KISWAHILI PAPER 2 - KCSE 2019 MOCK EXAMINATION - KAKAMEGA

Share via Whatsapp
  1. UFAHAMU
    Soma habari ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuata:

          Miaka michache iliyopita, kila aliyekuwa amesoma alikuwa na bahati ya kupata kazi katika ofisi za humu nchini. Wote waliofika darasa la saba au pengine kidato cha pili na zaidi wale waliofuzu mtihani wa kidato cha nne, walinyakuliwa juu kwa juu na wizara mbalimbali za serikali au pengine waliandikwa kazi na makampuni. Kwa vile kila moja wao alipata kazi ya kuajiriwa, hakuna aliyejishughulisha na kazi za mtu binafsi kama useremala, uashi, ukulima, uvuvi na kadhalika- kazi kama hizo ziliachiwa wale tu ambao hawakupata fursa ya kuenda shule.
        Siku hizi mambo yamebadilika. Licha ya kuwa na elimu ya darasa la saba au kidato cha pili na pengine cha nne, hata wale wenye shahada za vyuo vikuu nao pia wamezifungia shahada hizo mashubakani zikiota ukungu huku wenyewe wakijipurukusha kulima au kufuga; na wale ambao bado hawajakata shauri kama hili, wako barabarani wakipiga lami.
        Wakoloni walifanya kosa moja kubwa sana ambalo tumeligundua tu baada ya kunyakua uhuru wetu. Kosa lenyewe ni lile la kuwafanya wananchi waliopata elimu wasipende kushika kazi zinazochafua mikono.Walijua tu kwamba mashamba yao na hata mitambo yao ingalifilisiwa na ile ya waafrika; kwa hivyo ingaliwabidi hata wao waje wawatumikie wenyeji. Ndipo walipokata shauri kutowaamsha waliolala ili wasije wakalala wao.
         Katika karne hii, wataalamu wameshawishika kuitumia elimu yao kufanya kazi za mashamba, ujenzi na ufundi wa mitambo. Ijapokuwa baada ya kazi kama hizo mikono huwa imejaa tope au masizi, pato lake ni kubwa ajabu. Jambo la kuvutia zaidi katika makazi kama haya ni kwamba mwananchi huwa ni ‘bwana’ mwenyewe, hujitegemea mwenyewe bila kochokocho.
          Kila moja wetu yuaelewa kinaganaga kwamba kazi kama ya ukulima huleta donge kubwa zaidi ya kazi zote; kwani kila mfanyikazi humwelekea mkulima baada ya kumaliza kazi yake. Mkulima naye hutoa jasho jingi wakati wa kulima shamba. Baadaye atapekua magugu na visiki aviweke katika matita ili aviteketeze moto. Baada ya muda kidogo atapanda na angoje hadi mbengu zake ziaanze kuchipuza. Mara maua huchanua na mazao kujionyesha. Baada ya kuvuna, kazi yake kubwa huwa ni kuanika na kuanua nafaka zake. Wakati huo, mazao yake huwa yatanga, mara yuapanga mara yuapangua mipango juu ya uuzaji. Mazao yafikapo nyumbani, pengine mkulima huipamba nyumba yake na akawaita marafiki zake ili awakirimu kwa vyakula na vinywaji. Karamu ikiisha hana budi kupambua mapambo yote. Huyoo, aenda kuuza bidhaa zake; akirudi yuakaa raha mstarehe akila na kuburudika pamoja na familia yake. Je kuna kazi yenye raha zaidi ya ukulima?
          Watu wengi hufikiria maana ya neno ‘kulima' ni kushika jembe tu. Hiyo si kweli kwani kuna ukulima namna nyingi, kama vile ufugaji wa ng’ombe, mbuzi au kuku. Hata ufugaji wa samaki au utunzaji wa nyuki pia waweza kuitwa ukulima. Dhamira ya taifa letu changa ni kuwapatia mwangaza wananchi wake waliomo mashuleni, kwamba wangojewa kwa hamu wajiunge na wenzao katika kulijenga taifa lenye nguvu, ili katika kujisaidia wenyewe pia waongeze pishi katika kulipa taifa maongozi mema yasiyokinai kazi zilizokuwa zikiitwa ‘chafu' lakini ambazo ndizo hasa kiini cha maendeleo na kujitegemea.

    1. Kulingana na habari uliyosoma, ni mambo gani hasa yaliyochangia kupuuzwa kwa kazi za mtu binafsi?  (alama 3)
    2. Wakoloni walikuwa na lengo gani kwa kufanya waafrika waliosoma kuchukia kazi za mikono?       (alama 2)
    3. Unafikiri mwandishi wa taarifa hii alikuwa na dhamira gani kwa wasomaji wake? (alama 1)
    4. ‘Wamezifungia shahada hizo mashubakani zikiota ukungu huku wenyewe wakijipurukusha kulima au kufuga’ Mwandishi anamaanisha nini katika kauli hii? (alama2)
    5. Kwa nini wasomaji wa kisasa wameanza kufanya kazi ya ukulima?        (alama 3)
    6. Eleza maana ya semi hizi kama zilivyotumiwa katika taarifa:                  (alama 4)
      1. Kata shauri
      2. Kuwa bwana
  1. UFUPISHO
    Soma taarifa ifuatayo kisha jibu maswali yanayofuata kulingana na maagizo.

    Inaaminika kuwa majeruhi wengi katika mikasa ya ajali huaga au huathirika vibaya zaidi kutokana na hali mbaya ya uokoaji.Watu wengi ambao hujitolea kutoa majeruhi baada ya ajali kama za barabarani, maporomoko ya ardhi au nyumba huwa hawang’amui hata chembe jinsi ya kukabiliana na uokoaji. Hatima ya juhudi zao ambazo hulenga kutenda mema ni kuathirika zaidi kwa majeruhi.
    Hali ya ukoaji inaweza kurekebishwa kwa kutoa elimu ya huduma ya kwanza kwa umma. Elimu hii yahitajika na kila Mkenya kwani mikasa ya ajali za barabarani na nyinginezo inaendelea kutokea kila siku.
    Ajali zinazotokea, si ajabu kuona makundi ya waokoaji wakibeba majeruhi hobelahobela bila kuzingatia madhara wanayoweza kuwaongezea kutokana na ubebaji wao. Kutojua namna ya kumbeba majeruhi kunaweza kumhatarisha na hata kusababisha kifo.
    Kuna mambo mbalimbali ambayo makundi ya waokoaji yanatakiwa kuzingatia wakati yanatoa huduma ya kuokoa. Kwanza ni muhimu kuchunguza kama kuna hatari yoyote inayoweza ikatokea na kuwatia majeruhi na waokoaji hatarini zaidi. Makundi ya waokoaji yameweza kwa kuliingilia eneo la ajali mbumbumbu kama mzungu wa reli.
    Hatua ya pili ni kutafuta idadi ya majeruhi. Pana uwezekano wa majeruhi kutupwa mbali na eneo Ia ajali. Vivyo hivyo, kuna majeruhi ambao huweweseka baada ya ajali na kuanza kutembea wasijue wanakoelekea. Wengi wao huaanguka karibu na eneo la ajali au wakaenda mbali.
    Hatua ya tatu ni kuchunguza kama majeruhi amezimia, moyo unapiga na jinsi anavyopumua. Ili kuhakikisha kuwa majeruhi anapumua, mwokoaji atazame kama kifua kinapanda na kushuka. Halikadhalika, mwokoaji anaweza kusikiliza au kuguza kifua na kuona kama kuna ishara za kupumua. Iwapo majeruhi anapumua, mwokoaji amweke katika hali ambayo itaimarisha kupumua kwake. Anaweza akamlaza chali au kumgeuza kwa pamoja na kichwa chake ili kufungua mkondo wa hewa. Pia mwokoaji ahakikishe hamna chochote kinywani kinachoweza kumsakama. Ikiwa hapumui, mwokoaji anaweza kujaribu kumfanya apumue kwa kupuliza hewa mdomoni mwake.
    Fauka ya hayo, Upulizaji wa hewa utahakikisha kuwa damu inazunguka mwilini vizuri.
    Hatua nyingine ni kuchunguza vile amejeruhiwa. Chunguza kama majeraha ni vidonda tu au kuna kuvunjika kwa mfupa na kubainisha ni mfupa upi. Haya yatamwezesha mwokoaji kujua jinsi ya kumbeba majeruhi. Pakiwa na kuvunjika kwa mfupa, ni muhimu kutotumia kiungo kilichovunjika anapobebwa.
    Pia kuchunguza vile majeruhi amejeruhiwa, humwezesha mwokoaji kujua huduma ya dharura atakayotumia. Majeruhi akiwa anavuja damu sana, ni muhimu kuzuia uvujaji huu. Iwapo ni kidonda kidogo, kinahitaji kufungwa ili kuzuia uambukizaji. Mwokoaji anaweza kutumia kifaa chochote kilicho karibu kutolea huduma hizi. Kwa mfano, anaweza kupasua nguo ya majeruhi iii apate kitambaa cha kusaidia kuzuia kuvuja kwa damu au kumfunga kidonda.
    Hatua inayofuata ni kumhamisha majeruhi toka eneo la ajali hadi hospitalini. Mwokoaji anaweza kuwatumia watu wengine kutafuta msaada. Wanaweza kupiga simu wakitumia nambari za simu za dharura kama zile za polisi, wazimamoto au makundi ya wataalamu wa shughuli za ukoaji. Nambari hii ya simu huwa 999 popote na huwa haina malipo. Wanaopiga simu ni vyema kutoa maelezo ya mahali ambapo ajali imetokea, ama ya ajali na huduma za dharura zinazohitajika pamoja na idadi ya majeruhi. Iwapo makundi haya ya ukoaji yameahidi kufika, ni bora kuwasubiri.
    Ikiwa makundi ya wataalamu wa ukoaji hayakupatikana, ni jukumu Ia mwokoaji kuhakikisha majeruhi wamehamishwa na kupelekwa hospitalini. Majeruhi wakiwa wengi, ni bora kuanza na wale waliozimia au wenye matatizo ya kupumua kisha kuwaendea wanaovuja damu sana. Baadaye mwokoaji awasaidie waliovunjika mifupa huku akimalizia na wenye majeraha yasiyohatarisha maisha. Ni muhimu kuwabeba 
    majeruhi kwa kutumia machela. Hii hupunguza kuathirika zaidi kwa majeruhi. Iwapo hamna machela karibu, mwokoaji anaweza kuunda moja kwa kutumia vipande viwili vya mbao, blanketi, shuka au makoti.
    Ujuzi wa huduma ya kwanza ni mojawapo ya mambo muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo.

    Maswali:
    1. Fupisha aya tatu za kwanza kwa maneno 50-60 . (alama 5) ut.1
    2. Eleza kwa kutumia maneno 90 — 100, hatua zinazotakiwa kufuatwa wakati wa uokoaji. (alama 7) Ut.2

  2. MATUMIZI YA LUGHA
    1.  
      1. Taja sauti mbili ambazo ni irabu na wakati huo huo konsonanti.   (alama 2)
      2. Tambua sauti hafifu kati ya zifuatazo:                         (alama 1)
         /K/, /r/, /gh/,/ sh/, /w/
    2. Onyesha yambwa tendwa na yambwa tendewa katika sentensi hii. (alama 2)
      Mbunge wa Mtondo Kaskazini atawajengea wanakijiji josho kisha aghurie mjini.
    3. Andika kwa msemo taarifa (alama 3)
      “Sitakwenda sokoni leo ila nitakwenda kesho,” nikamjibu
    4. Eleza matumizi ya neno wale katika sentensi hii.             (alama 3)
      Wale walioiba ni mabanati wale ambao waliambiwa wale kabla ya kitendo hicho.
    5. Yakinisha sentensi hii.   (alama 1)
      Hapa napo sipo ninapotaka
    6. Changanua kwa vielelezo vya mistari / vishale. (alama 3)
      Mwanafunzi anapohepa shuleni huadhibiwa kikondoo.
    7. Andika kwa udogo (alama 2)
      Mtoto wa mzee yule aligongwa kwa nyundo alipofukuzwa na mbwa.
    8. Tumia kiunganishi alakulihali katika sentensi ili kubainisha matumizi yake.       (alama 1)
    9. Akifisha sentensi hii                                                                   (alama 3)
      mtafanya kazi hii mpaka lini mzee alisema nataka ikamilike leo kesho mtaanza nyingine
    10. Tunga sentensi ukitumia ‘A’unganifu mwafaka pamoja na nomino ulizopewa                                                                   (alama 2)
      1. Teo
      2. Liwali
    11. Eleza matumizi ya ni katika sentensi ifuatayo:      (alama 3)
      Rudini haraka! Amina ni mgeni hapa kwetu, nitamtembeza mjini
    12. Vitumie vihisishi vifuatavyo katika sentensi.                    (alama 2)
      1. Ebo!
      2. Kefule!
    13. Sentensi hizi zinaashiria nyakati gani?  (alama 2)
      1. Ninapokimbia huchoka sana
      2. Aendapo msikitini hujitia tohara
    14.  
      1. Imekuwa vigumu mwananchi kuelewa katiba
        (andika katika kauli ya kutendea)                                             (alama 1)
      2. Andika sentensi katika kauli ya kutendewa ukitumia kitenzi ‘cha’                                                                                                              (alama 1)
    15. Tumia vivumishi vya pekee kutunga sentensi zenye maana ifuatayo. (alama 2)
      1. bila kubagua
      2. bila kubakisha
    16. Eleza maana mbili za sentensi hii             (alama 2)
      Alinichezea na Baniani
    17. Tunga sentensi mbili tofauti kubainisha maana tofauti kati ya:       (alama 2)
      1. Pamba
      2. Bamba
    18. Mwalimu huyu atawatahini wanafunzi wote watakaofanya mtihani. (alama1)
      Anza: Wanafunzi wote
    19. Unda kitenzi kutokana na nomino hii (alama 1)
      Nomino                                                 kitenzi
      Ufisadi                                                 ……….......
  1. ISIMUJAMII 
    (Mdundo wa muziki) Kina mama mpo ……………! Kina siste nanyi ………. Are you there? Kampuni ya Platinium imewaletea mafuta mpya ya Silk. Mafuta hayo yana vitamin C, Sunscreen na yana marashi ya kupendeza. Ukiyatumia kwa wiki moja tu, ngozi yako itakuwa laini na nyororo kama ya kitoto kichanga. Nayo macho ya wote, Waaa! Yatakuwa kwako 24/7. Jinunulie! Jinunulie! Mafuta ya silk. Mafuta ya wanawake wa kisasa.
    1. Taja sajili iliyotumiwa hapa.                                                                                              ( alama 1 )
    2. Taja sifa nne za sajili hii.                                                                                                    Alama 4)
    3. Kwa nini Wakenya wengi hupenda kuchanganya na kubadili msimbo?              ( alama 5 )


MARKING SCHEME

  1.  
    1. Kuajiriwa na wizara mbalimbali za serikali kwa urahisi (kwa wale waliopata elimu):
      Kuandikwa kazi na makampuni
      Wakoloni walifanya kosa la kufanya waliosoma kuchukia kazi za mikono.
      Hoja zote tatu 3 x 1 = 3
    2. Walijua kwamba kama waafrika wangefanya kazi za binafsi / mikono, ingefilisha mashamba yao (ya wakoloni) kwani waafrika hao wenye elimu wangetumikia wenyeji.  1 x 2 = 2
    3. Anawatahadharisha wasomi dhidi ya kuchukia kazi za binafsi na kutarajia kuajiriwa. Anawataka wawe tayari kujitegemea baada ya kupata elimu.                     (alama 2)
    4. Anamaanisha kwamba watu waliopata shahada hawapati kazi za ofisi na hivyo huwajibika kufungia shahada hizo zao masandukuni na kuanza kufanya kazi za kibinafsi kama kulima, useremala n.k.
      Shahada hizo haziwafaidi kwa vyovyote maana haziwasaidii kujipatia riziki.
      Hoja moja 1 x 2 = 2
    5. Kazi ya ukulima ina pato kubwa – donge kubwa zaidi ya kazi zote.
      Kazi za kuajiriwa zimekuwa nadra kupatikana.
      (Hoja zote mbili alama 3)
    6.  
      1. Kata shauri – amua
      2. kuwa bwana – kuwa wa kuheshimiwa, wa kutegemewa na mwenye hadhi.
        (2 x 2 = 4).
  2. UFUPISHO Al 15
    1. – Hali mbaya ya uokaji husababisha vifo.
      Kuathirika zaidi kwa majeruhi.
      Waokoaji wengi hawana ujuzi.
      Wema wanaoutenda huletea madhara majeruhi.
      Wakenya wapewe mafunzo kuhusu huduma ya kwanza.
      Hatari na athari kwa majeruhi zitapungua.
      (Alama 1 kwa kila hoja zozote tano alama moja ya utiririko) 1x5 = 5
      Ut – 1
      Al = 6
    2. – Kuchunguza hali yoyote inayoweza kuhatarisha maisha ya majeruhi na waokoaji.
      Kutafuta idadi ya majeruhi karibu na eneo la ajali na hata mbali.
      Kuchunguza kama majeruhi wamezimia na namna wanavyopumua.
      Kuhakikisha njia za kupata hewa kwa majeruhi ni shwari.
      Walio na shida kupumua wasaidiwe.
      Kuchunguza namna ya kujeruhiwa ili kujua huduma ipi ya dharura itatolewa.
      Kubainisha namna ya kubeba majeruhi walio hatarini.
      Kupeleka majeruhi hospitalini washughulikiwe.
      Kuomba msaada wa polisi, wazimamoto au wataalamu ikiwezekana
      Alama 1 kwa kila hoja 7. alama 2 ya utiririko
      1x7 = 7
      Uti = 2
               9
      Adhibu makosa ya sarufi(alama 3), hijai (alama 3) na ziada ya maneno iwapo yatatokea 
  1. MATUMIZI YA LUGHA
    1.  
      1. /w/,/y/     (2x1=2)
      2. /k/ /sh/   (2x½=1)
    2. Yambwa tendwa – josho
      Yambwa tendewa – wanakijiji       (2x1=2)
    3. Nilimjibu (kuwa / kwamba) singeenda sokoni siku hiyo ila ningeenda siku iliyofuata
      (6x½=3)
    4. Wale – kiwakilishi kionyeshi / kiashiria
      Wale – kivumishi kionyeshi / kiashiria
      Wale – kitenzi                                     (3x1=3)
    5. Hapo napo ndipo ninapotaka
      Hapo napo ndipo nitakapo                   (yoyote 1x1=1)
    6. S – KN +KTü
      KN – N + Sü
      N – Mwanafunziü
      S – anapohepa shuleniü
      KT – T + Eü
      T – huadhibiwaü
      E - kikondooü                               (6x½=3)
    7. Kitoto cha kizee kile kiligongwa kwa kijundo kilipofukuzwa na ki (8x¼=2)
    8. Alakulihali – kwa vyovyote vile.
    9. ü “Mütafanya kazi hii mpaka lini?” ü Mzee alisema, “Nataka ikamilike leo, kesho mtaanza nyingine.” ü (kutuza)
      1- 0           2-½                 3-1             4-1          
      5-1 ½         6- 2             7- 2             8- 2½                 9- 3
    10. Teo za Abunuasi zimepotea
      Liwali wa kwanza amewasili shambani                             (2x1=2)
    11. Rudini -wingi wa wahusika
      ni -kitenzi kishirikishi kipungufu.
      nitamtembeza – kiambishi kiwakilishi cha nafasi (kiambato/tegemezi)
      mjini    -   kielezi                    ((3x1=3)
    12.  
      1. Ebo! Kuonyesha dharau
      2. kefule! Kinyume na matarajio (hasa kuhusu maadili) (2x1=2)
    13.  
      1. wakati maalumu
      2. Wakati wowote                                                           (2x1=2)
    14.  
      1. Imewia wananchi vigumu kuelewa katiba                   (1x1=1)
      2. cha – chiwa                                                                   (1x1=1)
    15.  
      1. -o-ote
      2. -ote                                                                                 (2x1=2)
    16. Mimi pamoja na Baniani tulichezewa.
      Yeye pamoja na Baniani walichezewa                               (2x1=2)
    17.  
      1. Pamba
        sufi ya mmea iliyo nyeupe na laini
      2. chakula au masurufu ya wakati wa safari
      3. visha mavazi mazuri ya kupendeza
      4. tia urembo
      5. tayarisha au panga vitu kwa uzuri
      6.  
        1. kuwa mahali aghalabu watu au wadudu
        2. bamba
          kamata mtu kwa nguvu”baka”
        3. ziba au zuia
        4. bati
        5. kitu chembamba chenye ubapa (bamba la upanga)
    18. Wanafunzi wote watakaofanya mtihani watatahiniwa na mwalimu huyu. (1x1=1)
    19. Ufisadi   fisidi   (1x1=1)
  1. ISIMU JAMII
    1. Sajili ya matangazo ya biashara.                                                                                         1 x 1
    2. Sifa
      1. Hajaa porojo nyingi
      2. Lugha huwa nyepesi na rahisi
      3. Lugha haizingatii kanuni za lugha
      4. Lugha ya kupiga chuku ili kushawishi wasikilizaji
      5. Mbinu ya kuchanganya na kubadili msimbo hutumika
      6. Mbinu ya picha na muziki hutumiwa ni kuzidisha mvuto kwa wasikilizaji
      7. Lugha ya mshawasha mno hutumika
      8. Lugha ya mkato hutumika                                                                                  4 x 1
        Zozote nne
    3. Kwa nini Wakenya huchanganya msimbo
      1. Kuonyesha umahiri wa lugha zote mbili
      2. Kuonyesha hisia k.m chuki, huzuni, furaha n.k
      3. Kufidia upungufu wa msamiati au lugha anayotumia kukosa msamiati
      4. Ili kujitambulisha na kundi linalotumia lugha Fulani
      5. Kujinasibisha na hadhi ya lugha iwapo katika jamii lugha moja ina hadhi kuliko nyingine
      6. Kutokana na ari ya kutaka kueleweka zaidi                                                         5 x 1
        Zozote tano

        Kusahihisha
        Makosa ya sarufi hadi nne      ½ x 4 =2
        Makosa ya hijai hadi nne        ½ x 4   = 2           
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI PAPER 2 - KCSE 2019 MOCK EXAMINATION - KAKAMEGA.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest