Kifo cha Suluhu summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine

Share via Whatsapp


Kifo cha Suluhu- Dominic Maina Oigo.

Mtiririko

Abigael na Natasha wanasimuliana masaibu yao yanayowalazimu kuwa kupe wa kunyonya wanaume.

Wamekulia eneo moja na kupatana na hali ngumu ya maisha hadi wakakinai.

Abigael yuko mwaka wa tatu na kapitia taabu tele.

Ameomba na kutafuta misaada, hata kwa gavana lakini hapati.

Natasha naye amesoma kwa zaidi ya miaka saba kutokana na ukosefu wa hela.

Huku wakila chumbani wanamoishi pamoja, Natasha anamtolea Abigael wazo la kumtilia Suluhu, mpenzi wake wa sasa, dawa ya usingizi ili apate fursa ya kumpora. 

Abigael anakutana na Suluhu kwenye chumba cha hoteli na anapomwandalia kinywaji, anamtilia dawa kwa maagizo ya Natasha na kumnywesha.

Suluhu anawazia kumshawishi awe mkewe wa kando akipata njia ya kumwangamiza mkewe.

Dawa inaanza kufanya kazi na hapo anavamiwa na usingizi mara moja.

Abigael anatoa kisu cha makali kuwili kwenye mfuko aliozoea kubeba ambao alinunuliwa na Suluhu, tayari kummaliza.

Anaamua kumpora kila kitu kabla ya kumwua.

Anatoa kibeti na kupata noti za shilingi mia mbili mbili.

Kuna vijikaratasi kadhaa. Kimoja kinasomeka vizuri.

Anagundua ni barua na kuamua kuisoma.  

Barua inatoka kwa Bi. Suluhu.

Anasema anaamua kumwandikia mumewe kwa kuwa amemtenga kabisa.

Anamkumbusha kazi yake ya kuuza makaa ilivyofika hatima ya ghafla, kisha akatwaa ubunge kwa mbinu azijuazo Bi. Suluhu.

Anajua matendo ya mumewe; msichana wa chuo kikuu aliyemtunga mimba na kumwacha na hawara aliyepangia chumba mjini.

Amevumilia kwa ajili ya watoto na kuwalea, na wa kwanza amekamilisha darasa la nane. 

Anasisitiza jinsi anavyompenda, wala hajawahi kumwendea kinyume.

Zaidi, anamwahidi kuwa hatasema maovu yake.

Alimuua mama Abigael akihofia sheria baada ya kunyakua shamba lake.

Haleti maendeleo kwa kuwa anawalipa wasichana wa vyuo vikuu baada ya kula nao uroda.

Pia anatafuta pesa za kulipa Bwana Ngoma aliyefadhili siasa zake.

Anamuasa akome tabia zake kwa kuwa hali yake ni bayana.

Bi. Suluhu yuko tayari kuaga. Anamshukuru kwa mema aliyomtendea kabla ya kubadilika, na yale aliyotendea wazazi wake kuwahadaa anampenda.

Anamlaumu mumewe kwa kifo chake anahotarajia kutokana na kukosekana nyumbani na uzinzi, vinavyomletea msongo wa mawazo.

Anakiona kifo cha suluhu iwapo kitamfanya mumewe arejee nyumbani kuwatunza watoto.

Angeweza kumwua mumewe kwa kumtilia sumu lakini hakuhiari.

Anamwomba amkome Abigael asimwambukize nakama.

Anaahidi atazidi kumuasa siku alizosalia nazo hata asipomsikia. 

Barua hii inamliza Aigael. Amejua kitendawili cha kifo cha mamake aliyepatikana ameuawa.

Anakunja karatasi zile na kuzirudisha kibetini.

Anajuta kuingilia ndoa ya Suluhu.

Anaona kifo cha Suluhu hakitafaa lolote.

Kifo kifaacho ni cha maovu na kupalilia utu.

Anachukua kisu chake na kuondoka.

Anachukua daladala kuelekea chuoni.

Anafanya uamuzi wa kutia bidii kujipa riziki na kumwachia Mungu wajibu wa hukumu.  

Ufaafu wa Anwani ‘Kifo cha Suluhu’. 

Suluhu ina maana ya kusawazisha mambo ili yawe sawa.

Pia inaweza kumaanisha kuwa na nguvu sawa.

Mada ‘Kifo cha Suluhu’ inaweza kufasiriwa kwa maana tofauti.Kwanza, kuna mhusika kwa jina la Suluhu.

Mada hii inaweza kufasiriwa kurejelea kifo chake.

Abigael ananuia kumwua Suluhu ili kulipiza kisasi kwa kumtumia kama tambara bovu na pia ampore pesa zake.

Amebeba dawa ya kumtia usingizi na kisu cha makali kuwili kumwangamiza.

Kifo hicho hakitukii kwani Abigael anaghairi nia.

Anaona kuwa kifo hicho hakitakuwa na maana yoyote baada ya kusoma barua ya Bi. Suluhu.

Anamwacha Suluhu usingizini na kuondoka kurudi chuoni.  

Mada hii pia inaweza kufasiriwa kwa maana ya kifo cha kusawazisha mambo, yaani kifo cha kuleta suluhu.

Natasha na Abigael wanakiona kifo cha Suluhu kuwa suluhu kwa tatizo lao la hela.

Abigael anataka kumwua kisha kupora mali yake.Bi. Suluhu anaona kuwa kifo chake kitakuwa kifo cha suluhu.

Kwanza, kitakuwa kikomo cha tabu alizopitia maishani.

Pia anasema ni suluhu iwapo kitamwezesha mumewe kurudi kuwashughulikia wanao.

Suluhu anapanga kumshawishi Abigael awe mkewe wa pembeni baada ya kuwazia jinsi ya kumwangamiza mkewe.

Anakiona kifo cha mkewe kuwa cha suluhu kwa kuwa kitamwezesha kuwa na Abigael. 

Abigael anaposoma barua ya Bi. Suluhu, anaona kuwa kifo cha Suluhu sio suluhu ya aina yoyote.

Kifo cha kuleta suluhu ni kifo cha maovu yote katika jamii na waja kukumbatia utu.

Suluhu anamwangamiza mamake Abigael akihofia kuwa atamchukulia hatua ya kisheria baada ya kunyakua shamba lake.

Kwa Suluhu, hiki ni kifo cha suluhu, kwani kitamwezesha kumiliki shamba hilo bila matatizo. 

Mada hii pia inaweza kutoa maana ya suluhu yenyewe kufa, yaani nia ya kusawazisha mambo kufeli.

Kwa mfano, wananchi wanamchagua Suluhu kuwasaidia. Wanamwona kama suluhu ya shida zao.

Hata hivyo, kifo cha suluhu yao kinatokea Suluhu anapozamia uzinzi na kuwatelekeza.

Abigael anapania kumwua Suluhu na kupoka pesa zake, jambo analoliona kama suluhu ya shida zake.

Hata hivyo, suluhu hii iliyopendekezwa na Natasha kwa shida zao inakufa baada ya Abigael kusoma barua ya Bi. suluhu, inayomfanya kughairi nia ya kumwua Suluhu.  

Dhamira ya Mwandishi.

Kusawiri matatizo ambayo wanafunzi wa vyuo vikuu hupitia katika shughuli za masomo, hasa wale waliotoka familia maskini.

Anatoa onyo kwa watekelezao maovu kwamba siku yao ya kugunduliwa itafika.

Kudhihirisha viongozi wasiowajibika wanavyotekeleza maovu na kuwapuuza raia waliowachagua.

Anadhihirisha matatizo ya ndoa, hasa ndoa za wakubwa zilizojawa na ufuska.

Kudhihirisha hali ya utabaka katika jamii kwa misingi ya hali za kiuchumi.  

Maudhui  

Elimu

Abigael na Natasha ni wanafunzi katika chuo kikuu kimoja nchini.

Wanapitia hali ngumu kupata masomo kwa kuwa wametoka katika familia maskini. Inawabidi kuwa kupe kwa kuwanyonya wanaume ambao wanawapa uroda.

Wanaishi katika chumba kimoja ili kugawana gharama.

Isitoshe, Natasha amesoma chuoni kwa zaidi ya miaka saba kutokana na hali yao ya kimaskini.

Wanatamani pia kuwa na maisha mazuri kama wasichana wengine wanaowaona lakini hawana namna.

Abigael anapambana na hali yake si kwa maombi tu bali pia kwa kutafuta msaada kwa gavana wao.

Juhudi zake zinagonga mwamba. Anakubali rai ya Natasha ya kumpora Suluhu ili wapate hela, japo anaghairi nia baadaye.

Bi. Suluhu pia anadhihrisha nafasi ya masomo katika barua yake.

Anamweleza mumewekuwa amewasomesha wanawe na anajua mumewe atafurahi kuwa mwanambee wao ametamatisha masomo ya msingi.  

Uzinzi/Ufuska/Ukware/uasherati

Abigael na Natasha wanawategemea wanaume kwa ajili ya kupata hela kutoka kwao huku wakiwapa uroda.

Abigael anamwambia Natasha kuwa hana budi kuendelea hivyo, ili kukimu familia yake; babake na wadogo zake.

Abigael anamweleza Natasha kuhusu Suluhu.

Anamnyonya hela na kumpa uroda akijua vyema ana mke.

Mkewe anapata dhiki tele kutokana na ukware wa mumewe na hata kuonekana mzee kuliko alivyo.

Abigael anasema kuwa atazidi kumnyonya Suluhu hadi ajue kutulia katika ndoa yake.

Abigael na Suluhu wanapatana kwenye chumba kufanya uzinzi.

Chumba hicho si kigeni machoni mwa Abigael, kwani Suluhu amemleta hapo awali ili kutimiza ashiki yake.

Hata anapanga kumwangamiza mkewe ili Abigael awe mkewe wa kando.

Mkoba anaobeba Abigael alinunuliwa na Suluhu kama kiwakilishi cha penzi lao la haramu.

Katika barua ya Bi. Suluhu, anaeleza ukware wa mumewe.

Amemtia mimba msichana wa chuo kikuu na kumtelekeza.

Amempangia chumba mjini mwanamke mwingine.

Anamweleza kuwa hatasema kuwa anashindwa kuleta maendeleo kwa kufuja pesa akiwalipa wasichana anaokula uroda nao.

Isitoshe, anasema kuwa uzinzi wa mumewe umemletea nakama.

Anamtaka amkome Abigael asije akamwambukiza.

Ndoa

Katika hadithi, tunashuhudia ndoa kati ya Suluhu na mkewe ambayo imejaa misukosuko.

Abigael anasema kuwa mkewe Suluhu hana amani katika ndoa yake licha ya mali tele ya mumewe.

Anapigwa na maisha na kukonda, hata kuonekana mzee kuliko umri wake.

Ana wasiwasi kuhusu aliko mumewe mara kwa mara.

Barua ya Bi. Suluhu inaonyesha uchungu wake katika ndoa isiyo na sitara.

Suluhu anamwacha mkewe na kuandama anasa na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Hata watoto analazimika kuwalea peke yake.

Bi. Suluhu anamkumbusha makubaliano yao wakati wa kufunga ndoa, ambayo mumewe anayapuuza.

Bi. Suluhu anaonyesha pia thamani ya ndoa ya kuweka siri kwa kumhakikishia mumewe kuwa hajawahi wala hatatoa siri zake anazojua.

Hatasema kuwa alishindwa kuleta maendeleo kwa sababu ya kufuja pesa akiwalipa wasichana kwa ajili ya uroda, na pia kumfidia Bwana Ngoma hela alizomkopesha akifanya kampeni.

Hatasema kuwa ndiye alimuua mama Abigael baada ya kunyakua shamba lake.

Bi. Suluhu anasema yuko tayari kufa na kifo chake kitahesabiwa haki.

Amechoka na dhuluma za mumewe, ambazo zinamwumiza pamoja na wanawe.

Anamshukuru kwa ghiliba kwa wazazi.Aliwatendea mengi kuwahakikishia kuwa anampenda.Isitoshe, anamwona Suluhu kuwa sababu ya kifo chake.

Hili ni kutokana na upweke anaomwachia na mawazo mengi.

Anapomtembelea daktari anaambiwa kuwa afya yake iko sawa ila mawazo tu.

Anamkumbusha anathamini mapenzi yao, ndio maana hakuwahi kumdhuru japo angeweza kumsumisha.

Anakiona kifo chake kuwa cha suluhu kwa kuwa kitamwezesha mumewe kurudi kuwatunza wanao.

Anamtaka kumkoma Abigael asije akamwambukiza nakama. Anahisi kuwa muda wa kujuta kila mara unaelekea tamati.

Barua hii inamfanya Abigael kujuta kwa kuingilia ndoa ya Suluhu na mkewe. 

Nafasi ya Mwanamke

Mwanamke anachukuliwa kama chombo cha starehe.

Abigael na Natasha wanawategemea wanaume kwa kila kitu, huku wakiwapa uroda.

Bi. Suluhu analalamikia tabia ya mumewe ya kuwalipa wasichana wa vyuo vikuu baada ya kula nao uroda.

Amemtia mimba msichana wa chuo kikuu na kumtelekeza.

Mwanamke anachukuliwa kama kiumbe dhaifu.

Suluhu anamtelekeza mkewe, wala hana la kufanya.

Analazimika kuvumilia na kumuasa mumewe kwa kuandika barua.

Hata muda wa kuzungumza naye kama mkewe hapatiwi.

Mwanamke ni mlezi.

Bi. Suluhu anawalea wanawe peke yake.

Hata mumewe anamwambia kuwa wana hao ni wake pekee.

Yule wa kwanza ametamatisha masomo ya shule ya msingi.

Abigael naye analazimika kuwalea wanuna wake baada ya mamake kufariki.

Hata babake anamtegemea!

Mwanamke ni muuaji.

Natasha anampa Abigael dawa ya kumtia usingizi Suluhu ili aweze kumwibia.

Anafika chumbani wanamokutana na Suluhu akiwa na kisu cha makali kuwili, tayari kumwangamiza.

Isitoshe, tunaambiwa kuwa kila kijusi kinapotunga wanakitungua.

Mwanamke ni mwenye tamaa.

Abigael na Natasha wana tamaa ya pesa, hali inayowasukuma kuwapa uroda wanaume.

Wanafikia hatua ya kumtilia Suluhu dawa ili waweze kumpora.

Mwanamke ni mwenye bidii.

Abigael na Natasha wanatia bidii kwa kila hali kufanikisha masomo yao.

Mkewe Suluhu naye anajitolea kwa kila hali kuwakimu wanawe baada ya mumewe kumtelekeza.

Umaskini

Hali ya umaskini inawatia matatani Abigael na Natasha.

Wanalazimika kuwavutia wanaume ili wapate hela za kukidhi mahitaji yao.

Wamekulia katika eneo moja na kupigwa na upepo wa maisha vilivyo.

Suala la kuwa na maisha bora kwao linabaki kuwa ndoto.

Abigael yuko mwaka wa tatu chuoni na amepitia taabu sana chuoni humo.

Hajapata wa kumwauni. Anatamani kuishi maisha bora lakini uchochole wa wazazi wake unamzuia.

Anatafuta msaada hadi kwa gavana lakini hapati wa kumfaa.

Natasha amesoma chuoni kwa miaka saba na bado hajahitimu, kutokana na umaskini.

Wanaamua kupangisha chumba kimoja na Abigael ili kugawana gharama.

Umaskini unawasukuma kumpangia maovu Suluhu.

Kabla ya kutwaa uongozi, Suluhu pia yuko katika hali ya umaskini.

Biashara yake ya kuuza makaa inaenda kombo baada ya ukataji miti na kuchoma makaa kupigwa marufuku.

Hata pesa za kupiga kampeni anakopeshwa na Bwana Ngoma.

Migogoro

Suluhu ana mgogoro na mkewe kutokana na kutowajibika kwake katika ndoa.

Anamwachia mkewe jukumu la kuwalea wanao peke yake.

Anamlalamikia kupitia barua ambayo Abigael anaipata kibetini na kusoma.

Abigael anagundua mgogoro kati ya mamake na Suluhu uliosababisha kifo chake.

Suluhu ananyakua shamba lake na kumwua ili kujilinda kutokana na sheria.

Anahofia kuwa huenda mamake Abigael akamchukulia hatua za kisheria. 

Abigael pia ana mgogoro na nafsi.

Anaondoka kwa nia ya kumuua Suluhu.

Anapoisoma barua kutoka kwa mkewe, anakirihika na kumwacha Suluhu.

Anaamua kumwachia Mungu suala la hukumu.

Anajuta kwa kuingilia ndoa ya Suluhu.MauajiAbigael amefiwa na mamake.

Anagundua ukweli wa kifo chake kupitia barua ya Bi. Suluhu kwa mumewe anapomtaja mumewe kuwa muuaji wa mamake kwa kuhofia sheria, baada ya kunyakua shamba lake.

Bi. Suluhu anasema kuwa yuko tayari kufa kutokana na dhiki aliyopatilizwa na mumewe, Suluhu.

Anasema kuwa kifo chake kitahesabiwa haki kwani kitaleta usawa katika familia yake.

Anahisi kwamba mumewe ndiye sababu ya kifo chake.

Abigael na Suluhu wanhusiana kwa muda mrefu.

Kila mara Abigael anapopata mimba, wanapanga mauaji kwa kutafuta mbinu murua ya kuangamiza kijusi.

Suluhu vile vile anatafuta njia ya kumwangamiza mkewe ili Abigael awe mkewe wa pembeni.

Abigael ana nia ya kumwua Suluhu.

Anafika kwenye chumba wanamokutana huku amebeba kisu cha makali kuwili.

Anamtilia dawa ya usingizi kwenye kinywaji na kukitoa kisu. Kabla ya kumuua, anaona waraka kutoka kwa mkewe.

Anapomaliza kuusoma, anaghairi nia.

Mabadiliko

Suluhu na Abigael wamekuwa wapenzi kwa muda mrefu.

Wanapatana katika mambo mengi.

Hata hivyo, Aigael anabadilika na kunuia kumwangamiza Suluhu.

Suluhu hana habari kuwa Abigael anaweza kubadilika kiasi cha kutaka kumtoa uhai.

Suluhu anaponuia kumwoa mkewe, anajitolea kuwasaidia wazazi wake kwa kila hali.

Anamfurahisha mkewe pia.

Baada ya ndoa, anamtelekeza mkewe kabisa na hata kumwachia majukumu yote ya malezi.

Anazurura huku na huku akila uroda na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Hali ya Suluhu ya kiuchumi pia inabadilika. Awali, anapata riziki kwa kuuza makaa.

Anabadilisha hali hii kwa kumkopa pesa Bwana Ngoma na kujitoma katika siasa na kutwaa uongozi.

Anaanza kuishi kifalme.

Baada ya Abigael kusoma barua ya mkewe Suluhu, anaghairi nia ya kumuua Suluhu kama alivyodhamiria.

Anaona kuwa kifo hicho hakitaleta mabadiliko yoyote, bali kifo kinachofaa ni kifo cha maovu katika jamii.

Pia anaonelea kuwa hakimu wa kweli ni Mungu tu.

Kutowajibika

Suluhu hawajibiki katika ndoa yake kama mume.

Anamtelekeza mkewe na kumwachia majukumu yote ya ulezi peke yake.

Hali hii inamfanya mkewe kusongwa na mawazo kila mara akitaabika kuwazia aliko mumewe.

Suluhu pia anatelekeza wajibu wake kama kiongozi kwa kutojali maslahi ya wale waliomchagua.

Anatumia pesa anazofaa kuwahudumia nazo kulipia uroda kutoka kwa wasichana wa vyuo vikuu na pia kumlipa Bwana Ngoma aliyemkopesha wakati wa kampeni zake.

Natasha na Abigael hawawajibikii ujana wao.

Wanajinufaisha kutoka kwa wanaume kwa kuwapa uroda.

Hali hii inawaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya zinaa na ukimwi.

Abigael anapohimili, anatungua mimba akishirikiana na Suluhu. 

Unafiki

Abigael anamwendea Suluhu kwa upole katika chumba cha starehe wanamokutana.

Anamnywesha kinywaji chake kama mtoto na kumfanya ajihisi kama mfalme.

Ukweli ni kuwa ametia kile kinywaji dawa ya kumpa usingizi Suluhu ili aweze kumdhuru.

Suluhu ni kiongozi aliyechaguliwa na watu akiwaahidi kuboresha maisha yao.

Hata hivyo, anatumia wadhifa huo kujistarehesha kwa kuwalipa wasichana wa vyuo vikuu wampe uroda.

Suluhu anataka kumwangamiza mkewe ili Abigael awe mkewe wa pembeni.

Anajitia kumjali sana Abigael ilhali ndiye alimwua mamake baada ya kunyakua shamba lake.

Suluhu anaposhtakia nia ya kumwoa mkewe, anawafaa sana wazazi wake ili kuwatanabahisha kuwa anampenda mwanao.

Hata hivyo, baada ya kumwoa, anamtelekeza kabisa katika ndoa wala hajali maslahi yake.

Anajistarehesha na wanafunzi wa vyuo vikuu.Maudhui mengine ni kama vile Uongozi, Tamaa na Ubinafsi, Ubabebdume/Taasubi ya Kiume, Usaliti, Ukatili, Dini na Udhalimu.  

Wahusika: Sifa na Umuhimu. 

Abigael

Ni mzinzi.

Anawapa uroda wanaume ili aweze kuwanyonya hela zao.

Anamwambia Natasha kuwa ataendelea kumnyonya Suluhu hadi atakapojua kutulia katika ndoa yake na kumthamini mkewe.

Ni muuaji.

Anafika kwenye chumba wanamokutana na Suluhu huku amejihami na kisu, tayari kumwangamiza, japo anaghairi nia.

Kila akipata uja uzito katika uhusiano wake na Suluhu, anakiangamiza kijusi.

Ni katili.

Anamkwamilia Suluhu licha ya kujua kuwa anamsababishia mkewe mateso.

Anajua kuwa mkewe hana amani, hadi anaonekana mzee kuliko alivyo.

Pia ana nia ya kumuua Suluhu.

Ni kigeugeu.

Suluhu anampenda na kumkidhia mahitaji yake yote.

Anamnunulia kifuko cha kubebea vitu, na hata yuko radhi kumwangamiza mkewe ili awe na Abigael.

Abigael anamgeuka na kutaka kumwangamiza.

Isitoshe, anatupilia mbali nia hiyo baada ya kusoma barua ya mkewe Suluhu.

Ni msomi.

Ni mwanafunzi katika chuo kikuu, ambapo yuko katika mwaka wa tatu.

Umuhimu wa Abigael

Ni kiwakilishi cha matatizo yanayowakumba wanafunzi wa vyuo vikuu.

Kupitia kwake, udunishwaji wa mwanamke katika jamii unadhihirika wazi.

Ni kiwakilishi cha wasichana wanaonyakua waume za watu na kuwasababishia dhiki wake zao.

Anawakilisha unafiki na ukatili uliopo katika jamii.

Kupitia kwake, umuhimu wa kupinga maovu na kukumbatia utu unawasilishwa.  

Suluhu

Ni mzinzi.

Anamwacha mkewe na kwenda kula uroda na wasichana wachanga.

Anampachika mimba msichana mmoja na kumwacha bila tumaini.

Ufuska wake umemletea nakama.

Ni muuaji.

Anamwua mamake Abigael asiwe kikwazo kwake baada ya kupoka shamba lake.

Pia anadhamiria kumwua mkewe ili kumpa nafasi Abigael awe mkewe wa kando.

Kila Abigael anapohimili, wanashirikiana kuangamiza kijusi.

Ni msaliti.

Anamsaliti mkewe kwa kumwendea kinyume licha yake kumpenda kwa dhati.

Anamsaliti Abigael kwa kumwua mamake.

Anawasaliti raia kwa kutojali maslahi yao.

Ni asiyewajibika.

Anamtelekeza mkewe na kumwachia jukumu la malezi ya wanao.

Mkewe anamwambia kuwa hata wanawe wanajua matendo yake.

Anamwambia mkewe kuwa wana ni wake(mkewe) peke yake.

Anaponda raha na wasichana kwa hela za kuwahudumia wananchi.

Ni mnafiki.

Anawasaidia wazazi wa mkewe ili kuwatanabahisha kuwa anampenda na kumjali.

Anapomwoa, anamtelekeza na kutojali maslahi yake.

Anawahadaa wananchi kumpa kura, kisha kutumia wadhifa huo kujistarehesha.

Anajitia kumjali Abigael hali alimwua mamake.

Ni fisadi.

Ananyakua shamba la mamake Abigael na kumuua ili kujikinga dhidi ya sheria.

Anapangia msichana mmoja wa chuo kikuu kuhitimu kabla ya wakati wake ili ampe uroda.

Ni katili.

Anamuua mamake Abigael baada ya kunyakua shamba lake.

Anapanga pia kumwangamiza mkewe.

Anawatelekeza wananchi kama kiongozi na kuzidi kuponda raha.

Umuhimu wa Suluhu.

Ni kiwakilishi cha viongozi wasiojali maslahi ya wananchi na kuwajibikia nyadhifa zao baada ya kukwea mamlakani.

Kupitia kwake, uozo katika jamii unabainika kwa uwazi.

Ni kiwakilishi cha matatizo yanayokumba ndoa kutokana waume wasiowajibikia majukumu yao.

Ni kiwakilishi cha ukatili katika jamii, hasa unaopelekea mauaji ya watu wasio na hatia.

Bi. Suluhu

Ni mvumilivu.

Anapitia mengi katika ndoa yake lakini anavumilia yote.

Mumewe hajali maslahi yake hata kidogo, na hata wanawe anawalea pekee.

Ni mlezi mwema.

Mumewe anamtelekeza na kumwambia wanao ni wake peke yake.

Anajitolea kuwalea wanawe kwa kila hali, na yule wa kwanza ametamatisha masomo ya msingi.

Ni mwaminifu.

Anamweleza mumewe kuwa hajawahi kumwendea kinyume hata mara moja katika ndoa yao.

Ni mwenye mapenzi ya dhati.

Anampenda mumewe kiasi kwamba hata yuko tayari kumfia.

Licha ya kumtelekeza, bado anatimiza wajibu wake.

Anamwambia kuwa hakuwazia kumwangamiza licha nafasi tele za kufanya hivyo kujidhihirisha. 

Ni msiri.

Anamhakikishia mumewe kuwa atatunza siri zake anazojua hata katika mauti.

Anamweleza kuwa hataambia yeyote kuwa ndiye alimuua mamake Abigael, kuwa anashindwa kuwahudumia raia kwa kula uroda na wasichana kwa hela za kuwahudumia na pia kumlipa Bwana Ngoma aliyemkopesha wakati wa kampeni.

Ni mwajibikaji.

Anawajibikia wajibu wake kama mke licha ya vitimbi vya mumewe.

Anamtunza mumewe na kuwalea wanawe peke yake.

Umuhimu wa Bi. Suluhu

Ni kiwakilishi cha udhalimu unaoendelezwa dhidi ya wanawake katika jamii.

Anawakilisha matatizo yanayowakumba wanandoa, hasa wanawake.

Ni kiwakilishi cha wanawake ngangari wanaosimama wima kuzihudumia familia zao licha ya kutelekezwa na waume zao.

Ni kielelezo cha uvumilivu katika masaibu ya maisha.

Natasha

Ni mzinzi.

Anashirikiana na Abigael katika shughuli za kuwapa uroda wanaume ili kupata hela za kukidhi mahitaji yao.

Ni mshauri.

Anampa Abigael mpango kabambe wa kumpora Suluhu baada ya kumtilia dawa ya kumpa usingizi.

Ni mkakamavu.

Hakati tamaa ya masomo licha ya umaskini wake.

Amesoma kwa miaka saba na bado hajahitimu na yuko tayari kuendelea na masomo yake.

Ni mwenye tamaa.

Anamweleza Abigael jinsi ya kumpora Suluhu kwani tatizo walilo nalo ni pesa tu.

Ana tamaa ya kupata hela kwa haraka.

Ni rafiki wa dhati.

Yeye na Abigael wamekulia katika kijiji kimoja na kupitia mengi katika maisha yao.

Anashirikiana na Abigael chuoni kwa kila hali. Wanaishi chumba kimoja na kupambana na dhiki za maisha pamoja.

Umuhimu wa Natasha.

Ni kiwakilishi cha dhiki na matatizo ya wanafunzi katika vyuo vikuu.

Kupitia kwake, ukware unadhihirika katika jamii, hasa miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Ni kielelezo cha marafiki wa kweli wanaofaana katika dhiki na faraja.

Ni kielelezo cha ukakamavu katika kuandama azma zetu maishani.  

Mbinu za Uandishi  

Tashbihi

…wakazungushwa kama pia.

Bila kufanya ajizi…, alimwamsha na hapo akaanza kumnywesha kinywaji kama mtoto mdogo.

Alijiona kama mfalme.…basi nirudishie mfuko kama ishara ya kutupa penzi kama jongoo na mti wake.

Umejibaidi nami kama ardhi na mbingu.Sitachoka kukuasa hata ikiwa ni mfano wa kumchezea mbuzi gambusi.

Abigael alimaliza kusoma waraka ule huku machozi yakimbubunjika kama maji kwenye maporomoko.

Kisa cha mke wa Suluhu kilikuwa kama msumari wa moto kwenye kidonda kibichi…

Akahisi kama mwiba wa kujidunga usioambiwa pole.

Tashihisi

…wakapigwa na upepo wa maisha, wakazungushwa kama pia na hatimaye kutapikwa na dunia yenyewe bila simile.

“Mtazame mkewe Suluhu alivyochakaa na kupigwa na dunia.”

Hapo alijituliza… akili yake ilizidi kumsuta kwa kuoa kijanajike ambacho hakikujua maana ya kumpenda.

Moyo ulimpapa na woga ukamvamia.Mara alichomoa kibeti kilichokuwa kimetuna na kushiba.Juu ya kitanda, kisu chake kilimkodolea macho kana kwamba kinamwuliza, “Umesahahu kilichokuleta humu.?”…matumaini yangu ni kuwa utabadilika kabla ya siku yako kubisha hodi.

Aliyaacha machozi yamtoke shibe yake kwani asingeweza kujizuia.

Barua ile ilimfichulia siri si haba.Kisu chake kilikuwa pale pale juu ya kitanda kikiendelea kumkejeli na kumcheka Abigael.

Istiara

…wakapigwa na upepo wa maisha.

Lakini hilo lilibakia kuwa ndoto.

Jitihada… pandashuka za maisha zikawa kibwagizo cha maisha yake.

Ukiongezea wasiwasi wa mara kwa mara kuhusu aliko mumewe, hapo unamwongezea shubiri kwenye ladha kali ya maisha yake.Bwana Suluhu, naomba ujirudi ewe kiziwi hapo ulipo.

Kila mtu sasa anazungumzia kuabiri kwako garimoshi ambalo dereva wake unamjua sawasawa.

Imekuwa safari ndefu yenye pandashuka... 

Sina budi kukushukuru kwa yale mema uliyonitendea kabla ya wewe kujigeuza na kuwa mumunye.

Kitendawili cha kifo cha mamake aliyepatikana ameuawa na watu wasiojulikana kilikuwa kimeteguliwa katika barua hii.

Maswali Balagha.

Ni nani angemsaidia Abigael na kumwondolea ukungu njiani?

“Kwa nini nisiitumie fursa hii angalau name mtu?

Kwa nini?...”Ingewezekana vipi wakati wamekaa katika uhusiano wao kwa zaidi ya mwaka na kila kijusi kilipotunga, njia bora za kukiondoa zilitumiwa?

“Umesahau kilichokuleta humu?”

Kwa nini unataka kujitia hamnazo kuhusu ahadi ulizotoa?

Umesahau namna tulivyohangaika… na hatimaye tukabandikwa majina ya ajabu?

Umesahau, Mume wangu?

Umesahau namna kazi yako ya kuuza makaa ilivyofikia hatima ya ghafla baada ya serikali kupiga marufuku ukataji wa miti katika eneo la Dafrau?

Ama cheo chako… kimekulevya na kukufanya usahau familia yako?

…wajua kwamba yule binti wa chuo kikuu uliyepanga ahitimu kabla ya wakati wake alinieleza ulivyoishia kumtunga mimba na kumwacha bila tumaini?

Na je, wajua kwamba hata yule hawara mwingine uliyeishia kumpangia chumba kule mjini ili nisijue alinieleza kila kitu?

Semi na Nahau

Sina budi- sina lingine, inanibidi

sikuitia bahari chumvi- sikusababisha jambo hili. hatuna be wala te- hatuna chochote.

ndoto ya alinacha- ndoto isiyoweza kutimia.

kupiga hatua- kutekeleza jambo la maana. amejaribu juu chini- amejaribu kwa kila hali.

kugonga mwamba- kukosa kufanikiwa.

chungu nzima- tele, -ingi.

amevuna kuwili- amefaidika mara mbili kwa tendo moja.

kujitia hamnazo- kujipurukusha, kupuuza ukijua.

kupiga marufuku- kukataza, kuharamisha.

kwenda segemnege- kwenda kombo, kuharibika kwa mambo.

Akamtupia jicho- akamwangalia mara moja.

Takriri

Lakini hilo lilibakia kuwa ndoto.

Tena si ndoto ya hivi hivi tu bali ndoto ya alinacha. 

TakririUmesahau namna tulivyohangaika…?

Umesahau, mume wangu? Umesahau namna kazi yako ya kuuza makaa ilivyofikia hatima ya ghafla… naamini umesahau!

Nimevumilia kwa miaka mingi kwa ajili ya wanetu.

Nimevumilia madhila yako kwa muda mrefu… Kwa muda wote nilioishi nawe… Kwa muda wote tuliokaa pamoja

…Sitawaambia kuwa ulishindwa kuleta maendeleo…

Sitawaambia. Narudia, sitawaambia!Usidhani kuwa sikuwa na uwezo wa kukomesha vitendo vyako viovu.

Usidhani sikuwa na uwezo wa kukutilia sumu kwenye chakula na kukuangamiza.

Usidhani sikuwa na uwezo wowote.

Abigael aliona sasa kifo ambacho kilihitajika ni kifo cha dhuluma…

Methali

Jitihada ikabakia kutoondoa kudura(Jitihada haiondoi kudura)

Amlaye nguruwe huchagua aliyenona.

Ukitaka kumuua nyani usimtazame usoni.

Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Afriti hafichikiAlihisi kama mwiba wa kujidunga usioambiwa pole(mwiba wa kujidunga hauambiwi pole)

Kinaya.

Abigael anasema kuwa babake anamtegemea kwa kila kitu.

Ni kinyume baba kumtegemea mwanawe, tena mwana anayesoma.

Ndiye anatarajiwa kumsaidia mwanawe.

Abigael anasema kuwa mkewe Suluhu hana amani kutokana na mali ya mumewe.

Ni ajabu mali ya mumewe kumkosesha amani badala ya kumfariji.

Ni kinaya kuwa Suluhu anatafuta njia ya kumwangamiza mkewe, ambaye anafanya kila awezalo kumvumilia.

Ndiye analea watoto wao peke yake.

Anamtunzia siri zake nzito.

Ajabu ni kuwa Abigael, anayemfanya kuwazia haya ananuia kujinufaisha kutoka kwake, hata yuko radhi kumwua.

Bi. Suluhu analazimika kumwandikia mumewe barua kumpasha ujumbe wake.

Ni kinaya kuwa hana muda wa kuwasiliana na mume wake.

Suluhu anamkodishia kimada wake nyumba mjini ili mkewe asijue, ila kimada mwenyewe anamweleza mkewe kila kitu.

Ni kinaya kwa Suluhu kumwambia mkewe watoto ni wake peke yake.

Wanaume hutarajiwa kuonea fahari watoto zaidi ya wake zao.

Isitoshe, Bi. Suluhu anasema kuwa anajua mumewe atafurahi kuwa mwanao wa kwanza amekamilisha masomo ya msingi, ambayo Suluhu mwenyewe hajachangia!

Bi. Suluhu anasema kuwa kifo chake kitahesabiwa haki.

Ajabu ni kuwa amepitia mengi mikononi mwa mumewe hadi kuhiari kufa. Kwa hakika, kifo chake hakiwezi kuwa haki.

Abigael anagundua kuwa Suluhu ndiye aliyemwua mamake kupitia kwa barua ya mkewe.

Ajabu ni kuwa badala ya ukweli huu kumtia machungu zaidi kumwua, unamfanya kughairi nia na kumwacha hai.

Barua

Bi. Suluhu anamwandikia mumewe barua kumweleza uchungu anaomsababishia.

Mumewe ametengana naye na hapati fursa ya kuzungumza naye.

Barua hii inaanguka mikononi mwa Abigael.

Inadhihirisha kero anazopitia Bi. Suluhu na ukatili wa mumewe, ikiwemo kumwua mamake Abigael.

Inamwonyesha Abigael anavyomsababishia mateso na hata hatari anayojiweka kuhusiana na Suluhu aliyebeba nakama.

Inamfunza umuhimu wa utu na kumfanya kughairi nia ya kumwua Suluhu

Majazi

Suluhu- Anaondokea kuwa suluhu kwa Abigael kwa kumkidhia mahitaji yake baada ya kumpa uroda.

Anafanyia suluhu ugomvi wake na mama Abigael kwa kumwua akihofia sharia.

Dafrau- Ina maana ya kumbo.

Ni eneo ambalo Suluhu anauzia makaa kabla ya ukataji miti kuharamishwa.

Biashara yake yake inapigwa dafrau.

Bwana Ngoma.

Anafadhili kampeni za Bwana Suluhu.

Anamsaidia kunogesha ngoma ya siasa.

Taharuki

Abigael anapotaka kumwua Suluhu, anatoa kibeti na kuona karatasi ambayo ni barua.

Tuna hamu naye kujua ni nini kilichomo.

Mwishoni mwa hadithi, tunabaki na maswali kadhaa.

Kwanza, Abigael hajatimiza maangano yake na Natasha. Atamwelezaje akifika chumbani?

Hatujaambiwa iwapo Suluhu ameisoma barua kutoka kwa mkewe au la.

Na je, akiamka pale ataweza kujua yaliyotukia?

Atachukua hatua gani?

Abigael sasa amejua Suluhu ndiye alimwua mamake.

Je, atamchukulia hatua za kisheria au atamwachia Mungu suala lote la hukumu?

Abigael anaamua kutia bidii kujiandalia riziki.

Je, ataacha tabia ya kuwanyonya wanaume kwa kuwapa uroda?

Kuchanganya Ndimi“You know what darling, I bought this watch at ten thousand dollars…”

“Take this, my love. Ni ishara ya penzi letu ambalo linaanza kuchipuza…”

Koja…mabinti hawa wawili waliokulia eneo moja, wakapitia tabu tumbi akidi, wakapigwa na upepo wa maisha, wakazungushwa kama pia na mwishowe wakatapikwa…

Abigael aliona sasa kifo ambacho kilihitajika ni kifo cha dhuluma, unyonyaji, udanganyifu, wivu, kinyongo, tamaa, chuki, wizi na kutowajibika.

Tadmini

Bi. Suluhu anasema mumewe amemzidi Mfalme Suleimani kwa kujitwika hadhi na kusahau kila kitu kina mwisho wake.

Mfalme huyu, katika Biblia, alijizidisha hadhi yake kuliko Mungu.

Bi. Suluhu analinganisha mateso yake na yale Mtume Paulo aliyopitia gerezani.

Anamwandikia mumewe kama Paulo alivyomwandikia Timetheo kumjuvya hayo mateso.

Anahisi kama Paulo, amevipiga vita vyema na ana taji mbinguni.Anamalizia waraka wake kama Paulo alivyomalizia nyingi za nyaraka zake kwa kumwambia mumewe Amani ya Mungu iwe naye.

Dayolojia.

Mazungumzo kati ya Natasha na Abigael chumbani mwao.

Yanatusaidia kuelewa dhiki wanazopitia na mikakati yao ya kupambana nazo.

Inadhihirisha pia elimu yao katika chuo kikuu na misukosuko wanayopitia.

Kisengerenyuma/ Mbinu Rejeshi

Abigael anakumbuka kuwa amewahi kuwa chumbani waliko awali.

Anakumbuka kauli za Suluhu kuhusu saa yake aliyodai alinunua dola elfu kumi.

Anapochukua dawa ya kumtilia kwenye kinywaji, anakumbuka maagizo ya Natasha.

Tunaambiwa kuwa Suluhu na Abigael walikuwa wamekaa katika uhusiano wao kwa mwaka na kila kijusi kilipotunga walikiondoa.

Anapotoa kisu kwenye mfuko wake, anakumbuka ulinunuliwa mfuko huo na Suluhu kama ishara ya penzi lao, pamoja na agizo la kuurudisha mapenzi hayo yakifa.

Bi. Suluhu pia anamkumbusha mumewe kule walikotoka.

Alikuwa akiuza makaa na biashara ikasambaratika baada ya ukataji miti kupigwa marufuku.

Anamkumbusha binti wa chuo kikuu aliyemtia mimba na kumtelekeza na hawara aliyempangia chumba mjini.

Isitoshe, anamkumbusha kuwa alimuua mamake Abigael baada ya kunyakua shamba lake, na pia Bwana Ngoma alimkopesha pesa za kampeni anazolipa na kusahau raia wake.

Pia hasahau kumshukuru kwa wema wake kabla hajabadilika kuwa mwovu.

Anamshukuru kwa msaada aliowapa wazazi wake kuwatanabahisha anampenda.

Sadfa

Abigael anatoa kibeti cha Suluhu ili kupora hela zake.

Kisadfa, anakutana na karatasi ambayo anagundua kuwa ni barua na kuamua kuisoma.

Katika barua ya Bi. Suluhu, ametaja maovu ya mumewe aliyoweka siri, ikiwemo kumwua mamake Abigael.

Barua hii inaanguka mikononi mwa Abigael kisadfa na kumsaidia kutegua kitendawili cha kifo cha mamake.

Mbinu nyingine zilizotumika ni pamoja na Nidaa, Mdokezo na Utohozi.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kifo cha Suluhu summary notes - Mwongozo wa Mapamazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?