Mazungumzo - Tanzu za Fasihi Simulizi Kiswahili Notes

Share via Whatsapp


Utangulizi

 • Maongezi ya mdomo yenye usanii.


Sifa za Mazungumzo

 1. Huwa maongezi yenye usanii mkubwa.
 2. Hutolewa mbele ya hadhira.
 3. Hutolewa mbele ya hadhira.
 4. Hutolewa kwa njia isiyokera.
 5. Huambatana na sherehe fulani k.m. taabili katika matanga.
 6. Hutegemea sauti na vitendo.
 7. Huhusisha matumizi ya ishara k.v. za uso, mikono na miondoko.
 8. Huhitaji ustadi wa kuzungumza ili kuteka hadhira.
 9. Hutolewa na watu wenye umilisi mkubwa wa lugha.


Vipera vya Mazungumzo

1. Hotuba

 • Maelezo yanayotolewa mbele ya watu kuhusu mada fulani.
 • Huhusisha mada maalum sio suala lolote tu.

Umuhimu

 1. Kuelimisha kwa kupa maarifa ya kukabiliana na maisha k.v. jandoni na arusini.
 2. Kuadilisha au kutoa nasaha hadharani.
 3. Huimarisha ukakamavu wa kuzungumza kadiri watu wanavyotoa hotuba hadharani.
 4. Kukuza ufasaha na umilisi wa lugha.
 5. Kupalilia kipawa cha uongozi.
 6. Kuelimisha kwa kupatia watu maarifa ya kukabiliana na changamoto za maisha.

Aina za Hotuba

 1. Risala
  • Hotuba inayowasilishwa mbele ya watu kueleza jambo fulani k.m. ya wafanyakazi kwa waajiri wao.
 2. Mhadhara
  • Hotuba inayotolewa kwa hadhira fulani kufafanua somo au mada fulani.
 3. Kumbukizi
  • Hotuba zinazohusu tukio fulani la kihistoria kuhusu mtu au kitu.
 4. Mahubiri
  • Hotuba zinazohusu masuala ya kidini.
 5. Taabili
  • Hotuba kuhusu aliyeaga dunia zinazohusu sifa zake nzuri.

2. Malumbano ya Utani

 • Mazungumzo ya kutaniana.

Aina

 1. Utani wa mawifi na mashemeji
 2. Utani wa marafiki
 3. Utani wa vijana
 4. Utani wa watoto
 5. Utani wa marika/ watu wa hirimu moja
  • Wewe ni mweusi kiasi kwamba ukiingia chumbani taa zinazimika.
 6. Utani wa mababu/mabibi na wajukuu
  • Ee mume wangu, mbona walala mapema hivi? Utawezaje kulilinda boma letu ikiwa wewe ndiwe wa kwanza kujizika kitandani.
 7. Utani wa maumbu (ndugu na dada)
  • Wewe unajifanya jasiri na juzi baba alikukemea kidogo tu ukaanza kutetemeka kama kondoo aliyenyeshewa.
 8. Utani wa mazishi
  • Afadhali umekufa tukakuzika, sasa maghala yetu yatasalimika.
 9. Utani wa makabila/ki ukoo
  • Wakikuyu wanapenda pesa kiasi kwamba maiti ikisikia mlio wa sarafu inaweza kufufuka.
  • Wakamba wa ukoo wa Akanga wanapenda nyama kiasi cha kula kijusi cha mbuzi.

Sifa

 1. Huwa kati ya watu wawili au makundi mawili ya watu.
 2. Hufanywa kwa kujibizana papo hapo.
 3. Hufanywa kwa njia isiyo ya kuudhi.
 4. Hutumia maneno ya mizaha.
 5. Hutumia lugha ya ucheshi.
 6. Hufanywa na watu wenye uhusiano mzuri.
 7. Huchukua njia ya ushindani kila mmoja akitaka kumpiku mwenzake.
 8. Watanianao huwa wamekubaliana kufanya hivyo.
 9. Hufanyika katika wakati unaofaa sio baada ya kukutana tu.
 10. Huhusisha masimango au kumkumbusha mtu wema uliomtendea.
 11. Hutumia chuku sana kusisitiza au kukejeli sifa fulani hasi.
 12. Huhusisha wakati mwingine utaniaji wa wasiokuwepo ukiambatanishwa na uigizaji wa kuchekesha.
 13. Hutegemea uhusiano ulio kati ya wanajamii au makabila.
 14. Huandamana na sherehe kama matanga.

Umuhimu

 1. Kuburudisha kutokana na ucheshi.
 2. Kuimarisha urafiki wa watu walio na uhusiano mwema wanaotaniana.
 3. Hustawisha ufundi wa lugha.
 4. Kukashifu tabia hasi k.v. ulafi, uchoyo, wivu, n.k.
 5. Kukosoa wanajamii kwa njia ya kejeli/dhihaka
 6. Kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya wahusika.
 7. Kuliwaza k.m. unaofanywa wakati wa maombolezo.
 8. Kukuza na kudumisha mila na desturi za jamii.
 9. Kukuza utangamano baina ya watu na wanajamii wanapokuja pamoja na kutaniana.
 10. Kuhimiza watu kujieleza kwa uwazi kwa kupunguza urasmi miongoni mwa wanajaii.
 11. Hudhihirisha uhusiano mwema baina ya watu wa jamii fulani.

Changamoto Sasa

 1. Mabadiliko katika jamii yaliyosababisha baadhi ya wanajamii kupoteza nyenzo hii.
 2. Kuingiliana kwa watu wa jamii mbalimbali.

3. Soga

 • Mazungumzo ya kupitisha wakati yasiyozingatia mada maalum.

Sifa

 1. Hutokea baina ya watu wa rika moja.
 2. Humithilisha uhalisia badala ya kuunakili.
 3. Hutumia chuku na kufanywa ljambo lionekane kama halina uhalisia.
 4. Hukejeli watu au hali fulani.
 5. Wahusika ni wa kubuni.
 6. Hutumia vichekesho kupunguza ukali wa ukweli uliomo.
 7. Wahusika hupewa majina ya wanajamii husika.
 8. Huwa na mafunzo au maadili.

Umuhimu

 1. Kuburudisha kwa kuchekesha.
 2. Kufunza maadili.
 3. Kukejeli matendo yasiyofaa katika jamii
 4. Kukuza ubunifu baina ya washiriki.
 5. Kufunza kuhusu matendo na tabia za kibinadamu.
 6. Huwa msingi wa utani unaokuwapo katika jamii.
 7. Kuonya na kutahadharisha dhidi ya tabia siyokubalika.

4. Mawaidha

 • Mazungumzo ya kutoa ushauri kuhusu jambo fulani.

Sifa

 1. Huwasilishwa mbele ya watu.
 2. Hugusia takriban vipengele vyote vya maisha ya binadamu.
 3. Aghalabu hutolewa na watu wenye umri mkubwa.
 4. Hulenga maudhui maalum na ya aina nyingi kutegemea jinsia, umri, shughuli, n.k.
 5. Hutumia lugha ya kubembeleza na isiyoonyesha ukali.
 6. Hutumia lugha ya kuathiri hisia.
 7. Huwa na ufasaha mkubwa wa lugha.
 8. Ni mawazo mazito kuhusu maisha.
 9. Hutolewa katika miktadha rasmi na isiyo rasmi.
 10. Ujumbe hulenga hadhira maalum k.m. ya kike au kiume.
 11. Hutumia fani nyingine za fasihi kama methali, misemo, ngano, nyimbo n.k. kupitisha mawaidha.
 12. Huibua maadili yanayohitaji kuzingatiwa.

Muundo wa Mawaidha

 1. Utangulizi
  • Kutoa kauli ya kuvutia makini ya hadhira k.v. ‘Utu uzima huenda na uwajibikaji’, au kueleza kiini cha mawaidha.
 2. Mwili
  • Kutoa wosia, maonyo, maelekezo kutegemea suala analotolea mawaidha akitumia jazanda, kupanda na kushuka kwa sauti, kimya, miondoko, kubadilisha kasi ya kuzungumza, kudondoa semi za watu maarufu, n.k.
 3. Hitimisho
  • Kuonyesha msimamo kuhusiana na suala analozungumzia.
  • Kushirikisha hadhira ili kujua msimamo wao kuhusu suala alilowausia.
  • Hadhira kutoa changamoto kuhusiana na mawaidha yanayotolewa.

Umuhimu wa mawaidha

 1. Kuelekeza jamii kimaadili.
 2. Kuelekeza kuhusu jinsi ya kukabiliana na changa moto maishani.
 3. Kushauri jinsi ya kutenda jambo fulani.
 4. Kujasirisha waoga na kuwapa ukakamavu.
 5. Kuwaondolea wanajamii ujinga.
 6. Kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi za jamii.
 7. Njia ya kipato kwa baadhi ya watu.
 8. Kuelimisha kuhusu maarifa ya kuendeshea maisha, majukumu na matarajio ya jamii.

5. Ulumbi

 • Uwezo na ustadi wa kuzungumza kwa uhodari mkubwa.

Miktadha Ambamo Ulumbi Hutumika Katika Jamii

 1. katika mijadala mbungeni
 2. katika hotuba za kisiasa
 3. katika mahubiri maabadini
 4. katika mijadala shuleni
 5. kortini
 6. katika shughuli za kijamii k.v. posa
 7. katika sala/dua
 8. katika maapizo
 9. katika malumbano ya utani
 10. katika majigambo/vivugo

Sifa

 1. Hufanywa mbele ya hadhira.
 2. Huwa na lengo maalum k.v. kushawishi, kuelimisha, kushauri n.k.
 3. Hutumia tamathali za usemi kwa ufanifu mkubwa k.v. chuku, misemo, methali, n.k.
 4. Lugha huwa yenye mvuto na ufasaha.
 5. Hutumia lugha yenye taharuki na ushawishi.
 6. Unenaji huambatana na utumizi wa ishara/ viziada lugha.
 7. Uwasilishaji huwa sahili na wenye ujumbe mzito.
 8. Huwa na urudiaji mwingi ili kusisitiza na kuvutia usikivu.
 9. Huwa na matumizi ya taharuki k.v. mtuo.
 10. Huwa na mtiririko mzuri wa mawazo.

Sifa za Mlumbi

 1. Asiwe mwoga ili kuweza kuzungumza hadharani.
 2. Asiwe na haya ili kuweza kuzungumzia mambo ya aibu inapobidi.
 3. Awe mchanganfu na mcheshi ili kunasa makini ya hadhira na kuzuia isikinai.
 4. Awe na ufahamu mpana wa utamaduni wa hadhira asitumie maneno na ishara zinazoweza kuwaudhi au kupingana na imani za hadhira.
 5. Awe na uwezo wa kuingiliana vizuri na hadhira ili aivutie.
 6. Awe na kumbukumbu nzuri ili ulumbi wake utiririke vizuri.
 7. Awe na uwezo wa kudramatisha ili kuonyesha picha fulani k.v. ishara za uso, mwili, miondoko kuonyesha picha ya analozungumzia.
 8. Awe na ujuzi na ufasaha wa lugha ili kuwasilisha mawazo kwa njia mwafaka na inayovutia.
 9. Aweze kubadilisha toni na kiimbo hadhira isikinai.
 10. Awe na uwezo wa kushirikisha hadhira k.v. kwa maswali ya balagha ili kuondoa uchovu wa kusikiliza.
 11. Awe na uwezo wa kutumia mtuo wa kidrama ili kuongeza taharuki, kusisitiza ujumbe na kuteka makini ya hadhira.

Umuhimu

 1. Hukuza uwezo wa kujieleza na kusema hadharani kwa kujiboresha kadiri anavyoendelea.
 2. Kigezo cha kuteulia viongozi wa baadaye kwani ushawishi humtambulisha mlumbi kama mwenye uwezo wa kuongoza.
 3. Kuelimisha jamii kwa njia isiyochosha.
 4. Kudumisha umoja na ushirikiano jamii inapokusanyika pamoja kusikilizaulumbi.
 5. Kuhamasisha na kuzindua jamii juu ya suala fulani.
 6. Kushawishi walengwa wakubali jambo fulani.
 7. Kukuza uwezo wa mwanajamii kushawishi na kupatanisha.
 8. Kushawishi watu wapende jambo fulani.
 9. Kuburudisha wasililizaji.

6. Maapizo

 • Maombi maalum ya kumtaka Mungu, miungu au mizimu kumwadhibu mhusika hasidi, mkinzani au muovu.

Mfano

Ikiwa kweli wewe ni mkazamwanangu,
Nami ndiye nilompa uhai mwana unoringia,
Anokufanya upite ukinitemea mate,
Chakula kuninyima, wajukuu kunikataza ushirika,
Miungu nawaone chozi langu, wasikie kilio changu,

Mizimu nawaone uchungu wangu,
Radhi zao wasiwahi kukupa,
Laana wakumiminie,
Uje kulizwa mara mia na wanao,
Usiwahi kufurahia hata siku moja pato lao,
Watalokupa likuletee simanzi badala ya furaha,
Wakazawanao wasikuuguze katika utu uzima wako!

Sifa

 1. Yalitolewa kwa waliokwenda kinyume na matarajio ya jamii.
 2. Yalifanywa mahali maalum k.v. makaburini, porini, chini ya miti mikubwa, n.k.
 3. Hutolewa kwa ulaji kiapo.
 4. Yalitolewa na mwathiriwa au watu maalum walioteuliwa.
 5. Maapizo huaminiwa yataleta maafa kwa jamii.
 6. Watoaji maapizo walikuwa walumbi.
 7. Maapizo hutumia lugha kali inayonuiwa kutia woga ili kutahadharisha dhidi ya maovu.

Umuhimu

 1. Kuonya na kutahadharisha wanajamii dhidi ya maovu.
 2. Kutambulisha jamii kwani kila mojawapo ina aina yake ya kuapiza.
 3. Kukuza umoja katika jamii kwani kaida na miiko hufanya wanajamii kujihisi kuwa kitu kimoja.
 4. Kuadilisha wanajamii kwa kujifunza kutenda mema ili kuepuka laana.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Mazungumzo - Tanzu za Fasihi Simulizi Kiswahili Notes.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest