Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - MECS Cluster Joint Pre Mock Exams 2021/2022

Share via Whatsapp

KISWAHILI
KARATASI YA 2
(LUGHA) 

  1. UFAHAMU
    Soma habari ifuatayo kisha ujibu maswali yatakayofuata

    Uchumi ni mfumo wa mapato na matumizi ya watu katika nchi fulani.Uchumi huu huhusisha sekta mbalimbali kama vile utalii,kilimo,sanaa,miongoni mwa sekta nyingine muhimu.Ukuaji wa kiuchumi hutegemea mambo kadha.Katika nchi zote ulimwenguni, sera za kisiasa huamua jinsi uchumi utakavyokua na kunawiri.Kama siasa hazitilii maanani sera za ukuaji wa kiuchumi, basi mapato ya nchi hiyo hugubikwa katika wingu kubwa la uchochole.

    Nchini Kenya, kwa mfano, kuna ulinganifu mkubwa kati ya siasa na ukuaji wa kiuchumi.Ukuaji wa kiuchumi hutegemea uteuzi wa maafisa wanaosimamia asasi muhimu sana katika usimamizi wa uchumi.Asasi hizi ni kama vile Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango ya Kitaifa na Ruwaza ya 2030, Mamlaka ya Ukusanyanji wa Ushuru(KRA), Benki Kuu ya Kenya (CBK), na Tume ya Kupambana na Ufisadi (KACC).Usimamizi wa asasi hizi huwa muhimu sana katika kuamua hatima ya uchumi wananchi hii.
    Katika mwezi wa Juni kila mwaka, Waziri wa Fedha husoma bajeti kwa wabunge.Katika maelezo yake iitwayo nakisi ya bajeti hujitokeza.Kabla ya bajeti kuandaliwa, Wizara ya Mipango huandaa hati iitwayo Usoroveya wa Kiuchumi.Baada ya kusomwa kwa bajeti, ni jukumu la wabunge kupitisha mswada wa kifedha unaohusisha wizara zote au kuutupilia mbali.Jukumu hili linafaa kutekelezwa kufikia tarehe 31 Oktoba ya kila mwaka kulingana na sheria.

    Wakati huo huo afisa anayejulikana kama Mhasibu Mkuu wa serikali huwa na jukumu la kuchunguza na kutathmini matumizi ya fedha ya wizara mbalimbali na kutoa ripoti yake kwa Kamati ya Uhasibu wa Umma bungeni (PAC).Kamati hii hutoa mapendekezo yake kwa Mkuu wa Sheria na pia kwa tume ya kupambana na ufisadi ili haki iweze kutekelezwa mahakamani iwapo dosari za kifedha zimefanyika.

    Benki kuu ya Kenya kupitia kwa gavana wake huwa na jukumu la kutoa ushauri kwa serikali kuhusu usimamizi wa kifedha, kuchunguza nguvu za shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni, kutoa sarafu za Kenya kwa umma na usimamizi wa benki zote nchini miongoni mwa majukumu mengine.

    Kwa upande mwingine, mamlaka ya ukusanyaji ushuru nchini huwa na jukumu la kuhakikisha kuwa malengo ya ushuru yamefikiwa na pia kuhakikisha kuwa hakuna mtu binafsi au kampuni yoyote inayokwepa kulipa ushuru.Iwapo kuna udanganyifu wowote, basi swala hili linafaa kuangaliwa na mahakama zetu kutekelezwa.

    Kwa jumla, sisi kama wananchi tunafaa kusaidia asasi hizi zote kufikia malengo yake ili tupate ukuaji wa kiuchumi utakaofaidi watu wote.Jambo hili litahakikisha kuwa pengo lililo kati ya walalahai na walalahoi walalahoi limezibwa.Sisi kama wananchi, tunafaa kuonyesha uzalendo wetu kwa nchi yetu kwa kulipa ushuru unavyotakikana, tukifuata mwito wa KULIPA USHURU NI KUJITEGEMEA.Mwisho tusaidie viongozi wetu katika kuendeleza sera mwafaka za kiuchumi ili nchi yetu ipige hatua kubwa katika ukuaji wa kiuchumi.Iwapo afisa yeyote atatuhumiwa kushiriki katika kashfa yoyote ya kuhujumu nidhamu ya kifedha, basi anafaa kukabiliwa vilivyo kisheria bila kujali hadhi yake ya kijamii au kisiasa.

    Maswali
    1. Ipe habari hii kichwa mwafaka. (alama 1)
    2. Uchumi ni nini? (alama 1)
    3. Ukuaji wa kiuchumi nchini Kenya hutegemea nini? (alama 1)
    4. Benki Kuu ya Kenya ina majukumu yepi? (alama 2)
    5. Mhasibu mkuu ana dhima ipi serikalini? (alama 1)
    6. Pendekeza hatua tatu za kufufua uchumi. (alama 3)
    7. Ufisadi umehujumu vipi ukuaji wa kiuchumi? (alama 2)
    8. Ni vipi Wakenya wanaweza kuonyesha uzalendo? (alama 1)
    9. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumiwa katika taarifa: (alama 3)
      1. Hatima . …………............................................................................................................
      2. Walalahai……………………………………………………………………………….
      3. Walalahoi………………………………………………………………………………

  2. UFUPISHO
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Visa vya dhuluma za kinyumbani vimeongezeka hivi majuzi, huku wanawake wakiangaziwa zaidi kwa kuwapiga waume zao.Kwa muda mrefu, visa ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa ni vya wanaume dhidi ya wake zao.Ni wazi kwamba wanaume kwa mara nyingi wanaopitia matatizo huogopa kuyatangaza hadharani.

    Hali ya kiuchumi imeathiri pakubwa familia nyingi.Pesa za kugharamia mahitaji muhimu kama chakula, mavazi na makazi zimekuwa adimu.Jambo hili linasababisha mivutano baina ya mume na mke inayoishia vita na wahusika kujeruhiwa.Wengine wameyapoteza maisha yao na wengine kulemaa kwa mili yao daima dawamu.

    Wake kwa waume wameyapuuza majukumu yao katika ndoa.Kuna waume ambao wanatumia mapato yao na ya familia kwa kupiga maji.Waume kama hawa hujigamba kuwa wao ni wakwasi na huwanunulia wenzao mvinyo huku familia zao zikiteseka kwa umaskini.Waume na wake walevi huwatukana wenzao na kwa hivyo migogoro katika ndoa kama hizi huwa haikomi.

    Wanandoa wengine wanajihusisha na mapenzi nje ya ndoa licha ya kula kiapo cha uaminifu wakioana.Usaliti huu hufanya watu wengine kulipiza kisasi kwa kuwapiga wenzao au kutomakinika katika ndoa.Matatizo ya kisaikolojia yamewafanya watu kushindwa kuzithibiti hisia zao.Kutoelewana kunapozuka, wao hupandwa na hamaki na huenda wakawatesa wake na waume zao.

    Ukosefu wa nasaha kwa wanandoa wengi umeleta shida nyingi.Wengi hawaelewi namna ya kutatua matatizo ya nyumbani.Kuna njia tofauti za kuepuka dhuluma nyumbani.Wanandoa wanafaa kudumisha upendo wa dhati kila wakati.Wake kwa waume sharti watekeleze majukumu yao nyumbani bila kuyaepuka.Mapenzi nje ya ndoa lazima yatupiliwe mbali ili muamana unaofaa uwepo.

    Licha ya changamoto tofauti katika ndoa, wanaohusika wanafaa wavumilie na kujaribu kuzika tofauti zao katika kaburi la sahau.Hawafai kuweka rekodi ya makosa ambayo wametendeana.Wosia unafaa kutolewa kwa wake na waume wote ili waelewe mikakati ya kukabiliana na matatizo mbalimbali yanayokumba ndoa.

    Viongozi wa kidini wafundishe watu maadili ili watu waepuke tamaa za kimwili zinazowasonga na kujihusisha na mapenzi nje ya ndoa.

    Ndoa inafaa iheshimiwe na watu wote kwani ndio msingi wa taasisi zile zingine kama jamii na nchi.Mawasiliano yanafaa yaimarishwe katika ndoa.Kukiwa na mazungumzo, matatizo mengi yatajadiliwa na kusuluhishwa ili kuepukana na dhuluma za aina zozote.

    Maswali
    1. Eleza kiini cha dhuluma za kinyumbani.(maneno 40-50).(alama 6;alama 1 ya mtiririko)
      Matayarisho
      Nakala safi
    2. Fupisha aya nne za mwisho ukizingatia ujumbe muhimu.(Maneno 60 – 70) (alama 9;alama 1 ya mtiririko)
      Matayarisho
      Nakala safi

  3. MATUMIZI YA LUGHA
    1. Andika vitamkwa vyenye sifa zifuatazo. (alama 2)
      1. Kipasuo ghuna cha ufizi
      2. Kikwamizo sighuna cha menoni
    2. Ainisha mofimu katika neno hili; (alama 3)
      Wanawalisha
    3. Tambua na ueleze aina za vitenzi katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
      Kalamu aliyokuwa nayo mwalimu ni ya mwanafunzi.
    4. Andika sentensi ifuatayo katika wingi (alama 1)
      Ua wake una ua zuri na kubwa.
    5. Tunga sentensi ukitumia vivumishi vya pekee kudhihirisha maana ya: (alama 2)
      1. Kutobagua
      2. Kumiliki
    6. Andika katika hali ya udogo (alama 2)
      Mbwa mwenye ukali alimfukuza mtoto.
    7. Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa
      “ Tutaondoka mwezi ujao kuelekea ughaibuni,” wambunge walisema. (alama 3)
    8. Eleza matumizi ya ‘po’ katika sentensi zifuatazo: (alama 3)
      1. Anapotembea, Mumo huimba.
      2. Atembeapo, Mumo huimba.
      3. Atembeapo Mumo, pana miiba.
    9. Yakinisha sentensi ifuatayo; (alama 1)
      Usipobisha hutafunguliwa wala kukaribishwa.
    10. Andika nomino mbili zinazoweza kuwekwa katika ngeli mbili tofauti na ubainishe ngeli hizo: (alama 2)
    11. Andika kinyume cha; (alama 2)
      Watoto wameombwa waanike nguo.
    12. Badilisha sentensi zifuatato ziwe katika kauli ulizopewa mabanoni. (alama 2)
      1. Mshtakiwa atatoa faini ya shilingi elfu moja.(Kutendwa)
      2. Ugonjwa wa saratani huwafanya watu wengi wafe.(Kutendesha)
    13. Bainisha yambwa na chagizo; (alama 3)
      Mkulima alivuniwa mahindi mwezi uliopita.
    14. Tumia neno “vizuri” katika sentensi kama: (alama 2)
      1. Kielezi
      2. Kivumishi
    15. Changanua sentensi ifuatayo ukitumia jedwali.
      Japo alifanya kazi zote, hakulipwa mapema. (alama 3)
    16. Eleza matumizi ya ritifaa katika:N’shamchukua. (alama 2)
    17. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo; (alama 2)
      Usalama ukiimarishwa watalii wengi watakuwa wanazuru humu.
    18. Onyesha muundo wa silabi katika neno lifuatalo. (alama 1)
      Mdau
    19. Tunga sentensi moja kudhihirisha tofauti kimaana kati ya vitate vifuatavyo.(alama 2)
      1. guna
      2. kuna

  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    1. Eleza sababu zinazowafanya watumizi wa lugha fulani kufanya makosa katika mazungumzo. (alama 5)
    2. Eleza sifa TANO za matumizi ya lugha katika muktadha wa maabadini. (alama 5)

MAAKIZO

  1. UFAHAMU
    1. Ipe habari hii kichwa mwafaka.
      • Uchumi
      • Ukuaji wa uchumi 1 x 1 = 1
    2. Uchumi ni nini?
      • Mfumo wa mapato na matumizi ya watu katika nchi fulani. 1 x 1 = 1
    3. Ukuaji wa kiuchumi nchini Kenya hutegemea nini?
      • Uteuzi wa maafisa wanaosimamia ofisi muhimu sana katika usimamizi wa uchumi.
        1 x 1 = 1
    4.  Benki Kuu ya Kenya ina majukumu yepi?
      • Kutoa ushauri kwa serikali kuhusu usimamizi wa kifedha.
      • Kuchunguza nguvu za shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni.
      • Kutoa sarafu za Kenya kwa umma
      • Kusimamia benki zote nchini.
        2 x 1 = 2
    5. Mhasibu mkuu ana dhima ipi serikalini?
      • Kuchunguza na kutathmini matumizi ya fedha ya wizara mbalimbali na kutoa ripoti yake kwa kamati ya Uhasibu wa Umma bungeni.
        1 x 1 = 1
    6. Pendekeza hatua tatu za kufufua uchumi.
      • kuziba pengo la kitabaka
      • Kulipa ushuru
      • Kuendeleza sera mwafaka za kiuchumi.
        3 x 1 = 3
    7. Ufisadi umehujumu vipi ukuaji wa kiuchumi?
      • Umechangia kwa kuwepo pengo kubwa baina ya walalahai na walalahoi.
      • Serikali imekosa kufikia malengo yake ya bajeti.
        2 x 1 = 2
    8. Ni vipi Wakenya wanaweza kuonyesha uzalendo?
      • Kulipa ushuru
      • Kuendeleza sera mwafaka
        1 x 1 = 1
    9. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumiwa katika taarifa:
      1. Hatima – Kilele/mwisho
      2. Walalahai – Matajiri/wakwasi/mabwenyenye
      3. Walalahoi – Fukari/Maskini
        3 x 1 = 3

  2. UFUPISHO
    1. Eleza kiini cha dhuluma za kinyumbani.(maneno 40-50).
      •  Hali ya kiuchumi yaani uhaba wa pesa.
      • Waume kwa wake kuyapuuza majukumu yao.
      • Mapenzi nje ya ndoa.
      • Matatizo ya kisaikolojia.
      • Ukosefu wa ushauri nasaha.
        (alama 6; alama 1 ya mtiririko)
    2. Fupisha aya nne za mwisho ukizingatia ujumbe muhimu.(Maneno 60 – 70)
      • Wanandoa wadumishe upendo wa dhati.
      • Wanandoa watekeleze majukumu yao ya nyumbani.
      • Kutupilia mbali mapenzi nje ya ndoa.
      • Kuweko kwa uvumilivu na kusameheana katika ndoa.
      • Ushauri kwa wanandoa
      • Viongozi wa kidini wanafundisha maadili.
      • Ndoa iheshimiwe.
      • Mawasiliano yaimarishwe miongoni mwa waliooana.
        (alama 9; alama 1 ya mtiririko).

  3. MATUMIZI YA LUGHA
      1.  Andika vitamkwa vyenye sifa zifuatazo.
        • Kipasuo ghuna cha ufizi
          /d/ 1 x 1 = 1
        • Kikwamizo sighuna cha menoni
          /th/
          1 x 1 = 1
      2. Ainisha mofimu katika neon hili;
        Wanawalisha
        wa – mofimu ya nafsi ya tatu wingi/ngeli ya A-WA wingi/nafsi ya watenda.
        na – mofimu ya wakati uliopo
        wa – mofimu ya nafsi ya watendwa/yambwa tendewa/shamirisho kitondo.
        l – mofimu ya mzizi wa neno
        ish – mofimu ya kauli ya kutendesha
        a – mofimu ya kiishio
        6 x ½ = 3
      3. Tambua na ueleze aina za vitenzi katika sentensi ifuatayo.
        aliyokuwa – kitenzi kishirikishi kikamilifu.
        ni – kitenzi kishirikishi kipungufu.
        2 x 1 = 2
      4. Andika sentensi ifuatayo katika wingi.
        Ua wake una ua zuri na kubwa
        Nyua zao zina maua mazuri na makubwa.
        1/0
      5. Tunga sentensi ukitumia vivumishi vya pekee kudhihirisha maana ya:
        • Kutobagua
          Atumie o – ote.Mfano: Chakula chochote kitaliwa.
          1 x 1 = 1
        •  Kumiliki
          Atumie – enye.Mfano:Mtoto mwenye kalamu aandike.
          1 x 1 = 1
      6. Andika katika hali ya udogo.
        Kijibwa chenye ukali kilikifukuza kitoto.
        4 x ½ = 2
      7. Andika sentensi ifuatayo katika usemi wa taarifa
        Wabunge walisema kwamba/kuwa wangeondoka (mwezi ambao ungefuata) kuelekea ughaibuni.
        3 x 1 = 3
      8. Eleza matumizi ya ‘po’ katika sentensi zifuatazo:
        • Anapotembea, Mumo huimba.
          Wakati maalum
          1 x 1 = 1
        • Atembeapo, Mumo huimba.
          Wakati wowote
          1 x 1 = 1
        •  Atembeapo Mumo, pana miiba.
          Mahali
          1 x 1 = 1
      9. Yakinisha sentensi ifuatayo:
        Ukibisha utafunguliwa na kukaribishwa
        1 x 1 = 1
      10. Andika nomino mbili zinazoweza kuwekwa katika ngeli mbili tofauti na ubainishe ngeli hizo:
        •  Maziwa – LI – YA na YA – YA
        • Kipepeo – KI – VI na A – WA
        • Uwele – U – YA na U – ZI
        • Kiti – KI – VI na A – WA
          4 x ½ = 2
          Kutaja nomino ni alama ½ , ngeli alama ½
      11. Andika kinyume cha;Watoto wameombwa waanike nguo.
        Watoto wameamrishwa waanue nguo.
        Watoto wamelazimishwa waanue nguo.
        Watoto wameshurutishwa waanue nguo.
        1 x 2 = 2
      12. Badilisha sentensi zifuatato ziwe katika kauli ulizopewa mabanoni.
        • Mshtakiwa atatozwa faini ya shilingi elfu moja
          1 x 1 = 1
        • Ugonjwa wa saratani huwafisha watu wengi.
          1 x 1 = 1
      13. Bainisha yambwa na chagizo.
        Mahindi – yambwa tendwa
        Mkulima – yambwa tendewa
        Mwezi uliopita – chagizo
        3 x 1 = 1
      14. Tumia neno vizuri katika sentensi kama:
        • Kielezi
          Otii alipita vizuri katika somo la Kiswahili.
          1 x 1 = 1
        • Kivumishi
          Viatu vizuri vimenunuliwa.
          1 x 1 = 1
          Hakiki sentensi ya mwanafunzi.
      15. Changanua sentensi ifuatayo ukitumia jedwali.
    S   
    KN KT 
     S  T E
     Japo alifanya kazi yote  hakulipwa  mapema
    1. Eleza matumizi ya ritifaa katika:N’shamchukua.
      Ritifaa imetumiwa kuonyesha kuwa kuna sauti ambazo zimedondoshwa.Ingekuwa nimekwishamchukua.
      Maelezo ni alama 1
      Kuandika neno hilo kikamilifu ni alama 1
    2. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo.
      Usalama ukiimarishwa – kishazi tegemezi
      watalii wengi watakuwa wanazuru humu – kishazi huru.
      2 x 1= 2
    3. Onyesha muudo wa silabi katika neno lifuatalo.
      Mdau – K – KI – I
      1 x 1 = 1
    4. Tunga sentensi moja kudhihirisha tofauti kimaana kati ya vitate vifuatavyo.
      • guna
        1. toa sauti nene ya kooni hali mdomo ukiwa umefunga.
        2. toa sauti ya kuonyesha kutoridhika, kulalamika au kushtuka kutokana na jambo ulilolisikia au kuliona.
      • kuna
        1. kwaruza ngozi kwa kucha au kitu chenye ncha au menomeno.
        2. kuwapo kwa vitu mahali;kitu, mtu katika mazingira maalum.
        3. Kuvutia mtu/fanya mtu apende.
        4. kwangua nazi au kiazi ili upate ungaunga au mbata.

          Mtahiniwa atunge sentensi moja tu. 1 x 2 = 2

  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    1. Eleza sababu zinazowafanya watumizi wa lugha Fulani kufanya makosa katika mazungumzo.
      1. Athari za lugha ya kwanza.
      2. Kutofahamu kanuni za kisarufi za lugha husika.
      3. Watu kuvunja lugha na kuitumia kimzaha, kwa mfano wasanii wa ucheshi.
      4. Kuzungumza au kuwaza kwa harakaharaka hivyo kukosa makini.
      5. Uhamishaji wa kanuni za lugha moja hadi nyingine.
      6. mzungumzaji kukosa msamiati mwafaka wa kutumia katika mawasiliano na hivyo kutumia maelezo marefu yanayochanganya lugha.

        Zozote 5 = alama 5
    2. Eleza sifa TANO za matumizi ya lugha katika muktadha wa maabadini.
      1. Hurejelea sura au aya ya maandishi matakatifu.
      2. Hubadilikabadilika kutegemea madhumuni, maudhui au matakwa ya msemaji.
      3. Hutumia lugha nyepesi au kama ni ngumu huhitaji mkalimani.
      4. Imesheheni vitisho, amri k.m. usipookoka,utaungua milele.
      5. Lugha hii imesheheni takriri nyingi nyingi ; Sema Aleluya!Sema Aleluya!
      6. Huwa imejaa matumaini ya baadaye kwa waumini.
      7. Hutumia lugha mseto na hata wakati mwingine kuhamisha msimbo.
      8. Lugha hii aghalabu hushirikisha viziada lugha.
      9. Huwa na msamiati wa kipekee k.m. okoka, Jehova, Biblia.
        5 x 1 = 1
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - MECS Cluster Joint Pre Mock Exams 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest