumbia macho. Hujaibambua ngozi yako ya zamani.
    Huwezi kuyang’amua kwa kuwa umeyafumbia macho. Hujaibambua ngozi yako ya zamani.
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      1. Haya ni maneno ya Babu
      2. Babu anazungumza na Majoka
      3. Majoka yumo katika chumba cha wagonjwa ambapo hali yake inaendelea kuimarika
      4. Babu anamsuta Majoka kuwa masaibu yanayompata ni ya kujitakia (atolee mfano)(zozote 4 ×1=04)

    2. Eleza mbinu za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 4)
      1. Nahau – umeyafumbia macho
      2. Jazanda – hujaibambua ngozi yako ya zamani – hujabadilika (afafanue)
      3. Ritifaa – Kuzungumza
        (zozote 2×2=04)

    3. Kwa kurejelea tamthilia nzima, thibitisha kuwa mzungumziwa hajaibambua ngozi yake ya zamani. Maovu yanayoendelezwa na Majoka (alama 12)
      1. Mauaji – Jabali
      2. Uharibifu wa mazingira – kuruhusu ukataji wa miti
      3. Tama ya mali – anataka kujenga hoteli ya kifahari katika Soko la Chapakazi
      4. Mwenye uchu – anataka kushiriki mapenzi na Ashua ofisini mwake
      5. Anawazuilia watu – Sudi amewahi kuzuiliwa. Ashua anazuiliwa bila hatia
      6. Anaendeleza mapendeleo – Asiya kupewa kandarasi ya kuoka keki
      7. Ukandamizaji wa vyombo vya habari – anafunga runinga ya mzalendo
      8. Mwenye dharau – andamdharau Tunu – kupendekeza aolewe na Ngao Junior
      9. Anaendeleza vitisho – anasema atashinda uchaguzi hata asipopigiwa kura
      10. Anaendeleza taasubi ya kiume – anamwambia Husda kuwa atamchafua akileta fujo.
      11. Anaendeleza unasaba – anataka kumrithisha mwanawe uongozi
      12. Anaendeleza ulaghai/hila – anaongeza mshahara kidogo na kuzidisha kodi.
        (Zozote 12 x 1 = 12)

  7.               
    1. Asasi ya ndoa imo hatarini katika jamii ya kisasa. Tetea kauli kwa mifano kumi katika tamthilia. (alama 10)
      1. Jicho la nje katika ndoa – Majoka amemwoa Husda lakini anamweleza Ashua kuwa anampenda
      2. Ushawishi – Ndoa inakabiliwa na ushawishi mwingi kwa mfano, Ashua anashawishika wakat Majoka anamweleza kuwa Sudi (mume wake) ni zebe.
      3. Ubinafsi/ tama – Husda anamwoa Majoka kwa sababu ya mali aliyokuwa nayo wala si mapenzi
      4. Ndoa za lazima – Mjoka anakubali kumwoa Husda ili kutimiza wajibu wake katika jamii kama kiongozi
      5. Kutowajibika – Ashua anamweleza Sudi kuwa mke ni matunzo
      6. Umaskini – Watoto wa Sudi na Ashua wanakosa chakula – Pili na Pendo
      7. Taasubi za kiume – Majoka anaagiza Chopi amtie HUsda mbaroni kwa dakika chache kisha amwachilie. Baadaye Majoka anamwamuru Husda aende nyumbani ampikie chapatti kwa kuku.
      8. Unafiki/ udanganyifu – Majoka anamweleza Husda kwamba ni chui ndani ya ngozi ya kondoo – alipenda mali ya Majoka bali si Majoka.
      9. Uasherati/ufuska – Asiya anashiriki amapenzi na Ngurumo ilia pate kandarasi ya kuoka keki
      10. Usaliti – Majoka anamsaliti Husda kwa kumweleza kwamba anampenda Ashua na anaweza hata kumfia.
        (Za kwanza 10 x 1 = 10)

    2. Eleza umuhimu wa Babu katika Tamthilia ya Kigogo. (alama 10)
      1. Babu anatiumiwa kuonyesha ukatili wa Majoka – Majoka ndiye aliyemuua Jabali.
      2. Babu anatumiwa kuendeleza maudhui ya uongozi bora – Babu anamhimiza Majoka kutenda wema, ajiepushe na dhuluma.
      3. Babu anatumika kuendeleza maudhui ya mabadiliko katika uongozi – anamweleza Majoka lazima hajabambua ngozi yake ya zamani
      4. Babu anatumiwa kufichua uozo Sagamoyo – anamweleza Majoka kuwa kisima kimeingiwa na paka na maji hayanyweki tena
      5. Anatumiwa kuonyesha changamoto katika uongozi- anamweleza Majoka kwamba lazima kiongozi awe na mpango na maono – safari ya kesho hupangwa leo.
      6. Anatumiwa kuonyesha athari za tamasha miongoni mwa viongozi – anamwelza atakayeruhusu kiu hiyo kumpinda ataingia kwenye mtego.
      7. Ametumiwa kuonyesha umuhimu wa ushirikiano katika uongozi- anasema mshumaa hauwezi kuisha moto unapowasha mwingine.
      8. Anatumiwa kuonyesha jinsi hekima humwezesha kiongozi kufanya chaguo la busara – anamweleza Majoka kuchagua sauti ya mtima bali si la sikio.
      9. Anatumika kusisitiza umuhimu wa uongozi bora katika jamii – anamweleza Majoka wema uwe taa miguuni na mwangaza kwa njia.
        (Zozote 10 x 1 = 10)

  8.      
    1. A. Chokocho: “Masharti ya Kisasa”
      “Mwanzoni bila ya shaka, mambo hayakufikia kiasi hicho. Pale alipokuwa kufa na kupona akimtafuta Kiadawa, alipokuwa kiguu na njia akimwinda kama kunguru mwerevu, moyoni mwake alidhani anafuata nyuki apate kula asali. Ajabu lakini, kwa nini misumari ya nyuki inamuuma sasa ila si wakti ule wa tama ya ushindi ilipokuwa mbali, mbingu na ardhi?”
      1. Bainisha vipengele vine vya kimtindo vilivyotumiwa kwenye dondoo. (alama 4)
        • Mbinu rejeshi- mambo hayakufikia kiasi hicho- anarejelea mamabo ambayao yalikwishafanyika awali.
        • Misemo- kufa kupona, kiguu na njia
        • Tashbihi- akimwinda kama kunguru mwerevu
        • Jazanda- nyuki na asali-ufanisi/mafanikio, Misumari ya nyuki (Kuathirika kwa masharti ya ndoa ya kisasa)
        • Tanakuzi- mbingu na ardhi
        • Balagha- kwa nini misumari ya nyuki inamuuma sasa ila si wakati ule wa tamaa ya ushindi ilipokuwa mbali, mbingu na ardhi?
        • Majazi – Kidawa- hii ni dawa ndogo (suluhu la muda mfupi tu)
          (Za kwanza 4x1=4)

      2. Onyesha jinsi mrejelewa alivyokuwa ameumwa na misumari ya nyuki. (alama 6)
        (Namna Dadi alivyokuwa ameathirika na masharti ya ndoa ya kisasa)
        • Dadi hafurahii kumwona mkewe akisimama njiani na kuzungumza na wanaume. Alihofia huenda wakamshawishi kimapenzi.
        • Kidawa kupenda kujipodoa, fasheni hii na ile ya mavazi haya na yale yanayoingia jijini.
        • Ingawa Kidawa alivalia buibui, hapendi kuziba uso wala kifua chake.
        • Ingawa Dadi anamsaidia Kidawa kazi za nyumbani, anasema yeye hatosheki – hataki kukubali kuwa mwanamume kazi zake ni za nje na sio za ndani.(uk.60)
        • Dadi hamtaki mkewe apite mtaani akitembeza bidhaa za kuuza kama vile kanzu, viatu na kanga kutoka uarabuni
        • Dadi hataki mkewe afanye umetroni usiku. Anasema usiku una giza na giza hufunika balaa. Kidawa hakataziki. (uk.61)
        • Dadi kulazimika kupanga uzazi- wana mtoto mmoja tu waliyepanga kuwa naye kwa uzazi wa kisasa.
        • Kila mara Kidawa alipokataa kufanya jambo humrejesha mumewe nyuma kwa maneno yaleyale yaliyoambatana na masharti ya ndoa ya kisasa- ikiwa angeyavunja basi na ndoa yao pia ingevunjika.
          (Zozote 6x1=6)

    2. A. Chokocho: “Tulipokutana Tena”
      “Mimi pia nilifurikwa na machozi lakini sikuyafuta. Nilibaki kushangazwa tu kusikia ukweli wenye makali yaliyochinja bila huruma”.
      Eleza kilichowaliza warejelewa katika dondoo hili. (alama 10)
      (Swali linalenga mateso ambayo Bogoa aliyapata kutoka kwa Bi. Sinai alipokuwa akiishi kwake kabla ya kutoroka - Mtahiniwa atolee mifano ndipo atuzwe)
      • Kulazimishwa kufanya kila kitu bila ya hiari yake
      • Kumtayarishia viungo vya upishi kama vile kumenya vitunguu maji, kumkatia shinyango za nyama, kumdondolea mchele n.k.
      • Kumchanjia kuni na kuchochea moto vyungu vilivyokuwa mekoni.
      • Kufagia nyumba na kufua nguo zote chafu.
      • Kuteka maji kisimani wakati yale ya bomba hayakuwepo.
      • Kuamka alfajiri kuchoma maandazii ya kuuza shuleni.
      • Kukoseshwa elimu na Bi. Sinai ili achuuze maandazi ilhali watoto wake walikuwa wakiendelea na elimu.
      • Hakupewa uhuru wa kucheza na watotoo wengine- alifanya hivyo kisiri tu.
      • Bogoa alipochelewa kurudi nyumbani, Bi. Sinai alimtafuta na kumpiga vibaya (uk. 116)
      • Bi. Sinai hakumpa Bogoa nafasi ya kuzungumza na wazazi wake walipokuja pale kwa Bi. Sinai
      • Bogoa kulazimika kula makoko na makombo kwenye sufuria huku wengine wakila kwenye sahani.Bi. Sinai kumtishia
      • Bogoa angemkata ulimi iwapo angeyasema yale aliyoyashuhudia pale kwake.Bi. Sinai kumchoma Bogoa kwa kijinga cha moto viganjani baada ya maandazi aliyokuwa akiyachoma kuungua.
        (Zozote 10x1=10)

  9. A. Abdulla Ali: “Ndoto ya Mashaka”
    Kwa nini matajiri wanazidi kutajirika na fukara wanazidi kufukarika na kudidimia?
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      • Haya ni maneno ya Mashaka.
      • Anakuwa akiyawaza maneno haya baada ya kutorokwa na mkewe.
      • Alikuwa kwenye chumba chake mtaa wa Tandale.
      • Alikuwa akiwazia namna kuna mwanya mkubwa kati ya watu wa tabaka la juu na tabaka la chini
        (Zozote 4 x 1 = 4)

    2. Fafanua umuhimu mnenaji (alama 3)
      • Kuendeleza maudhui ya uwajibikaji. Mlezi wake, Bi. Kidebe alipoanza kuugua alienda kutafuta vibarua vilivyowasaidia kujikimu kimaisha
      • Ananonyesha suala la umaskini. Anaishi maisha ya kimaskini kwenye mtaa duni wa Tandale. Hana godoro, meza wa kiti kwenye chumba chake.
      • Kuendeleza maudhui ya utu. Alipeleka nyumbani chochote alichopata kutoka vibaruani ili kimsaidie yeye pamoja na mlezi wake. Bi. Kidebe aliyekuwa mgonjwa
      • Anafunza mbinu-ishi kama vile bidii. Alishikiriana na Bi. Kidebe kulima vishamba vitatu walivyokuwa navyo. Walipanda mpunga, mihogo na migomba
      • Kuendeleza muadhui ya elimu. Amesoma hadi akamaliza chumba cha nane.

    3. Eleze maudhui yanayojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
      • Utabaka. Kuna tabaka la matajiri ambao wanaendelea kutajirika na kuna takaba la maskini ambao wanaendelea kumaskinika.

    4. Bainisha tamathali moja iliyotumika katika ndoo (alama.2)
      • Maswali balagha - Kwa nini matajiri wanazidi kutajirika na fukara wanazidi kufukarika na kudidimia (1 x 2= 2)

    5. Ufukara ni kikwazo kikubwa katika Maisha ya wananchi wa kawaida. Huku ukitoa hoja nane, tetea ukweli wa kauli hii ukirejelea Ndoto ya Mashaka. (alama 12)
      • Inawafanyu watu kukosa elimu. Mashaka anakosa elimu kutokana na umaskini. Anasoma tu hadi darasa la nane.
      • Ufukara unawafanya watukufanya kazi za vibarua. Mashaka anapobaleghe, anafanya kazi za vibarua kama kufyeka, kufua nguo na kupiga pasi, kuchanga kuni na kuchuma karafuu ili kuakidhi mahitaji yao.
      • Ufukara unawafanya watu kulima vishamba vidogo. Kutokana na umaskini, Mashaka na Biti Kidebe wanapewa vishamba vitatu. Viwili wanapanda mpunga na kingine wanalima mihogo na migomba.
      • Ufukara unafanya watu kufa kutokana na maradhi.Biti Kidebe analalamika kuumwa na miguu. Anasema kuwa ataingia kaburini na hiyo miguu. Anakosa pesa za kutafuta matibabu. Hatimaye anaaga dunia.
      • Ufukara unawafanya watu kuishi kwenye vyumba vidogo. Mashaka na Waridi na watoto wao wanaishi kwenye chumba kimoja kidogo. Chumba chenyewe kinakuwa hakiwatoshi.
      • Ufukara unawafanya watu kuishi kwenye nyumba zinazofuja. Mashaka na jamaa yake pamoja na wasak:atongewanaishi kwenye nyumba ambazo mvua inanyesha ndani kule
      • Tandale. Anasema kuwa mvua iliponyesha, wanatembeatembea vyumbani kuepuk matoneya mvua.
      • Ufukara unawafanya watoto wa watu kulala jikoni.Kutokana na umaskini, Mashaka analazimikakumwomba Chakupewa awaruhusu wanawe walale jikoni kwake. Anasem kuwa walilala huko kama nyau.
      • Ufukara unawafanya watu kukosa vyoo. Katika mtaa wa Tandale watu hawana vyakula Wanakwenda haja zote kubwa na ndogo kwenye karatasi na kuzitupa.
      • Ufukara unawafanya watu kuishi kwenye nyumba duni. Nyumba ambazo watn wanaishi kule Tandale hazijafuata utaratibu wa ujenzi. Eneo hilo linakuwa halijapimwa na Mipango Miji. Nyumba zenyewe zinapakana na vyoo na mitaro ya maji machafu.
      • Ufukara unawafanya watu ku/anya kazi duni zenye mishahara duni. Mashaka anafanya kazi duni ya ulinzi katika kampuni ya Zuia Wizi Security. Katika kazi hii, anasema mshahara wake ni mkia wa mbuzi. Kumaanisha ni mdogo sana.
      • Ufukara unafanya watu washindwe kumudu vitu muhimu vya nyumbani. Nyumba wanamoishi Mashaka na jamaa yake haina vitu vingi. Wanakosa pesa za kuvinunulia na mahali pa kiviweka. Wanakosa godoro, meza na hata kitanda.
      • Ufuukara unasabaisha kuvunjika kwa ndoa. Waridi anaposhindwa kuvumilia umaskini wa Mashaka, anaamua kutorokea kwa wazazi wake kule Yemeni pamoja na watoto wake.
      • Ufukaraunawa/anya watu kuishi katika mazingira duni. Mzingira ambamo Watandale wanaishi ni mabaya mno. Kuna mitaro ya maji chafu iliyopita karibu na nyumba hizo. Aidha kuna uvundo unaotokana na hayo maji machafu.
        (Za kwanza 10 x 1 = 10)

 

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mokasa II Mock Examination 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest