KISWAHILI PAPER 3 - KCSE 2019 BAHATI MOCK EXAMINATION (WITH MARKING SCHEME)

Share via Whatsapp

SEHEMU YA A:TAMTHILIA

  1. Lazima 
    Pauline: Kigogo
    Majoka alitumia njia nyingi kudhibiti uongozi wake. Thibitisha ukweli huu. (alama 20)

SEHEMU B: RIWAYA
K.Matei: Chozi la Heri
Jibu swali la 2 au 3

  1. Wanawake wamesawiriwa kwa mtazamo chanya katika jamii ya chozi la Heri. Jadili ukweli huu kwa kutoa ithibati mwafaka.                                                      (alama. 20)
  1. “Ni mara ngapi mimi na babako husafiri na kukupagaza ulezi wa ndugu zako hawa? …umeweza kumuelekeza… katika kipindi hiki ambacho anatafuta utambuaji. Wewe pekee ndiwe dawa ya hasira … ya kivolkano. Bila wewe malezi ya hawa wadogo wako yangekuwa magumu.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.                                                                 (alama 4)
    2. Tambulisha mbinu tatu za sanaa zilizotumika katika dondoo hili.              (alama 3)
    3. Eleza sifa sita za mhusika “babako” aliyerejelewa katika dondoo hili.       (alama 6)      
    4. “Ulezi ni ujima”. Thibitisha kauli hii kwa kurejelea dondoo hili na riwaya yote kwa jumla. (alama 7)

SEHEMU YA C:HADITHI FUPI
Kochokocho A na D. Kayanda(Wah.): (Tumbo Lisilishiba na Hadithi Nyingine)
Jibu swali la 4 au 5 

  1. Jadili matatizo yanayokumba sekta ya elimu huku ukirejelea hadithi zozote tano katika diwani ya Tumbo Lisiloshiba. (alama. 20)                                                                     
  1. “…hata mapenzi yako yawe mazito namna gani…ni bora kuliko kasoro ya mapenzi.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (al. 4)
    2. Tathmini umuhimu wa mnenewa.     (al 6)
    3. Thibitisha ukweli kuwa mapenzi yanayorejelewa yaligeuka na kuwa mazito kuliko ilivyotarajiwa na yakawa na kasoro nyingi.   (al.10           

SEHEMU YA D: USHAIRI
Jibu swali la 6 au 7

  1. Soma shairi hili kisha ujibu maswali.

    Jicho, tavumiliaje, kwa hayo uyaonayo?
    Kicho, utasubirije, maonevu yapitayo
    Kwacho, lijalo na lije, nimechoka vumiliyo
    Naandika!

    Moyo, unao timbuko, maudhui tuyasikiayo
    Nayo, visa na mauko, wanyonge wayakutayo
    Kwayo, sina zuiliko, natoa niyahisiyo
    Naandika!

    Hawa, wanotulimiya, dhiki wavumiliayo
    Hawa, mamiya mamiya, na mali wazalishayo
    Hawa, ndo wanaoumiya, na maafa wakutayo
    Naandika!

    Hawa, sioni wengine,kwao liko angamiyo
    Hawa, uwapa unene, watukufu wenye nayo
    Hawa, bado ni wavune, kwa shida waikutayo
    Naandika!

    Bado, wawapo mabwana, wenye pupa na kamiyo
    Bado, tafauti sana, kwa pato na mengineyo
    Bado , tuling’owe shina, ulaji pia na moyo
    Naandika!

    Maswali
    1. Shairi hili laweza kuwekwa katika bahari zipi? Thibitisha kila jibu lako     (ala4)
    2. Eleza dhamira ya mshairi           (ala2)
    3. Onyesha mifano miwili ya uhuru wa kishairi jinsi ulivyotumika katika shairi     (ala2)
    4. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari.         (al.4)
    5. Tambulisha kwa mifano mbinu zozote mbili za sanaa katika shairi.    (ala2)
    6. Fafanua sifa za kiarudhi zilizotumika katika ubeti wa tano. (al.3)
    7. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika shairi. (ala3)
      1. Zuiliko
      2. Wavune
      3. Wenye pupa na kamiyo.
  1. Soma shairi hili kisha ujibu maswali.

    Amka!
    Uondoe utandu machoni
    Uone mtandao duniani
    Uchawi wa karne hii
    Uunganishavyo watu.

    Amka!
    Uwe mtu mpya
    Uabiri mtandao ulimwenguni
    Ukuvushe milima na mabonde
    Ujuane na watu.

    Amka!
    Uwe na yako anwani
    Udhibiti wavuti mkononi
    Uone na uonekane kote
    Uzungumze na watu
    Ufurahie malimwengu

    Amka!
    Uone huu ulimwengu
    Ulivyofanywa mdogo sasa
    Ulivyopea kimawasiliano
    Unganike na watu.

    Amka!
    Ukalie tarakilishi
    Uangaze usioyajua
    Uwasiliane kwa meme
    Uunganike na watu.

    Amka!
    Uone nukulishi
    Ubebe yako rununu
    Useme na ulimwengu
    Useme na watu

    Maswali
    1. Lipe shairi hili anwani mwafaka.       (al. 2
    2. Shairi hili ni la aina gani? Thibitisha.         (al.2
    3. Andika maneno manne yanayotaja teknolojia ya kisasa. (al.2
    4. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha ya nathari.  (al.4
    5. Eleza toni ya shairi hili.            (al.2
    6. Tambulisha nafsi neni na nafsi nenewa.     (al.2
    7. Tambulisha kwa mifano mbinu mbili za lugha katika shairi hili.   (al.2
    8. Ni nini maana ya vifungu vifuatavyo kama vilivyotumika katika shairi.                (al.4 )
      1. Uchawi wa karne katika shairi
      2. Ukavushe milima na mabonde

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI

  1. Eleza sifa nne za kimtindo zinazopatikana katika methali za Kiswahili.        (alama 8)
  2. Eleza mbinu tatu ambazo hutumiwa kuzua misimu.                                      (alama 6)
  3. Ni jukumu la jamii kudumisha fasihi simulizi. Dhihirisha.                             (alama 6)


MARKING SCHEME

  1. Njia alizotumia Majoka kudhibiti uongozi wake
    • Majoka anatumia vyombo vya habari kufanya matangazo yake: mwezi mzima wa kusherehekea uhuru pamoja na kuzaliwa kwake bila kujali watu watakula nini wasipofanya kazi.
    • Majoka anapanga mauaji ya wanaompinga. Ajali iliyosababisha kifo cha jabali, kiongozi wa chama cha Mwenge, (Uk. 35).
    • Majoka anatumia Vyombo vya dola( askari) kuwafurusha waandamanaji pamoja na kuwaangamiza. Vijana watano waliuawa wakati wa maandamano.
    • Anatangaza kuwa maandamano ni haramu huku akiwataka polisi kutumia kutumia nguvu zaidi. Kenga anasema, “Tangaza kuwa maandamano ni haramu, kisha uwaamuru maafisa wa polisi watumie nguvu zaidi.
    • Anapanga kutumia wahuni kunyamazisha watetezi wa wachuuzi wa Sagamoyo. Kenga anataka kumwangamiza Tunu anaposema, “Lazima tuwawekee vidhibiti mwendo na hatimaye tuwakomeshe kabisa.
    • Anatoa amri ya kuwazuia wahisani wa wapizani wake kwa kudai kuwa Sagamoyo ina uwezo wa kujitegemea. Majoka anasema, “Na hawa wafadhili wao nao lazima wavunje kambi zao. Sagamoyo twajiweza.
    • Majoka anatoza kodi zaidi ya inavyohitajika. Wachuuzi wanalipa kodi na kitu juu yake. Anaongeza mishahara ya walimu na wauguzi lakini anaongeza kodi kwa asilimia kubwa.
    • Wasamoyo hawapewi uhuru wa kumchagua kiongozi wanaomtaka. Anapanga kuwa mtoto wake Ngao Junior atatangazwa kuwa mrithi wake.
    • Majoka anazima uhuru wa vyombo vya habari. Anatoa amri ya kufungwa kwa Runinga ya Mzalendo kwa kutangaza moja kwa moja maandamano yaliongozwa na Tunu.
    • Anawaamrisha askari kuwatawanya waandamanaji kwa vitoa machozi na risasi.
    • Anamrisha lini watu watazikwa:Majoka anaagiza Chopi kuhakikisha maiti ya Ngurumo imezikwa siku hiyo hiyo kabla ya jua kutua kwani hataki kilio wakati wa sherehe.
    • Majoka anafuga chatu, nyoka hatari na wenye sumu kali ambao huzunguka na hata kuwaangamiza Wasagamoyo ovyo. Ngao Junior na Ngurumo wanaangamizwa na chatu.Kutoa amri za kikatili:Katika siku ya kusherehekea uhuru, Majoka alimtaka mkuu wa polisi, Bwana Kingi kuwapiga risasi Tunu na Sudi kwa kuandaa mkutano nje la Soko la Chapakazi.
    • Propaganda:Nyimbo za kizalendo zinachezwa katika redio baada ya matangazo maalum ni njia mojawapo ya kuwafumba macho Wanasagamoyo. Nyimbo hizi zinalenga kuwafanya wananchi kuona kuona kuwa Majoka anaendeleza demokrasia.
    • Kutumia vikaragosi: Ngurumo pamoja na walevi wenzake wanaimba wimbo wa kumsifu Majoka kule mangweni.
    • Kutumia uongo:Jamii ya Majoka inaeneza uongo kuwa wapinzani wote ni watu ambao si wazaliwa wa jimbo la Sagamoyo na wanapaswa kuhama. (Uk 51-52).
    • Kutoa chatu kama kafara: Baada ya kifo Ngurumo, Majoka anamweleza Chopi kuwa lazima chatu mmoja atolewe kafara ili watu wajue kuwa usalama upo.
    • Kutumia wahuni kueneza uvumi:Majoka anatumia wahuni kueneza uvumi kuwa Sudi na Ashua ndio wanaowinda nafsi ya Tunu.
    • Kuchagua mashauri kutoka familia: Mashuri wake mkuu Bwana Kenga alikuwa ni binamu yake. Alikuwa nanamtumia kushawishi wasagamoyo kama Sudi ili wakubali matakwa yake.
    • Kumia vitisho:Alitishia Tunu, Sudi na Ashua walipoenda ofisini mwake.
    • Kupanga mauaji ya wapinzani: Majoka anapanga njama ya kuua Tunu ingawa kwa bahati yake Tunu, Chopi aliyepewa maagizo hakuyatimiza ipasavyo. Majoka na Kenga wanakubaliana kumuua Chopi ili asitoe siri zao.
    • Kuwaua wapizani wake: Majoka alishiriki kwenye njama za kumuua Jabali ambaye aliuawa kwa ajali.
    • Kuwazawadi wafuasi wake: Kenga alikuwa amegawiwa kipande cha ardhi katika soko la chapakazi. Mkewe Ngurumo mama Pima alipewa kibali cha kuuza pombe haramu.
      (Zozote 20x1)
  2. Mtazamo chanya wa wanawake
    • Amekengeuka: Terry anamwonya Ridhaa mumewe kutoshiriki imani za kishirikina maana zilimtia wasiwasi bure.
    • Wasomi: Wanawake waliosoma ni kama: Apondi, Neema, Bi.Tamasha, Tamira, Umulkheri, mamake Zohali.
    • Wapenda masomo: Tila, Chandachema, Mwanaheri, Tuama, Rehema, Pete. Hata kama wengine hawakuweza kuendelea na masomo.
    • Wavumilivu:Mwekevu kustahimili matusi ya wanaume na kutengwa na wanawake alipokuwa anapigania uongozi. Chandachema kuvumilia mengi baada ya kifo cha nyanyake.Neema alivumilia kero za wanajamii waliomwonea kwa kukosa mtoto.
    • Faraja katika ndoa/mwamba katika ndoa: Licha ya mwangeka kuwa na jumba kubwa na kuishi na babake alihitaji mtu “…alihitaji mtu wa kumpembeja, kumliwaza…mwenzi katika uzazi na malezi (uk.110). Ridhaa anamhimiza Mwangeka kuoa tena. Kiriri alimsihi Annete asiondoke na kumwacha pweke. Lunga alikufa baada ya mwaka mmoja wa kuachwa na Naomi.
    • Mwenye bidii kazini: Mwekevu alitia bidii kazini mwake akiwa mkurugenzi wa shirika la Chemichemi. Kwa bidii yake watu walipata maji ya visima.
    • Mwenye bidii masomoni: Umulkheri alitia bidii masomoni na kuwa mhandisi. Wengine kama Neema, Apondi walitia bidii masomoni na kupata ajira.
    • Mwenye bidii ya kupata riziki na kukimu familia: Mamake Kairu alifanya biashara yake ya kuuza samaki. Halua mkewe Shamsi licha ya ugumu wa maisha alijibidiisha kupata riziki.
    • Amewajibika kama mzazi: Mamake Tindi na Lemi aliwaruhusu kwenda matembezini lakini akawaonya wasichelewe kurudi nyumbani. Walipokosa kurudi alienda kuwatafuta. Mamake Kairu alihakikisha mtoto wake ako shuleni na kusoma licha ya ukosefu wa fedha.
    • Amewajibika kazini: Selume hangeondoka hospitalini baada ya zamu yake kabla ya kumtembeza muuguzi mwenzake (Meko) kwa wagonjwa.
    • Amewajibika katika kuwadhibu watoto: Mamake Mwangeka na mamake Mwangemi waliwadhibu wana wao kwa kumuiga babu yao.
    • Mcha Mungu: Wanawake katika makundi mbalimbali ya kidini walihusika pakubwa katika ugavi wa chakula cha msaada kwa wahasiriwa wa vita vya baada ya uchaguzi. Walikuwa wa CWA, Women’s Guild, Mothers Union. Lily Nyamvula alikiri kuwa mwokovu (born again) na hakutaka mumewe kufanya kazi ya uanajeshi.
    • Watumishi wa Mungu kwa kuwa watawa: Mtawa Pacha, Cizarina na Anastacia ni watawa waliotumikia Mungu kila siku bila kuolewa.
    • Wakarimu/wahisani:Wanawake wajane walikuwa wameanzisha makao ya watoto mayatima ya Jeshi la Wajane wa Kristu. Waliwapa hifadhi watoto wenye mahitaji kama Chandachema.
    • Viongozi: Mwekevu alichaguliwa kama kiongozi wa Wahafidhina. Tamasha alikuwa Mwalimu mkuu wa shule ya Kilimo. Mamake Zohali alikuwa mwalimu mkuu wa shule ya upili.
    • Msiri: Mamake Kipanga hakumweleza mwanawe kuhusu babake. Mamake Sauna hakumwambia kwa muda mrefu kuwa Maya hakuwa babake mzazi.
    • Jasiri: mamake Kairu aliongoza wanawe kumzika mwanawe aliyefia mgongoni. Mwekevu alipigania uongozi kwa ujasiri mkubwa.
    • Mwenye utu: Wanawake kadhaa wameonyesha utu kwa kuwasaidia waliokuwa na mahitaji. Wao ni kama: Nyanyake Chandachema, Neema, Apondi, Mwalimu Dhahabu n.k.
    • Msamehevu: Umulkheri pamoja na nduguze walimsamehe mama yao Naomi na kuamua kumtafuta.
    • Hatibu mzuri: Rachel Apondi alitoa hotuba nzuri ili kuwahimiza walinda usalama kuwajibika zaidi.
    • Wenye adabu njema/busara: Selume aliongea akiwa mbali kabla ya kuingia kibanda cha Kaizari kwenye kumjulia hali mkewe na binti zao. Alijua kuwa vibandani hakukuwa na faragha.
      (Zozote 20x1)
  3.  
    1. Muktadha                                                                                                                       (al. 4)
      Maneno haya yalisemwa na Rachel Apondi. Alikuwa akimwambia mtoto wake wa kupanga Umulkheri. Walikuwa katika hoteli ya Majaliwa walipokuwa wakisherehekea siku yake Umu ya kuzaliwa. Apondi anamshukuru Umulkheri kwa kuchangia katika ulezi wa dadake Sophie aliyekuwa mwepesi wa hasira.
    2. Mbinu tatu za lugha                                                                                                    (al.3
      • Swali la balagha   “…kukupagaza ulezi wa ndugu zako hawa?”
      • Istiari-Ndiwe dawa ya hasira
      • Utohozi-Kivolkano (volcano) (3x1)
    3. Sifa za Mwangeka                                                                                                           (al. 6
      • Mcha Mungu: Anashukuru Mungu baada ya kupata Umu ambapo anaona ni binti wa kufidia mwanawe Becky aliyekufa kwa ajali ya moto.
      • Mvumbuzi:Anavumbua gari kwa jina Ngokoo ambalo Mwangeka anadai ndilo lilikuwa ka kwanza la Kiafrika.
      • Mwenye ukiwa na upweke: Anaishi kwa ukiwa na upweke nyumbani kwake kutokana na kifo cha mkewe na mtoto.
      • Mwenye msimamo thabiti:Licha ya kushawishiwa na mkwewe aache kazi ya uanajeshi kwa kuwa inahusisha uuaji, haachi kamwe.
      • Mzalendo:Anadhihirisha uzalendo wake kwa kutaka kuwahudumia watu wengi katika udumishaji wa amani kama mwanajeshi katika Mashariki ya kati.
      • Mwenye bidii:Anasoma kwa bidii mpaka akajiunga na chuo kikuu na kusomea shahada ya uhandisi.
      • Mwenye mapenzi ya dhati kwa babake na mtoto wake wa kupanga Umulkheri: Anamkumbatia babake kwa mapenzi baada ya kuwasili kwa ndege katika uwanja wa kimataifa wa Ndege wa Rubia.
      • Mtambuzi: anatambua kwamba babake amezeeka zaidi na kushabihiana na babu yake Mwangeka, Mzee Msubili.
      • Mtundu: Kwa utundu wa kitoto ananyang’anywa babake stethoskopu na kuitia katika shingo ya yeye Mwangeka, kisha anamlaza babake kama mgonjwa ili amtibu.
      • Mwenye wasiwasi alipokuwa mdogo: Ana mashaka na udhaifu kutokana na kutokuwepo na babake Ridhaa alipokuwa ameenda katika shughuli za kimatibabu.
      • Mlezi Mwema: Akishirikiana na Mke wake Apondi wanamlea Umulkheri, Sophie na Ridhaa na kumsomesha hadi anafanikiwa.
      • Mkarimu: alionyesha ukarimu mkubwa sana kwa Umulkheri. Aidha baada ya Dick naye kupatikana, Mwangeka na mkewe walimtunza pia kama mwana wao.
      • Mdadisi: Kabla ya kujenga jumba lake alifanya utafiti wa kutosha kuhusu ardhi aliyotaka kununua. (6x1)
    4. Ulezi ni ujima
      Ulezi ni ujima inamaanisha kuwa ulezi ni wa watu wengi wakishirikiana; kwa ujumla si wa mtu mmoja au wazazi pekee. Yaani kila aliyewajibika anapaswa kuchangia. ( Tanbihi:Mwanafunzi aonyeshe isipokuwa mzazi mtoto alilelewa na watu wengine)
      • Umulkheri alilelewa na mamake Naomi kwanza. Baadaye anachukuliwa kama mtoto wa kupanga na Mwangeka na Rachel Apondi ambao wanamlea na kumsomesha.
      • Umulkheri aliwalea dadake Sophie na kumshauri wakati wazazi wake walikuwa wamesafiri. Ulezi huu ulisaidia kudhibiti hasira za Sophie.
      • Chandachema alilelewa na jirani Satua kwa muda mfupi. Baadaye akatunzwa na nyanyake. Nyanyake alipoaga akajikuta akillelewa na Tenge na mke wake Kimai. Mwishowe alijipata katika makao ya watoto ya Jeshi la Wajane wa Kristu akilelewa na wasimamizi wa shirika hilo.
      • Zohali alilelewa na wazazi wake na alipotoroka nyumbani alilelewa na Mtawa Pacha aliyemtoa katika aibu ya kukaa mitaani.
      • Sauna alilelewa na mamake na baba wa kambo Maya bila kujua kuwa si babake mzazi.
      • Mwaliko alilewa na dadake Umu baada ya mamake kuondoka.Baadaye akalelewa na watawa wa Benefactor kama Anastacia. Mwishowe akalelewa na Mwangemi na mkewe Neema.
      • Mwangeka na Mwangemi waliadhibiwa na babu yao Mwimo msubili kwa sababu ya kumuiga. Babu anahusika na malezi ya wajukuu wake na kuwaadabisha.
      • Mwalimu Dhahabu alichangia kaika ulezi wa mwanafunzi wake Umu. Alimshauri awe makini darasani. Pia alimkutanisha na wazazi wake wa kupanga.
      • Pete alilelewa na nyanyake baada ya wazazi wake kutengana kwa sababu baba alisingizia kuwa si mtoto wake kwani hafanani naye.
      • Cynthia analelewa na Neema baada ya wazazi wake kufariki. Anamlea kama mtoto wake.
      • Riziki Immaculata, kitoto kilichookotwa na Neema kikiwa kimetupwa njiani kinapelekwa katika makao ya watoto ya Benefactor na kuanza kulelewa na Mtawa Cizarina. (7x1).

        Hadithi fupi
  4. Matatizo yanayoathiri sekta ya elimu
    Mwalimu mstaafu
    • Watoto wasioelewa masomo bado kushinikizwa kuendelea na masomo na walimu wao. Kipawa cha Jairo kingegunduliwa mapema na aelekezwa na kushauriwa ipasavyo. Mwalimu Mosi alimshauri aendelee na masomo licha ya kwamba hakuwa anaelewa.
    • Wanafunzi kupewa matumani yasiyo na msingi. Jairo alipewa matumaini kuwa ujinga wake utaisha na aweze kupata mia kwa mia.
    • Wanafunzi kuwalaumu walimu kwa matatizo wanaojiletea. Jairo anamlaumu mwalimu Mosi kwa sababu ya ufukara wake ambao umesababishwa na ulevi.
    • Wanafunzi kupuuza ushauri wa mwalimu na kujipata kwa matatizo. Jairo alipuuza ushauri wa Mwalimu Mosi. Alishauriwa aepukane na ufuska lakini akadida.
    • Wanafunzi kufukuzwa shuleni kwa kukosa vifaa muhimu. Binti wa Jairo Sabina alifukuzwa shuleni kwa kukosa vitabu vya hisabati. Mwalimu Mosi alienda mjini ili akanunue. Hii husababisha muda wa masomo kupotea.

      Mapenzi ya Kifaurongo
    • Wazazi kukosa pesa za kugharimia mahitaji ya wanafunzi. Dennis Machora alikosa chakula na mavazi mazuri akiwa chuo kikuu.
    • Wanafuzi kujihusisha na mapenzi ya uongo wakiwa chuoni: Dennis alidanganywa na Penina na kukubali kuwa mpenzi wake wakiwa chuoni lakini baadaye akafukuzwa kama mbwa alipokosa kazi. Mapenzi kama haya hupoteza muda wa wanafunzi.
    • Ukosefu wa ajira:Wanafunzi kusomeshwa masomo yanayowaelekeza kupata kazi za kiofisi wala sio kujiajiri. Dennis alitafuta kazi aliyosomea kwa miaka kadhaa bila kupata.
    • Wahadhiri wasiowajibika: Badala ya Dkt Mabonga badala ya kuwajibika kuyajibu maswali ya wanafunzi anawatusi. Anatumia lugha changamano ambayo baadhi ya wanafunzi hawaelewi.
    • Wanafuzi wazembe: Katika kujibu swali la mwanafunzi Dkt. Mabonga anaashiria kuwa baadhi ya wanafunzi ni wazembe “kupiga ubwete” kwani wengine hawataki kufanya utafiti ili waelewe alichokuwa anasema mwalimu. Wanataka waelezwe kila kitu kama watoto. “Wanafunzi wa chuo kikuu si watoto” (uk. 14).
    • Wanafunzi kutoka tabaka la chini kujitenga. Hawataki kutangamana na wengine. Dennis anaingiliana na wanafunzi wengine kwa nadra sana.

      Shogake Dada ana Ndevu
    • Wanafunzi wanafiki wanaodanganya wazazi wao. Safia anadanganya wazazi wake ili Kimwana akubaliwe wadurusu pamoja. Badala ya kusoma walikuwa wanajihusisha na mapenzi.
    • Wanafunzi kujihusisha na mapenzi kiholela: Safia na Kimwana wanajihusisha na mapenzi huku wakisingizia kuwa wanasoma.
    • Wanafunzi kufa huku wakijaribu kuavya mimba. Safia alienda kiliniki kuavya mimba lakini akafa.
    • Wanafunzi kutumia dini kufunika uovu wao. Safia alikuwa anajifunika gubigubi na kuacha macho pekee hata akiwa ndani mwa nyumba. Kimwana naye alikuwa anavaa buibui ili kuficha jinsia yake.
    • Wazazi kutokuwa makini kuchunguza wanayofanya watoto wao. Bwana Masudi na Bi. Hamida hawakuwa makini kuhakikisha kama kweli Safia walikuwa wanadurusu.
    • Wazazi kuamini watoto zaidi katika maswala ya masomo yao bila uhakika. Safia alifaulu kuwadanganya wazazi wake.

      Mtihani wa Maisha
    • Wafunzi kukata tamaa ya kuishi baada ya kufeli mtihani:Samueli anafanya jaribio la kujiua baada ya kukosa kufaulu katika mtihani wake.
    • Wanafunzi wanaodaiwa karo hawapewi matokeo ya mtihani: Mwalimu mkuu wa shule alikosomea Samueli alikuwa na daftari iliyokuwa na majina ya wale waliodaiwa na shule ambao hawangepata matokeo yao.
    • Wanafunzi kutozingatia masomo: Shuleni Samueli hakuzingatia masomo. Alikuwa anaitwa na wanafunzi wengine “Rasta” kwa sababu ya mahoka yaani vituko vyake.Hajui mito katika bara la Afrika iko katika sehemu ipi. Anajidanganya kuwa anajua. (uk.135)
    • Wanafunzi kuwadanganya wazazi kuhusu matokeo ya mtihani: Samueli hakusema ukweli kuhusu matokeo yake lakini alidanganya wazazi wake.
    • Wazazi kuwaona wanafunzi walioanguka mtihani kama bure na wasio na faida. Wanashindwa kuwashauri. Babake Samueli anamtusi Samueli. “Anafaida gani huyu…sikuzaa mwana nilitoa maradhi tumboni.”

      Mame Bakari
    • Wanafunzi kutendewa uhalifu/kubakwa: Sara alibakwa siku moja jioni alipokuwa anatoka shuleni. Hii ni ishara ya ukosefu wa usalama kwa wanafunzi.
    • Masomo ya ziada/twisheni:Aghalabu masomo haya huwa yanaripiwa na huweza kuwa mzigo kwa wazazi wengine. Pia masomo haya hufanywa jioni wakati watoto wengine wameenda nyumbani.Hii huhatarisha usalama wa mwanafunzi. Sara alibakwa alipokuwa anatoka masomo ya ziada.
    • Mimba za mapema: Baada ya kubakwa Sara alipata mimba na hili lilisababisha kukatiza masomo yake pengine kwa muda.
    • Msongo wa mawazo (stress): Sara baada ya kugundua kuwa ni mja mzito alikuwa anajifungia chumbani na kulia na kuomboleza kwa sababu ya msongo wa mawazo.
    • Kufukuzwa shuleni kwa sababu ya ujauzito: Kulingana na maelezo ya Sara wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shuleni walifukuzwa. “Hii ni skuli ya wanafunzi, mama, sio wazazi” angeambiwa Sara na Mwalimu mkuu.                                                 (Hoja zozote 20x1)
  1.  
    1. Muktadha wa dondoo hili
      Mnenaji ni Dadi alikuwa anamwambia Kidawa katika hadithi ya Masharti ya Kisasa. Alikuwa akimjibu wakati Kidawa alimjia na kumuuliza iwapo kama angeweza swala la mapenzi. Dadi alikuwa ametafuta mapenzi kwa Kidawa kwa siku nyingi lakini akakataa.
    2. Umuhimu wa Kidawa
      • Anawakilisha mwanamke wa kisasa ambaye anataka kuolewa lakini kwa masharti.
      • Mfano wa wanawake wa kisasa wanaoweza kufanya kazi usiku na mchana na anayependa mitindo ya mavazi ya kisasa.
      • Ni mfano wa wanawake wenye msimamo thabiti. Tokea mwanzo alimwambia Dadi yeye ni mwanamke wa kisasa na hakubadilisha msimamo huo.
      • Ni kieleleza cha wanawake wanaoamini kuwa lazima wawe na mchango katika kutwalia jamii hata kama itawabidi wafanye kazi usiku.
      • Ni mfano wa wanawake wenye bidii katika maisha. Anafanya kazi za nyumbani, ya umetroni na mchana anauza bidhaa.
      • Ni kielelezo cha wanawake waaminifu katika ndoa licha ya kuwa alikuwa anafanya kazi usiku wakati mwingine. Alihiari kujiuzulu wakati aliona ndoa yake iko hatarini.
      • Ni mwangwi wa mabadiliko katika ndoa. Anadhihirisha kuwa siku za mwanamke kuonewa na kunyanyaswa zimeisha.
    3. Mapenzi kuwa mazito (kuwa na ugumu)
      • Masharti ya kidawa yamlemea Dadi anashindwa kufanya kazi za nyumbani. Aiona kuwa kazi za nyumbani zilipaswa kuwa za mke.
      • Kwa sababu ya kumshuku mkewe Dadi alishindwa kuongea na mkewe kuhusu wasiwasi aliokuwa nao.
      • Fasheni za kisasa na kujipondoaalikopenda Kidawa zilimfanya Dadi kuwa na wasiwasi kwamba anafanya hivyo ili afurahishe wanaume wengine.
      • Maneno ya “kutembeza bidhaa” mitaani ilimuudhi sana Dadi kila wakati Kidawa alipoyatumia.
      • Dadi alishindwa kula chakula alichoandaliwa na Kidawa kwa sababu alikuwa anafikiria jinsi mkewe anavyomwendea kinyume.
      • Wakati Kidawa alimuuliza Dadi kama anapendeza baada ya kuvaa, Dadi alishindwa kumjibu. Hakutaka kumsifu mkewe kwani alidhani anaenda kustarehe na wanaume wengine.
      • Dadi alichukizwa na tabia ya mkewe kusimama na kuongea na wanaume wengine
      • Kanzu ya Kidawa kumfika magoti Dadi aliona itawafanya wanaume wengine kumtumbulia macho kwa kumtamani. Kidawa aliamini mwanamke ana haki ya kuvaa anavyopenda.
      • Kidawa alimkashifu mumewe kwa kutofuata masharti ya ndoa na hata akikumbushwa hujifanya hayafahamu.
      • Kidawa anamkashifu Dadi kwa kusususia kula chakula na kukosa kuondoa vyombo juu ya meza.
      • Dadi alimnyamazia mkewe baada ya kukashifiwa kutofuata masharti ya ndoa.
      • Dadi alienda hadi shuleni anakofanya kazi ya umetroni mkewe ili kumchunguza kama alikuwa na uhusiano na mwalimu mkuu.
  1. Ushairi
    1. Tarbia   
      • Lina mishororo minne katika kila ubeti
      • Msuko  -Kibwagizo kimefupishwa
      • Ukara    -Vina vya nje vinatiririka katika beti zote ilhali vya ndani havitiririki.
      • Kikwamba           -Katika beti 3-5 neno moja ndilo linaanza kila mshororo.
      • Sakarani               -Kuna bahari kadhaa katika shairi.
    2. Kuwahimiza watu (hasa wanyonge) wainuke na kupinga maovu na maonevu wanayofanyiwa na matajiri wenye uwezo.
    3. Inkisari km vumuliyo-kuvumilia manaandika.
      Mazida kurefusha k.m angamiyo,vumiliyo n.k
      Tabdila k.m mamiya dadala ya mamia
    4. Hawa wanaotulimia wanavumilia dhiki
      Wao ni wengi na ndio huzalisha mali.
      Wao ndio wanaoumia na kupata mateso/taabu
      Wanayokumbana nayo.Ninaandika /ninasema
    5. Takriri-hawa,bado,mamiya.
      Balagha-uyaonaje?
      Inkisari-Hawa,nd
      Kinaya watukufu wenye nayo
    6. Kuna mishororo minne
      Kuna vipande vitatu katika mishororo ya kwanza mitatu na kimoja katika kibwagizo
      Vina vinatiririka/vinafanana
      Mizani 
      2,-6-8
      2-6-8
      2-6-8
      4
    7.  
      1. Cha kunizuia /kizuizi/kizingiti/uogozi/hofu/pingamizi
      2. Wachovu/dhaifu/hafifu
      3. Walio na tama kubwa /walafi/mabwanyenye
  1. Ushairi
    1. Anwani mwafaka:
      • Teknolojia
      • Teknolojia ya kisasa
      • Njia mpya ya mawasiliano
      • Usasa katika kuwasiliana
    2. Shairi hili ni huru kwani halizingatii arudhi: (2x1)
      • Mishororo imetofautiana katika beti mbalimbali. Mf. Ubeti 3 unamishororo 6
      • Mizani inatofautiana katika mishororo katika beti mbalimbali.
    3. Andika maneno manne yanayotaja teknolojia ya kisasa:( 4x1/2)
      • Mtandao
      • Wavuti
      • Tarakilishi
      • Nukulishi
      • Rununu
      • Meme
    4. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha ya nathari.                             
      • Mshairi anasema kuwa tuzinduke tupate kunufaika kwa matumizi ya nukulishi. Tubebe simu za mikononi ili tuwasiliane na ulimwengu wote wa watu uliomo.
    5. Eleza toni ya shairi hili.                                                                                                                               (al.2
      • Toni ya kuamrisha. Anaarisha watu wazinduke na kutumia teknolojia.
    6. Eleza nafsi neni na nafsi nenewa.                                                                                          (al.2
      • Nafsi neni-mweledi wa teknolojia/mwenye ujuzi wa teknolojia ya kisasa.
      • Nafsi nenewa-mtu mpya/asiye na ufahamu mpana wa teknolojia
    7. Mbinu za lugha
      • Jazanda-Uchawi wa karne(uvumbuzi wa ajabu)
      • Takriri-Amka, useme
    8. Maana ya vifungu vifuatavyo:
      • Uchawi wa karne -uvumbuzi/ uundaji wa mambo mapya ya kiteknolojia katika karne hii.
      • Ukavushe milima na mabonde-Uweze kuwasiliana na wengine ulimwengu kote (pembe zote za dunia/walio mbali)
      • Uwasiliane kwa meme-Uwasiliane kwa barua iitwayo meme kwa kutumia mtambo wa talakilishi.
  1. Fasihi simulizi
    1. Eleza sifa nne za kimtindo zinazopatikana katika methali za Kiswahili.(alama 8)
      1. Takriri:urudiaji wa maneno
        Bandu bandu huisha gogo
        Haraka haraka haina Baraka
      2. Taswira (picha)
        Njia mbili zilimshinda fisi
        Paka akiondoka panya hutawala
      3. Sitiari:mithilisha kitu kimoja na kingine moja kwa moja
        Mgeni ni kuku mweupe
        Ujana ni moshi
      4. Kejeli/dhihaka
        Uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti
        Maskini akipata matako hulia mbwata!
      5. Balagha:maswali yasiyohitaji jibu kwa vile jibu ni bayana
        Umekuwa mumumenye kuharibikia ukubwani?
        Pilipili usiyoila yakuashiani?
        Angurumapo samba mchezo ni nani?
      6. Tashbihi:ulinganisho kwa kutumia kilinganishi
        Mapenzi ni kama majani popote penye rotuba hujiotea.
        Jambo usilolijua ni kama usiku wa kiza.
      7. Kweli kinzani:hali inayopingana
        Mpanda ngazi hushuka.
        Kuinamako ndiko kuinukako
      8. Chuku:maneno yasiyo ya kweli
        Polepole za kobe hufikisha mbali.
        Ukiwa makini utayaona macho ya konokono
      9. Kinaya;kinyume na matarajio
        Ngoja ngoja huumiza matumbo
      10. Tashihisi/uhaishaji/uhuishaji
        Sikio la kufa haliskii dawa
        Siri ya mtungi muulize kata {Zozote 4x2.sifa alama 1mfano1
    2. Eleza mbinu tatu ambazo hutumiwa kuzua misimu.    (alama 6)                              
      1. Kutumia tanakali-neno mtutu-Bunduki/ hali ya kuachilia risasi
      2. Utohozi wa maneno
        Gava      -              Government.
        Hedi       -              Head
        Fadhee -              Father
      3. Maneno ya kawaida kupewa maana mpya
        Toboa   -              faulu
        Chuma -               Bunduki
      4. Matumizi ya tabdila
        Njaro     -              Ndaro
      5. Kufupisha maneno
        Kompyuta           -              komp.
      6. Kutokana na umbo/rangi ya kinachorejelewa
        Mfano Blue        -              Noti ya kitambo ya shilingi ishirini
        Tangi                     -              Mtu mwenye umbo nane
      7. Kutumia isitara au jazanda
        Golikipa                -              nyani
        Mtu mlafi            -              Fisi
      8. Kuunda maneno mapya kabisa;. mfano
        Kuhanya              -              Usherati
        keroro                  -              Pombe
        Kusikia ubao       -              Hisi njaa
        Ni kubaya            -              hali si nzuri [ 3x2]  
    3. Ni jukumu la jamii kudumisha fasihi simulizi. Dhihirisha.                            (alama 6)
      1. Kuendelea kufundisha Fasihi Simulizi shuleni
      2. Kufanya Fasihi Simulizi kuwa hai kiutendaji kupitia shehere na hafla tofauti za kiserikali  
      3. Kuhifadhi tanzu mbalimbali ili vizazi vijavyo viweze kuzifahamu mfano kwa kurekodi      
      4. Kufanya utafiti wa kina kuhusiana na tanzu za Fasihi simulizi.
      5. Kuhakikisha kuwa lugha za kiasili hazififii kwa vile ndizo chanzo cha Fasihi simulizi                           
      6. Kuonyeshwa kwa fani mbalimbali za Fasihi simulizi kwenye vyombo vya habari kama  kama runinga.
      7. Kuhimiza wanajamii hususan viongozi kuwasilisha ujumbe wao kwa kutumia fani za Fasihi simulizi kwa mgano hotuba, ulumbi, mawaidha nk.
      8. Kuhimiza wanajamii kuionea fahari jadi hii na kushiriki kikamilifu katika matumizi ya fani mbalimbali mfano nyimbo.
      9. Kusisitiza uendelezwaji wa fani zake katika mashindano ya shule na hata baina ya shule tofauti kimaeneo na kitaifa.   [6x1]
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI PAPER 3 - KCSE 2019 BAHATI MOCK EXAMINATION (WITH MARKING SCHEME).


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest