Wahusika, Sifa zao na Umuhimu wao - Mwongozo wa Bembea ya Maisha

Share via Whatsapp

AINA ZA WAHUSIKA KATIKA FASIHI

 1. Wahusika wakuu
  • Huchukua nafasi kuu na kukuza kazi ya fasihi.
  • Matendo yote muhimu huwahusu.
  • Dhamira kuu ya mwandishi na falsafa/ msimamo wake hudhihirika kupitia kwa wahusika wakuu.
 2. Wahusika wadogo
  • Hawana nafasi kubwa.
  • Aghalabu husaidia hadhira kujua zaidi mhusika mkuu na dhamira yake.
 3. Wahusika wasaidizi
  • Hujenga wahusika wakuu na kukuza maudhui. Aghalabu huja na kutoweka baada ya muda mfupi.
  • Uainishaji Mwingine wa Wahusika
 4. Wahusika bapa/ Wahusika wa mraba mmoja
  • Huwa hawabadiliki katika hulka/ sifa zao.
  • Mhusika bapa anaweza kuwa na tabia nzuri au hasi kuanzia mwanzo hadi mwisho.
 5. Wahusika duara/ wahusika wa miraba minne
  • Huweza kubadilika kisaikolojia.
  • Huwa na sifa nyingi.
  • Wahusika bapa vielelezo
  • Huwa na tabia za kubadilika ila hujikita katika mtazamo wa mwandishi na hadhira yake.
  • Aghalabu huwa wahusika wakuu na hutumiwa na mwandishi kuendeleza suala fulani.
 6. Wahusika bapa sugu
  • Wana sifa ya kutobadilika ila huwakilisha walio na tabia potovu katika jamii. Mhusika bapa sugu anayeweza kuwa mhusika mkuu.
 7. Wahusika hasidi/ wapinzani
  • Hulka zao ni kinyume na mtazamo wa maadili ya jamii.
  • Humpinga mhusika nguli.
 8. Mhusika nguli
  • Ni mhusika anayekinzana na mhusika hasidi kwani anawasilisha maadili katika kazi ya fasihi. Aghalabu huwa mhusika mkuu au mmoja wa wahusika wakuu.
 9. Mhusika shinda
  • Hukuza wahusika wengine kwa kuwa hupelekwa mbele kwa usaidizi wa wahusika wengine.
  • Huwa chini ya kivuli cha mhusika mkuu.
  • Kupitia kvake ndipo hadhira inapata sifa bayana za wahusika wakuu.

WAHUSIKA WA BEMBEA YA MAISHA

Yona

Ni mume wa Sara na pia ni mmoja wa wahusika wakuu. Anatambulika kama mhusika mkuu kwa sababu anahusika na takriban masuala yote yanayojadiliwa katika tamthilia hii. Ni kama kwamba kila kitu katika tamthilia hii kinamhusu.

Sifa zake:

 1. Mwenye bidii: Alikuwa mwalimu hodari aliyesifika kazini na udumishaji wa nidhamu shuleni. Aliijali kazi yake na hakusita kufunga vitabu kwenye baiskeli yake ili avisahihishe anapofika nyumbani hata siku za wikendi.
 2. Mtamaduni: Licha ya kujaliwa na mabinti waliofanikiwa maishani na kuiletea fahari jamii yake, msukumo wa wanajamii wa kumhimiza apate mtoto wa kiume ulimtikisa. Alikosa furaha kwenyenndoa yake kwa sababu ya kuamini mila na desturi za jamii yake.
 3. Mwenye rabsha: Yona alipoingilia ulevi wa kupindukia alibadilika kwa njia hasi. Alianza kumpiga mkewe hata akazirai na kumwagiliwa maji. Alishindwa kutekeleza wajibu wake kazini na hatimaye akafutwa.
 4. Mwenye majuto: Mwishoni mwa tamthilia anajirudi na kujisuta kuhusu matatizo aliyoisababishia familia yake na hasa mke wake na kuamua kuacha kunywa pombe.
 5. Mlevi: Yona aliposhinikizwa na wanajamii kuoa na kutafuta mtoto wa kiume aliingilia ulevi wa kiwango cha juu. Yona alianza kulewa kisha kumchapa mkewe.
 6. Katili: Yona ni katili na hana utu kwa sababu hata baada ya kumkuta bibi yake akiwa katika hali mbaya ya ugonjwa, anamuuliza kwa nini hajamwandalia chakula. Hakusaidia bibi yake katika mapishi.
 7. Ni msomi: Amesoma hadi Chuo kikuu. Alikuwa mtu wa kwanza pale kijijini kufuzu kutoka chuoni.
 8. Mbabe dume/mwenye taasubi ya kiume 
  Yona hakuweza kumsaidia Sara katika kufanya kazi za nyumbani. Aidha alimdhulumu sana mke wake hadi akawa mgonjwa.
 9. Mwajibikaji
  Yona anawajibika katika kusomesha watoto wake
 10. mkatili
  Anamchapa na kumtesa mkewe hadi anaugua
 11. Ana msimamo dhabiti
  Anakataa kutafuta mtoto wa kiume nje ya ndoa. Pia anakataa kukubali ushawishi wa kuoa mke wa pili ili amzalie mtoto wa kiume.
 12. mtamaduni
  anaamini mtoto wa kwanza hana budi kumsaidia mzazi.
 13. Mkosa shukrani
  Yona anakosa kuona mchango wa mwanawe Neema hata baada ya kumpeleka Sara hospitalini.anaona kwamba anafaa kufanya zaidi ya yale ambayo tayari amefanya.
 14. Mwenye tuhuma
  Anaamini kwamba Sara anamsema na watoto wake
 15. Msomi/Mwerevu 
  Kwa mazungumzo yake na Neema, tunapata kujua kwamba yeye ndio bado ana rekodi pale chuoni alikosomea. Pia, alikuwa mwalimu kuonyesha kwamba alikuwa na ujuzi na maarifa.

 16. Mweye huruma
  Anapoelewa hali ya bibi yake na kuona jinsi alivyohusika kuisababisha, anajitolea kumwangalia bibi yake kwa kumsaidia kazi na kushughulika kwa mahitaji yake.  

Umuhimu wake

 • Yona anadhihirisha masaibu ya uraibu wa pombe unaoweza kuvuruga maisha ya mtu yeyote pasipo kujali nafasi yake katika jamii. Pia, anadhihirisha kwamba vita dhidi ya uraibu wa pombe vinaweza shindwa ikiwa mikakati bora itatumika. Anadhihirisha ukweli wa methali kuwa muwi huwa mwema.
 • Yona anatumika kuonyesha kwamba mtu anaweza kubadili mwendo wake licha ya yale anayoaminia. Kupitia kwa Yona tunaona kwamba hatufai kujifunga kwa itikadi moja zaidi kupita hata pale yanatufanya vipofu kwa yanayofanyika mbele yetu. Tunapaswa kuwa na akili wazi na kuweza kukubali mabadiliko yanayofanyika katika jamii.

Sara

Sara ni mke wa Yona. Yeye pia ni mhusika mkuu kwa sababu anahusika na karibu masuala yote ya tamthilia hii. Ndoa yake ilikuwa na changamoto nyingi zikiwemo mahitaji ya kiuchumi, fujo za mumewe ambaye alikuwa akishiriki ulevi na ugonjwa wa moyo uliomkaba.

Sifa zake:

 1. Mvumilivu: Sara alivumilia mateso ya mume wake ambaye alimlaumu kwa kutopata mtoto wa kiume. Mume wake alimtesa kutokana na kosa ambalo kwa hakika halikuwa lake.
 2. Mpatanishi: Sara ni mpatanishi kwa kuwa alimshauri bintiye amwelewe mume wake ambaye alitii utamaduni uliomfanya asimkubali mkwe wake alale nyumbani kwao. Pia, alimshauri bintiye amshukuru mumewe kwa kumruhusu kutumia hela zake kumtibu yeye aliyekuwa anaugua.
 3. Mwenye utu: Sara aliijali ndoa yake na kumpenda mumewe licha ya fujo zake. Alikataa kukaa mjini na binti yake ili kumwepushia mume wake fedheha ya kujifanyia kazi zilizohusishwa na wanawake kama vile kuchota maji kisimani.
 4. Mwenye hekima: Maneno anayozungumza yana wingi wa hekima na busara. Anamweleza Asna asicheze na akili zake ijapokuwa hakupata elimu sawasawa.
 5. Mlezi mwema: Anawalea wanawe kwa kuwapa mawaidha ya busara. Anawanasihi kuheshimu ndoa, utamaduni na baba yao.
 6. Mtamaduni: Neema anatilia maanani tamaduni za jamii yake. Kwanza tunamwona akisema kuwa fimbo hurithiwa na mtoto wa kiume. Tena tunamwona akimtetea bwana yake kuhusiana na suala la kazi za jikoni na kuteka maji kisimani.
 7. Mwenye uhusiano mwema: Sara alikuwa na uhusiano mwema na Dina. Anapougua, Dina anakuja kumsaidia kwa kuwa walikuwa na uhusiano mwema.
 8. Mwenye msimamo thabiti: Hata baada ya kusutwa na kukejeliwa na wanajamii hakuyumbishwa na maneno yao. Aliwapenda mabinti zake kwa dhati. Hata ingawa anachapwa kichapo cha mbwa na bwana yake, hakutoka nyumbani kwake, alisimama kidete na familia yake.
 9. Mvumilivu
  Sara anavumilia mateso ya kuchapwa na mumewe.
  Aidha anakabiliana na changamoto mengi yanayokabili ndoa yake lakini anayavumilia ili familia yake isisambaratike.
 10. Mwenye bidii
  Wakati alikuwa na afya njema hakuwahi kosa kufanya kazi zake.
  Aidha anasaidiana na mumewe kufanya kazi ili kuwasomesha watoto wao.
 11. Mwajibikaji
  anawajibika kazini ili kusomesha watoto wake
 12. Mwenye shukrani
  Tofauti na Yona ,Sara anaona mchango wa Neema katika kumgharamia kimatibabu anapougua.
 13. Rafiki wa dhati
  Ni rafiki wa karibu sana wa Dina
 14. Mtetezi 
  Anawatetea wahusika tofauti kwa hadithi. Mwanzo wa hadithi, anamteta Neema mbele ya Yona. Ananmtetea Yona mbele ya watoto wake na hata kumtetea Bunju pia dhidi ya yale Asna anayomnenea. 

Umuhimu wake

 • Sara anakuwa kielelezo chema cha wanawake walio katika ndoa zenye misukosuko. Anavumilia na kufaulu kuwalea na kuwasomesha wanawe ingawa mumewe anamdhulumu.
 • Anaendelea kumtii mumewe na kumshauri bintiye amnasihi baba yake dhidi ya ulevi kwa heshima.
 • Sara anatumika kwa daraja ya kuleta pamoja itikazi za kitamaduni na za kisasa. Kwa yale anayofanya na anayonena, hatuwezi same anaegemea pande moja sana kati ya pande ya maisha ya kitamaduni na ya kisasa. Anawatetea tabia za wale wanaoegemea pande zote. Kwa hali yake anaweza kumbadilisha Yona na kwa mawaidha anaonekana kutaka kubadilisha fikra za Asna na hata Neema kuhusu ndoa.

Neema

Neema ambaye ni binti wa Yona na Sara ni mhusika mjenzi. Neema ni mke wa Bunju. Wasifu wa Neema unadhihirika kutokana na kauli zake na za watu wengine pamoja na matendo yake. Neema anadhihirisha sifa kadhaa:

 1. Mwenye bidii: Anadhihirisha mwelekeo wa mtu mwenye bidii tangu alipokuwa shule. Licha ya kwamba wazazi wake walikuwa hawajiwezi, alisoma kwa bidii na kufaulu katika masomo yake hadi Chuo kikuu.
 2. Mwenye moyo wa kujitolea: Neema aliipenda familia yake hata alipoolewa. Tofauti na wasichana wengine ambao hujitenga baada ya kuolewa, Neema aliendelea kuwa nguzo imara katika familia yao. Alijitolea kumpeleka mama yake hospitali na kugharamia ada iliyohitajika. Pia aliajiri wafanyakazi wa kuwasaidia wazazi wake.
 3. Mwenye busara: Neema alidhihirisha busara katika ndoa yake kwa kumheshimu mumewe na kushirikiana naye katika malezi ya watoto wao tofauti na baadhi ya wake ambao huvuruga ndoa zao kwa mivutano mambo yanapokuwa magumu.
 4. Mwenye upole. Hakujibizana na Asna dada yake wakati alikuwa akizungumza vibaya kuhusu ndoa yake na Bunju.
 5. Amekengeuka: Neema amezinduka kwa kujua kwamba kuna tamaduni ambazo hazifai kutiliwa maanani katika kizazi cha leo. Anamwambia Bunju kwamba kumkataza mama yake kulala kwao ni utamaduni uliopitwa na wakati.
 6. Mwenye heshima: Neema anamheshimu baba yake hata baada ya kuwatesa walipokuwa wachanga. Neema anamheshimu bwana yake pia. Anasema amempa heshima yake tangu walipofunga ndoa.
 7. Msomi
  Anapata elimu bora inayomwezesha kupata kazi nzuri. Neema amehitimu chuoni na kupata digrii mbili.
 8. Mwajibikaji
  Anawajibika kazini na kuhakikisha kuwa mamake amepata matibabu mazuri anapougua.
 9. Mkarimu/mwenye utu/mwenye huruma
  Anajitolea kugharamia matibabu ya mamake na hata kulipa karo ya Kiwa.
 10. Mwenye akili pevu
  Anafaulu katika masomo yake na kisha baadaye anajaliwa kupata kazi.

Umuhimu wake

 • Neema anajitokeza kuwa kielelezo chema cha akina mama wenye uwezo wa kiuchumi na kuonyesha kwamba inawezekana kudumisha amani kwenye ndoa bila ya kusababisha ushindani usio na manufaa.
 • Anadhihirisha na kuthibitisha kuwa hata mtoto wa kike anaweza kuwasaidia wazazi wake wanapotatizika hata akiwa kwenye ndoa. Hivyo basi, anasawiriwa kama nguzo muhimu ya kuupinga utamaduni unaomdhalilisha mtoto wa kike na kumtukuza mtoto wa kiume.
 • Neema anatumiwa na mwandishi kuonyesha mtu ambaye pia anakubali mabadiliko maishani. Neema anaona kwamba hapaswi sana kuegemea kwa upande wa maisha ya kisasa na akasahau jadi zake. Anantumiwa kuonyesha kwamba mtu anapswa kukubai mafunzo kwa wale waliopitia pia. Anaonekana kukubaliana nay ale anayoambiwa na mama yake kuhusu ndoa. Pia, mwandishi anamtumia kuonyesha nafasi ya mwanamke wa kisasa kwa jamii.

Asna

Bintiye Yona wa pili. Ni mdogo wake Neema. Asna ni mhusika msaidizi. Anamsaidia msomaji kuelewa baadhi ya masuala yanayojadiliwa katika tamthilia.

Sifa zake:

 1. Mwenye misimamo ya kipekee: Asna anasema kwamba si lazima msichana aolewe mara tu aingiapo utu uzima. Anaonelea kuwa watu wanastahili kupewa nafasi ya kufanya maamuzi. Anasema taasisi ya ndoa ndiyo taasisi pekee inayotolewa vyeti kabla ya watu kupita mtihani. Anazungumzia hali ya watu wawili wanaotoa ahadi za maisha kabla ya kufahamu ikiwa jambo wanalojiingiza litafanikiwa au la.
 2. Mwenye heshima: Hata ingawa msimamo wake kuhusu ndoa ni tofauti na ule wa dadake, bado anamheshimu kama mkubwa wake na kuiheshimu ndoa ya Neema ingawa anajua ina matatizo. Pia, anawaheshimu na kuwapenda wazazi wake.
 3. Amekengeuka: Asna anaelewa fika kwamba kuolewa ni kwa hiari ya mtu binafsi ila si kushinikizwa au kulazimishwa na utamaduni.
 4. Msomi: Asna amesoma na kuhitimu hadi Chuo kikuu.
 5. Mwenye chuki: Asna anachukia tabia za Bunju za kujifanya kuwa hana pesa ilhali anazo. Anachukia ubahili.
 6. Mvivu 
  Kwa maelezo yake, anaishi maisha ya tomboy ambapo hashughuliki sana.

 7. Mwoga
  ameogopa ndoa kabisa kwa kuangalia jinsi ndoa ya dada yake na mama yake zilivyokuwa.

 8. Mdaku 
  Anajaribu kuwadakua watoto wa Dina. Pia, anaonekana kushinda kumeongelea Bunju pale asipo.

 9. Asiye na huruma
  Kwa mazungumzo yake yote kuhusu Bunju, haelewi hali yake na jinsi amejitolea kufanya mengi kwa familia yao. Anashinda kwa maoni kwamba Bunju hajajitolea ya kutosha.

Umuhimu wake

 • Asna anawakilisha vijana ambao hawana azimio la kuolewa. Wao ni sehemu ya jamii na wanastahili kukubalika kama wale wenzao wenye imani kwenye taasisi ya ndoa. Hata hivyo, anavyoeleza Sara, na anavyodhihirisha Neema, vijana hawapaswi kuwa na msimamo mkali kuhusu taasisi ya ndoa kwa sababu changamoto nyingi zilizo katika taasisi ya ndoa zinavumilika kama ilivyo katika taasisi nyingine.
 • Asna anatumiwa kutoa taswira ya watu wanaojikwamisha kwa mambo ya kisasa na kuacha jadi zao nyuma. Asna ndio picha nzuri ya muacha mila mtumwa kwa sababu anaonekana kukataana na yale anayoambiwa kuhusu ndoa. Pia anauona umaskini wa mjini ukiwa afdhal kuliko wa kijijini ingawa uko mbaya zaidi.

Bunju

Bunju ni mumewe Neema.

Sifa zake:

 1. Mpenda haki: Bunju anamkubalia mke wake kutumia pesa zake kuishughulikia jamii yake ambayo ina uhitaji mkubwa baada ya Yona kufutwa kazi. Pia, mama mkwe anahitaji kutunzwa kwa hali na mali kutokana na hali yake ya kuugua kwa muda mrefu.
 2. Mwenye mapenzi: Bunju anampenda mkewe na wanawe na kutekeleza wajibu wake wa malezi kwa bidii.
 3. Mwenye bidii: Anajitahidi kazini na mara nyingi hata muda wa kustarehe hana. Bidii zake zinamwezesha hata kumnunulia mkewe gari.
 4. Ni mgumu wa pesa: Anajitokeza kama mwenye msimamo thabiti kuhusu matumizi ya pesa na hivyo kusawiriwa kama mtu mchoyo au bahili.
 5. Mtamaduni: Bunju anashikilia mila na desturi za jamii yake. Anapoziishi kwa kumkataza mama mkwe kulala nyumbani kwao, anaonekana kama mtu mchoyo na asiyejali maslahi ya mama mkwe wake. Mila na desturi zinamtawala na kumfanya asitangamane na mama mkwe hata akiwa amelazwa hospitalini. Hili Sio jambo jema.
 6. Msomi
  Anasoma kisha kupata kazi baadaye na kumnunulia mkewe gari.
 7. Mwajibikaji
  Anapofanya kazi anahakikisha kwamba ametekeleza majukumu yote nyumbani kwake hivi kwamba pesa zake mkewe amemwachia atumie anavyotaka. 
 8. Mwenye mapenzi ya dhati
  Anamnunulia mkewe gari,hii ni njia mojawapo ya kuonyesha mapenzi
 9. Mkali/ mtu imara -  Anakwama kwa msimamo wake. Kwa hadithi hii, Bunu haonekani kuwa mtu wa badilisha msimamo ovyo ovyo. Licha ya kuwamsaidizi, kuna yale ambayo anaonekana kujiwekea asiweze kupita hapo. Kwa mfano; anamwambia kwa mara Neema kwamba amemwachia mshahara wake bila kumwitisha ili afaye jinsi atakavyo. Hata hivyo, mambo yanapokaribia kupita zile tamaduni alizolelewa nazo, anakataa kama vile kumwacha Sara alale kwao

Umuhimu wake

 • Bunju anadhihirisha umuhimu wa kushirikiana katika ndoa. Anatoa kielelezo chema cha mume anayemjali mke wake. Ana moyo wa kusaidia.
 • Alimsaidia Neema wakati alipopata ajali na kumlipia gharama zote za matibabu.
  Anamsaidia Neema kwa kumruhusu atumie mshahara wake kusaidia wazazi wake. Kwa hiyo, anampatia Neema fursa ya kusaidia jamii yake bila pingamizi. Pia, Bunju anasimamia wanarika ambao bado wanathamini mila na desturi za kwao kwani mwacha mila ni mtumwa.

Dina

Ni mama wa umri wa makamu na jirani wa Sara na Yona.

Sifa zake:

 1. Mwenye moyo wa huruma: Sara anapougua, Dina anamsaidia kazi za nyumbani na kumpa moyo kuhusu ugonjwa alionao. Anamsifu Sara kwa bidii aliyonayo iliyomfanya kusomesha watoto wake hadi wakafikia Chuo kikuu licha ya masimango ya wanajamii na mateso ya mumewe.
 2. Mwenye ujirani mwema: Anapoitwa na Sara amsaidie kupikia bwana yake, anafika nyumbani mwa Sara kumsaidia katika shughuli hiyo.
 3. Mwenye roho safi: Hana kinyongo chochote kwa watoto au familia ya Sara. Anafurahia kufanikiwa kwa watoto wa Sara.
 4. Mwenye mapenzi ya dhati: Anamsaidia rakifi yake Sara kwa dhati.
 5. Rafiki wa dhati
  Ni rafiki wa karibu sana wa Sara.
  Anamsaidia kufanya kazi za nyumba anapougua.
 6. Mcha Mungu
  Mambo yake mengi anarejelea Mungu,anasema kwamba Mungu ni mkuu.
 7. Mlezi mwema
  Anashangaa kwa nini Kiwa hali vizuri, anataka awe na misuli.
 8. Mwenye busara
  Anampa Kiwa kauli ya busara kuhusu maisha.
 9. Mshauri mwema
  Anamshauri Sara kutofikiri sana mambo ya watu wengine bali ashukuru kwamba hata akiwa mgonjwa anapata msaada kutoka kwa mwanawe.

Umuhimu wake

 • Dina anadhihirisha usemi kwamba "Kidole kimoja hakiui chawa." Hii ni kutokana na kujitolea kwake kumsaidia Sara kazi za nyumbani anapokuwa anaugua. Ni kielelezo cha urafiki wa dhati na ujirani mwema. Ifahamike kwamba Sara asingeishi vyema na majirani, asingepata mtu wa kumsaidia.

Kiwa

Kijana wa kiume, mtoto wa Dina. Kama majirani wengine anashangazwa na bidii za watoto wa Sara na Yona. Kiwa ni mwanaume wa miaka 27. 

Sifa zake:

 1. Mwenye heshima: Anamheshimu mama yake na kushirikiana naye licha ya pato dogo analopata. Kupitia pato lake dogo, ameweza kubadilisha hali yao ya maisha pale nyumbani na kuinua maisha ya Dina.
 2. Mwenye roho safi: Anashangazwa na ufanisi wa majirani zake lakini hawaonei gere.
 3. Mdadisi: Kiwa anamuuliza mama yake maswali mengi kuhusu familia ya Yona.
 4. Ni kijana wa sasa
  Amezinduka na anaelewa kuwa dunia ya sasa haithamini kimo au kutetemeka kwa misuli bali inathamini akili pevu.
 5. Mwajibikaji
  Anawajibika kurudi nyumbani kumwona mamake.

Umuhimu wake

 • Umuhimu wa Kiwa unatokana na mambo mawili; ni kijana anayewajibika na kubadilisha maisha ya mama yake licha ya pato lake dogo. Kupitia kauli zake, anadhihirisha kuwa ufanisi maishani hautegemei jinsia bali bidii ya mtu binafsi.

Luka

Mwanakijiji ambaye ni jirani na rafikiye Yona. Ni mzee wa miaka 67

Sifa zake:

 1. Ana busara: Anakiri kwamba siku hizi watoto wa kike wameacha kutegemea waume zao na kuanza kuwajibikia familia zao kiuchumi.
 2. Mshauri mwema: Anamshauri Beni kuhusiana na masuala ya kitamaduni kwamba zamani tamaduni zilikuwa lakini sasa tamaduni zingine zimepitwa na wakati.
 3. Mwenye matumaini – Ingawa wanasema kwamba mila zao zinabadilika. Yeye anaona uzuri wake n ahata kuisifia. Ana sifu madaliko ya kijamii yanayohusu nafasi na majukumu ya wanawake.

Umuhimu wake

Anadhihirisha kwamba hata vijijini mabadiliko ya kimawazo kuhusu mtoto wa kike yameanza kukita mizizi. Anamchora Neema kama "simba wa kike" (uk. 67). Luka anatumiwa kutoa taswira ya wale wanaokubaliana na mabadiliko yanyofanyika katika jamii. Anaonekana kuunga mkono mabadiliko haya ingawa hayaendi sawa na mila na desturi zao.

Beni

Mwanakijiji ambaye ni jirani na rafikiye Yona. Beni ni rafiki yake Yona. Ni mzee wa miaka 63

Sifa zake:

 1. Mtamaduni: Anashikilia kuwa mtoto wa kiume ana manufaa kuliko wa kike. Anadai Neema hajali maslahi ya baba yake huku akijua kuwa Neema anamshugulikia mama yake ambaye ni mgonjwa. Hajakengeuka: Beni hajazinduka kwa kuwa hajui tofauti kati ya injinia na fundi wa mitambo.
 2. Mchochezi: Anadai kuwa Yona anafedheheshwa kwa kuachiwa kazi za kujipikia. Ni kama anaelekezwa na mkewe na wanawe. Ukweli ni kwamba mkewe alisafiri mjini kwa matibabu na kukaa kwa wanawe kwa siku chache tu. Beni anatawaliwa na taasubi ya kiume na si jirani mwema kwa Yona kwa kuwa anachangia kumchanganya akili.
 3. Mwenye kukata tamaa – Anaona mabadiliko yanayofanyika ya kijamii yatasababisha watu kusahau mila zao.

Umuhimu wake

 • Ni hasidi katika jamii. Watu wa aina hii huwachochea wenzao na mwisho kuwatenganisha na wake na familia zao. Yona anapuuza uchochezi wa Beni na kuonyesha kuwa sasa ameanza kupatwa na mwamko mpya.
 • Beni anatumiwa kutoa taswira ya wale waliokwamia tamaduni na mila za kale. Kulingana na mazungumzo yake, haoni yoyote mazuri yanayotokana na mabadiliko ya kijamii yanayofanyika.

Bela

Ni mfanyakazi wa nyumbani wa Neema. Ni mwanamke wa miaka 57. 

Sifa zake:

 1. Mwenye busara: Anazungumza na mwajiri wake, Neema, kuhusu matatizo anayoyapitia kwenye ndoa yake kwa busara na kumsihi kuvumilia. Anampa Neema mashauri kuhusu maisha. Anamwelewa Neema kwa hali yake ya kazi na kwa nini hawezi kumlea Lemi kwa njia ya karibu kama vile wazazi wapasavyo. 
 2. Mtu wa kutegemewa: Ni mfanyakazi wa kutegemewa. Ana uhusiano mwema na mwajiri wake na anaelewa kazi yake barabara. Anamkumbusha Neema kuhusu kazi za shule za Lemi kwa maana kuwa, anaelewa jukumu lake la kuwalea watoto wa Neema, anayeonekana kuwa mtu wa kazi nyingi.
 3. Mlezi mwema. Bela analea watoto wa Neema vizuri na kwa bidii.
 4. Mwenye bidii: Bela anafanya kazi ya kuwalea watoto wa Neema kwa bidii. Pia anasema kuwa mara nyingi yeye hakupatana na watoto wake kwa sababu ya shughuli ya kazi. Maneno hayo yanaonyesha alikuwa mwenye bidii hata kabla ya kuanza kufanya kazi kwa Neema.

Umuhimu wake
Anawakilisha wafanyakazi wa kiwango cha chini wanaowajibika, kuheshimu na kuthamini kazi zao.

Lemi

Lemi ni mtoto wa Bunju na Neema na ni mvulana wa miaka 10.

Sifa zake:

 1. Mtiifu: Lemi anawatii wazazi wake na pia mlezi wake Bela. Anatii amri ya mama yake anapoambiwa aende akafue hanchifu.
 2. Mwenye shukrani: Lemi anamshukuru mama yake Neema wakati alikumbushwa kufua hanchifu yake (uk. 48).
 3. Mdadisi: Lemi anauliza mama yake maswali kuhusu mama yake na bibi yake. Lemi anauliza mama yake (uk. 30) kwa nini hana raha na maswali mengine mengi. Pia anataka kujua ni kwa nini bibi yake hajakuja kumsalimu.
 4. Mwenye vipawa: Lemi ana kipawa cha kuimba na kucheza nyimbo kwa miondoko na minenguo (uk. 22).
 5. Mchangamfu - Kwa mazungumzo yake, anaonekana kuwa na maswali mengi kuhusu yale yanayoendelea.

Umuhimu wake

 • Lemi anawakilisha watoto wa baadhi ya wazazi ambao hawapati wakati mwingi wa kuingiliana na wazazi wao ambao mara mwingi wako kazini. Anawakilisha watoto ambao hulelewa na yaya.

Wahusika wadogo

Salome na Mina: Wahusika wadogo ambao wanatajwa tu. Hawashiriki moja kwa moja katika masuala ya tamthilia hii. Salome ni mwanawe Yona na Mina ni bintiye Bunju na Neema.

Salome

Ni Mhusika mtajwa. Yeye pia ni mwanawe kina Yona. Ana miaka 28.

Mina

Ni mhusika mtajwa. Ni msichana wa miaka 12 na mwanawe Bunju na Neema.

Kalasinga

Ni mhusika mtajwa , babake Yona.

Umuhimu wao
Wanakamilisha idadi ya watoto wa Yona na Bunju mtawalia. Idadi hii ni dhihirisho la usasa ambapo wazazi hawapati watoto wengi kutokana na hali ibuka za kiuchumi na za kijamii. Pia, wanaendeleza malezi ya kisasa ambapo watoto hawaonani na wazazi wao kwa kuwa wanahudhuria masomo ya bweni au nje ya nchi.

Ushauri muhimu kwa mtahiniwa

 1. Mtahiniwa sharti asome kitabu husika (Bembeaya Maisha) barabara na kukielewa.
 2. Mwongozo ni kurunzi ya kumulikia njia, kwa hivyo, mtahiniwa sharti aelewe aendako.
 3. Ni muhimu kusoma na kulielewa swali lililoulizwa. Ni vyema kujiuliza swali lifuatalo: Mtahini anataka habari gani kutokana na swali hili?
 4. Usitoke nje ya muktadha wa swali na kuandaa habari ambazo hazihusiani na swali uliloulizwa.
 5. Ikiwezekana, toa mifano kutoka kwenye tamthilia inayohusiana na jambo unalolifafanua ili kuweka jambo hilo wazi.

 

Join our whatsapp group for latest updates

Download Wahusika, Sifa zao na Umuhimu wao - Mwongozo wa Bembea ya Maisha.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?