Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Maranda Post Mocks 2020/2021

Share via Whatsapp

SEHEMU A: RIWAYA

Assumpta K. Matei: Chozi la Heri

  1. Lazima
    "Huyu ambaye mama alimwona kama gae, kumbe sasa ndiye chombo cha kunivusha bahari hii ya dhiki?."
    1. Eleza muktadha wa maneno haya. (alama 4)
    2. Bainisha mbinu mbili za lugha zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
    3. Kwa kurejelea wahusika mbalimbali riwayani, jadili mikakati kumi na minne waliyoichukua kuvuka bahari ya dhiki. (alama 14)

SEHEMU B: TAMTHILIA

Pauline Kea: Kigogo

Jibu swali la 2 au 3

  1. "Uliyavulia nguo sharti uyaoge. Kesho ya Pili na Pendo na watoto wengine iko mikononi mwetu.”
    1. Bainisha umuhimu wa tamathali mbili za usemi zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 4)
    2. "Ustawi wa nchi yoyote hutegemea vijana wake.” Jadili ukirejelea hoja kumi na sita kutoka tamthilia: Kigogo. (alama 16)
  2. "Afadhali hapa pana amani. Nikiwa hapa sikutani nawe na huyo kirukanjia wako. Si mwoane yaishe!" 
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Eleza jinsi mbinu inayojitokeza kwenye maneno yaliyopigwa mstari ilivyotumika katika tamthilia: Kigogo. (alama 9)
    3. "Asasi inayorejelewa katika dondoo imo hatarini." Thibitisha kwa mujibu wa tamthilia ya Kigogo. (alama 7)

SEHEMU C: HADITHI FUPI

Alifa Chokocho na Dumu Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine

Jibu swali la 4 au 5

  1. (Tulipokutana Tena - Alifa Chokocho)
    1. "Pale nilipokwenda kulelewa palikuwa jehanamu kwangu. Mara moja nilifahamu kwamba nilikuwa mtumwa wa nyumba hiyo."
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      2. Thibitisha kwa hoja nane kuwa mzungumzaji wa maneno haya alilelewa katika jehanamu. (alama 8)
        (Mapenzi ya Kifaurongo - Kenna Wasike)
    2. "Ninafuta chozi linalonichungulia machoni. Kwa nini ninalia sasa?' ninajiuliza." Kwa hoja nane, toa sababu zinazomfanya mzungumzaji kulia. (alama 8)
  2.  
    1. (Mtihani wa Maisha – Eunice Kimaliro)
      Fafanua kwa hoja kumi jinsi mwandishi alivyotumia mbinu ya uzungumzi nafsi kukuza wahusika katika hadithi hii. (alama 10)
    2. (Mwalimu Mstaafu - Dumu Kayanda)
      Kwa kurejelea hoja kumi, hakiki nafasi ya maudhui ya busara kwa mujibu wa hadithi hii. (alama 10)

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au 7

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

    Kutakapokucha kesho,
    Mlokubali dhoruba.
    Ikawajia kwa hutuba,
    Hatimaye ikateleza nyoyo zenu kuzibembeleza,
    Na ngazi wakapata kupanda
    Mtajutia matendo yenu.
     
      Watu wa kesho,
    Watatetewa na nani?
    Watakula na kunywa nini?
    Wawe na mipango gani?
    Atakayewaokoa ni nani?
    Naapa!
    Mie mwenye kuogopa,
    Moyoni n'akana pupa,
    Sitoridhia kuwapa,
    Mwangaza mloutupa,
    Kwa kukubali kutumiwa.
     
      Ewe nafsi yangu iliyotua!
    Rejelea,
    Takata,
    Fumbata,
    Tendata.
    Ole wenu nyie!
    Hakika watu waema,
    Watauka dunia hii,
    "Takuwa kama punje,
    Zihesabiwazo moja kwa moja,
    Siku hiyo bila shaka,
    Wataondolewa mipaka.
     
    Ole wenu watu!
    Nyinyi mpunjwao,
    Nyie mteswao,
    Nyinyi mnyonywao,
    Nyoyo zenu zikandamizwazo,
     
    Watesi wawatesao,
    Wabadilikao kila kuchao,
    Sisi tutajuaje nyuso zao?
         Kisha...
     
      tua

    (Watu wa Kesho - Nyamboga Daniel)
    1. Kwa kurejelea hoja tano, fafanua shauku alizonazo nafsineni kwa watu wa kesho. (alama 5)
    2. Fafanua mbinu za lugha alizozitumia mtunzi kufanikisha shairi hili. (alama 3)
    3. Fafanua muundo wa shairi hili. (alama 3)
    4. Eleza toni katika shairi hili. (alama 2)
    5. Tambua na ueleze idhini za mshairi zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 3)
    6. Andika ubeti wa tano katika lugha ya nathari. (alama 4)
  2. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali
    Raia mwema ni yule aliyejaa utii
    Si ubishi na kelele, akanywalo hasikii
    Ni mwasi huyo jinale, achunguzwe kwa bidii
    Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye.

    Uonapo uhalifu, usambe huuzuii
    Ndiyo uovu uvunjifu, kamawe huzingatii
    Mwananchi mwadilifu, hilo halikadirii
    Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye.

    Utii kama haupo, sheria haziagii
    Imani huwa haipo, na mema hayatujii
    Usalama hufa papo, mara nchi ikadhii
    Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye.

    Nia za watu watano, ambazo hazififii
    Uchao ni tangamano, si chusa hawachukii
    Hushinda kumi na tano, ambao hawatulii
    Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye.

    Kila raia nchini, ni ile au hii
    Ana hisa wastani, ingawa haitumii
    Hazuiliwi hanani, kusema hatumbukii
    Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye.

    (Utii-Malenga wa Mrima, UOP, 1977)
    1. Kwa hoja sita, fafanua kibwagizo cha shairi hili. (alama 6)
    2. Huku ukitolea mifano, fafanua uhuru wa mshairi katika shairi hili. (alama 3)
    3. Eleza nafsineni katika shairi hili (alama 2)
    4. Taja na ueleze bahari zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 3)
    5. Taja na ufafanue fani mbili zilizotumiwa katika shairi hili (alama 2)
    6. Andika ubeti wa tatu katika lugha nathari. (alama 4)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

  1. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

    Ewe malaika wangu
    Uloshuka toka mbinguni
    Mbingu kapasua kwa heri
    Siku nipokukopoa
    Ulinitia furaha iliyopasua kifua
    Tabasamu kipajini pako
    Ilinitia tumaini, ikanisahaulisha zingizi
    Ikayayeyusha madhila, ya utasa wa miaka kumi
    Ikapeperusha mbali, cheko la ukewenza.

    Sasa napolia, wanitonesha jeraha
    Wanirejesha misri, kwa vitimbi-vya Firauni
    Kwa vitisho vya muhebi
    Talaka kuahidiwa, hadi mbingu
    Lipofungua milango ya heri.

    Silie mwana silie, walimwengu watakusuta,
    Tangu hapo tanabahi
    Vidume humu mwenu
    Kulia havikuumbiwa,
    Machozi na kekevu ni za kike fahamu,
    Jogoo halii daima huwika
    Nikikuona kigugumika hivi wanitia hangaiko
    Tumaini kuzima
    Udhaifu kiandama
    Moyo kutia hamaniko,
    Ananipigania nani?
    Watesi king'ang'ania
    Changu kujitwalia?

    1. Bainisha aina ya wimbo huu. Thibitisha jibu lako. (alama 2)
    2. Bainisha jinsia inayoongolewa kwenye utungo huu. Thibitisha (alama 1)
    3. Eleza nafsineni katika utungo huu. (alama 1)
    4. Onyesha unyanyasaji wa kijinsia unavyojitokeza katika utungo huu. (alama 2)
    5. Eleza majukumu manne ya utungo huu. (alama 4)
    6. Iwapo umehudhuria utendaji wa kipera hiki nyanjani eleza mbinu tano utakazoziona zikitumika kuwasilisha kifungu hiki. (alama 5)
    7. Fafanua matatizo matano yanayokumba maendeleo ya fasihi simulizi (alama 5)


Marking Scheme

Assumpta K. Matei: Chozi la Heri

  1. Lazima
    "Huyu ambaye mama alimwona kama gae, kumbe sasa ndiye chombo cha kunivusha bahari hii ya dhiki?."
    1. Eleza muktadha wa maneno haya. (alama 4)
      • Ni kauli ya Umu/Umulkheri
      • Anajisemea
      • Katika jiji la Karaha
      • Alipokutana na Hazina na kukumbuka namna mamake alivyomdhalilisha Hazina apo awali/ Hazina alipokubali kumsaidia.
    2. Bainisha mbinu mbili za lugha zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
      • Jazanda - gae (mtu anayedharauliwa)
      • Kinaya - anayedharauliwa kuwa na manufaa
      • Taswira - chombo cha kunivusha bahari hii ya dhiki
      • Swali balagha - kumbe sasa ndiye chombo cha kunivusha bahari hii ya dhiki?
    3. Kwa kurejelea wahusika mbalimbali riwayani, jadili mikakati kumi na minne waliyoichukua kuvuka bahari ya dhiki. (alama 14)
      • Kubadilisha mazingira kmf, Umu, Chandachema, Zohali.
      • Kuwekeza ughaibuni kwa mfano Songoa
      • Kuhamia ughaibuni kmf, Annete na wanawe
      • Kumwaya dukuduku kmf, Umu, Zohali, Chanda chema, Kairu na Mwanaheri
      • Kuandama utu kmf Umu
      • Kuchukua msimamo imara kmf Zohali anapoua nasaba yake na kukabiliana na majitu yaliyojaribu kuhujumu utu wake. Dick anaamua kuacha ulanguzi.
      • Kufuata ushauri kmf Dick
      • Kuandama elimu kama nyenzo ya kujiondoa kwenye hali ya dhiki kmf Ridhaa, Kairu, Zohali, Chanda chema.
      • Ajira kmf Chanda chema, Pete (ili kukimu mahitaji ya kitoto chake)
      • Kuweka/Kuhifadhi siri kmf, Chanda chema anapoweka siri ya Bw. Tenge.
      • Ujasiri mali kmf Ridhaa
      • Kuzinduka na kujitetea mkf Zohali.
      • Kujiepusha na uraibu kmf Hazina, Kipanga.
      • Kuishi pamoja na kuliwazana kmf Mwangeka na Ridhaa.
      • Kuingilia kilimo kmf Lunga.
      • Kura kuhesabiwa upya ili ushindi wa Mwekevu uthibitishwe.
      • Kuchimba visima na mabomba kmf Ridhaa katika maeneo kame.
      • Kujenga kitua cha afya cha Mwanzo Mpya pale ambapo familia ya Ridhaa iliteketea.
      • Kukubali kushindwa kmf Mwanzi
      • Kuomba talaka kunamfanya Selume aanze kufanya kazi na kujitafutia riziki.
      • Kuoa upya ili kujiondolea upweke na fadhaa kmf Mwangeka, Apondi
      • Kuzaliwa kw Don Ridhaa kunamfidia Ridhaa mjukii na Mwangeka mwanawe.
      • Ushauri nasaha kmf Mwalimu Dhahabu kwa Umulkheri Kipanga.
      • Kutumia vyombo vya usalama kmf Umu kupiga ripoti kwenye kituo cha polisi.
      • Kuolewa/ndoa - mamake Sauna anakubali kuolewa na Bw. Maya ili kumwondoa katika umaskini.
      • Kulipa karo kidogo kidogo kmf Mamake Kairu.
      • Kusaka asili na fasili kmf Chanda Chema
      • Kupanga mtoto kmf Mwangemi na Neema.
      • Kuhimizana/kutiana moyo kmf Chanda chema, Kairu, Umu, Zohali na Mwanaheri.
      • Msamaha/Kusamehe kmf Dick anakubali kumsamehe mamake, Kipanga.
      • Kuimba/Kughani mashairi na nyimbo kmf Shamsi, Tila na wenzake wanaimba mbolezi, Terry alimwimbia, Mwangeka wimbo wa kumtuliza.
      • Kuunda vikundi vya uanaharakati kupiga vita mila na tamaduni potovu kama ukeketaji kmf Mzee Maarifa.
      • Kutafuta rasilimali zaidi kmf Mwimo Msubili
      • Kuwajuzi wazazi kmf Ridhaa
      • Wazazi kujukumika Kuzungumza na wanafunzi kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani, kmf Wazaziwe Ridhaa.
      • Imani/kuamini/ucha Mungu kmf Umu.
  2. "Uliyavulia nguo sharti uyaoge. Kesho ya Pili na Pendo na watoto wengine iko mikononi mwetu.”
    1. Umuhimu wa tamathali mbili za usemi.
      • Jazanda - kumewaka na kutateketea kuonyesha kupamba kwa harakati.
      • Nidhaa/siahi - Liwalo na liwe!-Kuonyesha uimara wa wanamapinduzi.
      • Msemo -Liwalo na liwe! Kuonesha uimara wa wanamapinduzi.
    2. Mchango wa vijana katika ustawi wa jamii.
      • Kupinga uongozi mbaya. Tunu na Sudi walishirikiana katika kumwondoa Majoka mamlakani.
      • Kupinga ufisadi - Tunu anapinga ufisadi wa Majoka wa kulinyakua soko la Chapakazi ili ajengeshe hoteli ya kifahari.
      • Kuendeleza maadili. Sudi-hakulala na Tunu licha ya kuwa pamoja kila wakati.
      • Kupinga tamaa. Mfano ni Tunu ambaye nia yake ya kumpinga Majoka si kuwa kiongozi bali kuleta mageuzi chanya katika jamii.
      • Kuna haja ya kuwa watu wenye bidii na wanaowajibika kazini. Sudi alifanya kazi yake ya kuchonga vinyago kwa bidii na uaminifu. Anakataa kishawishi cha Kenga kumchongea kinyago ili anufaike.
      • Sudi anatetea haki ya wanawake / kubadilisha mtazamo hasi wa watu kuhusu wanawake anachonga kinyago cha shujaa wa kike Sagamoyo ambaye ni Tunu.
      • Kukuza talanta - Sudi ni msanii wa kuchonga vinyago vizuri.
      • Tunu anatumia elimu kuifaidi jamii. Ni mwanasheria ambaye anatumia kisomo chake kutetea haki za Wanasagamoyo.
      • Kulinda katiba - Tunu anashtumu kitendo cha Majoka kumpa Asiya kibali cha kuuza pombe haramu kwani ni kinyume cha katiba ya nchi.
      • Kulinda uchumi - Sudi anakataa mradi wa kuchonga kinyago kwani kwake ni ubadhirifu mkubwa wa raslimali.
      • Tunu anamweleza Sudi kuwa kesho ya Pili na Pendo iko mikononi mwao ili kuonyesha umuhimu wa haki za watoto.
      • Kupitia kwa Tunu na Sudi, wanatudhihirishia umuhimu wa kusameheana na kutolipiza kisasi. Si kama walevi waliomgeuka Asiya na kumwaga pombe yake kwa kuwapunja.
      • Ashua na Tunu walikataa kazi walizopewa na Majoka ili kuonyesha umuhimu wa bidii na kujitegemea, hawategemei mapendeleo kutoka kwa viongozi.
      • Kupinga mauaji ya raia - Tunu ana mkakati wa kuwaleta wachunguzi kutoka nje kuchunguza upya ajali ya Jabali.
      • Tunu anataka watu wazingatie utu na anatoa tahadhari kwa Majoka kuwa yeye pamoja na watu wake watalipia kila tone la damu walilomwaga Sagamoyo.
      • Kurejesha haki kazini kwa kumpeleka Majoka mahakamani ili kupata fidia ya babake aliyefia katika Majoka and Majoka Company.
      • Tunu anaendeleza amani baina ya wananchi ili kuleta mabadiliko kwa kufanya maandamano ya amani.
      • Muungano na ushirikiano - Tunu anawaleta pamoja Wanasagamoyo wengi ili waweze kupigania haki yao.
      • Tunu anawaelekeza raia kuhusu uwajibikaji wao katika kuimarisha jamii. Anamkumbusha Sudi kuwa ana jukumu la kulinda uhuru, haki na maisha katika jamii.
      • Tunu anapinga na kuendeleza vita dhidi ya kufungwa kwa watu bila hatia. Anamwambia Majoka kuwa watamwachilia Ashua.
      • Tunu anawazindua watu kuhusu huduma walizonyimwa na viongozi kama maji, umeme, mazingira safi, elimu na kadhalika.
      • Kujiepusha na mienendo hasi - Siti anaamua kuacha kabisa tabia ya ulevi.
      • Jamii yenye ukarimu na upendo na kujali maslahi ya wengine - Tunu anamwagiza Siti awapeleke wanawe Sudi wapewe chakula na mamake Bi. Hashima.
  3. "Afadhali hapa pana amani. Nikiwa hapa sikutani nawe na huyo kirukanjia wako. Si mwoane yaishe!"
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      Ni Ashua kwa Sudi gerezani alipotaka kupewa talaka yake kwa sababu amechoka kupendwa kimaskini.
    2. Matumizi ya kinaya
      • Habari zinazotolewa na mjumbe ni za kinaya, kuwa Wanasagamoyo wafurahie ufanisi ambao umepatikana katika kipindi cha miaka tisini baada ya uhuru. Ujumbe huu ni kinaya kwa vile Sagamoyo hakuna maendeleo wala ufanisi. Watu wana njaa na wanakosa mambo ya kimsingi kama vile maji, elimu na matakwa mengine mengi.
      • Boza anadai kuwa kulipa kodi ni kujenga nchi na kujitegemea. Kauli hii ni kinaya kwa vile kodi wanayolipa Wanasagamoyo haitumiki kujenga nchi kwa vyovyote vile.
      • Sudi anasema kuwa katika kipindi cha mwezi mzima wa uhuru wale mali walizochuna kwa miaka sitini. Ni kinaya kwa kuwa hakuna walichovuna, viongozi wamejilimbikizia mali.
      • Boza anamwambia Sudi kuwa wanatia doa kwa kila jambo nzuri. Ni kinaya kwa vile hakuna mambo mazuri ambayo Majoka amefanya Sagamoyo. (uk 5)
      • Wanasagamoyo kusherehekea miaka sitini ya uhuru ni kinaya kwani hakuna cha muhimu kusherehekewa, hakuna maendeleo Sagamoyo.
      • Mzee Majoka kudai kuwa anamheshimu sudi ni kinaya. Majoka hana heshima kwa raia wake, nia yake ni kutaka Sudi amchongee kinyago. (uk13)
      • Kinaya kuwa sumu ya nyoka (dawa za kulevya) anayotengeneza Majoka katika kampuni yake inamdhuru hata mwanawe Ngao Junior. Tunaarifiwa kuwa Ngao Junior alikufa kutokana na sumu ya nyoka.
      • Majoka kudai kuwa takataka za soko zitaharibu sifa nzuri za jimbo la Sagamoyo ni kinaya kwa vile hakuna sifa nzuri Sagamoyo. Viongozi wanaendeleza maovu na hata kupanga mauaji.
      • Kauli ya Husda kuwa Ashua ni kimada wa Majoka ni kinaya kwa vile Ashua hana nia yoyote na Majoka. Amefika kwake kuomba msaada.
      • Ni kinaya kwa polisi Sagamoyo kutawanya waandamanaji. Polisi wanapaswa kulinda na kutetea haki za wananchi.
      • Majoka kusema kuwa Sagamoyo wanajiweza ni kinaya. Watu wana matakwa mengi, ni maskini, wana njaa na hata kupata ufadhili kutoka nje kwa miradi isiyo muhimu.
      • Ni kinaya Kenga anapomwambia Majoka aache moyo wa huruma, kwa sababu Majoka hana hata chembe cha huruma. Anapanga mauaji na kunyanyasa raia.
      • Majoka anaposema kuwa juhudi za Tunu kuandaa migomo hazitamfikisha mahali ni kinaya kwa vile Tunu wanafanikiwa katika maandamano yao na hata kuungwa mkono na wengi.
      • Ni kinaya kwa Ashua kumwambia Sudi kuwa ni kosa lake kutiwa ndani. Kosa ni la Majoka na njama yake ya kutaka kuchongewa kinyago.
      • Ashua anasema kuwa katika jela kuna amani na amechoshwa na Sudi. Ni kinaya kwani Ashua anapata maumivu akiwa jelani.
      • Uvumi unaoenea kuwa Sudi na Ashua ndio wanaowinda roho ya Tunu ni kinaya kwani wote hawa ni wanamapinduzi wanaopigania haki Sagamoyo.
      • Madai ya Ngurume ni kinaya kuwa tangu-soke kufungwa-Sagamoyo ni pazuri mno Eti mauzo ni maradufu ilihali watu hawana mahali pa kuuzia bidhaa zao, kufungwa kwa soko kunawahangaisha raia hata zaidi.
      • Ngurumo kusema kuwa pombe ni starehe ni kinaya kwani watu wanaangamia kutokana na pombe, wengine kuwa vipofu.
      • Watu wengi wanatarajiwa kufika katika uwanja wa ikulu ya Majoka kusherehekea uhuru siku ya sherehe lakini ni kinaya kwa kuwa ni watu kumi tu ambao wanafika.
    3. "Asasi ya ndoa imo hatarini." (alama 7)
      • Mapenzi yanayoegemea upande mmoja. Sudi anampenda Ashua kwa dhati, anajitahidi kwa udi na uvumba ili kumkidhi Ashua. Kila kitu anachokipata humletea ilhali Ashua haridhiki na hili.
      • Kutoaminiana, Ashua anamshuku mumewe kuwa ana mipango ya kimapenzi na Tunu.
      • Kukosa uvumilivu. Ashua amechoshwa na Sudi na anasema kuwa ni afadhali alipo jelani. Anadai kuwa, mawazo ya Sudi, hisia zake, nafsi yake na kila kitu chake kimesombwa na Tunu.
      • Tamaa na ubinafsi, Ashua ametawalwa na tamaa ya mali na kumwambia Sudi kuwa amechoka kupendwa kimaskini, anabadilika akiwa ndani kwa Majoka, awali alimpenda mumewe kwa dhati lakini baadaye anaomba talaka. Anafurikwa na tamaa na ubinafsi.
      • Lawama, Majoka anamlaumu Husda kuwa hampendi bali aliolewa na mali yake.uk 75)
      • Hakuna mapenzi ya dhati katika ndoa. Majoka hampendi Husda. Alimwoa ili kutimiza wajibu wake katika jamii na kama kiongozi, alipaswa kuoa. Alilia usiku huo baada ya kumwoa Husda lakini moyo na nafsi yake viko kwa Ashua. (uk. 75)
      • Ukware / ukosefu wa uaminifu. Majoka anampenda Ashua zaidi ya kumpenda hata anaweza kumfia. Anapanga njama ili kumpata. Majoka anakiri kuwa Ashua anamuua moyoni kwa penzi (uk 76).
      • Unafiki. Baadhi ya wanaume huoa ili kutimiza matakwa yao na wanawake huolewa kwa sababu ya tamaa ya mali na ubinafsi - Husda.
      • Ukosefu wa heshima katika ndoa. Wanaume wanapaswa kujidadisi na wakae na wake zao kwa heshima. Wanawake nao wanapaswa kujirudi vinginevyo asasi ya ndoa imo hatarini. (uk 77)
      • Kutotimiza wajibu wa ndoa sawasawa. Sudi anajitosa na kuzama katika siasa na kutelekeza majukumu yake kwa familia yake, jambo linaloleta mfarakano na mkewe Ashua.
      • Vitisho na hujuma, Majoka anamwuuliza Husda kama amemsahau kumaanisha humnyanyasa.
      • Uvumi / porojo. Mafatani wanadai kuwa Sudi ana uhusiano wa kimapenzi na Tunu jambo linalowafarakanisha na mkewe Ashua
  4.  
    1. "Pale nilipokwenda kulelewa palikuwa jehanamu kwangu. Mara moja nilifahamu kwamba nilikuwa mtumwa wa nyumba hiyo."
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
        Haya ni maneno ya Bogoa Bakari anawaambia mkewe Sakina, Sebu na mkewe Tunu, Kazu na mkewe Bi Temu (ataje angalau wahusika wawili ndipo atuzwe) Wamo katika kilabu ya Pogopogo. Bogoa anawasimulia hadithi kuhusu jinsi alivyotolewa nyumbani kwao na kupelekwa kwa Bi. Sinai aliyemtesa sana.
      2. Bogoa kulelewa katika jehanamu. (alama 8)
        • Kutengwa na wazazi - Bogoa anatengwa na wazazi na familia yake akiwa na umri wa miaka mitano tu. Anakosa mapenzi ya wazazi ambayo ni haki ya msingi ya kila mtoto.
        • Ajira ya watoto - Matajiri wanawafanyisha kazi watoto na kuwanyima haki ya kupata elimu, Bi. Sinai anampa Bogoa kazi za sulubu ingawa yeye Bogoa ni mtoto mdogo anayestahili kwenda shule. Anamlazimisha kuamka alfajiri achome maandazi kisha aende kuyauza shuleni.
        • Elimu - Jamii hii inawanyima elimu watoto kutoka jamii maskini. Badala ya kuenda shule, watoto hao wanafanyishwa kazi za sulubu. Bi. Sinai anasema Bogoa anafaa kutumwa bali si kusomeshwa.
        • Kunyimwa haki ya kucheza na kutangamana - Bogoa anakosa uhuru wa kucheza. Hapewi ruhusa ya kutangamana na watoto wenzake na wale wa Bi. Sinai
        • Lishe duni - Bogoa akiwa nyumbani kwa Bi. Sinai anakosa lishe bora ambayo ni haki ya kimsingi ya kila mtoto. Anakula makombo.
        • Kukosa usingizi wa kutosha - Watoto wana haki ya kupata usingizi wa kutosha. Bogoa alinyimwa haki hii ya kimsingi, ilibidi aamke alfajiri kuchoma maandazi kisha kwenda kuyauza shuleni.
        • Kuteswa na kupigwa/adhabu kali inayodhuru - Ni haki ya kila mtoto kuhisi salama na kupewa adhabu isiyomdhuru kisaikolojia na kimwili. Hata hivyo, Bogoa anapigwa kipopo, kutusiwa na hata kuchomwa viganjani kwa kijinga cha moto akiwa kwa Bi. Sinai.
        • Haki ya kujieleza - ni haki ya mtoto kutoa maoni yake kuhusu anavyohisi lakini Bi. Sinai anamtahadharisha Bogoa kuwa atamkata ulimi iwapo angemwambia yeyote Wanavyoishi ndani.
    2. Sababu zinazomfanya Dennis kulia. (alama 8)
      • Dennis na wanafunzi wengine wanakaliwa na ugumu wa masomo katika chuo kikuu.
      • Umaskini unatatiza masomo na mapenzi ya Dennis Machora.
      • Mapuuza ya wahadhiri kama Dkt. Mabonga
      • Njaa-Dennis alikuwa na unga wa kutengeneza uji kikombe kimoja bila sukari / Dennis alikosa chakula alikunywa uji (chamcha) wanafunzi wengine walitoka aila zenye nafasi. Mfano: Penina
      • Kutamauka. Masomo chuoni yanakuwa magumu kiasi kwamba Dennis na wanafunzi wenzake wanatamani kuyaacha.
      • Shirikizo la rika - Dennis alitamani kuvaa kama wenzake na vile vile kuwa na vifaa vya kieletroniki kama vya wenzake.
      • Wazazi wa Dennis wanafanya kazi ya vibarua. Walikuwa wachochole na hawakuwa na mali yoyote.
      • Dennis alikuwa mwanachuo wa tabaka la chini. Umaskini uliostakimu kwao hauna mfano. Kila asubuhi waamkapo, mipini ya majembe huwa mabegani mwa wazazi wa Dennis kutafuta kibarua cha kuwalimia matajiri mashamba.
      • Dennis anayamezea mate magari makubwa makubwa ya watu wenye nacho.
      • Dennis alihizika akiwa chuoni kutokana na umaskini wake anapowatazama wanafunzi wenzake walivyonenepa na kuwanda. Mavazi yao ni laini kutolca Uingereza, Ujerumani, Marekani, na Ufaransa.
      • Kutazamia shule za vijijini kumwibua bingwa katika mitihani ya kitaifa ni kama kutarajia kupata maziwa kutoka kwa kuku.
      • Mavazi ya Dennis ni duni, kula kwa shida.
      • Utabaka chuoni. Wenye jadi kubeli wanapita juu na wachochole wanapita chini ingawa wamo katika chuo kimoja na wanafanya masomo mamoja.
  5.  
    1. Mbinu ya uzungumzi nafsi kukuza wahusika
      Samueli
      • Mwenye majigambo: Anajitapa kwa mpenzi wake Nina kuwa ni bingwa masomoni. "...Mimi tangu hapo najijua bwana. Sina moyo wa bua. Mitihani hainibabaishi sana."
      • Mshirikina - kauli yake: "tena angaa sikukutana nap aka mweusi njiani siku zote za mitihani..."
      • Mwenye imani / kujiamini - alijiamini kwa uwezo wake masomoni. "lakini mimi mwenyewe najiamini. Lazima mtu ajiamini.
      • Mtamauka - Anakosa hamu ya kuishi na kuamua kujitoa uhai baada ya kupokea matokeo duni ya mtihani. "...kuishi kuna maana gani tena? Acha nijiondoe duniani niwaache wafanisi wafanikie..."
      • Bwege: Kutokana na majibu ya yale ambayo anasema anayajua, anaonyesha kuwa zuzu na si ajabu alifeli mtihani. "... Ninajua ya kwamba Mto Limpopo upo Misri na Mto Zambezi upo Tanzania..." .
      • Mcheshi: Anachekesha kwa kauli yake kuhusu mwalimu mkuu. Anasema: "Labda mwalimu mkuu kazidiwa na maumivu. Labda anataka kufanyiwa operesheni ya ubongo ama anahitaji maombi hasa atakuwa na akili razini tena"
      • Mcha mungu/msalihina-anamwomba Baba ampokee na amtengee nafasi mbinguni.
        "...Naja huko juu mbinguni mapema kidogo Baba. Nitengee nafasi..." 
      • Mpyaro - anamrejelea mwalimu mkuu kuwa hambe. Samueli anajisemea, "...Hajawahi kuniamini huyu hambe..."
      • Mwenye mtazamo hasi - anafadhaika na kujawa na mawazo mengi hasi baada ya kufeli mtihani. "...Hivyo ndivyo kusema sijui lolote wala chochote. Kwamba mimi si chochote wala lolote katika medani ya masomo?
      • "...Sasa vipi mambo yakiwa hivyo? Atanifikiriaje? Mwongo? Zuzu?..."
      • Mvumilivu - Alivumilia "miaka ya kirago cha kila siku cha kilomita sita kwenda shule ya upili ya Busukalala na kilometa sita kurejea nyumbani Busuamka"
      • Mwenye bidii: Anasema alikuwa akitembea mwendo wa kilomita sita kuenda shuleni kila siku na kuwa alihudhuria madarasa yake vizuri. "miaka ya kirago cha kila siku cha kilomita sita kwenda shule ya upili ya Busukalala na kilometa sita kurejea nyumbani Busuamka"
        Baba yake Samueli
      • Mwenye hasira - Samueli anasema kuwa hatayalewa matokeo yake duni. Samueli anajisemea "Mama anaweza kuelewa kidogo. Lakini baba! Nitamwelezaje haya?"
        Mama yake Samueli
      • Ni mwelewa - Samueli angaelewa matokeo yake duni. Samueli anajisemea "Mama anaweza kuelewa kidogo. Lakini baba! Nitamwelezaje haya?"
        Mwalimu Mkuu
      • Mwenye mapuuza. Samueli anasema hakuwahi kuamini uwezo wake masomoni. Samueli anajisemea, "...Hajawahi kuniamini huyu hambe..."
    2. Busara maishani
      • Mwalimu Mosi anawakumbusha watu wampigie Jairo makofi anapotoka jukwaani hata ingawa alimsimanga
      • Mwalimu Mosi alimshauri Jairo asinywe tembo kwani ni kitu kibaya.
      • Mosi alimshauri Jairo kuepukana na ufuska na asubiri hadi ndoa ndipo kuchuna ngozi.
      • Mwalimu Mosi alimpa Jairo matumaini kuwa uzuzu wake utakwisha na kwamba sufuri zake masomoni zitapisha mia kwa mia.
      • Mwalimu Mosi aliwapa watu wa tabaka la chini nafasi ya kuhutubu kama vile Jairo bila kuwatenga. Mikononi mwake mwalimu Mosi, watoto wengi walifinyangwa mpaka wakawa mawaziri, wahadishi, wahasibu na kadhalika.
      • Mwalimu Mosi alikuwa mwenye subira, shime na wa kutoa wosia wa kuwaelekeza wanafunzi.
      • Mwalimu Mosi anaamua kumpa Jairo zawadi zote alizoletewa baada ya kuona hali ngumu ya maisha anayopitia.
      • Jairo anaonyesha busara ya kuomba msamaha kwake Mwalimu Mosi baada ya kumwendea kwa hasira kuwa amemtorosha bintiye waishi mjini ila ilikuwa porojo.
      • Mwalimu Mosi akiwa angali mwalimu aliwafunza wanafunzi maadili mema yasiyotetereka na kuwatunza wote bila kuwadhulumu.
      • Mwalimu Mosi aliweza kujikakamua tangu utotoni na kujikwamua kutoka kwa ufukara.
      • Bi. Sera anaonyesha busara kwa kumkataza Mwalimu Mosi kuwafurusha mkewe Jairo na wanawe.
      • Familia ya Mwalimu Mosi inampa mke wa Jairo nyumba kwenye kiambo ambako anakaa na watoto wake.
      • Kijiji kizima kilikuwa na sulubu ya kumzuia Jairo asijitoshe mtoni baada ya kugundua uozo wake wa kuumbulia jina Mwalimu Mosi.
      • Mwalimu Mosi alitaka kuandika tawasifu ya maisha yake tangu utotoni na uwajibikaji wake maishani ili awaachie watu kielelezo cha kufuata.
      • Mwalimu mosi aliwapa wanafunzi wake nasaha na kuwa mkarimu, hekima, ustaarabu, uadilifu, uajibikaji, na mcheshi.
      • Wasemaji wengine katika hotuba zao walimsawiri Mosi kama mtu mkamilifu asiyekuwa na taksiri, mwalimu bora, mwadilifu, asiyeweza kudhuru yeyote na kiumbe kilichokamilika.
      • Wanafunzi na wazazi walitoa zawadi kwa mwalimu Mosi za kila nui.
      • Mwanafunzi mmoja wa zamani alijitolea kumpelekea mwalimu Mosi zawadi nyumbani kwenye gari lake aina ya pickup.
  6. USHAIRI
    1. Shauku za nafsineni (alama 5)
      • Wananchi wengi wanadanganywa na viongozi - nyoyo zenu kuzibembeleza -
      • Wananchi wanaishia kujutia kuwachagua viongozi wakipanda ngazini, mtajutia matendo yenu
      • Atakayewatetea kizazi cha kesho ni nani
      • Watakachokula
      • Hofu ya kufungwa
      • Hofu ya mateso ya kesho
      • Hofu ya kizazi chenye watu wema kupotea duniani
      • Hofu ya watu wakandamizao wengine -
      • Hofu ya watu wasioeleweka wabadilikao kila kuchao
    2. mbinu za lugha (alama 3)
      • Nidaa - naapa! Ewe nafsi yangu iliyotua!
      • Maswali ya balagha-watatetewa na nani? Watakula na kunywa nini? Wawe na mipango gani? Atakayewaokoa ni nani?
      • Mdokezo - kisha..... tua
      • Jazanda-dhoruba, kupanda ngazi
      • Taswira-kupanda ngazi
    3. Muundo wa shairi hili. (alama 3)
      • Shairi lina beti nane
      • Idadi ya mizani ya kila mshororo inabadilika badilika
      • Idadi ya mishororo katika kila ubeti inabadilika badilika
      • Ubeti wa shairi una kipande kimoja -
      • Shairi linafuata umbo la kwenda mbele na nyuma msuko suko) 
    4. Toni katika shairi. (alama 2)
      • Toni ya kiuanaharakati ni ujumbe wa kuwazindua wanajamii kuwachagua viongozi waliowajibika
      • Toni ya kuzindua-watakaokuja kesho wanaonywa
      • Toni ya kuhamazisha-nafsi yahu iliyotua, rejelea, fumbata, takata.
      • Toni ya kusuta - ole wenu! 
    5. Idhini za mshairi katika shairi. (alama 3)
      • inksari-'takuwa badala ya watakuwa, n'akana badala ya ninakana,
      • mazida-Waema badala ya wema
      • vikale - Watauka badala ya watakufa
    6. Anasema kuwa watu wema wataadimika duniani na kuwa kama punje zihesabiwazo moja moja. Anasema kuwa siku hiyo itakapokuja, watu wema wataondolewa mipaka na kufaidi kutokana na wema wao.
  7.  
    1. kwa hoja sita, fafanua kibwagizo cha shairi hili. (alama 6)
      • Raia mbishi
      • Raia ambaye hasikii hakanywalo
      • Aonapo uhalifu hauzuii
      • Huwa na nia mbaya ambazo hazijengi -
      • Hakadirii kuwa mtu mwema
      • Raia fisadi hana utii
      • Raia fisadi hupoteza usalama
    2. uhuru wa mshairi katika shairi hili. (alama 3)
      • inksari - akanywalo badala ya analokanywa, nchiye badala ya nchi yake
      • kuboronga / kufinyanga / kubananga sarufi / miundo ngeu ya kisarufi / ukiukaji wa kisintaksia/kisarufi - Ni mwasi huyo jinale badala ya jinale ni mwasi huyo, na mema hayatujii badala ya na hayatujii mema
      • vikale - usambe - usiseme
    3. raia mwadilifu-raia asiyetii, ni fisadi kwa nchiye
    4. bahari
      • mathnawi-beti katika shairi zina vipande viwili, ukwapi na utao
      • tarbia- kila ubeti una mishororo mine
      • ukara - vina vya nje vinatirirka,vya ndani havitiririki
    5. fani
      • tashhisi - usalama hufa
      • takriri - vina vya utao: i na kibwagizo: Raia asiyetii, ni fisadi wa nchiye.
    6. Anasema kuwa, kama nchi imekosa wananchi watiifu sheria hazipendezi wala mema kutujia kwa kuwa hakuna Imani. Usalama katika nchi haupo na nchi huishia kupotea. Kwamba raia asiyetii ni fisadi wa nchi yake.
  8. FASIHI SIMULIZI
    1. Bainisha aina ya wimbo huu. Thibitisha jibu lako. (alama 2)
      Bembelezi kwa sababu Mwimbaji anasema; -
      • Sasa unapolia wanitonesha jeraha.
      • Silie mwana silie
      • Vidume humu mwenu havikuumbiwa kulia.
      • Machozi ni ya kike jogoo halii.
      • Nilikuona kigugumika hivi wanitia hangaiko.
    2. Bainisha jinsia inayoongolewa kwenye utungo huu. Thibitisha. (alama 2)
      Jinsia ya kiume. Sababu:
      • Vidume humu mwenu havikuumbiwa kulia.
      • Jogoo halii
      • Machozi na kekevu ni za kike.
    3. Eleza nafsineni katika utungo huu. (alama 2)
      Nafsineni ni Mama mtoto. Mifano:
      • Kuahidiwa talaka mtoto aliapo.
      • Siku nilipokukopea ulinitia furaha.
      • Nilipokukopoa uliniondolea kicheko cha kuwa mke mwenza.
      • Madhila ya utasa wa miaka kumi uliniondolea.
    4. Onyesha unyanyasaji wa kijinsia unavyojitokeza katika utungo huu. (alama 3)
      • ✓ Nafsineni alipokosa kupata mtoto kwa miaka kumi aliitwa tasa na kutishiwa ukewenza.
      • ✓ Nafsineni alipokosa kupata mtoto kwa miaka kumi alitishiwa talaka.
      • ✓ Kauli ya nafsineni kwa mwanawe wa kiume kuwa Vidume humu mwenu havikuumbiwa kulia, Jogoo halii, Machozi na kekevu ni za kike ni za kukandamiza jinsia ya kike.
    5. Eleza majukumu manne ya utungo huu. (alama 4)
      Majukumu tano ya mbembelezi.
      • Hutumbuiza na kuongoa watoto ili walale au wanyamaze wanapolia.
      • Hutumiwa kama sifa kumsifu mtoto ambaye ni mtulivu.
      • Husawiri mfumo wa kiuchumi wa jamii husika. Ikiwa baba na msasi, mtoto anatajiwa kuwa baba ni msasi jasiri au yuko karibu kutoka usasini.
      • Husawiri mahusiano katika jamii. Kupitia bembelezi mlezi huweza kuibua migogoro iliyomo kati yake na wazazi wake au wazai wa watoto.
      • Hutakasa hisia ambazo mwimbaji huweza kuwa nazo.
      • Huwaelimisha watoto hata katika umri huu mchanga kuhusu mambo na shughuli mbalimbali katika jamii na umuhimu wake.
      • Huonya watoto dhidi ya tabia hasi. Mfano: Kulia ovyo.
      • Husawiri falsafa au mtazamo wa jamii kuhusu jinsia na matarajio ya jamii kwa jinsia fulani. Mfano: Machozi ni ya kike sio ya kiume.
    6. Mbinu za kuwasilisha nyimbo. (alama 5)
      • Ukakamavu wa kuweza kuimba hadharani.
      • Uchangamfu na ucheshi ili kunasa makini ya hadhira na kuzuia isikinai.
      • Ufahamu mpana wa utamaduni husika ili kuzuia kutumia maneno na ishara zinazoweza kuwaudhi au kupingana na imani za hadhira.
      • Kushirikisha hadhira kama vile kuimba, ili isikinai.
      • Kuingiliana vizuri na hadhira ili aivutie.
      • Kumbukumbu nzuri ili uimbaji utiririke vizuri.
      • Kudramatisha ili kuonyesha picha fulani kama vile kuiga toni, sauti, na kiimbo kulingana na swala wasilishwa.
      • Viziada lugha/ kutumia ishara za uso, mwili na miondoko kulingana na hali anayoimba.
      • Ufasaha wa lugha ili kuwasilisha mawazo kwa njia mwafaka na inayovutia.
      • Kubadilisha toni na kiimbo kulingana na hali tofauti anazoimba kama huzuni
      • Kutumia ufaraguzi kutegemea hadhira na kutoa mifano inayofahamika kutoka katika mazingira ya hadhira.
      • Kutumia mtuo wa kidrama ili kuongeza taharuki, kusisitiza ujumbe na kuteka makini ya hadhira.
    7. Matatizo yanayokumba maendeleo ya fasihi simulizi. (alama 5)
      • Uvumbuzi wa vyombo vya mawasiliano kama tarakilishi.
      • Mitambo ya kuchapisha na kuhifadhi maandishi.
      • Dini ya Kikristo ambayo inapuuza baadhi ya vitendo au miviga ya Fasihi Simulizi.
      • Elimu ya kisasa haitambui wala kuthamini Fasihi Simulizi sana.
      • Waandishi wengi wa Kiafrika hawashughuliki Fasihi Simulizi.
      • Vifo vya fanani.
      • Ushindani wa Fasihi Simulizi na burundani ya kisasa.
      • Kuimarika kwa fasihi andishi ambayo inapendwa kuliko Fasihi Simulizi.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Maranda Post Mocks 2020/2021.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest