Kiswahili Karatasi ya 3 - 2020 MOKASA JOINT MOCKS EXAMINATION (QUESTIONS AND ANSWERS)

Share via Whatsapp

SEHEMU YA A - FASIHI SIMULIZI

 1.  Niaje wazungu wanaweza kutunza vitu vikajaa kwenye friji. Yani nimeweka soda mbili tu kwenye friji lakini haitulii hadi nizinywe. Niko sebuleni nazunguka tu. Najaribu kuwaza vitu vingine lakini wapi akili inaniambia “My friend kunywa soda”.
  1. Taja na ueleze maana ya kipera hiki (alama 2)
  2. Utanzu wa kipera hiki huweza kuchukua nafasi muhimu katika fasihi simulizi. Thibitisha kwa hoja zozote sita. (alama 6)
  3. Ufanisi wa uwasilishaji wa utanzu huu unategemea fanani. Tetea kauli hii. (alama 4)
  4. Ni changamoto gani zinaweza kumkabili mwanafasihi nyanjani? (alama 4)
  5. Dokeza umuhimu wa kukusanya data nyanjani. (alama 4)

SEHEMU YA B - TAMTHILIA: KIGOGO na Pauline Kea

 1. “Udongo tungeliuwahi uli mbichi. Limekuwa donda ndugu sasa. Waliota ikakita na wakamea hata pembe.”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Taja na kueleza tamathali moja ya usemi inayojitokeza kwenye dondoo hili. (alama 2)
  3. Eleza sifa zozote nne za msemaji wa kauli hii. (alama 4)
  4. Dondoo hili linadhihirisha jinsi baadhi ya Wanasagamoyo walivyoshiriki kuivunja jumuiya yao. Fafanua. (alama 10)
 2. “Wananchi katika mataifa ya Afrika wanakumbwa na tatizo la uongozi mbaya.” Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa mujibu wa Tamthilia . (alama 20)

USHAIRI

 1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

  1. Sikilizeni wimbo huu:
  Niliokuwa mtoto nilitwa chacha
  Kwa matamshi yangu ya sasa
  Nilipokuwa mtu mzima niliitwa Manywele
  Nilipokuwa mwalimu nikaitwa Bure.

  2. Huu utakuwa wimbo wako
  Utakapostaafu urudipo nyumbani
  Umelewa kangara na nyayo zako
  Zikishindwa kulenga njia nyembamba vijijini.
  Utakuwa kichekesho cha watoto
  Watakaoukuita, Ticha! Popote upitapo.

  3. Kumbuka mwalimu utakapostaafu,
  Mijusi watataga mayai ndani ya viatu
  Vyako vilivyokwisha visiginino.
  Na ndani ya sidiria chakavu
  Zilizoshikizwa Kamba kwa pini
  Mende watazaliana ndani ya chupa tupu
  Za marashi na za bia.

  4. Na manyigu yatajenga ndani ya kofia
  Zilizosahaulika kutani
  Utakapokufa nge watazaliana
  Chini ya jiwe juu ya kaburi lako,
  Na mlevi fulani akipita atapenga
  Na kupangusa vidole kwenye jiwe pweke
  Mwanzo na mwisho wako ndio huo.

  5, Lakini wakati ungali hai
  Unaweza kubadilisha mkondo wa maji
  Lakini kwanza mzungumze. Wewe na mimi.
  Acha mioyo yote izungumzwe
  Baada ya kunyanyaswa
  Na kisha nusu mshahara.

  6. Utafundisha tena nyimbo kuwasifu viongozi?
  Utafundisha tena ngonjera?
  Utapeleka tena wanafunzi asubuhi
  Wakajipange barabarani kusubiri
  Mgeni afikaye saa kumi na apitapo
  Apunga tu mkono kuwatia kichaa cha shangwe
  Na huku nyuma mwasambaa na njaa? 

  7. Tazama hilo runda madaftari mezani
  Utalimaliza kwa mshahara mkia wa mbuzi?
  Tuzungumze. Ninyi na mimi.
  Acha mioyo yetu izungumze
  Mkiwa waoga na kujikunja kama jongoo
  Mtawekwa kwenye vijiti na kutupwa
  Nje ya ua, ndani mtawaacha
  Wacheza ngoma wakitunga nyimbo mpya

  8. Sikilizeni walimu,
  Anzeni kufundisha hesabu mpya
  Mjinga mmoja kujumlisha na wezi ishirini
  Ni sawa na sifuri. Hapana utawala
  Fundisheni historia historia mpya
  Hapo zamani za sasa
  Hapakuwa na serikali.

  9. Sikilizeni kwa makini
  Umoja hatuna
  Twasambaratika kama nyumba
  Tulicho nacho ni woga,
  Na kinachotuangusha ni unafiki.
  Lakini tusikate tamaa kama mbuni.
  Tukiupata umoja bado tunayo silaha.
  Kura.

  Maswali

  1. Thibitisha kwamba hili ni shairi huru. (alama 5)
  2. Eleza jinsi maudhui ya utamaushi yanavyojitokeza ukimrejelea nafsi-nenwa. (alama 4)
  3. Nafsi-nenwa anapaswa kujilaumu kwa masaibu yake. Thibitisha. (alama 2)
  4.  
   1. Bainisha nafsi-neni katika shairi hili. (alama 1)
   2. Jadili toni ya shairi hili. (alama 2)
  5. Eleza matumizi mawili mawili ya usambamba na jazanda katika shiri hili. (alama 4)
  6. Eleza maana ya kufungu kifuatacho:

   Mjinga mmoja kujumlisha na wezi ishirini ni sawa na sufuri. (alama 2)

 2. Ushairi

  Leo ‘mekuita,
  Kwa upole nitanena,
  Tabiya hii yako mwana
  Nikupe ya moyo
  “Kayatiye masikiyo
  Si yetu tujuwapo 
   
  Uli wa kulaza damu,
  Pahala nawe hudumu,
  Hutufai nawe humu,
   
  Na uzembe uzidiyo
  Uchaoni mbiyombiyo
  Na hiyo shambiroyo
   
  Wapendani naumi,
  Hulimi na walimi
  Haya sijaona mimi,
   
  Uniizia gange
  wataka ukajitenge
  Nakuasa ujichunge

  Mwiza kazi yu wa chira
  Asiyeta ajira
  Ndiye muja wa hasara,

  Ni andewaye tenge
  Wala hashiki shilange
  Hubomoa asijenge

  Unavitaka vya bure
  Lako ndizo hamurere
  Uchao ‘wa ‘tuza bure.

  Hulitoa jasho lako
  Umebaki mitiko
  Sizo zetu nyendo zako

  La mno lako ni ung’are
  Uturi ujirashire
  Hukosi kuzua ghere

  Uzirembe nyele zako
  Ukatembee kwa deko
  Na marashi ya mnuko

  Unazani utaoa?
  Jasho nalo hujatoa,
  Utaithibiti ndoa?

  Utamwoa wa nani?
  Utachokishika nini?
  Wa kukubali nani?

  Unafaa kujitoa,
  Na mali ukayazoa,
  Ndipo utapopoa

  Fanye kazi kwa manani
  Hamadi i kibindoni
  Ukamtafute mwendani

  Si mambo ya kutanga,
  Chunga utajikaanga
  Mchumba chumbiya mwenga

  Fi na huhu fi na yule
  Umetujile uwele
  Na yule ukamuole

  Utafanyani kiwatunga
  Na hilo likawe janga,
  Mwanangu hutochenga

  Himila wakahimile
  Na lije likulemele
  Na wote wakikujile

  Kisomo ndiyo unayo,
  Ujuzi unao kocho,
  Upate ukitakacho

  Shahada umejitwaliya
  hutaki kuutumiya
  Kile cha kukufaiya

  Mwana wa ‘ntiya kichocho
  Umekuwa kitumiwacho
  Unawapa wapendacho

  Kwona umejiachiya
  Kidhani wawatumiya
  Na wanachokutakiya

  Komu mwanangu ukome
  Usombombi uukome,
  Sitakwita te’niseme

  Usinifishe mveyeleo
  Ukome kwanzia leo
  Ishapita hii leo

  Ukware si kuwa dume
  Wa itaha ndiye dume
  Muungwana ja kimeme

  Dume ni ajira
  Anakheshimu nafseo
  Fikira nokwelezeo

  Mradi unayo masikizi
  Kazituwe nyendo hizi,
  Ukasuhubiye kazi,

  Haya umenisikiya
  Ukawe wa kutuliya
  Halafu itakufaiya

  Nakoma zaidi s’ezi
  Nimekuweko na juzi,
  Nimejizolea ujuzi,

  Yametosha mekwambiya
  Miyaka menipitiya
  Na ndiyo ha ‘nakupa haya


  Maswali
  1. Fafanua sifa za shairi hili. (alama 3)
  2. Kando na kigezo cha idadi ya mishororo, chambua bahari nyingine tatu za shairi hili. (alama 3)
  3. Huku ukitolea mifano mwafaka, fafanua mambo mawili aliyofanya mshairi ili kukidhi mahitaji ya kiarudhi. (alama 2)
  4. Andika ubeti wa nane kwa mtindo tutumbi. (alama 3)
  5. Tambua mbinu zozote mbili za lugha zilizotumiwa na mshairi. (alama 2)
  6. Eleza dhamira ya shairi hili. (alama 1)
  7. Tambua nafsi-nenewa katika shairi hili. (alama 1)
  8. Ni nini toni ya shairi hili? Eleza. (alama 2)
  9. Eleza maana ya misamiati ifuatayo kama iliyotumika katika shairi hili. (alama 2)
   1. ghere
   2. sitaha

SEHEMU YA D - RIWAYA YA CHOZI LA HERI

 1. “Msamehe ….., hakuna mja aliyekamilika.”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Eleza umuhimu mnenewa katika dondoo hili. (alama 4)
  3. Kwa kurejelea wahusika mbalimbali riwayani, thibitisha kuwa hakuna mja aliyekamilika. (alama 12)
 2. Jadili jinsi mwandishi wa riwaya hii alivyofaulu kutumia mbinu ya kinaya na sadfa. (alama 20)

SEHEMU YA E - TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE

 1. Safari ya elimu ni kama ua la waridi ambalo licha ya upendezaji wake, huzingirwa na miiba. Jadili adha za safari hii kwa hoja tano tano kutoka kwa kila mojawapo wa hadithi fupi zifuatazo: Mapenzi ya Kifaurongo, Mame Bakari, Mwalimu Mstaafu na Mtihani wa Maisha.MWONGOZO WA MOKASA 2020

 1. Fasihi simulizi

  Niaje wazungu wanaweza kutunza vitu vikajaa kwenye friji. Yani nimeweka soda mbili tu kwenye friji lakini akili haitulii hadi nizinywe. Niko sebuleni nazungukz tu . Najaribu kuwaza vitu vingine lakini wapi akili inaniambia ‘’ My friend, kunywa soda”
  1. Taja na ueleze maana ya kipera hiki.                   AL 2
   Kichekesho

   Ni mchezo mfupi ambao hupitisha ujumbe kwa njia au namna ya kuchekesha.
  2. Utanzu wa kipera hiki huweza kuchukua nafasi muhimu katika fasihi simulizi. Thibitisha kwa hoja zozote sita   AL 6

   • Huburudisha watazamaji na waigizaji wenyewe. Burudani hii mara nyingine hupumbaza.
   • Huhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii kama vile upashaji tohara, matambiko, majigambo, ngoma, miviga na michezo ya watoto hudumishwa kupitia maigizo.
   • Ni kitambulisho cha jamii; kila jamii ina Sanaa ya maigizo ya jamii husika. Miviga na sherehe za arusi na mazishi hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
   • Hukuza umoja na ushirikiano wa watu wanapojumuika kushiriki katika maigizo. Hao hujitambulisha kama jamii moja.
   • Ni nyenzo za kupitisha maarifa na amali za jamii kupitia michezo ya jukwaani. Husawiri mtazamo wa jamii kuhusu masuala mbalimbali kama vile woga, wizi na usaliti.
   • Hukuza ubunifu madhalan watoto wanaposhiriki michezo ya watoto, hujifunza kubuni michezo wakiwa wachanga na pia Sanaa ya uigizaji.
   • Hukuza kipawa cha uongozi katika michezo, huweza kujifunza stadi za uongozi
   • Ni njia ya kuimarisha urafiki. Kwa vile mizaha na utani katika malumbano hukuza urafiki na uhusiano bora
   • Huongoza jamii kupambana na na mazingira wanamojipata. Kutegemea imani ya wanajamii,matambiko yanaweza kuondoa matatizo katika jamii kama vile njaa, ugonjwa na ukame kwa kuomba Mungu
   • Maigizo huelimisha kupitia maudhui na hulka za waigizaji na kushauri nafsi zao, kuiga au kukashifu hulka hizo.
  3. Ufanisi wa uwasilishaji wa utanzu huu unategenea fanani. Tetea kauli hii.   (Alama 4)
   • Huwa mchangamfu na mcheshi kwa hadhira yake ili kuwafanya wapendezwe na hadithi
   • Anafahamu utamaduni wa jamii yake.
   • Anaifahamu hadhira yake vizuri na kusimulia kulingana na mapendeleo yao. wasichana au wavulana? vijana au wazee?
   • Huwa na uwezo wa ufaraguni - uwezo wa kubadilisha sehemu fulani za sanaa bila kujifunga na muundo asilia.
   • Mwenye kumbukumbu nzuri - uwezo wa kukumbuka
   • Mwenye uwezo wa kuigiza kwa kutumia viungo vyake, uso (ishara-uso) na sauti(kiimbo)
   • Mwenye uwezo wa kujenga taharuki kwa kusita kidogo ili kuvuta nadhari ya hadhira yake.
   • Hushirikisha hadhira yake katika nyimbo n.k
   • Mtambaji hodari na mkwasi wa lugha.
  4. Ni changamoto gani zinaweza kumkabili mwanafasihi nyanjani?( Alama 3)
   • Gharama ya utafiti-huenda gharama ikwa kubwa kiasi cha mtafiti kutoimudu. Baadhi ya mafanani au wahojiwa huenda wakadai walipwe kabla ya kutoa habari zozote.hivyo ikiwa mtafiti hana hela basi utafiti wake utakwamizwa.
   • Mtazamo hasi wa wanajamii kuhusu ujazaji wa hojaji huenda ukawafanya wengi wao kutojaza hojaji zao. Wanajamii wengine huweza kushuku kwamba mtafiti anawapeleleza na wakakataa kutoa habari.
   • Vizingiti vya kidini amabavyo hutokea pale ambapo baadhi ya wahojiwa wanaamini kwamba matendo ya fasihi simulizi k.v matambiko na uimbaji wa taarabu yanaenda kinyume na imani yao ya kidini.
   • Uchache wa wazee au wataalamu wa fasihi simulizi ,kukosekana kwa wazee wanaoweza kutamba ngano ama kueleza vipera vingine k.v vitendawili.
   • Matatizo ya mawasiliano na uchukuzi ikiwa mkusanyaji analazimika kwenda mbali kukusanya habari,hasa katika sehemu kame itakuwa vigumu iwapo hana gari.
   • Ukosefu wa usalama ,huenda mkusanyaji wa fasihi simulizi akavamiwa ,baadhi ya watu si wakarimu na huenda wakamshuku mtafiti na kuvamiwa.
  5. Dokeza umuhimu wa kukusanya data nyanjani.   (Alama 3)
   • Ukusanyaji husaidia kurekodi na kuhifadhi tamaduni za jamii mbalimbali kwa nia ya kuzipitisha kwa vizazi vijavyo.
   • Ukusanyaji huiendeleza fasihi simulizi kwa kurekodi vipera vya fasihi simulizi
   • Husaidia kuziba pengo la utafiti liliopo.
   • Ukusanyaji zaidi wa data za fasihi simulizi hutumiwa kama kiunzi cha uchunguzi wa kulinganisha fasihi simulizi za jamii mbalimbali.
   • Humwezesha mwanafunzi kupata maarifa au stadi za kufanya utafiti katika taalima nyingine za kijamii kama vile sosholojia.
   • Humpa mwanafunzi nafasi ya kushuhudia na kuathiriwa moja kwa moja na utendaji wa fasihi simulizi

TAMTHILIA : KIGOGO na Pauline Kea

 1. “Udongo tungeliuwahi uli mbichi. Limekuwa donda ndugu sasa. Waliota mizizi ikakita na wakamea hata pembe.”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili.        (alama 4)
   • Msemaji ni Kenga
   • Anamweleza Majoka
   • Walikuwa ofisini mwa Majoka
   • Walikuwa wakizungumzia jinsi ya kuwakomesha watetezi wa haki
   • Majoka anaahidi kuwanyamazisha anaposema dawa yao anayo. (4x1=4)
  2. Taja na kueleza tamathali moja ya usemi inayojitokeza kwenye dondoo hili. (alama 2)
   • Methali- udongo uwahi uli mbichi- kumaanisha wangewakomesha wapinzani walipoanza utetezi wao (kabla ya kupata nguvu zaidi)
   • Msemo- ndonda ndugu- kumaanisha tatizo ambalo haliishi (anarejelea jinsi kuna Tunu wanang’ang’ania kupigania haki za wanyonge)
   • Nahau- ota mizizi na mea pembe- nahau hizi zimetumiwa kuonyesha jinsi watetezi walivyo imara katika utetezi wao

    ( Ya kwanza 1x2=2) (kutambua ni alama 1, maelezoalama 1)
  3. Eleza sifa zozote nne za msemaji wa kauli hii.        (alama 4)

   Sifa za Kenga
   • Mbabedume/mwenye taasubi ya kiume - anaamini mwanamke hawezi kuwa shujaa Sagamoyo. Anashangaa sana Sudi anapomwonyesha kinyago cha shujaa wa kike alichokuwa akichonga.
   • Mpyaro - anamtukana Tunu kuwa yeye ni hawara.
   • Dhalimu - yeye na Majoka wanapanga vifo vya watu. Mfano ni mauajiyaJabali. Anapanga kuwaumiza watu kwa kutumia wahuni.
   • Fisadi – anajaribu kumhonga sudi kwa zawadi nyingi kutoka kwa Majoka. Aidha anapokea kipande cha ardhi ya pale sokoni alichomegewa na Majoka.
   • Mshauri mbaya - amnamshauri Majoka vibaya hasa kuhusiana na kutumia nguvu zaidi dhidi ya waandamanaji. Aidha anazua mpango wa kumtia Ashua kizuizini ili kumlazimisha Sudi kumchongea Majoka kinyago cha Ngao.
   • Mwenye majuto - anapozinduka, anakiri makosa yake ya kuwanyanyasa raia na kujiunga na wanasagamoyo
   • Msaliti - anamwacha Majoka na kujiunga na wanasagamoyo anapoona raia wanakaribia kufanya mapinduzi (Hoja 4x1=4)
  4. Dondoo hili linadhihirisha jinsi baadhi ya Wanasagamoyo walivyoshiriki kuivunja jumuiya yao. Fafanua.      (alama 10)
   • Ngurumo na wahuni wenzake kumshambulia Tunu na kumjeruhi vibaya.
   • Ngurumo kumsaliti Boza kwa kuzini na mkewe.
   • Kenga kumpa Majoka ushauri mbaya. Mfano, kufunga soko na kulipa kisasi dhidi ya wapinzani.
   • Majoka kumiliki kiwanda kikubwa zaidi cha kuzalisha sumu ya nyoka (dawa za kulevya zinazowahasiri vijana vibaya)
   • Majoka kuidhinisha ukataji wa miti- matokeo yake ni ukame na ukosefu wa chakula.
   • Majoka kutoa kibali kwa Asiya cha kutengeneza na kuuza pombe haramu inayowapofusha na kuwaua watu.
   • Majoka kuwafurusha wachuuzi sokoni. Ananyakua ardhi hiyo ili ajenge hoteli ya kibinafsi.
   • Majoka kuwapa wafanyakazi nyongeza ndogo ya mshahara huku akipandisha kodi
   • Uongozi wa Majoka kuwasaliti vijana kwa kutowapa ajira baada ya kufuzu mfano ni Tunu, Ashua na Sudi.
   • Viongozi kama Kenga kuwa na makundi haramu kama vile Kenga kuonekana akiwahutubia wahuni chini ya mbuyu.
   • Majoka kukopa pesa kutoka nje na badala ya kuendeleza maendeleo, anafuja pesa hizo kwa mradi wa kibinafsi wa uchongaji vinyago. Pesa hizo zitalipwa na umma kwa kipindi cha miaka mia moja.
   • Kampuni ya majoka kupandisha bei ya chakula kwenye kioski. Hii ni baada ya kulifunga soko.
   • Wizi wa kura- Majoka anazua mbinu za wizi wa kura kwa kuhofia ushindani na aendelee kusalia mamlakani.
   • Majoka kuwagawia wandani wake raslimali za umma. Mafano, Kenga anapewa kipande cha ardhi ya sokoni.
   • Ngurumo na walevi wenzake pale mangweni wanamdhalilisha Tunu. Anamweleza hawezi kumpigia kura, heri amchague paka kama si Majoka.
   • Majoka kuwatamani wanawake wengine licha ya kuwa na mke.
   • Majokma kuvitumia vyombo vya dola kudhulumu raia. Anawatumia polisi kuwaua vijana watano waliokuwa wanaandamana ili kupinga nyongeza ya bei ya chakula kwenye duka la kampuni.
   • Majoka kumchochea ashua dhidi ya mumewe Sudi- nia yake ni kuwatenganisha.
   • Majoka kupanga kukifunga kituo cha Runinga ya Mzalendo kinachowazindua wanasagamoyo kuzifahamu haki zao. (Hoja zozote 10x1=10)
 1.  
  • Unyakuzi wa mali ya umma – Majoka anaamua kulifunga Soko la Chapakazi ili kujenga hoteli ya kifahari.
  • Ubinafsi – Majoka anavibomoa vibanda vya Wanasagamoyo na kupanga kujenga hoteli yake ya kifahari.
  • Utepetevu/ukosefu wa uwajibikaji – wananchi wanalipa kodi lakini wanakosa huduma kusafishiwa soko na huduma za maji taka.
  • Vitisho – Majoka anatisha kumfuta Kingi kazi
  • Viongozi wamekosa maadili ya kikazi – Majoka anamrai Ashua mkewe Sudi ili aendeleze ufuska naye.
  • Kuwatesa wapinzani – Tunu na Sudi wanateswa lakini wanaendelea kupigania mageuzi
  • Kuvunja sheria – Majoka anampa Mamapima kibali cha kuuza pombe haramu ambayo ni kinyume na katiba
  • Wizi wa kura –Majoka anasema kuwa hata wasipompa kura atashinda
  • Ubaguzi katika utoaji wa kandarasi - kandarasi ya kuoka keki inatolewa kwa Asiya ambaye ni mke wa Boza
  • Matumizi mabaya ya pesa za umma – pesa zinatumiwa katika shughuli za kuchonga vinyago
  • Utawala wa kiimla na wa kutojali – Wanasagamoyo hawana usemi wowote; Majoka anasema kuwa atajenga hoteli watu wapende wasipende
  • Mauaji ya kikatili – watu wasio na hatia wanauawa; Jabali
  • Kuzwazulia watu wasio na hatia - Ashua anazuiliwa na Majoka bila kosa lolote
  • Wanasagamoyo wanakabiliwa na unyonyaji – bei ya chakula kwenye kioski cha kampuni imepanda maradufu tangu soko lilipofungwa
  • Kuwanyima wanasagamoyo haki ya kaundamana – wanaharamisha maandamano
  • Unasaba – Majoka anamwajiri Kenga ambaye ni binamuye kama mshauri wake mkuu
  • Viongozi wanatumia nafasi zao kuwaangamiza vijana - matumizi ya dawa za kulevya – wanfunzi katika shule ya Majoka Academy wadungana sumu ya nyoka
  • Utapeli - Kuwaongezea walimu mshahara na wauguzi na kuongeza kodi
  • Kurithisha uongozi – Majoka anapanga kutambulisha Ngao Junior kuwa kiongozi mpya mpya badala ya Wanasagamoyo kumchagua kiongozi wao
  • Kuruhusu biashara ya ukataji wa miti -
  • Matumizi mabaya ya vyombo vya dola – polisi wanatumiwa kuwatawanya waandamanaji.

USHAIRI

 1.  
  1. Hili ni shairi huru kwani :
   • Lina idadi tofauti ya mishororo katika ubeti ; kwa mfano, ueti wa kwanza ni sita na wa tatu ni saba.
   • Lina idadi tofauti ya mizani katika kila mshororo ; mshororo wa kwanza ni tia na wa pili ni kumi na nne katika ubeti wa kwanza.
   • Lina idadi tofauti ya vipande katika mishororo yake. Kwa mfano, lina vipande viwili katika mishororo mingi ila vipande vitatu katika ubeti wa pili mshororo wa sita, vipande viwili mshororo wa tatu ubeti wa tano.
   • Lina matumizi mengi ya alama za uakifishaji has aya kuulizia na mshangao kwa mfano, watakaokuita, Ticha ! … zilizoshikizwa kamba kwa pini, Utafundisha tena nyimbo kuwasifu viongozi ? Utafundisha tena ngonjera ?
   • Silabi za mwisho wa kila mshororo zinatofautiana.
   • Lina matumizi ya mishata kwa mfano, kumbuka mwalimu utakapostaafu – mijusi watataga mayai ndani ya viatu vyako vilivyokwisha visigino – Na ndani ya sidiria chakavu – zilizoshikizwa kamba kwa pini.  (zozote 5 x 1=05)
  2. Maudhui ya utamaushi
   • Mwalimu anakuwa bure/ hana chochote.
   • Mwalimu atakapostaafu akilewa atashindwa kutembea vizuri hivyo kuwa kichekesho cha watoto.
   • Mwalimu atavaa vyatu vilivyokwisha visigino.
   • Mwalimu atavaa sidiria chakavu zilizoshikizwa kamba kwa pini.
   • Mwalimu atakosa bia au marashi mpaka mende watazaliana kwenye chupa tupu.
   • Mwalimu apungukiwa tu mkono na mgeni kiongozi anayewaacha njaa licha ya kumwimbia sifo na kumsubiri kwa muda mrefu. (maelezo manne 4x1=04)
  3. Nafsi – nenwa ni mwalimu/ walimu –anapaswa kujilaumu kwa sababu:
   • Hana umoja (ushirikiano) na walimu wenzake hata wanasambaratika kama nyumbu.
   • Mwalimu ni mwoga. Anajikunja kama jongoo.
   • Mwalimu anafundisha nyimbo na ngonjera za kuwasifia viongozi wasiomfaidi.
   • Mwalimu anafanya kazi nyingi (kusahihisha rundo la madaftari) kwa mshahara mdogo. (mshahara wa mkia wa mbuzi)
   • Ni mnafiki.
  4.  
   1. Nafsi – neni ni mwalimu anayewazindua walimu wenzake waambae woga na kuanza kufundisha mambo mapya ya kuukosoa uongozi uliopo.
   2. Toni ya kukejeli/ kushutumu / kudhihaki walimu kwa kukubali kila aina ya madhila na kwa woga wa kupindukia.
    Anakejeli mwalimu atakavyostaafu akawa maskini wa kupindukia.
   3. Toni ya kushauri / kunasihi walimu kujiunga pamoja, kufundisha mambo yanayohusiana na mabadiliko na kuasi uoga. (Yoyote 1x2=02)
  5.  
   1. Matumizi ya usambamba /urudiaji

    Urudiaji wa miundo sawa ya mistari/ vipande
    Nilipokuwa mtoto niliitwa Chacha
    Nilipokuwa kijana niliitwa Chaupele
    Nilipokuwa mtu mzima niliitwa Manywele
    Nilipokuwa mwalimu nikaitwa Bure

    Urudiaji wa maneno

    Nilipkuwa, niliitwa,n utakapostaafu, utafundisha, sikilizeni

    Urudiaji wa mistari

    Acha mioyo yetu izungumze (2x1=02)

   2. Matumizi ya jazanda
    • Mende kuzaliana ndani ya chupa tupu za marashi na za bia – hali ya ufukara atamojipata mwalimu aliyestaafu.
    • Kuwekwa kwenye vijiti na kutupwa nje ya ua – kuondolewa katika nafasi za kuibua sera.
    • Wacheza ngoma – viongozi
    • Mjinga mmoja – kiongozi mkuu
    • Wezi ishirini viongozi waandamizi / mawaziri
    • Historia mpya – elimu mpya ya kimapinduzi   (2 x 1= 02)
  6. Maana ya mjinga mmoja kujumlisha na wezi ishirini ni sawa na sufuri – kiongozi mkuu mmoja ambaye hana busara / hekima aiandamana na baraza lake la washauri waliojaa ufisadi ni sawa na hali ya kutokuwa na kiongozi (1x2=2)
 2.  
  1.  
   • Lina mishororo mitatu katika kila ubeti
   • Lina vipane viwili,ukwapi na utao
   • Vina vya ndani/kati na nje vinabadilikabadilika kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.
   • Lina mizani kumi na sita katika kila mshororo kwa kila ubeti
   • Lina beti 16
  2. Mshororo wa mwisho unabadilikabadilika katika kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho
   • Mathnawi.Lina vipande viwili,ukwapi na utao
   • Ukaraguni,Vina vya kati na nje vinabadilikabadilika kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho
   • Sabilia.Mshororo wa mwisho wa unabadilikabadilika
   • Mandhuma.Ukwapi unatoa wazo kisha utao unakamilisha
  3. Inkisari.mifano,kayatiye
   • Kuboronga sarufi/kufinyanga lugha/kubanga lugha.Mfano,”nikupe yangu ya moyo “ badala ya “nikupe ya moyo yangu”

    -Tabdila.Mfano’ masikiyo’ badala ya `masikio’
  4. Unafaa kujitoa ufanye kazi kwa bidii/maanani
   Ukayazoe mali yako na ukishapata/ukishatia kibindoni,
   Ndipo utakapomtafuta mwandani/mwenzio/mke/mchumba
  5. Mubalagha/maswali ya balagha.Mfano “utamwoa wa nani?”
   -Msemo.Mfano kulaza damu
   Tashbihi.Mfano “muungwans ja kimeme”
   -Taswira.Mfano “na marashi ya mnuko”
  6. Ni kumshauri/kumwonya mwana aliyepata masomo dhidi ya uvivu/uzembe.Mzee/mzazi anamwonya mwanawe aepuke uzembe na starehe na afanye kazi kwa bidii ili awe na maisha mema siku za usoni.
  7. Mwana.Anaonywa na mzaziwe dhidi ya uvivu/uzembe wa kutofanya kazi.
  8. Kushauri
   Kuonya
  9.  
   1. ghere-Kukera/kufedhehesha/kusumbua
   2. sitaha -Heshima/ustaarabu/uungwana
   3.  Jadili toni ya shairi hili.  (alama 2)
  10. Eleza matumizi mawili mawili ya usambamba na jazanda katika shairi hili.     (alama 4)

Chozi la heri

 1.   
  1. Muktadha
   • Ni maneno ya mamake Sauna
   • Anamzungumzia Sauna
   • Ni katika kumbukizai za Sauna
   • Ni baada ya Sauna kutendewa unyama na babake mlezi
   • Sauna anabakwa na kuambulia ujauzito, hali inayobainisha mkondo wa maisha ya Sauna.
  2. Mnenewa ni Sauna
   • Dhuluma kwa watoto katika ndoa/ familia. Anabakwa na babake mlezi.
   • Kikulacho ki nguoni mwako. Anawaiba wanawe Lunga ilhali aliaminiwa kuwatunza.
   • Anaendeleza maudhui ya usaliti. Anatumia furs aya uaminifu wa watoto kuwaiba na kuenda kuwauza.
   • Ukatili wa mamake. Mamake anamshurutisha kuavya mimba na kujificha tukio hilo kuwa siri.
  3. Hakuna mja aliyekamilika(Walakini wa binadamu katika Chozi la Heri)
   1. Sauna
    • Ulanguzi wa watoto
    • Biashara haramu , kuwauzia watu maji machafu
   2. Mamake Sauna
    • kumshurutisha mwanawe Sauna kuavya mimba.
    • Kuficha maovu ya mumewe
    • Anatoroka mumewe (Bwana Kero) baada ya kufutwa kazi
   3. Bwana Kero
    • mlevi kupindukia hali inayomsababishia kufutwa kazi.
   4. Bwana Maya
    • kumpiga makonde mkewe kila wakati,
    • Kumtisha na kumtusi mkewe
    • Kumbaka mwanawe – Sauna
   5. Lunga
    • Tamaa ya kuwa mkulima. Kuharibu misitu
    • Kujigamba kuwa alitoka katika ukooo wa Kiriri
   6. Naomi
    • Anamtoroka mumewe na kumwacha katika upweke.
    • Alipenda kufanya nongwa na kulalamikia maisha duni baada ya kutolewa Msitu wa Mamba.
   7. Sally
    • Anakataa usuhuba wa Billy
    • Dharau, anaita jumba la Billy kiota. Hawezi kuishi kwenye kiota.
   8. Bwana Kalima
    • Laghai, anamfuta kazi Lunga kwa kisingizio cha kustaafisha wafanyikazi ili kupunguza gharama.
   9. Annette
    • Katili/ saliti ; anamwacha Kiriri katika ukiwa baada yao kufilisika
    • Alipenda kumsimanga mumewe kwa kuwaita watumishi wake ; vimada.
   10. Mzee Kedi
    • Katili,saliti ; anamchomea Ridhaa nyumba yake na kuingamiza ailayake.
   11. Zohali
    • Tamaa na ulimbukeni wa ujana unamsababishia ujauzito.
   12. Fumba
    • Anamringa Rehema mwanafunzi wake.
    • Anamtelekeza Chandachema kwa kumwachia bibiye malezi.
   13. Bwana Tenge
    • Mzinifu/asherati ; aliwaleta wanawake kwa nyumba wakati Bi.Kimai alikuwa shamba.
   14. Tindi
    • Kaidi ; anakosa kufuata ushauri wa mamake wa kurejelea nyumbani mapema – kabla ya saa kumi na moja magharibi.
   15. Mzee Buda
    • Mlanguzi wa mihadarati
    • Vitisho ; kumtishia Dick kusingiziwa wizi ili auawe.
   16. Shamsi
    • Mlevi kupindukia
    • Kuwapigia watu kelele usiku
   17. Subira
    • Kutamauka ; anashindwa kuvumilia nongwa na masimango ya mavyaa wake.
    • Anatoroka na kuwaacha wanawe na mumewe – Kaizari
   18. Kipanga
    • Mraibu wa dawa za kulevya
    • Ananusurika kifo kutokana na kangaara iliyowaua watu sabini.

 2. Jadili jinsi mwandishi wa Riwaya hii alivyofaulu kutumia mbinu ya kinaya na sadfa . Alama 20

  KINAYA
  • Kinaya ni maelezo ya mambo kinyume na yalivyo.
  • Mwangeka anashiriki udumishaji wa amani Katika Mahariki ya kati huku familia yake ikiangamia nyumbani kutokana na ukosefu wa amani.
  • Mzee Kedi anaua familia ya Ridhaa ilhali ni yeye aliyethamini masomo ya wapwaze.
  • Ni kinaya wenye maduka kufunga milango wakati jumba la Ridhaa lilipochomeka badala ya kuyaacha wazi watu wotorokee .
  • Ni Kinaya Lunga Kirir kuachishwa kazi baada ya kutetea wanyonge wasiuziwe mahindi yaliyokuwa na sumu.
  • Ni kinaya Sauna kujifanya mzuri ilhali anawaiba watoto
  • Ni kinaya Neema kupeleka mtoto kwa makazi ya watoto na mwishowe kwenda kupanga mtoto huko
  • Ni kinaya Naomi kutoroka mmewe nawanawe ilhali hapo baadaye anajilaumu
  • Ni kinaya nchi ambayo ¡na miaka hamsini kuonekana kama mtoto wa mika hamsini
  • Ni kinaya kuwa wafrika wanakuwa wafanyikazi katika mashamba yao chini ya wakoloni
  • Ni kinaya watu walioishi na Ridhaa kwa amani wanawageukia na kuchoma nyumba yake pamoja na familia yake
  • Ni kinaya vijana kumbaka lime na Mwanaheri mbele ya wazazi wao
  • Ni kinaya mamakwe kufukuza subira kwa kuwa hawakuwa wa jamii moja
  • Ni kinaya mzee Maya kumbaka mwanawe Sauna
  • Ni kinaya wazazi wa Zohali ambao ni wasomi kumtesa Zohali kwa ajili ya ujauzito
  • Ni kinaya Tuama kusifu utamad uni wa tohara za kike iIhali ndio sababu ya kuwa hospitalini
  • Ni kinaya watu wan chi ya Wahafidhina kumkataa kiongozi wa kike na ndiye anayewafanyia kazi
  • Ni kinaya kwa pete kutaka kujia kwa kuwa na watoto watatu akiwa umri wa chini ya mia ishirini na moja      Hoja zozote 10 X1=10

   SADFA
  • Sadfa ni kuwaleta wahusika kadhaa pamoja bila kukusudiwa.
  • Selume kufikiria kustaafu katika hospitali ya uma wakati Ridhaa alikuwa anamalizia ujenzi wa hospitali ya Mwanzo Mpya
  • Umu kukutana ana Hazina alipokuwa akimtafuta.
  • Safari ya Umu kuchelewa inamfanya akutane na Dick katika uwanja wa ndege.
  • Mwangeka kukutana na Apondi katika karakana ni sadfa.
  • Ni sadfa Umu, Dick na Mwaliko kukutana katika Hoteli ya Majaaliwa.
  • Inasadifiana kuwa wakati Selume anapotaka kiacha kazi katika hospitali ya umma ndio Ridhaa anama liza kujenga hospitali ya mwanzo mpya
  • Siku ya kuzaliwa kwa Umu inasadifiana nay a Mwangemi
  • Inasadifiana wakati Neema akienda ofisini ana kiona kitoto kilichokuwa kimetupwa
  • Umu na Dick wanakitana kisadfa katika uwanja wa ndege
  • Ni sadfa Mwaliko kupangwa na binamuye mwangeka aliyempanga nduguye
  • Inasadifu kuwa Dick alipokuwa akiwaza juu ya nduguye Umu alikuwa nyuma yake
  • Kukutana kwa wana wa Lunga katika hoteli ya Majaliwa ni sadfa
  • Ni sadfa kuwa Umu anapowaza sana juu ya maisha yake wenzake wana matatizo kumliko Hoja zozote 10 X1=10

 3. Safari ya elimu ni kama ua la waridi ambalo licha ya upendezaji wake, huzingirwa na miiba. Jadili adha za safari hii kwa hoja tano tano kutoka kwa kila mojawapo wa hadithi fupi zifuatazo: Mapenzi ya Kifaurongo, Mame Bakari, Mwalimu Mstaafu na Mtihani wa Maisha.

  Tanbihi: swali hili linamhitaji mtahiniwa kuonyesha changamoto zinazoikumba elimu.
  1. Mapenzi ya Kifaurongo
   • Ugumu wa kuelewa mambo shuleni – Dennis Machora na wenzake wanapata kugumiwa na mambo wanayofunzwa katika mhadahara chuoni. Kauli za Daktari Mabonga hazieleweki upesi.
   • Utabaka shuleni – Dennis mwenye jadi ya kimaskini anatatizwa na maisha chuoni anakojipata akitagusana na wenzake kutoka familia za kitajiri.
   • Kejeli za walimu – Daktari Mabonga anawajekeli wanafunzi wake kwenye mhadhara kila wanapomwuliza maswali .
   • Kuchekwa na wanafunzi wengine – Wanafunzi wanamcheka sana Dennis anapomwomba Daktari Mabonga kutumia lugha nyepesi katika mhadhara.
   • Kutamauka shuleni – Dennis anakatizwa tamaa na masomo anapoyaona kama madubwana ambayo hakujua yalitoka wapi.
   • Utashi /Umaskini huwakumba baadhi ya wanafunzi – Dennis anajipata na uhitaji wa vitu muhimu vikiwemo malazi bora, chakula n.k. Analazimika kulalia shuka zilizozeeka na kuchanikachanika na pia kunywa uji anapokosa chakula.
   • Upweke/Ubaguzi shuleni – Wanafunzi wa familia za kitajiri huona haya hujinasibisha na wenzao wasio na chochote. Dennis anajipata katika upweke kutokana na hili.
   • Anasa/ Mapenzi shuleni – Wanafunzi katika Chuo cha Kivukoni wanatumbukia kwenye anasa na masuala ya mapenzi , Dennis anawaona wenzake wakitembea huku wameshikana wawili wawili.
   • Kukosa kazi baada ya kusoma – Dennis anatafuta kazi bila ya mafanikio licha ya kuhitimu na shahada ya uanahabari kutoka kutoka chuoni.
  2. Mame Bakari
   • Mimba za mapema kwa wasichana – Sara anajipata na ujauzito unaomtatiza kimawazo akiwa mwanafunzi.
   • Kubakwa kwa wanafunzi wa kike – Sara anabakwa na janadume asilolijua majira ya saa tatu unusu akitoka ‘twisheni’.
   • Kutengwa kwa wanafunzi wajawazito – Sara anawazia kutengwa na watu wote wa kando na wa karibu.
   • Wanafunzi kukosa wa kuwasikiliza wanapopatwa na balaaa mishani - Sara anawaza jinsi ambavyo hakuna mtu ambaye angemwelewa baada ya kubakwa.
   • Kufukuzwa shuleni kwa wasichana wajawazito/ kukatiziwa masomo – Sara anawazia jinsi ambavyo mwalimu mkuu angemfukuza kwa kusema shule ni ya wanafunzi sio wamama.
   • Msongo wa mawazo/ Shinikizo za akilini – Sara anajiwa na wazo la kujitoa uhai, hata hivyo nalikomesha wazo hilo.
   • Uavyaji mimba – Wanafunzi wa kike huweza kulazimika kuavya mimba ili wafiche hali zao. Wazo hili liliwahi kumjia Sara na akalitupilia mbali.
   • Kuaibishwa – Sara anawazia ambavyo mwalimu mkuu angemwita mama hadharani.
  3. Mwalimu Mstaafu
   • Ubaguanaji kwa misingi wa wepesi wa kupata mambo darasani – Jairo alibaguliwa katika sherehe ya kustaafau kwa mwalimu Mosi kwa kuwa hakuwa hodari masomoni hivyo hakutajirika baada ya shule.
   • Dhana potovu ya baadhi ya wanafunzi – Jairo alikuwa na dhana ya kwamba mwalimu Mosi kwa kuendelea kumpa matumaini shuleni alikuwa anamharibia wakati.
   • Mtazamo hasi dhidi ya masomo – Jairo hakupenda masomo. Kwake waliosoma na kufanikiwa ni wakora.
   • Baadhi ya wanafunzi huwa na uwezo wa chini wa kuelewa mambo darasani – Jairo alipata sufuri ambazo mwalimu Mosi alimpa matumaini kwamba zingepisha mia mia.
   • Walimu kupata lawama kutokana na upungufu wa wanafunzi – Jairo anamlaumu Mwalimu Mosi kwa mapungufu yake shuleni.
   • Baadhi ya wanafunzi huzipuuza nasaha za walimu – Jairo alipuuza kabisa ushauri alioupata kutoka kwa Mwalimu Mosi kuhusu kuepuka ufuska, ulevi n.k.
  4. Mtihani wa Maisha
   • Wasi wasi utokanao na matokeo ya mtihani – Samueli anajipata moyo ukimtuta anapokwenda kuyapokea matokeo ya mtihani wake wa kidato cha nne.
   • Walimu kuwadunisha wanafunzi – Samueli anasema vile ambavyo Mwalimu mkuu hakuwahi kumwamini.
   • Dharau kutoka kwa walimu – Mwalimu mkuu anamwonyesha dharau Samueli anapoingia ofisini kuyapokea matokeo yake. Anamtupia matokeo yake badala ya kumpa kwa njia nzuri.
   • Wanafunzi kupumbazwa na sifa wanazopaliwa na wenzao – Samueli alipokuwa akisoma, alipumbazika na umaarufu kutoka kwa wanafunzi wengine akasahau kutia bidi. Wenzake walimtambua kama ‘rasta’ shuleni.
   • Kuvunjwa moyo na matokeo duni ya mtihani – Samueli anavunjika moyo anapopata matokeo duni ya mtihani.
   • Mapenzi ya mapema – Samueli anaingilia uhusiano wa kimapenzi na msichana kwa jina Nina.
   • Udanganyifu wa wanafunzi kwa wazazi wao – Samueli anamdanganya babake kuwa hakupata matokeo ya mtihani kwa kuwa hakukamilisha kulipa karo.
   • Baadhi ya wanafunzi huwakosea heshima walimu- Samueli anamrejelea mwalimu mkuu kama ‘hambe’.
   • Wanafunzi kwenda mbali kupata elimu – Samueli alilazimika kusomea shule iliyokuwa mbali na nyumbani.
   • Kusalitika kwa wazazi – Wazazi wa Samueli wanahisi kusalitika baada ya mtoto wao mvulana, waliyemtegemea sana kufeli mtihani wa kidato cha nne.
   • Elimu ya msichana kutodhaminiwa sana – Babake Samueli aliona fahari kumwona mtoto wa kiume akifanikiwa, licha ya kuwa binti zake wawili Bilha na Mwajuma walifaulu katika mtihani ya sekondari na walikuwa vyuoni.

    Tanbihi: Mwanafunzi anaweza kupendekeza hoja nje ya zilizotolewa kwenye mwongozo huu. Hivyo, mtahini atathmini hoja za mwanafunzi.

    Hoja tano kutoka kwa kila hadithi ( 5 × 4 = 20)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Karatasi ya 3 - 2020 MOKASA JOINT MOCKS EXAMINATION (QUESTIONS AND ANSWERS).


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest