Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kapsabet Mocks 2020/2021

Share via Whatsapp
 1. UFAHAMU (ALAMA 15)

  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.

  Mbuga ya Ziwa Nakuru, sasa imesafishwa katika mojawapo ya juhudi za kukabiliana na maji taka yanayoingia mbugani. Wasimamizi wa mbuga walitumia huduma za vijana wasiokuwa na ajira kutoka mitaa ya Bondeni, Kivumbini, Lake view, Free area na Flamingo kusafisha mito inayobeba uchafu huo.

  Vibarua walizoa jumla ya tani 1.5, na baadaye tani 4.2 idadi inayofikisha zaidi ya tani 6.0 kwa siku mbili mfululizo.Hili linaashiria jinsi kina cha uchafuzi wa mazingira kwenye ziwa Nakuru umeshamiri,na baadhi ya wafanyikazi wanaona litajwe kuwa janga la kitaifa linalokodolea macho mbuga nyingi humu nchini.

  Shughuli hiyo ilivutia hisia mseto huku maswali mengi kuliko majibu yakiibuka, endapo KWS ina bajeti ya kung’arisha mbuga za wanyama.

  Akizungumza na Taifa Leo, mwangalizi wa utalii kutoka mbuga ya wanyama ya Ziwa Nakuru Bw Sirman Kioko, alisema maji taka yamekuwa yakiingia kwenye mbuga kutokana na miundo msingi duni. Aliongezea kuwa maisha ya wanyama hasa simba, nyati, vifaru, chui, viboko na flamingo yalikuwa hatarini,kwa sababu ya maji taka yalikuwa yamebadili mkondo na kupenyeza kwenye mbuga.

  Miaka mitano iliyopita mbuga ya Nakuru ilikuwa na idadi kubwa ya ndege aina ya heroe ,lakini sasa wamebakia 200 tu. Hali hii itazidi kuwa mbaya,endapo idara husika haitaweka mikakati ya kutafuta suluhu la kudumu kwa wanyama pori wanaozidi kuangamia. Aidha uchafuzi katika ziwa Nakuru umefanya ndege kuhamia ziwa Bogoria ambapo inaaminika angalau chakula ni tele.

  “Tunakubali kuwa gharama ya kusafisha mbuga ni kubwa,lakini pia tunaomba umma kupunguza matumizi ya mifuko ya plastiki inayoziba njia za maji,”alisema.

  Pia aliongezea kuwa ni jukumu la mbuga kusafisha mazingira ya wanyama,lakini baraza la mji wa Nakuru pia lina nafasi kubwa ya kuhakikisha makazi ya watu ni safi,kwa kuzoa taka ipasavyo. Anaona kuna utepetevu mkubwa kutoka kwa usimamizi wa mazingira NEMA,wanaostahili kuweka sheria kali za kukabiliana na wale wanaoharibu mazingira.

  Aliongezea kuwa baraza la kusimamia huduma za wanyama pori (KWS),halina bajeti ya kusafisha mbuga na ndio sababu waliwaajiri vibarua saba kuendesha shughuli hiyo ya siku tatu. Uchafuzi wa mito inayoingia ziwa Nakuru hutokea msimu wa mvua ambapo maji hufurika na kusomba taka kutoka kwenye makazi ya watu.

  Wanyama wanaovutia watalii kama vile Nyati hupata maradhi pindi wanapokunywa maji chafu,yaliyochanganyika na mifuko ya plastiki. Licha ya KWS kumiliki kituo cha kufanyia utafiti aina ya maradhi mbalimbali yanayokabili wanyama bado hawajafanikiwa kwa asilimia kubwa kuyazuia.

  Hili linajiri siku moja tu baada ya wakazi wa mtaa wa Bondeni kuandamana barabarani wakilalamikia,ongezeko la kiwango cha takataka kwenye makazi ya watu. (Imenukuliwa kutoka kwa Gazeti la Taifa Leo)

  Maswali

  1. Ipe taarifa hii kichwa mwafaka. (alama 1)
  2. Eleza sababu zinazofanya Ziwa Nakuru kuchafuka. (alama 2)
  3. Ni nini madhara ya kuchafuliwa kwa Ziwa Nakuru? (alama 4)
  4. Eleza vizingiti vinavyofanya ziwa hili kuendelea kuchafuliwa. (alama 2)
  5. Toa mapendekezo yanayoweza kusaidia kumaliza uchafuzi wa Ziwa Nakuru kulingana na taarifa hii. (alama 4)
  6. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika taarifa. (alama 2)
   1. Kupenyeza
   2. Utepetevu

 2. UFUPISHO (ALAMA 15)

  Sekta ya kilimo nchini Kenya ni mojawapo ya mihimili ya uchumi na inachangia asilimia 25 ya pato la taifa (G.D.P.). Sekta hii inatoa ajira kwa asilimia 40 ya wakenya na zaidi ya asilimia 70 ya wanaoishi mashambani. Isitoshe, huchangia asilimia 65 ya mapato yanayotokana na mauzo ya nje ya nchi sawa na kutegemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wakenya wote kwa uhai wao kupitia kutoa ajira, ujira na usalama wa chakula. Nchini Kenya, kilimo kinakumbwa na changamoto na vitisho kama vile kupanda kwa gharama ya kawi, kubadilika kwa tabia ya nchi pamoja na misukosuko katika nchi jirani. Bila shaka kumarika kwa sekta hii kutahakikisha kustawi kwa uchumi mzima. Hivyo basi, sera na mifumo ya kiasisi inayosimamia sekta hii ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wote.

  Ili kuwakinga wanunuzi dhidi ya tishio la usalama wa chakula, serikali imetekeleza maamuzi mengi katika sekta ya kilimo. Kutokana na hali hii mbinu za kuusitiri umma zimepewa kipaumbele katika sera za nchi. Pamoja na hayo, sera za bei za bidhaa za kilimo, zenye kuwafaidi wazalishaji, nazo katika miaka ya hivi karibuni zimebainishwa na kushiriki kikamilifu pamoja na udhibiti wa serikali; ambayo miongoni mwa mengine, huamua bei za bidhaa zinazozalishwa pamoja na pembejeo. Kuhusu hifadhi ya nafaka, mnamo 2011 Kenya ilipanga kuongeza maradufu hifadhi hii ili kujikinga dhidi ya upungufu wa chakula kufuatia utabiri kuwa mvua imepungua.

  Baada ya kuukinga umma kutokana na athari za njaa, serikali ilielekeza juhudi zake kwenye hatua za kibiashara. Kufuatia upungufu wa chakula kumekuwa na juhudi za kupunguza ushuru wa uagizaji hasa wa mahindi, mchele na sukari. Sambamba na hayo, Kenya imekuwa ikiongeza hisa inayotengea Wizara ya Kilimo kufikia asilimia 10 ya jumla ya makadirio yake ya fedha ili kuafiki Azimio la Mapato linalosisitiza serikali zote kutenda hivyo.

  Maswali:

  1. Kwa maneno 35 – 40 fupisha aya ya kwanza ya kifungu hiki. (alama 6, 1 ya mtiririko)
   Matayarisho
   ...........................................................................................................
   Jibu
   ...........................................................................................................
  2. Kwa maneno 50-55, fafanua mikakati iliyochukuliwa na serikali ya Kenya ili kuimarisha kilimo. (alama 9, 1 utiririko)
   Matayarisho
   ...........................................................................................................
   Jibu
   ...........................................................................................................
 3. MATUMIZI YA LUGHA: (ALAMA 40)
  1. Taja ala zinazotumika kutamkia sauti /ch/ (alama 1)
  2. Tunga sentensi moja ukitumia nomino na kielezi kutokana na neno: enda (alama 2)
  3. Tunga sentensi ukitumia nomino katika ngeli ya ‘U-YA’ ili kuonyesha upatanisho wa kisarufi (alama 2)
  4. Eleza tofauti za sentensi hizi. (alama 2)
   1. Nilimpata huku.
   2. Nilimpata humu.
  5. Onyesha matumizi ya kiambishi ‘ji’ katika sentensi ifuatayo:
   Mkiambiaji alijibidiisha katika riadha (alama 2)
  6. Tumia vitenzi vifuatavyo kutunga sentensi katika kauli ya kutendeka
   1. Cha (alama 1)
   2. Pa (alama 1)
  7. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao KN(N) + KT (t + T + E) (alama 1)
  8. Tumia neno ‘Kama’ katika sentensi kama; (alama 2)
   1. Kitenzi
   2. Kihusishi
  9. Tunga sentensi moja ukitumia kiunganishi cha uteuzi (alama 2)
  10.  
   1. Kirai ni nini? (alama 1)
   2. Onyesha aina ya virai katika sentensi ifuatayo.
    Mwaka juzi alikwenda ulaya (alama 2)
  11. Kwa kutoa mfano mmoja wa sentensi eleza maana ya shamirisho kitondo (alama 2)
  12. Changanua sentensi ifuatayo kwa kutumia matawi: (alama 4)
   Ule mkongojo wa babu ulinunuliwa na fundi
  13. Tunga sentensi moja ukitumia vitate hivi: (alama 3)
   1. Kipofu
   2. Kibovu
   3. Kibofu
  14. Eleza mofimu zilizomo katika neno hili. (alama 3)
   Lililolila
  15. Tunga sentensi moja ukitumia kihisishi cha masikitiko. (alama 2)
  16. Tunga sentensi kuonyesha matumizi ya alama ya kibainishi. (alama 2)
  17. Andika katika usemi wa taarifa
   “Utaweza kuwa mwindaji mashuhuri ikiwa utayafuata mashauri yangu,”
   alisema mbunda. (alama 2)
  18. Tunga sentensi ukitumia kinyume cha kitenzi hiki: Ezeka (alama 2)
  19. Yakinisha sentensi ifuatayo:
   Tusingalienda hospitali, tusingalitibiwa. (alama 1)
 4. ISIMU JAMII: (ALAMA 10)
  1. Fafanua istilahi zifuatazo za isimu jamii (alama 2)
   1. Isimu
   2. Jamii
  2. “.......ah.....naomba kumwongelesha Chucho.....Naam, naam
   Chucho.......Hujambo? .....si.....sina neno......naam. Mjomba amezidiwa si wa maji si wa chakula....kweli?......Muuguzi mkuu amedhihirisha..... Yes......ok......yeah.....Ala! Ameishiwa na pesa.
   1. Tambua sajili husika katika dondoo hili. (alama 1)
   2. Kwa hoja zozote saba, eleza sifa za sajili hii. (alama 7)


Marking Scheme

 1.  
  1. Uchafuzi wa Mazingira / Ziwa Nakuru
  2.  
   • Maji taka kuingia mbugani
   • Miundo msingi duni
  3.  
   • kuhama kwa ndege
   • kuangamia kwa wanyama pori
   • maradhi kadha kwa wanyama pori
   • mkondo wa maji kuzibwa
  4.  
   • KWS kutokuwa na bajeti ya kusafisha mbuga
   • Utepetevu wa NEMA kwa kukosa kuweka sheria kali.
  5.  
   • Baraza la mji kuhakikisha makazi ni safi
   • Baraza la mji kuzoa taka kutoka makazi ya watu
   • Wananchi kuhimizwa kupunguza matumizi ya vitu vya plastiki
   • Kuweka bajeti ya kusafisha mazingira
  6.  
   1. Kupenyeza - Kupita katikati
   2. Utepeteve - ulegevu/uvivu
 2.  
  1.  
   • Sekta ya kilimo inachangia asilimia 25 ya pato la taifa
   • Inatoa ajira kwa asilimia 40 ya wakenya
   • Huchangia asilimia 65 ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje.
   • Hutegemewa na asilimia 80 ya wakenya kwa uhai
   • Kustawi kwake kutaimarisha uchumi

    (Hoja 5 x 1 = alama 5)
  2.  
   • Serikali inatekeleza maamuzi mengi katika kilimo
   • Mbinu za kuustiti umma zimepewa umbele
   • Sera ya bei za bidhaa za kilimo zimeleta kushiriki kikamilifu na udhibiti wa serikali
   • 2011 Kenya ilipanga kuongeza maradufu hifadhi ya nafaka
   • Serikali imeelekeza juhudi katika sekta ya kibiashara
   • Juhudi za kuhakikisha usalama wa chakula zimekuwepo/zimetekelezwa
   • Serikali imekuwa ikiongeza hisa inayotengewa Wizara ya Kilimo katika makadirio yake.
    (Zozote 7 x 1 = 7)
 3.  
  1. Kaakaa ngumu na baba la ulimi
  2. Nomino -> Mwendo, Kielezi -> Nilimpata mwendoni
  3. Ugonjwa huo umehatarisha maisha
   Magonjwa hayo yamehatarisha maisha.
  4.  
   1. Pahala pasipo dhahiri
   2. Pahala palipo dhahiri (undani)
  5. Mkimbiaji -> Mtendaji
   alijibidiisha -> kirejeshi cha mtenda
  6.  
   1. Mtoto hakukubali kuachika haraka na mamake
   2. Pesa si kitu kinachopeka vivi hivi.
  7. Maji yangali yanamwagika mtaroni
  8.  
   1. Mfugaji anakama ng'ombe
   2. Aliruka kama masai.
  9. ama/au - Utakula wali au ugali?
  10.  
   1. Neno au fungu la maneno ambayo hayana muundo wa KN na KT hivyo hayana maana kamili
   2. Mwaka juzi - KN/RN
    alikwenda ulaya - RT
  11. Ni nomino inayotendewa kitendo au inayonufaika kutokana na utendaji wa kitendo.

  12.  swap2
  13. Kipofu mwenye kibofu kibovu ametibiwa.

   Kipofu - mtu asiye na uwezo wa kuona
   kibovu - kibaya/kilichooza/kisichofaa
   Kibofu - mpira unaotiwa upepo (baluni)/kiungo cha mwili kinachobeba mkojo (bladder)
  14. li - li - lo - li - l - a
   li -ngeli
   li - wakati uliopita
   lo - kirejeshi
   li - yambwa tendwa
   l - mzizi
   a - kiishio
  15. Yarabi! Mola amlaze pema
  16. (') Ng'ombe
  17. Mbunda alisema kuwa angeweza kuwa mwindaji mashuhuri ikiwa/kama angeyafuata mashauri yake.
  18. Ezua - Wajenzi waliezua paa la nyumba.
  19. Tungalienda hospitali tungalitibiwa
 4.  
  1.  
   1. Sayansi inayochunguza matumizi ya lugha.
   2. Kundi la watu wenye uhusiano na maingiliano mbalimbali.
    Kundi la watu wenye uhusiano wa aina fulani.
  2.  
   1. sajili ya simu/rununu/simu tamba
   2.  
    • hutumia sentensi fupi fupi
    • kuna matumizi ya maswali na majibu
    • hutumia takriri
    • Huhusisha kuchanganya ndimi
    • Kanuni za kisarufi hukiukwa
    • Hulenga moja kwa moja kiini cha habari
    • kuna kukatizana kalima
    • kuna maamkizi

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kapsabet Mocks 2020/2021.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest