Fadhila za Punda summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Fadhila za Punda- Rachel Wangari.

Mtiririko

Lilia anagutuka kutoka usingizini kwa hofu.

Anamsubiri mumewe Luka. Amelala kochini ili amfungulie haraka.

Anagundua kwamba bado hajafika kama alivyodhania, lakini hili halimpunguzii hofu, kwani ana hakika kuwa atakuja tu, tena kwa hasira tele kwa kukosa kupokea simu yake, ambayo ilipigwa akiwa bafuni.

Ni saa nane za usiku na watu wamelala.

Anafahamu kuwa mumewe haji na kuamua kuelekea kitandani kulala.

Anapita kwenye kioo kilichopasuka, tokeo la pigo moja la awali la mumewe.

Anajiona alivyobadilika, kovu shavuni na donda linaloelekea kupona kipajini.

Anakumbuka uso wake awali ulivyokuwa laini na wa kupendeza, na kushangaa hasa sababu ya Luka, mumewe, kubadilika na kuwa mkali hivi.

Hatimaye analala. 

Tunarejeshwa awali, Lilia alipomwona Luka mara ya kwanza, katika kanisa la babake, alipoingia ghafla tu.

Alilazimika kukaa karibu na Lilia kwa kuwa ndipo palikuwa na nafasi.

Alivaa mavazi ya kimaskini, lakini alipoomba kuimba, aliisikia sauti yake iliyokuwa tamu ajabu, iliyompendeza hata babake Lilia. 

Babake Lilia ni mjane kwa miaka mitatu, lakini kila mara Lilia anamwondolea mawazo ya marehemu mkewe, kwanza kwa jinsi wanavyofanana na pia kwa ule ulimi wake usiotulia.

Anamweleza kuhusu Luka na sauti yake yake ya kipekee.

Anapomsumbua kuhusu kijana huyo, anaamua kumwalika ofisini Jumapili inayofuata.

Mhubiri anajuta kuchelewa kupata mtoto mwingine kabla ya mkewe kufariki kwa ajali. 

Shinikizo la kuoa tena haliridhii, kwani haoni yeyote anayeweza kujaza pengo la mkewe.

Anampa mamake Luka kazi ya kusafisha kanisa, naye Luka anajiunga na shule ya msingi kwa hisani ya mhubiri.

Anaondokea kuwa mwerevu.

Urafiki wake na Lilia unamtia mchungaji kiwewe, na hivyo anamtuma Luka kwa mhubiri rafikiye upande mwingine wa nchi.

Urafiki wao haukatishwi na hili. 

Wanazidi kuwasiliana kwa simu na barua.

Wanakutana tena katika chuo kikuu kimoja.

Baba anamwonya bintiye lakini hamsikizi kutokana na mapenzi. 

Lilia anamkumbusha babake kuhusu amri ya Mungu ya mapenzi.

Luka anamsisitizia kuwa ana nia safi kwa mwanawe na ataka kumuoa.

Japo hisia fulani zinamfanya kutomwamini Luka, hana ushahidi na pia hataki kumvunja moyo bintiye.

Anawapa Baraka zake. Wakati huu Lilia ni meneja wa benki moja.

Luka anaongoza mahubiri kanisani kutokana na uzee wa baba Lilia, mhubiri mkuu.

Kanisa linakua na kufurika hadi mahema kuongezwa. 

Baba Lilia anafariki na Luka kuchukua uongozi kamili wa kanisa.

Anamshinikiza mkewe kuacha kazi ili atunze fedha za kanisa, japo kuna mhasibu anayefanya kazi nzuri.

Anamtaka kukaa nyumbani na kuandamana naye anapohitajika.

Umaarufu wa Luka unazidi hadi anafika ikulu. 

Luka anaamua kuingilia siasa japo mkewe hapendezwi.

Anauza kanisa, lakini Lilia ananyamaza kulinda ndoa.

Kampeni zanamchosha Lilia hadi siku moja anapokataa kabisa kushiriki, akiwa na uja uzito wa miezi mine.

Luka anaudhika na kuondoka nyumbani.

Jioni ya siku inayofuata, anapelekwa hosppitalini na majirani na kupoteza uja uzito.

Luka hahuzuniki sana, kwa kuwa hataki kuwa mzazi wakati wa uchaguzi. 

Luka anafaulu kuwa gavana lakini anawasahau wananchi.

Anakuwa mzinzi. Anapohamia kasri la gavana, anamsahau mkewe na kumtaka kubaki vijijini ili awe karibu na raia.

Anamtembelea mkewe wikendi. 

Anapata taarifa kuwa mumewe ana vimada, lakini haamini hadi anapomtembelea ofisini bila habari na kumpata na mwanamke mwingine.

Wanazozana na kuamrishwa arudi nyumbani, jambo analotii.

Jioni hiyo, Lilia anapigwa na kuonywa vikali dhidi ya kwenda ofisi bila idhini ya mumewe.

Hatimaye anaishia kutawishwa, haongei na watu kwa hofu ya kupigwa.

Anamwona mumewe akiandamana na yule mwanamke aliyepata ofisini, anayetaniwa kuwa mshauri wake. 

Wakati mmoja anaamua kuripoti polisi.

Anapofika, anapelekwa kwa mkuu wa kituo.

Mkuu huyu anaposifia ukarimu wa mumewe waliyekuwa pamoja wiki jana, anajua kuwa hatasaidika.

Anadanganya kuwa anamtafuta askari polisi aliyemfaa siku moja na kujiendea. Anatoka kwa hofu akijua Luka ataambiwa.

Siku mbili zikapita, kisha siku ya tatu ndipo akakosa kupokea simu yake, naye Luka akakosa kufika.

Luka anafika siku tano baada yake kutembelea kituo cha polisi na kumpiga vibaya hadi anapopoteza fahamu na kutoweka.

Anaiona simu yak chini na kuichukua, na kumpigia mama mkwe na kuzirai tena.

Anapopata fahamu, yuko mikononi mwa mama mkwe anayemhudumia.

Anamlaani Luka kwa anayomtendea mkewe licha ya fadhila za baba Lilia kwake.

Anampigia Luka kumwamrisha atume ambulensi, akimtishia kupiga simu polisi na kituo cha habari.

Anakata na kuendelea kumshughulikia mkaza mwanawe.

Kabla ya fahamu kumtoka, Lilia anasikia mlio wa ambulensi.

 Anapogutuka, anajipata peke yake kitandani kwenye chumba cha hospitali.

Mama mkwe anamtembelea kila siku kumuunguza, wala hajamwona mumewe.

Siku ya nne, anamwona mtu kando yake, hamtambui kwani amefungwa bendeji usoni, nao mguu umeinuliwa.

Mama mkwe anapokuja, anaelekea kwa kile kitanda.

Akija, anawahudumia wote wawili.

Anamrejelea kuwa gavana, lakini Lilia haelewi ni gavana yupi na kwa nini wamo chumba kimoja, naye mama mkwe hana nia ya kumweleza. 

Mgonjwa mwenzake anaanza kutembelewa na marafiki na wafanyakazi waliokunja nyuso.

Anawasikia wauguzi wakisema huenda asitembee tena kutokana na ajali aliyopata, ambayo nusura imwangamize.

Lilia anaelewa mambo siku ya nne, mama mkwe anapofika na kumwita mgonjwa kwa jina, Luka!

Anamweleza kuwa kiruukanjia wake aliondoka baada ya kusikia hawezi kutembea tena. Lilia naye ameruhusiwa kwenda nyumbani.

Anapomwangalia mumewe, anadhani anaona chozi likitoka kwenye jicho la kushoto ambalo halijafungwa bandeji. 

Ufaafu wa anwani ‘Fadhila za Punda’. 

Anwani hii inatokana na methali isemayo, ‘Fadhila za punda ni mashuzi’, kama ilivyotumiwa katika hadithi yenyewe.

Pia huweza kuwa ‘Fadhila za punda ni mateke’.

Matumizi ni kwa ambaye hulipa hisani kwa nuksani, yaani wema kwa uovu.

Fadhila za punda, hivyo basi, ina maana ya matendo mabaya kutoka kwa mtu aliyetendewa mema.

Mada hii inaafiki hadithi. Luka ana fadhila za punda.

Kwanza, kanisa ambalo linamlea na kumjenga akiwa maskini anaponeemeka analiuza bila kujali.

Umaarufu na utajiri anaopata hapa unamtia kiburi sana. 

Luka analipa fadhila za Lilia kwa mashuzi.

Lilia ndiye anampigania kwa mhubiri hadi anaposaidiwa kimaisha na kimasomo, akasoma hadi chuo kikuu. 

Lilia vile vile anapigania penzi lake kwa Luka kwa kila hali. Anatia bidii kuhakikisha mapenzi yao yanadumu kila babake anapojaribu kuwatenganisha.

Hata maonyo ya baba mtu hayamfanyi kubadili msimamo. Hatimaye wanaruhusiwa kuoana. 

Licha ya haya yote, anamtesa Lilia katika ndoa yao kwa kipigo cha kila mara kutokana na visingizio vya hapa na pale, kama vile chakula kukosa chumvi ya kutosha na kuchelewa kumfungulia.

Anamtia makovu katika uso uliokuwa mzuri na mwororo awali. 

Licha ya kutopenda siasa, Lilia anamsaidia Luka katika azma yake ya kuwa gavana hadi anapofaulu.

Hata hivyo, anamdhalilisha na kumtelekeza anapotwaa wadhifa huo na kutomjali kabisa. 

Lilia anampenda mumewe kwa dhati ya moyo na yuko tayari kufanya kila awezalo kulinda ndoa yake.

Anaridhia matakwa ya Luka na kuwa mwaminifu kwake.

Luka kwa upande wake, badala ya kulipa fadhila hizi kwa kuwa mume mwema, ana vimada wa pembeni wal hafanyi lolote kumficha mkewe ukweli huu. 

Baba Lilia anamtendea Luka mengi. Anafadhili elimu yake na kumlea kama mwanawe na hatimaye kumkubalia kumwoa bintiye.

Anapofanikiwa baadaye, anaanza kumtesa bintiye aliyeahidi kumtunza. 

Luka anpiga kampeni kabambe katika azma ya kuwa gavana, nao wananchi wanamuunga mkono.

Anapofanikiwa, halipii fadhila zao kwani anawasahau kabisa, wala dhiki yao haimshtui. 

Kimada wake Luka pia anakejeli fadhila za Luka. Anamzuzua na kumfanya kumsahau kabisa mkewe wa ndoa. Anaandamana naye kila mahali akiwa gavana.

Anapopata ajali na kulazwa hospitali, kimada huyu anamtoroka baada ya kusikia hawezi kutembea tena. 

Dhamira ya Mwandishi 

Kuonya dhidi ya kuwaamini waja wanaojitia ucha Mungu, kwani unaweza kuwa bandia.

Ucha Mungu si kilemba cheupe tu. Ni vyema kufanya uchunguzi wa ndani kabla ya kumwamini yeyote.

Anadhamiria kutoa ushauri kuhusiana na nafasi ya mzazi katika makuzi ya mwanawe au wanawe na jinsi ya kutekeleza malezi kwa tija.

Ananuia pia kutoa maonyo kwa viongozi wasiowajibikia wajibu wao wanapotwikwa mamlaka kuwa siku yao itafika.

Kuonya watenda maovu kuwa siku ya kuyalipia itakuja, kwani malipo ni hapa hapa duniani.

Kuonya dhidi ya uvumilivu usio na tija katika ndoa za dhuluma ambao unaweza kuleta madhara yasiyomithilika kwa wahusika.

Kudhihirisha jinsi mwanamke anavyodhulumiwa katika jamii na jinsi anavyoweza kukabili na kupinga dhuluma hizi.

Kuonyesha sura za migogoro katika jamii na jinsi zinavyoathiri maisha.

Maudhui

Mapenzi na Ndoa

Mapenzi ndiyo chemchemi inayochangia ndoa.

Kuna ndoa ya babake Lilia ambayo ilitawaliwa na mapenzi, kwani wakati huu mkewe ashaaga.

Kila mara mhubiri huyu anamkumbuka.

Hata anashindwa kuoa mke mwingine kutokana na mapenzi yao ya dhati.

Anapatwa na huzuni tele baada ya kuaga kutokana na ajali ya barabarani.

Mwandishi anasema kuwa lau si ulimi wa bintiye usiotulia, dhiki ya kuachwa na mkewe ingemsukuma kaburini.

Fahari kuu ya ndoa inadhihirika kupitia kujaliwa kwao binti huyu, Lilia, ambaye anfanana na mamake. 

Ndoa kuu, hata hivyo, ni kati ya Luka na Lilia.

Mapenzi yao yanaanza Lilia anapomwona Luka kwenye kanisa la babake, huku amevalia kimaskini.

Sauti yake tamu inamvutia mara moja na hapo haachi kumwaza.

Mapenzi yake kwa Luka yanamsukuma kumwomba babake amsaidie.

Babake anampeleka katika shule ya msingi na kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa.

Anamwelimisha hadi chuo kikuu, yote kwa ajili ya bintiye anayempenda Luka kwa dhati. 

Usuhuba kati ya wawili hawa unaanza mapema, tangu wakiwa wachanga.

Unamtia kiwewe babake Lilia, ambaye anajaribu kila mbinu kuwatenganisha bila mafanikio.

Anapompeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri mwenzake, bado wanawasiliana kwa barua na simu.

Bintiye anamsisitizia amri ya Mungu ya mapenzi na kumtaka awape baraka zake.

Licha ya hisia za hofu kwa Luka, anawaruhusu kuoana. 

Ndoa yao inaenda vizuri hadi babake Lilia anapofariki.

Hapo Luka anabadilika na kuwa mwovu. Anamshinikiza mkewe kuacha kazi na kumtawisha.

Hatimaye anaamua kujitosa katika siasa na mkewe anatakiwa kuwajibika, licha ya kuwa hapendi siasa.

Anapokataa kushirikiana naye baada ya muda, anamkumbusha kuwa wanawake ni wengi na kumwacha pekee nyumbani.

Analazimika kukimbizwa hospitalini na majirani na anapoteza uja uzito wake wa miezi minne, lakini Luka hahuzuniki sana.

Anaamini bado upo muda wa kupata watoto. 

Mambo yao yanaharibika kabisa Luka anapokuwa gavana. Anaanza kuwa na vimada, huku akimlazimisha mkewe kuishi vijijini ili awe karibu na raia.

Anamtembelea wikendi lakini hana muda naye, shughuli muhimu kwake ni kujiandaa kwa ajili ya wiki inayofuata.

Mkewe anapomtembelea bila habari na kumpata na mwanamke mwingine, hajali chochote bali anamfokea mkewe na kumtaka arejee nyumbani na kuacha ujumbe Jioni hiyo anaporudi nyumbani, Luka anampiga mkewe vibaya, huku akimkanya dhidi ya kufika ofisini kwake bila taarifa na kutoheshimu wageni wake.

Huu unaondokea kuwa mwanzo wa vipigo vya mara kwa mara.

Ata kuhusiana na marafiki na majirani ananyimwa.

Mumewe anaandamana na yule kimada wake katika hafla zote bila haya. 

Lilia anaamua kuripoti polisi lakini anaghairi anapogundua mkuu wa polisi anajuana na mumewe.

Anahofia usalama wake kutokana na kisa hicho, akijua mumewe atajua, pamoja na kukosa simu yake akiwa bafuni.

Hofu yake inaondokea kuwa ukweli, kwani Luka anaporejea, anampiga vibaya hadi anapozirai na kumwacha.

Anapopata fahamu, anamwita mama mkwe anayemwauni kwa kumpeleka hospitali.

Hata haamini Luka anaweza kumfanyia Lilia hivi! 

Haibainiki ndoa ya Luka inachukua mkondo gani mwishowe.

Mkewe anatibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini, hali Luka mwenyewe amelazwa baada ya kupata ajali.

Kimada wake naye amemtoroka baada ya kusikia huenda asiweze kutembea tena maishani. 

Nafasi ya Mwanamke Katika Jamii.

Mwanamke katika jamii hii amepatiwa nafasi finyu sana, licha ya kuwa na mchango wa kipekee.

Kwanza, mwanamke anadhihirika kuwa mpenzi wa dhati ya moyo.

Mhubiri anamkumbuka mkewe waliyependana kwa dhati na ambaye anapofariki, anashindwa kabisa kuoa mke mwingine wa kujaza pengo lake.

Anashinikizwa na wahubiri wenzake, wazee wa kanisa na hata washirika wake lakini anashindwa kabisa kumwoa mwingine.

Lilia anapomwona Luka mara ya kwanza tu, anampenda kwa dhati hasa kutokana na sauti yake ya kupendeza.

Anamshinikiza babake hadi anapompa mamake kazi ya kusafisha kanisa na hata kumpeleka Luka shule.

Majaribio ya babake kuwatenganisha hayazai matunda kwani Lilia yuko mstari wa mbele kumpigania Luka wake hadi wanaporuhusiwa kuoana na baba kuwapa baraka zake. 

Hata Luka anapoingilia siasa, Lilia anamsaidia licha ya kutopenda siasa.

Anamvumilia na ukware wake na kubaki kuwa mwaminifu siku zote.

Anampiga mara kwa mara, lakini anazidi kumshughulikia kama mumewe hadi anampiga na kumsababisha kulazwa hospitalini.

Wanakutana huko baada ya Luka kupata ajali ya barabarani na kupoteza uwezo wa kutembea.

Hatujui ndoa yao inachukua mkondo gani. Mamake Luka pia ana mapenzi ya kipekee.

Anampenda mwanawe Luka na anajitolea kumlea vyema licha ya umaskini wake.

Lilia anapopoteza fahamu baada ya kipigo, anachukua simu na kumpigia.

Anafika mara moja na kumhudumia. Anampigia mwanawe na kumlazimisha kutuma ambulensi, kisha kumpeleka Lilia hospitalini na kumuuguza. 

Mwanamke pia anachukuliwa kama kiumbe dhaifu cha kuendeshwa na kuelekezwa na mwanamume.

Luka anampa mkewe maagizo anayotaka kila mara.

Anamkataza kujumuika na marafiki na anapofanya hivyo anampiga vibaya.

Anamlazimisha kukaa nyumbani kama mtawa na kumtaka kumpigia simu akitaka kufika ofisini.

Anapokosa simu yake akioga, anaingiwa na hofu kuu, kwani anajua yatakayofuatia.

Luka anampiga mara kwa mara hadi mwisho anapolazwa hospitalini. 

Mwanamke pia anasawiriwa kama chombo cha kumstarehesha mwanamume.

Luka anamwambia mkewe kuwa wanawake ni wengi anapokataa kuandamana naye katika kampeni.

Kulingana naye, ni rahisi kwake kupata wanawake wengine.

Anapokuwa gavana, ana vimada wengi wala hajali hili linavyomwathiri mkewe.

Anapomtembelea anampata na mwanamke mwingine.

Badala ya kuwa na haya anamfokea na kumlaumu.

Mwanamke yule naye pia anaendelea kuhusiana na Luka kimapenzi licha ya kujua ana mke. 

Mwanamke pia anachorwa kama msaliti.

Kimada wa Luka anajua kuwa ana mke lakini bado anasuhubiana naye na hata kuandamana naye katika shughuli rasmi.

Hajali machungu anayomletea mkewe Luka.

Isitoshe, anamtoroka Luka anapomhitaji zaidi, pale anapopata ajali na kupoteza uwezo wa kutembea. 

Usaliti

Luka anamsaliti babake Lilia.

Mzee huyu anajitolea kumfaa kwa kila hali tangu akiwa mchanga.

Anamsomesha na kumpa uongozi wa mahubiri katika kanisa lake.

Anapofariki, anauza kanisa lake kwa nia ya kujifaidi binafsi.

Pia anamsaliti kwa kuvunja ahadi aliyotoa ya kumlinda bintiye, kwani baada ya kumwoa anaanza kumtesa. 

Luka pia anamsaliti mkewe Lilia.

Kwanza, anamsaliti kwa kumwendea kinyume licha ya uvumilivu wa madhila ya mumewe na pia uaminifu wake.

Pia, mkewe anapigania penzi tangu wakiwa wachanga.

Anamshinda hata babake anayemshuku Luka.

Licha ya haya yote, Luka anamtesa kwa mapigo ya kila siku hadi mwishowe anapolazwa hospitalini kwa mapigo haya.  

Luka pia anasaliti dini na imani kwa kutumia kanisa kwa ajili ya manufaa ya kibinafsi.

Kanisa linakua na kuimarika chini ya mahubiri yake, lakini linapokua, analigeuza biashara.

Hatimaye analiuza na kuingilia siasa.

Anasaliti dini na Imani pia kwa kubadilika na kuwa laghai, mkware, dhalimu miongoni mwa maovu mengine. 

Kimada wa Luka anamsaliti kwa kumwacha anapomhitaji zaidi.

Licha ya kumtelekeza mkewe kwa sababu ya kimada huyu, anamwacha kwenye kitanda cha hospitali anapopoteza uwezo wake wa kutembea.Isitoshe, anamsaliti Lilia kwa kuhusiana na mumewe akijua vyema amemwoa. 

Dini

Jamii hii imejikita katika dini ya kikristo.

Dini inachukua mkondo wake wa kuwapa waja tumaini na kuwatia shime.

Dini pia inasaidie walio katika taabu kuwa na tumaini la maisha. 

Lilia anakutana na Luka mara ya kwanza katika kanisa. Wako katika darasa la mabaleghe anapofika.

Sadfa kuwa ni pale alipokaa tu Lilia penye nafasi anaiona kama ni Mungu anamjaribu.

Anaketi na masomo kuendelea. Mwishoni mwa somo anapatiwa nafasi ya kujitambulisha.

Anamtukuza Mungu kwa wimbo unaowapendeza waliomo humu, hata mhubiri anayekuja kuwajulisha muda umekwisha.

 Lilia pia amelelewa katika misingi ya kikristo, kwani babake, Lee Imani ni mhubiri.

Anamlea pekee baada ya mkewe kuaga kutokana na ajali ya barabarani. 

Dini ndiyo inayopalilia penzi kati ya Luka na Lilia.

Lilia anamwomba babake wamsaidie Luka kama dini inavyoelekeza.

Babake anakubali kumpeleka shule na pia kumpa mamake kazi ya kusafisha kanisa.

Wanapojuana wakiwa watoto, Luka na Lilia ni marafiki wa kufa kuzikana.

Wanapoingia ujanani, babake Lilia anahofia usalama wa bintiye na kujaribu kuwatenganisha kwa kumpeleka Luka upande mwingine wa nchi kwa mhubiri rafikiye.

Bado wanawasiliana kwa simu na barua. 

Mhubiri huyu anapotilia shaka mwelekeo wa uhusiano wa bintiye na Luka, bintiye anamkumbusha mahubiri yake mwenyewe kila mara kuwa Mungu ni upendo.

Anamwambia kuwa hafai kumbagua Luka au kuona kama hamfai.

Lee Imani analazimika kumuuliza Luka kuhusu nia yake kwa Lilia, naye anasisitiza kuwa ana nia safi kabisa.

Licha ya mashaka aliyo nayo, hana lingine ila kuwapa Baraka zake. 

Lilia anamshawishi babake kumpa Luka jukumu la kuhubiri kanisani, jukumu ambalo anatekeleza vilivyo.

Anahubiri na baada ya muda, kanisa linafurika hadi mahema kuongezewa. Washirika wanampenda sana.

Watu wanatoka nchi za mbali kufuatilia miujiza huku. Lee anapofariki, Luka anageuza kanisa kuwa kitega uchumi.

Anamwachisha mkewe kazi yake ya umeneja wa benki ili aje kutunza pesa za kanisa, japo kuna mhasibu anayefanya kazi vizuri.

Baada ya muda, anauza kanisa lile na kuingilia siasa. Anasahau kabisa mambo ya dini na kubadilika kabisa.

Anawatenga watu waliomchagua, anamtesa mkewe na kuwa mkware kupindukia. Mkewe naye anaishi kumwombea kwa imani kuwa atabadilika siku moja. 

Migogoro

Mwanzo wa hadithi unadhihirisha mgogoro mkuu katika kisa hiki. Lilia yuko katika hali ya wasiwasi mkuu huku akimsubiri mumewe.

Amezoea vitimbi vya mumewe anayemjia kwa makeke kila siku.

Anapopita karibu na kioo akielekea kwenye chumba cha kulala, mabadiliko katika uso wake yanadhihirisha migogoro ya awali kati yake na mumewe.

Kwanza, kioo chenyewe kimepasuka. Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona shavuni, zote kumbukumbu za mapigo ya awali.

Lilia anapokumbuka walivyokutana na Luka, tunapata taswira ya migogoro ya awali.

Anapompenda Luka, anazua mgogoro kati yake na babake, ambaye hapendelei sana ukaribu kati yao.

Anahofia usalama wa bintiye.

Hata hivyo, Lilia anamsisitizia kwamba mapenzi ni moja kati ya amri za Mungu wala hafai kumbagua Luka au kumwona hafai. 

Hisia za Lee Imani, babake Lilia, kumhusu Luka zinazua mgogoro kati yake na nafsi yake.

Japo Luka anamhakikishia kuwa nia yake kwa bintiye ni safi, hisia fulani zinamfanya kumshuku.

Hatimaye, kwa ajili ya furaha ya bintiye, analazimika kuwapa baraka zake. 

Baada ya babake Lilia kufariki, ndipo migogoro inaanza kati yao. Luka anauza kanisa lao.

Japo hakubaliani na hatua hii, Lilia ananyamaza ili kutunza ndoa yake.

Mumewe anamwachisha kazi na kumtaka kubakia nyumbani, na hatimaye kumtawisha.

Anapoingilia kampeni, anambembeleza aghairi nia lakini anakataa kabisa.

Anamlazimisha Lilia kuandamana naye japo yeye hapendi masuala ya siasa.

Wakati mmoja anaambulia vitisho anapokataa katakata kuandamana naye, huku akimkumbusha kuwa wanawake ni wengi. 

Migogoro kati ya wawili hawa inazidi Luka anapotwaa ugavana. Anamtaka mkewe kukaa vijijini eti ili awe karibu na raia.

Mumewe anafika huko wikendi wala hana wakati wake, anajiandalia masuala ya wiki inayofuata.

Wakati mmoja anapomtembelea bila habari, anampata na mwanamke mwingine.

Luka hajali chochote bali anamlaumu mkewe kwa kumtembelea bila taarifa.

Anaporejea nyumbani jioni hiyo, anampiga vibaya mkewe na kumwonya dhidi ya kutoka nje ya nyumba. 

Mafarakano yanazidi baada ya tukio hili.

Luka anampiga mara kwa mara anapotangamana na majirani na marafiki.

Lilia ashakuwa mtawa. Anapoamua kuripoti, anaambulia patupu baada ya kugundua mkuu wa polisi anayeenda kupigia ripoti anajuana na mumewe.

Isitoshe, siku ya tatu baada ya kufika kituoni, anakosa simu ya mumewe akiwa bafuni, na hapo anajua kuwa yuko hatarini.

Anangoja mumewe, ambaye anafika siku mbili baadaye. 

Luka anamvamia mkewe tena na kumvuta nywele kumwelekeza kwenye chumba cha kulala, ambapo anampiga kwa ngumi, mateke na makofi.

Anamvunja mkono na hatimaye anapoteza fahamu. Luka mwenyewe hajali bali anaondoka na kumwacha pale.

Anahofia hata kuwaita majirani kumwauni kwa kumwogopa mumewe. Hatimaye, anaiona simu yake na kuamua kumpigia mama mkwe. 

Simu ya Lilia kwa mkwewe inaibua mgogoro kati ya Luka na mamake hasa anapomjulisha ni Luka aliyetekeleza hayo.

Mama mtu anashangazwa na ukatili wa Luka kwa mkewe licha ya fadhila alizotendewa na babake Lilia.

Anampigia simu na kumwamrisha atume ambulansi, huku akimkumbusha kuwa akichelea, simu itakayofuata itaelekea polisi kisha kituo cha habari.

Hana lingine ila kumtii mamake. 

Mabadiliko

Lilia anapoelekea kwenye chumba cha kulala, anapita karibu na kioo na hapo kushuhudia mabadiliko yaliyokumba uso wake.

Awali, ngozi yake ilikuwa laini bila alama yoyote na kila mara ilifanya vidu vya kupendeza alipotabasamu, tena tabasamu lenyewe halikukosa usoni mwake.

Sasa hivi, uso huo umebadilika pakubwa.

Ana kovu shavuni na donda linaloelekea kupona kipajini.

Isitoshe, siku hizi anatabasamu kwa nadra sana. 

Luka pia anakumbwa na mabadiliko. Anapokutana na Lilia mara ya kwanza, ni maskini, mchafu asiyeonekana kuwa na lolote la maana.

Hata hivyo, Lee Imani anambadilisha anapomkaribisha kwake na kumpeleka shule.

Anasahau umaskini na kuzidi kufana.

Anaanza kufanya hata uhubiri, na hatimaye anaimarika hadi kiwango cha kuwa gavana. 

Mabadiliko pia yanamkumba Luka katika sekta ya maadili.

Anapomwoa Lilia, ni mhubiri na mcha Mungu mkubwa.

Watu wanatoka pembe zote kufuatilia miujiza katika kanisa lake.

Anawajaza wengi imani kutokana na mahubiri yake.

Hata hivyo, babake Lilia anapoaga, anabadilika ghafla.

Kwanza, anageuza kanisa lile kitega uchumi na kuliuza.

Anawania ugavana na kuwa laghai, mzinzi na katili mkubwa asiyejali maslahi ya watu waliomchagua. 

Lilia anaathiriwa zaidi na mabadiliko ya Luka.

Wanapofunga pingu za maisha, maisha ni raha mstarehe kabla ya Luka kubadilika.

Anamwachisha kazi na kubadili taaluma kutoka kuwa mhubiri na kujitoma katika siasa.

Pia anabadilika na kuanza kumtesa mkewe.

Anampiga mara kwa mara na kumwendea kinyume na vimada wengine.

Anamtelekezea kijijini wala hamjali tena.

Anamchukulia kama kiumbe asiye na sauti anayefaa kuendeshwa huku na huku. 

Maudhui mengine katika hadithi hii ni pamoja na Elimu, Umaskini, Kazi, Utabaka, Familia na Malezi, Ulaghai, Ubabedume, Uwajibikaji, Uongozi, Kutowajibika, Uzinzi na Kifo/Mauti.  

WAHUSIKA:

Sifa na Umuhimu Lilia 

Ni mwenye mapenzi ya dhati.

Anapompenda Luka, anafanya kila jambo kuhakikisha amempata.

Anamsisitizia babake kuwa Luka pia anastahili mapenzi.

Hata anapomtesa, ananyenyekea kwake kwa imani kuwa atabadilika. 

Ni mvumilivu.

Mumewe anampiga kila mara na hata kumwumiza, lakini anajitia moyo huku akiomba kuwa atabadilika.

Ni mcha Mungu.

Ana imani thabiti ya kidini.

Anamweleza babake kuhusu amri ya Mungu ya mapenzi.

Anakutana na Luka kanisani na anapokuwa mwovu, anamwombea kwa imani kuwa atabadilika. 

Ni mpelelezi.

Anapomweleza babake kuhusu Luka anapomwona kanisani, tunaambiwa kuwa macho yake mapelelezi hayakosi kuchunguza na ulimi wake kutangaza matokeo ya uchunguzi huo.

Anafahamu kuwa mumewe ana vimada wa nje licha ya kuwa anatawishwa. 

Ni mwoga.

Anapomgoja mumewe, amejawa na hofu.

Anaamka roho mkononi na pumzi zikimwenda mbio.

Mumewe anapofika baada ya kukosa simu yake, anamfungulis huku akitetemeka kwa hofu kubwa. 

Ni mpenda amani.

Anafanya kila awezalo kuepuka ugomvi na mumewe.

Ananyamaza anapouza kanisa. Anakatiza ukuruba na majirani kuepuka migogoro na kumwombea mumewe abadilike. 

Ni msomi.

Anatia bidii katika masomo yake na kufaulu katika viwango vyote hadi kufikia chuo kikuu. 

Umuhimu wa Lilia

Ni kiwakilishi cha wanawake wanaokandamizwa katika jamii kwa misingi ya kijinsia.

Anadhihirisha sura tofauti za migogoro katika jamii na jinsi inavyoathiri maisha.Kupitia kwake, madhila yanayowapata wanawake katika ndoa yanadhihirika.

Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika jamii 

Luka

Ni mwenye bidii.

Anatia bidii katika kila afanyalo.

Anapoanza kuhubiri, anachukua muda mfupi kupata umaarufu hata kumliko mhubiri mkuu.

Licha ya kuzaliwa maskini, anatia bidii hadi kuwa gavana. 

Ni laghai.

Anajitia ucha Mungu bandia, kumbe ni mwovu kupuindukia.

Anajiaminisha kwa babake Lilia.

Anapokufa, anauza kanisa na kuanza kumtesa bintiye.

Anajiaminisha kwa wapiga kura lakini anawapuuza wanapomchagua. 

Ni mzinzi.

Licha ya kuwa na mke, ana vimada wengine nje.

Mkewe anapomtembelea ofisini, anampata na mwanamke mwingine ambaye ni kimada wake.

Anaandamana na kimada wake katika shughuli zake huku watu wakitania kuwa ni msaidizi wake. 

Ni msaliti.

Anamsaliti mkewe Lilia kwa kumtesa licha ya poenzi lake la dhati.

Anamsaliti babake Lilia kwa kuuza kanisa lake anapofariki na kumtesa bintiye.

Anasaliti dini na nafsi kwa kubadilika kuwa mwovu. 

Ni katili.

Hana hata chembe cha utu.

Anampiga mkewe mara kwa mara bila huruma.

Anamwacha anapozirai wala hajali.

Mamake anapomwamrisha kutuma ambulansi, anasita hadi anapomtishia kuripoti polisi na kumwanika kwenye kituo cha habari. 

Ni mnafiki.

Anajipendekeza kwa babake Lilia na kujitia wema. Anajinufaisha kwa kumwoa bintiye na kutajirika kupitia kanisa lake.

Anawashawishi watu kumchagua kuwa gavana, lakini nia yake ni kujinufaisha. 

Ni mwenye dharau.

Anamdharau mkewe na kumdhalilisha.

Anapomtembelea, anamfokea na kumwambia amwachie sekretari ujumbe.

Anampiga jioni hiyo, huku akidai kuwa haheshimu wageni wake.

Ni msomi.

Anakutana tena na Lilia katika chuo kikuu baada ya bidii zake katika masomo. 

Umuhimu wa Luka 

Ni kiwakilishi cha viongozi wanaowatelekeza wapiga kura baada ya kuwakweza mamlakani Kupitia kwake, ubabedume unadhihirika na madhara yake katika jamii. 

Ni kiwakilishi cha wanafiki wa kidini wanaowafumba macho wengine na kuitumia kujinufaisha Kupitia kwake, mshahara wa watenda maovu unawasilishwa kwa msomaji

Lee Imani(Babake Lilia) 

Ni mcha Mungu.

Ni mhubiri mkuu katika kanisa.

Anawalisha kondoo wa Mungu kwa neno vilivyo. 

Ni mwenye mapenzi ya dhati.

Anampenda mkewe kwa dhati.

Tunaambiwa kuwa lau si uchangamfu wa bintiye, kumbukumbu za mkewe waliyependana kwa dhati zingemsukuma kaburini.

Anashindwa kabisa kuoa tena.

Pia anampenda bintiye kwa dhati. 

Mwenye tahadhari.

Anapogundua ukaribu kati ya Luka, anahofia madhara yake kwa bintiye na kumtuma Luka upande mwingine wa nchi kuwatenganisha.

Anachelea kuwapa baraka zake kwa hisia za shauku dhidi ya Luka.Ni mwenye utu.

Anajitolea kumsaidia Luka kwa kila hali.

Anamkaribisha nyumbani, kumlipia karo na hata kumpa mamake kazi. 

Ni mkakamavu.

Anaposhikilia lake, habadili msimamo.

Anabaki pekee baada ya kifo cha mkewe.

Rai za wahubiri wengine, waumini na marafiki zake hazibadili msimamo wake. 

Ni mwajibikaji.

Anatekeleza wajibu wake kila mara, kama mzazi na pia mhubiri.

Anawalisha chakula cha roho waumini.

Anamshauri bintiye na kumpa baraka zake anapoona mapenzi yake kwa Luka. 

Ni mlezi mwema.

Anamlea bintiye kwa staha chini ya misingi ya kidini.

Anaondokea kuwa mwenye heshima na bidii na mke mwema kwa Luka. 

Umuhimu wa Lee Imani 

Anawasilisha nafasi ya mzazi katika malezi na maisha ya mwanawe kwa jumla

Ni kiwakilishi cha imani na dini na nafasi yake katika kujenga jamii. 

Anadhihirisha matatizo yanayowakumba wazazi wanaojukumika kulea wanao peke yao.

Kupitia kwake, wema miongoni mwa wanajamii unadhihirika. 

Mama Luka.

Ni mwenye bidii.

Anajitolea kwa kila hali kumkimu mwanawe licha ya matatizo mengi.

Hatimaye anapatiwa kazi na babake Lilia kunadhifisha mazingira ya kanisa, anayoitekeleza vilivyo. 

Ni mwajibikaji.

Anapopokea simu ya Lilia baada ya kupigwa na Luka, anawajibika kumshughulikia kwa kumpeleka hospitalini na kumtunza.

Anamshughulikia Luka pia anapolazwa humo baada ya ajali. 

Ni mwerevu.

Anapompigia mwanawe simu, anasita kutuma ambulensi.

Anamtishia kumripoti kwa polisi na kituo cha habari, jambo linalomlazimu kumtii mara moja. 

Ni mwenye utu.

Anaacha shughuli zake na kumwendea mkaza mwanawe.

Anampeleka hospitalini kisha kumtunza kila mara hadi anapopata afueni. 

Umuhimu wake

Anawakilisha majukumu na nafasi ya mzazi katika malezi na makuzi ya mwanawe.

Ni kielelezo cha wakwe wanaojali maslahi ya wakaza wanao 

Anadhihirisha nafasi na umuhimu wa fadhila katika jamii. 

Mbinu za Uandishi

Tashbihi 

Atakuja tu, labda ghamidha itakuwa imezidi, imefura kama hamuri lililotiwa hamira.

Sasa kucheka kwake kulikuwa nadra kama kupatwa kwa mwezi.

 Swali likajitunga akilini mwake, na kama mwangwi, likawa linajirudia tena na tena.

Shati lenyewe limekuwa mararu, limemganda kama kigaga. 

Watoto waliokuwa na hamu kutoka nje wakawa watulivu kana kwamba viti vimekuwa sumaku.

Wamefika nusu safari, bintiye katulia kama maji mtungini. 

Sasa kazi kukilea kitoto chao, kibinti hiki kilichomlanda mamake kama shilingi kwa ya pili.

Badala yake liliuchochea, kama moto kuvuvia. 

Nia yangu nyeupe kama pamba. 

Sasa mumewe anataka kujisiriba uchafu ule na kama mchezea tope, atarukiwa tu.

Ona umbo lako sasa, kama nguruwe.

Kisha kofi likaandamwa na teke lililomlaza kochini kama zigo lililosukumwa likajiangukia ovyo.

Ilikuwa kama kuchokoza nyuki. Lilia alimfungulia mlango akitetemeka kama unyasi upepo uvumapo. 

Tashihisi

Saa ukutani ilimwambia saa nane za usiku, 

Fikra zimechoka, mwenyewe hajiwezi; nusura yake usingizi uliomsomba, ukampa utulivu, japo wa muda tu. 

Kama si ulimi wa bintiye ambaye hatulii, kihoro kingemvamia labda hata kumvuta kuelekea kaburini.

Lakini hawakujua ajali ya barabara ingeyafuta maisha ya mama mtu. 

Nguo zilezile, usafi bado unampiga chenga.

Lakini dhiki ziliwaandama. 

Istiara

Isije ikawa mwenye nyumba kaja na yeye mpangaji akachelewa kumfungulia mlango.

Mbona Luka akageuka kuwa mzigo wa moto, habebeki, habebeki kamwe? 

Yamekolezwa ladha na sauti, asali kando. 

Akatamani kufika nyumbani apumzike, kazi ya kuwalisha kondoo wa Mungu si kazi rahisi.  

Lilia, malaika wake, hampi utulivu wa kuwazia sana kuhusu upweke wake.

Naye wembe masomoni, akili zake sumaku, hunasa yote wafunzayo walimu.

Kaloa, katota hili penzi la jogoo la mji. 

Na ule ulimi wake uliodondoka asali, waumini wakampenda.

Kwake siasa ni mchezo mchafu.Lilia akatambua rangi halisi ya mumewe.

Tamaa ndiyo ibada yake, Ulaghai sasa ndiyo ibada yake kubwa, mhubiri keshakuwa mhadaifu. 

Ulimfanya mkeo ngoma kwa sababu ya hawara ambaye hakuthamini hata chembe. 

Semi na Nahau

roho mkononi, pumzi zikimwenda mbio- yaani kwa wasiwasi tele.

nyanyaso moto mmoja- yaani tele, zisizokoma.hakuwa na budi- alilazimika,

hakuwa na lingine yalikuwa yale yanayodaiwa kumtoa nyoka pangoni- yalivutia sana akawa hoi- akachoka sana. 

kufunga pingu za maisha- kuoana.

unampiga chenga- unamheparafiki yake wa kufa kuzikana- rafiki mkubwa/wa dhati.

 binti hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini- hasikii lolote wala yeyote. kumvunja moyo- kumuumiza hisia. 

wakafunga pingu za maisha- wakaoana. Lilia alipigwa na butwaa- alishangaa alipokataa katakata- alipokataa kabisa. 

kumuunga mkono- kumsaidia kutimiza azma yake, kukubaliana naye. hajali habali- hajali hata kidogo, hajali chochote. 

utajua kilichomtoa kanga manyoya shingoni- utaingia mashakani/utaumia.

Akamkaribisha kwa mikono miwili- akamkaribisha vizuri, kwa ukuruba mzuri.

amepata nafuu- hali yake imeimarika/ afya yake imeimarikaaage dunia- afariki, akufe. 

Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi 

Lilia anapopita karibu na kioo, anaona mabadiliko usoni mwake; kovu na donda linaloelekea kupona.

Yanamkumbusha vita vya awali vya mumewe, na sura yake ya zamani. 

Anakumbuka alipokutana na Luka kanisani, akampenda na kumsihi babake wamsaidie.

Wakaenda shule pamoja hadi wakaoana na babake kuaga, huku akimwachia Luka usukani wa kanisa. 

Anakumbuka mabadiliko ya Luka baada ya babake kuaga; kuuza kanisa na kuanza kumdhulumu.

Akaingilia siasa licha ya kujaribu kumshawishi, na kutwaa ugavana, kisha akageuka katili. 

Anakumbuka zaidi hatua yake ya kumripoti ilivyotibuka baada ya kugundua mkuu wa kituo ni rafiki ya mumewe, na wasiwasi uliompata akijua mumewe ataambiwa. 

Lilia anapofika katika kituo cha polisi, mkuu wa kituo anamweleza kuwa alikuwa na mumewe Lilia siku iliyotangulia katika hoteli moja. 

Mama Luka anapompeleka Lilia hospitali, anashangaa vipi Luka amesahau fadhila alizofanyiwa na babake Lilia.

Mamake Luka anamkumbusha alivyomgeuza mkewe ngoma kwa ajili ya kimada asiyemjali.

Alimweleza kuwa alikuja siku ya kwanza kumwona, kisha siku ya pili akageuka na kuondoka aliposikia hawezi kutembea tena. 

Maswali Balagha

Mbona ikawa hivi?

Mbona Luka akageuka kuwa mzigo wa moto, habebeki, habebeki kamwe?

Nitapata wapi mwandani kama mke wangu marehemu? 

Afanye nini baba mtu? Chuo kimoja, bahati gani hii? Mume wako? Tena lipi haliwezi kusubiri hadi mwisho wa juma? Je, huyu mwenzangu kapiga simu naye? Bwana gavana, uko hapa? 

Gavana yupi huyu na mbona wako chumba kimoja?

Siku nne wamekuwa chumba kimoja na mumewe na hana habari? 

Yu wapi yule kirukanjia wako? Wajua yuko wapi? … waona sasa? Atakutunza nani? Atakuuguza nani, maana kwako fadhila za punda ni mashuzi!

Taharuki.

Kisa kinapoanza, tunaachwa na maswali mengi.

Tunashangaa ni nani haswa Lilia anayengoja na kwa nini anamwogopa kiasi hicho.

Kumbukumbu zake zinatujibu baadaye. Baada ya masimulizi kuhusu matukio ya awali katika maisha ya Lilia, ni wazi kwamba mumewe atamtesa akirejea.

Tunabaki na hamu kubwa ya kujua tendo atakalofanya akirejea baada ya mkewe kukosa simu yake na kujaribu kumripoti polisi.

Lilia anapoamka na kupata mtu mwinine kalazwa kando yake, hajui ni nani.

Tunabaki na hamu ya kujua ni nani hadi mama mkwe anapoeleza baadaye, ndipo tunafahamu ni Luka.

 Mwisho wa hadithi pia unatuacha na maswali mengi.

Hatujui maisha ya Luka yanachukua mkondo gani baada ya kupoteza uwezo wa kutembea, hatujui iwapo mkewe atamtunza, hatujui iwapo atabakia kuwa gavana.

Hatujui kama mienendo yake itabadilika au atabakia katili alivyo. 

Kinaya

Tunaambiwa kuwa Lilia ana tabia za kiutu uzima wala hana marafiki wa umri wake.

Ni ajabu kwa kuwa aghalabu watu huwa na marafiki wa umri wao. 

Babake Lilia anawatenganisha Luka na bintiye ili kukatiza urafiki wao.

Badala yake, tendo hili linachochea zaidi urafiki huo.

Luka anamwachisha mkewe kazi kwa madai ya kumtaka kudhibiti pesa za kanisa.

Kinaya ni kuwa bado yupo mhasibu wa kanisa anayefanya kazi nzuri. 

Luka anamtaka mkewe kuandamana naye katika kampeni ili watu waone kiongozi anayethamini ndoa na familia.

Ukweli ni kuwa hamthamini mkewe wala familia.

Hata mkewe kupoteza mimba si hoja kwake. 

Luka anampiga mkewe kwa kumtembelea bila habari akidai anamwaibisha na kuwafanya wapinzani wake kusema ameshindwa kudhibiti mkewe, sembuse kaunti nzima.

Ukweli ni kuwa Luka anajiaibisha mwenyewe kwa vitendo vyake, na kaunti imemshinda kudhibiti. 

Lilia anapomwuliza mumewe kuhusu mwanamke wanayeandamana, anapokea kichapo, huku Luka akimwonya kuwa akichezea ukarimu wake atajipata nje akiombaomba.

Ukarimu wake si ukarimu. 

Methali

Mvumilivu hula mbivu. 

Usione wembamba wa reli ukashangaa garimoshi kupita pale.

Mstakabali wa binadamu ni usiku wa gizaYaliyopita si ndwele Umdhaniaye ndiye kumbe siye Kuro haisemi uongo Lisemwalo lipo, kama halipo li njiani laja. Mwanzo wa ngoma ni leleFadhila za punda ni mashuzi Uliacha mbachao kwa msala upitao Taswira 

Sura ya Lilia anapojitazama kiooni na ile ya awali; “kovu shavuni, donda linaloelekea kupona kipajini.

Alikumbuka sura aliyozoea kuiona.

Lile kovu shavuni halikuwepo, badala yake ngozi nyororo,iliyojishobwekea na vidu kudhihiri kila alipocheka.” 

Luka anapoingia kanisani mara ya kwanza.

“Nywele zilikuwa matimutimu, uso umechora mistarimieupe… Shati refu limemfika magotini, upande mmoja halikuchomekwa kiunoni.

Shati lenyewe lilikuwa mararu, limemganda mwilini kama kigaga.

Suruali fupi ambayo uzi umetokeza kiunoni, bila huo uziingejidondokea.” 

Kipigo cha kwanza cha Lilia; “Jioni ile alipofungua mlango…,alipokezwa kofi ambalo lilimfanya kuona vimulimuli.

Kisha kofi likaandamwa na teke lililomlaza kochini…”Taswira ya kipigo kinachomlaza hospitali; “Lilia alimfungulia mlango akitetemeka kama unyasi upepo uvumapo.

Mara akashikwa nywele, karibu zing’oke.

Kisha akabururwa hadi kwenye chumba cha malazi.

Si kipigo hicho.

Si makofi, si ngumi, si mateke, tena ya mtu aliyevaa buti.” 

Tabaini 

Si bughudha hizo, nyanyaso moto mmoja.

Si utamu wa maneno huo!

Ni yale yanayodaiwa kumtoa nyoka pangoni.

Si wahubiri wenza, si wazee wa kanisa, si washiriki, waote walimtaka kuoa tena… Na si kichapo hicho alichochapwa.

Si makofi, si ngumi, si mateke, tena ya mtu aliyevaa buti.

Tanakali za Sauti Alitega sikio ndi! Chumba cheupe pe!Lilia alikuwa amelala fofofo, 

Sadfa

Anapoelekea kwenye chumba cha kulala, Lilia anasadifu kupita mkabala na kioo, na hapo anayaona mabadiliko ya sura yake.

Luka anapoingia kanisani, inasadifu kuwa nafasi iliyo wazi ni pale tu alipoketi Lilia, hivyo analazimika kuketi naye.

Pia, mjo wake unasadifiana na funzo linaloendelea kuhusu kumpenda jirani, Lilia anauona mjo huo kama mtihani kutoka kwa Mungu kuhusu funzo hilo. 

Luka anapowasilisha wimbo wake, inatokea sadfa kuwa mhubiri ndio anakuja kuwataarifu muda umekwisha, na hapo anaisikia sauti yake tamu. 

Babake Lilia anafanya kila juhudi kuwatenganisha Lilia na Luka.

Sadfa inawakutanisha tena wanapohudhuria chuo kikuu kimoja.Inasadifu kuwa Lilia anapomtembelea Luka ofisini mwake bila taarifa, kimada wake pia amefika, hali inayozua mtafaruku kati yao. 

Lilia anapofika kuripoti mumewe, anaitiwa mkuu wa polisi. Inasadifu kuwa mkuu huyo anajuana na mumewe, na hata walikuwa pamoja siku iliyotangulia.

Lilia anapogutuka baada ya kuzirai kutokana na kipigo cha mumewe, hajui amwite nani kwani mumewe anamkataza kuwa na urafiki na majirani.

Kisadfa, anaiona simu yake chini ya kitanda na anapoibonyeza, nambari anayokutana nayo kwanza ni ya mama mkwe. 

Lilia na mumewe wanakutana hospitalini kisadfa.

Lilia akiuguza majeraha ya kupigwa naye, Luka anahusika kwenye ajali na kuletwa pale pale alipolazwa Lilia. 

Majazi

Lilia. Anamlilia babake hadi anapokubali kumsaidia Luka.

Analilia ndoa yake Luka anapobadilika na kuanza kumpiga.

Anamlilia Mungu kwa maombi ambadilishe mumewe.

Anapopigwa na kuzirai, anachukua simu na kumlilia mkwewe.

Imani. Jina la babake Lilia.

Anawajaza watu imani katika dini kwa kuwa yeye ni mhubiri.

Licha ya shauku yake kwa Luka, anamruhusu kumwoa Lilia akiwa na imani wataishi vyema.

Anamsaidia Luka kupata elimu na hata kumpa mamake kazi. 

Luka. Ni jina la mmojawapo wa waandishi wa Biblia na wahubiri wa injili ya Yesu.

Kabla ya kuingiwa na uovu, Luka ni mhubiri mzuri mwenye waumini wengi na anayefahamika sana.

Watu wanatoka pembe zote kuja kupokea miujiza kwake.Mbinu nyingine ni kama vile Utohozi, Lakabu, Kejeli, Nidaa, Takriri, Dayolojia, Kuchanganya Ndimi, Chuku na Uzungumzi Nafsia. 

Join our whatsapp group for latest updates

Download Fadhila za Punda summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?