Utangulizi - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp

Utangulizi

Mwongozo huu una nia ya kuwa mwanga gizani kwa wasomi wa diwani ya ‘Mapambazuko ya Machweo na Hadithi nyingine, kwa kutoa maelezo maridhawa kuhusiana na hadithi tofauti zilizomo humu.

Ili kufanikisha hili, mwongozo huu umeangazia masuala kadhaa katika hadithi.

Kabla ya kwenda katika hadithi binafsi, ni vyema kuangazia vipengele Fulani vya diwani. 

Mada: Mapambazuko ya Machweo. 

Mada ya diwani za hadithi fupi huwa ni mada ya mojawapo wa hadithi zilizomo.

Hata hivyo, sharti iwe mada ya kuvutia wasomaji na pia yenye kubeba uzito katika diwani husika.

Lnafaa kuwa mada ambayo ina uzito wa kutosha kubeba ujumbe wa diwani. 

Mada ‘Mapambazuko ya Machweo’, ina athari ya kipekee kwa msomaji.

Mapambazuko ni majira ya alfajiri, kabla ya jua kuchomoza hali Machweo ni wakati wa jioni, jua linapotua.

Ukinzani katika mada unazua taharuki kwa msomaji, ambayo inamtuma kupitia hadithi za diwani hiyo ili kufahamu vipi Mambazuko yanatukia wakati wa Machweo.  

Mada hii inaleta fikra tofauti. Kwanza, ujumbe wake unaweza kurejelea hali ya mafanikio baada ya tabu tele.

Isitoshe, majira haya yananweza kurejelea umri, mapambazuko yakirejelea ujana nayo machweo uzee.

Inaweza pia kumaanisha mafanikio katika machweo ya maisha(uzee).  

Mada hii, hivyo basi, inabeba taarifa muhimu kwa ajili ya diwani nzima.

Suala la matumaini au mafanikio katika/baada ya taabu limesawiriwa katika hadithi nyingi kwenye diwani hii.

Hivyo, tunaweza kusema mada hii imefumbata ujumbe wa diwani nzima.

Mifani ya hadithi zinazodhihirisha hali ya ‘Mapambazuko ya Machweo’ ni kama’Mapambazuko ya Machweo’, ‘Fadhila za Punda’, ‘Toba ya Kalia’, ‘Nipe Nafasi’, ‘Ahadi ni Deni’, ‘Sabina’ na nyinginezo.

Hivyo basi, ni wazi kwamba mada ‘Mapambazuko ya Machweo’ inafaa kabisa kwa diwani hii.  

Jalada:

Jalada katika diwani ya hadithi fupi aghalabu hubeba ujumbe wa hadithi iliyobeba anwani.

Hali si tofauti katika diwani hii. Jalada linaakisi hali katika hadithi ya ‘Mapambazuko ya Machweo. 

Kuna bwana aliyevaa suti ambaye anaingia kwenye gari. Haikosi huyo ni Makutwa, anayemiliki gari la kibinafsi pekee mjini Kazakamba. 

Kando yake, kuna mwanamume na mwanamke wanaoonekana kuwa katika hali ya majibizano kwa jinsi walivyoinua mikono, mwanamume mkono wa kulia na mwnamke mkono wa kushoto nyuso zikielekeana.

Hawa bila shaka ni Makucha na mkewe Macheo ambao wana mjadala mara kwa mara kuhusiana na suala la Makutwa kumkebehi Makucha.  

Kando ya wawili hao pembeni kulia, kuna kimeza kidogo chenye vifaa fulani na kiti chake. Haikosi hapo ni sehemu anapouzia vitafunio Makucha.

Pembeni kulia kulia nako kuna sehemu ya nyumba, ambayo itakuwa ya Makucha na mkewe Macheo.  

Mbele yao mbali kidogo, kuna watoto wadogo wanaoonekana kuwa katika shughuli za kuzoa mchanga.

Hawa ni watoto ambao Makutwa anawatumikisha katika mgodi wake kinyume cha sheria.  

Hali ya anga inadhihirisha kwamba ni wakati wa machweo. Kuna jua ambalo linaelekea kutua na anga imetamalaki rangi ya samawati.

Mchanga walikokanyaga wahusika wote unatuhakikishia ni mandhari ya mji wa Kazakamba.  

Kuutumia Mwongozo.

Mwongozo huu umechambua kila hadithi kwa mapana na marefu.

Umeangazia masuala tofauti tofauti katika hadithi zote, ili kuhakikisha kwamba maomaji anaelewa yanayoshughulikiwa kwa ubainifu wa kipekee.

Masuala haya yanaanzia kwa mtiririko wa hadithi na ufaafu wa anwani hadi mitindo ya uandishi.

Masuala yaliyoshughulikiwa ni pamoja na;  

Dhamira ya Mwandishi.

Ni lengo la mwandishi, yaani sababu ya kuandika hadithi husika.

Inaeleza ujumbe ambao mwandishi alinuia kupitisha kwa msomaji. Inaweza pia kuelezwa kama mafunzo ambayo msomaji anapata kutokana na kusoma hadithi husika.

Dhamira inaweza kuwa kupitisha ujumbe kwa njia tofauti ikiwemo kuonya, kusawiri hali Fulani katika jamii au kuelimisha kuhusu suala fulani.

Maudhui

Ni masuala nyeti yanayoshughulikiwa katika hadithi. Ni mambo makuu hasa kuhusu jamii yanayoibuka kutokana na kusoma hadithi Fulani.

Baadhi ya maudhui yanayojitokeza katika hadithi nyingi ni pamoja na elimu, utamaduni, mapenzi na ndoa, migogoro na migongano, uzinzi, ulaghai na unafiki, usaliti, nafasi ya mwanamke, ubabaedume na mengi mengine.  

Wahusika

Ni watu au viumbe ambao wanatumiwa na mwandishi kuwasilisha ujumbe wake kwa hadhira.

Katika hadithi zote, wahusika waliotumika ni binadamu, wanaoakisi jamii halisi.

Wahusika hawa hutofautiana kwa hulka(sifa) kulingana na ujumbe toofauti ambao mwandishi anawatumia kupitisha.

Hivyo basi, kila mhusika, wahusika wakuu na wasaidizi huwa na sifa zake na umuhimu katika hadithi.  

Mbinu za Uandishi. Ili kuleta mvuto, mwandishi hawezi kutumia lugha iliyo kavu.

Lazima aifinyange lugha na kuisuka kipekee ili kuleta mnato kwa msomaji anapoanza kupitia kazi yake.

Kuna aina tofauti za mitindo ya uandishi ambayo hutumika kutimiza hili.

1. Istilahi za Lugha/ Tamathali za Usemi  

Tashbihi/Tashbiha/Mshabaha.

Hii ni mbinu ya kufananisha vitu viwili vyenye sifa sawa kwa kutumia vihusishi vya ulinganisho kama vile mithili ya, kama, sawasawa na, mfano wa na nyinginezo.

Kwa mfano; Kamau ni mrefu mithili ya twiga.

Istiara/Sitiari.

Hii ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili vyenye sifa sawa moja kwa moja bila kutumia vihusishi vyovyote.

Kwa mfano; Siku hizi amekuwa wali wa daku(yaani ameadimika, haonekani) 

Tashihisi/Uhuishi/Uhaishaji.

Ni mbinu ya kuvipa sifa za uhai vitu visivyo na uhai kama vile kuongea, kutangamana na kutekeleza mambo ya kibinadamu.

Kwa mfano; hofu ilimkumbatia. 

Methali.

Ni tungo fupi zilizogawika katika sehemu mbili ambazo hubeba ujumbe wenye hekima.

Huwa na maana ya juu, inayotokana na maneno yaliyotumiwa na maana ya ndani isiyohusiana na maneno hayo, ambayo huongoza matumizi yake.

Kwa mfano; mla na miwili hana mwisho mwema. 

Semi(Misemo na Nahau).

Ni tungo fupi zinaoundwa kwa kuunganisha maneno, na ambazo maana yake na matumizi huwa tofauti na maneno yaliyotumika.

Kwa mfano; enda segemnege- haribika, enda kombo. 

Takriri/ Uradidi.

Ni mbinu ya kurudiarudia neno au fungu la maneno kwa nia ya kutilia mkazo hoja fulani au kusisitiza.

Uradidi huu unawea kutumiwa na mwandishi moja kwa moja katika usimulizi au ukatumiwa na mhusika katika mazungumzo.

Kwa mfano;misitu kwa misitu ya mahindi na maharagwe. 

Tabaini.

Ni mbinu ya kutumia ukinzani kwa nia ya kudhihirisha wingi.

Aghalabu hudhihirika kwamatumizi ya ‘si’ ya ukanushi.

Kwa mfano; kila kitu kwake kilipendeza, si macho, si uso, si mavazi, si viatu, si sauti. 

Chuku.

Ni matumizi ya maelezo yaliyotiliwa chumvi kwa ajili ya kuonyesha uzito wa jambo au hoja fulani, na pia kumtumbuiza msomaji.

Maelezo huelezwa kwa kiasi cha kuchekesha, kwani huzua hali ambazo ni wazi haziwezekani, lakini zinazokubalika kifasihi.

Kwa mfano; hasira zake zingeweza kuivunja bilauri kwa kuiangalia tu. 

Balagha/Maswali Balagha.

Ni mbinu ya kutumia maswali yasiyohitaji majibu, kwa kuwa aidha majibu yako wazi, hayapo au hayahitajiki.

Maswali haya husaidia kuelewa fikra za mhusika, kutoa taarifa zaidi au kumchochea msomaji kuwaza zaidi.

Kwa mfano; kwa nini haya yanipate mimi? 

Uzungumzi Nafsia/Monolojia.

Ni mbinu ambapo mhusika hujizungumzia mwenyewe aidha kwa sauti au akilini.

Huwezesha msomaji kujua mawazo, maoni au mipango ya mhusika.

Kwa mfano; “Muradi haya yashatokea, sina budi kukubali,” Mercy alijisemea moyoni. 

Tanakali/ Tanakali za Sauti.

Ni mbinu ya kuiga milio au sauti zinazotokea katika hali tofauti za kimazingira au sauti za wanyama na vitu tofauti.

Kwa mfano; kriii! Kriii! Kriii! Simu yangu ilikiriza. 

Dayolojia.

Ni mbinu ya kutumia mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wahusika wawili katika usemi halisi. Mawasiliano haya huhusu mada fulani wanayochangia wote.

Mbinu hii busaidia kuonyesha mkinzano wa kimawazo, migogoro, maoni gofauti ya wahusika, n.k. 

Kuchanganya Ndimi/ Lugha Mseto.

Hii ni mbinu ya kutumia lugha mbili tofauti katika usemi, Kiswahili na lugha nyingine. Mara nyingi, maneno kutoka lugha ya pili huandikwa kwa mtindo wa italiki.

Aghalabu huwa Kiingereza lakini yaweza kuwa lugha nyingine kama lugha ya mama, Kiarabu, n.k. kwa mfano; “Mwanao ni mzima. He’s out of danger.” 

Utohozi.

Ni matumizi ya maneno kutoka lugha nyingine, aghalabu Kiingereza yaliyobadilishwa muundo na matamshi kuwa ya Kiswahili.

Kwa mfano. Daktari(doctor), begi(bag), ticket(tiketi),n.k 

Kejeli/ Stihizai/ Dhihaka.

Ni mbinu ya kutumia maneno ya kumsimanga mtu, tukio au suala fulani.

Hali hii huweza kupunguza uzito wa hali au jambo au kumtilia mtu hamu ya kubadilika.

Inaweza kutumiwa na mwandishi mwenyewe katika maelezo ya suala au mhusika kwa mwingine.

Kwa mfano; alipata alama 10 katika hisabati.

Kweli alijaribu, kama binadamu. 

Nidaa.

Ni mbinu ya kudhihirisha hisia za ndani kwa kutumia vihusishi na alama ya hisi(!).

Kwa mfano, alifurahi sana kufika nyumbani.

Popote ambapo alama hiyo imetumika, hiyo ni mbinu ya nidaa.

Mtihani mkuu kwa mwanafunzi ni kufahamu hisia ambazo zinaakisiwa na alama hiyo.

Zinaweza kuwa furaha, huzuni, mshangao, mtamauko, hasira, amri, n.k.

Laiti angalijua!

Koja.

Ni mbinu ya kudhihirisha wingi wa vitu kwa matumizi ya koma kwa ajili ya kuorodhesha.

Mbinu hii inaweza kuwasilisha kuwepo kwa lukuki ya vitu au mfuatano wa matukio mengi.

Kwa mfano; Maria alifika nyumbani, akavua sare za shule, akaoga, akaenda mtoni kuchota maji, akapika, akala na kulala.

Mdokezo.

Ni mbinu ya kuachia mambo yakining’inia, yaani kuacha bila kukamilisha ujumbe fulani kwa kutumia alama za dukuduku(…).

Inaweza kuwa sehemu inayoweza kujazwa, itakayoelezwa mbeleni au kumwachia msomaji kujijazia.

Pia inaweza kuwa zao la kukatizwa kalima wakati wa mazungumzo. Kwa mfano; aliingia ndani na kusubiri akijua wazi kuwa mgaagaa na upwa…

Tasfida.

Ni mbinu ya kutumia msamiati wenye adabu ili kuepuka lugha chafu.

Hutumika kuepuka lugha inayoweza kuzua hisia hasi au kutia kinyaa.

Kwa mfano, mja mzito badala ya kuwa na mimba, kubaua/kutabawali au kwenda haja ndogo badala ya kukojoa.

Tadmini.

Ni mbinu ya kutoa marejeleo katika misahafu(vitabu vya kidini) kama vile Biblia na Korani, na kuyahusisha na hali fulani katika kazi ya kifasihi.

Kwa mfano; ukaidi haujaanza leo, ulianza na Adamu na Hawa kwenye bustani la Edeni.

Tanakuzi.

Ni mbinu ya kutumia maneno yenye kinyume katika sentensi moja na kuzua kauli zenye ukinzani.

Aghalabu hutumika kuonyesha hali ya utata. Kwa mfano; asali iligeuka shubiri.

Alikufa na kufufuka ilipobidi.

Lahaja.

Ni matumizi ya maneno ya lahaja tofauti za Kiswahili ambayo hayapo katika Kiswahili sanifu.

Upekee wake ni matumizi ya maneno yasiyo ya Kiswahili sanifu bali vilugha vyake. Kwa mfano; kahawa tungu(kahawa chungu), mwananti kuivunda nti(mwananchi kuivunja nchi).  

2. Mbinu za Kimtindo 

Sadfa.

Ni mtindo ambapo matukio mawili yanayohusiana hutukia kibahati kwa wakati mmoja, au kwa mfululizo kama kwamba yamepangwa.

Matukio haya aghalabu huwa na matokeo fulani. Kwa mfano; kukutana na msaada wakati wa tatizo bila kutarajia.

Kinaya.

Ni mtindo ambapo matukio huenda kinyume na matarajio yetu, aidha kulingana na mfululizo wa awali wa matukio, au kwa kuyalinganisha na maisha halisi.

Pia mbinu hii inaweza kudhihirishwa kupitia kwa usemi wa mhusika.

Kwa mfano; kumpa hongera mtu aliyefeli au kusherehekea baada ya kufeli.

Majazi.

Ni mtindo wa kuwapa wahusika majina kulingana na tabia au maumbile yao.

Majina haya huitwa majina ya majazi/kimajazi. Kwa mfano; mtu katili anaweza kupatiwa jina ‘Kedi’.

Taswira.

Mtindo wa kutoa maelezo ya ndani kuhusu suala fulani kiasi cha kujenga picha ya kile kinachorejelewa kwenye akili ya msomaji.

Kuna taswira toofauti kama vile mwonekano, mnuso au harufu, hisi na mguso, kulingana na picha inayozalishwa.

Kwa mfano; kaptura yake nyeusi iliyochakaa ilirembwa kwa viraka vya kila rangi, hungetambua rangi yake asilia. 

Taharuki.

Ni mtindo wa kutoa maelezo taratibu kwa kusaza habari fulani ili kumtia msomaji hamu ya kujua zaidi.

Pia huweza kumwacha msomaji akining’inia mwishoni mwa kisa na kumwacha kujijazia kuhusu masuala fulani.

Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi.

Ni mtindo wa kurejelea matukio yaliyotukia muda uliopita, lakini yenye uhusiano na yale yanayosimuliwa.

Yanaweza kurejeshwa na msimulizi au mhusika fulani kupitia kumbukumbu zake.

Kiangaza Mbele/Kisengerembele/Kionambele.

Ni mtindo wa kudokeza mambo yatayotukia mbele kabla hayajatukia, na kuyahusisha na yale yanayotukia wakati huo.

Utabiri.

Ni mbinu ambapo mhusika hudokeza jambo kisha likatukia baadaye bila yeye kutarajia.

Tofauti yake na Kiangazambele ni kwamba utabiri huwa jambo la kukisia au kudokeza tu, bila uhakika wake wa kutokea.

Jazanda.

Ni ufananisho wa mzito wa vitu viwili visivyo na uhusiano wa moja kwa moja, ambavyo hulinganishwa na kulinganuliwa kwa njia ya mafumbo.

Kwa mfano, Bi. Sarafu alilalamika kuwa jembe la mumewe lilishindwa na kazi.

Ishara.

Ni mambo, vitu au matukio ambayo huonekana au kutukia kabla ya jambo fulani yanayoashiria.

Mambo haya huwa na uhusiano fulani na matukio yanayoashiria. Kwa mfano; milio ya bundi inayomtia mhusika wasiwasi kabla ya janga fulani kutokea.

Ritifaa.

Ni mtindo ambapo mhusika aliye hai humzungumzia mhusika aliyefariki kama kwamba yuko hai na anamsikia.

Huweza kuonyesha uhusiano kati yao, kueleza hisia za ukiwa au kumtakia neema.Lakabu.

Ni matumizi ya majina ya kupanga kuwarejelea wahusika.

Majina haya huambatana na sifa fulani za mhusika.

Tofauti na majazi ni kuwa lakabu huwa majina ya kupanga, bali si majina halisi ya wahusika.

Ushairi Nyimbo.

Barua

Mwingiliano wa Vipengele.

Ni muhimu kuelewa kwamba kuna mwingiliano wa kipekee katika vipengele hivi tofauti vya hadithi, kwani haviwezi kushughulikiwa kwa ukamilifu.

Baadhi ya mwingiliano ni kama ufuatao;Dhamira ya Mwandishi na Maudhui.

Dhamira ndiyo huongoza maudhui ambayo yanashughulikiwa katika hadithi.

Hivyo basi, mambo haya mawili huingiliana pakubwa.

Dhamira ndiyo hufungua nafasi kwa maudhui ya hadithi.

Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha maovu yanayotendewa wananchi na wanasiasa au viongozi, lazima kuwepo maudhui ya siasa au uongozi au yote.

Dhamira na Wahusika. Kila dhamira huwasilishwa kwa kutumia mhusika au wahusika fulani.

Bila wahusika, dhamira haiwezi kutimizwa wala wahusika hawawezi kuwa na maana bila dhamira.

Sifa za wahusika zinalingana na dhamira na kubwa zaidi, umuhimu wao huhusiana moja kwa moja na dhamira ambayo wanatekeleza.

Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha madhila ya wanawake katika jamii, lazima awepo mwanamke anayetekeleza dhima hiyo.

3. Maudhui na Wahusika.

Maudhui huwasilishwa kupitia kwa wahusika pia. Vitendo vya wahusika ndivyo huzalishwa maudhui yanayoangaziwa katika hadithi.

Hivyo basi, kuna uhusiano mkubwa kati ya sifa za wahusika na maudhui.

Kwa mfano, kukiwepo na maudhui ya usaliti, lazima kuwepo mhusika msaliti, iwapo kuna maudhui ya tamaa na ubinafsi, lazima kuwepo mhusika mbinafsi na mwenye tamaa.

Hivyo basi, ni vyema msomaji kuoanisha masuala haya pale ambapo hayashughulikiwa yote mawili.

Maudhui na Mtindo/Mbinu za Uandishi.

Kuna pia mwingiliano wa kadri kati ya vipengele hivi.

Japo si kila mara haya hutokea, baadhi ya mbinu huingiliana na Maudhui. Baadhi ya mbinu husawiri maudhui fulani.

Kwa mfano, mtindo wa kinaya aghalabu huhusiana pakubwa na maudhui ya usaliti.

Mbinu tofauti pia hubeba maudhui mengine kama vile dayolojia, ushairi, nyimbo, n.k.

Mtindo na Wahusika.

Mitindo pia huweza kusaidia kuelewa wahusika na hulka zao zaidi. Kwa mfano, mbinu za majazi na lakabu husaidia katika kuelewa sifa za wahusika fulani.

Mbinu nyingine zinazoleta haya ni kama dayolojia, kinaya, uzungumzi nafsia na nyinginezo.

Kutokana na maelezo haya, ni muhimu kutilia maanani kila ujumbe unaopatikana kwenye hadithi zote ili kuimarisha uelewa wake na pia kuwa na uwezo wa kukabiliana nazo katika mtihani.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Utangulizi - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?