KISWAHILI PAPER REPORT - KCSE 2017 REPORTS

Share via Whatsapp

3.2 KISWAHILI (102)



3.2.1 Utangulizi

Matokeo ya mtihani wa Kiswahili, hasa ya karatasi ya pili na ya tatu, yamekuwa yakiyumba mwaka baada ya mwingine tangu kuanzishwa kwa mtaala mpya. Watahini wamekuwa wakishuhudia kushuka kwa viwango vya majibu yanayotolewa na watahiniwa. Kadhalika, kumekuwa na kushuka na kupanda kwa asilimia ya watahiniwa wanaotuzwa gredi za juu. Uchanganuzi huu unanuiwa kutathmini utendaji wa watahiniwa katika karatasi mahususi, na katika somo la Kiswahili kwa jumla. Jedwali lifuatalo linaonyesha matokeo ya mtihani wa somo la Kiswahili katika kipindi cha miaka sita (2012 hadi 2017).

Jedwali 10: Matokeo ya mtihani wa Kiswahili (2012 - 2017)

Mwaka Karatasi Watahiniwa Upeo Alama ya Wastani Alama Tenganishi
2012 1
2
3
Jumla
433,886



40
80
80
200
10.43
29.06
32.14
71.62

3.63
10.77
15.15
25.71

2013 1
2
3
Jumla
445,555



40
80
80
200
18.46
29.92
34.82
83.19
5.44
12.68
14.92
29.77
2014 1
2
3
Jumla
482,122



40
80
80
200
20.17
32.27
42.93
95.36
5.26
12.60
15.81
29.88 
2015 1
2
3
Jumla
521,159


 
40
80
80
200
20.86
36.12
38.80
95.76
5.19
13.50
15.38
31.02
2016 1
2
3
Jumla
571,176


 
40
80
80
200
18.23
34.11
25.67
77.97
5.53
13.83
12.87
29.07
2017 1
2
3
Jumla
610,392


 
40
80
80
200
18.84
25.45
25.15
69.43
5.23
11.79
13.42
27.49

 

Kutokana na jedwali hili, pamoja na takwimu na ripoti nyingine za uchanganuzi wa karatasi za mitihani ya Kiswahili ya mwaka huu, imedhihirika kwamba kwa jumla:

  1. Alama ya wastani ya karatasi ya kwanza (102/1) ya mwaka 2017 imebakia katika kiwango sawa na ya mwaka 2016 ambapo alama ya wastani ilikuwa 18.23 ikilinganishwa na 18.84 ya mwaka huu.
  2. Karatasi ya kwanza bado haijawatenga vyema wanafunzi bora na wale hafifu.Hili linadhihirishwa na alama tenganisho (5.23) ambayo iko chini sana ikilinganishwa na alama ya tenganisho ya kikaida (15.00). Hali hii inaweza kusababishwa na watahini kuongozwa na kutawaliwa na mtazamo nafsi wakati wa kuzitathmini insha za watahiniwa na kuishia kuwaweka katika viwango sawa au vinavyokaribiana.
  3. Alama ya wastani ya karatasi ya pili imeshuka sana kutoka 34.11 ya mwaka 2016 hadi 25.43 mwaka 2017.
  4. Karatasi hii iliweza kuwatenga vyema wanafunzi bora na wale hafifu. Alama tenganisho ilikuwa 11.79, japo alama hii imeshuka kutoka 13.83 ya mwaka 2016.
  5. Utendaji wa watahiniwa katika karatasi ya pili (102/2) uanaendelea kuzorota. Ruwaza za matokeo zaonyesha kuwa matokeo ya karatasi hii yamezidi kuyumba tangu mwaka wa 2009 Alama ya wastani ilishuka kwa takriban alama kumi(10) mwaka 2010, ikapanda kwa takriban kiwango hichohicho mwaka 2011, na baadaye kushuka kwa alama kumi na nne nukta thelathini (14.30) mwaka 2012. Mwaka 2013 ilipanda kwa kiasi kidogo mno, mwaka 2014 2.35, na mwaka 2015 kwa takriban alama 4. Mwaka 2016 alama ilishuka kwa takriban alama mbili, ilhali mwaka 2017 alama hii ilishuka kwa zaidi ya alama 8.
  6. Matokeo ya karatasi ya tatu (102/3) ya mwaka wa 2017 yamebakia katika kiwango kilekile ambapo alama ya wastani ilikuwa 25.65 yakilinganishwa na 25.15 ya mwaka huu.
  7. Alama wastani ya somo la Kiswahili kwa jumla imeshuka kutoka 77.97 mwaka 2016 hadi 69.43 ya mwaka huu.
  8. Asilimia ya watahiniwa wanaopata gredi A na A- ni ndogo mno.
  9. Alama wastani ya somo hili bado haijafikia kiwango cha kuiridhisha.

3.2 Uchanganuzi wa karatasi mahususi



3.2.1 Kiswahili Insha (102/1)

Jedwali 12: Matokeo ya Karatasi ya kwanza ya miaka 2012 - 2017

Mwaka 2012 2013 2014 2015 2016 2017
Alama ya wastani 10.43 18.46 20.17 20.86 18.23 18.84
Alama ya Tenganisho 3.63 5.44 5.26 5.19 5.53 5.23


Jedwali hili laonyesha kwamba kwa kipindi cha miaka sita (2014-2017), utendaji wa watahiniwa katika karatasi hii umekuwa ukiyumba .Tathmini ya kazi halisi za watahiniwa imebainisha kwamba asilimia kubwa ya watahiniwa sasa haimudu kujieleza kwa lugha iliyokomaa. Pia, idadi ya watahiniwa wanaopata alama za chini zaidi imepungua kiasi. Kadhalika, bado kuna asilimia kubwa ya watahiniwa wanaopata chini ya nusu ya alama zilizotengewa karatasi hii. Hata hivyo, imebainika kwamba idadi ya watahiniwa wanaoteua swali linalohusiana na methali imeongezeka kiasi, japo bado i chini. Hili linadokeza kwamba ule mtazamo wa kijadi kuwa insha zinazohusiana na methali huwa ngumu umeanza kubadilika. Tazama uchanganuzi wa swali la kwanza ambalo ndilo lililokuwa la lazima.

Lazima

Shirika la kigeni la Tugawane limeanzisha kiwanda cha kutengenezea matofali katika eneobunge lenu. Mwandikie barua Mhariri wa Gazeti la Mzalendo ukitoa maoni yako kuhusu faida na changamoto zinazoweza kutokana na mradi huu.

Swali hili lilimhitaji mtahiniwa kuandika barua kwa mhariri kuhusu umuhimu wa kiwanda cha kufyatulia matofali ambacho kimenzishwa na shirika la kigeni. Watahiniwa wengi walimudu kuzingatia muundo wa nje wa utungo wa aina hii.

Hata hivyo, tungo za watahiniwa zilidhihirisha kwamba wengi wamekosa ubunifu.Wengi hawakuweza kujadili hoja zilizotarajiwa; wakashindwa kukuza mada kikamilifu. Ni muhimu kukumbuka kuwa watahiniwa walikosa ubunifu hata katika maswali yale mengine.

Imebainika kwamba wanafunzi wengi hawasomi kwa mapana, hivyo hawadiriki kushughulikia masuala ibuka ipasavyo katika tungo zao.

3.1.2 Ushauri kwa walimu

Walimu wawatayarishe wanafunzi wao katika maeneo yote bila ubaguzi, kulingana na mahitaji ya silabasi ya Taasisi ya Ukuzaji Mitaala Nchni.



3.1.3 Mapendekezo

  1. Walimu wazidi kuwapa wanafunzi mazoezi zaidi katika uandishi wa kiuamilifu.
  2. Walimu watumie silabasi ya K.I.C.D ili kuelekeza ufundishaji wao. Mwongozo unaotolewa na KNEC kuhusu mada na stadi zinazotahiniwa, pamoja na vitabu vya fasihi vinavyotahiniowa, utumiwe kujalizana na silabasi ya KICD.
  3. Wanafunzi wahimizwe kusoma kwa mapana, na kwa kina (magazeti, majarida, kazi za kifasihi, na vitabu katika nyanja anuwai) ili kujifahamisha kuhusu matukio ya kila siku katika jamii na mazingira yao-kitaifa na pia kimataifa. Hili litapalilia ubunifu wao na kuwawezesha kumudu maswali yanayohusu masuala nyeti/masuala ibuka/ masuala mtambuko iwapo yatatahiniwa. Haitoshi kujifunga katika masuala yaliyo vitabuni pekee
  4. Wanafunzi wahamasishwe kufasiri maswali kwa uangalifu mkubwa huku wakizingatia maneno muhimu.


3.2.2 Kiswahili Lugha (102/2)

Jedwali 13: Matokeo ya Karatasi ya pili (102/2) ya miaka 2012 hadi 2017

Mwaka 2012 2013 2014 2015 2016 2017
Alama ya Wastani 29.06 29.92 32.27 36.12 34.11 25.45
Alama ya Tenganisho 10.77 12.68 12.60 13.50 13.83 13.42


Matokeo ya karatasi ya 102/2 yameshuka kwa kiwango cha kutia wasiwasi kutoka 34.11 mwaka 2016 hadi 25.45 mwaka huu.

Swali la kwanza, la tatu na la nne ndiyo yaliyowatatiza watahiniwa zaidi. Asilimia kubwa ya watahiniwa hawakumudu kujibu maswali yaliyowahitaji kutumia ujuzi wao kupata majibu. Haya ni maswali yanayolenga kukuza stadi za kiwango cha juu cha utambuzi. Tutachanganua swali la tatu.

MATUMIZI YA LUGHA: Alama 40)

  1. Andika tofauti moja kati ya sauti zifuatazo: (alama 2)
    1. /ng'/na/gh//
    2. /v/ na /f/
    3. /r/na /l/
    4. /m/na /n/
  2. Andika maneno yenye miundo ifuatayo: (alama 2)
    1. konsonanti, konsonanti, konsonanti, irabu, konsonanti, irabu
    2. konsonanti, konsonanti, irabu, konsonanti, irabu
  3. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mawili ya kiambishi : o. (alama 2)
  4. Andika sentensi zifuatazo upya kulingana na maagizo. (alama 2)
    1. Mhalifu alisamehewa kwa sababu alinyenyekea. (Geuza maneno yaliyopigiwa mstari kuwa nomino.)
    2. Waigizaji wengine wameingia jukwaani. (Tumia kivumishi cha idadi chenye kuonyesha nafasi katika orodha.)
  5. Tunga sentensi ukitumia kirai kihusishi kama kielezi. (alama 1)
  6. Unganisha sentensi zifuatazo kwa viunganishi mwafaka. (alama 2)
    1. Kheri aliweza kutujengea hospitali. Atajenga zahanati pia.
    2. Zumari anasomea Uanasheria. Vilevile Maki anasomea Uanasheria.
  7. Onyesha miundo miwili ya nomino katika ngeli ya A - WA. (alama 2)
  8. Tunga sentensi katika wakati uliopo hali isiyodhihirika. (alama 1)
  9. Andika sentensi ifuatayo katika umoja. (alama 1)
    Maseremala walilainisha mbao hizo wakatutengenezea meza.
  10. Andika upya sentensi zifuatazo kulingana na maagizo. (alama 4)
    1. Kaumu amewafanya mifugo wangu wanywe maji, (Anza kwa: Mifugo wangu , usitumie, "amewafanya'.)
    2. Wanakijiji wanaishi karibu na msitu. Wanakijiji hawawavamii wanyama. (Unganisha kuunda sentensi ambatano.)
  11. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa. (alama 1)
    Ngoma hizo zao ziliibwa na wezi wale.
  12. Tumia 'kwa' katika sentensi kuonyesha:
    1. sehemu ya kitu kizima (alama 1)
    2. namna tendo lilivyofanyika (alama 1)
  13. Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa. (alama 2)
    Kusoma kwa mapana kutapalilia ubunifu wa wanafunzi hawa wenu," mtaalamu akatuambia.
  14. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
    Viwanda vikianzishwa mashambani idadi ya wanaohamia mjini itapunguzwa. (alama 2)
  15. Tunga sentensi zenye miundo ifuatayo. (alama 2)
    1. KN (N + RH) + KT (Ts + T)
    2. KN (V+ N) + KT (t + v)
  16. Ainisha yambwa katika sentensi ifuatayo.
    Mhunzi alimfulia miukuu wake pete ya shaba. (alama 2)
  17. Bainisha maana mbili zinazojitokeza katika sentensi ifuatayo.(alama 2)
    Bedui alimrushia tufe.
  18. Alama za mtajo hutumiwa kufungia maneno halisi ya msemaji. Tunga sentensi mbili kuonyesha matumizi mengine mawili ya alama za mtajo. (alama 2)
  19. Andika sentensi ifuatayo upya kwa kutumia kinyume cha maneno yaliyopigiwa mstari.
    Mwanafunzi mkakamavu huzingatia masomo yake. (alama 1)
  20. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya rithi na ridhi. (alama 2)

  21. Tunatumia simile tunapotaka mtu atupishe.......tunapoomba kitu............... kinusurike, na kefule............................. na jambo, (alama 1)
  22. Andika visawe vya maneno yafuatayo: (alama 1)
    1. ndoa
    2. omba
  23. Andika sentensi ifuatayo upya kulingana na maagizo. (alama 1)
    Maeneo haya yana uyoga. (Anza kwa: Uyoga.)


Maswali katika sehemu hii yalilenga mada mbalimbali za kisarufi kama zilivyopendekezwa na silabasi. Maswali yalimhitaji mtahiniwa kutumia ujuzi wake wa dhana za kisarufi kujibu maswali aliyopewa. Watahiniwa wengi sana walishindwa kumudu dhana za kimsingi za kisarufi kama vile kuandika katika umoja, miundo ya maneno, kuandika visawe na uchanganuzi wa sentensi za kimsingi.. Wengine walishindwa kujibu maswali ya kimsingi ya mtamshi bora.Kadhalika watahiniwa wengi mno walipoteza alama katika maswali yote, hata ya ufahamu na ufupisho, kutokana na makosa ya sarufi na hijai. Wengine hawakumudu kuandika ufupisho ipasavyo.

  1. Sauti:
    1. /ng'/ ni nazali na/gh/ni kikwamizo.
    2. ni ghuna na /f/ sighuna.
    3. /r/ ni kimadende na /l/ ni kitambaza.
    4. /m/ hutamkiwa midomoni ilhali /n/ ni ya ufizi.
      (4x1/2) (alama 2)
  2.  
    1. Mfano : mbweha, ngwena, ndwele (alama 1/0)
    2. Mfano : ndama, mkate, ngama, ndizi, mkeka (alama 1/0)
  3. Matumizi ya kiambishi O
    Mifano
    1. Kirejeshi cha nafsi ya tatu wingi - Wafanyakazi walioajiriwa wana bidii.
    2. Kirejeshi cha ngeli ya U- I - Umoja
      Mguu uliotibiwa umepona.
    3. Kirejeshi cha ngeli ya U - ZI - umoja
      Ufa uliozibwa ni huu.
    4. Kirejeshi cha ngeli ya U-YA- umoja
      Ugonjwa huu ndio uliotibiwa.
    5. Kirejeshi cha ngeli ya U-U-
      Wema aliotuonyesha ulituvutia.
    6. Kuonyesha tokeo la kitu/kuonyesha nomino/unominishaji
      1. Mtafiti umetoa toleo jipya la kazi hiyo.
      2. Mti umetoa zao lingine
      3. Mkato huu wa nywele haupendezi.
    7. Kuonyesha kinyume
      1. Mwangi aliuchomoa mkuki ardhini (2x1) (alama 2)
  4.  
    1. Mhalifu alipata (alipewa) msamaha kwa sababu (kwa) unyenyekevu wake. (alama 1/0)
    2. Waigizaji wa kwanza/wa mwisho wameingia jukwaani.( alama1/0)
  5.  
    1. Mama huyo aliwapenda wanawe kwa dhati. (RH/E)
    2. Bendera ilikuwa juu ya mlingoti. ( RH/E)
    3. Mkurugenzi aliwasili kabla ya mkutano kuanza. (RH/E)
    4. Kaire ni mrefu kuliko baba yake.( RH/E) V. (alama 1/0)
  6.  
    1. (Ikiwa/ Kama) Kheri aliweza kutujengea hospitali sembuse zahanati!
      Kheri aliweza kutujengea hospitali kwa hivyo atatujengea zahanati (pia). (alama 1/0)
    2.  Zumari na Maki wanasomea Uanasheria. (alama 1/0)
  7. Majibu yafuatayo yanaweza kutolewa:
    1. Nomino zinazoanza kwa ‘m' katika umoja na 'wa' katika wingi.
      Mfano: Mbunge - Wabunge
    2. Zinazoanza kwa 'mw' katika umoja na 'wa' katika wingi.
      Mfano: Mwanasheria - Wanasheria
    3. Nomino za pekee zinazotaja watu. Maria ametutembelea.
    4. Zinazoanza kwaʼki' katika umoja na vy' katika wingi.
      1. Kijana huyu ameheshimika.
        Vijana hawa wameheshimika.
      2. Kiboko angalimajini.
        Viboko wangali majini.
    5. Ambazo hazina mianzo maalum ila huchukua viambishi A-WA vya upatanisho wa kisarufi.
      Kwa mfano, simba, kuku, bata, mama, baba.
      Simba huyu amehifadhiwa.
      Simba hawa wamehifadhiwa. (2x1) (alama 2)

      Mtahiniwa atoe mfano ili kutuzwa alama 1 kwa kila jibu.
  8. Kiambishi ‘a’ cha njeo kitumiwe.
    1. Wanariadha wacheza uwanjani,
    2. Jua lachomoza asubuhi.
    3. Sisi twasoma vitabu.
    4. Mwalimu afundisha darasani. (1x1) (alama 1/0)
  9. Seremala alilainisha ubao huo akanitengenezea meza. (alama 1/0)
  10.  
    1. Mifugo wangu wamenyweshwa maji na Kaumu. (alama 2/0)
    2. Wanakijiji wanaishi karibu na misitu lakini ila balisilhali hawawavamii wanyama. (alama 2/0)

      Tanbihi
      Sentensi sharti iwe na vishazi viwili huru. Kimoja kikiwa kitegemezi, basi hiyo haitakuwa ambatano, hata kama atakuwa ametumia kiunganishi ambatani kama vile "lakini' na 'ila."
  11. Magoma hayo yao yaliibwa na majizi yale alama 1/0
  12.  
    1.  
      1. Watoto watatu kwa kumi hupata chanjo hiyo.
      2. Wengine walipata tisa kwa kumi katika tamrini hiyo. alama 1/0
    2.  
      1. Sara alifanya kazi kwa bidi.
      2. Polisi waliandamana moja kwa moja hadi kituoni.
      3. Mchinjaji alikata nyama kwa kisu. alama 1/0

        Tanbihi

        Hata pale kwa' inapotumiwa kuonyesha ala/kitumizi, huonyesha pia jinsi tendo lilivyofanyika.
  13. Mtaalamu alituambia kwamba kusoma kwa mapana kungepalilia ubunifu wa wanafunzi hao wetu. alama 2/0
  14.  
    1. Viwanda vikianzishwa mashambani – kishazi kitegemezi
    2. Idadi ya wanaohamia mjini- kishazi kitegemezi
    3. Itapunguzwa - kishazi huru 2 x 1 = 2
  15.  
    1.  
      1. Umati wa watu ulikuwa ukimshangilia.
      2. Kisu cha baba kinahitaji kunolewa alama 1/0
    2.  
      1. Mwenye duka angali mwaminifu.
      2. Yule dalali alikuwa shupavu.
      3. Huyu mtoto ni mtiifu.
      4. Lenye mpini lilikuwa lake. alama 1/0
  16. Mjukuu wake -yambwa tendewa (kitondo)
    Pete ya shaba - yambwa tendwa (kipozi)

    Tanbihi  2 x 1=2
    Ikumbukwe kwamba sharti yambwa kamili ijitokeze. Kwa mfano, mjukuu anayerejelewa ni wake, hivyo yambwa tendewa itakuwa mjukuu wake wala si mjukuu tu.
  17.  
    1. Alirusha tufe kwa niaba ya mhusika huyo.
    2. Alirusha tufe kuelekea kwa mhusika huyo.
    3. Alirusha tufe ya mhusika huyo.
    4. Alimrusha mhusika huyo kwa sababu ya tufe.
  18. Matumizi yafuatayo yajitokeze:
    1. Kufungia neno la kigeni- "mukimo"
    2. Kuonyesha neno lina maana nyingine na unayomaanisha, k.m. binamu kumaanisha 'mpenzi'.
    3. Kufungia anwani- “Pendo la Karaha"
    4. Kuonyesha neno halijakubaliwa katika lugha unayoandikia unayozungumza. 2 x 1 = 2
  19. Mkakamavu – mzembe/mvivu/mnyonge/goigoi/mtepetevu/dhaifu huzingatia – hupuuza/ hutelekeza 2 x 1/2=1
    Maana zifuatazo zijitokeze:
  20. Rithi – kupata mali/maarifa au ujuzi kutoka kwa mtu/makala fulani
    Ridhi – kukubali au kupendezwa na jambo/kutoa ruhusa jambo litendeke. alama 2/0

    Tanbihi
    Kwa vile tunatahini matumizi ya maneno haya, anaweza kuvinyambua vitenzi, mradi ile maana ya kimsingi inajitokeza.
  21.  
    1. hamadi
    2. tunapoudhika/tunapokasirishwa 2 x 1/2=1
  22.  
    1. doa-dosari, kosa, hitilafu, ila, baka.
    2. omba – rai, sihi, sali
  23.  
    1. Uyoga hupatikana kwenye maeneo haya.
    2. Uyoga hupatikana katika maeneo haya.
    3. Uyoga upo kwenye maeneo haya. alama 1/0


MAPENDEKEZO

  1. Walimu waendelee kuwapa wanafunzi mazoezi katika vipengele vyote vya kisarufi.
  2. Wanafunzi wasisitiziwe kwamba baadhi ya maswali ni ya stadi za juu kama matumizi/ utekelezaji na usanisi Wasitarajie kila mara kupata maswali ya kuchopoa majibu moja kwa moja kutoka kwenye vifungu au kukariri kutoka kumbukumbu zao.
  3. Wanafunzi wapewe mazoezi ya ufahamu na muhtasari mara kwa mara huku mtiririko ufaao ukisisitizwa ili wapate kuzoea kutumia viunganishi kutiririsha hoja katika kujibu maswali ya muhtasari.
  4. Walimu wasisitize vipengele vya kimsingi vya sarufi kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne.
  5. Mwelekeo mseto katika ufunzaji uzingatiwe zaidi. Mathalan mwalimu anaweza kutumia fasihi kufunzia mada tata za sarufi, kama vile aina za sentensi. Hili litachangia katika kulihuisha somo la sarufi na kuwafanya wanafunzi kulichangamkia.
  6. Walimu na wanafunzi watalii maeneo yote ya sajili bila ya kujifunga kwa chache tu ambazo ni za kawaida.
  7. Masuala yote katika silabasi yafundishwe katika upana wake bila kubagua.




3.2.3 Kiswahili Fasihi (102/3)

Matokeo ya karatasi ya tatu (102/3) ya miaka ya 2012 hadi 2017

Mwaka 2012 2013 2014 2015 2016 2017
Alama ya wastani 32.14 34.82 42.93 38.80 25.67 25.15
Alama ya Tenganisho 15.15 14.92 15.81 15.38 12.87 13.42


Matokeo haya yanaonyesha kuwa utendaji wa watahiniwa katika karatasi hii unaendelea kuyumba. Tathmini ya karatasi halisi za watahiniwa ilibainisha kwamba asilimia kubwa ya watahiniwa, hata wale wanaopata alama za juu zaidi katika karatasi hii, haimudu kuwasilisha hoja kwa njia komavu. Kazi za watahiniwa zimepwezwa na makosa mengi ya kisarufi, kimuundo na hijai. Kadhalika, pameibuka mtindo wa kuwasilisha hoja kwa ufupi mno, kiasi cha kuwafanya baadhi ya watahiniwa kupoteza alama. Maswali ya ushairi yanaepukwa na watahiniwa wengi mno. Hata wale wanaodiriki kuyafanya, wanaambulia alama za chini mno. Imebainika kwamba baadhi ya masuala ya kimsingi ya ushairi hayafunzwi, hivyo yanapotokea katika mtihani watahiniwa wengi hupoteza alama.
Tutachanganua swali la kwanza kwani ndilo lililokuwa la lazima.

Lazima (20 marks)

Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali.

Walikuja mahasidi, ah, walikuja
Nyayo zao zikirindima, ah rindima
Kwa ghamidha ya uadui, oo uadui
Wali wakibeba sime
Wali wakibeba mata
Wali wakibeba mienge
ya moto kutangazia
kwao kuwasili


Walikuja kwa ndimi
zilohimili cheche
matusi kutumwaiya.
Hawakujua ya kwamba
mbele ya mhimili huno wetu
wao wali vipora.
Kwenye Mlima wa Sugu, walituvamia.
Aliwakabili Mbwene
Mwana wa Ngwamba, ee Mbwene
Aliwakabili Mbwene kwa kitali kikali.
Wali wametuteka ja samaki kwenye dema
Wali wamewapukutisha
wetu mabarobaro
Aliwakabili Mbwene
Ee Mbwene, Mwana wa Ngwamba
Aliwakabili
kwa hamasa za ujana
kwa uchungu wa kuumbuliwa
wa wetu wana.

Aliwakabili Mbwene
Nao wakalipiza shambulizi
kwa kujidai majagina
walijibwaga uwanjani
Laiti wangalijua wanajikabidhi
viganjani mwa Mbwene.
Aliwakabili Mbwene, ee
Mwana wa Ngwamba, shujaa asoshindwa
alipigana kitali
cha kufa na kupona
kuiopoa jamii yetu,
kuirejesha hadhi yetu.
kuirejesha mifugo yetu
kuwarejeshea wakulima vikataa vyao
kuwaokoa vipusa wetu
nyara waliotekwa, ati walipiza kisasi.

Aliwakabili Mwana wa Ngwamba
Aliwakabili Upepo wa Kusi
Hata kikomo cha mapambano kilipofika
Wagundi walijua kwamba
Walikuwa na Mwana, ee Mwana
Mbwene, ee Mwana wa Ngwamba
Hakuwa na kifani, ee kifani
Alipigana nao, ee Mwana wa Ngwamba
Kwa siku kumi bila tonge wala tone la maji
Kwetu kukenda kicheko cha wokovu
Kwao kukenda kilio.

  1. "Huu ni wimbo wa sifa.” Thibitisha kauli hii kwa kutoa mifano mitatu kutoka kwenye utungo huu. (alama 3)
  2. Andika sifa tatu za jamii ya nafsineni katika utungo huu. (alama 3)
  3. Huku ukitoa mifano, bainisha vipengele vinane vya kimtindo ambapo nafsineni imetumiwa kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu. (alama 8)
  4. Tungo za aina hii zinaendelea kufifia katika jamii yako. Fafanua hoja sita utakazotumia kuishawishi jamii yako kukinga dhidi ya hali hii. (alama 6)


Swali hili lilimhitaji mtahiniwa:
Kubainisha sifa za nyimbo za sifa, kutambua sifa za jamii iliyouzaa wimbo huu, mbinu za uwasilishaji wa nyimbo za aina hii, na umuhimu wa nyimbo hizi/mikakati ya kuzidumisha nyimbo za aina hii. Uchanganuzi wa majibu ya watahiniwa umedhihirisha kuwa asilimia kubwa ya watahiniwa haimudu maswali yanayowahitaji kutumia ujuzi wao kujibia. Udhaifu huu pia umejitokeza katika majibu yao kwa maswali mengine.

  1.  
    1.  
      1. Kuonyesha Mbwene kama aliye jasiri- aliwakabili kwa kitali kikali.
      2. Kumrejelea Mbwene kama shujaa asiyeshindwa- hawakujua kwamba mbele ya mhimili huu wetu walikuwa vipora.
      3. Kumtajaanayesifiwa kwa majina mbalimbali-Mbwene, Mwana wa
        Ngwamba, Upepo wa Kusi, Mhimili.
      4. Kumsawiri kama bingwa wa kupindukia- Hakuwa na kifani.
      5. Kusifia ushindi//kitali alichopigana. Wagundi walijua walikuwa na
        mwana wa Ngwamba/kwetu kukenda kicheko.
        (3x1) Kutaja-1/2 Mfano-1/2
        (alama 3)
    2.  
      1. Ni wakulima- kurejesha vikataa.
      2. Ni wafugaji – kurejesha mifugo.
      3. Utekaji nyara - kuwaokoa vipusa wetu.
      4. Mazoea ya uchokozi/ kupigana vita- walikuja kwa ndimi zilizojaa
        matusi...aliwakabili Mbwene, nao wakalipiza....
        (3x1) Kutaja- 1/2 Mfano-1/2
        (alama 3)
    3.  
      1. Matumizi ya vihisishi ili kuibua hisia/kusisitiza ujumbe - ah, ee
      2. Usambamba
        -wali wakibeba sime
        -wali wakibeba mata
        - wali wakibeba mienge
        - kuirejesha hadhi yetu
        -kuirejesha mifugo yetu
      3. Sitiari- wali vipora
      4. Tashbihi – ja samaki kwenye dema
      5. Lakabu - Upepo wa Kusi.
      6. Nahau - cha kufa na kupona -kitali kikali.
      7. Chuku- kupigana (Ngwamba) kwa siku kumi bila kula wala kunywa,
      8. Tanakuzi - kicheko - kilio
      9. Miundo ngeu ya sentensi/ kufinyanga sarufi
        -wetu mabarobaro
        - matusi kutumwaiya
        - wa wetu wana
      10. Inkisari- zilohimili, kukenda.
      11. Taswira- utungo unasawiri picha ya mapigano.
      12. Matumizi ya mistari mishata ili kuibua taharuki- ya moto kutangazia... (8x1) Kutaja- 1/2 Mfano-1/2
    4. Mtahiniwa aonyeshe umuhimu wa nyimbo za sifa. Baadhi ya hoja ni:
      1. Kuwatambua mashujaa
      2. Kurithisha utamaduni wa jamii
      3. Ni kitambulisho cha jamii.
      4. Hutumiwa kuwafunza vijana mbinuishi kama vile ujasiri, kutoa
        maamuzi yafaayo.... shujaa anahitaji kutoa maamuzi kwa kuzingatia mahitaji ya jamii yake.
      5. Hukuza uzalendo, jamii inaweza kuwatumia wanaosifiwa kama
        vielelezo vya uzalendo.
      6. Hupitisha historia ya jamii, hivyo kuwafunza vijana kuhusu kwa
        mfano, maadui wa jamii zao, vita vilivyopiganwa na mafanikio
        yaliyofikiwa.
      7. Ni nyenzo ya kurithisha fani yenyewe ya uimbaji. viii. Hukuza ubunifu. Kadiri vijana wanavyosikiliza nyimbo za aina hii
        zikiimbwa, ndivyo wanavyojifunza mitindo mbalimbali ya utungaji na uwasilishaji.
      8. Hutumiwa kuonya dhidi ya matendo hasi kama vile usaliti/ huadilisha.
      9. Ni njia ya kupitisha maarifa, kama vile ya kupigana vita. Mtu
        kufahamu: ni lini atashambulia, ni lini ataepuka shambulizi.
      10. Hukuza utangamano/ushirikiano. Watu wanapoimba nyimbo hizi
        pamoja hujihisi kuwakundi moja linalomuenzi shujaa mmoja.
      11. Ni njia ya kujiburudisha.
      12. Ni nyenzo ya kupitisha wakati, badala ya kujiingiza kwenye vitendo visivyofaa.
      13. Hupitisha amali na tamaduni za jamii. Desturi za jamii hutajwa katika baadhi ya nyimbo.
    5. Mtahiniwa anaweza pia kupendekeza njia za kudumisha kipera hiki. Baadhi ni:
      1. Kuzihifadhi kwenye maandishi
      2. Kuzihifadhi kwenye kanda
      3. Kuzifanyia utafiti
      4. Mashindano ya tamasha za muziki
      5. Kuzifunza shuleni
      6. Kuwahimiza vijana kuzitunga
        (6x1) Kutaja- 1/2 Mfano/ kueleza-1/2
        (alama 6)
        Tanbihi
        Mtahiniwa anaweza pia kujadili hasara za kutourithisha utungo wa aina hii, akawa anaionya jamii yake dhidi ya kutourithisha.



3.4 MAPENDEKEZO

  1. Walimu wafundishe vitabu vilivyoteuliwa kwa ukamilifu wake huku wakizingatia vipengele vifuatavyo vya uchanganuzi wa kazi za kifasihi:
    1.  Dhamira na maudhui
    2. Fani , kama vile:
      • Mandhari
      • Ploti
      • Usimulizi
      • Wahusika
      • Muundo
      • Mtindo, kama vile tamathali za usemi, urudiaji, nk
  2. Wanafunzi wahimizwe kutambua masuala muhimu yanayojitokeza katika hadithi zote katika diwani teule ya hadithi fupi.
  3. Wanafunzi wawekewe misingi bora katika fasihi simulizi tangu kidato cha kwanza.
  4. Walimu wawafundishe wanafunzi wao istilahi muhimu zinazohusiana na ushairi ili kuupalilia ukakamavu wao katika kuyajibu maswali ya ushairi.
  5. Mbinu za kuchanganua Ushairi zifunzwe katika upana na kina kulingana na kiwango hiki.


3.5 Hitimisho

Kutokana na uchanganuzi wa hapo juu, ni dhahiri kwamba matokeo ya somo la Kiswahili bado hayajafikia kiwango cha kuridhisha. Ni watahiniwa wachache mno waliofikia viwango vya juu vya utendaji katika karatasi zote tatu. Asilimia kubwa ya watahiniwa inapata chini ya alama wastani katika karatasi zote.

Ni matumaini yetu kwamba walimu na wanafunzi watafaidi kwa uchanganuzi uliotolewa. Kadhalika tunawahimiza kuyatilia maanani mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti hii ili kuimarisha matokeo ya somo hili.

Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI PAPER REPORT - KCSE 2017 REPORTS.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest