Print this page

KCSE 2012 Kiswahili Paper 2 with Marking Scheme

Share via Whatsapp
  1. UFAHAMU: (Alama 15)

    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Nchi nyingi duniani zimetia sahihi mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watoto. Haki hizi ni pamoja na uhai, lishe bora inayootosha na makazi bora yaliyo salama. Hali kadhalika, kila mtoto ana haki ya kupata elimu. Elimu inafaa kutolewa bure, iwe inayofaa na inayopatikana kwa urahisi. Isistoshe, mtoto hafai kupigwa, kudunishwa wala kubaguliwa kwa namna yoyote ile; iwe kitabaka, kirangi, kijinsia na vinginevyo. Mtoto hapaswi kufanya kazi za kitumwa, nzito na za kushurutishwa. Vile vile, mtoto ana haki ya kutunzwa na kulindwa dhidi ya hali yoyote inayoweza kumhatarisha. Fauka ya haya mtoto anastahili kushirikishwa katika kufanya maamuzi yanayoweza kumwathiri maishani. Pia mtoto ana haki za kupata huduma za afya, mahitaji maalum na habari kuhusu masuala mbalimbali. Pamoja na hayo, mtoto anastahili kupendwa na kuheshimiwa kimawazo na kihisia.

    Haki za watoto zinatakiwa kulindwa na kila mwanajamii, serikali na wazazi wakiwa katika mstari wa mbele. Hii ndiyo sababu serikali za mataifa mengi zimeshirikisha haki hizi katika katiba na sheria za nchi husika. Yeyote anayezikiuka anapaswa akuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Walakini, haki hizi bado zinakiukwa. Watoto wengi kote dunuani wananyimwa haki zao. Kuna watoto ambao hawajawahi hata kupata kibanda cha kuweka ubavu. Wengi wa hawa wamejipata wakiselelea kwenye mitaa na hata majaa ya miji na vijiji mbako hulazimika kupitisha usiku hata katika majira ya kipupwe na masika! Wengine hawapati chakula; licha ya kuwa wanatakiwa kupata chakula chenye lishe bora. Kwao kutarajia mlo awamu tatu kwa siku ni njozi; kwani hata awamu moja ni adimu kupata! La kusikitisha ni kwamba wale wanaotarajiwwa kuwa vigogo wa kuzilinda haki hizi ndio wanaoongoza katika kupalilia ukiukaji wazo. Kila siku tunasikia na kushudia visa vya watoto kupigwa, kushinikizwa kufanya kazi za sulubu kipunda, kunyanyaswa kijinsia, kuishi katika mazingira hatari au kuuawa. Baadhi ya wahusika na vitendo hivi hasi huwa wazazi au jamaa wa karibu kama vile wajomba, shangazi, au wahudumu wa nyumbani.

    Madhila wanayoyapata watoto hayatokei tu katika mazingira ya nyumbani. Mateso huvuka mipaka na kufikia ngazi ya kimataifa. Watoto wengi katika mataifa yenye fujo hutekwa na kutumikishwa vitani. Linalokata maini ni kwamba baadhi ya viongozi katika mataifa haya hawafanyi lolote kuwanusuru. Lao huwa kuwatazama watoto wanaotakiwa kuwalinda wakigeuzwa kuwa mababe wa kuua na kuuana. Watoto hawa huvishwa magwanda ambayo miili yao minyonge haiwezi kuyahimili. Pia hulazimika kuyavaa mabuti ya kijeshi ambayo huwa nanga kwao kubeba, licha ya bunduki zinazokaribia kuwazidi uzani.

    Mojawapo ya mambo ambayo viongozi nchini humu walilenga shabaha kuyafikia baada ya kujinyakulia uhuru ni elimu kwa wote. Hata hivyo, hii imekuwa kama ndoto isiyotabirika katika baadhi ya janibu. Ni kweli kwamba sera ya elimu bila malipo katika shule za msingi nchini humu inaendelea kutekelezwa. Hata hivyo, asilimia ya watoto na hata watu wazima wasiojua kusoma na kuandika ingali kubwa. Jukwaa la vijiji nchini humu na hata katika mataifa mengine ya ulimwengu wa tatu limesheheni idadi kubwa ya watoto wasioenda shuleni. Kichocheo kikuu cha hali hii ni kwamba wazazi na walezi wamejipata katika lindi la ufukara uliokithiri. Hata wanapojitahidi kujinyanyua na kujikuna wajipatapo kuyakidhi mahitaji ya kielimu ya wanao, wao hujipata wakitapatapa katika katika kinamasi hicho hicho cha ulitima. Matokeo ni kwamba watoto wa matajiri wanaendelea kuelimika huku wa maskini wakibakia kwenye kiza cha ujinga. Wanaong’ang’ania kuwepo kwa elimu bila malipo kana kwamba waotandoto mchana.

    Hali ilivyo sasa hivi inadai kuwa mimi na wewe tufanye kazi hima tuungane mikono na kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu utekelezaji wa haki za watoto. Twapaswa kuhimiza serikali zetu kufanya kila ziwezavyo kuhakikisha kuwa watoto wote wako shuleni. Nasi tushirikiane kutoa huduma kwa watoto kukomesa dhuluma, mateso na dhiki kwao. Haitoshi kupeleka miswada bungeni kuhusu haki za watoto na kupitisha kuwa sheria. Twastahili kubadilisha misimamo yetu kuhusu haki hizi na kuzilinda kwa dhati.

    1. Huku ukitoa mifano minne, eleza hali ya kinyume inayojitokeza katika aya ya pili. (alama 4)
    2. Eleza namna hali ya usalama inavyoathiri utekelezaji wa haki za watoto kwa mujibu wa kifungu. (alama 3)
    3. Kwa kurejelea aya ya nne, onyesha mchango wa serikali katika kuwajibikia haki za watoto. (alama 3)
    4. –“Wanang’angania kuwepo kwa elimu bila malipo ni kanankwamba ni waota ndoto mchana.” Thibitisha kauli kwa kurejelea kifungu. (alama 2)

    5. Eleza maana ya misamiati ufuatao kama ulivyotumika katika taarifa. (alama 3)
      1. Vigogo ……………………………………………………….
      2. Huwa nanga kwao …………………………………………
      3. Kujikuna wajipatapo ………………………………………….

  2. UFUPISHO (alama 15)

    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Wataalamu mbalimbali wmekuwa wakifanya utafiti kuhusu Ziwa Viktoria. Juhudi hizi za uchunguzi zimekuwa zikionyesha kwamba ziwa hili ambalo ndilo la pili kwa ukubwa miongoni mwa maziwa mengine yenye maji matamu duniani linaangamia taratibu. Inakisiwa kuwa kukauka kwa ziwa hili kutahatarisha maisha ya wato zaidi ya milioni 30 ambalo hulitegemea kwa chakula na mapato. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Masuala ya Bahari na Uvuvi nchini ulionyesha kuwa Ziwa Viktoria linaangamia kwa kiasi cha mita tatu kila mwaka. Hivi sasa baadhi ya fuo zilizokuwa kwenye ziwa hili upande wa Kenya zimekauka. Mandhari ya fuo hizi nayo yameanza kutwaa sura mpya. Badala ya kpata madau na wavuvi wakiendesha shughuli zao katika maeneo haya, huenda isiwe maajabu kuwapata watoto wakicheza kandanda.

    Rasilimali za samaki ziwani humu zinaendelea kudidimia huku wavuvi wkitupwa kwenye biwila umasikini. Walisema wasemao kwamba akosaye la mama hata la mbwa huamwa. Wavuvi wamebuni mikakati ya kukabiliana na hali hii ambayo inatishia kukiangamiza kizazi chao. Wengi wao wameamua kufanya biashara maarufu kwa jina, ‘bodaboda,’ wengine wameingilia kilimo baada ya kushindwa kujikimu kimaisha kutokana na uvuvi. Wavuvi wanaoendelea kuvua samaki katika ziwa hili wamejipata katika hali ngumu ya kiuchumi. Hali hii imewalazimisha baadhi yao kuanza kuvua samaki katika maji ya mataifa jirani; jambo ambalo limewachongea, wengi wakitiwa mbaroni huku wengine wakinyanyaswa na maafisa wa usalama wa mataifa hayo majirani.

    Sekta ya uchukuzi na mawasiliano nayo imeathirika si haba, shughuzi za uchukuzi katika ziwa hili zimetingwa na gugu-maji ambalo limetapakaa kote ziwani. Mbali na gugu-maji hili, shughuli za kilimo za kunyunyuzia maji zimetanzwa. Kadhalika, kupungua kwa viwango vya maji humu ziwani ni changamoto nyingine ambayo inawashughulisha wanaharakati wa mazingira. Inahofiwa kuwa mataifa ya Afrika Mashariki yanalipoteza ziwa hili hatua kwa hatua. Hakika, wanasayansi wa masuala ya bahari wameonya kuwa ziwa hili litakauka katika kipindi cha karne ijayo!

    Ni dhahiri kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki ina jukumu la kulitunza ziwa hili kwa jino na ukucha. Serikali za nchi husika, hususan Kenya, Uganda na Tanzania zinapaswa kutekeleza sheria zinazodhibiti shughuli za uvuvi katika ziwa hili. Mathalan, kuna haja ya kuvua kwa misimu ili kukinga dhidi ya kuangamia kwa rasilimali za samaki. Wavuvi nao hawana budi kushauriwa kuhusu umuhimu wa kufuata kanuni za uvuvi zilizowekwa na kutahadharisha kuhusu madhara ya kuendesha uvuvi kiholelea. Sheria kuhusu aina za nyavu za kuvulia pia inapaswa kutekeleza vilivyo. Aidha, kuna haja ya serikali za muungano huu kukomesha shughuli za kilimo kandokando mwa ziwa hili, pamoja na kwenye mito iliyo katika ujirani wa ziwa lenyewe. Hatua hii itasaidia kukomesha kusombwa kwa udongo na mbolea kutoka mashambani hadi ziwani. Hali kadhalika, muungano huu unapaswa kuweka sheria za kusimamaia matumizi ya maji. Hili litawadhibiti raia wenye mazoea ya kubadhiri maji.

    Isitoshe, serikali za mataifa ya Afrika Mashariki hazina budi kuchunguza viwanda vinavyotupa taka ndani ya ziwa hili. Mbali na kuchafua maji, viwanda hivi vinaangamiza mimea na wanyama wa majini. Uchunguzi huo unapaswa pia kuhusisha mito inayomiminia maji katika ziwa hili. Viwanda vyote vinavyotumia maji ya mito kama vile: Nzoia, Yala, Sondu-Miriu, Awach, Kuja na Kagera vinastahili kuchunguzwa pia.

    Juhudi za kufikia ustawi wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki zinapaswa kutulia maanani uhifadhi wa Ziwa Viktoria. Kukauka kwa ziwa hili ni sawa na kukauka kwa maazimio na ndoto zote za serikali za nchi husika za kuboresha hali ya maisha ya raia wake. Wakati ni sasa.

    1. Fupisha aya tatu za kwanza kwa maneno 70 – 75. (alama 9, 1 ya mtiririko)
    2. Huku ukitumia maneno 50 -55, eleza masuala muhimu ambayo mwandishi anaibua katika aya ya tatu za mwisho. (alama 6, 1 ya mtiririko)

  3. MATUMIZI YA LUGHA: (alama 40)

    1. Huku ukitoa mifano, fafanua dhana ya mzizi wa neno. (alama 2)
    2. Onyesha matumizi ya kiambishi ‘ku’ katika sentensi ifuatayo:
      Amani atakutengenezea mpini wa jembe kisha aelekee kule kwao. (alama 2)

    3. Andika vitamkwa vyenye sifa zifuatazo: (alama 2)
      Irabu ya mbele, wastani …………………………………………….
      Kipasuo ghuna cha kaakaa laini …………………………………….

    4. Tumia kivumishi kionyeshi kisisitizi cha karibu pamoja na nomino ngeli ya YA – YA kutunga sentensi. (alama 2)
    5. Tunga sentensi moja katika wakati uliopita hali timilifu. (alama 2)
    6. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao: (alama 2)
      KN (N) + KT (T+E) + U + KN (N) + KT (T+E)
    7. Huku ukitoa mfano, eleza maana ya sentensi changamano. (alama 2)
    8. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya koga na konga. (alama 2)
    9. Tunga sentesi moja yenye nomino dhahania na nomino ya jamii. (alama 2)

    10. Nyambua vitenzi vifuatavyo katika kauli kauli zilizo kwenye mabano. (alama 3)
      1. Nywa (tendesha) ……………………………………………
      2. La (tendeana) ……………………………………………….
      3. Vaa (tendwa) ……………………………………………….

    11. Akifisha sentensi ifuatayo kubainishadhana tatu tofauti.
      Julius Kiptoo mwanawe Kung’u na Justine wlikiletea kijiji chao sifa. (alama 3)

    12. Ainisha maneno yaliyopigiwa mstari.
      Naam, ameleta machache. (alama 2)

    13. Tunga sentensi yenye kitenzi kishirikishi kikamilifu. (alama 2)
      1. Eleza maana ya shadda. (alama 1)
      2. Onyesha panapotokea shadda katika neno: ‘mteremko’. (alama 1)

    14. Andika visawe vya maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 2)
      Sahibu yake alishikwa na kisunzi.

    15. Bainisha virai vilivyopigiwa mstari.
      Ubaguzi wa kijinsia umekashifiwa na viongozi wenye msimamo thabiti mno. (alama 3)

    16. Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa.
      “Shughuli yetu itamalizika kesho,” mama aliwambia Juma. (alama 2)

    17. Bainisha kiima na chagizo katika sentensi ifuatayo:
      Watahiniwa hao walisoma maswali yote kwa makini. (alama 2)

    18. Ainisha sentensi ifuatayo kwa kuzingatia jukumu/dhamira yake.
      Funga majani matano matano kwa kila fungu. (alama 1)

  4. ISIMU JAMII (alama 10)

    Eleza kwa ufupi jinsi mambo yafuatayo yanavyodhibiti mitindo ya lugha.
    1. Mazingira (alama 4)
    2. Madhumuni (alama 2)
    3. Malezi (alama 4)


MARKING SCHEME

  1.  
    1.  
      • Watoto wananyimwa haki licha ya kuwa katiba inalazimu haki hizi kutimizwa.
      • Mojawapo ya haki za kimsingi ni makazi na hali watoto wanalala mitaani.
      • Watoto hawapati chakula na hali wanatakiwa kupata lishe bora.
      • Wanaotakiwa kulinda haki za watoto ndio wanaozikiuka kwa kuwapiga, n.k.
      • Wazazi na jamaa wa karibu wanashiriki katika unyanyasaji wa watoto.
        (4 x 1 = 4)
    2.  
      • Mataifa yasiyo na amani huchangia katika ajira ya watoto. Watoto kutumikishwa vitani.
      • Ghasia hupalilia utekaji nyara - watoto wanatekwa kwa lazima na kupelekwa vitani.
      • Watoto kuumbuliwa kwa kugeuzwa mababe wa vita.
      • Watoto kutengwa na familia zao.
      • Dhiki za kimwili na kisaikolojia kwa kuvishwa mavazi mazito na kubebeshwa bunduki nzito.
        (3 x 1 = 3)
    3.  
      • Kubuni sera/mpango wa elimu bila malipo.
      • Utekelezaji wa sera hii unaendelea.
      • Viongozi baada ya uhuru kubuni mpango / kuandika malengo ya kufikia elimu kwa wote
      • Kuna wanaopigania haki ya kuwa kwa elimu bila malipo licha ya matatizo yaliyopo. (Wanaong'ang'ania kuwepo kwa elimu bila malipo).
        (3 x 1 = 3)
    4.  
      • Asilimia ya watoto na watu wazima wasiojua kusoma bado ni kubwa.
      • Pengo la kielimu kati ya watoto wa matajiri na maskini bado inaendelea kuwa kubwa. 
      • Maskini hawamudu kushughulikia mahitaji ya kielimu ya wanao. 
      • Maskini bado wanalazimika kushughulikia mahitaji ya kielimu ya wanao.
      • Miswada inapelekwa bungeni na kupitishwa ila haki hazishughulikiwi kikamilifu.
        (2 x 1 = 2)
    5.  
      1. Vigogo - walio katika mstari wa mbele / mabingwa.
      2. Huwa nanga kwao - huwa mazito kwao.
      3. Kujikuna wajipatapo - kujaribu kujinyanyua kulingana na uwezo wao.
        (3 x 1 = 3)
  2.  
    1.  
      • Uchunguzi unaonyesha Ziwa Viktoria linaangamia polepole.
      • Kukauka kwa ziwa (inakisiwa) kutahatarisha maisha ya watu zaidi ya milioni 30 wanaolitengemea kwa chakula na mapato.
      • Utafiti wa Taasisi ya Masuala ya Bahari na Uvuvi ulionyesha ziwa linaangamia kwa mita mia tatu kila mwaka.
      • Fuo zimekauka upande wa Kenya.
      • Shughuli nyingine mbali na uvuvi zinaendelezwa.
      • Kupungua kwa rasilimali za samaki kunatishia kuangamiza uvuvi.
      • Wavuvi wameingilia biashara nyingine.
      • Wengine wanavua katika maji ya mataifa mengine na kuhatarisha usalama wao.
      • Gugu-maji limetatiza shughuli za uchukuzi na ukulima.
      •  Kupungua kwa kiwango cha maji-kunatishia kukauka kwa ziwa hili.
        (yaliyomo - hoja 8 x 1 = 8)
        Mtiririko = 1
        (alama = 9)
    2.  
      • Serikali za nchi husika (Afrika Mashariki) ziweke sheria za kudhibiti shughuli za uvuvi.
      • Wavuvi washauriwe kufuata kanuni za uvuvi zilizowekwa.
      • Serikali za muungano zikomeshe shughuli za kilimo kandokando mwa ziwa na kwenye mito jirani.
      • Sheria za kudhibiti matumizi mabaya ya maji ziwekwe.
      • Viwanda vinavyotupa taka humu vichunguzwe.
      • Juhudi za ustawi wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki zizingatie uhifadhi wa Ziwa Viktoria.
      • Ziwa likikauka maazimio na malengo ya serikali husika ya kuboresha hali ya maisha yanaangamia
        (yaliyomo - hoja 5 x 1 = 5)
        Mtiririko = 1
        (alama = 6)
  3.  
    1.  
      • Mzizi wa neno ni sehemu ya neno inayobeba maana ya kimsingi/maana ya kileksia ya neno. 
      • Sehemu hii haibadiliki hata neno likinyambuliwa / likiambishwa.
        mfano: som-a, gand-a, sahau-liw-a, ag - a kimbi-li-a, baba, kuku, tak - a
        Sehemu zilizopigiwa mstari ndizo mizizi ya maneno husika.
        Kueleza - 1. mfano 1 = alama 2

        Tanbihi

        Kuna mizizi huru (kama vile baba, mama, zuri, sahau) na mizizi tegemezi/funge (kama vile som katika soma). Mtahiniwa anaweza kutoa mfano wowote, mradi asadikishe anaelewa dhana ya mzizi.
    2. Atakutengenezea - nafsi ya pili (umoja) / mtendewa /yambwa tendewa (kitondo) -
      kule - mahali kusikodhihirika/kiambishi cha ngeli ya mahali. (Ku - Ku)
      (alama 1)
    3.  
      1. Irabu ya mbele, wastani. /e/  (alama 1)
      2. Kipasuo ghuna cha kaakaa laini. /g/   (alama 1)
    4. Marashi yaya haya / haya haya ndiyo aliyonunuliwa.
      Nomino nyingine: mate, maziwa, mafuta, mazingira n.k. (alama 2)
    5. Maisha yalikuwa yamemwendea vyema. (viambishi li, me) (alama 2)
    6. Mifano: -
      • Mandu huandika vyema lakini Kani huandika vibaya.
      • Maskauti walitembea kijeshi ila wanafunzi hawakuvutiwa kamwe.
      • Maria atasafiri kesho ilhali Zaina atasafiri mtondo.
      • Mwalimu alituita tena lakini Komu hakuitika katu.
      • Terry alielekea kushoto na Ndua alibaki katikati.

        Tanbihi 
               (alama 2/0)
        1. Hii ni sentensi ambatano.
        2. Mtahiniwa lazima abainishe muundo wa sentensi ambatano. (
        3. Mtahiniwa akikosa sehemu moja atuzwe sufuri (0).
        4. Aina yoyote ya kielezi inaweza kutumiwa mradi mtahiniwa abainishe mpangilio ufaao wa maneno.
        5. Viunganishi ambatani vitumiwe/asitumie viunganishi vitegemezi.
    7.  
      • Sentensi changamano huwa na kishazi kimoja huru na kingine kitegemezi.
      • Huweza kuwa na vishazi vyote viwili vitegemezi.
      • Vishazi huunganishwa kwa viunganishi vitegemezi kama vile, ikiwa, kama, ingawa, iwapo, ki, nge, ngali, ka virejeshi k.v. amba na 'o' rejeshi, nk. 
        Mifano
        1. Jamvi lililonunuliwa limechakaa.
        2. Usahihishaji ukimalizika mapema wanafunzi watapata matokeo.
        3. Wafanyakazi walijitahidi wakamaliza kazi mapema.
        4. Ingawa alikuwa maskini aliwaelimisha watoto wake wote.
        5. Mvua ingalinyesha mapema tungalipata mavuno bora.
        6. Kama unataka kumwona daktari njoo mapema.
    8.  
      1. Koga
        • uchafu
        • fanya maringo
        • ondoa uchafu mwilini kwa kutumia maji na sabuni
      2. Konga
        • kuzeeka
        • kunywa kinywaji/ maji ili kupunguza kiu
        • kusanya pamoja/ kukutanisha watu pamoja

          Tanbihi
          Mtahiniwa anaweza kutumia / kuibua maana yoyote mradi kila mojawapo ibainike katika sentensi.
    9.  
      • Nomino dhahania - utu, furaha, urembo, wepesi, wema, wivu. 1x1 = alama 1
      • Nomino ya jamii - Kikosi, mkungu, chane, funda, tano, darasa, mfano - darasa la wanafunzi, jeshi, kikosi, umati, halaiki, timu, jamii, familia, hadhira n.k.
        1x1 = alama 1
    10.  
      1. Nywa - nywesha/nywisha
      2. La - liana
      3. Vaa - valiwa
    11. Mifano 
      • Julius Kiptoo, mwanawe Kung'u na Justine walikiletea kijiji chao sifa. (Wahusika watatu)
      • Julius Kiptoo (mwanawe Kung'u) na Justina walikiletea kijiji chao sifa. (Wahusika wawili) (Julius Kiptoo ni mwana wa Kung'u)
      • Julius Kiptoo, mwanawe, Kung'u na Justina walikileta kijiji chao sifa. (Wahusika wanne). (mwanawe - mwana wa Julius Kiptoo au mtu mwingine)
      • Julius, Kiptoo (mwanawe Kung'u na Justina)walikiletea kijiji chao sifa. (Wahusika wawili). (Kiptoo ni mwana wa Kung'u na Justina)
        Tanbihi
        1. Huu ni mfano wa sentensi tata.
        2. Lazima dhana tatu zijitokeze.
        3. Mtahiniwa si lazima / hahitajiki kuelezea maana, viakifishi vinatosha.
    12. Naam-kihisishi
      Machache - kiwakilishi / kiwakilishi cha idadi ya jumla.  (alama 1)
    13.  
      • Muli alikuwa mwalimu wetu.
      • Huyu anaonekana mzima.
      • Teddy amekuwa mpole.
      • Swali limetuwia gumu.     (alama 2)
        (Kitenzi kiwe na kiambishi nafsi au cha ngeli na cha wakati au cha hali)
    14.  
      1. Shadda ni mkazo unaotiwa katika neno au silabi wakati wa kutamka (alama 1)
      2. m-te-re-'m-ko
        Tanbihi
        • Mkazo utiwe kwenye silabi ya pili kutoka mwisho wa neno.
        • Si lazima atenge silabi.
        • Anaweza kupigia mstari
    15. Sahibu - rafiki/mwandani                 (alama 1)
      Kisunzi - kizunguzungu/ kisulisuli        (alama 1)
    16.  
      • wa kijinsia - kirai (ki) husishi (neno kuu ni kihusishi 'wa')    (alama 1)
      • viongozi wenye msimamo (kirai nomino) (neno kuu ni nomino: viongozi) (alama 1)
      •  thabiti mno - kirai(ki) vumishi (neno kuu ni kivumishii thabiti   (alama 1)
        Tanbihi
        • Uainishaji ufanywe kimuundo wala si kimajukumu. Kwa mfano, 'wa kijinsia ni kirai husishi wala si kirai vumishi, japo kinafanya kazi kama kivumishi.
    17. Mama alimwambia Juma kwamba shughuli yao ingemalizika siku ambayo ingefuata. (alama 2/0)
    18.  
      • kiima - watahiniwa hao   (alama 1)
      • chagizo - kwa makini   (alama 1)
        Tanbihi
        • Kiima ni sehemu ya sentensi ambayo ndiyo habari zake zinatolewa katika kiarifu cha sentensi. Aghalabu huwa kikundi nomino ambacho hutokea kabla ya kitenzi, na kwa kawaida huwa ndicho mtenda katika sentensi.
        • Chagizo ni sehemu ya sentensi ambayo huja baada ya kitenzi au yambwa. Huwa kielezi/kirai elezi au hata kirai husishi ambacho kinafanya kazi kama kielezi. Ni sehemu ya ziada katika sentensi na huweza kuondolewa bila kuathiri maana ya kimsingi ya sentensi.
    19. Sentensi agizi/amrishi/ amri 
      (inatoa maagizo / maelekezo)     1x1 = 1
  4.  
    1. Mazingira
      • Mzungumzaji huchota msamiati kutoka mahali anapozungumzia. Kwa mfano, atatumia msamiati wa sokoni akiwa sokoni. Pia kuna lugha ya mahakamani, kwenye mazishi, maabadini n.k. - Mazingira huathiri kiimbo na hata kidatu. Kwa mfano, mtu akiwa darasani huzungumza kwa kidatu cha chini.
      • Mazingira huathiri uteuzi wa msimbo/lugha/lahaja ambayo mtu anatumia. Kwa mfano, mazingira rasmi humtaka mtu kutumia lugha rasmi kama vile Kiingereza na Kiswahili sanifu.
      • Mazingira hudhibiti kiwango cha usanifu na urasmi wa lugha. Kwa mfano, mazingira yasiyo rasmi hayahitaji kutumia lugha yenye urasmi au usanifu, mtu anaweza kutumia hata simo/misimu.
      • Mazingira hudhibiti mtindo nafsi wa mtu. Kwa mfano, mtu katika mnada au biashara ya rejareja huweza kujirudiarudia ili kuwavutia wateja.
      • Ishara anazotumia mtu hudhibitiwa na mazingira. Zipo ishara nyingine za uso au hata miondoko ambayo haikubaliwi/ni mwiko katika baadhi ya tamaduni / mazingira.
      • Mtu anayeishi katika mazingira magumu / makali / ya unyanyasaji huelekea kutumia lugha kali au pengine ya matusi, pengine ili kujihami.
        4x1 = 4
    2. Madhumuni
      • Lengo la mawasiliano huathiri jinsi mtu anavyotumia lugha. Kwa mfano, mtu anapoonya hutumia lugha yenye toni kali. Anapotaka kushawishi hutumia lugha ya upole.
      • Madhumuni huathiri uteuzi wa msimbo/lahaja/lugha, Kwa mfano, kiongozi anapotaka kuonyesha utangamano na mwanakijiji mwenzake huelekea kutumia lugha ya mama badala ya Kiingereza au hata Kiswahili. Kiongozi huyo huyo huelekea kutumia Kiingereza anapotaka kumtenga mwanakijiji mwenzake.
      • Madhumuni huathiri kiimbo na shadda. Mtu anapotaka kusisitiza jambo hutia shadda kwenye maneno, au dhana anazotaka kusisitiza. Wakati mwingine hupandisha sauti ili kuwiana na hali ya msisitizo.
        2 x 1 = 2
    3. Malezi
      • Mtoto aliyelelewa kwa kudhibitiwa huinukia kutoweza/kutomudu kujieleza vyema kwa sababu ya woga aliojazwa.
      • Mtoto aliyelelewa katika mazingira ya unyanyasaji hutumia lugha kali ya kujihami.
      • Mtoto akilelewa na wazazi wnaozungumza lugha mbili zaidi ya mbili huweza kujifunza / kutumia lugha zote mbili.
      • Mtoto aliyelelewa akihimizwa kujieleza huinukia kuwa na uwezo/ukakamavu wa kujieleza. - Mtoto asipofunzwa lugha ya mama hushindwa kujieleza kwa lugha hiyo.
      • Mtoto hufunzwa kuepuka matumizi ya msamiati/lugha ya aibu/kali, kwa hivyo kutoitumia katika mazungumzo.    4x1

        Tanbihi
        Sheria na kaida zote za usahihishaji wa karatasi hii zitumike.
Join our whatsapp group for latest updates

Download KCSE 2012 Kiswahili Paper 2 with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Read 5347 times Last modified on Monday, 08 November 2021 06:21

Related items

Get on WhatsApp Download as PDF