KISWAHILI PAPER 2 - KCSE 2019 BAHATI MOCK EXAMINATION (WITH MARKING SCHEME)

Share via Whatsapp
  1. UFAHAMU (ALAMA 15)
    Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuatia

    Kitengo cha familia Kimesakamwa na wimbi kali la mabadiliko katika jamii. Namna ambavyo familia zinaendeshwa siku hizi ni tofauti na taratibu za azali. Waama hakuna kipenge cha maisha yetu ambacho hakijaathiriwa na kile ambacho kimekuja kujulikana kama ‘usasa’.

    Familia nyingi hasa katika maeneo ya mijini zinategemea sana watu wa kuajiri kuzishughulikia. Wazazi wengi hawatengi muda wa kukaa nyumbani na watoto ili kuwapa mwongozo na mapenzi yaliyo muhimu katika hatua mbalimbali za ukuaji wao. Wazazi huondoka mapema sana kwenda kazini na kurejea wakiwa wamechelewa mno. Watoto wao wakati huo huwa ama hawajaamka au tayari washalala. Kwa upande mwingine wapo wazazi ambao wanafanya kazi katika miji iliyo mbali na wanapokaa watoto wao au nchi za kigeni. Uhusiano kati ya mzazi na mtoto unakosa rotuba ya kuuneemesha na matokeo yake huwa ni vijana waliokosa mwelekeo. Walivyosema Waswahili, samaki hukunjwa akiwa bado mbichi. Tabia za watoto hawa zinaweza tu kuandaliwa katika maadili wakiwa wadogo.

    Tofauti kati ya wazazi, Pamoja na kuzaliwa kwa watoto nje ya ndoa kumebadilisha sura ya kitengo cha familia. Tofauti na zamani, hii leo utapata familia ambazo zinaendeshwa na mzazi mmoja – anaweza kuwa baba au mama tu. Ni kweli kwamba mtoto huhitaji malezi ya wazazi wote wawili. Mwongozo wa ushirikiano wa wazazi wote wawili ni imara na bora zaidi kuliko wa mzazi mmoja. Hii haimaanishi kuwa mtoto hawezi kulelewa vizuri na mzazi mmoja au vibaya na wazazi wote. Mtoto huweza kukosa huduma za kimsingi kwa kosa lisilo lake.

    Jukumu la jamii katika malezi ya watoto limepungua. Zamani malezi ya mtoto yalikuwa jukumu la kila mwanajamii. Mtoto alipothubutu kufanya kosa aliweza kuadhibiwa palepale na mwanajamii yeyote ambaye hakusita kujitwika jukumu la mzazi. Hata hivyo hali ni tofauti hii leo. Kumwadhibu mtoto wa mtu ni kichocheo tosha cha kuleta mfarakano usiokwisha katika jamii. Kila mtu anauchelea ugomvi wa kujitakia. Kila mtoto sasa anaelewa na vipimo vya mzazi wake na siyo vya jamii pana. Watoto nao wamegundua hili na hawakusita kujivika mavazi mawili tofauti, zuri mbele ya wazazi wao na jinginelo popote pasipo hao wazazi. Sasa wazazi wanaweza kuishi na wahalifu waliokubuhu bila kufahamu.

    Jambo lingine linalohusiana na hilo ni kutupiliwa mbali kwa tamaduni za Kiafrika. Ni kama jamii iliyotupa jongoo na mti wake. Si siri kuwa kuna masuala ya kitamaduni yaliyopitwa na wakati na ambayo inahalisi kuyapiga teke. Hata hivyo hatuwezi kukitia kila kipengee cha tamaduni zetu jalalani. Utamaduni wetu mbali na kututambulisha kama jamii, pia hutekeleza jukumu adhimu la kutuwezesha kuyaona mambo kwa mtazamo mmoja. Mtazamo huo mmoja ndio unaotupa umoja wetu. Hatuwezi kuwa na utangamano bila kuwa na uzi unaotufunga Pamoja. Maadili ya jamii hayawezi kubainika bila ya watu kuwa na Mwongozo na mtazamo mmoja kuhusu hali yao ya maisha.

    Familia za kisasa zina idadi ndogo za watu ikilinganishwa na hapo awali. Hali ngumu ya maisha imewasukuma watu katika kupata watoto wachache ambao wanaweza kumudu kuwalea vizuri. Nako kupungua kwa nafasi za ajira kunawazuia vijana kuingia katika nikahi mapema. Hali hii imechangia katika kupunguza idadi ya watu na pia kupunguza kasi za uchipukaji wa familia mpya. Hali ngumu ya maisha imepunguza upana wa familia kama ilivyokuwa awali. Siku hizi mtu na mkewe au mumewe Pamoja na watoto wanaikamilisha familia. Vikoa vimekwisha na kubaki kuwa kila mtu na lake. Wengine hawako tayari kuwatilia pondo ndugu zao.

    Maswali
    1. Kwa mujibu wa taarifa eleza matatizo yanayoweza kuikabili familia inayoendeleshwa na mzazi mmoja. (alama 2)
    2. Ni nini kiini cha utengano wa wazazi katika ndoa. (alama 1) Jadili nafasi ya utamaduni katika kuijenga jamii bora kwa kurejelea makala. (alama 2)
    3. Kwa nini familia za kisasa zina idadi ndogo ya watu? (alama 2)
    4. Taja huku ukitoa mifano ya tamathali zozote tatu za lugha zilizotumiwa katika taarifa. (alama 3)
    5. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa kifunguni. (alama 5)        
      1. Kimesakamwa –
      2. Mfarakano usiokwisha
      3. Wahalifu waliokubuhu
      4. Vikoa vimekwisha
      5. Kujivika mavazi mawili
  2. UFUPISHO
    Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yafuatayo

    Ki1a walimwengu wanapotajiwa kuwa shambulizi la kigaidi limetokea mahali fulani, wimbi la taharuki huwakumba. Mashambulizi ya kigaidi yameongezeka katika siku za hivi majuzi ambapo kundi Ia watu linalohisi kuwa linaonewa na kukandamizwa huitumia mbinu ya kushambulia kwa kuvizia, hasa kutumia mabomu au kuteka ndege na kutishia kuilipua na wakati mwingine kuilipulia angani. Kuna mabomu yaliyotegwa na kulipuka katika maegesho ya magari au kwenye vizuizi vya magari. Mengine hutegwa na kulipuliwa katika afisi, mikahawa, makao ya watu, n.k. Katika baadhi ya mashambulizi, wapo waliojitoa mhanga ambao hujilipua katika shambulizi

    Makundi ya watu wanaohasimiana ndio chanzo cha matendo ya kigaidi. Kundi linalohisi kuwa linaonewa au ambalo kweli linaonewa na ambalo ni dhaifu kuliko lile jingine, hufanya juu chini kushambulia kisirisiri. Nia ni kulipisha kisasi kwa jambo wanalohisi wamehiniwa. Kwa kuwa kundi hilo hudhani kuwa dhaifu halina njia wala uwezo wa kuyakabili moja kwa moja matendo waliyotendewa au wanayoendelea kutendewa, njia ya pekee, kwa maoni yao, huwa hii ya kushambulia kwa kushitukiza. Kiini cha uonevu kinaweza kuwa dini, uchumi, maamuzi ya kisiasa au jambo lingine lolote lile. Kinachobainika katika suala zima Ia mashambulizi ya kigaidi ni kuwa lipo jambo ambalo linazikera nyoyo za kundi fulani Ia watu walio wanyonge ambao huona kuwa njia ya pekee ya kudhihirisha hisia zao ni kupitia mashambulizi ya aina hii.

    Mashambulizi ya aina hii yana athari zake nyingi. Kuna watu wanaouawa na wengine wengi kulemaa. Maisha ya watu hawa au jamaa zao wanaowategemea hubadilika na kujaa mvurugano uliokithiri. Kuna watoto ambao ndoto zao za kupata elimu zimetumbukia nyongo baada ya wazazi wao kuzikwa hai katika vifusi. Mbali na kukosa elimu na mahitaji mengine ya kimsingi, watoto hawa hupatwa na matatizo ya kisaikolojia baada ya kuona maafa yaliyowafika wavyele wao. Hata wale wanaosalimika kutoka kwenye vifusi hivi hawaishi kuandamwa na majinamizi yasiyoisha.

    Mashambulizi ya kigaidi hayaathiri tu watu pamoja na kuharibu mali ya thamani ya lukuki ya pesa. Zipo athari nyingine hasi ambazo hudhihiri. Kwa mfano usalama wa nchi huwa mashakani. Wananchi na wageni vilevile hujihisi kuwa dhaifu na dhalili katika nchi illyovamiwa. Serikali husika hujikuta katika shutuma kwa kushindwa kutambua mipango hiyo mapema na kuzuia hasara ya nyoyo na mali. Aidha, jamii ya kimataifa huiona nchi hiyo kama yenye kukosa usalama na hivyo kuwaonya raia wake dhidi ya kuizuru. Iwapo nchi husika inategemea utalii kama kitega uchumi muhimu, basi hukosa wateja na waajiriwa katika sekta hii kupigwa kalamu.

    Tatizo la ugaidi si Ia nchi moja au mataifa fulani mahususi wala hakuna nchi au taifa linaloweza kudai kuwa haliwezi kukabiliwa na tishio la kigaidi. Kuanzia Dar es Salaam, Nairobi hadi New York na London au hata Cairo hadi Riyadh na Baghdad, sote tunakabiliwa na tatizo hili hili. Hakuna ajuaye lini, vipi au wapi magaidi wamedhamiria kutekeleza unyama huu

    Labda swali Ia kujiuliza ni kwamba; Je, upo uwezekano wa mwenendo huu wa kuwaangamiza watu, wengi wa wahasiriwa wakiwa wale wasio na hatia, kudhibitiwa na kumalizwa kabisa? Serikali za nchi mbalimbali zimejaribu kutumia uwezo wao wa kiuchumi na kiteknolojia ili kujaribu kuiondoa hali hii. Njia waliyoitumia ni ya mtutu wa bunduki ambapo makombora mazito yaliyogharimu pesa nyingi yanadondoshwa katika makao ya washukiwa. Hata katika hatua hii nayo, upo uwezekano mkubwa wa kuuawa watu wasio na hatia vilevile. Pia ni wazi kwamba uhasama unalipwa kwa uhasama na matokeo yake ni ulipizaji kisasi usioisha. Amani inakuwa nadra. 

    Juhudi za ulimwengu kulaani vitendo hivi ni nzuri ila hazitoshi. Utumiaji nguvu kutafuta ufumbuzi wa kitendawili hiki si suluhisho. Kama wanavyoeleza wanasosholojia, kila kitendo kina sababu zake zilizofichama. Sababu hizo ndizo kichocheo cha vitendo vinavyojidhihiri. Hivyo basi jukumu lipo katika kutambua vichochezi vya mashambulizi na kujitahidi kuvitatua kwa njia ya mashauriano yaliyojengwa katika nia safi ya kuleta usawa na usalama duniani.

    Wapo watu wanaoona kuwa vitendo vya mataifa yaliyoendelea kwa nchi changa ndivyo kilele cha ugaidi. Watu wanaona kuwa tabia ya mataifa hayo yenye uwezo kiuchumi na kiteknolojia kuamua na kudhibiti sera na imani za nchi changa ni ugaidi uliokubuhu. Vikwazo hivi huwaacha viongozi hoi na wananchi kuteseka kufuatia ulazimishaji wa sera za kiuchumi na kisiasa zisizohusiana na mahitaji ya watu wa nchi husika wala kuambatana na mahjtajj ya nchi hizi. Hii ni hali inayoyatia mataifa yanayoendelea katika wasiwasi usioisha kutokana na dhiki zisizoisha kusababishwa na mataifa ya kigeni.

    UFUPISHO
    1. Kwa kutumia maneno yasiyozidi 80, fupisha aya ya pili, tatu na nne. (alama 10)
      alama1, mtiririko
    2. Eleza njia zinazotumiwa na mataifa ulimwenguni kupambana na ugaidi. (Maneno 40) alama 5; 1 ya mtiririko

  3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1.  
      1. Taja vigezo viwili vya kuanisha irabu. (alama 1)
      2. Tofautisha sauti zifuatazo.(alama.2)
        /a/ na /i/
        /e/ na /o/
    2. Ainisha aina za vivumishi katika sentensi ifuatayo.(alama. 2)
      Mwalimu mzee alitufundisha vizuri ile mada ngumu.
    3. Eleza maana ya kirai. (alama.1)
    4. Tunga sentensi iliyo na kirai kivumishi na kirai nomino chenye muundo wa W+ V (alama 1)
    5. Andika sentensi hii upya bila kubadilisha maana ukitumia “O” rejeshi. (alama 2)
      Mwanafunzi alitumwa nyumbani juzi na hajapata karo hadi leo.
    6. Badilisha sentensi ifuatayo iwe katika hali ya udogo wingi.
      Kono lake lilivimba baada ya kuumwa na jibwa.                        (alama 2)
    7. Tunga sentensi iliyo: (alama 3)
      Kitenzi kishirikishi kikamilifu
      Kivumishi kimilikishi nafsi ya pili wingi
      Kiwakilishi cha nafsi ya tatu tegemezi wingi.           
    8. Kanusha sentensi ifuatayo kisha ueleze maana yake katika hali kanushi (alama 2)
      Angeongoza darasa lake, angepewa tuzo.
    9. Onyesha sehemu za kisarufi katika neno lifuatalo. (alama 2)
      Kililiwa
    10. Kanusha katika hali timilifu wakati uliopita.
      Kamati ya uchaguzi iliandaa ripoti kuhusu utovu wa nidhamu shuleni. (alama 2)
    11. Changanua kwa kutumia mchoro wa matawi
      Hatukuondoka na yeye japo tulirudi naye.                                 (alama 4)
    12. Tumia kiambishi KA katika sentensi ili kuleta dhana ya: (alama 2)
      1. Wakati usiodhihirika
      2. Kuonyesha matokeo yanayosababishwa na kitendo.
    13. Chane kwa mtama_________________ kwa udongo.          (alama 1)
    14. Eleza maana ya fungu tenzi. (alama 1)
    15. Taja aina mbili za fungu tenzi. (alama.2)
    16. Geuza sentensi hii hadi usemi halisi.
      Wanakijiji walikuwa wanataka kujua iwapo vipakatalishi vya shule za msingi vingeweza kuinua kiwango cha elimu.                                                            (alama 3)
    17. Eleza maana ya yambwa.   (alama 1)
    18. Tunga sentensi iliyo na: shamirisho kipozi na chagizo cha kiasi kamili. (alama.2)
    19. Tunga sentensi kwa kutumia kiunganishi cha wakati.(alama 2)
    20. Andika visawe vya maneno yaliyopigigwa mstari . (alama 2)
      Tulienda kusali siku ya Jumapili.
  4. ISIMU JAMII
    Eleza changamoto zinazokumba ukuaji wa lugha ya Kiswahili nchini Kenya.                        ( alama 10)


MARKING SCHEME

UFAHAMU

  1.  
    1. - Mtoto anaweza kukosa huduma za kimsingi
      - Watoto hukosa mwelekeo
      2x1=Alama 2
    2. Tofauti kati ya wazazi/wazazi kutoelewana katika ndoa 1x1 = Alama 1
    3. – Utamaduni huwezesha jamii kuyaona mambo kwa mtazamo mmoja.
      - Hutuwezesha kuwa na umoja
      - Hututambulisha Kama jamii
      - Hukuza maadili miongoni mwa wanajamii
      Zozote 2x1 = Alama 2
    4. - Kwa sababu ya hali ya ngumu ya maisha inayowafanya watu kupata watoto wachache   wanaoweza kumudu kuwalea
      - Kupungua kwa nafasi za ajira huwazuia vijana kuingia kwa nikahi mapema.
      2x1 = Alama 2
    5. Misemo – kuingia katika nikahi →kuolewa
      Methali – samaki hukunjwa akiwa bado mbichi
      Tashhisi – kitengo cha familia kimesakamwa na wimbi kali la mabadiliko
      3x1 = Alama 2
    6.  
      1. Kimesakamwa – kimesongwa / kimekabiliwa sana.
      2. Mfarakano usiokwisha – ugomvi usio na kikomo
      3. Wahalifu waliokubuhu – wahalifu / watenda maovu waliobobea / waliozoea
      4. Vikoa vimekwisha – utangamano / ujamaa umekwisha
      5. Kujivika mavazi mawili – Kuwa na tabia aina mbili – nzuri na mbovu
        5x1 = Alama 5.
  2. UFUPISHO
    1. - Makundi ya watu wanaohasimiana ndio chanzo cha ugaidi.
      -Nia huwa ni kulipiza kisasi kwa vile kundi moja hujihisi kuwa dhaifu.
      - Kiini cha uhasama huwa dini, uchumi au siasa
      - Mashambulizi haya huwa na athari nyingi k.v.
      -Watu kuuawa
      -Ulemavu
      -Kuvuruga maisha ya watu
      -Elimu huvurugwa
      -Matatizo ya kisaikologia
      -Kuharibu mali
      -Usalama wa nchi huwa mashakani
      -Utalii huathiriwa
      Hoja zozote 9 x1 = 9
      Utiririko 1x1 = Alama 1
    2. -Njia zinazotumiwa kupambana na ugaidi
      -Kutumia mtutu wa bunduki / kushambulia magaidi
      -Kulaani vitendo vya kigaidi
      -Kujaribu kutambua vichochezi vya mashambulizi na kujaribu kuvitatua kwa mashauriano
      -Kuwekewa vikwazo kwa mataifa yaliyo na magaidi
      4x1 = Alama 4
      Utiririko = Alama
  3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. Taja vigezo viwili vya kuanisha irabu. (alama 1)
      mkao wa midomo
      sehemu ya ulimi kinywani
    2. Tofautisha sauti zifuatazo.(alama.2)
      /a/ na /u/
      /a/ ni sauti ya chini kati ilhali /u/ ni sauti ya nyuma juu
      /a/ midomo hutandazwa ilhali /u/ midomo huviringwa
      /e/ na /o/
      /e/ sauti ya mbele kati /o/ sauti ya nyuma kati
      /e/ midomo hutandazwa /o/ midomo huviringwa
    3. Ainisha aina za vivumishi katika sentensi ifuatayo.(alama. 2)
      Mwalimu mzee alitufundisha vizuri ile mada ngumu.
      Mzee – kivumishi jina, ile- V kionyeshi/ kiashiria, ngumu- sifa,
    4. Eleza maana ya kirai. (alama.1)
      fungu la maneno lisilo na muundo wa kiima kiarifa au kipashio cha kimuundo cha sentensi ambacho hakiwasilishi maana kamilifu.
    5. Tunga sentensi iliyo na kirai kivumishi na kirai nomino chenye muundo wa W+ V (alama 1)
      Mwanafunzi yule mwerevu alisoma kile kizuri.
                        Kirai kivumishi      kirai nomino(W+V)
    6. Andika sentensi hii upya bila kubadilisha maana ukitumia “O” rejeshi. (alama 2)
      Mwanafunzi alitumwa nyumbani juzi na hajapata karo hadi leo.
      Mwanafunzi aliyetumwa nyumbani juzi hajapata karo hadi leo.
    7. Badilisha sentensi ifuatayo iwe katika hali ya udogo wingi.
      Kono lake lilivimba baada ya kumwa na jibwa.                     (alama 2)
      Vijikono vyao vilivimba baada ya kumwa na vijibwa.
    8. Tunga sentensi iliyo: (alama 3)
      Kitenzi kishirikishi kikamilifu.
      Mama angali nyumbani.
      Kivumishi kimilikishi nafsi ya pili wingi
      Vitabu vyenu vinahitajika.- mzizi –enu uwepo.
      Kiwakilishi cha nafsi ya tatu tegemezi wingi.        
      Wanasoma vitabu vyao. Kiambishi wa
    9. Kanusha sentensi ifuatayo kisha ueleze maana yake katika hali kanushi (alama 2)
      Angeongoza darasa lake, angepewa tuzo.
      Asingeongoza darasa lake, asingepewa tuzo.
      Maana: aliongoza vizuri na akapewa tuzo
    10. Onyesha sehemu za kisarufi katika neno lifuatalo. (alama 2)
      Kililiwa
      Ki- ngeli
      li- wakati uliopita
      l- mzizi
      iw - kauli
      a-kiishio
    11. Kanusha katika hali timilifu wakati uliopita.
      Kamati ya uchaguzi iliandaa ripoti kuhusu utovu wa nidhamu shuleni.     (alama 2)
      Kamati ya uchaguzi ilikuwa haijandaa ripoti kuhusu utovu wa nidhamu shuleni.
    12. Changanua kwa kutumia mchoro wa matawi
      Hatukuondoka na yeye japo tulirudi naye.                             (alama 4)
      S1 +U + S2
      S1---- KN--0
      KT-----T+H+W
      U---japo
      KN--O
      KT-------T+W
      BSBBDER1234
      Mwanafunzi achore mchoro wa matawi
    13. Tumia kiambishi KA katika sentensi ili kuleta dhana ya: (alama 2)
      Wakati usiodhihirika
      Mwalimu kaondoka.
      Kuonyesha matokeo yanayosababishwa na kitendo.
      Alisoma sana akapita mtihani
    14. Chane kwa mtama shumbi kwa udongo.    (alama 1)
    15. Eleza maana ya fungu tenzi. (alama 1)
      Ni kitenzi kilichoundwa kwa viambishi tofautitofauti.
    16. Taja aina mbili za fungu tenzi. (alama.2)
      fungu tenzi kama sentensi sahili
      fungu tenzi kama kishazi tegemezi
    17. Geuza sentensi hii hadi usemi halisi.
      Wanakijiji walikuwa wanataka kujua iwapo vipakatalishi vya shule za msingi vingeweza kuinua kiwango cha elimu.                                                       (alama 3)
      Vipakatalishi vya shule za msingi vitaweza kuinua kiwango cha elimu?” wanakijiji waliuliza.
    18. Eleza maana ya yambwa.   (alama 1)
      yambwa ni nomino tendwa au tendewa
    19. Tunga sentensi iliyo na: shamirisho kipozi na chagizo cha kiasi kamili. (alama.2)
      Mwanafunzi alisoma kitabu mara tatu.
      Kitabu- kipozi
      Mara tatu- chagizo cha kiasi
    20. Tunga sentensi kwa kutumia kiunganishi cha wakati.(alama 2)
      Mwizi aliwawaiba kondoo halafu akawachinja.
      Kisha,baadaye
    21. Andika visawe vya maneno yaliyopigigwa mstari . (alama 2)
      Tulienda kusali siku ya Jumapili.
      Kusali- kuomba, kuabudu
      Jumapili- dominika               
  4. ISIMU JAMII
    Eleza changamoto zinazokumba ukuaji wa lugha ya Kiswahili nchini Kenya.                      ( alama 10)
    1. Athari za lugha ya kwanza / kigeni.
    2. Kinadunishwa – Kiswahili huhusishwa na wasiosoma.
    3. Matumizi ya sheng’
    4. Ukosefu wa vifaa kama vile vitabu
    5. Vyombo vya habari.
    6. Ukosefu wa utafiti.
    7. Vipindi vichache shuleni.
    8. Sera mbovu ya lugha nchini
      Ondoa nusu ( ½ ) alama kwa kila kosa la hijai – hadi 4
      Ondoa nusu ( ½ ) alama kwa kila kosa la sarufi hadi makosa 4.
      (Hoja zozote 5x2)
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI PAPER 2 - KCSE 2019 BAHATI MOCK EXAMINATION (WITH MARKING SCHEME).


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest