Ushairi Simulizi - Tanzu za Fasihi Simulizi Kiswahili Notes

Share via Whatsapp


Utangulizi

 • Ushairi simulizi ni utanzu unaojumuisha tungo zote zenye mapigo ya kimuziki, mawazo, hisia na hoja.
 • Utanzu huu huwasilishwa kwa njia ya mdomo kutumia lugha ya mkato yenye mpangilio maalumu wa maneno katika mishororo.
 • Ushairi simulizi huimbwa, hughaniwa au hukaririwa ni muhimu kutaja hapa kuwa ushairi simulizi hutofautiana na mashairi ambayo huandikwa kwa lengo la kuwasilisha mbele ya hadhiri katika mashindano ya tamasha za muziki au yanayowasilishwa katika hasia maalumu.


Sifa za Ushairi Simulizi

 1. Ushairi simulizi huwasilishwa kwa njia ya mdomo mbele ya hadhira kwa kukaririwa, kughanwa au kuimbwa. Nyimbo kwa mfano huimbiwa watu hata hivyo, baadhi ya mashairi huimbwa na watu bila kuhusisha hadhira nyimbo za kazi mara nyingi hazina hadhira.
 2.  Hubuniwa papo hapo na kuwasilishwa kwa hadhira au tungo za awali huwasilishwa kutoka kwa kumbukumbu za mwasilishaji.
 3.  Tungo za mashari simulizi hutolewa zikiambatana na ala za muziki, uimbaji wa nyimbo huambatana na ala kama njuga na marimba aidha anayejigamba huweza kutumia ala kama vile mkuki anapojigamba.
 4.  Ushairi simulizi ni sehemu ya utamaduni wa jamii na hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, nyimbo za jandoni (nyiso) na tendi, kwa mfano hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
 5.  Ushairi simulizi hutumia lugha yenye mvuto mkubwa, yenye mapigo yaliyopangwa kwa muwala na urari.
 6.  Utungo wa ushairi simulizi huweza kuwasilishwa na mtu mmoja kama ilivyo katika majigambo au kundi la watu kama vile nyimbo nyingi na ngonjera.
 7.  Ushairi simulizi hubadilika kulingana na anayeuwasilisha, hadhira na wakati.Wimbo mmoja unaweza kuimbwa kwa mahadhi mbalimbali kulingana na mwimbaji, mwasilishaji anaweza kubadilisha wimbo au shairi wakati wa kuimba, kukariri au kughani kutegemea hadhira yake.
 8. Hadhira huweza kushiriki katika uwasilishaji wa mashairi simulizi, mwimbaji, kwa mfano, anaweza kuishirikisha hadhira yake katika uimbaji kwa kupiga makofi.
 9.  Uwasilishaji wa mashairi simulizi, kwa kawaida huandamana na uigizaji. Mwimbaji kwa mfano huambatanisha maneno yake na vitendo kama vile ishara za uso, ishara za mkono, miondoko mbalimbali na upigaji makofi.
 10.  Ushairi simulizi hufungamana na shughuli au muktadha maalumu mathalani nyimbo hufungamana na shughuli tofauti tofauti kama vile:
  1.  Hodiya-nyimbo za kazi.
  2. Kimai-nyimbo za uvuvi na shuguli za majini.
  3. Mbolezi-nyimbo za kuomboleza/matanga.
  4. Wawe-nyimbo za kilimo.
 11. Ushairi simulizi una miundo mbalimbali, unaweza kuwa na beti zilizo na kibwagizo kila ubeti unaweza kuwa na idadi tofauti tofauti za mishororo, kama vile 2,3,4,5,6,7 na zaidi.
 12.  Ushairi simulizi unaweza kuwa na urari wa vina na mizani au ukakosa kuwa nao, kilicho muhimu zaidi ni mapigo ya muziki yanayofanya utungo huo uweze kuimbika.
 13.  Ushairi simulizi, kama tanzu nyingine za fasihi simulizi hutumia lugha ya kitamathali, kunaweza kuwa na misemo, nahau, methali, ishara, taswira, jazanda na istiara.


Uainishaji wa Ushairi Simulizi

- Mashairi simulizi yanaweza kuainishwa kwa kutumia vigezo mbalimbali kam vile.

 1.  Maudhui
  1. Mapenzi-hupitisha jumbe za mapenzi.
  2. Kutuliza-kuna nyimbo za bembea au bembelezi zinazowatuliza watoto.
  3. Kuomboleza-mbolezi huimbwa wakati wa msiba.
  4. Kusifu-sifa huimbwa kujisifu mashujaa au waliofaidi umma na kustahili kutambuliwa.
  5. Siasa-nyimbo za siasa huwasilisha jumbe za kisiasa.
 2. Muktadha au mahali pa uwasilishaji
  1. Nyiso-nyimbo za jandoni.
  2.  Mbolezi-zinazoimbwa kwenye mazishi au kwenye maombolezi.
  3. Nyimbo za harusi.
  4.  Nyimbo za matambikoni ambazo hutolewa wakati wa kutoa kafara au sadaka kwa mizimu, labda baada ya janga.
  5.  Nyimbo za kazi.
 3. Mtindo wa uwasilishaji
  1. Maghani hutolewa kwa kalima bila kuimbwa.
  2.  Nyimbo huwasilishwa kwa mahadhi ya kupanda na kushuka.
  3. Shairi utungo unaokaririwa.
  4.  Tendi au Rara husimuliwa kwa mapigo ya kishairi.
  5.  Ngonjera huwasilishwa kwa kujibizana.
 4.  Mwasilishaji
  1.  Majigambo huwasilishwa na anayejigamba
  2.  Kwaya - uimbaji wa watu wengi


Umuhimu wa Ushairi Simulizi

 • Ushairi simulizi kama kipengele cha fasihi simulizi una umuhimu wa kijumla licha ya kuwa kuna vitanzu mbalimbali vinavyotekeleza majukumu tofauti.
 • Majukumu ya ushairi simulizi hutofautiana kutoka jamii hadi jamii, hata hivyo kuna majukumu ya kijumla kama vile
  1.  Ushairi simulizi hutumiwa kupitisha maarifa au mafunzo ya jamii fulani nyimbo za jandoni, za harusi na dini hutumiwa kupitisha mafunzo maalumu.
  2.  Ni nyenzo ya kuhifadhi na kupitisha utamaduni na historia ya jamii kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa mfano, tendi zinazosifu mashujaa huendeleza historia ya jamii hiyo kwa kuonyesha matukio kama vile nyimbo za jandoni (nyiso) husawiri utamaduni wa jamii kuhusu jando na kuuhifadhi.
  3.  Hukashifu tabia hasi kwa nia ya kuhimiza urekebishaji wa tabia hizo nyiso kwa mfano, hukashifu woga, hivyo vijana waoga huhimizwa kujirekebisha. Maghani na nyimbo za kisiasa hukashifu tawala dhalimu.
  4.  Ni nyenzo kuu ya kukuza umoja na uzalendo miongoni mwa wanajamii kupitia kwa nyimbo zinazosifu mashujaa wa vita, huhimiza vijana kuzionea fahari jamii zao na kujitoa mhanga kuzitumikia aidha wanajamii wanapojumuika pamoja kuimba au kughani katika hafla fulani, hujihisi kuwa kitu kimoja, hivyo uzalendo hujengeka.
  5.  Ni nyenzo ya kutakakasa hisia kupitia kwa mashairi au nyimbo, watu hutoa hisia za moyoni na kutakaza nyoyo zao mfano mwafaka ni nyimbo na mashairi ya mapenzi ambayo kwayo mtu humtolea mpenzi wake hisia. Rara pia hutumiwa kutekeleza jukumu hili.
  6.  Huelimisha, hukosoa na kurekebisha jamii nyimbo hutoa maadili ya kuonya na kuelimisha wanajamii nyimbo au mashairi ya sifa, tendi hata mbolezi huonyesha matendo mazuri ya anayeimbiwa na kukashifu wanaoenda kinyume na matakwa ya jamii.
  7. Husawiri mfumo wa jamii fulani kisiasa, kiuchumi na kijamii baadhi ya nyimbo huonyesha shughuli za kiuchumi za jamii kama vile ufugaji. Hodiya (nyimbo za kazi) huonyesha shughuli mbalimbali kama vile uwindaji, kilimona uvuvi. Majigambo pia husawiri mifumo ya jamii kisiasa na kijamii.
  8.  Huonyesha falsafa na imani za jamii husika kuhusu masuala fulani. Mbolezi huonyesha imani za jamii kuhusiana na kifo. Majigambo husawiri falsafa ya jamii kuhusu ushujaa.
  9.  Ni nyenzo kuu ya kuhamasisha wanajamii. Nyimbo za kisiasa na kizalendo zimetumiwa na tawala kama nyenzo ya kueneza propaganda za kisiasa.
  10.  Hukuza ubunifu anayekariri, huimba au kughani mashairi huhitajika kubuni mbinu zifaazo za uwasilishaji. Kwa kufanya hivi, uwezo wake wa kubuni hukuzwa.
  11.  Hukuza usanii wa lugha wanaotunga na kuimba mashairi huhitajika kubuni mbinu zifaazo za uwasilishaji kwa kufanya hivi, uwezo wake wa kubuni hukuzwa.
  12.  Husaidia wanajamii kukabiliana na hali ngumu na kuwahimiza wasikate tama kwa mfano mbolezi husawiri na kusawiri kifo kama faradhi kwamba humfika yeyote, hivyo hisia za mwemeo hupungua aidha nyimbo huhimiza waliokwenda vitani au wanaofanya kazi wasikate tamaa.
  13. Ushairi simulizi hustarehesha na kufurahisha wanajamii tungo za ushairi simulizi huvutia hisia, huburudisha na kusisimua mwili na akili.


Vipera vya Ushairi Simulizi

 • Ushairi simulizi una vipera vitatu:
  • Nyimbo
  • Maghani
  • Ngonjera
  • Mashairi Mepesi

Nyimbo

 • Nyimbo ni tungo za kishairi zenye mahadhi ya kupanda na kushuka kwa sauti, muwala na mapigo ya kimuziki na huwasilishwa kwa kuimbwa, nyimbo hutambuliwa kwa sifa tatu;
  1.  Huwepo kwa hadhira inayotumbuizwa
  2.  Muziki unaoimbwa kwa sauti
  3.  Matumizi ya ala

Sifa za Nyimbo

 1. Sifa bainifu ya nyimbo ni kwamba hutolewa kwa mahadhi ya kupanda na kushuka kwa sauti.
 2.  Nyimbo hutumia lugha ya mkato yenye mpangilio maalumu wa silabi, mishororo na beti zenye mapigo ya kimuziki.
 3.  Nyimbo hutumia lugha nzito yenye kuibua taswira na hisia nzito kama za mapenzi, huzuni na furaha.
 4.  Nyimbo zinapoimbwa, maana nyingi huandamana na ala za muziki kama vile ngoma, baragumu, msewe na zumari.
 5.  Katika jamii za kiafrika, nyimbo hufungamana na muktadha fulani kuna nyimbo za kazi harusi jando na unyago kuzaliwa kwa mtoto, kumpa mtoto jina, ibada na matambiko.
 6.  Baadhi ya vifungu katika nyimbo hurudiwarundiwa vifungu hivi huitwa vibwagizo, viitikio au mikarara ya nyimbo.
 7.  Nyimbo nyingi huandamana na ucheshaji wa viungo kama vile mabega kupiga makofi na mapigo ya miguu.
 8.  Kimsingi, nyimbo ziliimbwa na makundi ya watu kwa hadhira hai. Hata hivyo, kuna nyimbo zinazoimbwa na mtu mmoja kwa hadhira yake au hata bila hadhira.

Umuhimu wa  Nyimbo

 1. Nyimbo hutambulisha jamii kwa kusawiri shughuli na maisha ya jamii iliyozibuni mathalan nyimbo katika jamii ya wakulima zitasheheni msamiati unaohusu shughuli za kilimo kama vile kuvuna, kupanda na kupalilia.
 2.  Nyimbo humwezesha binadamu kutakasa hisia zake kupitia kwa nyimbo, binadamu hutoa hisia za moyoni kama vile kujutia kosa alilofanya, mapenzi ama huzuni. Mbolezi humsaidia aliyehathiriwa kutoa hisia za huzuni. Nyimbo za mapenzi kama vile chombezi, humwezesha mpenzi kumfichulia mwenzake hisia za moyoni.
 3.  Ni mbinu mojawapo ya kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii rekodi za matukio muhimu katika jamii huweza kuhifadhiwa kwa nyimbo na kupitishwa kwa vizazi.
 4.  Nyimbo hutumbuiza hutumiwa kama burudani, kufurahisha, kustarehesha na kusisimua.
 5.  Hupitisha amali na mambo ambayo jamii inayothamini, amali hizo hurekodiwa katika nyimbo mbalimbali kama vile za kazi na kurithishwa vizazi vya jamii hiyo. Mawaidha na thamani za jamii hukaririwa katika nyimbo kama nyenzo za kuzirithisha.
 6. Nyimbo hutumiwa kuhamasisha watu na kuchochea hisia za kuchangamkia jambo fulani. Nyimbo za kisiasa, kwa mfano huweza kuchochea hisia za kuungana pamoja kutetea haki au kuunga mkono jambo fulani.
 7.  Nyimbo huakisi ukwasi wa tamaduni za jamii umbuji (ufasaha wa kujieleza) na ujamii (mvuto na uzuri wa kazi ya sanaa) wa jamii hujitokeza katika nyimbo huteuzi wa maneno,ishara na ujumbe katika nyimbo huonyesha ukwasi wa jamii hiyo kifani.
 8.  Hukuza ubunifu miongoni mwa wanajamii, uimbaji ni kipawa na nyimbo hupalilia kipawa hiki.

Aina Mbalimbali za Nyimbo

Bembelezi /bembea/bembe/pembezeji

 •  Hizi ni nyimbo zinazowafanya watoto walale au watulie wanapolia, zinapoimbwa.
   

Sifa

 •  Bembea huimbwa kwa utaatibu kwa sauti na mahadhi ya chini.
 •  Huimbwa na wazazi au walezi wa watoto kuwaliwaza na kuwabembeleza watoto walale.
 •  Huwa fupi.
 •  Bembea hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine kutokana na thamani za jamii hiyo.
 •  Huimbwa kwa kurudiarudia maneno au kibwagizo wakati mwingine hata nyimbo mzima huimbwa kwa kurudiwarudiwa.
 •  Hutumia lugha shawishi na wakati mwingine hutolewa ahadi za kumnunulia mtoto zawadi.
 •  Aghalabu zinapoimbwa, mtoto huwa amebebwa kwa mbeleko na mwimbaji kutoa mapigo ya kumpapasa.
   

Umuhimu

 •  Hutumbuiza na kuongoa watoto, bembea hupumbaza na kumfanya mtoto anyamaze au alale anapolia
 •  Hutumiwa kama sifa kumsifu mtoto mtulivu, husifu pia somo ya mtoto huyo au wazazi wake.
 •  Husawiri mfumo wa kiuchumi wa jamii husika, ikiwa baba ni msasi, mtoto atarajiwa kuwa baba ni msasi jasiri au baba yake yuko karibu kutoka usasini.
 •  Huonyesha au kusawiri uhusiano katika jamii kupitia bembea, mlezi huweza kuibua migogoro iliyomo kati yake na wazazi wake au wazazi wa mtoto, hivyo kuonyesha uhusiano kati ya waajiri na wajiriwa.
 •  Hutakasa hisia ambazo mwimbaji huweza kuwa nazo
 •  Humwelimisha mtoto, hata katika umri huu mchanga, kuhusu mambo na shughuli mbalimbali katika jamii na umuhimu wake au thamani yake katika jamii.
 •  Husawiri falsafa au mtazamo wa jamii kuhusu jinsia na matarajio ya jamii kwa jinsia Fulani katika bembea, mlezi anaweza kutaja kuwa machozi ni ya kike iwapo anamtuliza mtoto mwanaume, majukumu ya mtoto wa kiume kwa jamii pia huweza kutajwa mlezi huweza kumtajia mtoto wa kike kuwa anatarajiwa kuwa mlezi mwema.
 •  Huwaonya watoto dhidi ya tabia hasi. watoto huonywa dhidi ya kulia onyo kwani kulia hukumbusha mtu mambo mabaya.
   

Mfano

Ewe malaika wangu
Uloshuka toka mbinguni
Mbingu kapasua kwa hei
Siku nipokukopoa
Ulinitia furaha iliyopasua kifua
Tabasamu kipajini pako
Ilinitia tumaini, ikanisahaulisha zingizi
Ikayeyusha madhila, ya utasa wa miaka kumi
Ikapeperusha mbali cheka la ukwenza.
Sasa napolia, wanitonesha jeraha
Waniregesha misri, kwa vitimbi vya firauni
Kwa vitisho vya muhebi
Talaka huahidiwa, hadi mbingu.
Lipofungua milango ya heri,
Silie mwana silie, walimwengu watakusuta.
Tangu hapo tanabahi
Vidume humu mwenu
Kulia hari kuumbiwa
Machozi na kekevu ni za kike fahamu
Jogoo halii, daima huwika
Nikikuona kigugumika hivi wanitia hangaiko
Tumaini kuzima
Udhaifu kiandama, moyo kitia hamaniko
Atanipigania nani
Watesi king’anga’ania chake kujitwalia?

Zoezi

 1.   
  1. Je, mtoto huyu ni wa kike au kiume?
  2. Thibitisha
 2.  
  1. Mwimbaji ni nani au ana uhusiano gani na anayeimbiwa?
  2. Thibitisha.
 3.  Andika sifa tatu za jamii ya mwimbaji
 4.  Andika mbinu za lugha zilizotumiwa
 5.  Andika majukumu sita ya wimbo wa aina hii.
  • Hutumbuiza watoto na kuwaongoa
  • Hutumika kumsifu mtoto mtulivu
  • Husawiri mfumo wa kiuchumi wa jamii husika
  • Husawiri uhusiano katika jamii kupitia migogoro
  • Hutakasa hisia ambazo mwimbaji huweza kuwa nazo
  • Huwaonya watoto dhidi ya tabia hasi.

Mbolezi /nyimbo za matanga/tahalili

 •  Hizi ni nyimbo ambazo huimbwa wakati mtu amefariki au wakati wa maafa ama katika halfa za kuadhibisha makumbusho.

Sifa

 1.  Mbolezi hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine kutegemea imani ya jamii kuhusu kifo na pia kulingana na aliyekufa.
 2.  Huimbwa kwa njia ya kuwafariji waliofiwa
 3.  Husifu aliyekufa kwa kawaida mbolezi hutoa sifa chanya au nzuri za aliyekufa watu mashuhuri katika jamii huweza kutungiwa mbolezi zao mahususi zinazowasifu na kutuja michango yao kwa jamii.
 4.  Hufungamana na muktadha maalum, mbolezi huimbwa tu katika matanga au wakati wa kuomboleza jambo fulani.
 5.  Huimbwa kwa toni ya huzuni na pengine uchungu ili kuibua hisia za ndani za mwombolezaji.
 6.  Huimbwa kwa mwendo wa utaratibu.
 7.  Huonyesha imani ya jamii husika kuhusu kifo.

Majukumu

 1. Husawiri msimamo wa jamii kuhusu kifo wapo wanaoamini kuwa kifo husababishwa na maovu au pepo fulani na watakao kashifu kifo, watu wengine hutambua kifo kama mlango wa kuingia katika uzima wa milele (kidini)
 2.  Kuwaliwaza waliofiwa, na kuwasaidia kukabiliana na uchungu au uzito wa kumpoteza mpendwa wao.
 3.  Hutoa wasifu wa aliyekufa
 4.  Ni njia ya kutakasa moyo na hisia za aliyefiwa, aliyefiwa huweza kutumia mbolezi kutoa hisia zake za huzuni kwa njia hii, anaweza kupunguza uzito wa kumpoteza mwenzake.

Mfano

“Kama kesho itapambauka
Jua la kinjano kuchomoza
Kuangazia siku mpya
Siku isio tumaini
Siku bila mimi mama mtu.
Kumbuka ewe kipenzi
Usiache chozi kufurika
Kuyeyusha makini yako inuka, mwanangu inuka
Silie daima, yote yatatengenea’’
Mpenzi mama ulolala usingizi usio na mzindushi
Nalikumbuka vyema hili ni beti uloniandikia
Kitandani ukiwa, ukiuguza donda.
Donda walokusababisha walimwengu mahasidi
Ela nataka ujue, kamwe yote si shwari kama uliponambia
Hayawezi kuwa shwari kwa mlezi kikembe
Hayawezi tengea kwa yatima alozungukwa
Na waja wenye tama kila kitu kurithi,
Hayawezi kuwa shwari kumtazama mwezio,
Ulotwambia tumwite baba na kumstahi,
Ati ni amri ya muumba
Akitoka na muhebi, pumbao apata yeye
Wafurahia ulochuma wewe.
Najitahidi mpenzi mama
Ukakamavu kujipa
Machozi kuyafuta
Ela hino kumbuka
Kuondoka kwako huko
Hatukukutarajia japo hukuisha kunikumbusha
Ziraili liingia ja mwewe
Na kukwiba mithili ya kifaranga
Mama yake akitazama.

MASWALI

 1.   Andika sifa za mbolezi zinazojitokeza
  • Huimbwa kwa toni ya huzuni na uchungu kwani anayeimba ana huzuni kwani amempoteza mama.
  • Inadhihirisha imani ya jamii inatajwa kuwa ziraili alimwiba mama
 2.  Andika mbinu zilizotumiwa
  •  Tashbihi-ziraili liingia ja mwewe
  •  Inksari-walokusababishia.

Nyiso

 •  Nyiso n nyimbo zinazoimbwa jandoni(wavulana ) na unyagoni (kwa wasichana ) kila jamii hata hivyo ina desturi zake zinazozingatiwa kama kigezo cha kuvusha vijana kutoka utotoni na kuingia utu uzima.

Sifa

 1. Zilitoa sifa kwa waliotiwa jandoni (waliopashwa tohara) wazazi na wasimamizi wao.
 2.  Ziliimbwa kuwapa wavulana ujasiri wa kukabili kisu cha ngariba
 3.  Zinatoa mafunzo kwa wavulana kuhusu majukumu yao mapya baada ya kutiwa jandoni.
 4.  Katika baadhi ya jamii, nyiso huimbwa usiku wa kuamkia siku ya kupasha tohara
 5.  Maudhui katika nyiso hutofautiana kutoka jamii hadi nyingine.
 6.  Maudhui yanaweza kuwa ya kuonya dhidi ya kutoa siri, kuwaandaa kwa uchungu watakaohisi au kukejeli woga.

Majukumu

 1.  Hutumika kuwaondoa kihisia wanaotarajia wanaotahiriwa kuwapa ari ya kuwapa kisu cha ngariba
 2.  Huwajuza wanaotahiriwa kuhusu majukumu mapya na matarajio ya jamii yao kwao, huwafahamisha kuwa wamevuka na ni muhimu kuwaandaa kiakili kwa majukumu ya utu uzima
 3.  Huonyesha furaha ya vijana wanaotoka katika utoto na kuingia utu uzima.
 4.  Huhimiza ujasiri na kukebehi woga.
 5.  Huhimiza uzalendo na kuonea fahari utamaduni wa jamii, wanaohiriki jandoni hujitambulisha na jamii zao zaidi na hivyo uzalendo huimarika.
 6. Nyiso hutoa nasaha kwa vijana, huwafahamisha kuhusu matarajio ya uchungu, matarajio ya utu uzima husa dhidi ya woga na umuhimu wa kuhifadhi siri watakazopewa.
 7.  Huburudisha waliohudhuria shughuli hii.
 8.  Huleta umoja miongoni mwa wanajamii, vijana waliotahiriwa wakati mmoja hujitambulisha kama ndugu.

Mfano

Ewe kiii
Ulozowea kujificha
Nyuma ya mama kujikinga, dhidi ya milio
Ya radii ilo juu mbinguni
Jua kesho ni siku ya siku
Siku ya kujua mbichi na mbivu
Kutofautisha jogoo na vipora
Ngaribu taposhika, chake kijembe
Ndipo utakapojua bayani
Ukoo wetu si wa kunguru
Ikiwa u tayari
Kisu kukidhihaki
Si thubutu kamwe, wanjani kuingia
Ije kuniabisha miye, amiyo na akraba nzima.

Nyimbo za kisiasa

 •  Hizi ni nyimbo ambazo huimbwa katika shuguli au miktadha ya kisiasa.nyimbo za kisiasa huwa na maudhui mapana kama vile mapambano, propaganda, kuzindua, kuhamasisha, kukejeli, kuburudisha, kuhimiza au kutia ari.

Sifa

 1.  Huwa na maudhui mapana kama vile mapambano, propaganda n.k
 2.  Huimbwa katika shughuli au miktadha ya kisiasa.
 3.  Huonyesha hali ya mwenye nguvu kumwonea mnyonge.
 4.  Huburudisha hutumbuiza na kustarehesha watu katika shughuli za kisiasa au za kitaifa.
 5.  Hutumiwa kuwatuliza na kuliwaza wahasiriwa wa migogoro ya kisiasa.

Jukumu

 1.  Hukuza umoja wa kisisa miongoni mwa washiriki .wakati wa kupigania uhuru, nyimbo hizi zilitumiwa kama nyenzo za kuwaunganisha watu.
 2.  Huzindua na kuhamasisha watu, huwapa watu k.m wafanyi kazi, ari ya kupigania haki zao. Nyimbo za kisiasa huwatanabahisha watu kuhusu haki zao na kuwahimiza kupigana dhidi ya unyanyasaji.
 3.  Husawiri mfumo wa kisiasa na kijamii wa jamii husika na maoni ya wananchi kuhusu mfumo huo. Je, wanaupenda au wanaupinga?
 4.  Husawiri migogoro iliyopo katika jamii, je ni ya unyanyasaji, uongozi mbaya, unyonyaji, ubinafsi, usawa na uhuru?
 5.  Hutumiwa kueneza propaganda za kisiasa, baadhi ya nyimbo za kisiasa huimbwa ili kusawiri uzuri wa utawala fulani.k.m KANU yajenga nchi, ni wimbo wa kisiasa ulionuia kuwavutia watu kukipenda chama hiki cha kisiasa.
 6.  Huimiza uzalendo na mshikamano wa kitaifa, nyimbo za taifa ni mfano wa nyimbo za kisiasa zinazohimiza raia kuionea fahari nchi yake na kuishi kwa undugu.
 7.  Huweza kutumiwa kama rekodi ya matukio ya kihistoria katika jamii Fulani, baadhi ya nyimbo za kisiasa huzungumzia mapambano dhidi ya ukoloni na historia ya mapambano hayo.
 8.  Hutumiwa kukashifu uongozi mbaya.
 9.  Hutumiwa kama sifo kuwasifia viongozi waadilifu na mashujaa wengine wa kisiasa kama vile Harry thuku,Dedan kimathi, Arap moi, Jaramogi Odinga, Kenyatta wa nchini Kenya
 10.  Huburudisha, hutumbuiza na kustarehesha watu katika shughuli za kisiasa au za kitaifa.
 11.  Hutumiwa kuwaliwaza na kupoza waasiriwa wa migogoro ya kisiasa.

Mfano

Mabeberu watu wabaya
Walimfunga kombozi
Nia yao ikiwa moja
Kudidimiza jamii yetu
Katika lindi la istiimari
Ela hawakufua dafu
Mabarobaro waliingia msituni
Bunduki wakashika
Kupigana, kupigania ‘wiyathi’
Beberu lipoona
Vita vimechacha
Tama iliwatoka
Wakasalimu amri
Uhuru wakatoa
Hawakutoa kwa hiari
Hilo usisahau
Wazalendo walipigana
Kwa jino au ukucha
Uhuru tukapata
Kombozi akashika sukani

Nyimbo za sifa/sifo

 •  Nyimbo za sifa pia huitwa sifo.ni nyimbo ambazo hutoa sifa za mtu fulani, sifo husifu michango na mafanikio ya watu katika jamii ni muhimu kutaja kuwa nyiso, mbolezi na nyimbo za arusi hutumiwa kama sifo.

Sifa

 1.  Sifo husifu na kutukuza watu ambao wamefanya jambo fulani k.m husifu maarusi, waliohitimu jandoni, viongozi wa kisiasa, kiuchumi na kijamii, mbolezi na walioshinda mashindano ya michezo au wa kumiliki kitu, kipawa au hali fulani.
 2.  Sifo hutumia sitiari kwa usanifu mkubwa, huwalinganisha wanaosifiwa na wanyama ili kuonyesha sifa fulani k.m kiongozi anaweza kufananishwa na simba ili kuonyesha ujasiri
 3.  Sifo hutumiwa katika miktadha mbalimbali ya kijamii kama vile miviga.
 4.  Huimbwa kwenye jando kuwasiu mashujaa na kuwapongeza kwa kuingia katika utu uzima
 5.  Huimbwa kwenye mazishi kama taabili/taabini kuwasifu na kuwakumbusha waliokufa.
 6.  Huimbwa kwenye arusi kuwasifu maarusi.
 7.  Huimbwa katika sherehe za kutawazwa kwa viongozi au wafalme.
 8. Kuna sifo za kidini zinazomsifu Mungu au mitume kwa mfano kasida ya mzia zinamsifu mtume mohammed.
 9.  Sifo pia huweza kuimbwa na mtu au watu binasfi wakijisifu – majigambo au vivugo.
 10.  Sifo huasi au kuonyesha thamani ya jamii zinazothamini ujasiri wa kivita, nyingine nasaba tukufu, ufugaji wa mifugo wengi, kilimo au arusi.
 11.  Sifo hupiga chuku sifa za anayesifiwa.

Majukumu

 1.  Sifo husifu matendo ya viongozi au watu mashujaa katika jamii
 2.  Hutangaza mafanikio au mchango wa mtu au watu wanaosifiwa kwa jamii, anayeimba sifo hutaja mambo ambayo anayesifiwa alitenda au ametenda.
 3.  Hukuza uzalendo, sifo huwahimiza vijana kuiga matendo mazuri ya wanaosifiwa, kwa njia hii, watu hujifunza kuionea fahari jamii na kuwa tayari kuitolea mchango wao.
 4.  Kuweka kumbukumbu au rekodi ya matukio ya kihistoria, wimbo unaomsifu shujaa wa vita, k.m huonyesha vita alivyopigana, alipigana na nani na lini na mbona
 5.  Huonyesha msimamo na mitazamo ya jamii fulani kuhusu maswala mbalimbali, wimbo unaosifu uzalendo wa mtu fulani, vilevile unaweza kuonyesha chuki kwa usaliti.
 6.  Hutambua mchango wa watu mbalimbali kwa jamii, sifo hutaja majina ya wanaosifiwa kwa nia ya kutambua na kutambulisha juhudi zao
 7.  Huburudisha, sifo nyingi hutumbuiza, hutuliza na hupumbaza akili.

Nyimbo za kazi/hodiya

 •  Nyimbo za kazi pia huitwa hodiya, ni nyimbo zinazoimbwa na watu wanapofanya kazi huwa kama kihamasishaji kwa wanaoifanya kazi fulani au zinaonyesha mazingira yao ya kazi, hofu zao shida zao, matumaini na ndoto zao.

Sifa

 1.  Maneno ya nyimbo hizi huwa ni ya kuhimiza.
 2.  Urefu wake hutegemea kazi na vifungu fulani vinaweza kurudiwarudiwa.
 3. Mdudo hutegemea kazi inayofanywa, iwapo kazi itafanywa kwa utaratibu mdundo utafuata hali hiyo.
 4.  Huimbwa wakati watu wanapofanya kazi kila aina ya kazi ina hodiya yake, kwa mfano; wawe /vave ni nyimbo za wakulima. Kimai ni nyimbo zinazohusishwa na ubaharia.
 5.  Huimbwa na kundi la wafanyakazi au mtu mmoja wakati anapofanya kazi yake binafsi
 6.  Nyimbo hazihusishi ngoma kwa kuwa watu wote walishiriki kazi.

Majukumu

 1.  Huhimiza watu kutia bidii na kuendeleza kazi bila kufa moyo.
 2.  Hukashifu uvivu na utegemezi, baadhi ya nyimbo za kazi hukashifu wasiopenda kazi
 3. Hurahisisha kazi kwa kupunguza fikra za uchovu, watu wanapofanya kazi wakiimba kazi huonekana kuwa nyepesi na muda kupita kwa kasi.
 4.  Husawiri imani, mitazamo na thamani za jamii husika kuhusu kazi jamii inathamini kazi gani? Uzembe na bidii kazini huchukuliwaje? Kazi inapewa nafasi gani?
 5. Huonyesha changamoto ambayo wafanyakazi hukabiliana nayo katika kazi zao, je, wanahofia nini kazini? Wana matumaini gani katika kazi zao?
 6.  Hujenga ushirikiano, watu wanapoimba wanapofanya kazi pamoja hujenga ushirikiano; pia huhimizwa katika baadhi ya nyimbo za kazi.

Mfano

Viongozi walisema
Turudi mashambani
Makonde kushughulikia
Mimea kupalilia
Tutie ghera ndugu
Tujifunge masembo
Udongo tutifue
Samadi tutie
Magugu tung’oe
Kilimo tuimarishe
Pasiwe wa kutuvuta
Misri kuturudisha
Kwa pato la kufutia chozi
Ukame tatwandama
Mashamba tukiachilia
Mmomonyoko kuyatoa
Tutabaki mikunguni
Kutegemea wahisani.

Nyimbo za mapenzi

 •  Nyimbo hizi zinaimbwa kueleza hisia za mapenzi, zinasimamia maoni ya jamii kuhusu mapenzi mtu anaweza kumsifu mpenzi au kusikitika kwa kuachwa na mpenzi, nyimbo hizi huwa na maudhui ya mapenzi.

Sifa

 1.  Huelezwa kwa maneno matamu yenye hisia nzito.
 2.  Zinaweza kuwa sifa, yaani zikaimbwa kumsifu mpenzif fulani.
 3.  Huthibitisha mapenzi.
 4.  Huwa na maudhui mbalimbali kulingana na lengo la mwimbaji k.m
  1.  Kuonyesha kusalitiwa au wivu.
  2.  Kuomba uchumba.
  3.  Kumsifu mpenzi-husifu umbo au hulka yake.
  4.  Kutambua uhusiano mzuri na mwenziwe na kumbembeleza mpenzi.

Majukumu

 1.  Kusifu tabia au umbo la mpenzi, yaani hutaja tabia chanya na umbo zuri la mpenzi.
 2.  Kutakasa hisia za anayeimba, mwenye mapenzi huweza kutumia nyimbo kutoa hisia zake za huzuni, furaha au kupumbazika kwa kufanya hivi anaweza kupunguza uzito wa hisia alizonazo.
 3.  Huburudisha, nyimbo za mapenzi huburudisha anayezisikiza.
 4.  Hukuza ubunifu, nyimbo za mapenzi hubuniwa kwa ubingwa wa hali ya juu ili kuibua hisia za mapenzi, huzuni au huruma.
 5.  Ni nyenzo ya kupitisha maarifa au elimu, nyimbo za arusi hutumiwa kutoa mawaidha ya unyumba kwa maarusi wapya aidha matarajio ya jamii na majukumu yao mapya kama bibi na bwana hupitishwa kwa nyimbo.

Mfano

Tina analia tina analia
Chozi lausaliti undani wake
Undani ambao ameuficha kwa miaka na mikaka
Undani ambao japo anachelea kutangaza asije
Akaonekana apendaye chongo
Itabidi kuuto kuumwaga mtama
Na kiini chozi hili ni kwamba imewadia
Imewadia siku kanisani kwenda,
Kujitia pingu pingu za aushi

 

 

MASWALI

Jibu maswali yafuatayo ukirejelea wimbo huu

 1.  Ainisha utungo huu kimaudhui.
  •  Ukatili-bibi arusi anapoenda kufanya arusi, bwana arusi haonekani
  •  Mapenzi-mwanamke huyu anaonekana kuwa alimpenda sana mchumba wake.
  •  Usaliti-mchumba wa mwanamke huyu, tina anamsaliti kwa kukosa kuja arusini
 2.  kwa mujibu wa wimbo huu, jadili kwa mifano nafasi ya mwanaume katika jamii
  •  Msaliti-mchumba wa tina anamsaliti kwa kukosa kkufika pale katika arusi ili amwone tina
  •  Katili-pia anamwacha tina pale bila yakumwambia kuwa hangependa kumwoa.
 3.  Toa mifano ya tamathali za usemi zilizotumika
  •  Uradidi-tina analia, tina analia
  •  Methali-apendaye chongo…(huita kengeza )
  •  Nahau- kumwaga mtama.
 4. Fafanua umuhimu wa aina ya tungo hii katika jamii yako.
  •  Huthibitisha mapenzi baina ya watu Fulani
  •  Hutakaja hisia za anayeimba, baadaye anapunguza uzito wa hisia hizo
  •  Huburudisha wale wanaosikiliza
  •  Hukuza ubunifu kwa wanaobuni nyimbo hizo na kuziimba.

Nyimbo za watoto/chekechea

 •  Nyimbo za watoto pia huitwa nyimbo za chekechea

Sifa

 1.  Huimbwa na watoto wakati wa kucheza ili kuifanya michezo ipendeze,au wanapofanya shughuli zao za kitoto.
 2.  Huwa na matumizi ya takriri kwa kiasi kikubwa
 3.  Ni maarufu katika shule za malezi kama vile chekechea
 4.  Watoto hufunzwa na kuimba nyimbo hizi
 5.  Maudhui yake hutegemea aina ya mchezo na jamii husika
 6. Lugha yake ni sahili au nyepesi
 7.  Aghalabu huwa fupi
 8.  Huandamana na miondoko kwa kiasi kikubwa

Umuhimu

 1.  Hutumiwa kama burudani, ni nyenzo muhimu ya kujipumbaza na kupitisha wakati
 2.  Hukuza ubinifu miongoni mwa watoto hujifunza nyimbo zinazooana na michezo yao
 3. Hukashifu tabia hasi, watoto hutumia nyimbo hizi kuwakashifu walio na tabia hasi k.v uchoyo.
 4.  Hukuza utangamano, watoto wanapokuja pamoja kucheza na kuimba, hawajali tofauti zao za kinasaba na huwa kama watu wa jamii moja.
 5.  Hutambulisha jamii, kila jamii ina nyimbo za watoto ambazo hufungamana na utamaduni pamoja na thamani za jamii hiyo.
 6.  Hukuza kumbukumbu za watoto, kwa sababu ya kukariri vifungu mara nyingi.

Mfano

Kitoto kivivu aia aia
Kikienda skuli aia aia
Saa tatu hazijafika aia aia
Ndicho hicho chalia njaa aia aia
Ticha’ naona njaa aia aia
Malimu hadiriki kuandika lolote aia aia
Kitoto machozi yatoka aia aia
Hadi ruhusa kipewe aia aia
Kitazame kilo ndani ya chupa aia aia
Ndipo kitulie aia aia

Maswali

 1.  Andika maadili yanayojitokeza katika wimbo
  •  Bidii –inakashifu uvivu
  •  Tabia njemma- inakashifu tabia ya kulia onyo na kusumbua
  •  Masomo-watto wanahimizwa kwenda shuleni
 2.  Taja mbinu za lugha zilizotumiwa
  •  Uradidi- aia aia
  •  Utohozi -ticha
 3. Andika miktadha mitatu ambayo nyimbo za watoto hupatikana
  •  Watoto wanapocheza
  •  Watoto wanapopewa elimu.

Jadiya/jadiia

 • Ni nyimbo za kitamaduni ambazo huimbwa na kupokezwa kwa mdomo kutoka kizazi kimoja hadi kingine, kila jamii ina jadia zipokezwazo kwa vizazi vyake kimaudhui, nyimbo hizi husimulia mambo mengi hasa yaliyotukia katika historia ya jamii kama vile matendo ya shujaa fulani, mateso, njaa na ucheshi.

Kongozi

 •  Ni nyimbo za mwaka, huimbwa wakati wa kukaribisha mwaka mpya.

Nyimbo za dini

 •  Huimbwa katika shughuli za kidini

Kimai

 •  Uhusisha shughuli za kibaharini

Nyimbo za vita

 •  Huimbwa na askari wakati wa vita

Nyimbo za usasi

 •  Huimbwa na wasasi wanapokwenda au kutoka usasini
 •  Husifu mtu fulani kwa mchango wake katika jamii

Nyimbo za kuzaliwa kwa mtoto

 •  Huonyesha au kuathimisha kuzaliwa kwa mtoto.

Maghani

 • Ni ushairi ambao hutolewa kwa kalima (nusu kuimba nusu kuongea kama afanyavyo padre) badala ya kuimbwa tofauti kati ya maghani na nyimbo ni kuwa maghani hayaimbwi, hata hivyo kimaudhui maghani ni sawa na nyimbo kama za kazi, maombolezi au siasa; kama ilivyo katika nyimbo.

Sifa

 1.  Ni fungu za kishairi, yaani yana sifa za kishairi za kuwa na mapigo ya kimuziki na maneno mateule yenye muwala (mtiririko) mzuri wa mawazo
 2.  Husimulia matukio kwa kirefu hasa yanayotambwa
 3.  Hutungwa papo hapo na kusemwa au kutongolewa mbele ya hadhira.
 4.  Hutungwa kwa ufundi mkubwa
 5.  Hutolewa na mtu mmoja au kundi la watu

Umuhimu

 1.  Kuchochea wanotaka kuwa shujaa
 2.  Kutoa sifa nzuri za kuigwa au kutumiwa kukosewa
 3.  Kuelezea usuli wa mtu, asili au nasaba ya mtu kitu jambo au familia.
 4.  Kudhihirisha uhodari wa kutenda

Aina za Maghani

 1. Maghani ya kawaida
  • Ambayo hugusia maswala ya kawaida kama mapenzi, siasa, harusi, kazi, maombolezo n.k.
  • Husemwa/huganwa tu bila kusimuliwa.
 2. Maghani Simulizi
  • Maghani ambayo husimulia hadithi kuhusu tukio la kihistoria
  • Huhusu, mtu, tukio, kitu, mnyama, n.k.

   Sifa
  • Hutokea kama hadithi.
  • Husimulia tukio la kihistoria.
  • Ni ndefu.
  • Waimbaji wake huitwa manju/yeli.
  • Huandamana na ala kama zeze, marimba, n.k.

Tofauti kati ya maghani ya kawaida na maghani simulizi

Maghani ya kawaida   Maghani simulizi
 Ni fupi  ni ndefu
 Haitumii ala  Hutumia ala
 Huhusu maswala ya kawaida  Huhusu maswala ya kihistoria 
 Husemwa  Huimbwa

Maghani ya Kawaida

 1. Vivugo/majigambo
  1. Utungo wa kujisifu au kujigamba.

   Sifa
  2. Hutungwa baada ya ushindi wa harakati ngumu k.v. kesi, kumuua simba, kuoa msichana aliyependwa na wengi n.k.
  3. Fanani ni mwanamme.
  4. Hutungwa papo hapo.
  5. Hutungwa na kughanwa na mhusika mwenyewe.
  6. Hutumia chuku k.m. kujisifu kupita kiasi.
  7. Anayejigamba hujipa jina la kiistiari k.m. mnyama.
  8. Mhusika huvaa maleba yanayooana na tukio analojisifia.
  9. Kuna kutaja jina na ukoo wa baba na mama.
  10. Anayejisifu huahidi kutenda maajabu zaidi.
 2. Pembezi/pembejezi
  • Aina ya tondozi inayokusudiwa kusifu watu aina fulani katika jamii kutokana na matendo au mchango wao. k.v. watawala, walezi wazuri, mashujaa wa vita, waganga mashuhuri hata wapenzi waliopigania pendo lao.

   Mfano
   Nani kama wewe mama?
   Nani anokufana ‘mwaitu’
   Subira uliumbiwa
   Bidii nd’o jina lako la pili
   Moyo wenye heba
   Msimamo usoyumba
   Anoelekeza kwa imani
   Anoadhibu kwa mapenzi makuu
   Mzazi, mlezi na rafiki wa dhati
   Tangu siku za kusimama dede.
 3. Tondozi
  • Utungo wa kutukuza watu, wanyama na vitu.  k.v. watu mashuhuri, wapenzi, mifugo, miti mikubwa.

   Mfano
   Kipungu kipungu
   Nani kama yeye?
   Hashindiki kwa nia
   Hashindiki kwa shabaha
   Hulenga binguni
   Hutia ghera kufikiwa peo
   Peo zisofikika kwa wanokata tama
   Kipungu, kipungu, hachi tufani za anga.

Maghani Simulizi

 1. Sifo
  • Tungo za kusifu watu kutokana na matendo yao ya kishujaa.
  • Sifa zake hukaribiana na za tenzi hasa ikiwa ni shujaa anasifiwa.
 2. Tendi/tenzi
  • Ushairi mrefu unaoelezea maisha ya mashujaa tangu kuzaliwa hadi kufa kwao. k.v. Utenzi wa Fumo Liyongo, Sundiata, Shaka Zulu, Wang`ombe waihura n.k.
  • Utungo huu waweza kuwa wimbo wa sifa au utendi!

   Mfano
   Asiyemjua mjua aliongwe atamjua
   Namjuza kwa sifa zake alizokuwa nazo
   Alisimika ufalme uliosifiwa
   Akawa shujaa asiyetishwa

   Sifa
  • Huwa masimulizi yanayotolewa kishairi.
  • Hutoa wasifu wa shujaa.
  • Huwa na matumizi ya chuku.
  • Wahusika hupewa sifa zisizo kawaida (kiungu).
  • Ni masimulizi mrefu.
  • Matumizi ya sitiari k.v. kulinganisha wasifiwa na wanyama wakali.
  • Huangazia matendo ya mashujaa.
  • Husimulia matukio ya kihistoria.
  • Huimbwa pamoja na ala ya kimziki.
  • Hutungwa papo kwa papo na kuhifadhiwa katika ubongo.
  • Hujumuisha mbolezi zinazoonyesha anguko la shujaa.

   Lengo
  • Kuburudisha wanajamii.
  • Kusifu mashujaa wa jamii.
  • Kukuza uzalendo kwa kuhimiza wengine kuwaiga mashujaa.
  • Kukuza ubunifu kwa kutunga papo hapo.
  • Kuimarisha uwezo wa kukumbuka kwa kutungwa na kuhifadhiwa akilini.
  • Kuburudisha waliohudhuria sherehe ampapo yanatolewa.
  • Kuhifadhi na kuendeleza tamaduni za jamii
  • Kukuza ufasaha wa lugha kwa fanani.
  • Kufunza maadili.
 3. Rara
  • Hadithi fupi na nyepesi za kishairi zenye visa vya kusisimua.

   Mfano
   Alichukua mkoba wake
   Akanipa kisogo
   Kana kwamba hakunijua
   Kana kwamba hakusema, “Hadi mauko”.
   Hakujali penzi letu
   Hakujali wana
   Ambao ndiye alowapa uhai
   Alijua nilimpenda
   Ila hata hilo alijipa kujipurukusha
   Akayoyomea
   Akamezwa na ulimwengu.

   Sifa
  • Huhusu mambo ya kubuni au ya kweli k.v. sherehe ya uhuru, kesi ya mauaji, n.k.
  • Huhusu maswala ibuka na ya kawaida.
  • Hadithi huwasilishwa katika beti.
  • Huimbwa.
  • Huandamana na ala za mziki.
  • Hutolewa kwa toni ya kitanzia.
  • Huwa na visa vya kusisimua.
  • Huwa na ucheshi wenye kinaya.
  • Maswala hayatoleai kwa uwazi bali hufumbwa na kudokezwa.
  • Huwa na uigizaji/utendaji.
  • Mambo yanayosimuliwa hupigwa chuku.
 4. Rara nafsi
  • Ushairi ambao hutungwa na mtu kuelezea hisia, matatizo na fikra zake mwenyewe.

   Mfano

   Muda umefika wa pingu kutiwa
   Kutiwa silisili, kwani si utashi wangu
   Ukoo waniuza, mithili ya kondoo sokoni
   Mwambieni shangazi kwaheri nampigia
   Hata angataka kuniopoa hawezi
   Kwani mahari imetolewa
   Mifugo kikwi nduguye amepokea
   Kwaheri mama, kwaheri dada.

   Sifa
  • Hugusia maswala yanayoathiri hisia za mtu binafsi kama vile mapenzi, usaliti, talaka, kifo.
  • Huwasilishwa kwa njia ya uimbaji unaoandamana na ala ya mziki.
  • Mzungumzaji huzungumza moja kwa moja na hadhira au aliyeandikiwa rara hiimkewe, mpenziwe, mwanawe, Mungu, miungu.
  • Hutolewa katika miktadha k.v. mazishi kusifu aliyekufa, harusi na Bi. Arusi kama ameshinikizwa kuolewa.

Ngonjera

 • Mashairi ya kujibizana/kulumbana-yenye muundo wa kimazungumzo.

  Sifa
 • Huwa na wahusika wawili au zaidi.
 • Mhusika mmoja huuliza jambo na mwingine hujibu.
 • Huendelezwa kwa njia ya wimbo.
 • Wahusika kupingana mwanzoni.
 • Wahusika huafikiana kufikiwa mwisho.

  Umuhimu
 • Majibizano hukuza ubunifu kwa kila mmoja kuonyesha umaarufu.
 • Kukuza ujasiri wa kuzungumza hadharani.
 • Kuimarisha stadi ya kuongea.
 • Kuburudisha hadhira.

Mashairi Mepesi.

 • Mashairi ya kawaida ambayo hupatikana katika ushairi simulizi.
 • Hujumuisha mashairi mafupi ya kihisia, kimapenzi, kusifu na kukosoa watu.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Ushairi Simulizi - Tanzu za Fasihi Simulizi Kiswahili Notes.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest