KISWAHILI PAPER 3 - 2019 MOKASA II MOCK EXAMINATION

Share via Whatsapp

Maagizo:

 1. Andika jina lako na nambari yako ya usajili katika karatasi ya majibu uliyopewa
 2. Jibu maswali manne
 3. Swali la kwanza ni la lazima.
 4. Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu ya Riwaya, Tamthilia, UshairinaFasihiSimulizi.
 5. Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja
 6. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
 7. Karatasi hii ina kurasa 8 zilizopigwa chapa.
 8. Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.

SEHEMU YA A: HADITHI FUPI   

Alifa chokocho na Dumu Kayanda: Tumbo Lisiloshiba

 1. Lazima

“Doa ndio kawaida inayobainisha maisha ya mwanadamu.”Onyesha ukweli wa kauli hii kwa mujibu wa hadithi za: Shogake Dada ana Ndevu, Mame Bakari, Shibe Inatumaliza na Mtihani wa Maisha.                                                                                               (alama 20)                                                                                                              

SEHEMU YA B: RIWAYA

Assumpta Matei: Chozi la Heri

Jibu swali la 2 au la 3

 1. Alijiona kama mfa maji ambaye anakabiliwa na mtutumo wa mawimbi ya misiba, mmoja baada ya mwingine.
 • Bainisha muktadha wa dondoo hili.  (alama 4)
 • Eleza sifa tatu za anayerejelewa katika dondoo hili.    (alama 3)
 • Eleza tamathali ya usemi iliyotumika katika dondoo hili.   (alama 2)
 • Fafanua masaibu yaliyomkumba mrejelewa.    (alama 3)
 • Huku ukitolea mifano riwayani, jadili matatizo yanayowakumba wanajamii katika ndoa.                                                                                                       (alama 8)
 1. Eleza ufaafu wa anwani Chozi la Heri. (alama 20)

                                          

SEHEMU YA C: TAMTHILIA

Pauline Kea: Kigogo

Jibu swali la 4 au 5

 1. “Hivi vishahada vyao wanavyovipata siku hizi vinawavimbisha vichwa!”
 • Eleza muktadha wa dondoo hili.     (alama 4)
 • Taja tamathali zozote mbili zinazojitokeza katika dondoo hili.   (alama 2)
 • Eleza changamoto zilizomkabili mrejelewa na wenzake.   (alama 14)
 1. Mwandishi wa Kigogo amefanikiwa sana katika matumizi yake ya mbinu ya jazanda na kinaya. Fafanua ukweli wa kauli hii kwa kurejelea tamthilia.                (alama 20)

SEHEMU YA D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au 7

 1. Ipo Siku
  Jua la mashariki limezibwa
  Na machweo ya magharibi
  Tukabaki kuhesabu siku
  Na kila sekunde inayopita
  Ikilifyatua shaka jipya
  Ambalo bado kidogo
  Litakuwa limeliua tumaini
  Na sumu yake kulipuka hadharani
  Ulimwengu ushuhudie.
  Ni upeo wa sayansi:
  Waundapo silaha
  Mabomu ya masafa ya mbali
  Yanayomwaya yake mimweso
  Na kutudonoa
  Kama yule jogoo
  Wa radi.
  Ni upeo wa uhayawani:
  Tuundapo silaha
  Mabomu ya masafa ya karibu
  Au zana za kukingia wao jogoo
  Asitudonoe na kututia mautini
  Katika yetu ardhi
  Walipoishi na kuzikwa wetu wahenga.
  Ni udikteta sisi kuongozana vibaya
  Ni udikteta viongozi kuwaua wapinzani
  Ni unyama watu kupigwa risasi
  Ni unyama wananchi kuteswa
  Lakini
  Ni demokrasia wao kutuvamia
  Na yetu ardhi kukalia
  Ni demokrasia kuwaua viongozi wetu
  Pamoja na wananchi kwa yao makombora
  Yenye kiu ya damu yetu.
  Ni haki kutukatia mifereji ya maji
  Tukanyauka na kujifia kama vipando
  Katika majira magumu ya ukame?
  Ni utu kuwatesa watoto wetu
  Waliojisabilia kuipigania nchi katika ushinde
  Katika ardhi hii tulopawa
  Naye Mola Moliwa?
  Lakini fahamuni:
  Tofauti kati ya hadithi fupi na ndefu
  Ni kuwa ndefu huchukua mrefu wakati kuisha
  Na ile fupi huchukua muda mfupi
  Zote lakini zina miisho
  Na hii nayo ipo siku
  Ukingoni itafika
  Hatimaye watoto wetu wapate tena
  Jioni kuitamani
  Jioni isiyo na mimweso
  Mimweso ya kutishia wao uhai
  Na mingurumo na mirindimo
  ya kutangaza yao maangamizo!
  Najua sitokuwepo hili kushuhudia
  Lakini kwangu itakuwa si kitu
  Muhimu ni wajukuu wafahamishwe
  Kuwa hapa nilipita na kushuhudia
  Binadamu akiutekeleza unyama
  Alioupindua juu chini, nje ndani
  Kama funzo la demokrasia
  Kwa ulimwengu kipofu!

Maswali

 1. Eleza toni ya shairi hili.      (alama 1)
 2. Taja na kueleza nafsi – neni katika shairi hili.                 (alama 2)
 3. Jadili matumizi ya mbinu zifuatazo katika shairi hili.
  Kinaya         (alama 3)
  Usambamba         (alama 3)
  Jazanda        (alama 3)
 4. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari.        (alama 4)
 5. Eleza muundo wa shairi hili.              (alama 4)
 1. INSANI TWAJILAANI

Ya wapi silika hino, ya kwenda kinyumenyume?

Nilijibu hata kwa wino, majibuyo niyasome,

Kuno ‘geuza maneno, na kuyafanya maleme,

Haramu kuwa halali, insani twajilaani.

Insiya jilaani, ni bora wazi niseme,

Kukubalia idhini, mimba wakazikateme,

Hiyo nayo haki gani, wasiyoona mit ume,

Haramu kuwa halali, insani twajilaani.

Twajilaani laana, kijitakia ujume,

Nayo habari hatuna, twajiletea ukame,

Pia habari hatuna, ni wana sio vimeme,

Haramu kuwa halali, insani twajilaani.

Muswada siyo halali, wakuviavya vikembe,

Utawapea halali, mabinti wetu watambe,

Magulamu ja fahali, nao wakame pembe,

Haramu kuwa halali, insani twajilani.

                                                          

Kuavya mimba ni dhambi, ya kumuudhi Rahimu,

Laana twajaza tumbi, ya moto wa jahanamu,

Tuache vino vitimbi,turudie utimamu,

Haramu kuwa halali, insani twajilani.

Jambo hili nawambia, litazidisha ukware,

Ni ya uvundo tabia, ni afueni tuisare,

Tuweze kuitubia, tuwache zino parare,

Haramu kuwa halali, insani twajilani.

Muida ndio sinao, nina mengi ya kusema,

Wapigania hakio, zingatia nayosema,

‘sipashe mswada huo , ni madhambi ya kuchoma,

Haramu kuwa halali insani twajilani.

MASWALI

 1. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili (alama 1)
 2. Eleza muundo wa shairi hili (alama 4)
 3. Kwa kutolea maelezo mwafaka,tambua bahari tatu katika shairi hili (alama 3)
 4. Eleza tamathali mbili za usemi zinazojitokeza katika shairi na utolee ithibati (alama 2)
 5. Onyesha jinsi idhini ya mtunzi ilivyotumika kutimiza arudhi katika shairi hili (alama 4)
 6. Bainisha toni ya shairi hili          (alama 1)
 7. Tambua maudhui mawili yanayotawala shairi hili (alama 2)
 8. Tambua madhara matatu ya uavyaji mimba             ( alama 3)

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI

 1. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Mtu A: Tulienda kwa hiyo sherehe jana…

Mtu B: Ooh! Kumbe ulipata ngiri mbili za kiingilio?

Mtu A: Nilivaa chupa woiyee!

Mtu B: Ulimuona yule kijana Kamba?

Mtu A: Hehehe! Yule huringa mbaya…

Mtu B: Huyo alitoka mbio aliposikia kumethuka…

Maswali

 1. Tambua kipera cha utanzu wa semi kinachohusishwa na kifungu hiki. (alama 1)
 2. Fafanua umuhimu wa kipera hiki.        (alama 5)
 3. Ngomezi ni nini?(alama 2)
 4. Jadili sababu ambazo zimesababisha kuzorota kwa matumizi ya ngomezi katika jamii ya kisasa.       (alama 6)
 5. Jadili sifa za sogora zinazojitokeza nyanjani wakati wa utafiti. (alama 6)


MARKING SCHEME

SEHEMU YA A: HADITHI FUPI   

Alifa chokocho na Dumu Kayanda: Tumbo Lisiloshiba

 1. Lazima

“Doa ndio kawaida inayobainisha maisha ya mwanadamu.” Onyesha ukweli wa kauli hii kwa mujibu wa hadithi za: Shogake Dada ana Ndevu, Mame Bakari, Shibe Inatumaliza na Mtihani wa Maisha.(alama 20)                                                                                                              

Majibu yaliyopendekezwa:

Swali hili linatahini uozo. Doa iangaliwe kama mapungufu ya tabia ila si hali (umaskini)

Shogake Dada ana Ndevu

 • Mkadi anasemwa kuwa mwenye sura nzuri ila ana mienendo mbi. Bi. Hamida anaeleza kuwa tabia zake mbaya afadhali zile za mbwa koko ithibati ya kuwa hakuwa mwadilifu (Uk 29)
 • Safia anawahadaa wazazi wake kuwa Kimwana ni shoga yake ambaye walisaidiana kudurusu masomo. Ukweli ni kuwa Kimwana ni mpenzi wake ( Uk 30)
 • Kimwana anajibeba kwa heshima kuu hata wazazi wake Safia wakaishia kumwamini. Anajitanda buibui na hasemi nao. Hivi hawapati kutambua kuwa ni mwanaume ambaye alijitia kuwa mwanamke ili apate fursa ya kutoshelezana kimahaba na Safia. (Uk 31)
 • Kimwana na Safia wanajitia kujifungia chumbani “kusoma pasi na usumbufu”. Baadaye inabainika kuwa kubukua huku walikozamia kulikuwa ni kutoshelezana kimwili ( Uk 32)
 • Ujasiri wa Safia na Kimwana kurushana roho wazazi wake Safia wakiwa sebuleni ni uozo usio kifani. Haiwapigi mshipa kwamba wapo pale nyumbani watu wazima ambao wasingekubaliana na kitendo kile kuendelea. Wanawakosea heshima kwa kushiriki ya faraghani wakifahamu fika kuwa walikuwepo mahali pale.
 • Safia anapopambazukiwa kuwa amehimili, anasingizia ugonjwa. Mamaye amsailipo kuhusu kubadilika kwa hali zake anasisitiza kuwa alikuwa kapimwa zahanatini na kubainika kuwa mgonjwa wa malaria sugu; hasemi ukweli.(Uk 33)
 • Safia anawazia kuavya mimba aliyokuwa ameihimili. Anakufa katika harakati za “kufanikisha” njama hii mbaya. (Uk 35)
 • Bwana Masudi na Bi. Hamida wanaonyesha uozo mkubwa. Wanafanya kikao cha kuwasema watoto wa wenzao. Kwa mfano, wanamwumbua Mkadi kwa matendo yake. (uk 29)
 • Bwana Masudi na Bi. Hamida wanayatelekeza majukumu yao ya uzazi. Hawa wanashawishika kirahisi kuwa Kimwana ni shogaye Safia. Hawafanyi jitihada zozote kumjua wala kufahamu ikiwa kwa kweli wawili hawa walikuwa wakijifungia kusoma kama walivyosingizia. Hatimaye Safia anakuwa mja mzito.
 • Ni dhahiri kuwa katika jamii hii wapo wahudumu wa sekta ya afya ambao wako radhi kuwasaidia wasichana wanaotaka kuavya mimba kutekeleza kitendo hicho haramu. Safia anakufa akisaidiwa kuavya mimba pale katika kliniki. (uk 35)

Shibe inatumaliza:

 • Mzee Mambo anashikilia wadhifa wa waziri kivuli ila anakiri kuwa hana kazi maalum. Anapata mshahara kwa kutofanya lolote. Anakiri kwamba hana kazi hata moja tu Huku ni kuuibia umma na serikali. (uk 36-37)
 • Serikali inaendeleza ubadhirifu. Mzee Mambo anakiri kuwa na vyeo viwili na hana kazi yoyote ile aifanyayo. Hata katika wizara ambapo yeye ni waziri wa kivuli yupo waziri anaye fahamika. (uk 37). Licha ya kufahmu hivi serikali inampa nyadhifa anazozishikilia tu.
 • Mzee Mambo amejawa unafiki. Licha ya kuwa ni bayana hata kwake kuwa anafaidi pasipofaa anaeleza jinsi wakati mwengine yeye hujivika uchamungu na kujiliwaza kwa maandishi matakatifu. (uk 37).
 • Mzee Mambo anaongozwa na tamaa na ubinafsi. Anakiri kuwa vyeo vyake vinampa fursa ya kupakua mshahara. Anajinaki kuwa yeye si wa kupewa mshahara bali wa kujipakulia, kupapia na kufakamia. Huu ni uroho na ubinafsi wa hali ya juu. (uk 37)
 • Mzee Mambo anatumia raslimali za umma visivyo. Sherehe za kuadhimisha mwanawe mmoja kuota meno na mwenziwe kuingia nasari zinapeperushwa moja kwa moja na runinga ya taifa. Magari kutoka ikuluni yanasafirisha, chakula,jamaa zake,mapambo na hata maji kwa sherehe hii. (uk 38-39)
 • Sasa na Mbura pia wanakiri kuwa wanafanya mengi katika wizara ya mipango na mipangilio ila hawana lolote la mno wanalolifanya. (uk 38). Usemi huu unaonyesha watu wasiofahamu majukumu yao wala kuyachukulia kwa umuhimu unaofaa.
 • Tamashani, Sasa na Mbura sawa na wageni wengine wote wanakula kilafi. Wanaonekana kurudi awamu kadha kujitilia chakula tena chenyewe shinda! Maelezo haya yanatuonyesha watu waliotawaliwa na uroho mno. (uk 41).
 • J na wenzake serikalini wanaelezwa kuchota mabilioni ya fedha kwa sherehe inayoandaliwa na Mzee Mambo. (uk 42). Huu ni ufisadi mkuu.
 • Pia, D.J huyu anamiliki duka kubwa la dawa ambalo linasambaziwa dawa zenyewekutoka bohari kuu ya dawa za serikali. Kwa jinsi hii analiibia taifa na haswa wagonjwa ambao wanazitegemea dawa zile kupata nafuu. ( uk 43)
 • J anaelezwa kupata huduma za kimsingi bila ya kuzilipia ilhali wananchi wengine wa kawaida wanazilipia licha ya ufukara wao. (uk 43) Hali hii inabainisha ubinafsi na ufisadi uliomtawala pamoja na waliotwika jukumu la kuhakikisha kuwa huduma hizi zimewafikia wote.
 • Mbura anaangazia uroho uliowatawala waja. Anasema kuwa waja walikula vyao navya wenzao. (uk 44). Kauli hii inaashiria kutoridhika na yale ambayo mja amejaliwa. Uroho wao unawatuma kula hata vya vizazi ambavyo havijazaliwa.
 • Ubaguzi wa kitabaka umebainika. Mbura anazidi kusaili sababu ya walio mamlakani au karibu nayo kuzidi kula kwa niaba ya wenzao. (uk 44). Anasikitika kuwa wao wanazidi kuyajaza matumbo yao ilhali wananchi wa kawaida wanazidi kudhikika.
 • Watu wametawaliwa na ukatili. Mbura anaeleza kuwa watu wanauana kwa mabomu, risasi na kunyongana kwa sababu ya kutafuta faida za kibinafsi. (uk 44)
 • La kusikitisha ni kwamba ingawa waja wanafahamu kuwa wanatenda yasiyofaa, hawaonekani kujali lawama. Wamehalalisha haramu na kuyafanya matendo hayo ya kawaida mno. (uk 44)

Mame Bakari:

 • Sara anabakwa na janadume moja katili. Janadume hili linaongozwa na uchu wa kujitosheleza kimwili kumhujumu Sara vibaya hivyo. (uk 47)
 • Janadume linalombaka Sara lianaelezwa kuwa na haraufu kali ya kutuzi. Hili halijali mambo ya kimsingi kama usafi wa mwili. (uk 47)
 • Jamii inaonyeshwa kuwa isiyowahurumia wasichana wanaobeba mimba ama kwa kubakwa ua kwa kushiriki mahaba kwa hiari yao. Sara anawazia kutengwa na kukashifiwa na jamii yake pindi watakapogundua uja uzito wake. (uk 48)
 • Babaye Sara anaonyeshwa kuwa katili/ mkosa utu. Sara anaeleza sababu za kutomjuza kuwa alikuwa amebakwa. Anasema kuwa babaye alikuwa mkaidi ambaye alikuwa na tabia ya kutoamini maafa ya mwengine. (uk 48)
 • Wanaume wanaonyeshwa kuwa wasio utu. Inabainika kuwa hata mwanamke anapobakwa mwanaume halaumiwi bali ni mwanamke aliyehasiriwa. (uk 48)
 • Usaliti umebainishwa. Sara anawazia jinsi wengi wa jamaa zake, majirani na wanafunzi wenziwe wangetengana naye pindi uja uzito wake ungebainika. (uk 49)
 • Uavyaji wa mimba Kwa kipindi kifupi Sara anawazia kuitungua ile mimba aliyoihimili ila anajirudi. Mawazo haya ya kutungu amimba ni ishara tosha kuwa shughuli hiyo ipo na inaendelezwa katika jamii yake. (uk 50)
 • Umma unaolifumania janadume lililombaka Sara katika kisa tofauti cha ubakaji, unalipiga kipopo. Ingawa kitendo chake cha ubakaji ni cha kikatili, ni ukatili mkubwa kumpiga hata kumwua badala ya kumfikisha kituoni kufunguliwa mshtaka.

Mtihani Wa Maisha:

 • Ufidhuli wa waja Samueli aingiapo afisini kuyapokea matokeo yake anakumbana na mwalimu mkuu ambaye katika mawazo yake anamweleza kuwa hambe ambaye hakuwahi kumwamini. (uk 132). Huu ni ukosefu mkuu wa heshima.
 • Mwalimu Mkuu anadhihirisha dharau kwa namna anavyoingiliana Samueli. Anamtupia bahasha yenye matokeo yake, kitendo kinachodhihirisha jinsi alivyomdunisha Samueli. (uk 133)
 • Babaye Samueli ni mwenye taasubi ya kiume. Aliwaona binti zake kuwa wanawake Ingawa walikuwa wamefikia ufanisi mkubwa nasomoni hakuwathamini kama alivyomthamini Samueli. (uk 136) Fahari yake ilikuwa kumwona Samueli akifaulu.
 • Wanafunzi wanashiriki mahusiano ya kimapenzi wangali wachanga. Samueli anahusiana kimapenzi na Nina ingawa wote ni wanafunzi wa umri mdogo. (uk137)
 • Samueli anawadanganya wazazi wake kuwa hakupewa matokeo yake kwa kuwa hakuwa amekamilisha kulipia karo yake. Ukweli ni kuwa alikuwa amefeli mtihani na Licha ya kuyajua hayo na kuwa nayo, hakuwataka hawa kuyatambua. 9Uk 137)
 • Ukatili pia umejitokeza katika kazi hii. Babaye Samueli anafika kidimbwini ambako |Samueli alikuwa anajaribu kujitoa uhai akiwa amebeba kamba aliyokusudia kumpa ajinyongee na kufilia mbali. Hamwonei huruma katika hali zile za utamaushi. (uk 139).

Tanbihi:

 • Ni sharti mwanafunzi aangazie hadithi zote nne.
 • Kila hadithi ina mifano tosha ya uozo kwa hivyo mwanafunzi aaangazie mifano mitano mitano ya uozo kutoka kwa kila hadithi.

Swali hili ni wazi kwa hivyo mwanafunzi asihiniwe kwa kupendekeza hoja za ziada. Mradi ana hoja atuzwe kwa hoja zozote tano(5×4=20) kwa kila hadithi.

 • Baada ya kupata hoja tano, nyingine zichukuliwe kuwa za ziada.

SEHEMU YA B: RIWAYA

Assumpta Matei: Chozi la Heri

Jibu swali la 2 au la 3

 1. Alijiona kama mfa maji ambaye anakabiliwa na mtutumo wa mawimbi ya misiba, mmoja baada ya mwingine.
 • Bainisha muktadha wa dondoo hili.                                     (alama 4)
 1. Ni maneno ya mwandishi/msimulizi.
 2. Anamrejelea Lunga Kiriri Kangata
 3. Ni baada ya kutolewa katika Msitu wa Mamba.
 4. Moyo wa Lunga ulikuwa umekataa kuyakubali mazingira mapya katika Mlima wa Simba.

                             (4×1=04)

 • Eleza sifa tatu za anayerejelewa.                                                                 (alama 3)
 1. Msomi – alikuwa anasomea kilimo ambapo baadaye aliajiriwa kama Afisa wa Kilimo nyanjani.
 2. Mhifadhi mazingira/mwajibikaji – aliasisi Chama cha Watunza Mazingira wasio na Mipaka akiwa shuleni. Anawahutubia kuhusu uhifadhi wa mazingira.
 3. Mwenye bidii – baada ya kustaafishwa anafanya kazi ya ukulima kwa bidii hadi anaitwa jina la msimbo ‘ mkulima namba wani’.
 4. Mwenye msimamo thabiti – licha ya rai za wakubwa anapinga tendo la kuwapa raia mahindi yaliyoharibika.
 5. Mtetezi wa haki – anahiari kupoteza riziki ili kuyaokoa maisha ya wanyonge wasio na hatia.
 6. Mwenye tamaa- anapoona uzuri wa zao la mahindi katika shamba la babake, anapatwa na uchu unaolemaza uadilifu wake.
 7. Mwenye mapenzi ya dhati – anajisabilia kwa hali na mali kumridhia na kumpendeza mkewe.

                                         (3×1=03)

 • Eleza tamathali ya usemi katika dondoo.                                                  (alama 2)
  Tashbihi – alijiona kama mfa maji
  Kutaja 1 kueleza 1
 • Fafanua masaibu yaliyomkumba mrejelewa                                             (alama 3)
 1. Kuachishwa kazi kwa kupinga uagizaji wa mahindi mabaya.
 2. Kufukuzwa katika Msitu wa Mamba hivyo kupoteza mali yake yote.
 3. Anakosa pesa za kuwapeleka wanawe hata katika shule za watu wa kima wastani kwa sababu alilipwa fidia isiyotosha.
 4. Anawapoteza ndugu na marafiki zake.
 5. Kuachwa na mkewe Naomi.
 6. Kufurushwa kutoka kwa Kiriri wakati wa wa zahama baada ya kutawazwa.
  Mtahiniwa aonyeshe tatizo (hoja) kisha atolee mfano(3×1=03)
 • Huku ukitoa mifano riwayani, jadili matatizo yanayowakumba wanajamii katika ndoa.                                                                                                      (alama 8)
 1. Wanaume kushtakiwa kwa kubaka wake zao. Tete anasema kuwa sheria hiyo inamnyima mwanaume haki ya kuhusiana kimapenzi na mkewe.
 2. Upweke katika ndoa unaosababisha majonzi na hata kifo - Kiriri anaaga dunia kutokana na kihoro cha kufilisika na ukiwa alioachiwa na mkewe, Annete.
 3. Umaskini unasambaratisha ndoa. Ndoa ya Lunga na Naomi inavunjika kutokana na hali ya umaskini.
 4. Kuna uzinifu katika ndoa - Bwana Tenge alizini na wanawake wengi mkewe Bi. Kimai alipoenda mashambani.
 5. Wakwe kuingilia ndoa - Ndoa kati ya Subira na Kaizari inavunjika kwa kuwa Subira alihisi kuwa anaonewa hasa na mama mkwe; vivyo hivyo na ile ya Selume.
 6. Kutofautiana kimsimamo/ kisiasa - Selume analaumiwa kwa kumuunga mkono Mwekevu ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa muwaania kiti waliyemuunga mkono wakweze. (uk. 30)
 7. Ukabila - Selume anaachwa na mkewe na kumwoa mke mwingine kutoka kabila lake.
 8. Kukosa kupata watoto katika ndoa -Neema anakosa kujaliwa kupata watoto.
  Mtahiniwa aonyeshe tatizo (hoja) kisha atolee mfano(8×1=08)
 1. Eleza ufaafu wa anwani Chozi la Heri. (alama 20)
  • Ridhaa analia machozi ya huzuni wakati ambapo jamaa zake wakiwemo Becky, Terry, Tila na Lily Nyamvula wanateketeza. Baadaye analia chozi la heri wakati mwanawe Mwangeka anapofunga ndoa na Apondi.
  • Machozi ya huzuni yalimtoka Umulkheri alipoenda kituo cha polisi kuripoti kupotea kwa ndugu zake, Dick na Mwaliko. Baadaye analia chozi la furaha anapokutana kisadfa na Dick kwenye uwanja wa ndege.
  • Mwangeka anampoteza mkewe wa kwanza, Lily Nyamvula hivyo kujawa na machozi ya huzuni. Hata hivyo, anapata heri anapopendana na Apondi na hatimaye kufunga ndoa.
  • Watoto wa wakimbizi katika kambi wanakosa chakula hivyo kulia machozi ya njaa. Baadaye wanapata heri pale ambapo wanaletewa vyakula na mashirika yasiyo ya kiserikali na yale ya kidini.
  • Selume anajawa na huzuni na kilio baada ya kupata habari kuwa mume wake alikuwa amekwisha kuoa msichana wa kikwao hivyo hakujua pa kwenda wala kama angekutana tena na mwanawe, Sara. Hata hivyo, anapata heri Ridhaa anapomshauri na kuahidi kumtafutia kazi.
  • Neema anahuzunika kwa kukumbuka kisa cha Riziki Immaculata, kitoto alichookota na kuogopa kukichukua na kukitunza na hatimaye kukosa mtoto. Baadaye anapata machozi ya furaha/ heri anapokubaliwa kumchukua Mwaliko kama mwanawe wa kumlea.
  • Dick analazimishwa kushiriki katika biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya na Buda. Baadaye, Dick anaacha biashara hiyo na kujistawisha katika biashara ya vyombo vya mawasiliano. Anasema kuwa siku aliyokutana na Umu katika uwanja wa ndege ilikuwa siku ya heri kwani alipewa nasaha na Umu zilizomfunza thamani ya maisha.
  • Umulkheri analia machozi ya uchungu kila mara anapowakumbuka ndugu zake; Dick na Mwaliko. Baadaye analia machozi ya furaha wote wanapokutana kisadfa katika hoteli ya Majaliwa.
  • Umulkheri anapotoroka kwao baada ya nduguze kuibwa hajui anakoenda. Anamtafuta kijana ombaomba aliyemsaidia siku moja bila kuwa na matumaini ya mafanikio. Anapokaribia kukata tamaa anakutana na kijana huyo, Hazina. Hivyo, Umulkheri analia machozi yaliyojaa furaha na huzuni. Anafurahi kwa sababu Hazina alifaulu kujitoa katika maisha ya utegemezi. Anahuzunika kwa sababu huenda nduguze, Dick na Mwaliko wamechukua nafasi ya Hazina.
  • Lime na Mwanaheri wanadhulumiwa kwa kubakwa na vijana wakati wa ghasia baada ya uchaguzi. Baadaye wanapata nafuu baada ya kuhudumiwa na vijana wenzao ambao walitumwa kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa huduma za ushauri na uelekezaji.
  • Ridhaa anapatwa na ugonjwa wa shinikizo la damu baada ya familia yake na mali yake kuteketezwa moto. Hata hivyo, anapata ushauri na uelekezaji kutoka kwa wataalamu mbalimbali hivyo kuweza kudhibiti ugonjwa huo.
  • Awali maisha ya Mwangemi na Neema yalijaa huzuni kwa kukosa mtoto. Wanapata heri wakati ambapo wanakubaliwa kumlea Mwaliko.
  • Chandachema anatelekezwa na wazazi wake kwa kuzaliwa nje ndoa. Analelewa na bibi yake. Bibi anapofariki, Chandachema anateseka kwa kukosa wa kumlea. Hata hivyo, anapata heri anapopelekwa katika makao ya watoto mayatima ya Jeshi la Wajane wa Kristu. Anajitahidi masomoni ili awe mwanasheria au afisa mkuu wa maslahi ya kijamii.
  • Hazina anaishi maisha ya kuombaomba mtaani na vijana wengine. Hatimaye anafanikiwa wakati ambapo serikali inawaokoa kutoka kinamasi cha uvutaji gundi na matumizi ya mihadarati. Anapelekwa shuleni ili kupewa mafunzo kuhusu mbinu za kukabiliana na changamoto za maisha.
  • Lunga anaachishwa kazi na Shirika la Maghala ya Nafaka kwa kupinga uagizaji wa mahindi yenye sumu. Hata hivyo, anapata heri anapojistawisha na kutajirika kwa kilimo katika Msitu wa Mamba.
  • Kifo cha Mandu kinamwachia Apondi kilio na majonzi hata akachelea kuhusiana na mwanamume mwingine asije akafa. Hata hivyo, heri inamjia anapopendana na Mwangeka na hatimaye kufunga ndoa.
  • Wahafidhina wanakumbwa na matatizo wanapolazimika kutorokea Msitu wa Mamba kama wakimbizi kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivyo, baadhi yao akiwemo Ridhaa wanabahatika kurudi nyumbani kutokana na jitihada za wanaharakati wa kupigania haki za kibinadamu: Oparesheni Rudi Edeni.
  • Ridhaa anahuzunika shuleni anapochukiwa, na wanafunzi wenzake kumuambaa wakidai kuwa yeye alikuwa Mfuata Mvua. Baadaye anapata heri baada ya mamake kuzungumza na mwalimu wake aliyewashauri wanafunzi hao. Hivyo, anapata utulivu na kutia bidii katika masomo yake.
  • Zohali anasikitika wazazi wake wenye nafasi wanapomtelekeza. Anapata makao kwa Mtawa Pacha anakinaika na kupata heri.
  • Mwekevu anapotangazwa mshindi wa uongozi wafuasi wa Mwanzi wanazusha zahama ili asitawazwe. Hatimaye Mwanzi anakubali matokeo na hali ya utulivu kurejea.
   {Mtahiniwa aonyeshe namna mhusika alivyopata tatizo na baadaye kupata afueni/heri} (20×1=20)

SEHEMU YA C: TAMTHILIA

Pauline Kea: Kigogo

 1. “Hivi vishahada vyao wanavyovipata siku hizi vinawavimbishwa vichwa!”
 • Muktadha wa dondoo
 1. Haya ni maneno ya Majoka
 2. Anamzungumzia Kenga
 3. Wamo Ofisini mwa Mzee Majoka
 4. Ni baada ya Majoka kusoma kwenye gazeti kwamba Tunu aliongoza maandamano na hata kuwahutubia wanahabari.   (4×1=04)
 • Tamathali zozote mbili zinazojitokeza katika dondoo hili.
 1. Nahau - vinawavimbisha vichwa kuwafanya wenye kiburi.
 2. Keli/ dhihaka – hivi vishahada vyao kudhalilisha shahada.
 3. Nidaa – vinawavimbisha vichwa! Hisia/ hasira ya Majoka.
 4. Jazanda – vimbisha vichwa – kuwa na kiburi

(2×1=02)

 • Changamoto zilizomkabili mrejelewa na wenzake. (alama 14)
 1. Kujerehiwa – Tunu anapigwa na kujeruhiwa na vijana wahuni.
 2. Usingiziaji – Tunu anasingiziwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Sudi.
 3. Kuenezwa kwa propaganda – Tunu anaambiwa kuwa Sudi anawinda roho yake.
 4. Serikali kufunga vyombo vya habari – Runinga ya Mzalendo
 5. Mauaji ya waandamanaji – waandamanaji watano wanauawa.
 6. Wafuasi wake kutaka kukata tama – Sudi alitaka kuacha harakati za kupigania haki awashughulikie watoto.
 7. Kudhalilishwa – Ngurumo anamwambia kuwa hana wasifu wowote katika Sagamoyo.
 8. Kukabiliana na watu waliojaa taasubi za kiume – Ngurumo anamwambia kuwa hawezi kumpigia mwanamke kura pengine paka wake.
 9. Kukabiliana na masimango ya walevi – walevi wanamwimbia Tunu wimbo wa kumsimanga kuwa alistahili kuwa ameolewa.
 10. Kupokea vitisho kutoka kwa viongozi - Majoka anamwambia kuwa mcheza na tope haachi kurukiwa
 11. Changamoto ya kukabiliana na vishawishi – Majoka anajaribu kumshawishi Tunu kukubali kuolewa na mwanawe (Ngao Junior)
 12. Kuzuiliwa kwa wafuasi wake – mkewe Sudi (Ashua) anazuiliwa
 13. Changamoto ya kuwashawishi walevi kuhudhuria mikutano yao. Ngurumo anasema kuwa hawawezi kuhudhuria mkutano wa Tunu bali watenda kwa kigogo wao kwa dhifa.
 14. Ubaguzi wa kijinsia – Majoka anakashifu maasi ya Tunu kuwa yanaongozwa na mwanamke.

Mtahiniwa aonyeshe hoja kisha atolee mfano (14×1=14)

 1. Mwandishi wa Kigogo amefanikiwa sana katika matumizi yake ya mbinu ya jazanda na kinaya. Fafanua ukweli wa kauli hii kwa kurejelea tamthilia.                              (alama 20)

Jazanda

 • Sudi anachonga kinyago cha kike chenye urembo wa nafsi – kinyago hiki kinaashiria Tunu anayepigania haki za Wanasagamoyo kwa moyo wake wote. (urembo wa nafsi) uk.10
 • Husda anamweleza Ashua kwamba hawezi kumtoa tonge kinyani hivi hivi. Tonge linaashiria Majoka (mume wake) yaani hawezi kumnyang’anya mume wake hivi tu uk27
 • Majoka anamweleza Kenga kuwa hatatumia bomu kuulia mbu. Bomu inaashiria nguvu nyingi wabomu ni wanyonge (watu wadogo) uk 35
 • Majoka anamweleza Kenga, Tunu anacheza na samba anayenyonyesha. Samba inaashiria Majoka uk 37
 • Tunu anamweleza Majoka kuwa yeye ni kunguru ; kunguru hapa inaashiria woga wa Majoka wa kukubaliana na ukweli wa wapinzani wake uk 45
 • Majoka anamweleza Tunu kuwa Ashua hatoki ila kwa masharti, panya amejileta kwa paka. Panya ni Ashua naye paka ni Majoka uk 46
 • Ashua anamweleza Sudi kama mbuzi anajua kukata kamba, binadamu je? Wamepotea
 • Mbuzi anaashiria Ashua
 • Kukata kamba – inaashiria Ashua kupata usaidizi kutoka kwa mwanamume mwingine (Ashua kuomba usaidizi kwa Majoka)
 • Sumu ya nyoka – inaashiria dawa za kulevya
 • Swila / chatu – wanaashiria askari wa Sagamoyo uk 69
 • Pango la joka – mahali penye hatari kubwa uk 5
 • Safari ya Majoka ya unyambuaji nafsi na usafishaji nafsi- kumuonyesha Majoka maovu yote aliyoyatenda.
 • Jazanda ya keki – rasilmali za nchi
 • Keki za uroda – mapenzi ya Asiya kwa Ngurumo
 • Sauti ya mtima – sauti chanya
 • Sauti ya sikio – kelele za watu
 • Kukata mguu wa Tunu – kumuua
 • Kigogo – kiongozi mweye mamlaka. Kwa mfano, Majoka

(Hoja 10 × 1=10)

Kinaya

 • Mjumbe katika matangazo anarejelea ufanisi ambao umepatikana tangu uhuru ilhali raia wa Sagamoyo wanaishi maisha ya dhiki (hawana maji, elimu duni)
 • Mjumbe kudai utumwa uliondolewa ilhali wanajamii wanaishi katika utumwa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa mfano , soko linafungwa , dhuluma ya kutiwa kizuizini bila sababu na Tunu kuvunjwa mguu.
 • Mjumbe kudai hawatakubali kutawaliwa kimabavu ilhali Majoka anawadhulumu - anafunga soko akiwa na nia ya kujitwalia na kujenga mkahawa.
 • Majoka kusifiwa kuwa kiongozi shupavu ilhali anawaumiza wapinzani wake na hata kuwaua kwa Tunu.
 • Husda kumlaumu Ashua kuwa hana ‘time’ ya wanawake huku ashiki juu ya Ashua inamtawala.
 • Badala ya Majoka kuwalinda Wanasagamoyo kama kiongozi , anatumia vyombo vya dola kuwajeruhi na kuwaua raia wanaondamana.
 • Majoka kudai Sagamoyo inajiweza huku raia wake wanaselelea katika uhitaji kwa nyenzo zao za kuchumi kudhibitiwa na uongozi wa Majoka kwa mfano Soko la Chapakazi.
 • Majoka kumwambia Tunu kwamba kosa halilipwi kwa kosa na yeye anaendeleza kisasi dhidi ya Sudi kwa kumuoa Ashua ambaye alimtamani.
 • Majoka kuona kuwa Tunu amenaswa na utandabui wa kikoloni ilhali anautumia ukoloni mamboleo kuwagandamiza wenyeji wa Sagamoyo – anajinufaisha kwa mali ya umma kama vile Soko la Chapakazi.
 • Ni kinaya kuwa Ashua anadai kuwa kizuizini kuna amani kuliko nyumbani anakoteswa na Sudi ilhali Sudi anajitahidi awezavyo kuikimu jamii yake wala hamtesi mkewe kama kizuizini.
 • Kinaya kwamba Majoka anapanga sherehe ya maadhimisho idumu kwa mwezi mmoja ilhali wananchi / wafanyibiashara hawana chakula kwa kuwa Soko la Chapakazi limefungwa (Ashua na watoto hawana chakula)
 • Ni kinaya kwamba kifo cha Ngurumo hakimsikitishi Majoka ilhali alikuwa kibaraka chake badala yake anaagiza azikwe haraka.
 • Kenga na Kingi wanatusiwa na Majoka na kuitwa wasaliti ilhali Majoka mwenyewe ndiye msaliti wa Wanasagamoyo kwa kuwanyima ulinzi, chakula na kazi zao.
 • Majoka anamsaliti mkewe Husda kwa kumtamani Ashua.
 • Boza anadai kulipa kodi na kujenga nchi na kujitegemea lakini hiyo wanayolipa inamfaidi Majoka. Anatumia vyombo vinavyonunuliwa na kudumishwa na kodi ya wananchi kuwadhulumu.
 • Madai ya Majoka kwamba anamheshimu Sudi ni kinaya kwani Majoka hamheshimu yeyote.
 • Madai ya Majoka kuwa uchafu / taka ingeharibu jina zuri la Sagamoyo ni kinaya kwani Sagamoyo haisifiki kwa lolote zuri.
 • Ashua alimlaumu Sudi kwa kosa la yeye kutiwa kizuizini ilhali kosa lilikuwa la Majoka.
 • Ngurumo anadai kwamba Sagamoyo ni mahali pazuri tangu Soko la Chapakazi lifungwe lakini hiki ni kinaya kwani mahangaiko yamekithiri.
 • Ngurumo kudai pombe ni starehe ilhali pombe inaangamiza Wanasagamoyo na hata wengine kuwa vipofu.
 • Kinaya kwamba Majoka na vibaraka wake walitarajia uwanja wa ikulu ufurike watu kusherehekea siku ya uhuru lakini ni watu kumi tu waliohudhuria.
 • Ni kinaya kwamba ukoloni ulidaiwa kung’olewa lakini hasa unaotawala ni ukoloni kupitia kwa Majoka.

                 (Hoja 10 × 1=10)

SEHEMU YA D: USHAIRI

 1. Ipo Siku
 • Eleza toni ya shairi hili

Toni ya kukashifu/kushtumu/kukejeli - mataifa ya magharibi yanadhalilisha mataifa ya mashariki                                                                                 (alama 1/0)

 • Taja na kueleza nafsi – neni

Ni mwananchi mzee ambaye ameshuhudia udhalimu/ukandamizwaji ambao umekuwa ukiendelezwa na mataifa yaliyoendelea katika nchi yake.    (Atambue nafsineni na kutoa maelezo – alama 1/0)

 • Jadili matumizi ya mbinu zifuatazo katika shairi hili.

(i) Kinaya

 • Ni kinaya kuwa mashariki wakiongozana vibaya ni udikteta ilhali ni demokrasia kwa magharibi kuwavamia.
 • Ni kinaya kuwa mataifa ya mashariki yakiunda zana / silaha ni uhayawani ilhali mataifa ya magharibi yakiunda silaha / zana ni upeo wa sayansi.
 • Ni kinaya kuwa mataifa ya magharibi yanaona kuwa ni demokrasia kuwaua viongozi wetu ilhali ni udikteta viongozi kuwaua wapinzani           (3×1=3)                    

(ii)Usambamba  

 • Miundo sawa ya mistari/ mishororo – Ni udikteta sisi kuongozana vibaya
 • Ni udikteta viongozi kuwaua wapinzani
 • Urudiaji wa maneno – udikteta, unyama, demokrasia, upeo
 • Urudiaji wa silabi - ni (ubeti wa nne)                                                                                                  

(3×1=3)                    

(iii)Jazanda

 • Jua la mashariki – mataifa ya mashariki kudhalilishwa /kuzuiwa kuendelea na mataifa ya magharibi.
 • Sumu – hasira za wadhulumiwa
 • Jogoo – ala za kushambulia
 • Mimweso – vita / silaha za mataifa ya magharibi
 • Mifereji ya maji – kukatiza ufadhili au misaada ya mataifa yanayoendelea
 • Kuhesabu siku – kukata tama

                                 (Atolee maelezo 3×1=3)                    

 • Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari.

Mshairi anasema kuwa anajua / anafahamu kuwa hatakuwa ili kuona japo hilo si muhimu. Aidha, anasema kuwa ni heri vizazi vijavyo viweze kuelezwa kuwa aliweza kuona binadamu akiendeleza makuruhu hayo. Vilevile, alifanya mageuzi. Anakamilisha kwa kusema kuwa hilo lilifanywa ili iwe mwanga kuhusu uongozi mwafaka kwa dunia.

(Jibu liandikwe kwa aya moja – alama 4×1=04)                                        

 • Eleza muundo wa shairi hili.  
  • Shairi hili lina beti saba
  • Idadi ya mishororo katika kila ubeti inatofautiana mfano:
   Ubeti wa kwanza – mishororo tisa
   Ubeti wa pili – mishororo saba
  • Idadi ya mizani inatofautiana katika kila mshororo
  • Kila mshororo una kipande kimoja isipokuwa mshororo wa sita katika ubeti wa mwisho ambao una vipande viwili
  • Mshororo wa mwisho katika kila ubeti unabadilikabadilika
  • Silabi za mwisho katika kila mshororo zinatofautiana                                                                                                    

(4×1=04)

 1. INSANI TWAJILAANI
  1. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili (alama1)
   Mshairi anadhamiria kukashifu uavyaji wa mimba
  2. Eleza muundo wa shairi hili(alama4)
   Shairi lina beti saba
   Kila mshororo limegawika katika vipande viwili (ukwapi na utao)
   hairi lina kibwagizo (haramu kuwa halali, insani twajilaani)
   Kila ubeti una mishororo minne
   Vina vya kati na mwisho vinabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine
   Mizani kumi na sita katika kila mshororo(Nukuu kibwagizo) alama 4×1=04)
  3. Kwa kutolea maelezo mwafaka,tambua bahari tatu katika shairi hili (alama 3)
   Tarbia- kila ubeti una mishororo minne
   Ukaraguni   -vina vya kati na vya nje vinabadilika katika kila ubeti
   Sakarani – bahari zaidi ya moja {Bahari hizo zitajwe na kuelezwa ndipo atuzwe)
   Mathnawi – kila mshororo ina vipande viwili(3×1=03)
  4. Eleza tamathali mbili za usemi zinazojitokeza katika shairi na utolee ithibati (alama 2)
   Kinaya - haramu kuhalalishwa(kibwagizo)
   Tashbihi – magulamu ja fahali (ubeti wa 4, mshororo wa 3)(2×1=02)
  5. Onyesha jinsi idhini ya mtunzi ilivyotumika kutimiza arudhi katika shairi hili (alama 4)
   Inkisari -majibuyo badala ya majibu yako .      
   Inkisari imetumika kutosheleza idadi ya mizani
   Mazida -Muida badala ya Muda
   Mazida imetumika kutosheleza idadi ya mizani
   Lahaja hino badala ya hii.
   Imetumika ili kupata urari wa vina

   (Tanbihi sehemu mbili za swali zishughulikiwe)(4×1=04)
  6. Bainisha toni ya mshairi (alama 1)
   Toni inayotawala shairi ni ya kusikitisha. Mshairi anasikitishwa na uavyaji mimbaalama 1/0 (maelezo yatolewe)
  7. Tambua maudhui mawili yanayotawala shairi hili (alama 2)
   Wosia/Ushauri – mshairi anawapa wosia wanajamii kuhusu madhara ya uavyaji mimba
   Ukatili   -uavyaji ni kuwaaua watoto(2×1=02)
  8. Tambua madhara matatu ya uavyaji mimba                                                       (alama 3)
   Mabinti watatamba kwa kupewa idhini ya kuavya (ubeti wa 4, mshororo wa 2)
   Ni dhambi, kwa hivyo itawaletea laana itakayoathiri nafsi na Maisha yao kwa jumla
   Litazidisha ukware katika jamii. (ubeti wa 6, mshororo wa 1)
   Laana(3×1=03)

 

 1. SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
 • Tambua kipera cha utanzu wa semi kinachohusishwa na kifungu hiki. (alama 1)
  Misimu (huzungumzwa na watu wachache kwa mfano, wa rika)
 • Fafanua umuhimu wa misimu(alama 5)
 1. Huwa ni kitambulisho cha kundi fulani la watu.
 2. Hutumiwa kuhifadhi siri za watu wanaoitumia misimu hii.
 3. Hutumiwa kama njia mojawapo ya kuzua hisi mbalimbali miongoni mwa wanaoitumia kama vile uchangamfu,
 4. Huondoa ukinaifu wa msamiati uliozeeka na hivyo kuongeza ladha katika mazungumzo.
 5. Huwaunganisha wanaoitumia
 6. Huondoa urasimi katika matumizi ya lugha.
 7. Hutumiwa kama tasfida katika lugha – kuiondolea lugha makali.
 8. Huonyesha migawanyiko iliyopo katika jamii (matabaka tofauti hutumia lugha kwa namna ya kipekee)
 9. Ni hifadhi ya mila na desturi za jamii kwani huonyesha namna lugha ya jamii ilivyokua.
 10. Ni nyenzo ya kukuza lugha – pale ambapo kauli mbalimbali huimarika na kutumika katika lugha kama msamiati sanifu au semi.

(5×1=05) Akikosa sehemu ya (a) asipate sehemu ya (b)

 • Ngomezi ni fasihi ya ngoma/ uwasilishaji wa fasihi kwa mapigo ya ngoma bila kutumia maneno.(2×1=02)
  Maingiliano kati ya watu mbalimbali
  Wingi wa viwanda na majumba marefu marefu
  Njia za kisasa za mawasiliano, kwa mfano simu.
  Uhaba wa zana kama baragumu na zumari.
  Mabadiliko ya maisha yameleta ubinafsi.
  Uhamiaji wa watu kutoka jamii mbalimbali hadi maeneo ya mijini.
 • Sifa za sogora
 1. Mbunifu katika mapigo ya ngoma.
 2. Aelewe tamaduni za hadhira yake.
 3. Amudu lugha ya hadhira yake.
 4. Ayafahamu mazingira ya hadhira yake.
 5. Ashiriki mapigo ya ngoma pamoja na washirika wake.
 6. Aweze kutumia jukwaa kikamilifu/ miondoko mbalimbali ; si kusimama katika eneo moja.
 7. Anavaa maleba yanayohusiana na ngoma yake.
 8. Awe na uwezo wa kubadilisha sauti na midundo ya ngoma akicheza.

(6×1=06)


Download KISWAHILI PAPER 3 - 2019 MOKASA II MOCK EXAMINATION.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest