Utangulizi wa Isimu Jamii - Isimu Jamii Notes

Share via Whatsapp

 



Utangulizi

Isimu Jamii (social linguistcs) - ni tawi la isimu (elimu ya lugha) linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia.

Isimu- ni uchunguzi wa lugha kisayansi.

Jamii – ni kundi filani la watu wenye uhusiano fulani.



Mambo Yanayoshughulikiwa Katika Isimu Jamii

  1. Tofauti katika lahaja za lugha kama vile Kiswahili cha lamu(kiamu), cha Mombasa(kimvita), cha unguja(kiunguja), cha bara.
  2. Tofauti katika matumizi ya lugha baina ya makundi tofauti tofauti katika jamii. Mfano wazee na watoto,vijana na wabunge.
  3. Matumizi ya lugha kutegemea miktadha tofauti kama vile kazini, nyumbani, sokoni, n.k.
  4. Mtazamo wa watu kuhusu lugha. Je, wanaitukuza au wanaitweza?
  5. Jinsi mtu anavyotumia lugha kutegemea uhusiano na wazungumzaji au mada husika.
  6. Lahaja mbalimbali za lugha ya Kiswahili.


Umuhimu wa Isimu Jamii

  1. Huwafunza watu kaida za lugha ili waweze kuitumia ipasavyo kutegemea mila na desturi.
  2. Humsaidia mzungumzaji au mwandishi kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha na usahihi.
  3. Humpa anayetumia lugha uwezo wa kutambua, kutofautisha na kutumia mitindo mbalimbali ya lugha kutegemea mahitaji.
  4. Hufunza maadili ya jamii hasa yanayohusiana na matumizi ya lugha kutegemea uhusiano. Mf. Mtu na mkwewe, mtoto na mzazi, mwajiri na mwajiriwa.
  5. Hufunza mbinu za mawasiliano pamoja na mbinu za kupata maana kamili.
  6. Hudhihirisha utamaduni wa jamii.
  7. Humsaidia msemaji au mwandishi kutambua makosa mbalimbali yanayojitokeza wakati wa kuzungumza au kuandika.
  8. Hufunza mbinu za kuwaelewa watu tunaotagusana


Maana ya Mawasiliano

Utaratibu ambao huwawezesha viumbe kupashana ujumbe ambao unahusisha mwasilishi na mpokeaji wa ujumbe.

Njia Ambazo Kwazo Mwanadamu Huwasiliana

  1. Mgusano na ukaribianaji
  2. Mavazi
  3. Sauti
  4. Ishara za mwili.


Lugha

Ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa na wanadamu katika mawasiliano.

 

 

Sifa za Lugha

  1. Hakuna lugha iliyo bora kushinda zingine. –zote ni sawa.
  2. Kila lugha ina sifa zake.
  3. Lugha hubadilika kutegemea mazingira, aina ya tukio, wakati na matumizi ya lugha hiyo.
  4. Lugha ina uwezo kukua, mfano Kiswahili kimebuni msamiati TEHAMA (Teknolojia ya habari na mawasiliano.)
  5. Lugha pia hufa kwa msamiati wake kupotea n.k

Sababu za Kufa/Kufifia kwa Lugha.

  1. Lugha moja kusonewa hadhi na isiyoonewa hadhi hufifia.
  2. Sababu za kiuchumi – watu huishi mijini na kuacha lugha ya kwanza.
  3. Lugha kuwa na idadi ndogo ya wazungumzaji.
  4. Ndoa za mseto.
  5. Kuhamia kwingine – watu huishi na kuingiliana na kundi jingine.
  6. Mielekeo ya watu – wanapoipendelea lugha moja na kuidharau nyingine.
  7. Kisiasa – Lugha moja kupendelewa kuliko nyingine na viongozi.

Umuhimu wa Lugha

  1. Hutumika kwa mawasiliano.
  2. Lugha ni chombo ambacho hutusaidia kujieleza na kutoa mawazo yetu.
  3. Hujenga uhusiano baina ya watu.
  4. Ni kitambulisho cha taifa, mtu binafsi na utamaduni.
  5. Lugha ni chemchemi ya uchumi mf. Mtangazaji au mwalimu wa Kiswahili.
  6. Huweza kuunganisha watu kama jamii moja.


Istilahi za Isimu Jamii

Isimu (linguistics)

Ni mtalaa ambao huchunguza, huchanganua na pia kuchambua na kufafanua lugha kama mfumo wa mawasiliano baina ya wanadamu.

Lugha

Ni chombo cha mawasiliano baina ya watu. Lugha huzingatia mpangilio maalum wa sauti, maneno na sentensi.

Sajili

Ni mukhtadha/rejista mbalimbali au mitindo maalum ya lugha katika mazingira/hali mbalimbali. Mifano ya sajili ni kama vile lugha ya hospitalini, shuleni, sajili ya dini, biashara, kisiasa, michezo,

Fonolojia

Ni tawi la sayansi ya isimu linaloshughulikia uchunguzi wa mfumo wa sauti katika lugha fulani, kwa mfano ugawanyaji wa irabu na konsonanti. Fonolojia hutumika kuunda alfabeti katika lugha fulani. Aghalabu kila lugha hutumia mfumo fulani wa sauti mahususi katika lugha hiyo pekee.

Fonetiki

Huchunguza sauti zinazotamkwa na binadamu bila kuzingatia lugha yoyote.

Mofolojia (au sarufi maumbo)

Ni tawi la isimu linalochunguza maneno ya lugha fulani, aina za maneno katika lugha, hasa upangaji wa mofimu mbalimbali zitumikazo kwa ajili ya kuunda maneno hayo. Kwa mfano, lugha ya Kiswahili hutumia mbinu kadhaa kuunda maneno kulingana na mpangilio wa mofimu. Kwa mfano, neno 'lima' linaweza kutumika kuunda maneno mengine katika Kiswahili k.m mkulima, kilimo, nimelima, limika n.k Katika kubadilisha mofimu hizi, tunaweza kubadilisha neno moja kutoka aina moja(kitenzi) hadi nyingine (nomino) n.k

Sintaksi (au sarufi miundo)

Ni tawi la isimu au taaluma ya sarufi inayoshughulikia jinsi vikundi vya maneno na sentensi mbalimbali zinajengwa katika lugha. Sintaksia huangazia kanuni au sheria za lugha. Kila lugha huwa na sheria zake za kuambatanisha maneno kama vile jinsi ya kufuatanisha vitenzi, nomino na vielezi. Kwa mfano: Mtoto yako shiba ni sentensi isiyokuwa na sintaksi. Sentensi sawa ingekuwa: Mtoto wako ameshiba.

Semantiki

Ni tawi la isimu linalochunguza maana halisia (mantiki) ya maneno, kifungu au sentensi katika lugha. Sentensi isiyokuwa na mantiki ni sentensi inayotoa maana ambayo haiwezekani katika uhalisia. Sentensi inaweza kuwa sawa kisintaksia lakini iwe na makosa ya kimantiki. Kwa mfano: Kiatu cha mbwa kimefutwa kazi kwa sababu kumi ni kubwa kama hewa.

Diglosia

Hali ya kuwa na lugha mbili tofauti katika taifa, zilizo na majukumu tofauti k.m nchini Kenya Kiswahili ni lugha ya taifa, Kiingereza ni lugha ya ofisini/rasmi.

Polyglosia

Hali ya kuwa na lugha nyingi tofauti(zaidi ya tatu) katika taifa, zilizo na majukumu tofauti.



Aina za Lugha Katika Isimu Jamii

Lafudhi

Ni upekee wa mtu katika matamshi (accent) unaoathiriwa na lugha ya mama, mazingira yake ya kijiografia au kiwango ujuzi wake wa lugha. Mfano: rara badala ya lala, papa badala ya baba.

Sababu za kuwa na lafudhi.

  1. Kwa sababu za athari ya lugha ya mama.
  2. Kwa sababu za athari ya lugha zingine zinazomzunguka mzungumzaji.
  3. Kwa sababu ya kasoro fulani iliyoko katika ala za matamshi za mzungumzaji.

Lahaja

Ni vijilugha vinavyoibuka kwa lugha moja kuu kutokana na tofauti za kijiografia baina ya wazungumzaji wa lugha hiyo. Kwa mfano lugha ya Kiswahili ina lahaja kadhaa kama vile Kimtang'ata, Kilamu, Kimvita, n.k. Tofauti baina ya lufudhi ni kama msamiati, muundo wa sentensi au matamshi.

Lugha rasmi

Ni lugha inayotumika katika shughuli za kiofisi ama ya wakati wa mawasiliano rasmi katika taifa fulani. Kwa mfano, lugha rasmi nchini Kenya ni Kiingereza.

 

Lugha rasimi

Ni mtindo wa lugha uliotumiwa na mtu/watu fulani mashuhuri (zamani) na ambao huonekana kuwa mtindo bora wa lugha unaofaa kuigwa na wengine. Kwa mfano lugha ya Shakespeare.

Lugha ya taifa

Ni lugha inayoteuliwa na taifa fulani kama chombo cha mawasiliano baina ya wananchi, kwa maana inazungumzwa na wananchi wengi katika taifa hilo. Lugha ya taifa, nchini Kenya ni Kiswahili; Uganda ni Kiganda.

Lugha Sanifu

Ni lugha iliyokarabatiwa na sheria zake (k.v muundo wa sentensi, msamiati, sarufi, n.k) kubainishwa na kuandikwa, na kwa hivyo huzingatia sarufi maalum na upatanisho sahihi wa sentensi. Kwa mfano: Kiswahili sanifu - ni lugha isiyokuwa na makosa ya kisarufi.

Lingua Franka

Ni lugha inayoteuliwa miongoni watu wenye asili tofauti wasiozungumza lugha moja ili iwe lugha ya kuwaunganisha katika shughuli rasmi au za kibiashara.

Sifa za lingua franka

  1. Huwa ni lugha ua mawasiliano kati ya watu wenye lugha zaidi ya moja.
  2. Yaweza kuwa lugha ya kwanza ya mzungumzaji au lugha ya pili na kwa watu wengine lugha wa kigeni
  3. Hukiuka mipaka ya kitamaduni
  4. Hukutanisha watu wa asili mbalimbali.
  5. Hukiuka mipaka ua kimaeneo - inaweza kutumiwa katika maeneo mapana.
  6. Hutumiwa na watu ambao lugha zao za mama ni tofauti.

Umuhimu wa lingua franka

  1. Huleta ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama vile, kibiashara, kiuchumi, kielimu, kidini nk
  2. Huleta umoja miongoni mwa watumiaji wake hasa wale wenye tamaduni tofauti
  3. Hurahisisha mawasiliano hasa katika jamii inayogawika katika misingi ya lugha.

Njia za uzambazaji wa linguafranka

  1. Vita- kwa mfano lugha ya kigiriki iliweza kueneza kupitia vita. Kifaransa pia kilienezwa kupitia vita hasa wakati wa utawala wa Napoleon Bornaparte
  2. Biashara- kisawhili kimeweza kuenea kutokana na dhima yake katika biashara
  3. Ukoloni- kifaransa, kiingereza na kireno zimeweza kuenea kupitia utawala kama nyenzo
  4. Elimu- lugha kama kiingereza zimeweza kuenezwa kwa kutumika kwenye mafunzo katika nchi nyingi za ulimwengu
  5. Nguvu za kisayansi na teknolojia- Nguvu za kisayansi na teknolojia za Amerika zimechangia kuenea kwa kiingereza katika ulimwengu hasa kwa sababu ya istilahi mpya zinazoibika kila uchao.

Pijini

Ni lugha inayozaliwa kutokana na mchanganyo wa lugha zaidi ya moja. Kwa mfano. Sheng' (lugha ya vijana mitaani nchini ni lugha iliyoibuka kutoka kwa Kiswahili na Kiingereza).

 

Sifa za pijini

  1. Haina wazungumzaji asilia.
  2. Huwa sahili na irabu za kawaida.
  3. Haijakomaa kimsamiati.
  4. Hukiuka kanuni za lugha.
  5. Huwa haina wenyeji au wazungumzaji wazawa.
  6. Hutumia ishara kwa sababu ya uhaba wa msamiati.

Krioli

Ni pijini iliyokomaa na kukubalika.

Sifa za krioli

  1. Huwa na wenyeji kwa mfano; Krioli ya Haiti, Kridi ya Jamaica
  2. Huwa na miundo thabiti ya kisarufi.
  3. Huwa na msamiati shabiti unaoweza kutungiwa kamusi.
  4. Huwa na matumizi mapana katika Nyanja za siasa, muziki, vyombo vya habari na kadhalika.

Lugha mame

hii ni lugha isiyokua na ambayo hubaki kati umbo lake la awali. Kwa mfano lugha ya Kilatini haibadiliki na hivyo hutumika katika kubuni majina ya kisayansi, n.k.

Lugha azali

Ni lugha inayozaa lugha nyinginezo.

Misimu

ni lugha yenye maneno ya kisiri ambayo hutumiwa na kikundi fulani cha watu katika jamii, inayoeleweka tu baina yao. Misimu huibuka na kutoweka baada ya muda.

Uwili lugha

Uwezo wa mtu kuzungumza lugha mbili.

Sababu zinazochangia kuwepo kwa uwingi lugha

  1. Ndoa za mseto
  2. Ujirani wa makabila / mataifa tofauti
  3. Sera za lugha za wakoloni.
  4. Sera za lugha za nchi.-lugha rasmi na lugha ya taifa huweza kuwa tofauti.
  5. Mavamizi / vita huwalazimu wananchi kuhamia kwingine hivyo kuwafanya kujifunza lugha geni.
  6. Dini
  7. Elimu
  8. Umataifa / udiplomasia
  9. Uchumi na biashara
  10. Mwingiliano wa watu katika jamii.

Aina za uwililugha

  1. Uwililugha sawia - Hii ni hali ya kuwa na uwezo wa kuzimudu zile lugha mbili
  2. Uwililugha kupendelea - Ni hali ya kuwa na mwegemeo wa kuionea fahari mojawapo ya lugha unazozijua
  3. Uwililugha kupokea - Hii ni hali ya kujibu lugha moja kutumia nyingine, kwa mfano mtoto anapozungumziwa kiingereza akajibu kwa Kiswahili
  4. Uwililugha uliolala - Ni hali ya kuwa ugenini na kulazimika kuisahau lugha yake kwa muda.
  5. Uwililugha mfu - Ni hali ya lugha moja kumezwa au kufifia na kutotumika tena.

Tofauti Kati ya Kuchanganya Ndimi na Kuhamisha Ndimi

  1. Kuchanganya ndimi – hali ya kutumia zaidi ya lugha moja katika mawasiliano . matumizi haya hujikita katika sentensi moja / mzungumzaji anatoka kidogo katika lugha moja na kuingilia nyingine kasha akarejelea lugha awali.
  2. Kuhamisha ndimi – kubadilisha mkondo wa mazungumzo kutoka lugha moja hadi nyingine ambapo msemaji ana umilisi wa zaidi ya lugha mbili.

Sababu za kuchanganya na kuhamisha ndimi

  1. Kupungukiwa na msamiati wa kutumia
  2. Kujitambulisha na kundi fulani la watu mf waliosoma, wanahirimu n.k
  3. Kujihusisha na lugha inayoenewa fahari
  4. Kutaka kuonyesha kuwa una uwezo wa kutumia lugha mbili au zaidi
  5. Kutaka kufafanua dhana fulani k.m uyoka (x-ray)


Kaida katika jamii ambazo matumizi ya lugha hutegemea

Mazingira/muktadha

Hutegemea mazingira ya wazungumzaji k.v. ofisi, sokoni, mahakamani, kanisani n.k.

Umri

Vijana wana namna ya kutumia lugha inayojihusisha na mitindo mipya tofauti na wazee wanaotumia msamiati wenye hekima na ushauri

Uhusiano

Kuna mahusiano ya aina nyingi, kwa mfano mtoto atatumia lugha kwa njia tofauti katika kuwasiliana na wazazi wake tofauti na vile atazungumza na watoto wa rika lake

Jinsia/uana

Unyenyekevu hujitokeza katika mazungumzo ya wanawake ambayo ni tofauti na ya wanaume. Lugha ya wanaume huwa na fujo, kiburi na hali ya kutojali sana. Wanawake watajikita katika mapambo ilhali wanaumewatajikita katika siasa.

Madhumuni/lengo

Lengo la mzungumzaji humlazimu kuchagua mtindo atakaoutumia kuufikisha ujumbe wake.

Mada

Swala linalozungumziwa hulazimu mtu kuteua msamiati unaohusiana na mada yenyewe. Kwa mfano, iwapo ni kuhusu kilimo, msamiati wa ukulima utatamalaki mazungumzo

Hali ya mtu

Mgonjwa atazungumza kwa upole wakati mlevi atazungumza kiholela bila kuchagua maneno

Cheo cha mtu/hadhi

Madaraka ya mtu huchangia msamiati wa kutumia. Hali ya kuamuru hujitokeza katika lugha ya waajiri ilhali upole na adabu hutumiwa na waajiriwa.

Utabaka

Hadhi ya mzungumzaji inaweza kuathiri uchaguzi wa msamiati. Watu wa tabaka la juu watapenda kuchagua maneno ya kifahari ilhali wale wa tabaka la chini watatumia maneno ya kawaida.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Utangulizi wa Isimu Jamii - Isimu Jamii Notes.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Read 67427 times Last modified on Thursday, 08 October 2020 06:55
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest