KISWAHILI PAPER 3 - 2019 LANJET JOINT MOCK EXAMINATION

Share via Whatsapp

SEHUMU YA A
RIWAYA: CHOZI LA HERI
(Assumpta K. Matei)

  1. “… wino wa Mungu haufutiki…”
    1. Eleza muktadha wa maneno haya (alama 4)
    2. Taja na uelembinu moja ya lugha iliyotumiwa katika dondoo hii (alama 2)
    3. Fafanua ukweli wa kauli hii kwa kuzingatia hoja zozote kumi na nne kutoka katika riwaya ya Chozi la Heri (alama 14)

SEHEMU YA B
TAMTHILIA: KIGOGO
(Pauline Kea)                         
Jibu swali la Pili ama la Tatu

  1. “Mambo yamekwenda kombo Sagamoyo, sio siri tena.”
    1. Fafanua sifa na umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya (alama 6)
    2. Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa hoja kumi nan ne kutoka katika tamthilia ya kigogo   (alama 14)

                                                            Au

  1. “Ushahidi itatoka wapi kama kipanga ndiye hakimu kwenye kesi ya kuku?”
    1. Eleza muktadha wa maneno haya (alama 4)
    2. Fafanua mbinu mbili za lugha zilizotumiwa katika dondoo hii (alama 4)
    3. Fafanua haki kumi na mbili za Wanasagamoyo na uonyeshe jinsi ziivyokiukwa (alama 12)

SEHEMU YA C
HADITHI FUPI: TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE

(Alifa Chokocho na Dumu Kayanda- Wahariri)

Jibu swali la Nne ama la Tano

MKUBWA

  1. “… Basi niache nitafute pesa. Muhimu mniunge mkono…
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
    2. Fafanua sifa zozote nne za mzungumziwa (alama 4)
    3. Fafanua athari ya vitendo vya mzungumzaji wa maneno haya katika jamii (alama 12)

                                                            Au

  1. Jadili suala la uozo wa maadili katika jamii huku ukirejelea hadithi zozote nne katika diwani ya Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine (alama 20)

SEHEMU YA D

USHAIRI

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu masuali
    Ujuaji kwa fasili, kujifanya watambua,
    Ujuaji kiwasili, majitapa huwadia,
    Ujuaji kwa asili, kujibeba bila nia,
    Ujuaji jambo kali, binadamu tagundua.
    Ujuaji kila hali, usijitie wajua,
    Ujuaji takudhuli, matatani kutumbua,
    Ujuaji si mwimili, wa Mungu kudurua,
    Ujuaji jambo kali, binadamu tagundua.
    Ujuaji mkatili, elimuni kubagua,
    Ujuaji tafisili, zako mali kupungua,
    Ujuaji kiakili, epukana julangua,
    Ujuaji jambo kali, binadamu tagundua.
    Ujuaji jua kali, mambo mengi gharimia,
    Ujuaji lokidhili, biasharayo tafumua,
    Ujuaji hutufeli, masikini kutujia,
    Ujuaji jambo kali, binadamu tagundua.
    Ujuaji tena ghali, mambo mengi unaua,
    Ujuaji wafadhili, misa’da kudidimia,
    Ujuaji kila hali, hupati kusisimua,
    Ujuaji jambo kali, binadamu tagundua.
    Ujuaji hawajali, kukwambiya solijua,
    Ujuaji takufeli, maishani ‘tojijua,
    Ujuaji si asali, ni mbaya tatambua,
    Ujuaji jambo kali, binadamu tagundua.

    Kutoka: Meja S. Bukachi (Uketo wa Fasihi, uk 120- 121)

    MASWALI
    1. Lipe shairi hili anwani mwafaka. (Alama 1)
    2. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili. (Alama 2)
    3. Mwandishi anasema kuwa ujuaji ni nini? (Alama 2)
    4. Taja tamathali za lugha zilizotumika katika shairi hili. (Alama 2)
    5. Fafanua uhuru wa ushairi alioutumia malenga. (Alama 4)
    6. Weka shairi hili katika bahari mbalimbali. (Alama 3)
    7. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (Alama 4)
    8. Vifungu vifuavyo vina maana gani katika shairi?
      1. Majitapa
      2. Gudurua

SEHEMU YA E

FASIHI SIMULIZI

Soma utungo ufatao kisha ujibu maswali

Ndimi Kisoi, dume la ukoo mtukufu
Ulojipambanua kwa mabingwa
Wchezaji hodari wa ngoma
Ndimi dume lililoingia nyanjani
Makoo yakatetema
Yakang’ang’ania, gozi kusakata name.
Kijiji kizima kilinijua
Wazee walinienzi
Wakamiminika kiamboni
Mabinti kunikabidhi.

Kutoka: Assumpta K. Matei (Fani ya Fasihi Simulizi, uk 113)

Maswali

  1. Tambua kipera hiki cha fasihi simulizi (alama 2)
  2. Jinsia ya nafsi neni ni gani? (alama 2)
  3. Eleza sifa zozote nane za kipera hiki cha fasihi simulizi (alama nane)
  4. Fafanua umuhimu wa kipera ulichokitaja hapo juu katika jamii (alama 8)


MARKING SCHEME

SEHUMU YA A
RIWAYA: CHOZI LA HERI
(Assumpta K. Matei)

  1. “… wino wa Mungu haufutiki…”
    1. Eleza muktadha wa maneno haya (alama 4)
      Haya ni maelezo (usimulizi wa) mwandishi. Anarejelea mawazo ya Mwangeka. Mwangeka alikuwa kaketi mkabala mwa kidimbwi cha kuogelea, nje ya jumba lake kandokando ya ufuo. Anakumbuka methali aliyozoea kumtolea mpinzani wake daarasani kila wakati Mwangeka alipomshinda mpinzani huyo.
    2. Taja na ueleze mbinu moja ya lugha iliyotumiwa katika dondoo hii (alama 2)
      Methali- wino wa Mungu haufutiki
    3. Fafanua ukweli wa kauli hii kwa kuzingatia hoja zozote kumi na nne kutoka katika riwaya ya Chozi la Heri (alama 14)
      Methali/ Kauli hii imejikita katika suala la ujaala. Ujaala ni nadharia inayosisitiza uwezo na nguvu za Mwenyezi Mungu. Husisitiza mambo ambayo hupangwa kufanyika na ambayo mwanadamu hana uwezo wa kuyadhibiti wala kuyaepuka hata ajaribu kwa njia gani. Jinsi yalivyopangwa na Mwenyezi Mungu ndivyo yanavyosalia kuwa na kutendeka kwa njia iyo hiyo.
      1. Ridhaa hakuwa mkazi asilia wa msitu wa Heri. Alikuwa 'mfuata mvua', kama walivyoitwa walowezi na wenyeji kindakindaki. Hakupachagua mahali hapa, majaaliwa yalitaka, na majaaliwa yana nguvu (uk 8).
      2. Akirejelea Umu na Dick, mwandishi anasema kuwa ‘Hata waliposikia kwa mbali sauti ikitangaza kuwa abiria wanaoabiri ndege Tumaini waanze kuingia, walijua jaala ilikuwa imewakutanisha, kwamba hawatawahi kutengana tena’ (uk 128).
      3. Pete anaeleza kuwa aliichukia jaala iliyompa mama anayejali maslahi yake tu, alichukie maumbile yaliyomweka kwenye jinsia ya kike, alichukia kitoto alichohimili kwenye mji wake. Haya yote ni majaliwa (uk 149).
      4. Pete alijaribu kukiangmiza kitoto chake cha pili. Alijaribu kukiavya mara nne kwa vidonge ila ikashindikana (uk 151).
      5. Pete alikuwa mzazi mchanga mwenye watoto watatu na kila mmoja alikuwa na baba yake (uk 152).
      6. Sauna alilelewa na Bw. Maya ambaye hakuwa baba yake mzazi. Maya ndiye anayemharibia Sauna maisha (uk 155).
      7. Mwengemi anamshawishi Neema azingatie kupanga kwa mtoto kwani walikuwa wamejaribu kupata mtoto kwa miaka mitano lakini wakashindwa (uk 159).
      8. Neema anakumbuka jinsi Mungu alivyompa mtoto (aliyemwokota) akasisitiziwa na Mtawa Cizarina kuwa naye anaweza kumpanga Immaculata bali akakataa, sasa anatamani mtoto (uk 163).
      9. Ujaala unamleta Mwaliko katika kituo cha watoto cha Benefactor na hatimaye kupangwa na Mwangemi na Neema (uk 165).
      10. Kila mara Mwaliko hujiuliza moyoni kwa nini jaala ilimnyima Neema mwana (uk 168).
      11. Mwangemi alimhakikishia Mwaliko kuwa licha ya kutembelea vituo mbalimbali asiwapate ndugu zake, hana shaka kuwa ndugu zake wako hai na siku moja watakutana (uk 170).
      12. Ujaala unawakutanisha ndugu watatu waliotenganishwa miaka mingi iliyopita (Umulkheri, Dick na Mwaliko). Dick anaamini kuwa kweli ni milima tu isiyokutana (uk 186).
      13. Mwaliko anamkumbusha Mwangemi kuwa kwenda kwao hotelini kulikuwa kumewaletea heri. Kuliwapanulia familia yao (uk 190).
      14. Ujaala uliwafanya binamu wawili, Mwangeka na Mwangemi, kuwapanga wanawe Lunga; Umu, Dick na Mwaliko.
      15. Majaliwa yalimwepusha Mwangeka kuangamia pamoja na jamaa wake katika mkasa wa moto.

SEHEMU YA B
TAMTHILIA: KIGOGO
(Pauline Kea)                         
Jibu swali la Pili ama la Tatu

  1. “Mambo yamekwenda kombo Sagamoyo, sio siri tena.”
    1. Fafanua sifa na umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya (alama 6)
      Maneno haya yalisemwa na Kombe

      Sifa za Kombe
      Fisadi. Anaila keki aliyopewa na Boza, keki iliyoletwa na Kenga.
      Mwenye heshima. Anamshukuru Ashua kwa chai aliyowaletea(uk 3).
      Mwenye msimamo legevu. Katika mazungumzo yao na Boza na Sudi, hadhihirishi waziwazi ni upande upi anaouunga mkono.

      Umuhimu wa Kombe
      Anawakilisha wananchi wenye tamaa na hujipata kuendeleza ufisadi.
      Ni kielelezo cha heshima na adabu katika jamii.
      Ni kiwakilishi cha watu ambao hawana msimamo thabiti. Watu walio tayari kuunga mkono upande wowote almuradi wajinufaishe.
      Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa hoja kumi nan ne kutoka katika tamthilia ya kigogo   (alama 14)
      • Maji machafu (uchafuzi wa mazingira) yalipita mataroni na kueneza harufu mbaya kila mahali bila uongozi wa Sagamoyo kuliona hili kuwa tatizo (uk 2).
      • Soko la Chapakazi limebadilishwa na kufanynwa uwanja wa kumwagia kemikali(uk 2).
      • Wafanayabiashara polisi wanaangaishwa na wanaosanya ushuru kwa kuwaitisha kitu kidogo na wengine kitu kikubwa (uk 2-3).
      • Serikali kutangaza mwezi mzima wa kusherehekea uhuru bila watu kufanya kazi ilhali haijali watakachokula watu (uk 4).
      • Serikali ya Sagamoyo haina mipango maridhawa ya kimaendeleo. Majoka anamiliki kampuni kubwa ya sumu ya nyoka badala ya miradi muhimu (uk 4).
      • Kuna ufisadi unaomfanya Asiya kupata kandarasi ya uokaji keki ya uhuru kwa kujuana na Husda bali si kwa kufuzu na kufaulu (uk 7).
      • Utawala wa Sagamoyo ni wa kimabavu. Kenga anamlazimisha Sudi amchongee Majoka kinyago cha Ngao licha ya kujua kuwa uongozi wa Majoka ni wa udhalimu (uk 9).
      • Kombe, mshiriki wa karibu wa Kenga anakiri kuwa mambo yameenda kombo Sagamoyo (uk 15).
      • Uongozi unafunga soko la Sagamoyo. Soko hili ndilo kitegauchumi pekee kwa Wanasagamoyo (uk 25).
      • Kuna maandamano ya mara kwa mara na yasiyotatuliwa katika jimbo la Sagamoyo, wanachi wanapigania haki zao.
      • Majoka anawatumia polisi wake vibaya ili kujidumisha uongozini. Polisi wanawanyanyasa na kuwadhulumu wananchi bila Majoka kujali.
      • Sagamoyo kuna uongozi wa ubinafsi. Majoka anataka kuendeleza ubinafsishaji wa uongozi wa Sagamoyio kwa kumtangaza rasmi Ngao Junior kuwa mrithi wake (uk37).
      • Kuna unyakuzib wa mali ya umma. Majoka analifunga soko na kuinyakua sehemu hiyo ili ajenge hoteli ya kifahari (uk 45).
      • Wanasagamoyo wanalalamika kuwa wanatozwa kodi ya juu mno (uk 2).
      • Bei ya chakula kwenye kioski cha kampuni inapandishwa mara dufu baada ya soko kufunwa (UK 17).
      • Majoka amepaotokwa kimaadili. Anamwandama Ashua na kutaka kumdhulumu kimapenzi. Ashua anapokataa, Majoka anamfunga jela (uk 22).
      • Majoka anaeleza jinsi Jabali alivyouawa pamoja na wapinzani wengine (uk 35).
      • Wafanyakazi wa Sagamoyo wanadhulumiwa. Kenga na Majoka wanapanga jinsi watakavyowaongeza wafanyakazi mshahara kidogo kisha wauchukue kwa kuongeza kodi.
      • Majoka anwaamuru polisi kutumia vitoza machozi ili kuwatawanya waandamanaji (uk 38).
      • Tunu anamkabili Majoka na kubainisha udhalimu alioufanya ikiwemo umwagaji damu (uk 43)
      • Tunu anavunjwa mguu kwa amri ya Kenga na Majoka (uk 54, 68).
      • Kenga na Majoka wana mpango wa kumwangamiza Chopi kwa sababu amebaini siri zao (uk 68).
      • Ngurumo ananyongwa na chatu (uk 69).

                                                            Au

  1. “Ushahidi itatoka wapi kama kipanga ndiye hakimu kwenye kesi ya kuku?”
    1. Eleza muktadha wa maneno haya (alama 4)
      Haya ni maneno ya Ashua. Anamwambia Majoka. Walikuwa ofisini mwa Mzee Majoka. Ni baada ya Majoka kumkumbusha Ashua kuwa alimpa kazi katika Majoka and Majoka Academy akakataa. Ashua anadai kuwa wanafunzi katika shule hizo hawafuzu, huwa makabeji kwa kudungana sumu ya nyoka. Majoka anajitete na kusema kuwa hizo ni tetesi tu. hakuna ushahidi.
    2. Fafanua mbinu mbili za lugha zilizotumiwa katika dondoo hii (alama 4)
      Balagha- Ushahidi itatoka wapi kama kipanga ndiye hakimu kwenye kesi ya kuku?
      Jazanda- kipanga ni wenye uwezo wanaowakandamiza wanyonge
      Kuku ni mwananchi mnyonge
    3. Fafanua haki kumi na mbili za Wanasagamoyo na uonyeshe jinsi ziivyokiukwa (alama 12)
      Haki ya kuishi. Majoka anapanga njama za kuwaangamiza wapinzani wake. Anamuua Jabali.
      Haki ya huduma bora kwa wananchi. Majoka anawakandamiza Wanasagamoyo. Tunu anamkumbusha Sudi kuwa walipokuwa chuoni walikula yamini kutetea na kulinda haki za wananchi (uk 18).
      Haki ya kufanya biashara. Majoka anafunga soko la Chapakazi ili alinyakue. Ashua anamweleza Majoka kuwa kufungwa kwa soko si haki kwani watu wengi wanalitegemea soko lenyewe(uk 25).
      Ashua anaitetea haki ya wanafunzi kupata elimu bora. Anaeleza kuwa wanafunzi katika Majoka and Majoka Academy huwa makabeji (mbumbumbu) na wamenyimwa haki ya elimu bora (uk 26).
      Haki ya ndoa na familia. Majoka hana uaminifu wa ndoa. Anataka mapenzi na Ashua ambaye ni mke wa Sudi. Husda anatetea haki yake ya ndoa. Anapompata Ashua na Majoka, anadai kuwa ataua mtu (uk 26).
      Haki ya kupata fidia. Majoka anawazungusha Tunu na mamake katika mahakama baada ya kifofo cha babake Tunu. Tuna anaitetea haki yake ya kuelimishwa na Majoka baada ya babake kuaga dunia akifanya kazi katika kampuni yake Majoka. Anatetea haki ya kufidiwa kwa hasara waliyoipata (uk 44).
      Haki ya kutoumbuliwa. Tunu anamuumbua Majoka kwa kusema kuwa kampuni zao ni za kihuni. Anasema kuwa kina Majoka wanawachinja watoto wa watu. Majoka anaitetea haki yake kwa kumweleza Tunu kuwa mtu kusingiziwa kosa lisilo lake ni hatia (uk 43).
      Haki ya kufanya upendavyo. Sudi anakataa mradi wa kumjongea Majoka kinyago na kuchonga shujaa wa kike. Majoka na Kenga wanakiuka haki hii na kutumia mbinu zote ili kumfanya Sudi awachongee kinyago.
      Haki ya kupiga na kupigiwa kura. Majoka anawakandamiza wapinzani wake na kuwatusi Wanasagamoyo kwa kumfuata Tunu.Tunu anaeleza kuwa lengo lake ni kutetea haki za wengine wala si kutafuta kura (uk 45).
      Haki ya kupendwa. Majoka hampendi mkewe, Husda. Ashua anatetea haki za wanawe. Anamtaka Sudi awatafutie chakula na kuwavisha (uk 48).
      Haki ya lishe bora. Wanawe Sudi wanalala bila kula kutokana na umaskini wa Sudi na Ashua.
      Haki ya kuandaa maandamano. Wanasagamoyo wanaoandamana wanafurushwa na polisi.
      Haki ya afya njema na mazingira safi. Kuna uchafu kila mahali sokoni. Tunu anamfahamisha Mamapima kuwa kuuza pombe haramu ni hatia (uk 61).
      Haki ya usawa wa kijinsia. Majoka anatishia kuwachafua Husda na Ashua. Anasema kuwa mwanamke ni mwanamke tu. Husda anawatetea wanawake kwa kushauri kuwa wanaume wajidadisi na kuyachunguza upya mahusiano yao na wanawake wao (uk 76).

SEHEMU YA C
HADITHI FUPI: TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE
(Alifa Chokocho na Dumu Kayanda- Wahariri)
Jibu swali la Nne ama la Tano
MKUBWA

  1. “… Basi niache nitafute pesa. Nitauza cha kuuza…”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
      Haya ni maneno ya Mkubwa. Alikuwa akimwambia Mkumbukwa. Mkubwa amemtembelea Mkkumbukwa. Ni baada ya kupewa habari na kijana mmoja kuwa biashara ya unga hufanywa na viongozi na ina hela nyingi. Mkubwa anamwendea Mkumbukwa ilia pate ushauri wake. Mkumbukwa anamweleza Mkubwa kuwa mchafukoge kinachojalisha ni pesa wala si kisomo.
    2. Fafanua sifa zozote nne za mzungumziwa (alama 4)
      Ni mshawishi. Anafaulu kutumia ujuzi wake wa siasa kuwanasihi Wanamchafukoge kumchagua Mkubwa.
      Ni fisadi. Anakubali kushirikiana na Mkubwa katika uuzaji wa dawa za kulevya. Aidha, anawahonga Wanamchafukoge ili wampigie Mkubwa kura.
      Ni mwenye huruma. Baada ya kushikwa, anageuza msimamo wake na kujiondoa kwenye biashara ya dawa za kulevya. Anamwonya Mkubwa dhidi ya kuwadhulumu vijana. Anawahurumia vijana waliofungwa jela.
      Ni mwenye msimamo thabiti. Anapogundua hila za Mkubwa, anakataa kabisa kushiriki biashara yake ya dawa za kulevya.
    3. Fafanua athari ya vitendo vya mzungumzaji wa maneno haya na wenzake katika jamii     (alama 12)
      • Mzungumzaji ni Mkubwa. Vitendo vyake vinajikita katika ulanguzi wa dawa za kulevya. Dawa hizi zinaiathiri jamii (vijana) kwa njia zifuatazo.
      • Huwafanya vijana kutojielewa. Mkubwa akielekea pwani kununua pweza, aliwakuta vijana waliokuwa wamelaliana kutokana na kutumia unga. Walikuwa kama kuku na vifaranga walioona mwewe (uk 142).
      • Huwafanya vijana kupotoka kimaadili. Mmpjawapo wa vijana waliotumia unga anamtisha Mkubwa kwa upyoro wake. Anamuuliza kama wanakula kwake na kumuita ‘makande’. Mkubwa anakupuka mbio.
      • Huwafanya vijana kuwa na hisia zisizo za kawaida. Kijana mmoja anamtusi Mkubwa na kumlaumu kwa kumwangusha na ndege. Anasema kuwa alikuwa anakata kona anaenda kwa Obama.
      • Watu, hasa viongozi hutumia biashara ya dawa za kulevya ili kujitajirisha. Hujenga majumba makubwa, maduk ana kununua magari ya bei.
      • Viongozi wanatumia pasipoti za kidiplomasia kuepuka kusachiwa bandarini wala kwenye uwanja wa ndege. Hili huwawezesha kusafirisha dawa za kulevya zinazoiathiri jamii.
      • Tama ya mali inawafanya viongozi kuwaonga wapiga kura ili wachagulie, bila ya kujali kiwango chao cha elimu. Mkubwa anauza shamba ilia pate milioni kumi za kuwaonga wapiga kura.
      • Vijana wanaoshikwa baada ya kutumia dawa walizouziwa na wakubwa wanateswa. Wakiwa ndani hawana haki. Kula ni kifo, malazi ni kifo,kukoga ni kifo, kufua ni kifo, kila kitu ni kifo.
      • Dawa hizi zinasababisha ubaguzi mkubwa katika jamii. Viongozi matajiri wanaachiuliwa kwa ulanguzi wa dawa huku vijana maskini wakiendelea kukaa ndani. Mkubwa anafanya mazungumzo na mkuu wa polizi, Ng’weng’we wa Njagu na kesho yake Mkumbukwa anaachiliwa.
      • Dawa za kuelvya huwafanya watu kuwehuka. Katika ndoto yake, Mkubwa anawaona vijana wachafu wakifanyiana vitendo vichafu. Anawaona watu wamehamaki hawana raha. Wizi umezidi mitaani. Miongoni mwa viajana wale ‘wala unga’ ni watoto wake wa kiume. Anatoka mbio. Kawa chizi.

                                                            Au

  1. Jadili suala la uozo wa maadili katika jamii huku ukirejelea hadithi zozote nne katika diwani ya Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine (alama 20)
    Mapenzi ya Kifaurongo
    • Maadili ya walimu na wakufunzi yameanza kurora. Dkt. Mabonga ndiye mhadhiri. Dkt. Mabonga anawakata wanafunzi tamaa ya kukisoma Kiswahili. Hayajibu maswali wanayomuuliza kwa kuyaona kuwa maswali ya wanafunzi wa kidato cha kwanza. Aidha, anawataka wautumie msamiati wake ambao wanafunzi wengi wanauona kuwa usiku wa giza.
    • Chuoni, Dennis anakumbwa na tatizo kubwa la utabaka. Wanafunzi kutoka familia zenye nafasi walikuwa na simu za thamani, wengine walibeba vipakatalishi na iPad zao mikononi (uk 13) huku naye asiweze kupata hata chochote. Umaskini huu ulileta mpaka kati ya wanafunzi maskini na tajiri wasiweze kukaribiana.
    • Kuna mapenzi ya kiholela baina ya wanafunzi. Siku moja Dennis akiwa chumbani mwake baada ya kupika uji wa mahindi bila sukari kutokana na umaskini wake, Penina, binti yake Bw. Kitime, Katibu wa Kudumu katika Wizara ya Afya (uk 19) anabisha mlangoni pake.
    • Penina anamweleza kuwa lengo la kuja kwake ni kumtaka wawe wapenzi. Anamweleza hadharani kuwa kando na mapenzi ya wazazi, kuna mapenzi mengine anayoyakosa na anayataka kutoka kwake Dennis. Dennis anasita kujihusisha kwa mapenzi na msichana huyu wa kitajiri kwa kuhofu kutemwa tena; mapenzi ya kifaurongo.
    • Wanakuwa kwenye mapenzi. Mapenzi yao yanadumu kwa muda wa miaka miwili. Wanapomaliza chuo, wanahamia kwenye mtaa wa watu wa pato la wastani, Newzealand, licha ya kuwa hawajapata kazi. Wazazi wake Penina wanawalipia kodi.
    • Dennis anatafuta kazi kwa kila njia bila mafanikio. Anakosa kazi katika shirika la uchapishaji magazeti kwa kushindwa kujibu swali moja la kwanza.
    • Kukosa kazi kunamfanya Penina kumwamrisha asanye kila kilicho chake na aondoke. Akamfukuza na kumtaka aione nyumba yake paa. Mapenzi ya kifaurongo yakatimia mwisho wake

      Shogake Dada Ana Ndevu
    • Safia ni mwanawe Bw. Masudi na Bi Hamida. Yupo shule ya msingi akisubiri kufanya mtihani wa kujiunga na shule ya upili. Ni msichana hodari sana masomoni; kila mtihani akishika nambari ya kwanza.
    • Wazazi wake Safia, hasa Bi Hamida anamwonea mwanawe fahari na kujawa na kiburi kinachomfanya kuwasimanga wasichana wa wazazi wengine walioshindwa kujitunza kama Safia wake, aliyejitandaza ushungi na kujifunika hata awapo nyumbani. Bi Hamida anamhurumia Mkadi, mtoto wa Habiba Chechei (uk 29), tabia zake ni za dosari.
    • Safia anawaomba wazazi wake ruhusa wamkubalie amlete shogake; Kimwana, nyumbani kwao ili wadurusu naye   masomo. Wazazi wake wanamkubalia ombi lake.
    • Kimwana akawa yuaja amejitandaza kila mahali kama ilivyo desturi yao. Wazazi wake Safia wakawashauri wawe     wakijifungia ndani wanapodurusu ili wasisumbuliwe na watoto.
    • Siku zilipopita, Safia akaanza kubadilika na kutapika. Wazazi wake wakamshuku lakini wakaamua kuwa si vyema   kumwazia mtoto wao vibaya.
    • Kitendawili kiliteguliwa na Lulua – kidugu chake Safia. Kitoto hiki kilimweleza mamake kuwa siku moja Subira         alipokuja kucheza nao mchezo wa kujificha, alienda chumbani kwa dadake kujificha. Alimpata Safia amelala kitandani na shogake Kimwana; naye kimwana alikuwa na ndevu.
    • Simu ya mkononi ya Bwana Masudi ilipoita na kuipokea, anapata habari kuwa Safia kafariki katika kliniki alikoenda kuavya mimba.

      Mame Bakari
    • Hadithi hii inamhusu Sara. Anakumbuka kisa kilichomtokea zamani na kumwacha kwenye huzuni na uchungu. Alitamani jambo hili lisingekuwa la kweli.
    • Analikumbuka janadume lililomvizia siku moja akitoka darasa la ziada (twisheni), likamwangusha na kumbaka kisha likamwacha amezirai. Anapoamka ndipo anapogundua kuwa amebakwa.
    • Tokeo la kisa hiki ni kwamba Sara alipata ujauzito. Aliogopa kumwambia baba yake kwa kuhofia kukaripiwa na hata kufukuzwa nyumbani. Aliogopa kutengwa na kusemwa na jamii.
    • Aliwaza jinsi mwalimu mkuu angemfukuza shule. Aliwaza jinsi dunia ilivyobadilika na kumkandamiza mwanamke hata awe ndiye mdhulumiwa. Jamii inamkweza mwanamume licha ya ukatili wake.
    • Baada ya tafakuri, Sara anaamua kumdokezea rafiki yake, Sarina, kuhusu matatizo yake. Wanakubaliana kuyaweka siri hadi Sara atakapojifungua. Sarina anamhudumia Sara kwa moyo na ari wakisubiri siku iwadie ajifungue.
    • Siku moja Sara na Sarina walimhadithia Beluwa (dadake Sarina – daktari) kuhusu kisa cha Sara. Beluwa akaahidi kuwa akimhudumia Sara mara kwa mara. Aliahidi kuliweka jambo hili siri.
    • Siku moja Beluwa alimtaka Sara kufika hospitalini kwake kwa matibabu zaidi. Sara na Sarina waliandamana hadi       hospitalini ambako walimkuta babake Sara na mamake wakimsubiri.
    • Sara alipigwa na bumbuazi asijue la kufanya. Aligutuka hajielewi. Aliporudiwa na fahamu, babake anamnyamazisha na kumweleza kuwa kosa si lake. Anamtaka Sara ajifungue mtoto wa kike awe ‘Mame Bakari’, mkewe wa utani. Malipo yote ya kuutunza ujauzito wa Sara yaligharamiwa na babake hadi akajifungua.
    • Mtoto alipozaliwa kuliandaliwa sherehe. Watu wengi wakawa wanasherehekea mafanikio ya Sara. Mara kelele zikaanikiza kutoka nje. Sara alipotoka, alikuta ni lile janadume lililombaka limekabiliwa na umati. Anachukua tofali     kulimaliza lakini analihurumia. Ghafla, umati unalivamia na kuliangamiza.Nizikeni Papa Hapa
    • Suala la mapenzi ya kiholela miongoni mwa vijana limechacha. Otii amepelekwa hospitalini madaktari wakashindwa kumponya na kuamuru arudishwe nyumbani. Amekonda sana.
    • Wanachama wa Chama cha Watu wa Nyumbani wanakusanyika na kuanza kujadiliana jinsi ya kuchangisha pesa za kununua jeneza, mavazi ya kumvisha maiti pamoja na pesa za kukodisha magari ya kumchukua maiti hadi kwao Sidindi, karibu na Kisumu ilhali Otii angali hai. Otii anawaeleza kuwa anataka akifa azikwe palepale Kisumu Ndogo. Mwenyekiti wa Chama cha Watu wa Nyumbani anampuuza.
    • Pale kitandani Otii anaukumbuka wakati wake akiichezea Bandari FC. Alikuwa mchezaji hodari na tegemeo. Watangazaji wote wa kandanda walimwangazia. Aidha, aliichezea timu ya taifa, Harambee Stars.
    • Alicheza kwa kujituma hadi mambo yalipoharibika alipovunjika mguu kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza – Tanzania wakati wa mechi ya nusu fainali kuwania kombe la klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati. Alikuwa karibu kuwafunga wapinzani wake Yanga alipovunjwa mguu.
    • Baada ya kupona, Otii akaamua kuasi soka na kuanza kazi ya mshahara duni katika Halmashauri ya Bandari kutokana na kutelekezwa na serikali na Bandari FC.
    • Siku moja akiwa kwenye klabu, anadondokewa na Rehema Wanjiru na mwishowe wanakuwa wapenzi. Rafikiye Otii anamwonya dhidi ya wasichana warembo wa Mombasa. Otii anajilinganisha na nzi afiaye kidondani na kukiri kuwa hamwachi Rehema. Wanashiriki ngono isiyo na kinga.
    • Muda mrefu unapita bila Otii kuonana na Rehema wake. Baadaye anaelezwa kuwa Rehema alirudi kwao Meru; bila hata kumuaga. Aidha, anapata habari kuwa Rehema ni mgonjwa na muda mfupi baadaye anapata khabari za kifo cha Rehema.
    • Otii naye anaanza kuona dalili za ugonjwa wake. Hana udole. Anaendesha, vipele mwilini, kukohoa kusikokoma. Otii aliugua kwa miaka minne. Kabla ya kifo chake, alitoa kauli moja tu “Nizikeni papa hapa.”
    • Wanachama wa Chama cha Watu wa Nyumbani waliutia mwili wa Otii kwenye jeneza la kifahari na magari yakaanza safari ya kuupeleka mwili nyumbani kwao Sidindi. Gari linapofika Mtito Andei, kunatokea ajali mbaya inayosababisha kifo cha watu arubaini baada ya magari sita kusagikasagika. Mwenyekiti wa Chama cha Watu wa Nyumbani anaponea   bila jeraha lolote. Anajuta mbona hakuusikia wito wa Otii aliyesisitiza.

SEHEMU YA D
USHAIRI

MASWALI

  1. Lipe shairi hili anwani mwafaka. (Alama 1)
    ujuaji
  1. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili. (Alama 2)
    Mwandishi anadahamiria kuonesha na kuonya wanadamu dhidi ya kujifanya kuwa wajuzi wa kila kitu.
  1. Mwandishi anasema kuwa ujuaji ni nini? (Alama 2)
    Kujifanya watambua
    Kujibeba bila nia
  1. Taja tamathali za lugha zilizotumika katika shairi hili. (Alama 2)
    Takriri- ujuaji
    Tashihisi/ tashhisi/uhuishi- ujuaji biasharayo tafumua
  1. Fafanua uhuru wa ushairi alioutumia malenga. (Alama 3)
    Kuboronga/ kufinyanga sarufi- elimuni kubagua- kubagua elimuni
    Inkisari- misada- Misaada
    Lahaja- kidhili- kidhiri
  1. Weka shairi hili katika bahari mbalimbali. (Alama 3)
    Mathnawi- lina vipande viwili katika kila mshororo wa ubeti
    Mtiririko- vina vyake vyote, vya nadani na vya nje vinafanana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho
    Kikwamba- neno ‘ujuaji’ linarudiwarudiwa mwanzini mwa kila mshororo.
  1. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (Alama 4)
    Ujuaji ni mkatili kwani husababisha ubaguzi katika masomo na kufanya mali zako kupungua. Ujuaji si msingi wa mpango/ kudura wa/za Mungu. Mwanadamu atagundua kwamba ujuaji ni jambo kali.
  1. Vifungu vifuavyo vina maana gani katika shairi?
    Majitapa- maringo
    Gudurua- nguvu/ uwezo wa Mungu

SEHEMU YA E
FASIHI SIMULIZI
Maswali

  1. Tambua kipera hiki cha fasihi simulizi (alama 2)
    Majigambo
  2. Jinsia ya nafsi neni ni gani? (alama 2)
    Mwanamume- dume la ukoo mtukufu
  3. Eleza sifa zozote nane za kipera hiki cha fasihi simulizi (alama nane)
    1. Hutungwa na kughaniwa na mhusika mwenyewe.
    2. Hutungwa kwa usanii mubwa. Anayejigamba hutumia sitiari, vidokezi, ishara na urudiaji.
    3. Anayejinga husimulia tukio katika maisha yake.
    4. Aghalabu hutungwa na kughaniwa na mhusika mwanamume.
    5. Huwa na matumizi mengi ya chuku. Anayejisifu hujinaki kupita kiasi.
    6. Hutolewa kwa nafsi ya kwanza.
    7. Anayejigmba huweza kubeba baadhi ya vifaa vyake vya kazi kutegemea analojigamba kwalo.
    8. Majigambo aghalabu hutungwa papo kwa hapo.
    9. Anayejigamba hutaja usulib wake wa kinasaba.
    10. Wanaojigamba mara nyingi huwa walumbi au washairi wanaoelewa kwa kina wanalolitongoa.
    11. Maudhui makuu katika majigambo ni ushujaa.
  4. Fafanua umuhimu wa kipera ulichokitaja hapo juu katika jamii (alama 8)
    1. Hukuza ubunifu. Kadiri mtu anavyotunga na kughani ndivyo anavyoimarisha ujuzi wake wa kubuni mitindo mipya ya utunzi na uwasilishaji.
    2. Hukuza ufasaha wa lugha. Watunzi wengi wa majigambo huwa walumbi.
    3. Ni nyenzo ya burudani. Huongoa waliohudhuria sherehe ambapo yanatolewa.
    4. Hudumisha utu nautambulisho wa mwanamume katika jamii. Kupitia kwa majigambonwanaume walidhihirisha nafasi yao katika jamii.
    5. Ni nyenzi ya kuwafanya watu waheshimiwe. Mtu alipofanya kitendo cha kishujaa alijigamba ili aheshimiwe.
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI PAPER 3 - 2019 LANJET JOINT MOCK EXAMINATION.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest