Utangulizi - Mwongozo wa Bembea ya Maisha

Share via Whatsapp

Bembea ya Maisha ni hadithi iliyoandikwa kwa njia ya mfano wa kuigiza. Mwandishi ni Dr Timothy Arege.

VIGEZO MUHIMU KATIKA UCHAMBUZI WA TAMTHILIA HII

 1. Dhamira/ Lengo/ Mintarafu/ Kusudi: Nijambo linalokusudiwa na mwandishi/ lengo kuu la mwandishi
 2. Maudhui: Jumla ya maswala yanayozungumziwa na mwandishi
 3. Falsafa: Msimamo wa mwandishi kuhusu jambo fulani
 4. Muwala: Mtiririko wa vitushi/ mawazo katika kazi ya Bembea ya Maisha
 5. Usuli: Asili /hali inayomzunguka mwandishi na ambayo humchochea kuandika kazi ya fasihi k.m. usuli wa mwandishi waweza kuwa anazungukwa na jamii iliyojaa uongozi mbaya / ufisadi ndiyo maana anaandika kuhusu maudhui
 6. Mandhari: Mahali ambapo wahusika wanatekelezea kazi ya K.m. njiani, shuleni n.k.
 7. Wahusika: Ni viumbe ambao huendeleza mawazo ya mwandishi katika kazi ya Wahusika waweza kuwa binadamu, Wanyama, viumbe halisi au wa kidhahania (wa kufikirika tu).

AINA ZA WAHUSIKA KATIKA FASIHI

 1. Wahusika wakuu
  • Huchukua nafasi kuu na kukuza kazi ya fasihi.
  • Matendo yote muhimu huwahusu.
  • Dhamira kuu ya mwandishi na falsafa/ msimamo wake hudhihirika kupitia kwa wahusika wakuu.
 2. Wahusika wadogo
  • Hawana nafasi kubwa.
  • Aghalabu husaidia hadhira kujua zaidi mhusika mkuu na dhamira yake.
 3. Wahusika wasaidizi
  • Hujenga wahusika wakuu na kukuza maudhui. Aghalabu huja na kutoweka baada ya muda mfupi.
  • Uainishaji Mwingine wa Wahusika
 4. Wahusika bapa/ Wahusika wa mraba mmoja
  • Huwa hawabadiliki katika hulka/ sifa zao.
  • Mhusika bapa anaweza kuwa na tabia nzuri au hasi kuanzia mwanzo hadi mwisho.
 5. Wahusika duara/ wahusika wa miraba minne
  • Huweza kubadilika kisaikolojia.
  • Huwa na sifa nyingi.
  • Wahusika bapa vielelezo
  • Huwa na tabia za kubadilika ila hujikita katika mtazamo wa mwandishi na hadhira yake.
  • Aghalabu huwa wahusika wakuu na hutumiwa na mwandishi kuendeleza suala fulani.
 6. Wahusika bapa sugu
  • Wana sifa ya kutobadilika ila huwakilisha walio na tabia potovu katika jamii. Mhusika bapa sugu anayeweza kuwa mhusika mkuu.
 7. Wahusika hasidi/ wapinzani
  • Hulka zao ni kinyume na mtazamo wa maadili ya jamii.
  • Humpinga mhusika nguli.
 8. Mhusika nguli
  • Ni mhusika anayekinzana na mhusika hasidi kwani anawasilisha maadili katika kazi ya fasihi. Aghalabu huwa mhusika mkuu au mmoja wa wahusika wakuu.
 9. Mhusika shinda
  • Hukuza wahusika wengine kwa kuwa hupelekwa mbele kwa usaidizi wa wahusika wengine.
  • Huwa chini ya kivuli cha mhusika mkuu.
  • Kupitia kvake ndipo hadhira inapata sifa bayana za wahusika wakuu.

FANI ZA FASIHI/ MITINDO KATIKA FASIHI

Fani ni mbinu ambazo hutumiwa na mwandishi anapoiandika kazi ya fasihi. Fani hujumuisha:

 1. Mitindo ya lugha: Pia huitwa matumizi ya lugha, mitindo ya lugha, tamathali za lugha, mbinu za lugha au tamathali za usemi.
 2. Mintindo ya uandishi: Pia huitwa fani za mwandishi, mbinu za uandishi, mbinu za sanaa au mbinu za usanii.

FANI ZA LUGHA (TAMATHALI ZA USEMI)

Ni maneno, sentensi au misemo inayotumiwa kuwasilisha kazi ya fasihi. (Senkoro; 1982). Zinajumuisha:

 1. Takriri/ Uradidi (Repetition): Takriri ni mbinu ya lugha ambayo kwayo maneno au silabi fulani hurudiwa. Lengo kuu la takriri huwa ni kusisitiza jambo fulani na kuwavutia wasomaji wawazie jambo hilo.
 2. Maswali Balagha/ Mubalagha (Rhetoric; questions): Haya ni maswali ambayo hayahitaji majibu. Jibu la swali la balagha huwa akilini mwa anayeulizwa au anayesoma kazi fulani ya fasihi au huwa tayari analijua. Dhima ya maswali balagha huwa kutoa mawazo au hisia za ndani za mhusika au kuweka jambo fulani wazi. Aidha hulenga kusisitiza usemi fulani na kuwasilisha maudhui.
 3. Methali: Ni kauli fupi ya kimapokeo inayosheheni maana na ujumbe na ambayo huwa na mizizi katika jamii. Methali huwa na wingi wa hekima na hutumiwa kupigia mfano. Huwa na maana iliyofumbwa.
 4. Tanakali ya sauti: Ni mbinu ambapo mwandishi huiga tendo fulani na kulipa matamshi au maandishi.
 5. Tashbihi/ Tashbiha/ Mshabaha: Ni ulinganishi/ umithilishaji (usio wa moja kwa moja) wa kitu na kingine kwa kutumia maneno kama vile: ja, mfano wa, mithili ya, kama, sawasawa, ungedhani ni n.k.
 6. Istiara/ Sitiari: Ni ulinganisho wa kitu na kingine kwa njia ya moja kwa mojae Ulinganishi huu hufanywa bila kutumia vifananishi.
 7. Nidaa: Ni maneno ambayo hutumiwa kuonyesha hisia za wahusika. Hutumika kuonyesha hisia za furaha, huzuni, masikitiko, mshangao, mshtuko n.k.
 8. Jazanda: Mwandishi hutaja kitu fulani ambacho kwa kawaida kinaweza kuonekana kuwa na maana ya kawaida ila kinapochunguzwa zaidi kinaonekana kuwa na maana ya ndani kuliko ile ya kawaida. Jazanda ni sawa na kilichositiriwa ndani mwa neno au maneno fulani.
 9. Mdokezo: Mbinu ambapo mhusika mmoja hutaja jambo kisha mwenzake hulikamilisha au mhusika hutoa wazo/ jambo na kumwacha msomaji kulikamilisha. Aidha, mdokezo waweza kutokea palipo na upinzani ambapo mhusika mmoja anaweza akatoa jambo huku mwenzake akilikamilisha atakavyo kwa kumpinga au kumkejeli.
 10. Tabaini: Tabaini ni mbinu ya lugha ambapo mwandishi hutumia maneno kueleza jambo linaloeleweka waziwazi na msomaji. Ni maelezo ya kina kuhusu j ambo. Waandishi wengi hutumia takriri/ neno moja ili kuibua tabaini. K.m. urudiaji wa 'ni' na 'si'. K.v. Walifika watu wa janibu mbalimbali: si wanawake, si wanaume, si vijana, si watoto — wote walijumuika kumuaga gwiji wa taarabu.
 11. Taniaba: Taniaba yatokana na 'kwa niaba ya'. Kitu/ Jambo hutumiwa kuwakilisha au kufanya kwa niaba ya kitu/ jambo jingine. K.m. chaki ni taniaba ya mwalimu; jembe ni taniaba ya mkulima ilhali bunduki ni taniaba ya askari.
 12. Utohozi: Ni mbinu ya kuswahilisha maneno ya lugha nyingine ili yatumike kama ya Kiswahili. K.m. skwota — Squatter, ekisirei X-ray n.k.
 13. Tasfida/ Tauria/ usafidi (Euphemism): Matumizi ya lugha ya adabu/ ya sitara/ ya nidhamu. K.m. Natoka kutabawali (Haja ndogo) badala ya natoka kukojoa; Alijifungua badala ya alizaa n.k.
 14. Chuku/ Udamisi (Exaggeration/ Hyperbole): Mbinu ya kuongeza chumvi katika jambo. Mwandishi hueleza jambo kwa namna inayozidi hali halisi ya jambo hili. K.m. watu waliohudhuria matanga walikuwa wamcjaa pomoni hivi kwamba hapakuwa na nafasi ya nzi kupita.
 15. Ucheshi/ Kichekesho (Humour): Maneno yanayozua furaha. Msomaji hucheka kutokana na namna mwandishi alivyolieleza jambo.
 16. Kejeli: Pia huitwa dhihaka, kebehi, stihizai au mcheko. Ni kumfanyia mtu, jambo au kitu dhihaka au kumdunisha mtu au kitu kwa kuonyesha kuwa anachosema hakina thamani.
 17. Lakabu: Mbinu ya mhusika kupewa au kubandikwa jina na wahusika wengine au yeye mwenyewe kujibandika jina linaloambatana na sifa zake.
 18. Kuchanganya ndimi (Code mixing): Pia inaitwa kuchanganya lugha, kuchanganya msimbo au ndimi mseto. Ni mbinu ya kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili. K.m. Sina time ya wanawake.
 19. Kubadili msimbo (Code switching): Pia huitwa kuhamisha msimbo, kuhamisha ndimi au kuhamisha lugha. Ni mbinu ya kuchopeka sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Utofauti kati ya kuchanganya ndimi na kubadili ndimi ni kuwa katika kuchanganya ndimi, mwandishi huchanganya maneno ya Kiswahili na lugha nyingine katika sentensi moja ila katika kubadili ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi sanifu za Kiswahili.
 20. Ritifaa: Ni mbinu ya kuzungumza na mtu asiyekuwepo au aliyekufa. K.m. Mbona umeamua kuniacha duniani?
 21. Taashira (Symbolism): Ni mbinu ya kutumia lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani.
 22. Majazi: Mwandishi huwapa wahusika majina yanayoambatana na tabia au hulka zao.

FANI ZA UANDISHI (MBINU ZA SANAA)

 1. Taharuki (Suspense): Ni mbinu ya kumpa msomaji hamu/ tamaa ya kuendelea kusoma ili kujua kitakachofanyika baadaye.
 2. Sadfa (Coincidence): Matukio mawili hutokea kwa wakati mmoja bila kutarajiwa, kupangwa au kukusudiwa.
 3. Barua/ Waraka: Wahusika huandikiana barua. Nyimbo na Mashairi
 4. Ndoto/ Njozi/ Ruiya: Maono ya mhusika akiwa amelala.
 5. Uzungumzi nafsia/ Mjadala nafsia: Mhusika hujizungumzia mwenyewe.
 6. Mbinu rejeshi/ Kisengere nyuma: Mwandishi hurejelea mawazo ya msomaji kwa matukio ya awali hasa kupitia kwa masimulizi.
 7. Kinaya: matukio katika kazi ya fasihi kuwa kinyume na matarajio ya msomaji au hali halisi.
 8. Usemaji kando: Mhusika anayezungumza na wenzake hutafuta faragha labda kwa kuzungumza bila kumhusisha mwenzake au kupinda kichwa. Mhusika mmoja anaweza kuwa anamsengenya mwenzake/ au anapinga maoni ya mhusika mwenzake.
 9. Tadmini: mbinu ya kuchukua mtindo wa lugha au maneno kutoka kwa matini nyingine na kuweka katika matini fulani. Kwa mfano kuchukua vifungu vya Biblia kutoka matini ya Biblia na kuyatumia katika tamthilia. K.m. Amini amini nakwambia. (Kigogo).
 10. Hotuba: mazungumzo ambayo hutolewa kwa hadhira na mtu mmoja. Mazungumzo haya aghalabu huhusu jambo maalum.
 11. Tashihisi: pia huitwa uhuishi, uhaishaji au uhuishaji. (Personification): Ni mbinu ya kuvipa vitu visivyo na uhai sifa za au kutenda kama kitu kilicho na uhai.
 12. Utabiri/ ubashiri: Ni mbinu ya kueleza kuhusu mambo ambayo yatatokea baadaye.
 13. Mhusika ndani ya mhusika: mhusika fulani huiga maneno au matendo ya mhusika mwingine na kutenda kama yeye.
 14. Mbinu maarifa mtambuka: Msanii kuingiza maarifa ya taaluma (uwanja mwingine wa kitaaluma) katika kazi yake.
 15. Taswira: Ni mbinu ya mwandishi kutoa maelelzo kuhusu jambo au mtu yanayojenga picha (Mawazo ya akilini) ya jambo au mtu huyo hivi kwamba msomaji huona picha kamili ya kitu/ jambo au mahali hapo. Dhima ya taswira huwa kumwezesha msomaji aelewe zaidi jambo husika.

Aina za taswira

 1. Taswira muonjo/ mwonjo: msanii anaweza kutueleza namna chakula kilionjwa hadi msomaji akataka adondokwe na mate.
 2. Taswira oni: msanii hutoa maelezo hadi msomaji akaona picha ya kitu/ jambo fulani mawazoni.
 3. Taswira hisishi: msanii anaweza kueleza hisia za mhusika fulani kama furaha, majonzi n.k.
 4. Taswira msanii anaeleza jinsi ambavyo alisikia jambofulani kwa nakini.
 5. Taswira mnuso: msanii anaeleza mambo kuhusu harufu anayoingiamua kupitia pua,
 6. Taswira mguso; msanii anaeleza alivyohisi kwa mguso.

Katika maandalizi ya kuukabili mtihani(kuyajibu maswali), ni vyema mwanfunzi azingatie mambo yaliyo hapa chini ili aweze kuyamudu maswali yatakayotokana na kazi anazozishughulikia.

 • Isome kazi mara kadhaa ili kuifahamu kazi husika ndani nje. Kuisoma kazi mara moja na kujidanganya kuwa umeielewa si vyema. Hakikisha kuwa umeyafahamu mambo yote muhimu katika kazi ya fasihi na kuyahifadhi katika ncha za kucha zako(yakumbuke kwa urahisi).
 • Wakati wa kusoma kazi hizi, hakikisha kuwa una penseli ili kupiga nmstari mambo yote muhimu k.m mbinu za lugha, wahusika, nk. Vile vile hakikisha unaongeza pembeni mambo yote muhimu yanayojitokeza unapoendelea kutagusana na kazi.
 • Fahamu kuwa sehemu hizi tatu hutahiniwa. Kila sehemu hubeba alama 20.
 • Wakati wa kuyajibu maswali ya mtihani, mwanafunzi achague maswali ambayo anayamudu vilivyo ili kujizolea alama nyingi zaidi.
 • Mwanafunzi vilevile asipuuze mambo mawili yafuatayo wakati wa kuukabili mtihani;

Mambo ya Kuzingatia katika kujibu maswali ya Fasihi

Hati

Hati ni mwandiko yaani namna mtu anavyoandika. Hati huwa kigezo muhimu sana katika mtihani. Ni vyema mwanafunzi aandike kwa hati inayosomeka vyema kwa urahisi. Ukiandika kwa hati 'nadhifu' mtahini hatatatizika kuisoma kazi yako wala kutumia muda mwingi akijaribu kuisoma kazi yako. Ni vyema uzingatie namna ulivyofundishwa kuandika herufi katika chekechea. Herufi zingine zisizoeleweka ambazo wanafunzi huweza kuandika si za Kiswahili na hazina maana katika Kiswahili, ziepuke.

Makosa ya kisarufi

Japo makosa haya hayaadhibiwi katika karatasi hii ya 102/3, ni vyema mwanafunzi ayaepuke mno. Makosa haya yakikithiri yanaweza kuupotosha usahihi wa jibu kiasi cha mtahini kuamua kukuadhibu na bila shaka utakuwa umepoteza alama. Makosa mengine ya kuingiza herufi zisizo za Kiswahili kama vile 'X', 'C' nek katika kuendeleza maneno ya Kiswahili visivyo pia hupotosha umantiki na usahihi wa jawabu.

JINSI YA KUKABILIANA NA MASWALI

Baada ya kuisoma kazi yoyote ile ya Fasihi Andishi, mtihani hufuata. Kwa hivyo ni vyema kujihama na mbinu za kuyakabili maswali.

Mwanzo, fanya utafiti zaidi kuhusu usuli wa kazi unayasoma, falsafa au mtazamo wa mwandishi n.k. Ihakiki kazi yenyewe kwa undani ili kuhakikisha umeelewa maudhui, wahusika, matumizi ya lugha, mandhari na fani nyingine zilizomo. Ili kujitayarisha kuyajibu maswali katika mtihani wa fasihi, ni muhimu kuelewa kuhusu Uteuzi wa maswali.

Tatizo kubwa linalowakumba watahiniwa katika mtihani wa fasihi ni uteuzi wa maswali. Kati ya maswali saba yanayotahiniwa, mtahiniwa anatakiwa kuchagua maswali manne.
Ikumbukwe kuwa Riwaya, Tamthilia na Hadithi Fupi ni kati ya maswali haya saba yaliyotahiniwa. Kwa hivyo, hakikisha unaangazia yafuatayo katika sehemu hii;

 1. Uzito wa swali - kadiria uzito wa maswali kwa kuangalia alama zinazotolewa kando ya swali. Swali la alama 20 linahitaji hoja kumi zilizojadiliwa vyema.
 2. Hoja za kutosha. Usivamie maswali bila kuwa na hakika kama una hoja za kutosha kuyajibu kwani huenda utakwama katikati. Kama swali lina alama 20, hakikisha una hoja kumi zenye uzito.
 3. Kulielewa swali - Elewa swali na kuangalia kama lina vijisehemu. Iwapovijisehemuvyake vinahusiana na sehemu ya kwanza, jihadhari usije ukakosa kuonyesha uhusiano huo. chukua muda kuchagua swali, kwa
 4. Kuchagua swali kuandika vidokezo vya kulijibia kando ya swali lenyewe. Ni vyema kuchagua swali ambalo utapata zaidi ya alama 15.
 5. Kuyaelewa maagizo kumbuka kuwa, maswali hutungwa ili kujibiwa kwa kuzingatia maagizo. Unapaswa kulichukua jukumu la kusoma, kuelewa na kufuata maagizo. Kwa mfano, kuna maswali ambayo ni ya lazima, na maswali ya kuchagua. Kadhalika, maagizo hufafanua jinsi ya kuchagua maswali, k.v. jibu swali la tatu au la nne. Usijibu maswali mawili kutoka kitabu kimoja na kadhalika.
 6. Kuuelewa msamiati wa swali -- pamoja na maagizo, zingatia pia msamiati wa swali. Kwa mfano unapoambiwa - taja na ueleze, lazima uelewe kwamba, mtahini katika mwongozo wake wa kusahihisha, atakuwa na tuzo yakutaja mambo manne, kwa mfano, aghalabu utakuta neno manne limekolezwa wino.

Hakikisha kuwa una hoja nne zilizo sahihi. Iwapo utaandika hoja zaidi ya nne, mtahini atachukua hoja nne za mwanzo tu, hata kama umezikosea na hatatuza hoja zinazofuata japo zitakuwa sahihi.

AINA ZA MASWALI

Kuna aina mbalimbali za maswali. Kila moja yazo huwa na mahitaji yake. Kuna aina mbili za maswali yanayotokea katika tamthilia na vitabu vingine viteule: maswali ya insha na maswali ya muktadha wa dondoo.

Maswali ya insha huandikwa kwa nathari. Jiepushe na kudondoa hoja au kuziorodhesha. Wakati ambapo maswali ya insha yanahitaji majibu ya kina na hoja zilizofafanuliwa kikamilifu, yale ya muktadha yanamhitaji mtahiniwa awe ameielewa tamthilia kwa undani ili aweze kufafanua muktadha wa dondoo alilopewa bila kukatizika. Hii itamwezesha kulitambua dondoo lilikotolewa kwa urahisi.

Katika kufafanua muktadha wa dondoo, mtahiniwa anahitajika kujibu maswali manne kwa usahihi:

 1. Nani anaongea?
 2. Anaongea aongea na nani?
 3. Wakiwa wapi au katika hali gani?
 4. wanaongea kuhusu jambo gani?

Ushauri muhimu kwa mtahiniwa

 1. Mtahiniwa sharti asome kitabu husika (Bembeaya Maisha) barabara na kukielewa.
 2. Mwongozo ni kurunzi ya kumulikia njia, kwa hivyo, mtahiniwa sharti aelewe aendako.
 3. Ni muhimu kusoma na kulielewa swali lililoulizwa. Ni vyema kujiuliza swali lifuatalo: Mtahini anataka habari gani kutokana na swali hili?
 4. Usitoke nje ya muktadha wa swali na kuandaa habari ambazo hazihusiani na swali uliloulizwa.
 5. Ikiwezekana, toa mifano kutoka kwenye tamthilia inayohusiana na jambo unalolifafanua ili kuweka jambo hilo wazi.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Utangulizi - Mwongozo wa Bembea ya Maisha.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?