- Kukanusha
- Kukanusha Wakati Uliopita (LI)
- Kukanusha Wakati Timilifu (Uliopita Muda Mfupi) (ME)
- Kukanusha Wakati Uliopo (NA)
- Kukanusha Wakati Ujao (TA)
- Kukanusha Wakati wa Mazoea (HU)
- Kukanusha Wakati Usiodhihirika (A)
- Kukanusha KI ya Masharti (KI)
- Kukanusha PO ya Wakati (PO)
- Kukanusha Hali ya Uwezekano (NGE)
- Kukanusha Hali ya Uwezekano (NGALI)
- Kukanusha Amri/Agizo (-a/-e)
- Kukanusha Viunganishi vya Kujumuisha (NA, KA)
- Kinyume
Kukanusha
- Kukanusha ni kukataa au kukana kauli.
- Mara nyingi tunapokanusha, tuanaongeza kiambishi 'HA-' mwanzoni mwa kitenzi. Hata hivyo, kiambishi hicho hubadilika katika nafsi ya kwanza na ya pili umoja. Angalia jedwali lifuatalo.
KIAMBISHI MATUMIZI MFANO SI nafsi ya kwanza si-ku-wa-on-a HU nafsi ya pili hu-ni-faham-u HA nafsi ya tatu ha-ta-chuku-a - Viambishi vya wakati na vya hali pia hubadilika kama ilivyoonyeshwa katika ifuatavyo:
Kukanusha Wakati Uliopita (LI) - 'KU'
- Kajuta alimpigia kura. - Kajuta hakumpigia kura.
- Nilikupa nafasi yako. - Sikukupa nafasi yako.
Kukanusha Wakati Timilifu (Uliopita Muda Mfupi) (ME) - 'JA'
- Maziwa ya nyanya yamemwagika. - Maziwa ya nyanya hayajamwagika.
- Viwete wametembea. - Viwete hawajatembea.
Kukanusha Wakati Uliopo (NA) - '-I'
- Unasoma sentensi ya kwanza. - Husomi sentensi ya kwanza.
- Zinafanana na nyota. - Hazifanani na nyota.
Kukanusha Wakati Ujao (TA) - 'TA'
- Jua litawaka sana. - Jua halitawaka sana.
- Watakaribishwa kwenye malango ya lulu. - Hawatakaribishwa kwenye malango ya lulu.
Kukanusha Wakati wa Mazoea (HU) - '-I'
- Polisi wa jiji kuu huchukua hongo. - Polisi wa jiji kuu hawachukui hongo.
- Bendera hufuata upepo. - Bendera haifuati upepo
Kukanusha Wakati Usiodhihirika (A) - '-I'
- Anita ampenda Kaunda. - Anita hampendi Kaunda.
- Chema chajiuza, kibaya chajitembeza. - Chema hakijiuzi, kibaya hakijitembezi.
Kukanusha KI ya Masharti (KI) - 'SIPO'
- Ukimwadhibu mtoto, atapata adabu njema. - Usipomwadhibu mtoto hatapata nidhamu..
- Bei yake ikishuka, nitainunua. Bei yake isiposhuka, sitainunua.
Kukanusha PO ya Wakati (PO) - 'SIPO'
- Ulalapo usiku zima stima - Usipo lala usiku usizime stima
- Mtoto aliapo mnyonyeshe. - Mtoto asipo lia usimnyonyeshe
Kukanusha Hali ya Uwezekano (NGE) - 'SINGE'
- Ningekuwa nakupenda ningekwambia mapema. - Nisingekuwa nakupenda nisingekwambia mapema.
- Zingekuwa nyingi, wangeziiba. - Zisingekuwa nyingi, wasingeziiba.
Kukanusha Hali ya Uwezekano (NGALI) - 'SINGALI'
- Khadija angalisoma kwa bidii angalikuwa na cheo kikubwa. - Khadija asingalisoma kwa bidii asingalikuwa na cheo kikubwa
- Yangalikuwa mabivu yangalianguka yenyewe. - Yasingalikuwa mabivu yasingalianguka yenyewe
Kukanusha Amri/Agizo (-a/-e) - 'SI'
- Peleka kikapu hiki kwa nyanya. - Usipeleke kikapu hiki kwa nyanya.
- Chakula kiliwe. - Chakula kisiliwe.
- Mpende adui yako. - Usimpende adui yako.
- Waambieni watu wa mataifa yote. - Msiwaambieni watu wa mataifa yote.
Kukanusha Viunganishi vya Kujumuisha (NA, KA) - 'WALA'
- Bafi alikuzaba kofi na kukupiga teke. Bafi hakukuzaba kofi wala hakukupiga teke.
- Mama amepika chakula tukala pamoja. Mama hajapika chakula wala hatujala pamoja
Kinyume
- Maneno ya kinyume ni maneno yenye maana inayopingana.
- Inafaa ikumbukwe kwamba kuna tofauti kati ya kinyume na kukanusha. Kukanusha ni kukataa ujumbe wa sentensi bila kubadilisha maneno. Tunapokanusha, tunabadilisha viambishi pekee ili kupinga wazo la sentensi.
- Maneno ya kinyume huwa maneno mengine tofauti kabisa ambayo yanapingana kimaana bila kubadilisha maendelezo ya neno.
Kinyume cha Kawaida
Hisia, hali, dhana n.k
- vita - amani
- furaha - kilio
- nuru - giza
- shibe - njaa
- mwanzo - mwisho
Kinyume cha Sifa
Sifa zinazopingana kimaana
- tamu - chungu
- kubwa - dogo
- nzuri - mbaya
- nyeupe - nyeusi
Kinyume cha Jinsia (Uume - Uke)
Majina ya kijinsia moja yanabadilishwa na kuwa jinsia ile nyingine.
- baba - mama
- mumewe - mkewe
- mjomba - shangazi
- kaka - dada
- babu - nyanya
- mvulana - msichana
- ghulamu - banati
- shaibu - ajuza
Kinyume cha Uhusiano
Kinyume cha vitu au dhana mbili zinazohusiana.
- mwalimu - mwanafunzi
- daktari - mgonjwa
- mzazi - mwana
- kiongozi - mfuasi
Kinyume cha Vitenzi
Tunabadilisha vitenzi kwa kuweka vitenzi vingine vyenye maana inayokinzana
- ongea - nyamaza
- penda - chukia
- sifu - kashifu
- simama -keti
- lia - cheka
- tabasamu - nuna
- enda - kuja
Kinyume cha Kutendua
Vitenzi vinaweka katika kauli ya kutendua ili kuvikanusha.
- fumba - fumbua
- ficha - fichua
- vaa - vua
- anika - anua
- kunja - kunjua
Download Kukanusha; Kinyume - Sarufi na Matumizi ya Lugha Kiswahili Notes.
Tap Here to Download for 50/-
Get on WhatsApp for 50/-
Why download?
- ✔ To read offline at any time.
- ✔ To Print at your convenience
- ✔ Share Easily with Friends / Students