Print this page

Kenya Certificate Of Secondary Education(KCSE 2013) Kiswahili Karatasi ya Pili with Marking Scheme

Share via Whatsapp
  1. UFAHAMU (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Gari lake kuukuu lilikuwa linapambana na barabara yenye mashimo yaliyoshiba na kutapika maji ya mva ambayo sasa ilikuwa inaanza kupusa. Japo daima alipambana na usukani kunako mashimo haya yaliyotosha kuitwa magenge, alishukuru kwa hali hii. Vipi angeweza kulidhibiti gari lake hili kwenye barabara iliyosakafiwa nayo ikahitimu? Magurudumu haya yaliyong’ara kama upara wa shaibu aliyekula chumvi hadi ikamwogopa yangetii uelekezi wake? Mara ngapi gari hili limetaka kumwasi barabarani? Haya yalikuwa baadhi ya maswali yaliyompitika akilini. Hakujitakalifu kutaka kuyapa mji maana mara ile mawazo yake yalitekwa na kubwagwa katika nchi ya mbali – nchi ambayo aliiona kama sinema akilini mwake.

    Alipofika nyumbani, aliliegesha gari lake na kufululiza ndani. Siku mbili zilikuwa zimepita akiwa pale kazini. Madaktari kama yeye hawakuwa wengi. Aalikuw amiongoni mwa madaktari wenye ujuzi katika hospitali hii ya kitaifa. Wenzake wengi walikuwa wamehamia ughaibuni wlikokwenda kutafuta maisha. Mshahara wao wa mkia wa mbuzi uliwasukuma na kuwatema nje ya nchi yao. Wengi wa waliohamia ng’ambo waliona vigumu kubaki katika ajira ambayo kivuno chake kilishindwa kumvusha mtu hata nusu ya kwanza ya mwezi. Malalamisha ya kulilia ujira wa heshima yaligonga kwenye masikio yaliyotiwa zege. Na kweli wanavyosema, mwenye macho haaambiwi tazama. Basi wlitazama hapa na pale wakaona penye mianya na matumaini, nao wakaiandama.

    Hadi leo hii hamna la mno lililofanyiika. Ndiyo maana Daktari Tabibu anarudi nyumbani tangu kuingia kazi hiyo juzi alfajiri. Hafanyi kwa kuwa katosheka, maana pia yeye ana dukuduku. Ana shaka ya mustakabali wake ikiwa mazingira ni haya ya kumsoza, maana umri nao unazidi kumla. Japo anatia na kutoa, mizani ya hesabu yake imeasi ulinganifu.

    Daktari Tabibu waama ni mfungwa. Ametekwa na kuzuiwa katika kupenda na kuchukia mambo. Ni kama mti uliodumaa. Anatamani barabara nzuri za lami. Anatamani mshahara wa kuwezesha kukidhi mahitaji yake na kutimiza majukumu yake ya kimsingi. Jana amesema na rafiki yake aliye ng’ambo kwa simu ambayo sasa imetulia mkabala naye. Ingawa mwenzake huyu alikuwa mchangamfu na kumdokolea hali ya maisha kuridhisha kule ugenini kama vile wanataaluma kuenziwa, yapo vilevile yaliyomtia unyonge moyoni. Upweke ndio uliomtia fukuto kuu. Licha ya hela zote hizo za kupigiwa mfano, watu hawana muda wa kutembeleana na kujuliana hali au hata kukutana tu mkahawani wakashiriki mlo. Eti kila mtu na hamsini zake. Halafu ipo changamoto ya hali ya hewa. Baridi ya ng’ambo haifanyi mzaha katika kumtafuna mtu. Ni hali tofauti na ile aliyoizoea.

    Daktari Tabibu alizitia kauli za rafiki yake kwenye mizani ya moyo wake. Akawaza ikiwa kweli si bora kulemazwa na mzizimo ugenini badala ya kuishi katika kinamasi cha kuumbuliwa nyumbani. Kisha punde lilimjia wazo la marehemu nyanyake na wengine kama yeye waliofadhili masomo yake kupitia kwa serikali na kwa njia ya kodi. Je, ni usaliti huu? Vipi aikimbie nchi kabla ya kuihudumia ilhali imemjenga hadi kuwa daktari? Na je, wafanyakazi wake wa nyumbani watakwenda wapi? Atawaambiaje kuwa sasa ahitaji huduma zao kwa kuwa anakimbia nchi yake?

    Mawazo yake yalikatizwa na simu iliyolia na kumshtua. Alipolitazama aliiona imeng’ara kwa mwangaza ulioweka wazi jina la mpigaji. Alifahamu kuwa leo hii tena dharura nyingine ilikuwa inamwalika hospitalini. Mwili wake ulimsaliti ingawa moyo wake lilimkumbusha kuwa lisilobudi hutendwa. Hapo ndipo alipoiinua ile simu tayari kusem ana mwenzake upande wa pili.

    “Haloo!” Sauti nyororo kutoka upande wa pili iliita.
    “Haloo!”
    “Naam! Dharura nyingine tena daktari. Unaombwa kuokoa maisha mengine tena!”
    “Haya. Ila mawazo ninahitaji kujimwagia maji”, na pale pale akaikata ile simu.

    Daktari Tabinu aliingia hamamuni huku kajifunga taulo kiunoni tayari kuoga. Aliyafungulia maji lakini ule mfereji uligoma kutapika maji. Ulikuwa umekauka kabisa. Daktari Tabibu aliduwaa pale. Aliufunga ule mfereji kabla ya kuiaga bafu.
    1. Eleza sababu nne zinazowafanya wataalamu kuhamia nchi za nje. (alama 4)
    2. “Hakuna masika yasiyokuwa na mbu.” Thibitisha kauli hii kwa kurejelea hali ya waliohamia ng’ambo. (alama 3)
    3. Fafanua athari tatu zinazoikumba nchi ya msimulizi kutokana na uhamiaji ng’ambo wa wataalamu. (alama 3)
    4. Eleza mchango wa teknolojia kwa kurejelea kifungu. (alama 3)
    5. Eleza maana ya msamiati ufuatao kulingana na taarifa.(alama 2)
      1. Kuyapa maji
      2. Fukuto
  2. UFUPISHO: (alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Wakenya walipoipitisha katiba mpya waliiadhinisha mfumo wa ugatuzi. Katika mfumo huu, mamlaka ya serikali kuu katika uongozi, usimamizi na utumiaji wa rasilimali za nchi hupunguzwa. Kiasi fulani cha mamlaka hutwaliwa na maeneo ya ugatuzi. Suala hili halikuzinagtiwa katika katiba ya awali ambapo mamlaka yote yalikuwa mikononi mwa serikali kuu. Kutokana na upana na wingi wa maeneo nchini, iliiwia vigumu serikali kuu kuhakikisha kwamba kulikuwa na usawa wa kimaendeleo katika sehemu zote nchini.

    Kwa mujibu wa katiba mpya, serikali kuu haina budi kuyasaidia maeneo yote ya ugatuzi ili yaweze kujinyanyua kiuchumi na kuboresha hali zamaisha za wakazi wake. Vilevile ni jukumu la kila eneo la ugatuzi kuweka mikakati madhubuti ili kuchunguza na kubainisha rasilimali zote katika meneo husika. Hili litasaidia kuvumbua rasilimali ambazo zinaweza kuchangia katika ustawishaji wa maeneo haya. Maeneo haya pia yanatakiwa kutafuta mbinu zinazofznikisha uzalishaji au utumiaji wa rasilimali hizi kwa njia endelevu. Mojawapo ya hizi mbinu ni uongezaji thamani katika rasilimali yoyote inayozalishwa kwenye eneo mahususi.

    Maeneo mengi ya ugatuzi nchini humu yanategemea kilimo cha ufugaji kama mhimili wa uchumi. Licha ya kuwa nguzo, kilimo hiki hakijawahi kupigwa darubini vizuri kwa lengo la kukiimarisha ili kiwanufaishe wenyeji kikamilifu. Aghalabu wafugaji wengi huandama mbinu za jadi za ufugaji ambazo haziwahakikishii ongezeko la mapato. Isitoshe, wafugaji hawa wanakabiliwa na tatizo katika soko la mifugo ambapo wengi hupunjwa na matapeli. Pamoja na haya, baadhi ya wakazi huuza mifugo nje ya nchi wakiwa wazimawazima bila kuwazia matokeo ya kitendo hiki. Si ajabu kuwaona ng’ombe, ngamia, mbuzi na kondoo wakipakiwa kwenye malori na kusafirishwa nje ya nchi. Ukweli ni kwamba jambo hili ni hatari sana, si kaw uchumi wa maeneo husika tu, bali pia kwa Kenya kwa jumla. Hii ni kwa kuwa walionunua mifugo wazimawazima wanaweza kuhiari kutowachinja na badala yake kuwatumia kama mbegu za kuzalisha mifugo wao. Hapa pana hatari ya maeneo haya kupoteza wateja kwani baada ya muda huenda wanaonunua mifugo wakajitosheleza na kukosa kuja kuwanunua mifugo wengine. Hali ikiwa hvyo, maeneo yaliyotegemea soko hili huenda yakalipoteleza taratibu, na bila shaka kupoteza natija inayotokana na soko lenyewe.

    Ili kudhibiti hali hii, itakuwa bora ikiwa viwanda vya kuchinjia mifugo na kupakia nyama vitajengwa katika maeneo haya ya ugatuzi. Hili litawezesha wakazi kuuza nyama badala ya kuuza mifugo wazimawazima. Fauka ya haya, maeneno haya yatajikinga dhidi ya kupoteza bidhaa zinazotokana na mifugo. Hizi ni kama vile ngozi, kwato na pembe bila shaka zina natija kuu. Ngozi kwa mfano, ni bidhaa muhimu sana katika sekta ya utengenezaji wa mavazi na mifuko. Viwanda vinavyotumia ngozi kama malighafi vikijengwa katika maeneo haya, wakazi wake watanufaika si haba. Mathalani, viwanda vya kutengenezea viatu, mishipi, mifuko na nguo vikianzishwa, wawekezaji watalazimika kuanzisha viwanda vingine vitegemezi. Kadhalika ni dhahiri kwamba bidhaa zinazotokana na ngozi huhitaji kutiwa nakshi. Kuanzishwa kwa viwanda hivi basi kutazua haja ya kuanzishwa kwa viwanda vya kutengenezea rangi, pamoja na maduka ya kuuza bidhaa yenyewe. Isitoshe, gundi ya kugandisha bidhaa hizi itahitajika, hivyo kusababisha haja ya kuanzishwa kwa kiwanda cha gundi. Matokeo ya shughuli hizi zote ni kuzalishwa kwa nafasi anuwai za kazi kwa wakazi. Hili litakuwa na matokeo zaidi chanya, hususan kwa vijana. Badala ya kushiriki ulevi na burudani zinazowahatarisha, wataweza kujitafutia riziki kwa viwanda hivi.

    Juu ya hayo, mfumo wa ugatuzi utayawezesha maeneo husika kugezea thamani utoaji wa huduma za kijamii na kuitawala kulingana na mahitaji ya maeneo haya. Ni muhimu hata hivyo kuzingatia kwamba kila eneo la ugatuzi lina upekee wake, nao vipaumbele hutofautiana kulingana na maeneo. Kuna yale ambayo yanasisitiza usalama, mengine ujenzi na uimarishaji wa miundomsingi kama vile barabara, vituo vya afya na hata taasisi za elimu. La muhimu ni wakazi wa maeneo husika kubainisha ni lipi litatekelezwa kwanza.

    Kinga na kinga ndipo moto uwakapo. Kufanikiwa kwa mfumo wa ugatuzi kutategemea juhudi za kila mkazi wa eneo husika. Ni muhimu kila mkazi kujiona kuwa mmiliki wa eneo zima la ugatuzi na kuwajibika katika kuliendeleza kwa hali na mali. Uwajibikaji huu unajumuisha uteuzi wa viongozi wenye muono mzuri na ambao watawawezesha kuyafikia malengo yao ya kimaendeleo. Hakika, mustakabali na uwepo wa eneo la ugatuzi utakuwa zao la maamuzi ya wanaeneo. Vilevile ufanisi wa maeneo ya ugatuzi utakuwa msingi wa ufanisi wa taifa kwa jumla.
    1. Fupisha ujumbe wa aya ya tatu kwa maneno 85-90. (alama 8, 1 ya mtiririko)
    2. Kwa kutumia maneno 75-80, bainisha masuala ambayo mwandishi anaibua katika aya tatu za mwisho. (alama 7, 1 ya mtiririko)
  3. MATUMIZI YA LUGHA: (Alama 40)
    1.        
      1. Eleza maana ya sauti mwambatano. (alama 2)
      2. Andika sauti mwambatano inayotamkiwa kwenye ufizi. (alama 1)
    2. Andika sentensi ifuatayo upya ukibadilisha neno lililopigiwa mstari kuwa kielezi.
      Komu ameshona nguo nzuri na kuiuza sokoni. (alama 1)
    3. Tunga sentensi mojamoja kubainisha; (alama 4)
      1. Kihusishi cha wakati
      2. Kivumishi cha pekee chenye maana, “bila kubagua.”
    4. Andika sentensi ifuatayo kwa hali yakinishi.
      Askari wasipopiga doria au kushirikiana na raia hawatakuwa wametuhakikishia usalama. (alama 2)
    5. Bainisha mofimu katika neno:
      Atamnywea (alama 3)
    6. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya udogo.
      Madebe hayo yatasafirishwa pamoja na nyundo hizi. (alama 2)
    7. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo;
      Ingawa mshahara wake si mkubwa anaikimu familia yake. (alama 2)
    8. Tunga sentensi tatu ukionyesha matumizi matatu tofauti ya kiambishi ‘li’. (alama 3)
    9.        
      1. eleza maana ya sentensi ya masharti. (alama 1)
      2. Tunga sentensi ya masharti. (alama 2)
    10. Tumia kiwakilishi cha ‘a ‘ unganifu katika sentensi kuonyesha:
      1. Umilikaji (alama 2)
      2. Nafasi katika orodha au nafasi katika kundi. (alama 2)
    11. Tunga sentensi yenye kikundi tenzi chenye muundo ufuatao:
      Kitenzi kisaidizi. Kitenzi kikuu, nomino (alama 2)
    12. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili tofauti ya kistari kirefu. (alama 2)
    13. Unganisha sentensi zifuatazo kwa sentensi moja bila kurudia kitenzi.
      Osore amempigia Ngungui simu. Ngungui amempigia Osore simu. (alama 2)
    14. Andika upya sentensi ifuatayo ukibadilisha vitenzi vilivyomo kuwa nomino:
      Mayaka anapotumbuiza huchekesha sana. (alama 2)
    15. Andika maana tatu ya neno: kanda. (alama 3)
    16. Andika visawe viwili vya nahau: enda kombo. (alama 2)
  4. ISIMU JAMII (Alama 10)
    Soma makala haya kisha ujibu maswali. 

    Haya ng’ara … Ng’ara leo! Nguo motomoto. Ng’ara leo kwa bei rahisi. Hamsini hamsini shati. Kuona ni bure. Bure kwa bure. Shika mwenyewe ujionee. Bei nafuu. Bei ya starehe. Haya haya. Usikose mwanangu! Hamsa! Fifty! Hamsa! Fifty! Hamsa na nyingine.
    1. Bainisha sajili ya mazungumzo haya. (alama 2)
    2. Eleza sifa nane za sajili hii kwa kurejelea kifungu hiki. (alama 8)


MARKING SCHEME

  1. Ufahamu
    1.        
      1. Kuharibika kwa miundomsingi/barabara mbovu
      2. Mishahara duni
      3. Malalamishi yao kutosikilizwa
      4. Kutothaminiwa kwa utaalamu
      5. Kukosa huduma za kimsingi k.v. maji
      6. Kuvutiwa na maisha ya kuridhisha huko ng’ambo
      7. Kutokuwa na matumaini ya mustakabali mwema nchini.
        4 x 1 - alama 4
    2. Masika ni hali nzuri au manufaa.
      Ng’ambo kuna maisha ya kuridhisha kama vile kuthaminiwa kwa wanataaluma.
      1x1 - alama 1
      Hata hivyo, kuna dosari zifuatazo:
      1. Upweke
      2. Ubinafsi
      3. Baridi
        2x1
        (Jumla - alama 3)
    3.    
      1. Umma kutofaidika kutokana na huduma za wataalamu wake licha ya kuwafadhili
      2. Kuwaachia mzigo wa kazi wataalamu wachache waliobaki
      3. Kuwapoka riziki wafanyakazi, k.v. walioajiriwa na wataalamu hawa
      4. Kulazimika kufanya kazi kwa saa nyingi, kama vile Dkt. Tabibu
        3 x 1 - alama 3
    4.    
      1. Huwezesha kuwasiliana na jamaa walio mbali, kwa mfano, Daktari na rafiki yake wanawasiliana kwa simu.
      2. Huwezesha kuwafikia watoaji huduma patokeapo dharura, kwa mfano Daktari anapigiwa simu nyumbani.
      3. Hurahisisha usafiri - gari la Daktari.
      4. Hurahisisha kupata huduma ya karibu ya maji- bomba la maji nyumbani kwa
        Daktari.
        3 x 1 - alama 3
    5.       
      1. Kuyapa mji - kuyawazia/kuyapa nafasi ya kuyajibu
      2. Fukuto - wasiwasi/mashaka/dukuduku/kutokuwa na utulivu/hamaniko
        2 x 1 - alama 2
  2.    
    1.      
      1. Katiba mpya iliidhinisha mfumo wa ugatuzi ambao hupunguza mamlaka ya
      2. serikali kuu katika usimamizi wa rasilimali.
      3. Eneo la ugatuzi hutwaa kiasi fulani cha mamlaka.
      4. Ugatuzi utahakikisha usawa wa kimaendeleo nchini kinyume na awali.
      5. Serikali isaidie maeneo yote kujiimarisha.
      6. Maeneo yaweke mikakati ya kutafiti na kubainisha rasilimali/zilizomo.
      7. Kuvumbua rasilimali mwafaka kutasaidia ustawi.
      8. Wanamaeneo watafute mbinu za kuongezea thamani rasilimali.
      9. Kilimo cha ufugaji ni nguzo ya maeneo mengi na kinahitaji kuimarishwa kwa kuandama mbinu za kisasa za uzalishaji.
      10. Ipo haja ya wanaeneo kukabiliana na matatizo yanayohusiana na soko ili kukinga dhidi ya kupoteza wateja.
      11. Ipo haja ya kujenga viwanda vya kuchinjia mifugo na kupakia nyama.
      12. Baadhi ya wafugaji huhasirika kwa kuuza mifugo wazimawazima.
      13. Wafugaji wengine hutapeliwa.
        7x1=7
        Mtiririko = 1
        alama - 8
    2.    
      1. Ujenzi wa viwanda vya kuchinjia na kupakia nyama utakinga dhidi ya kupoteza bidhaa zinazotokana na mifugo.
      2. Kujenga viwanda hivi kunasababisha ujenzi wa viwanda tegemezi.
      3. Hili litawezesha kuzalisha nafasi za kazi.
      4. Kutakuwa na kuongezea thamani utoaji wa huduma za kijamii na kiutawala.
      5. Kuzalisha nafasi za kazi kwa vijana kutasaidia kuwaadilisha vijana zaidi.
      6. Kila eneo lina vipaumbele tofauti; wakazi wabainishe kipaumbele chao.
      7. Ugatuzi unahitaji ushirikiano.Kila mwanaeneo awajibikie maendeleo ya eneo.
      8. Wanaeneo washiriki kuteua viongozi wenye muono mzuri.
      9. Ufanisi katika maeneo ya ugatuzi utachangia katika ufanisi wa taifa kwa jumla.
        6x1=6
        Mtiririko = 1
        (alama = 7)
  3.    
    1.      
      1. Sauti mwambatano ni sauti mbili au zaidi zinazotamkwa kama sauti moja (k.v.
        konsonanti na kiyeyusho. Kwa mfano /tw/
        Au
        Sauti moja ambayo ni muungano wa sauti mbili au zaidi. Kwa mfano konsonanti mbili au tatu. Kwa mfano,/nd/ mb/ ngw/
        1 x 2 - (Alama 2)
        Au
        Sauti ambayo huundwa kwa konsonanti mbili au tatu zinazotamkwa kama sauti moja, kwa mfano, /ndw/ katika ndwele,ngw/katika jangwa
      2. mf: / nd/ - katika unda
        / nz/ - katika mwanzo
        / tw/ - katika twalika
        / nw/ - katika shonwa
        /zw/ - katika tuzwa
        /sw/ - katika naswa
        /ndw/ - katika undwa
        1x1 - (Alama 1)
        Mtahiniwa atumie kielezi cha namna kama ifuatavyo.
    2. Komu ameshona nguo vizuri na kuiuza sokoni
      au
      Komu aliuza nguo sokoni baada ya kuishona vizuri.
      (Alama 2)
    3.      
      1. Watumie kihusishi cha wakati kama vile, kisha, tangu, halafu, kabla ya, hadi, mpaka, kwa, hata, kufikia, kuanzia. Mfano:
        Amekuwa hapa tangu asubuhi.
        Aliwasili halafu akaondoka.
        (Alama 1)
      2. Watumie mzizi - o - ote pamoja na nomino / viwakilishi katika ngeli mbalimbali.
        Kwa mfano: Mwalimu alitaka kumtuma mtoto yeyote.
        Nzi hula kitu chochote.
        Hakuweza kula tunda lolote. n.k
    4. Askari wakipiga doria na kushirikiana na raia watakuwa wametuhakikishia usalama.
      (Alama 2)
      (Alama 3)
    5. ....
    6. Videbe hivyo vitasafirishwa pamoja na vijundo hivi.
      au
      Vijidebe hivyo vitasafirishwa pamoja na vijijundo hivi.
      2x1 - (Alama 2)
    7.      
      1. Ingawa mshahara wake si mkubwa - tegemezi
      2. anaikimu familia yake - huru
        2x1 (Alama 2)
    8. Matumizi ya ‘Kiambishi ‘li’
      1. Kiambishi cha wakati uliopita - Musa alitutembelea.
      2. Kiambishi cha ngeli - Tunda liliiva
      3. Kiambishi cha kauli tendea - Yule alikukimbilia au Mtoto amekalia kigoda.
        3 x 1 (Alama 3)
    9.      
      1. Ni sentensi inayoonyesha kutegemeana kwa matendo au hali. (Alama 1)
      2. Watumie viambishi na maneno yanayoonyesha kuwa kufanikiwa au kutofanikiwa kwa tukio au tendo moja kunategemea kufanikiwa kwa tukio au tendo lingine. kwa mfano: nge, ngali, ki, kama, iwapo n.k.
        1. Wanafunzi wangefika mapema wangempata mwalimu.
        2. Kotu angalisoma kwa bidii angalifaulu.
        3. Mvua ikinyesha mapema tutapata faida.
        4. Iwapo unataka ufanisi jibidiishe.

          Tanbihi
          Mtahiniwa anaweza kuandika katika hali kanushi kama ville:
        5. Mkulima asingalipanda mapema asingalipata mazao mengi.
        6. Huyu asipojihadhari ataharibikiwa.
        7. Iwapo hutaanza safari mapema utachelewa.
        8. Kama utaanza shughuli mapema hutatatizika.
        9. Lazima asome kwa bidii ili afanikiwe
          (Alama 2)
    10.      
      1. La Katunda linapendeza.
        Au
        Tindi anataka cha mwenziwe.
      2. Atumie viwakilishi vya idadi halisi vinavyotumia a - unganifu. Kwa mfano:
        Wa tatu atatuzwa shaba.
        Au: Mwalimu anamuita wa nne.
        1x2 - (Alama 2)
    11. Mifano ifuatayo au zaidi inaweza kujitokeza.
      Kairu hajawahi kupalilia mtama.
      TS T N
      Au
      Huyu ataweza kukupa ufadhili.
      TS T N
      Au
      Wanafunzi hawa wangali wanafanya mtihani.
      TS T N
      Au
      Musa alikuwa anawafundisha wanawe.
      TS T N
      1x2 - (Alama 2)
      alama 2/0
    12.      
      1. Hutumiwa kutilia mkazo maelezo/kutoa maelezo zaidi/kufafanua au kuonyesha kusisitiza. Kwa mfano:
        Alinunua matunda — maembe, machungwa na matango.
      2. Hutumiwa kuonyesha kubadilika kwa maoni. Kwa mfano:
        Waite wale — hapana, hawa.
      3. Kuonyesha msemaji/usemi halisi, kwa mfano
        Utengano ni udhaifu duma
        2x1 (Alama 2)
    13. Sentensi ibainishe kauli au hali ya kutendeana. Osore na Ngungui wamepigiana simu.
      Au
      Osore and Ngungui wamepigania simu
      1x2 (Alama 2)
    14. Utumbuizaji wa Mayaka una ucheshi mwingi/sana.
      Au
      Kutumbuiza kwa Mayaka kuna ucheshi mwingi/sana.
      Au
      Kutumbuiza kwa Mayaka kuna kuchekesha kwingi/sana.
      1x2 - (Alama 2)
    15. Kanda
      1. kutomasa
      2. eneo
      3. aina ya mfuko
      4. mtu asiyeaminika/laghai/ayari
      5. wingi wa ukanda/mshipi
      6. malipo kwa mganga
      7. makasia ya kuogelea
      8. utepe/mshipi unaotumiwa kunasia sauti/picha
      9. mtu asiyesimika/hanithi 3 x 1 (Alama 3)
    16.      
      1. enda mvange
      2. enda upogo
      3. enda segemnege
      4. enda arijojo
      5. enda mrama
      6. enda benibeni
      7. enda shoro
      8. enda tenge 2 x 1 (Alama 2)
  4. Isimujamii
    1. Biashara/sokoni/kunadi au kutangaza bidhaa (Alama 2)
    2.      
      1. Matumizi ya chuku - kuona ni bure, bure kwa bure, bei ya starehe
      2. Urudiaji - ng’ara, ng’ara, haya haya
      3. Matumizi ya misimu ya biashara kama vile: nguo motomoto hamsa, ng’ara,
      4. Lugha shawishi - shika mwenyewe ujionee, usikose mwanangu, bei nafuu
      5. Kauli fupifupi - kuona ni bure, bei nafuu
      6. Lugha nyepesi - kifungu chaeleweka bila tatizo.
      7. Kuchanganya ndimi - fifty fifty/Hamsa fifty
      8. Matini huwa fupi. Tangazo hili ni fupi.
      9. Kuzungumza na mteja moja kwa moja - Haya ng’ara, usikose mwanangu.
      10. Kutumia mafumbo ambayo huenda yasieleweke na asiyekuwa na makini.
        mf. Hamsa fifty/Hamsa na nyingine - kumaanisha mia, wala si hamsini.
      11. Kujinasibisha au kujitambulisha na mteja. Mtangazaji anamwita mnunuzi mwanangu ili kujenga ukuruba baina yao, hivyo kumvutia.
      12. Matumizi ya porojo - bure kwa bure, bei ya starehe.
        8x1 alama 8

        Tanbihi
        1. Masharti yote ya usahihishaji wa karatasi ya pili yazingatiwe.
        2. Ni muhimu mtahini kuwa makini kufasiri ipasavyo majibu ya watahiniwa asije akawahini.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kenya Certificate Of Secondary Education(KCSE 2013) Kiswahili Karatasi ya Pili with Marking Scheme.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Read 3707 times Last modified on Tuesday, 09 November 2021 13:13

Related items

Get on WhatsApp Download as PDF