Semi - Tanzu za Fasihi Simulizi Kiswahili Notes

Share via Whatsapp


Utangulizi

  • Semi ni kauli fupi za kisanaa zenye maana na mafunzo yaliyofichika. Semi hutoa mafunzo kwa njia ya kufumba, mafunzo katika semi hutokana na imani ya jamii ambayo imezibuni mifano ya semi ni methali, vitendawili, misemo, nahau, misimu, lakabu, mafumbo, chemshabongo na vitanza ndimi. Semi pia huitwa tungo fupi au tungo bainifu.


Sifa za Semi

  1. Semi hufumba ujumbe wake kwa mfano maana ya ndani ya nahau “piga kalamu’ ni ‘futa kazi’ ilhali maana ya juu ni ‘kuchapa au kugonga kalamu methali pia huwa na maana iliyofumbwa aidha vitendawili hufumba jibu.
  2. Hutumia picha (taswira) na ishara kupitisha ujumbe wake, mtu anaposema ‘kwetu ni jehanamu; ile picha ya jehanamu inajichora akilini mwa msikilizaji, jehanamu hapa inamanisha mahali pabaya penye mateso mengi
  3. Maana ya semi hupatikana katika jamii iliyozibuni, methali “mgaaga na upwa hali wali mkavu” kwa mfano itaeleweka na jamii za pwani.Vile vile katika tashbihi weupe au weusi, hulinganishwa na vitu mbalimbali kutegemea jamii na mazingira yake.mathalani, watasema –eupe kama maziwa au theluji-eusi kama mpingo, lami au makaa kutegemea vifaa vinavyopatikana katika jamii husika.
  4. Huwasilisha ujumbe mrefu kwa maneno machache mfano ni methali ‘juhudi si pato’ ambayo imefupisha ujumbe mrefu kuwa mtu huweza kufanya bidii sana na akakosa kufanikiwa, Semi huwasilisha ujumbe kwa njia ya mkato tofauti na hadithi ambazo ni masimulizi marefu.
  5. Semi ni tanzu tegemezi, hii ina maana kwamba semi hutokea kuambatana au kutegemea tanzu nyingine kwa mfano methali hutolewa katika muktadha wa mazungumzo ya kutoa mawaidha au mwishoni mwa hadithi kama funzo la hadhi lakabu, misimu, misemo na nahau pia hupatikana katika utanzu wa mazungumzo.


Umuhimu wa Semi

  1. Semi huelimisha, vitendawili, methali, mafumbo na nahau zote hutoa mafunzo ya aina Fulani; methali “mwenda pole hajikwai “hutoa maarifa ya kufanya mambo bila pupa.
  2. Hukuza uwezo wa kufikiria, vitendawili, methali na mafumbo humhitaji mtu kufikiria ili kupata ujumbe uliofumbwa.
  3. Hutambulisha jamii na wanajamii, kila jamii huwa na semi mahususi zinazohusu shughuli zake, misimu kwa mfano hutumiwa na kundi fulani katika jamii.Methali mkulima ni mmoja walaji ni wengi inatambulisha jamii inayohusika katika kilimo, kitendawili kimoja kinaweza kuwa na majibu tofauti kutegemea jamii na mazingira yake.
  4. Hukuza utangamano, wakati wa kutegeana vitendawili; kwa mfano watu huja pamoja aidha misimu hujenga uhusiano wa karibu miongoni mwa watu wanaoitumia, lakabu nazo hutumiwa na watu walio na uhusiano wa karibu.
  5. Huburudisha, baada ya shughuli za kazi watu hujumuika pamoja katika vikao vya kujiburudisha ambapo hutegeana vitendawili na hushiriki katika vitanza ndimi ili kutuliza bongo na kusisimka.
  6. Huhifadhi utamaduni, semi hufumbata desturi za jamii zinapopitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, utamaduni huo hufunzwa na kuhifadhiwa.
  7. Husawiri mitazamo ya jamii kuhusu masuala Fulani, je, jamii inachukia nini? Inahimiza nini? Kupitia kwa methali bidii ya mja haiondoi kudura tunafahamishwa kwamba jamii hii inaamini kuwa binadamu yumo chini ya uwezo wa Mungu nahau, lakabu, vitendawili na mafumbo pia hufumbata tajiriba ya jamii.
  8. Hututasfidia lugha, nahau, misemo, misimu na lakabu hutumiwa badala ya msamiati mkali /wenye aibu, badala ya kusema ‘kuzaa’tunasema ‘kujifungua’
  9. Hukuza lugha, semi huyapa maneno maana mpya au maana ya ziada. Misimu huweza kukubaliwa na kuwa nahau rasmi za lugha kwa njia hii msamiati wa lugha hupanuliwa.


Vipera vya Semi

Methali

  • Methali ni semi fupifupi za kimapokeo zenye kueleza fikira, maarifa, hekima na mafunzo yanayotokana na uzoefu wa jamii mahususi. Methali hutumia taswira na mafumbo, chukulia kwa mfano, fimbo ya mbali haiui nyoka, utungo huu ni mfupi na unatumia neno ‘fimbo kama fumbo la ‘suluhisho’
  • Methali ni tanzu tegemezi kama ilivyotajwa kutumika kwake hutegemea tanzu nyingine. Methali hutokea katika mazungumzo mazito kama vile kutoa mawaidha au kama kielelezo na kifupisho cha hadithi si utanzu unaoweza kujisimamia kama tanzu nyingine kama vile hadhithi, ushairi au mazungumzo.

Sifa

  • Methali ni kauli fupi ambazo hutolewa kwa mtindo wa kishairi kinyume na jinsi kauli za kawaida zinavyowasilishwa.
  • Methali zina sifa za kishairi, huwa na vipande vyenye mizani inayolingana na kwamba ni mshororo mmoja.
  • Maudhui katika methali huchotwa katika jamii zinamozaliwa, maudhui hutokana na tajriba na mambo yanayoathiri jamii.
  • Huwa na muundo maalumu wenye sehemu mbili, kwa mfano. Aliye juu, mngoje chini sehemu ya kwanza hudokeza wazo na ya pili hulikamilisha kwa kukubali au kukataa.
  • Hujengwa kwa tamathali nyingine za usemi na mbinu za lugha kama vile kinaya, taswira na takriri, methali kukopa arusi kulipa matanga imejengwa kwa sitiari.
  • Methali hueleweka na jamii iliyozibuni kwani hubuniwa kutokana na mazingira ya jamii husika.
  • Methali zina sifa ya utegemezi na huingiliana na tanzu nyingine za fasihi.
  • Hutumiwa mwishoni mwa ngano kufupisha maadili ya ngano hiyo.
  • Hutumiwa kubuni lakabu, mtu ambaye huwasaliti marafiki anaweza kuitwa ‘kikulacho’ kutokana na methali ‘kikulacho ki nguoni mwako’
  • Hutumiwa katika tanzu za kimaandishi kama vile riwaya na tamthilia ili kuongeza ladha katika usimulizi.
  • Hutumiwa katika mazungumzo ya kawaida na ulumbi kuleta mvuto.
  • Hutumiwa katika nyimbo na mashairi
  • Hutumika katika hotuba rasmi au hata mahakamani mshtakiwa, mlalamishi na mahakimu wanaweza kutoa maoni yao kutumia methali.
  • Hutumika katika kutoa mawaidha
  • Methali huelezea ukweli ambao unakubalika na jamii ambao imebuniwa
  • Tofauti na vitendawili ,methali hazina muktadha maalumu wa kutolewa. Hazitengewi vikao vya kutolewa
  • Methali ni mali ya jamii, kama tanzu nyingine za faihi simulizi hakuna anayeweza kudai kumiliki methali
  • methali huambatana na mazingira ya jamii iliyozizaa, hulka, itikadi, tamaduni na tajriba zake busara fulani huwasilishwa kutegemea mazingira ya jamii kwa

    mfano.
    - Ulingo wa kwake haulindi manda
    - Kamba ya mbali haifungi kuni
    - Fimbo ya mbali haiui nyoka
  • Methali zina matumizi mapana.methali moja huweza kuwa na majukumu mbalimbali kama vile kuonya, kuelekeza na kufunza.
  • Methali huwa na maana ya ndani na nje, maana ya nje hutokana na maana halisi ya maneno yaliyoiunda. Vilevile, methali hupewa maana ya ndani yenye fumbo lililofumbwa na maneno yanaoiunda.

Majukumu

  • Huelimisha, methali hutumiwa kupitisha maarifa ya kijamii kwa wanajami. Abebwaye hujikaza huonyesha kuwa unapopata usaidizi nawe pia jikaze kutia bidii, usingoje tu usaidizi.
  • Huadilisha. methali hufunza maadili kama uvumilivu kwa mfano ‘mstahimilivu hula mbivu’
  • Husawiri mitazamo na falsafa za jamii. Fulani kuhusu masuala mbaliimbali. Je, jamii inapenda nini? Inachukia nini? Methali ucha mungu si kilemba cheupe hudhihirisha kuwa jamii huchukia unafiki.
  • Hutambulisha jamii, kila jamii ina methali zake maalum zinazoitambulisha.
  • Huongeza ladha katika mazungumzo na maandili, mazungumzo na maandishi yenye matumizi mazuri ya methali huvutia.
  • Hubudisha, katika jamii nyingine, methali hutengewa vipindi vya kutolewa na makundi yanayoshindana, hii ni njia mojawapo ya kutuliza bongo.
  • Hurithisha utamaduni wa jamii, methali ni zao la utamaduni husika na hupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine hivyo utamaduni huweza kurithiwa.
  • Hufariji, methali huwatuliza na kuwaliwaza watu wanapokabiliana na matukio au hali zinazohuzunisha, kwa mfano hakuna refu lisilo na ncha.
  • Hukuza uwezo wa kufikiri, mtu huhitajika afikiri kwa makini na kuoanisha msamiati uliotumika kwa hali ya maisha ili kupata maana.
  • Hukuza ushirikiano na mshikamano wa jamii. Katika jamii ambazo methali hutengewa vikao, watu hujumuika pamoja hivyo kukuza ushirikiano na mshikamano.

Uainishaji wa methali

  1. Muktadha
    • Ile kuelewa methali, ni muhimu kujua mazingira, tamaduni na hali zilizozizaa methali hizo methali ambazo zimezaliwa katika muktadha au mazingira sawa huweza kuwekwa katika kundi moja.
  2. Maudhui
    • Maudhui na fani ndiyo hutawala methali, maudhui katika methali ni mengi na mapana kama zilivyo jamii na shughuli zao, methali ambazo huwa na maudhui sawa huwekwa katika kundi moja, baadhi ya maudhui yanayojitokeza katika methali za Kiswahili ni ya
      1. Malezi
        - Mchelea mwana kulia hulia mwenyewe
        - Samaki mkunje angali mbichi
        - Asiyefunzwa na mamake hufunzwa na ulimwengu.
      2. Kazi
        - Kazi mbi si mchezo mwema.
        - Mchagua jembe si mkulima.
        - Kazi ya bakuli husiri.
        - Kazi isiyo faidi kutenda si ada.
      3. Ushirikiano
        - Kidole kimoja hakivunji chawa.
        - Jifya moja haliinjiki chungu.
        - Umoja ni nguvu utengano udhaifu.
  3. Mtindo au fani
    • Mbali na maudhui, methali hutawaliwa na fani pia. Fani katika methali hudhihirika katika muundo, tamathali za semi na taswira inayoibuliwa, methali ambazo huundwa kwa kutumia fani sawa huweza kuwekwa katika kundi moja.
    • Methali zifuatazo zimeundwa kwa kutumia kweli kinzani
      - Simba mwenda pole ndiye mla nyama.
      - Kuinamako ndiko kuinukako.
  4. Jukumu
    • Methali huweza kuanishwa kulingana na majukumu yake. Je, methali inasifu, inakashifu, inahimiza, inaonya ama inafariji?
    • Methali zifuatazo hutumiwa kuonya:
      - Mwenye pupa hadiriki kula tamu.
      - Asiyeangalia huishia ningalijua.
      - Usione kwenda mbele kurudi nyuma si kazi.
  5. Maana
    •  Methali zote zenye maana sawa huweza kuwekwa katika kundi moja, kwa mfano.
      - Damu ni nzito kuliko maji
      - Meno ya mbwa hayaumani
      - Mtoto wa nyoka ni nyoka
      - Mwana wa mhunzi asiposana, huvukuta.
    • Methali zenye maana zinazokinzana pia zinaweza kuainishwa pamoja, kwa mfano. Mvumilivu hula mbivu. Ngoja ngoja huumiza matumbo. Mtu pweke ni uvundo. Nahodha wengi chombo huenda mrama.

Fani katika methali

  1. Sitiari
    - Sitiari ni mbinu ya kulinganisha kitu na kingine bila kutummia maneno ya kulinganisha, methali zinazoundwa kwa sitiari ni pamoja na:
    1. Mgeni ni kuku mweupe, hapo mgeni anafananishwa moja kwa moja na kuku mweupe kuonyesha mgeni hutambulika haraka akiwa kundini.
    2. Ahadi ni deni, ahadi inafananishwa na deni kuonyesha kuwa ni sharti mtu kutimiza ahadi.
  2. Takriri
    - Takriri ni mbinu ya kurudiarudia maneno au sauti kwa nia ya kusisitiza methali zenye takriri ni kama vile;
    1. Ngoja ngoja huumiza matumbo.
    2. Haba na haba hujaza kibaba.
  3. Tashbihi.
    - Tashbihi ni tamathali ya usemi na inayo linganisha vitu kwa kutumia maneno ya kulinganisha kwa mfano:
    1. Kawaida ni kama sheria.
    2. Jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza.
  4. Tanakali za sauti
    - Hizi ni miigo ya sauti zinazotolewa na kitu au zinazotokea tendo linapotendeka. Methali zinazotumia tanakali za sauti ni kama vile, Chururu si ndo ndo ndo!
  5. Taswira
    - Taswira ni picha zinazojengeka akilini mwa mtu baada ya kusoma, kutazama au kusikia maelezo fulani. Taswira hizi hutokana na tajriba pamoja na mazingira ya mtu ifuatayo ni mifano ya methali zinazotumia taswira.
    • Mti mkuu ukigwa wana wa ndege huyumba.
    • Mpanda farasi wawili hupasuka msamba.
  6. Kweli kinzani
    - Katika kweli kinzani, maana ya maneno hukinzana kijuujuu (husikika kuwa haiwezekani) lakini ikichunguzwa kwa undani kuna ukweli fulani uliofichika, ifuatayo ni mifano ya methali zinazotumia ukinzani.
    • Wagombanao ndio wapatanao.
    • Ukupigao ndio ukufunzao.
  7. Chuku
    - Chuku ni mbinu ya kuongezea sifa kitu zaidi ya kilivyo, mifano ya methali zinazotumia mbinu hii ni:
    • Usipoziba ufa utajenga ukuta.
    • Mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi.
  8. Taashira au ishara
    - Katika taashira, kitu kimoja huashiria kingine. Mifano ya methali zenye taashira.
    • Kimya kingi kina mshindo mkuu.
    • Kuku mgeni hakosi kamba mguuni.
  9. Dhihaka stihizai au kejeli
    - Hii ni mbinu ya kufanya mzaha au kudharau tabia au mienendo isiyofaa, kwa mfano.
    • Hawi musa kwa kuchukua fimbo.
    • Ucha mungu si kilemba cheupe.
  10. Tashihisi au uhuishaji
    - Tashihisi ni mbinu ya kukipa kitu sifa za kibinadamu au kitu kisicho hai kupewa sifa za kitu kilicho hai
    mfano
    • Adhabu ya kaburi aijuaye ni maiti.
    • Siri ya mtungi aijuaye kata.
  11. Balagha
    - Maswali yasiyo hitaji majibu maswali haya humchochea mtu kufikiri.
    - Methali hizi zimeundwa kwa mbinu ya swali ambalo linamhitaji mwenye kuambiwa kufikiria.
    • Pilipili usiyoila yakuwashiani?
    • Mavi usoyala wayaingiani kuku?
  12. Tanakuzi
    - Hii ni mbinu inayotumia maneno au kauli zinazopingana, katika tanakuzi sehemu moja ya methali huwa na maana inayopingwa na sehemu ya pili.
    • Tamaa mbele mauti nyuma.
    • Mpanda ngazi hushuka.
    • Pole pole ya kobe humfikisha mbali.
  13. Kinaya
    - Kinaya ni kinyume cha matarajio au cha hali ilivyo kwa mfano.
    • Kigumba kwa nguruwe kwa mwanadamu ki uchungu.
    • Kikiharibika cha fundi kikiongoka cha bwana swedi.

Muundo wa methali

  • Methali kwa kawaida huwa na muundo na wenye sehemu mbili sehemu ya kwanza hudokeza wazo nayo ya pili hulikamilisha mfano.
    1. Baada ya shida, mkasa.
    2. Debe shinda, haliachi kutika.
    3. Dawa ya moto, ni moto.

Uchambuzi wa methali

  • Maswali yafuatayo husaidia kuchambua au kuhakiki methali
    1. Methali imerejelea vifaa gani au inahusu nini? K.m Wanyama, binadamu ama vifaa vya nyumbani?
    2. Methali imebuniwa kwa kutumia tamathali gani na mbinu gani za kifasihi? k.m uradidi , kinaya, balagha n.k
    3. Methali inaibua taswira gani? Methali ‘simba mwenda pole ndiye mla nyama ‘inaibua taswira ya utulivu makini na subira, kwamba ukitaka kufanikiwa ni sharti uwe na subira.
    4. Methali inakupa wazo gani kuhusu jamii? Methali mtu pweke ni uvundo inaonyesha kuwa jamii husika inachukia utengano.
    5. Je, kuna methali nyingine inayokaribiana kimaana au inayopingana na hii?
    6. Je, methali imejikita katika mazingira ama muktadha gani? Kwa mfano.
      - Jogoo wa shamba hawiki mjini (mashambani /mjini)
      - Mgaagaa na upwa hali wali mkavu (pwani)
      - Ucha mungu si kilemba cheupe (dini)
    7. Je, dhamira ya methali yenyewe ni gani? Inanuia kuonya, kushawishi, kufahamisha au kusifu? Kwa mfano ‘mali bila daftari hupotea bila habari’ inaelimisha; uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti ina kejeli ilhali ‘hakuna refu lisilokuwa na ncha” inaliwaza.

Vitendawili

  • Kitendawili ni kauli yenye fumbo ambalo hutolewa kwa hadhira hai ili ilifumbue jibu la kitendawili ndilo fumbo lenyewe.

Sifa

  1. Kwa kawaida, vitendawili ni semi fupifupi zinazotumia lugha ya mkato.kwa mfano ’pa’funika ‘pa’funika (jibu; nyayo wakati wa kutembea )
  2. Vitendawili hutolewa kwa hadhira ili vifumbuliwe hivyo, hadhira yake ni hai na tendi.
  3. Hutumia lugha ya picha au taswira na vina ukwasi wa tamathali za semi.
  4. Vitendawili huhitaji watu au makundi mawili ili kukamilisha uwasilishaji wavyo mtu wa kwanza hutega na mwenzake hutegua.
  5. Vitendawili huwa na muundo au fumyula maalumu ya uwasilishaji kwa mfano
    Mtegaji: kitendawili
    Mteguaji: tega!
    Mtegaji: nyumba yangu haina mlango
    Mteguaji: yai
  6. Vitendawili huwasilisha kwa mtindo wa majibizano kati ya mtegaji na mteguaji mteguaji akishindwa kutegua, huhitajika kutoa mji ndipo kupewa jibu na mtegaji
  7. Kitendawili ni fumbo au swali liilofichika ambalo huhitaji jibu.
  8. Fumbo au jibu la kitendawili hufahamika tu na jamii ambamo kitendawili hicho kimezaliwa, kitendawili kinaweza kuwa na majibu mawili kutegemea mazingira ya jamii kwa mfano, vitendawili vifuatavyo huweza kuwa na jibu zaidi ya moja.
    - Wanangu wawili husabihiana majibu tui na maziwa Jibu; unga na majivu.
    - Mwarabu kasimama kwa mguu mmoja jibu uyoga; mwavuli.
  9. Vitendaili ni sanaa ambayo kwa kiasi kikubwa hutegemea uwezo wa mtu kutambua na kuhusisha au kulinganisha vitu katika mazingira yake, kwa mfano ili kufumbua fumbo la kitendawili mbili mbili hadi pwani, lazima mtu aweze kuhusiaha vitu viwili ambavyo daima hufanya jambo pamoja (jibu macho ) macho hutazama pamoja, hulala pamoja na hulia pamoja.
  10. Vitendawili huingiliana na tanzu na vipera vingine vya fasihi simuliza kwa mfano ngano za mtanziko hutumia vitendawili, hasa katika fomyula ya ufunguzi wa ngano. Aidha vitendawili hutangulia vikao vya kusimulia hadithi au hutegwa baada ya vikao hivyo.
  11. Vitendawili hubadilika kutegemea wakati au kipindi cha kihistoria na maendeleo ya jamii, kitendawili kimoja kinaweza kuundwa au kutolewa kwa maneno tofauti kulingana na kipindi cha wakati kinapotumiwa kwa mfano.
    - Mwarabu wangu nimemtupa biwini (machicha ya nazi)
    - Mzungu katupwa jalalani (machicha ya nazi) maneno tofauti (mwarabu na mzungu) katika vitendawili hivi viwili ambavyo vina jibu moja yanaonyesha viliathiriwa na nyakati tofauti za kihistoria.
  12. Vitendawili ni sanaa inayotendwa kwa hivyo hujisimamia yenyewe tofauti na methali ambazo kwa kawaida ni sanaa tegemezi. Hutegewa vikao maalumu na kutolewa.
  13. Kimaudhui, vitendawili hushughulikia masuala katika nyanja zote za maisha ya binadamu na mzingira yake. Maudhui haya hutofautiana katika jamii mbalimbali ingawa baadhi yao huingiliwa
  14. Vitendawili vinaweza kuwa sahili (rahisi) na vingine changamano 

- Vitendawili ni semi maarufu sana miongoni mwa watoto, katika jamii nyingine watoto na watu wazima hushiriki.Miongoni mwa wakamba, kwa mfano watu wazima walishindana kutegua vitendawili hata kuliko watoto.

Umuhimu

  1. Vitendawili huelimisha, vitendawili hujumuisha masuala mengi katika mazingira ya jamii.
  2. Hali hii inavifanya kuwa na uwezo mkubwa wa kuelimisha watu kuhusu mazingira yao aidha mtu akikosa jibu haadhibiwi zaidi ya kutoa mji.
  3. Huburudisha.vitendawili huwapumbaza na kuwapumzisha wanaoshiriki katika utegaji ua utegauaji wavyo.
  4. Hufundisha kaida na maadili ya jamii, vitendawili huwa na utaratibu fulani unaofuatwa na ambao washiriki wanapaswa kuuheshimu na kuuzingatia, hii ni njia moja ya kuadilisha kwa kuwa kila jambo maishani lina kaida zake zinazoheshimiwa.
  5. Hukuza ubunifu na stadi ya kufikiri haraka, mteguaji wa kitendawili sharti afikiri na kuoanisha yaliyotajwa na mazingira yake ili kupata jawabu.Vitendawili hukuza ari ya kufikiria na kudadisi mazingira.
  6. Vitendawili hudhihaki na kukejeli watu, hali au tabia hasi katika jamii.hukashifu matendo hasi na kusifu yale chanya
  7. Husawiri mitazamo na itikadi ya jamii kuhusu hulka fulani, kwa mfano nyumbani kwetu kuna papai lililoiva sana lakini nashindwa kulichuma (jibu: kaka au dada) inaonyesha kuwa ndoa kati ya dada na kaka hairuhusiwi.
  8. Hukuza uwezo wa kukumbuka vitendawili hutumiwa kama chemshabongo ya kujaribu uwezo wa mtu kukumbuka na kuhusisha mambo
  9. Huleta umoja na ushirikiano katika jamii, watu hujumuika wakati wa kutegeana vitendawili kwa njia hiyo utangamano huimarika.
  10. Hutambulisha jamii kila jamii huwa na vitendawili vinavyoonyesha mazoea, hali, tajriba na mazingira ya jamii husika.
  11. Huchochea tabia ya udadisi, uzoefu wa kutafuta kiini cha kitendawili hujenga tabia ya kutaka kufichua jambo lililofichika kwa kujaribu kupata jibu la jambo katika kitendawili wanajamii huimarisha ari yao kutafiti mambo ili kubaini kiini chake.
  12. Vitendawili hukuza na kusambaza ujuzi wa lugha, vitendawili vina ukwasi mkubwa wa lugha na tamathali za semi kwa hivyo ni nyenzo kuu ya kukuza na kusambaza maswala ya lugha katika jamii.

Fani katika vitendawili

Muundo

  • Kama tulivyotaja awali, vitendawili huwa na fomyula au muundo maalamu wa uwasilishaji.
    - Kitangulizi ambacho hutolewa na mtegaji.
    1. Mtegaji: kitendawili
    2. Hadhira humpa ruhusaya kutega. Mteguaji: tega!
    3. Mtegaji hutoa kitendawili mtegaji: Fatuma mchafu
    4. Jibu hutolewa na mteguaji: Mteguaji: nguruwe (kosa)
    5. Jibu likikosekana mtegaji huomba mji: Mtegaji :Umenoa
      Nipe mji.
    6. Mteguaji hutoa mji mteguaji :Ninakupa migingo
    7. Mtegaji akipewa mji hutoa jawabu sahihi: Mtegaji: Nilienda migingo, watu wa migingo wakaniambia nikija niwasalimu.
      Jibu lake ni ufagio

Mtindo

  • Vitendawili hutolewa kwa mtindo wa majibizano, majibizano haya huwa kati ya mtegaji na mteguaji na hadhira ya wasikilizaji utaratibu ulioelezwa katika muundo huzingatiwa na mtegaji na mteguaji /hadhira.

Lugha

  1. Sitiari
    • Aghalabu, vitendawili hutumia sitiari k.m
      - Fatuma mchafu (ufagio) hapa fatuma ni sitiari ya ufagio.
      - Saa yetu kadiri inavyotembea ndivyo inavyopunguza nguvu (moyo) saa ni sitiari ya moyo.
      - Jani la mgomba laniambia habari zinazotoka ulimwenguni kote ( gazeti /jarida) jani la mgomba ni sitiari ya gazeti /jarida.
  2. Tashihisi /uhuishaji
    • Wakati mwingine, vitendawili hutumia mbinu inayoipa kitu kisicho hai sia za kibinadamu k.m
      - Akizungumza kila mtu hubabaika (radi) hapa radi imepewa sifa ya kuzungumza kama binadamu sauti kali ya radi huwaogofya binadamu.
      - Amenifunika kote kwa blanketi lake jeusi (giza) giza limepewa sifa ya binadamu ya kumfunika mwingine.
      - Daima nasaabisha mafarakano (ukewenza) ukewenza umerejelewa kwa nafsi ya kwanza.
  3. Taashira
    - Faiza akiniona ajificha (mzee kobe) kinachoashiriwa na kujificha kwa Faiza ni kobe.
    - Chonge la nyoka huuma walio mbali (ugonjwa) chonge la nyoka linaashiria ugonjwa.
  4. Stihizai /dhihaka/kejeli
    • Vitendawili vinavyobuniwa kwa dhihika hutumiwa kukashifu mienendo hasi katika jamii pia hueleza sifa ya kitu kwa njia ya dharau k.m
      - Akivaa miwani hafanyi kazi vizuri (mlevi) kitendawili hiki kinakashifu ulevi
      - Babangu amevaa koti la chuma (mzee kobe)
      - Upara wa mwarabu unafuka moshi (chai ya maziwa )
      - Uzi mwembamba umefunga dume kubwa (usingizi)
  5. Kweli kinzani
    • Vitendawili vya aina hii huundwa kwa hoja mbili zinazopingana k.m
      - Ajenga ingawa hana mikono (ndege) ndege hana mikono kama binadamu hata hivyo hujenga kiota.
    • Ana meno lakini hayaumi (kichana) meno ya kichana hutumiwa kuchana wala si kuuma.
    • Hufa ikifufuka (bahari kupwa) maji ya bahari huwa (kutoka ufukweni)na kurejea.
  6. Takriri
    • Kuna vitendawili vinavyoundwa kwa tanakali za sauti .kwa mfano
      - Aliwa yuala,ala aliwa-(papa)
      - Amezaliwa ali,amekufa ali,na amerudi ali (nywele)
      - Mama kazaa mtoto kazao mtoto na mtoto kazaa mtoto (kuku na yai)
  7. Tanakali za sauti
    - Chubwi’-(jiwe likianguka ndani ya maji)
    - Prr’ mpaka ‘makka’- (utelezi )
    - ‘Pa’funua ‘pa’funika – (nyayo wakati wa kutembea )
  8. Taswira
    • Baadhi ya vitendawili vimeundwa kwa jinsi ya kuibua taswira au picha mbalimbali.k.m
      - Nimemwona bi kizee akijitwika machicha –(Mvi)
      - Ameingia shimoni akiwa uchi, akatoka amevaa nguo-(mbegu)
  9. Utata
    • Baadhi y vitendawili huweza kufasiriwa kwa njia zaidi ya moja tunasema kitendawili cha aina hii kina utata. Utata katika vitendawili husababishwa na hali kwamba jibu la kitendawili hutokana na mazingira.watu tofauti huweza kuwa na majibu tofauti kwa kitendawili hicho hicho kutegemea hali ambayo inawazunguka.

      Kwa mfano
      - Inachurura inaganda (asali au gundi )
      - Gari la kila mtu (miguu au jeneza au kifo )
  10. Vitendawili vinavyohusiana na methali
    - Ukichukua mama chukua mtoto –(sagio /jiwe dogo la kusagia linalopitishwa juu ya jiwe kubwa ) methali: ukivuta sagio uchukue kabisa na jiwe dogo la kusagia
    - Mzee amekufa na vyombo vimevunjikavunjika (kifo cha kiongozi husababisha matatizo ) methali :mti mkuu ukigwa wana wa ndege huyumba

    Mfano
    1. Ndege wengi baharini (nyota angani )
      1. Taswira
      2. Istiari
    2. Natembea shambani – (wembe wa kunyolea ukiwa kichwani
      1. Taswira
      2. Tashihisi
    3. Pambo juu ya jiwe (upara )
      1. Taswira
      2. Sitiari
      3. Dhihaka /stihizai
    4. Hulia huku akiunganisa (cherehani)
      1. Tashihisi
      2. Taswira
    5. Hukopa lakini halipi-(kifo)
      1. Ukinzani
      2. Tashihisi
      3. Kinaya
    6. Kisiki chetu hakikui (mbilikimo )
      1. Stihizai /kejeli
      2. Sitiari
      3. Taswira

Kufanana na Kutofanana kwa Methali na Vitendawili

  1. Methali na vitendawili hufanana kwa vile.
    1. Ni tungo fupi
    2. Huwa na maana fiche
    3. Hutumia lugha inayojenga taswira
    4. Huupata maana kulingana na jamii
    5. Hufumbata ukweli Fulani wa kijamii
    6. Huweza kutumiwa katika shughuli rasmi kama vile katika maamuzi ya kesi na utoaji hotuba.
    7. Huweza kutekeleza majukumu sawa k.m kuonya kuburudisha au kunoa bongo.
  2. Methali na vitendawili hutofautiana kama ifuatayo.
    Vitendawili Methali
    Kimuundo, huwa na fomula mahususi ya uwasilishaji Haina fomula
    Fumbo lake lazima lifumbuliwe papo hapo Fumbo halifumbuliwi hapo
    Huwa maarufu zaidi miongoni mwa watoto Huwa maarufu miongoni mwa wazee
    Hutolewa katika vikao maalum  Si lazima pawe na vikao maalumu
    Huwa na hadhira tendi Si lazima pawe na hadhira tendi
    Huwasilishwa na mtegaji na mteguaji Huwasilishwa na mtu moja tu

Misimu

  • Misimu ni semi za muda ambazo hubuniwa na kutumiwa katika mazingira maalumu katika kipindi maalumu cha wakati, msimu huitwa pia simo. Misimu inaweza kupata mashiko katika jamii na kukubaliwa kama msamiati au semi rasmi za lugha.

 

Dhima

  1. Kutambulisha makundi mbalimbali ya watu
  2. Huhifadhi siri za watumiaji
  3. Kuibua hisia mbalimbali
  4. Hukuza lugha
  5. Huhifadhi historia ya jamii.
  6. Hutasfidi lugha
  7. Hukuza uwezo wa kufikiri au kudadisi
  8. Hukuza ushirikiano na utangamano
  9. Huondoa urasmi katika mazungumzo

Sifa

  1. Misimu ni semi au msamiati ambao huzuka na kutoweka baada ya muda Fulani.
  2. Hutumiwa na wanajamii katika mawasiliano ya makundi fulani k.m kuna misimu ya vijana ya wafanyakazi katika vyombo vya usafiri na hata ya watoto.
  3. Hutumiwa na wanajamii katika mawasiliano yao katika kipindi fulani cha wakati na mahali fulani
  4. Ingawa misimu huzuka na kutoweka baada ya muda, baadhi ya misimu hudumu na kukubalika kama semi au msamiati sanifu wa lugha husika kwa mfano neno chai (kwa maana ya hongo ) lilianza kama msimu, kisha likashika na kukubalika kama msemo sanifu.
  5. Msimu hupata maana yake kutoka kwa watumiaji pamoja na muktadha wa mahali na wakati, kwa mfano neno sare ni msimu uliopata maana katika sekta ya usafiri wa matatu likimaanisha kubebwa bila malipo.

Uainishaji wa misimu

- Misimu hutofautiana kwa kutegemea

  1. Wahusika – kuna misimu ya vijana, mabaharia au wanafunzi neno beste hutumiwa na vijana kumaanisha rafiki
  2. Matilaba – kuna misimu ya kuendesha biashara neno ‘kungara ‘linamaanisha kuvaa nguo inayopendeza na ‘sare’ lina kubebwa kwenye matatu bila kulipa nauli.
  3. Vifaa- kuna misimu ya vyakula, pesa na vyombo vingine .maneno ‘nyaki’ ni nyama na ‘ashu’ ni shilingi kumi.
  4. Mahali- kila eneo huibua misimu yake.gari la uchukuzi kwa uma nchini Kenya ni ‘matatu na nchini Tanzania ni ‘daladala ‘
  5. Wakati au kipindi - misimu hubadilika kulingana na wakati au kipindi kwa mfano, wakati wa uchaguzi wa 2002 nchini Kenya kulizuka neon unbwogable lililomaanisha wasioshindwa na lika toweka katika muktadha baadaye.

Lakabu

  • Lakabu ni jina la msimbo au jina la kupanga ambalo mtu hujibandika ama hubandikwa kutokana na sifa zake za kimaumbile kitabaka, tabia au kimatendo.
  • Aghalabu lakabu huwa neno moja au fungu la maneno lililo na maana fiche au ya kisitiari sifa zinazodokezwa katika lakabu zinaweza kuwa za kusifu, kudhalilisha au kukosoa.

Sifa

  1. Lakabu si jina la mtu ni jina tu la kupangwa.
  2. Lakabu aghalau huwa neno au fugu la maneno lililo na maana iliyofumbwa.
  3. Lakabu huoana na sifa za mhusika inaweza kusifu kukejeli au kufanyia tashtiti tabia hasi ya mhusika lakabu baba wa taifa moja kwa moja inaashiria sifa nzuri za mhusika na kumsifu kwa upande mwingine lakabu kama kangumu inaashiria tabia ya uchoyo.
  4. Lakabu hupatikana katika tanzu na vipera vingine nya fasihi simulizi kama vile sifo, malumbano ya utani na majigambo (vivugo) ambapo wahusika hujipa majina ya kupanga ya kujitapa.
  5. Lakabu huundwa kwa lugha ya picha au taswira na sitiari kwa mfano, lakabu ‘nyayo’ ya Raisi mstaafu inatumia sitiari inamfananisha na nyayo za mtu hivyo kutupa taswira ya kujipata kufuata falsafa ya mtu mwingine.
  6. Ingawa lakabu si jina halisi la mtu, huweza kudumu na kufanya jina halisi la mtu kusahaulika kwa mfano Sonko.

Umuhimu/dhima

  1. Kusifiwa kwa matendo chanya ya mhusika.
  2. Hukashifu au kukejeli matendo mabaya ya mhusika.
  3. Ni kitambulisho cha mhusika husawiri tabia au hali ya mtu fulani ka maneno machache.
  4. Hutumiwa kama ishara ya hesima katika jamii ambamo kumtaja mkazamwana kwa jina lake ni mwiko, baba mkwe huibua lakabu ya kumrejelea mkazamwanawe.
  5. Hutumiwa na baadhi ya wahusika kuficha utambulisho wao baadhi ya waandishi hujibandika majina ya uandishi ili kuficha majina yao halisi.
  6. Hutumiwa na wahusika kujigamba na kujinaki katika majigambo, anayejigamba hujipa lakabu ili kujinaki na kuonyesh ubingwa wake.
  7. Hutumiwa kuhifadhi siri wakati mwingine watu humpa mtu fulani lakabu ili wanapomrejelea isijulikane ni nani.
  8. Hukuza uhusiano bora hasa miongoni mwa watani katika kutaniana watu huweza kubandikana majina.
  9. Hutumiwa kuondoa urasmi katika mahusiano ya kijamii.

Vitanza Ndimi

  • Vitanza ndimi ni kauli au sentensi zenye maneno ambayo yana mfuatano wa sauti zinazotatanisha kimatamshi.Vitanza ndimi huundwa kwa maneno yenye sauti zinazokaribiana sana kimatamshi kimsingi, katika jamii nyingi za kiafrika watu hufurahia kucheza na maneno kama njia ya burudani. Watoto kwa mfano, wana mazoea ya kucheza na maneno na sauti katika michezo na nyimbo zao

Sifa

  1. Kimsingi, vitanza ndimi ni mchezo wa maneno na sauti.
  2. Huundwa kwa maneno ambayo yana sauti zinazokaribiana kimatamshi maneno haya huweza kuwa na maana nyingi au yenye kukabiriana kimaana.
  3. Ukinzani wa maneno kisauti na kimaana huyafanya matamshi ya maneno kuutatiza ulimi.

Mifano ya vitanza ndimi

  1. Wataita wataita wataita taita.
  2. Waite wale wana wa liwali wale wali wa liwali.
  3. Cha mkufuu mwanafuu ha, akila hu, cha mwanafuu hu, akila ha.

Dhima

  • Vitanza ndimi hukuza matamshi bora mtu anapotamka kwa haraka na kwa usahihi, hutia makali stadi zake za kimatamshi. Kupitia hali hii uzoefu wa kutamka vyema hujengwa.
  • Hukuza uwezo wa kufikiri kwa haraka, baadhi ya vitanza ndimi hutatanisha kuwaza haraka ili kuteua neno sahihi la kutamka.
  •  Kuburudisha, kimsingi vitanza ndimi vilinuiwa kuibua ucheshi na kuchangamsha hadhira.
  • Hukuza ubunifu, anayebuni vitanza ndimi anahitaji kuwa na ujuzi mpana wa lugha na ubunifu ili kuteua maneno yanayokaribiana kimatamshi na kimaana.
  • Hukuza lugha, vitanza ndimi vilivyobuniwa katika vipindi mbalimbali huhifadhiwa na kupitishwa kwa vizazi vijavyo kama malighafi katika kipera cha vitanza ndimi.
  • Huhifadhi utamaduni na kuurithisha, maarifa ya kipera cha vitanza ndimi yasingehifadhiwa na kurithishwa kama vipera vingine vya fasihi simulizi, tusingevisoma leo.
  • Ni kitambulisho cha jamii, vitanza ndimi huakisi mazoea ya jamii husika kila jamii ina vitanza ndimi vyake mahususi.
  • Hujenga uhusiano bora wa kirafiki, ucheshi unaoibuliwa na vitanza ndimi hujenga uhusiano bora miongoni mwa washiriki.

Mafumbo na Chemshabonga

  • Mafumbo ni kauli zenye maana iliyojificha, mafumbo hutumia lugha fiche au ya kiistiari pamoja na tamathali nyingine za usemi. Humtaka anayeambiwa kudadisi mazingira yake na kufikiria ili kupata maana, mafumbo huchemsha bongo za wale wanaoshiriki katika kuyafumbua ingawa vitendawili ni aina za fumbo tunadai kwamba mafumbo kwa kawaida ni semi ndefu kuliko vitendawili.
  • Kuna mafumbo yaitwayo chemshabongo, chemshabongo ni maswali ambayo humtaka mtu kutumia akili na ujuzi kuyajibu. Maswali mengi ya aina hii ni ya kimapokeo, mengine hubuniwa na msemaji ili kukidhi mahitaji ya hadhira mahususi. Baadhi ya chemshabongo kwa hakika ni hesabu tu nyingine hutolewa kwa mraba unahitaji kujazwa

Mfano

  1. Nina kilo moja ya mchanga na kilo moja ya pamba kipi kizito zaidi, mchanga au pamba?
    - Jibu: vyote vina uzito sawa kwa vile uzito wavyo ni sawa (kilo moja)

Sifa

  1. Ni semi zinazofumba jambo.
  2. Huhitaji mtu kuwaza ili aweze kubuni fumbo lenyewe.
  3. Shughuli, maumbile au vitu vilivyo katika mazingira ya jamii kama vile mifugo, njia za usafiri na nyenzo za biashara vinaweza kufumbiwa.
  4. Baadhi ya mafumbo hufananisha kitu kilichotajwa katika fumbo na mazingira halisi.
  5. Baadhi ya mafumbo huwa marefu na mengine huwa mafupi.
  6. Mafumbo huhitaji mantiki ili kuyatmbua. Mfano nina chui mbuzi na majani ya kuliwa na mbuzi je nitafanya aje ili nivuke ngambo ile …

Dhima /umuhimu

  1. Hukuza uwezo na wepesi wa kufikiri ili kufumbua fumbo ni lazima mtu afikiri kwa makini na wakati mwingine kwa upesi.
  2. Hustawisha ubunifu fumbo hufumbuliwa kwa kuoanisha yaliyomo katika fumbo, tajiriba na mazingira hivyo mtu hutumia kiwango fulani cha ubunifu ili kupata maana aidha shughuli ya kufumbua huhitaji watu kuwa wabunifu.
  3. Hukuza maarifa ya kukabiliana na changamoto na kutumia mantiki kusuluhisha mambo.

Nahau

  • Nahau ni fungu la maneno ya kawaida lenye maana ambayo haitokani moja kwa moja na maana za maneno yaliyoziunda, nahau piga kalamu si kuchapa kalamu bali ni ‘kufuta mtu kazi’

    Mifano mingine ni.
    - Piga maji- Lewa.
    - Kujitia hamnazo – Kujifanya hujui.
    - Kukata kamba- Kufa.
    - Kunja jamvi- Maliza shughuli.
    - Kwenda nguu- Kukata tama.
    - Piga vijembe- Kusema kwa mafumbo.
    - Kumwaga unga- Kuachishwa kazi.
    - Ndege mbaya- Bahati mbaya.
    - Kupata jiko- Kuoa.
    - Shingo upande- Bila kutaka.

Sifa za nahau

  • Nahau huundwa kwa lugha ya mkato iliyo na ujumbe mzito wa mafumbo k.m kidudu mtu-mfitini.
  • Nahau mbili au zaidi zinaweza kuwa na maana moja k.m jamvi la wageni/bao la mkahawani –kahaba.
  • Nahau moja inaweza kuwa na maana zaidi ya moja k.m kushika mguu-kuomba radhi /kutoa shukrani kupiga mbio.
  • Maneno katika nahau hupoteza sifa zake za kawaida na kuchukua maana nyingine iliyo tofauti kabisa .k.m kula chumvi –kuwa mzee.
  •  Nahau huundwa kwa maneno mawili au zaidi. k.m kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa-danganya. Bega kwa bega - pamoja.
  • Nahau huweza kuundwa kwa mitindo mbalimbali au kwa maneno ya kategoria mbambali k.m
    1. Kitenzi na nomino –piga chuku, andika meza
    2. Kitenzi na kitezi-kufa kupona,pata shika
    3. Kitenzi na kielezi –jikaza kisabuni, kufa kikondoo
    4. Noino na nomino-askari kanzu, domo kaya
    5. Nomino na kitenzi-mguu haumshiki, damu kumkauka.
    6. Nomino na vivumishi –nyoat njema, ndege mbaya

Dhima ya Nahau

  • Nahau hukuza lugha, nahau huyapa maneno maana tofauti na maana ya kawaida kwa njia hii hupanua msamiati wa lugha.
  • Nahau huipa lugha, badala ya kutumia maneno yaliyozoeleka, nahau hutumiwa kukoleza ladha ya lugha.
  • Nahau pia hutumiwa kupunguza ukali wa jambo linalorejelewa k.m jicho la njeuasherati.Nahau huweza kutumika pia kuhifadhi siri ili wanatengwa wasielewe, si watu wote wanaoelewa maana ya nahau zote.

Misemo

  • Misemo ni semi ambazo zinabeba ukweli wa kijumla, hutumika kueleza mambo mbalimbali yanayokubali ukweli huo. Misemo hutumiwa kutoa ujumbe kwa muhtasari mfano zaidi.
    1. Binadamu ni udongo –kumaanisha binadamu aliumbwa kwa udongo na hufa na kurudi udongoni.
    2. Mwili haujengwi kwa mbao-mtu lazima ale ili apate kujenga mwili au kunenepa hauwezi kujengwa kwa mbao.
    3. Umaskini si kilema-kumaanisha kuwa mambo hubadilika ukizaliwa katika umaskini si lazima uishi na ufe ukiwa maskini.
    4. Lila na fila havitangamani –ubaya na wema hayaendi pamoja.
    5. Ndio kwanza mkoka ualike maua –kumaanisha ndio mambo yamezidi kushika kasi.
    6. Mgomba haupandwi changaraweni ukamea –jambo njema halifanywi mahali pabaya likapendeza.
  • Baadhi ya misemo hutumiwa kama methali kwa mfano, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Semi - Tanzu za Fasihi Simulizi Kiswahili Notes.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest