Fani - Mbinu za Lugha, Mbinu za kishairi na Mbinu za Kimuundo - Mwongozo wa Bembea ya Maisha

Share via Whatsapp

Menyu ya Urambazaji:

MBINU ZA LUGHA, MBINU ZA KISHAIRI NA MBINU ZA KIMUUNDO

Mifano ya mbinu za uandishi ni kama (Mbinu za Kimuundo)

  1. Kinaya  (irony) - Kinaya ni hali ya mambo katika riwaya/hadithi kuwa kinyume na matarajio.
  2. Taharuki (suspense) - ni mbinu ya kusimulia au kuandika riwaya/hadithi kwa kutumia maneno na kujenga hali inayozua hamu kwa hadhira; hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye; hamu ya kutaka kuendelea kusoma/kusikiliza.
  3. Sadfa (Coincidence) - Sadfa ni kugongana kwa vitendo viwili vinavyohusiana kana kwamba vilikuwa vimepangwa japo havikuwa vimepangiwa. 
  4. Mbinu Rejeshi/Kisengere Nyuma (Flashback) - mwaandishi husimulia hubadilisha wakati wa masimulizi na kusimulia namna kisa kilivyokuwa wakti fulani uliopita.\
  5. Kisengere Mbele/Utabiri (Flash Forward) - Mwandishi anapobadilisha wakti na kusimulia mambo yatakavyokuwa siku za usoni,kabla ya kuwa, huwa anatumia mbinu ya utabiri.
  6. Upeo wa Juu (Climax) na Upeo wa Chini (anticlimax)
  7. Uzungumzi nafsiya(monologue)- Ni aina ya monolojia itolewayo na mhusika mmoja akiwa jukwaani pekee Mbinu hii hutumiwa kuwasilisha maoni, hisia na fikra za mhusika kuhusu jambo fulani
    Usemaji kando - Hii ni mbinu ambayo mhusika mmoja anasema maneno kwa hadhira au mhusika mwingine huku wenzake kwenye jukwaa wakijifanya kutosikia anachosema mhusika huyo.
  8. Wimbo
  9. Barua

MATUMIZI YA LUGHA

Mwandishi ametumia mbinu za Kiswahili za uandishi ili kuweza kuirembesha hadithi na pia kumsadia msomaji kuwa na maelezo zaidi nay ale yanayofanyika. Mfao wa mbinu/ tanakali hizi za fasihi ni kama:

  1. Tashbihi (similies)-Ulinganishi kwa kutumia viunganishi kama, mithili, mfano na sawa.
  2. Sitiari/ Istiara(metaphor)-Ulinganishi usio wa moja kwa moja. Mfano;huyu ni fisi.
  3. Tashhisi/Uhaishaji(personification) -Kukipa kitu sifa ya uhai. Mfano;maji yalicheka
  4. Chuku/udamisi(hyperbole) -Kutia chumvi au kufanya kitu kionekane kikubwa sana au kidogo sana. Mfano;kijana alitoa sauti kama kipaza sauti.
  5. Tanakali za sauti (onamotopoeia/ ) - Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika.
  6. Takriri (repetition) - Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Isitoshe, takriri inaweza kujitokeza kwa kurudia rudio wazo fulani katika kazi ya sanaa. 
  7. Tanakuzi (paradox)- Tanakuzi ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokanushana. Pia huitwa takriri tanakuzi
  8. Taswira (imagery)-  Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
  9. Majazi (figurative language/ symbolic meaning) - ni mbinu ya mhusika kuwa na jina lake rasmi (jina la kuzaliwa) linaloambatana na tabia/mienendo/sifa zake.
  10. Lakabu (nickname) - ni mbinu ya mhusika kupewa/kubadikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa zake au kulingana na uhusiano wao.
  11. Misemo na nahau (idioms)- Nahau na misemo hutumika kupitisha ujumbe wa mwandishi kwa kutumia maneno ambayo hayamaanishi katika hali halisia. Misemo hutumika sana katika fasihi na katika mazungumzo ya kawaida ili kufanya lugha iwe ya kupendeza. 
  12. Maswali ya balagha(rhetorical questions) - Mhusika au msimulizi huuliza maswali yasiyohitaji majibu.
  13. Uzungumzi nafsiya (self dialogue)- Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote.
  14. Utohozi (loan word) - Ni kuswahilisha maneno ya lugha nyingine, yatamkike kama ya Kiswahili.
  15. Kuchanganya ndimi(mixing tongues) - Kuingiza maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili.
  16. kuhamisha ndimi - Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu
  17. Kejeli (sarcasm)- Ni kutumia lugha inayoonyesha kudharau au kufanya kitu kiwe kidogo sana kuliko kilivyo
  18. Jazanda (symbolism)- ni kunga ya utunzi ambapo lugha inatumia kusawiri picha fulani kutokana na maelezo yanayotumia maneno teule au tamathali za usemi.

Mwandishi wa tamthilia ya Bembeaya Maisha ametumia mbinu mbalimbali za lugha na za kimuundo ili kuwasilisha dhamira na maudhui yake.

Mbinu za lugha

  • Lugha ya kitamthilia ni lugha maalumu. Hii ni kwa sababu inatumika katika utanzu wa kijukwaa. Jukwaa la uigizaji humpatia mwandishi fursa ya kutumia lugha ambayo sharti iambatane na uigizaji. Vilevile, kuna lugha ya uigizaji ambayo inaweza kuhusisha uteuzi wa maneno wenye urari kama katika ushairi.
  • Katika tamthilia ya Bembeaya Maisha, mwandishi ametumia lugha kwa njia mwafaka ili kutekeleza malengo yake. Tamathali za usemi zimetumika kwa wingi.

Taswira

  • Twasira ni dhana ambayo hutumia maneno ili kumchorea msomaji picha fulani katika fikira au akili yake. Pia huitwa jazanda.
  • Inawezekana mwandishi kutumia taswira za kimaelezo au zile zilengazo hisi za mwanadamu kama vile joto, mnuso, mguso na usikivu.

Mifano

  • Taswira inajitokeza kwenye maneno yaliyo kwenye mabano au yaliyoandikwa katika hati ya kiitaliki. Maelezo hayo yanatuchorea picha akilini mwetu.
    Yanatufahamisha na kutujulisha dhahiri wakati, mahali na matendo yanapofanyikia.
  • Kwa mfano, katika onyesho la kwanza sehemu ya kwanza maneno yaliyo kwenye mabano yanatuonyesha kwamba onyesho linafanyika wakati wa alasiri, mahali ni nyumbani kwa Sara, tunaona Sara akichukua vidonge vya dawa na kuvimeza
  • kabla ya kuketi kwenye kochi jipya. Tunaona namna ukuta wa nyumba ya Sara umepambwa na picha za familia. Takriban maneno yote yaliyo kat:ika hati ya kiitaliki yanatuchorea picha fulani akilini, hivyo yanajenga taswira.
  • Taswira katika tamthilia hii pia imejidhihirisha kupitia kwa maneno yanayosemwa na wahusika. Kupitia usemaji wa wahusika, msomaji anapata taswira fulani kuhusiana na namna mhusika anavyozungumza. Kutokana na maneno yao, msomaji hupata taswira sikivu ambayo inamdhihirishia toni au kiimbo anachotumia mhusika lengwa.
  • Katika Onyesho I Sehemu I; mazungumzo kati ya Sara na Yona yanatuonyesha taswira sikivu ya toni wanayotumia, Yona anatumia toni ya juu naye Sara anatumia toni ya chini. Maneno Yao yanatuchorea picha akilini kuhusu wanavyozungumza.
    Taswira ya aina hii ndio inayowezesha tamthilia kuigizwa jukwaani kwa kutumia toni au kiimbo kinachofaa.
  • Anwani ya tamthilia hii inatuchorea picha akilini. Neno bembea linarejelea kifaa ambacho mara nyingi hutumika na watoto kuchezea. Kifaa hiki huenda juu na chini na kurudi nyuma na mbele. Hivyo basi,
  • BEMBEA YA MAISHA ni taswira fikirivu, msomaji anaposoma anwani hii anapata mawazo mengi kuhusu maisha ambayo anayalinganisha na bembea. Msomaji anatarajia kupatana na maisha ambayo yana panda shuka au ambayo yanayumbisha anaposoma tamthilia nzima. Hali hii inadhihirika wazi kwa kuwa anwani Bembea ya Maisha imejidhihirisha katika maelezo na matendo ya wahusika katika tamthilia nzima.

Mifano ya taswira inayojitokeza katika dondoo

  1. ...Miaka inaposonga mnatuona...kama..kama vile tambara bovu. Tambara lisilomjia hata mpiga deki akilini (uk. 4). Maneno haya yanatumiwa na Yona yakielekezewa mkewe. Maneno haya yanaonyesha namna wanaume hawana umuhimu wowote kwa wanawake katika jamii ya tamthilia hii.
  2. ...Wewe unaona rangi ya mwisho wa kinachoelea. Kabla kielee kimepigwa shoka, kimeonja misumeno aina aina, kimetambaliwa na randa, kimestahimili makali ya patasi na kupapaswa na mikwaruzo ya msasa (uk. 10). Haya ni maneno ya Dina akimweleza Kiwa kuhusu maisha ya mabinti wa Yona na Sara. Maneno haya yanatujengea taswira ya maono. Msomaji anaposoma maelezo haya anaona picha ya watu walioishi kuteseka, kunyanyaswa na kwa jumla watu walioishi maisha magumu sana kisha kufanikiwa baadaye.
  3. ...Nilikuwa kimbaumbau mwiko wa pilau. Upepo mchache tu ungeniyumbisha kamajani kavu wakati wa kipupwe (uk. 10). Haya ni maneno ya Sara akimweleza Dina. Maneno haya yanatuonyesha taswira ya maono. Tunaona namna mwili wa Sara ulikuwa umedhoofika na afya yake kuzorota kwa kukondeana kama ngonda hadi kufikia kiwango cha kupeperushwa na upepo.
  4. ...Mkulima hodari libasi yake huwa imechakaa na kuchoka lakini moyoni anabaki kama theluji kwa kutosheka na tija ya sulubu zake. Huwezi kumlinganisha na mkulima wa nguo safi zilizopigwa pasi zikanyooka (uk. 18). Haya ni maneno ya Sara ya kumpongeza Neema kwa juhudi zake za kujiendeleza kimaisha. Analinganisha hali hii na ya mkulima ambaye amelazimika kufanya kazi ngumu shambani na kupata vuno zuri. Ili afanikiwe sharti nguo zake zichafuliwe na udongo na mchanga. Kama angaliogopa kuchafuka basi mkulima asingelifanikiwa.
  5. ...Mwanangu usitake kuhoji alacho kuku. Utachafukiwa roho umchukie kuku bure. Wala usitake kujua asali ameitengenezea nini nyuki. Hutaila. Maadamyameshakujayapokee (uk. 20). Kupitia maneno haya, Sara anampatia Neema moyo ili ajikaze na kumvumilia mumewe kwa kupuuza udhaifu wake kwani asipofanya hayo ndoa yake na Bunju inaweza kuingia doa.
  6. ... Bembea inapolika na kukatika haiwi mwisho wa mchezo. Huungwa na mchezo kuanza tena (uk. 21). Sara analinganisha mchezo wa watoto wa kubembea na maingiliano ya ndoa. Mchezo wa bembea humalizika kwa sababu bembea imekatika na uhusiano wa ndoa hutatizika wanandoa wanapokosa kuvumiliana.
  7. Ni kama mti mchanga kwenye chaka la miti mikubwa mirefu. Unaishi kutapia hewa na jua. Unajitahidi kutoa Shingo kila wakati kuung'ang'ania mwanga huo. (uk. 26) Haya ni maneno ya Neema akimweleza Bela namna watu wa tabaka la chini hulazimika kufanya bidii ili kujinyanyua kutokana na mnaso wa umaskini. Hali hii inalinganishwa na jinsi miti michanga inavyong'an<ana kuufikia mwanga porini.

Misemo

Misemo ni aina ya semi fupi zenye ukweli ambazo hutumiwa kuelezea mambo yenye kuafiki ukweli huo. Mwandishi ametumia mifano kadhaa ya misemo katika tamthilia hii.

Mifano

  • Kutupigajeki (uk. 3) - Kumpa mtu msaada au kusaidia.
  • Amewafaa wanuna kwa hali na mali (uk 2) - Kuwa msaidizi wa hali ya juu kwa mtu.
  • Bahati ya mtende (uk 3) – Kuwa na bahati kubwa
  • Kuadimika kama wali wa daku (uk. 5) - Ni kutoonekana kwa muda mrefu sana.
  • Kufanya nongwa (uk. 12) - Kusongwa na moyo kutokana na jambo linaloudhi.
  • Kila limfikalo mwanadamu ni mpango wa Manani (uk. 12) - Imani kuhusu majaaliwa ya kwamba tunayokutana nayo ni mpango wa Mwenyezi Mungu.
  • Kupiga makasia chombo kinapopungukiwa na upepo (uk. 14) Kutoa msaada wakati hali ngumu inapomkabili mwenzako.
  • Kichwa kimeudara mto (uk. 1) - Kichwa kimelala juu ya mto.
  • Tiwa vinywani (uk. 6) - Semwa sana na watu.
  • Bongo za sumaku (uk. 7) - Bongo zinazoweza kushika mambo kwa urahisi.
  • Sisimkwa na malaika (uk. 12) - Kuwa na wasiwasi.
  • Nisiyatie machungu moyoni (uk. 12) - Nisihuzunike, nisiwe na wasiwasi.
  • Watoto ni baraka (uk. 18) - Watoto ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu.
  • Fungulia milangoya heri (uk. 18) - Achilia baraka.
  • Ingiajakamoyo (uk. 44) - Patwa na wasiwasi.
  • Ponza roho (uk. 44) - Jiingize katika matatizo.
  • Ana bidiiya mchwa (uk. 45) - Bidii kubwa.
  • Kutokuwa na kabaya ulimi (uk. 48) Kutojizuia, kusema sana na kila wakati.
  • Kuwa chiniya amri (uk. 49) - Kuwa mtiifu.
  • Ujana ni moshi (uk. 52) - Ujana ni sawa na moshi ambao ukienda haurudi.
  • Ndoa ni mtihani mkubwa (uk. 53) - Ndoa ina matatizo mengi; inahitaji hekima.

Nahau

Nahau ni aina ya semi ambazo huundwa kwa fungu la maneno ya kawaida yanayozua maana tofauti na ile ya maneno hayo. Nahau ni maneno ya busara ambayo hutumiwa kueleza kitu kutokana na mifano katika maisha. Ni bayana kwamba nahau hutokana na mazingira ya watumiaji wa lugha husika. Nahau hutumiwa kupamba lugha na kupunza ukali wa maneno. Nahau hutumika kupitisha ujumbe wa mwandishi kwa kutumia maneno ambayo hayamaanishi katika hali halisia. Misemo hutumika sana katika fasihi na katika mazungumzo ya kawaida ili kufanya lugha iwe ya kupendeza

Mifano

  1. Kichwa kimeudara mto (uk 1) – Amekuwa akilala/ amekuwa usingizini
  2. Kutupa jogoo na mti wake (uk. 3) - Inamaanisha kuachana na jambo kabisa. Sara anarejelea jinsi ambavyo baadhi ya wasichana wanavyowasahau ndugu zao wanapoolewa.
  3. Bahatiya mtende (uk. 3) - Ni kubahatika sana kwa njia isiyotarajiwa.
  4. Kutupiga jeki (uk 3) – Kusaidia/ kutoa msaada
  5. Kikapu cha mama kimejaa ndago (uk. 6) - Usemi unaoashiria mtu aliyefanikiwa. Usemi huu unamrejelea Sara ambaye alikuwa na uhitaji siku za nyuma lakini sasa bintize wanamfaa kwa hali na mali.
  6. Maji kuzidi unga (uk. 11) - Hali kuwa tatizi au ngumu kukabiliana nayo.
  7. Utakuwa unajivulia nguo (uk. 14) - Utakuwa unajiaibisha.
  8. Nyotayajaha (uk. 19) - Bahati.
  9. Tumeyaacha maji ya mbizi tukaingia maji ya mbuzi (uk. 20) Tumetoka kwenye hali ngumu na sasa tumeingia kwenye hali nafuu.
  10. Taaridhi isiyo kifani (uk. 24) - Udadisi; hali ya kuuliza uliza au kuchunguza mambo.
  11. Bora punda afe mzigo ufike (uk. 27) - Kutomjali mfanyakazi bora tu kazi ifanyike. Hata anayeifanya akidhurika Sio hoja.
  12. Fanya ajizi (uk. 1) - Legea, kuwa mvivu, zembea. Zika katika giza la kina cha moyo (uk. 7) - Nyamazia jambo au fanya kuwa siri.
  13. Angukiwa na nyotayajaha (uk. 19) - Bahatika.
  14. Piga kalamu (uk. 19) - Achisha kazi.
  15. Walimwengu sasa wanavaa sare moja (uk. 24) - Watu wamebadilika; wameachana na ya kitambo na wanafuata ya sasa. Akili za madongo kuinama (uk. 23) - Akili hafifu zisizo imara.
  16. Mchele umeingia mchanga (uk. 26) - Mambo yameharibika.
  17. Poa moto (uk. 26) - Tuliza hasira; kuwa mpole.
  18. Bunju ni mkono wa birika (uk. 33) - Ni mchoyo.
  19. Chombo kingezama (uk. 62) - Mambo yangeharibika.
  20. Kujipiga kifua (uk. 63) - Kujigamba.
  21. Kata shauri (uk. 70) - Amua.
  22. Sikuwa na picha nzima (uk. 74) - Sikuwa na ufahamu wa kutosha.

Mbinu ya majazi

Majazi ni mbinu ambayo mwandishi hutumia kuwapa wahusika majina kulingana na tabia zao. Mbinu hii inadhihirika kupitia kwa wahusika kama vile:

  • Bunju - jina Bunju ni la kimajazi. Bunju alipewa jina hili lililolinganishwa na mnyama mwenye sumu lakini sumu hiyo huondoka baada ya kusafishwa. Bunju ana tabia mbaya inayolinganishwa na sumu ya mnyama huyo. Kwa mfano, alionekana kuwa na ukali kwa mambo ya kusaidia Neema katika matibabu ya mama mkwe (Sara). Baada ya kushawishiwa kwa muda na Neema, ukali huo unamwondoka na kumweleza Neema kwamba atamsaidia kulipa gharama ya matibabu ya mama yake (uk. 40). Anamwambia atampiga jeki.
  • Neema - Neema ni jina la kimajazi. Neno neema lina maana ya kufanikiwa au kustawi. Mwandishi amempa Neema jina hili kutokana na sifa za kustawi na kufanikiwa maishani. Neema amefanikiwa kusoma hadi Chuo kikuu na kustawi kwa digrii mbili, amefanikiwa kupata kazi nzuri, amefanikiwa kupata mume anayemjali na kushughulikia maisha ya familia yake na pia amefanikiwa kuwalipia karo dada zake hadi Chuo kikuu. Kwa kifupi, mhusika Neema amefanikiwa kwa kiasi kikubwa maishani.
  • Sara - mhusika Sara amepewa jina hili kutokana na namna alivyosemwa na wanajamii. Neno sara lina maana ya kutapakazwa au kuenezwa kila mahali. Jina la Sara lilienezwa na wanajamii kila mahali. Alisemwa sana na kutukanwa kwa kuwa hakuwa na watoto wa kiume (uk. 13). Alisemwa kotekote ikiwemo makanisani na magengeni. Kwa sababu hii mwandishi akampa mhusika huyo jina, Sara.

Lakabu

  • Lakabu ni mbinu ambayo mwandishi hutumia kuwapa wahusika majina mbali na majina yao halisi. Lakabu huwa ni jina la kupanga au jina la kutania. Mhusika ametumia mbinu hii kuwarejelea wahusika kama vile:
  • Ema – Neema (uk 27)
  • Buu – Bunju (uk 27)
  • Kalasinga - hili ni jina alilojipa baba yake Yona. Alijipa jina hili kwa kuwa alikuwa Mwafrika wa kwanza kufanya kazi kwa Mhindi. Mhusika huyo alijifunza Kihindi na kufanikiwa kukimudu vizuri baadaye akajipa jina Kalasinga. Kalasinga si jina lake halisi ila ni jina la kupanga.

Tasfida

Tasfida ni matumizi ya maneno yanayoficha ukali wa hali fulani. Mwandishi anatumia mbinu hii kupitia kwa mifano ifuatayo:

  • Sara: Hata nikiitwa nitaondoka nikiwa nimeridhika (uk.13). Haya ni maneno ya Sara akirejelea ufanisi wa watoto wake ambao walikuwa wanachekwa na majirani kutokana na fikra kuwa hawawezi kufaulu kwa sababu ya uhitaji wa wazazi wao. Sara anamaanisha kwamba hata
  • akiaga dunia atakuwa ametekeleza azimio lake la kuwasaidia watoto wake kufaulu maishani.
  • Bunju: Unataka nifurahi ghaya wakati huna kamba ya ulimi (uk. 48). Haya ni maneno ya Bunju kwa Neema. Bunju anatumia tafsida kwa kutumia neno"kamba ya ulimi," kuficha ukali fulani. Maneno haya yanamaanisha kwamba Neema anaongea sana au anaropokwa na maneno.
  • Dina: wewe umekua ukampata Yona kipenzi cha maji (uk. 10). Kipenzi cha maji ni maneno yenye maana ya mtu anayependa pombe; mievi
  • Sara: watt/ walituona masikini wa watoto. Maskini wa kizazi (uk. 55). kupindukia. Maneno haya yametumiwa kurejelea mtu asiye na uwezo wa kupata mtoto, badala ya kutumia maneno ya moja kwa moja na makali kama vile gumba au tasa.

Kuchanganya ndimi

Kuchanganya ndimi ni mbinu inayotumiwa na mwandishi kuonyesha hali ya kuzungumza lugha mbili au zaidi kwa pamoja. Mwandishi wa tamthilia hii ametumia mbinu hii katika uandishi wake kama ishara ya maudhui ya elimu na pia kusawiri hadhi ya wahusika fulani kama walioelimika.

Mifano:

  1. Culture shock (uk. 46) - Usemi huu unamaanisha hali ya kushangazwa na mienendo ya watu ambao wana utamaduni tofauti au mazoea tofauti na yale ambayo mtu aliyatarajia.
  2. Homework (uk. 40). Asna anasema Lemi amempa homework. Hii ina maana kuwa amempa kazi ya ziada. Pia ukurasa 49, Bunju anasema kuwa "ninamsaidia kufanya homework".
  3. Boarding school (uk. 27). Usemi huu una maana ya shule ya bweni.
  4. First class(uk. 28). Usemi huu unamaanisha kiwango cha juu zaidi cha kupita mtihani wa Chuo kikuu.
  5. Flying doctors (uk. 41). Usemi huu unamaanisha madaktari ambao husafirishwa kwa ndege ili kufika haraka mahali penye wagonjwa mahututi.
  6. My foot (uk. 26). Mwandishi ametumia usemi huu kukejeli. Bunju anatumia usemi huu kumkejeli mke wake Neema. Ni usemi unaotumiwa katika jamii ya kisasa na vijana kwa lengo la kutupilia mbali mawazo ya watu wengine.
  7. Hii Servant Quarter inanitosha (uk. 31). Asna anatumia neno servant quarter kurejelea chumba anamoishi jijini. Chumba cha aina hii aghalabu hutumiwa na wafanyakazi wadogo kwenye boma la mwajiri wao. Kwa hivyo, iwapo Asna anaishi mtaa wa kifahari, hana nyumba ya kifahari huko bali anaishi katika chumba kidogo tu.
  8. I wish wangeelewa (uk. 72). Neema anatumia maneno I wish kuonyesha matamanio yake kwa wale wanaopewa kibarua kujua kuwa waajiri wao wanapitia magumu ili kupata mali kidogo waliyonayo.
  9. Akili zako bado sharp kabisa (uk 73). Katika muktadha wa matumizi usemi huu una maana ya kuelewa mambo kwa upesi au kwa haraka.
  10. Mum (uk. 47). Lemi anatumia jina hili kumwita mama yake. Mum ni jina la Kiingereza linalomaanisha mama.
  11. Kesho una time umpeleke huyu out? (uk. 48). Katika muktadha wa matumizi, neno out lina maana ya 'ziara'. Yaani kwenda kuburudika na kujivinjari. Lemi alitaka kupelekwa out wakacheze na kuogelea pamoja na watoto wengine. Nalo neno time limetumiwa kuonyesha 'nafasi'.
  12. Tomboy (uk. 52). Hii ina maana ya msichana anayeishi na kutenda mambo kama mvulana.
  13. Eti alama. My foot (uk 26)
  14. Nimeamka mum (uk 30)
  15. Nilipata culture shock(uk 46)
  16. Nikimaliza , kkesho tutakwenda out? (uk 47)
  17. Kwanini mum? (uk 47)
  18. Kesho una time umepeleke huyu out? (uk 48)
  19. Ooh noo! Kila kitu kishapangwa (uk 50)

Kubadili msimbo

Hii ni mbinu ya kubadilisha lugha wakati wa mazungumzo na kuanza kutumia lugha nyingine tofauti na ile ya kwanza. Mwandishi ametumia mbinu hii katika tamthilia kuonyesha hekima au elimu..

Mfano;
If wishes were horses beggers would ride
(uk. 72). Maneno haya yalisemwa na Yona kwa Neema. Mhusika Yona anabadili msimbo kutoka kwa lugha ya Kiswahili hadi lugha ya Kiingereza kwa kutunga sentensi nzima. Ni kauli inayodhihirisha majuto na nia ya mabadiliko kwa upande wa Yona.

Maswali ya balagha

Hii ni njia ya usemi ambayo hutumia maswali yaliyokusudiwa kusababisha athari fulani bila kutarajia majibu.

Mtindo huu umetumiwa na Sara anayeuliza:

  • (Kwa ukali.) Hivi mtoto una akili wewe? Babako aende kuteka maji kisimani? Wazee wenziwe watamwonaje? Kijiji kitasema nini? Kwamba amesomesha watoto ambao wameniweka jijini ili baba yao ataabike hiyo ndiyo heshima?(uk. 44)
  • Sara alikusudia kuonyesha hisia zake kuhusu kuendelea kukaa kwake mjini na kumsababishia mumewe izara. Usemi huu pia unaendeleza maudhui ya utamaduni, migogoro, na nafasi ya mwanamke katika jamii pamoja na kusawiri sifa za Sara.
  • Mbinu hii imetumika pia katika mazungumzo nafsia ya Neema (uk. 41). Anajiuliza: Leo tungekuwa wapi bila Bunju? ...Mtu huyo atakosaje kuwa zawadi kwako? Maswali haya yanadhihirisha mabadiliko katika hisia za Neema juu ya mumewe Bunju. Anaanza kumthamini zaidi.

Mhusika au msimulizi huuliza maswali yasiyohitaji majibu.

  • Umeona wapi mtu asiyehusiana kwa damu kufanya aliyoyafanya Bunju? (uk 35)
  • Si ni malaika huyo?(uk 35)
  • Huna simile? ( uk 45)
  • Au mimi ni sanamu tu hapa? (uk 50)

Utohozi

Utohozi ni mbinu ya kubadili maumbo ya maneno ya lugha moja na kuyafanya yachukue muundo wa lugha nyingine. Mwandishi ametumia majina ya kutoholewa kutoka lugha ya Kimombo hadi lugha ya Kiswahili. Mifano

  • Hospitali (uk. 51) - neno hili limetoholewa kutoka kwa neno la Kiingereza hospital.
  • Familia - limetokana na neno la Kiingerezafamily.
  • Skuli - limetoholewa kutoka neno la Kiingereza school.
  • Presha (uk. 11) - limetoholewa kutoka neno la Kiingereza pressure.
  • Daktari (uk. 12) - limetoholewa kutoka neno la Kiingereza doctor.
  • Afisini (uk. 27) - limetokana na neno la Kiingereza office.
  • Kliniki (uk. 14) - neno hili limetokana na neno la Kiingereza clinic.
  • Hoteli (uk. 42) - jina hili limetoholewa kutoka kwa neno la Kiingereza hotel.
  • Rekodi (uk. 73) - neno lililotoholewa kutoka neno la Kiingereza record.
  • Mapeni – penny/pennies
  • Chingamu – chewing gum
  • Tikiti – ticket
  • Soksi – socks
  • Digrii – degree
  • Kompyuta - computer
  • Kampuni – company
  • Gesi – gas
  • Gia – gear
  • Resi – race
  • Hospitali – hospital
  • Glasi – glass
  • Shiti – sheet
  • Wodini – ward
  • Seli – cell
  • Mashine – machine
  • Bili – bill
  • Wikendi – weekend
  • Hanchifu – handkerchief
  • Sola – solar
  • Stuli – stool
  • Galoni – gallon
  • Silabasi – syllabus
  • Baiskeli – bicycle
  • Injinia – engineer
  • Kochi – couch
  • Teknolojia – technology
  • Timu –team

Tashbihi

Huu ni usemi wa ulinganisho au ufananisho wa vitu viwili au zaidi kwa kutumia maneno ya ulinganishi: kama vile, kama, mithili ya, mfano wa na kadhalika.

Mifano

  1. Tafunwa kama chingamu (uk. 6); kusemwa sana na watu.
  2. Kutuona kama tambara bovu (uk. 4); ni kuonekana vibaya au kitu kisicho na thamani.
  3. Hayayalikuwa kama vishindo vya mashua na Sisi kama bahari (uk. 56); maana ya tashibihi hii kulingana na matumizi ya muktadha ni kwamba matatizo ya maisha yao yanafananishwa na hali ya mashua kupita kwenye bahari na kwamba walistahimili na kufaulu..
  4. Tunaendeshwa kama tiara (uk. 23); kuendeshwa hivihivi. Kazi kama safari ya ahera (uk. 23); kazi ambayo inachosha; isiyokamilika.
  5. Ni wazi kama mchana (uk. 3) - jambo lisilofichika, lisilo siri.
  6. Mwili mzima mfano wa bua (uk. 4) mwepesi mno. - mwili hauna nguvu, ni
  7. Ni kama msafiri katikajangwa (uk. 7) - mtu mwenye kiu au tamaa ya kupata kitu fulani.
  8. Mwanadamu sawa na tumbo, hakinai (uk. 8) - mwanadamu hatosheki.
  9. ponyoka kama maji kwenye viganja (uk. 10) - jambo lisiloweza kuzuiwa.
  10. Upepo ungeniyumbisha kamajani kavu (uk. 12) - upepo ungempeleka kokote ufanyavyo majani makavu.
  11. Maisha yamekuwa mfano wa gurudumu kwenye gari la masafa marefu (uk. 23). Hata gurudumu likichoka halina hiari. Litaenda tu namna litakavyovingirishwa. Watu hawana chaguo ila kuendelea na maisha yajavyo.
  12. Kujisikia kama abiria kwenye gari liendalo kasi (uk. 29) - kuwa na wasiwasi; kutotulia.
  13. Konda kama ng'onda (uk. 32) - konda kupindukia. Mwoga kama kunguru (uk. 34) - mwoga sana.
  14. Safi kama pamba (uk. 35) — bila doa, uzuri uliokamilika. Hospitali za kijijini ni kama seli (uk. 42) - hali yake ni mbovu.
  15. Watoto wa siku hizi wanakua mithili ya mchicha (uk. 43) wanakua kwa kasi.
  16. Ana moyo kamajiwe (uk. 45) - ana moyo mgumu; si mwepesi wa kutoa; ni mchoyo.
  17. Kuteleza kama sabuniya povujingi (uk. 56) - kushindwa kumudu hali yake.

Methali

Methali ni aina ya semi ambayo huwa na muundo maalumu. Hueleza ukweli fulani wenye maana pana na unaoweza kufasiriwa kwa njia mbalimbali.
Methali hukusudia kuonya, kuelekeza, kuadhibu, kusuta, kulaumu, kushauri na kadhalika. Methali huwa imebeba maana pana kuliko maneno yenyewe.
Tamthilia ya Bembea ya Maisha imetumia mbinu ya methali kwa wingi.

Mifano:

  1. Mungu hamwachi mja wake (uk. 8). - Mcha Mungu anapopitia magumu, Mungu huwa anamsaidia kwa hali yake hatimaye
  2. Kigumba kwa nguruwe kwa binadamu ki uchungu (uk. 63).
  3. Baada ya dhiki faraja (uk. 6).- Baada ya kupitia hali ngumu, mambo hua kuwa rahisi/ mtu huja kupata utulivu. 
  4. Njia haimuagulii msafiri (uk. 6). - Mtu huwa hasumbuliwi na hali yake/ mazoea yake. Ina maana ya kwamba mtu huwa anajipata kuzoea hali yake.
  5. Binadamu mchoyo kwa lake lakini mkarimu ajabu kwa la mwenziwe (uk. 5).
  6. Mlango mmoja ukifunga, macho huiona mingine mingi (uk. 56).
  7. Majirani ni kufaana / leo kwangu kesho kwako (uk 11)
  8. Mwacha mila ni mtumwa (uk. 58).
  9. Mgala muue na haki yake mpe (uk. 66).
  10. Hakuna kizuri kijacho kwa urahisi (uk. 67).
  11. Kutoa ni moyo, usambe ni utajiri (uk. 2)
  12. Mtu hujikuna ajipatapo (uk. 2)
  13. Mungu si Athumani (uk. 10)
  14. Mungu hamtupi mja wake (uk. 10)
  15. Leo kwangu kesho kwal<0 (uk. 11)
  16. Mungu hamwachi mja wake (uk. 11)
  17. Safari ya kesho huungwa leo (uk. 16)
  18. Mrina haogopi nyuki (uk. 18) - Mtu huwa haogopi hali yake. Binadamu huwa anazoea hali yake.
  19. Hakuna refu lisilokuwa na ncha (uk 18) – Kila kitu huwa na mwisho hata kiwe kimekawia kwa muda.
  20. Papo kwa hapo kamba hukata jiwe (uk. 21)
  21. Mwana wa yungwi hulewa (uk. 21)
  22. Kipendacho roho hula nyama mbichi (uk. 21)
  23. Ya kale hayanuki (uk. 24)
  24. Mapema ina sudi (uk. 25)
  25. Afikaye kisimani mapema hunywa maji maenge (uk. 25) - Anayetangulia kufanya kitu hupata kuifanya kwa hali ya kutosumbuliwa. Kwa maana ya juu, anayefika kisimai mapema hupata maji bado hayajachafuliwa.
  26. Samaki hukunjwa angali mbichi (uk. 26) - inatuonya kwamba tuyashughulikie mambo mapema kabla kuharibika.
  27. Msafiri kafiri angawa tajiri (uk. 31) - msafiri hana haja na hali ya bara bara ila tu afike kule aendako. Kwa hali ya Asna, upweke wa mashambani haufai kujalisha ila tu aweze kujikimu kimaisha badala ya kung’ang’ana mjini bure. 
  28. Mwindaji huwa mwindwa (uk. 32) - 
  29. Ng'ombe halemewi na nunduye (uk. 35) - Mtu huwa hasumbuliwi na hali yake/ mazoea yake. Ina maana ya kwamba mtu huwa anajipata kuzoea hali yake.
  30. Mali ya bahili huliwa na mchwa (uk. 45)
  31. Mgala muue na haki umpe (uk. 66)
  32. Paka wa nyumba hawingwi (uk 36) – Paka wa nyumbani huwa hafukuzwi. Mtu huwa haufukuzwi kwao/ alikozoewa.
  33. Wanasema mwenye macho haambiwi tazama (uk 41) – Ni methali mabayo inawahimiza watu wamweze kumakinika nay ale yanayotendeka kwa mazingira yao. 
  34. Msema husahau msemewa hasahau (uk 45) - Mwenye kusema {hasa kwa ubaya] Husahau aliyoyasema lakini mwenye kutajwa kwa ule ubaya hawezi kabisa kuyasahau maneno hayo
  35. Dalili ya mvua siku zote ni mawingu (uk 49)- Kila kitu kina kiashiria chke cha awali kabla hakija fanyika.
  36. Hawajui mwacha mila ni mtumwa (uk 58) - Ni vyema mtu akapathamini kwao kwa sababu ndipo alipotokea na kumemfanya kuwa vile alivyo. Ni vyema kuendelea kulinda yanayohusiana na wewe badala ya kukumbatia mambo yasiyo ya asili yako. Ni vyema kukumbuka kwenu.
  37. Kigumba kwa nguruwe kwa binadamu kichungu (uk 63) - Hii ni methali ambayo hutumiwa kumsuta mtu ambaye hupenda kuwahujumu wengine na ikifika wakati wake kuhujumiwa hulalamika na kujiona kana kwamba anaonewa

Methali katika tamthilia ya Bembeaya Maisha zimetumika kutekeleza yafuatayo:

  • Kupamba lugha na kuipa mvuto wa kisanaa.
  • Kuendeleza maudhui na dhamira ya mwandishi, hasa kuhusu suala Zima la bembea ya maisha.

Sitiari

Ni mbinu ya lugha inayotumia ulinganisho wa moja kwa moja wa kitu na kingine. Kitu kimoja husemwa kuwa kingine. Mifano ya sitiari katika tamthilia ya Bembea ya Maisha.

  1. Mbegu ipandwayo haina budi kuzaa na izaapo mazao yake huvunwa. Mtu huitakasa sahani yake akijua itamfaa tena. (uk. 1-2). Yona analinganisha wanawe (Asna na Neema) na mbegu, mazao yake, na mavuno. Pia, anawalinganisha na sahani ambayo aliitakasa imfae.
  2. Katika uk. 2, Sara anasema kuwa Neema ana 'mzigo' wa familia yake. Mzigo umetumiwa kama sitiari ya majukumu mengi au mazito.
  3. Vilevile, kwenye uk. 2, Yona anasema kuwa fimbo ya mzee hurithiwa na mtoto wa kwanza. Fimbo ni sitiari ya nafasi ya mzee katika familia.
  4. Ukurasa wa 3, Sara anasema kwamba wachapakazi hodari ni njozi iliyopotea. Hii ina maana kuwa hawapatikani.
  5. Mimi mzigo (uk. 4) - mtu ambaye ni tatizo kwa jamaa zake, anayetekelezewa majukumu yake yote.
  6. Amekuwa na kimo cha sindano (uk. 5) - amekuwa mwembamba sana.
  7. Neema ni chuma cha reli (uk. 6) - Neema ana nguvu za kustahimili changamoto za maisha.
  8. Katika uk. 8, mvua ya baraka iliwanyea Yona na Sara. Mvua ya baraka ni sitiari ya watoto ambao Yona na Sara walibarikiwa kuwapata.
  9. Dina anaeleza kuwa watu walimtaka Yona kutafuta mtoto wa kiume ili "utambi wa ukoo wake usizime" (uk. 10). Utambi wa ukoo ni sitiari ya kizazi cha ukoo.
  10. Ukurasa wa 11, dunia ni nyumba ya mitihani. Hii ina maana kuwa dunia ni mahali pa changamoto nyingi.
  11. Sara anasema kuwa alipoanza kuugua alikuwa kimbaumbau mwiko wa pilau (uk. 12) - hii ina maana kuwa alikuwa mwembamba na mithili ya mwiko wa kupikia pilau.
  12. Safari hii ni maji ya mbizi (uk. 16) - safari ni ndefu Maisha ya siku hizi si maji ya kunywa (uk. 23). Maisha si rahisi au mepesi.
  13. Mamangu mzazi ni mboni ya jicho kwetu (uk. 30) - mama mzazi ni mwangalizi wao.
  14. Nyumbani, hiki ni kizimba cha kuku (uk. 31) - ni chumba kidogo na duni.
  15. Maisha ni mshumaa usio mkesha (uk. 32) maisha ni mafupi na hayapo daima.
  16. Sara na Bunju ni chanda na pete (uk. 36) - wanalingana katika maoni yao, ni wamoja.
  17. Mifuko inazidi kuwa king'onda (uk. 41) - inaendelea kuishiwa
  18. Akili za Yona zinatajwa kuwa sumaku (uk. 43) - zinashika mambo haraka.
  19. Nina jeshi lake (uk. 46) - nina watoto wake.
  20. Bunju anamweleza Neema kuwa kuwa yeye (Bunju) ni kichwa na Neema ni shingo (uk. 49). Hii ina maana kuwa Bunju ndiye kiongozi wa nyumba naye Neema ni msaidizi wake.
  21. Ujana ni moshi (uk. 52) - ujana ni kitu kinachopita na kikienda hakirudi.
  22. Ndoa ni mtihani mkubwa sana (uk. 53) ndoa ina majaribu mengi.
  23. Luka anamrejelea Neema kama 'simba wa kike anayenguruma' (uk. 61). - hii ina maana kuwa Neema ana sauti, usemi au hadhi sawa na ya mtoto wa kiume.
  24. Watoto walikuwa nyota ya jaha (uk. 61) — ina maana kuwa watoto wa Sara na Yona walikuwa bahati kubwa kwao.
  25. Mwanamume ni mto wa kifuu (uk. 67) - ina maana kuwa mwanamume amesawiriwa kama mtu hatari.
  26. Sasa rudini mzalishe mbegu nzuri (uk. 68) - wawasaidie watoto wengine kukua vyema kama wao; wawe mfano kwa wengine.
  27. Shikeni usukani muwe marubani wa kweli ili ndege ipae angani (uk. 68) - chukueni nafasi ya kuleta maendeleo kijijini.
  28. Si kifyefye ni chuma cha reli (uk 5) - Maneno haya ni ya kumsifia Neema jinsi alivyokuwa mwenye busara na kumakinika.
  29. Dunia ni nyumba ya mitihani (uk 11) - Kwa matumizi, yanaelewa kwamba maisha yamejawa na majaribu.
  30. Nilikuwa kimbaumbau mwiko wa pilau (12) - Sara anaeleza hali yake ilivyokuwa imezorota awali. Anaeleza hali ya kukonda na kukosa nguvu.
  31. Ana bidii ya mchwa (uk 45) - Maneno haya yanaeleza jinsi Bunju alivyokuwa na bidii
  32. Au mimi ni sanamu tu hapa? (uk 50) – Swali hili linaulizwa kuonyesha kwamba aliona haonekani kama mtu.
  33. Ndoa ni bembea (uk 54)- Hadithi yote inazunguka sitiari hii. Maisha ya wahusika inalinganishwa na Bembe jinsi ilivyo na changamoto na faraja zake, kuenda juu na chini mbele na nyuma mithili ya bembea.
  34. Tuna simba wa kike anayenguruma (uk 61) – Hii ni sifa ya Neema kulingana na jinsi alivyojikimu kimaisha.

Tashihisi

Tashihisi ni mbinu ya mwandishi kuvipa viumbe visivyo na uhai sifa za uhai au za kibinadamu. Pia huitwa uhuishi.

  • Katika uk. 5, Kiwa anasema kuwa mvua yenyewe imefanya ugeni. Kiwa analinganisha mvua na mgeni, na hivyo kuipa mvua sifa za uhai.
  • Katika uk. 6, Dina anasema kuwa maradhi yamemgeuza Sara kuwa ngoma.
    Katika mfano huu, maradhi yamesawiriwa kuwa yenye uwezo wa kumpiga Sara kama vile mtu anavyopiga ngoma.
  • Katika uk. 9, Dina anamweleza Kiwa kuwa "dunia mwanangu imetufunza Sisi wazee wenu". Katika mfano huu, dunia imepewa uwezo wa kutoa mafunzo. Hii ina maana kuwa matukio mbalimbali duniani yana uwezo mkubwa juu ya maisha ya mwanadamu.
  • Tashihisi pia imetumika katika uk. 38. Neema analalamika kuhusu maradhi yasiyosikia dawa. Anasema, maradhi "yakitaka huzichezea dawa mwajificho. Dawa zikiingilia huku, maradhi hutokezea pale, hali pesa zinakwenda, shughuli zinasimama". Vitu hivi vitatu: maradhi,pesa na shughuli vinasawiriwa kuwa na uwezo fulani ambapo maradhi yanazidi uwezo wa vyote viwili.
  • Vilevile, tashihisi imetumika katika uk. 39 ambapo Bunju anamwambia Neema kuwa "chumba chenyewe kinajisemea". Hii ni baada ya Bunju kufika nyumbani kwake na kupendezwa na uzuri wa chumba hicho. Mfano huu una athari ya kusisitiza uzuri wa chumba hicho usiofichika.
  • Mbinu hii pia imetumika katika uk. 56 ambapo Sara anasema kuwa agongo liliyamega maadili" ya Yona kimyakimya na taratibu uwajibikaji wake ukawa umemponyoka. Gongo ni aina ya pombe kali.
  • Mwandishi wa Bembea ya Maisha ameisawiri pombe hii kuwa na uwezo juu ya mwenendo wa maisha ya mtu na kuweza kumdhuru mtu huyo.
  • Vilevile, katika uk. 62, Beni anasema kuwa Yona alikuwa mwalimu mwenye bidii kabla "tembo kunyoosha mikono yake na kumdaka". Mfano huu, sawa na ule uliotangulia hapo juu, unadhihirisha uwezo mkubwa wa pombe kumteka na kumyumbisha mtu.

Tashbihi

Ulinganishi kwa kutumia viunganishi kama, mithili, mfano na sawa/ sawa na

  1. Mwili mzima mfano wa bua (uk 4) – Sara anaeleza jinsi hali yake ilivyodhoofika.
  2. Mwenye akili ncha ya sindano (uk 5)- Aliye mwerevu sana.
  3. Ni kama kamba iliyomfunga ng’ombe (uk 9) – Wanakwenda na mkondo ambao maisha unawapeleka nao.
  4. ….mikono inatetemeka kama lumbwi (uk 21) – Mikono inatetemeka sana
  5. Mnaishi kama mchwa kwenye kichunguu (uk 31) – Wanaishi kwa hali duni. Nyumba za ni ndogo na hazina nafasi za lumtosha mtu.
  6. Ulivyokonda kama ng’onda (uk 32) - Kueleza mhusika amekonda sana.
  7. Mwoga kama kunguru (uk 34)
  8. ….safi kama pamba (uk 35)
  9. Kiguu na njia kama siafu (uk 45)- Inamweleza Bunju kama mtu aliye shughulika sana.

Chuku

Kutia chumvi au kufanya kitu kionekane kikubwa sana au kidogo sana.

  1. Anapokuangalia unahisi anasoma fikra zako (uk 5) – ana macho makali/ anaonekana kuwa na hekima na kumakinika sana
  2. Upepo kiasi ungeniyumbisha kama jani kavu wakati wa kipupwe (uk 12)- Kuonyesha jinsi Sara alivyokosa nguvu za kimwili/ jinsi hali yake ya afya ilivyokuwa imedhoofika.
  3. Mji una joto utadhani ndio kitovu cha jua (uk 16) – Mji ulikuwa n ajoto jingi sana.
  4. Nikipata Bunju wangu nitakuwa nikilia hadi naenda hospitalini kuongezwa machozi (uk 34) - Maneno haya ni ya Asna yanaweza kuwa na maana mbili. Kwanza, Ansa angefurahia sana kumpata bwana atakayempenda jinsi Sara na Neema wanampenda Bunju. Pili, kulingana na fikra za Asna kuhusu Bunju, tunaweza kujua kwamba Asna hampendelei Bunju. Kwa hivyo, machozi haya yanaweza kuwa ya huzuni kwa hali ya kuwa na bwana ambaye kwa maoni yake hajitolei ya kutosha kama Bunju
  5. Mjukuu wangu hatofautishi kondoo mbzuzi na mbwa. Wote hao kwake ni mbwa (uk 59)- Maneno haya yanatumiwa kuonyesha jinsi watoto wa kisasa wamelelewa kwa umbali na mila na desturi zao. Wameishi mjini na hata kufikia mahali hawajui yoyote kuhusu mashambani

Taswira

  • Taswira ni dhana ambayo hutumia maneno ili kumchorea msomaji picha fulani katika fikira au akili yake. Pia huitwa jazanda.
  • Inawezekana mwandishi kutumia taswira za kimaelezo au zile zilengazo hisi za mwanadamu kama vile joto, mnuso, mguso na usikivu.

Mifano

  • Taswira inajitokeza kwenye maneno yaliyo kwenye mabano au yaliyoandikwa katika hati ya kiitaliki. Maelezo hayo yanatuchorea picha akilini mwetu.
    Yanatufahamisha na kutujulisha dhahiri wakati, mahali na matendo yanapofanyikia.
  • Kwa mfano, katika onyesho la kwanza sehemu ya kwanza maneno yaliyo kwenye mabano yanatuonyesha kwamba onyesho linafanyika wakati wa alasiri, mahali ni nyumbani kwa Sara, tunaona Sara akichukua vidonge vya dawa na kuvimeza
  • kabla ya kuketi kwenye kochi jipya. Tunaona namna ukuta wa nyumba ya Sara umepambwa na picha za familia. Takriban maneno yote yaliyo kat:ika hati ya kiitaliki yanatuchorea picha fulani akilini, hivyo yanajenga taswira.
  • Taswira katika tamthilia hii pia imejidhihirisha kupitia kwa maneno yanayosemwa na wahusika. Kupitia usemaji wa wahusika, msomaji anapata taswira fulani kuhusiana na namna mhusika anavyozungumza. Kutokana na maneno yao, msomaji hupata taswira sikivu ambayo inamdhihirishia toni au kiimbo anachotumia mhusika lengwa.
  • Katika Onyesho I Sehemu I; mazungumzo kati ya Sara na Yona yanatuonyesha taswira sikivu ya toni wanayotumia, Yona anatumia toni ya juu naye Sara anatumia toni ya chini. Maneno Yao yanatuchorea picha akilini kuhusu wanavyozungumza.
    Taswira ya aina hii ndio inayowezesha tamthilia kuigizwa jukwaani kwa kutumia toni au kiimbo kinachofaa.
  • Anwani ya tamthilia hii inatuchorea picha akilini. Neno bembea linarejelea kifaa ambacho mara nyingi hutumika na watoto kuchezea. Kifaa hiki huenda juu na chini na kurudi nyuma na mbele. Hivyo basi,
  • BEMBEA YA MAISHA ni taswira fikirivu, msomaji anaposoma anwani hii anapata mawazo mengi kuhusu maisha ambayo anayalinganisha na bembea. Msomaji anatarajia kupatana na maisha ambayo yana panda shuka au ambayo yanayumbisha anaposoma tamthilia nzima. Hali hii inadhihirika wazi kwa kuwa anwani Bembea ya Maisha imejidhihirisha katika maelezo na matendo ya wahusika katika tamthilia nzima.

Alama za duku duku

  1. Nilikuwa ninasema…ninasema… (uk 8)
  2. …kuhusu….kuhusu (uk 21)

Majazi ni mbinu ambayo mwandishi hutumia kuwapa wahusika majina kulingana na tabia zao. Mbinu hii inadhihirika kupitia kwa wahusika kama vile:

  • Bunju - jina Bunju ni la kimajazi. Bunju alipewa jina hili lililolinganishwa na mnyama mwenye sumu lakini sumu hiyo huondoka baada ya kusafishwa. Bunju ana tabia mbaya inayolinganishwa na sumu ya mnyama huyo. Kwa mfano, alionekana kuwa na ukali kwa mambo ya kusaidia Neema katika matibabu ya mama mkwe (Sara). Baada ya kushawishiwa kwa muda na Neema, ukali huo unamwondoka na kumweleza Neema kwamba atamsaidia kulipa gharama ya matibabu ya mama yake (uk. 40). Anamwambia atampiga jeki.
  • Neema - Neema ni jina la kimajazi. Neno neema lina maana ya kufanikiwa au kustawi. Mwandishi amempa Neema jina hili kutokana na sifa za kustawi na kufanikiwa maishani. Neema amefanikiwa kusoma hadi Chuo kikuu na kustawi kwa digrii mbili, amefanikiwa kupata kazi nzuri, amefanikiwa kupata mume anayemjali na kushughulikia maisha ya familia yake na pia amefanikiwa kuwalipia karo dada zake hadi Chuo kikuu. Kwa kifupi, mhusika Neema amefanikiwa kwa kiasi kikubwa maishani.
  • Sara - mhusika Sara amepewa jina hili kutokana na namna alivyosemwa na wanajamii. Neno sara lina maana ya kutapakazwa au kuenezwa kila mahali. Jina la Sara lilienezwa na wanajamii kila mahali. Alisemwa sana na kutukanwa kwa kuwa hakuwa na watoto wa kiume (uk. 13). Alisemwa kotekote ikiwemo makanisani na magengeni. Kwa sababu hii mwandishi akampa mhusika huyo jina, Sara

Kuhamisha ndimi

Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu

  1. If wishes were horses beggar would ride (uk 72)

Jazanda

Jazanda ni kunga ya utunzi ambapo lugha inatumia kusawiri picha fulani kutokana na maelezo yanayotumia maneno teule au tamathali za usemi.

  1. Hali ya nyumba ya Asna- upweke

Mfano, kukosa stima, kitanda kilivyo, upishi wa mlo wa uji, umbo na mwili wa Asna
Kila mara mwandishi anapotuonyesha jinsi nyumba ya Asna ilivyo, anatuonyesha hali ya umaskini Asna aliyoish nayo. Hali hii inamfanya hata mama yake Asna, Sara, kumsihi arudi mashambnai kwa kumwambia upweke aliyoishi nayo ni ya hai ya juu sana.

Mbinu za kishairi

Mbinu za kishairi ni sehemu muhimu ya matumizi ya lugha katika tungo za kitamthilia. Miongoni mwa mbinu hizo muhimu ni takriri.

Takriri

Takriri ni urudiaji wa sauti, silabi, neno au sentensi za namna moja zinazofuatana kwa karibu. Takriri hupamba lugha katika fasihi na pia kuvuta nadhari ya msomaji au msikilizaji.
Mwandishi wa tamthilia ya Bembeaya Maisha ametumia mbinu ya takriri katika kazi yake. Mifano:

  • Sara: ... Ulikuwa umenila kiasi cha kuniacha chicha. (uk. 2).
  • Kiwa: Dunia ya leo haithamini kimo, inathamini akili. Haitaki kututumua misuli, inataka tambo la fikira. (uk. 5).
  • Dina: Dunia hii sasa tunaishi katika hofu. Tunahofu hata tusichokifahamu. (uk. 9).
  • Dina: Wewe unaona rangi, tena rangi ya mwisho wa kinachoelea. Kabla kielee kimepigwa shoka, kimeonja misumeno ainaaina, kimetambaliwa na randa, kimestahimili makali ya patasi, na kukapaswa na mikwaruzo ya msasa. (uk. 10).
  • Sara: Wewe unajua yote yaliyosemwa, hadharani na faraghani. Si makanisani, si magengeni. (uk. 13). Sara: Tena hodari wa misemo na nahau. Wala hawana simile
  • kutuloweka kwenye misemo na nahau zao. Hawana simile mwanangu!
  • Sara: Tumeyaacha maji ya mbizi na kuingia kwenye maji ya mbuzi. (uk. 20).
  • Neerna: Kikijanjaruka hakitakuwa na budi ila kurauka. (uk. 25).
  • Neema: Usingepikika, usingelika. (ul<. 41).
  • Neema: Mwenyewe huyo analipia kila kitu. Ninakwambia kila kitu! (uk. 41).
  • Asna: Ndoa imeyatia doa maisha yako. (uk. 53).
  • Sara: Hizo juu-chini chini-juu ndizo utamu wake. (uk. 54).
  • Asna: Elimu ni muhimu mama. (uk. 55).
  • Sara: Mungu hakupi yote. Akikupa hiki, anakunyima kile.
  • Akikupa yote yatakushinda. (uk. 55). Sara: Watu walituona maskini wa watoto.
    Maskini wa kizazi. (uk. 55).
  • Sara: Wakatulaumu na kutusema bila simile. Bila simile! (uk. 56).
  • Yona: Malezi yameachiwa yaya. Nyumba ni ya yaya. (uk. 59).
  • (xviii) Yona: Asubuhi niko skuli majira ya alfajiri, kiboko mkononi...
  • Jioni darasani tena, kiboko mkononi. (uk. 62).
  • Yona: Nilishindwa kuingia kazini kila siku. Nilishindwa kuishi bila kulewa. (uk. 62).
  • Yona: Yabarikiwe mashamba yetu.
  • Beni: Ibarikiwe mimea yetu.
  • Luka: Vibarikiwe vizazi vyetu. (uk. 64).
  • Neema: Kwenye hujuma na kuchimbana, kwenye ugomvi na mivutano, kwenye chuki na uhasama wa kitoto, kwenye tembo na gumzo lisiloisha, penye uchimvi na kusutana (uk.65).
  • Sara: Anza polepole. Anza na baba yenu. Badala ya kumkabili, mshawishi.
    Atakuelewa. Akikuelewa atauendeleza ujumbe. (uk. 69).
  • Yona: Siku zangu za uzeeni lazima nizitumie kumwangalia mke wangu mgonjwa.
    Lazima nimshukuru kwa vitendo kwa jinsi alivyojitolea kuijenga familia yetu. Kwaheri pombe. Buriani. (uk. 70).

Ishara na taashira

Ishara katika fasihi hutumiwa kurejelea kitendo, hali au kitu kinachodokeza au kuonyesha dalili ya kitu kingine. Nayo taashira ni alama mahususi ambazo huhusishwa na hali fulani katika jamii.

  1. Katika uk. 1, Yona analalamika kuwa nyumba haifuki moshi. Kufuka kwa moshi ni ishara ya upishi. Kutokuwepo kwa moshi ni ishara na pia taashira kuwa hakuna kinachopikwa.
  2. Mwangaza hafifu unaotokana na taa ya sola katika chumba cha Asna mjini ni ishara ya maisha ya Asna. Mwangaza huu hafifu unaashiria kuwa ingawa Asna anaona anaishi maisha mazuri na katika mtaa wa kifahari, mazingira anamoishi si mazuri sana. Uzuri wake ni hafifu. Chumbani humo hamna vitu vya thamani vinavyoendana na maisha ya kifahari. Ishara hii ni kama kejeli kwa maisha anayoishi Asna.
  3. Katika uk. 6, Dina anasema kuwa njia, sawa na moyo wa mwanadamu imejaa giza. Mfano huu unatumia giza kama ishara au taashira ya mambo yasiyojulikana au yasiyoweza kutabirika.
  4. Katika uk. 61, Luka anaeleza kuwa kijiji kina mwanga kutokana na ufanisi wa watoto wa Yona. Katika mfano huu, mwanga umetumiwa kuashiria maendeleo yanayotokana na elimu. Baadhi ya maendeleo hayo ni watoto kupata kazi, kuwajengea wazazi wao nyumba na kununua gari na kuenda nalo kijijini.
  5. Vilevile, mbinu ya ishara imetumika katika uk. 15 ambapo Dina anapika kwa kuni mbichi zinazomfanya Sara kuondoka nje kwa sababu ya moshi. Kuni mbichi zinaashiria umaskini na hali ngumu ya maisha ya kijijini. Pia, ni ukosefu wa maendeleo. Hali hii inaweza kutofautishwa na mjini ambako watu wanapika kwa kutumia jiko la gesi.
  6. Ishara pia imetumika pale ambapo tunaelezwa kuwa Salome alipata First Class katika mtihani wake wa Chuo kikuu (uk. 28). First Class imetumika kama ishara ya hekima na bidii masomoni.
  7. Katika uk. 33, Sara anamwambia Asna kuwa Bunju ashanunua leso yake akavaa mpaka ikazeeka. Leso ni ishara ya zawadi au kirimu kwa mama mkwe. Hivyo basi, Sara anamtaka Asna atafute mume amletee zawadi au amkirimu.

Tabaini

Ni mbinu ya fasihi ambapo jambo husisitizwa kwa kutumia kikanushi 'si'. Mbinu hii imetumiwa na mwandishi wa Bembea ya Maisha mara kadhaa.

Mifano:

  • Asna: ...nyumbani pakigeuka kuwa kambi ya jeshi nitafanyaje! Amri si amri, masharti si masharti! Asna anasisitiza hali ya ndoa anayoiona kuwa haifai.
  • Sara: Wewe unajua yote yaliyosemwa, hadharani na faraghani. Si makanisani, si magengeni. Sara anasisitiza kuwa watu waliwasema kila mahali, hata makanisani, mahali pasipofaa kusengenywa mtu.

Tanakuzi

Ni tamathali ya usemi inayolinganua mawazo kwa kutumia mkinzano wa maneno, virai au sentensi kwenye miundo yenye usambamba.

  • Katika uk. 1, Yona anasema kuwa "njaa haileti shibe". Hapa kuna mkinzano baina ya njaa na shibe.
  • Katika uk. 9, Kiwa anasema kuwa dunia imekuwa ngumu kama "mwanga uletao kivuli". Mkinzano upo baina ya mwanga na kivuli.

MBINU ZA KIMUUNDO

Mbinu za kimuundo hutumiwa na mwandishi kuendeleza msuko wa kazi ya fasihi. Mwandishi wa tamthilia ya Bembea ya Maisha ametumia mbinu kadhaa za kimuundo kujenga msuko wa tamthilia yenyewe.

Mifano

Uzungumzi nafsia

Ni aina ya monolojia itolewayo na mhusika mmoja akiwa jukwaani pekee yake. Mbinu hii hutumiwa kuwasilisha maoni, hisia na fikra za mhusika kuhusu jambo fulani.

  • Mbinu ya uzungumzi nafsia imetumika (uk. 38) ambapo Neema anazungumza pekee yake na kudhihirisha hisia zake kuhusu maradhi yasiyosikia dawa.
    Anasema maradhi hayo yanamfukarisha mtu. Mtu huwa hana la kufanya ila kumwomba Mungu amwepushie. Ni wazi kuwa maradhi yana uzito usiostahilimika.
  • Mbinu hii pia imetumika katika (uk. 41) kwenye mazungumzo ya kibinafsi ya Neema. Neema anajisemea kuhusu Bunju. Anasema kuwa Bunju ni zawadi kwake kwa kuwa alimsaidia wakati alipatwa na ajali na kuwachwa katika hali mahututi. Tunamwona pia akikumbuka maneno ya mamake kuhusu Bunju, kuwa Bunju ni mmoja wao. Anakiri kuwa zamani hakuona hivyo kwa kuwa mtazamo wake kuhusu mumewe ulikuwa hasi. Sasa, kwa sababu ameahidiwa kusaidiwa kulipa gharama ya hospitalini ya Sara, mtazamo wake kuhusu Bunju unabadilika na anmuona kama zawadi kwake.
  • Uzungumzi nafsia pia unatokea katika mazungumzo ya Yona (uk. 70). Yona anamhurumia mke wake Sara kwa sababu ya ugonjwa uliodhuru. Anasema awali aliona kuwa ni kama mzaha kuwa mkewe anaugua. Anajilaumu kuwa angejua hangemfanyia madhila mkewe, angemtunza na Silesi za maisha wangezila zijavyo. Tunapata nia na mwelekeo wa Yona kwa kurejelea mazungumzo yake.
    Anasema ni lazima awache njia zake za awali za unywaji pombe na kutoshughulikia familia yake.
  • Mkondo anaochukuwa ni kubadilisha tabia na kuahidi kwamba siku zake za uzeeni atazitumia kumwangalia mke wake Sara.

Usemaji-kando

  • Hii ni mbinu ambayo mhusika mmoja anasema maneno kwa hadhira au mhusika mwingine huku wenzake kwenye jukwaa wakijifanya kutosikia anachosema mhusika huyo.
  • Mbinu hii humsaidia msomaji kuelewa nia na kuibua msimamo wa mhusika kuhusu mhusika mwingine, wazo au kitu fulani kinachozungumziwa katika kazi ya fasihi kinyume na anayosema au kufanya akiwa na wahusika wengine.
    Mwandishi wa tamthilia ya Bembea ya Maisha ametumia mbinu hii katika kazi yake.
  • Mbinu hii imetumika katika mazungumzo baina ya Bela na Neema (uk. 24). Bela anaposisitiza kumwuliza Neema sababu ya kutowacha Sara alale kwake ili wapige gumzo, Neema anageuka kando na kuuliza kwa nini Bela aendelee kuulizia kuhusu hilo. Ni wazi kuwa Neema hataki kuzungumzia suala hilo lihusulo mila na tamaduni. Ana hisia hasi nalo.
  • Mbinu ya usemaji-kando pia imetumika katika uk. 29-30. Neema anainuka na kuihutubia hadhira. Analalamikia hali ngumu ya maisha yanayokwenda mbio kama gari liendalo kwa kasi. Anashangaa iwapo Bunju anamwelewa kama ilivyokuwa hapo awali kwa kuwa hataki kumsaidia kumlipia mama yake matibabu. Anajiuliza iwapo anaweza kumwacha mamake ateseke kwa sababu ya ugumu wa maisha.

Mbinu rejeshi

  • Mbinu rejeshi ni sehemu katika kazi ya fasihi inayozungumzia matukio katika wakati uliopita. Pia huitwa kiangaza nyuma. Mbinu hii imetumika katika sehemu mbalimbali katika tamthilia ya Bembea ya Maisha. Kimsingi, mbinu hii imetumika kutofautisha maisha ya jana na ya leo, kuendeleza maudhui ya utamaduni na mabadiliko. Dina anaturejesha nyuma kiwakati katika mazungumzo yao na Siwa ambapo anasimulia kuhusu maisha ya awali ya familia ya Yona na Sara (uk. 7). Kupitia mbinu hii, tunapata kuelewa shida ambazo Sara na Yona walipitia, hasa masimango ya watu waliowasema kwa kukosa kupata watoto.
  • Katika (uk. 51) Bunju na Neema wanaturejesha nyuma kwenye ajali iliyompata Neema. Bunju anasema alimpata Neema akiwa mahututi.
  • Neema anakiri kuwa ilikuwa ajali mbaya sana ambayo ilisababisha vifo vingi. Hata hivyo, Neema alinusurika baada ya kupangiwa matibabu na Bunju. Mfano huu unaendeleza sifa ya utu na ukarimu alionao Bunju.
  • Mbinu rejeshi pia imetumika katika uk. 62 kupitia mazungumzo baina ya Beni, Luka na Yona. Hususan, Yona anakumbuka maisha yake ya awali alipokuwa kijana na mwalimu. Yona anaeleza kuwa alikuwa anarauka kwenda shuleni, akiwa na kiboko mkononi na hakupenda wanafunzi kuchelewa kufika shuleni. Vilevile, anakumbuka namna alivyovibeba vitabu kwenye baiskeli yake kwenda kuvisahihisha wikendi. Mfano huu unadhihirisha bidii yake kabla pombe haijamwathiri na kumbadilisha.
  • Mfano mwingine wa mbinu rejeshi umetumika katika uk. 64 ambapo Neema anakumbuka usafiri wa zamani kabla mabadiliko ya kiteknolojia. Anasema kuwa zamani wangechukua siku tatu kupambana na barabara ya vumbi, na mvua iliponyesha, kulikuwa hakuendeki mpaka barabara ikauke ndipo safari iendelee. Sara anachangia na kusema kuwa mwendo ulikuwa wa kobe na safari ilikuwa ya kuchosha. Mfano huu unaendeleza maudhui ya mabadiliko ya kiteknolojia na mgogoro baina ya jana na leo.

Sadfa

Sadfa katika fasihi ni hali ambapo matukio mawili hutokea kwa wakati mmoja bila kupangwa na kwa namna ya kushangaza au inayoashiria bahati.
Mbinu ya sadfa imetumiwa mara kadhaa katika tamthilia ya Bembeaya Maisha.

  • Kwanza, mbinu ya sadfa imetumiwa katika (uk. 34) ambapo Sara na Asna wanazungumza kuhusu ndoa ya Neema na Bunju wakiwa nyumbani kwa Asna mjini. Ghafla, na bila kutarajiwa, Neema anaingia bila kubisha. Asna anashtuka.
  • Vilevile, katika (uk. 71) Sara anamweleza Neema aende kuandaa kiamshakinywa. Neema anaitikia wito wa mama yake na kusema kuwa ataandaa kiamshakinywa mara moja. Hata hivyo, Yona anawaeleza kuwa alikuwa ameshaandaa tayari. Hii ni sadfa na pia kinyume cha matarajio. Neema anaonyesha kushangazwa na kitendo hicho cha babake.
  • Kupatana kwa Neema na Bunju ilikuwa kwa ajali. Bunju ndiye aliwaita daktari aina ya Flying Doctors na maisha ya Neema yakaokolewa.
  • Neema anapomwitisha pesa Bunju za kuongezea za matibabu, Bunju alikuwa anatoka ili aende kumwona rafiki yake waliokuwa wafanye shughuli pamoja na kwa bahati angelipwa.
  • Ugonjwa wa Sara unamfanya asiwezekufanya kazi na umalazimu Yona ashughulike zaidi kama vile Sara alivyolazimika kushughulika zaidi baada ya Yona kupoteza kazi.

Taharuki

  • Taharuki ni hali katika kazi ya fasihi inayoibua matarajio au hali ya kutojua kitakachofanyika hatimaye.
  • Mwandishi wa tamthilia ya Bembea ya Maisha ametumia mbinu ya taharuki kuendeleza msuko wa tamthilia yenyewe na kumpa msomaji hamu ya kusoma zaidi kujua kitakachotokea.

Mifano

  1. Katika onyesho la kwanza sehemu ya kwanza (uk. 1-2), mwandishi anaeleza kuhusu ugonjwa wa Sara. Pia, Asna anaeleza kuwa Sara ataishia
  2. kumeza vidonge maisha yake yote kwa sababu ya ugonjwa huo. Kisha, mwandishi anaonyesha Sara akisafirishwa mjini na kulazwa katika hospitali ya bei ghali iliyo na huduma bora na wataalamu hodari kuliko hospitali za kijijini. Mwandishi anampa msomaji hamu ya kuendelea kusoma kujua iwapo ugonjwa wa Sara utapona.
  3. Katika uk. 10, Dina anamweleza Kiwa kuhusu namna Yona alivyoanza kulewa kupindukia na kuanza kumpiga mkewe Sara kipigo cha mbwa. Hali hii ya Yona na Sara pia inamulikwa kupitia kwa mazungumzo ya Asna na mamake Sara. Msomaji anapata hamu ya kutaka kujua iwapo ulevi wa Yona ulipungua au ulifikia kikomo.
  4. Katika uk. 28, mwandishi anadokeza kuhusu mgogoro baina ya Neema na mumewe Bunju. Bunju anakataa kumsaidia Neema kulipia gharama ya hospitalini kwa ajili ya matibabu ya Sara. Hata hivyo, katika
  5. uk. 40, Bunju anabadilisha msimamo na kuahidi kusaidia "baadaye", kisha anaondoka. Msomaji anapata hamu ya kutaka kujua iwapo Bunju alitimiza ahadi hiyo.
  6. Mfano mwingine wa taharuki unazuliwa na mgogoro baina ya Asna na mamake Sara kuhusu haja ya ndoa (uk. 52-53). Asna anasema kuwa kuolewa ni hiari ya mtu, na kuwa ndoa ni dhuluma. Kwa upande mwingine, Sara anamhimiza Asna kutafuta mchumba aolewe amletee wajukuu na zawadi kutoka kwa mumewe. Msomaji anapata hamu ya kujua iwapo Asna aliishia kuolewa au la.

Kinaya

  1. Asna anakataa kurudi kijijini kwa umaskini licha kuishi kwa umaskini zaidi mjini.
  2. Asna anashinda akimwingilia Bunju kwa kusema hajitolei ya kutosha licha ya Bunju kuwasomesha yeye an dada yake Salome.
  3. Yona anauliza Neema amemfanyia lipi kubwa licha ya Neema kuwaandikia wafanyikazi n ahata kuwapa pesa za mahitaji yao.
  4. Bunju anamlaumu Neema kwamba hamshughulishi kwa maamuzi ila ni yeye alimwambia asimshugulishe kwa mambo ya kwao.
  5. Beni anamwingilia Yona na watoto wake wa kike lakini anakasirika pindi wake anatajwa.
  6. Licha ya nafasi ya mwanamume kuwa juu kuliko ya wanawake, watoto wasichana wa kijiji hicho waliotajwa (watoto wa Yona) wamehitimu kuliko wale wa kiume waliotajwa (Kiwa na mtoto wa Beni)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Fani - Mbinu za Lugha, Mbinu za kishairi na Mbinu za Kimuundo - Mwongozo wa Bembea ya Maisha.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?