Kiswahili Paper 2 Questions with No Answers - Maseno Mock Exams 2020/2021

Share via Whatsapp

Kenya Certificate of Secondary Education
102/2- KISWAHILI -Karatasi ya 2
(LUGHA)
Muda: Saa - 2 ½

Maagizo

 1. Jibu maswali yote.
 2. Majibu yote yaandikwe katika nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali.
 3. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
 4. Usitoe ukurasa wowote kutoka kwenye kijitabu hiki.
 5. Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.


Maswali

 1. UFAHAMU

  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.

  Katiba ni utaratibu wa sheria unaoweka mpango wa jamii kuendesha mambo.Ni muhimu kila raia ajue katiba ya nchi yake.

  Katiba yaweza kuwa imeandikwa au haikuandikwa. Katika jamii za jadi, katiba ilihifadhiwa na kupokezwa kwa mdomo. Mtindo wa kuandika katiba ulianza nchini Marekani mwaka 1787. Ingawa katiba hii imefanyiwa mabadiliko hapa na pale,bado ni ileile. Kenya ilipowekwa chini ya himaya ya Uingereza mwaka 1895, ilianza kutumia katiba ya Uingereza. Baada ya masetla wa kikoloni kujikita, Kenya kuwa koloni. Hii ililazimu pawe na katiba nyingine mwaka 1920. Waafrika waliupinga mfumo huu kwa sababu haukuwahusisha kikamilifu kwenye masuala ya uongozi. Utetezi wa wanasiasa uliilazimisha serikali ya Uingereza kuitisha makongamano mbalimbali kama vile lile la Devonshire na mengine ili kurekebisha katiba. Waafrika hawakuridhika. Wakaendelea kudai katiba mwafaka. Harakati hizi zilileta kuitishwa kwa kongamano la katiba la Lancaster. Lengo lilikuwa kuandika katiba itakayotumiwa nchini hadi leo. Kati ya wajumbe walioenda Uingereza kuandika katiba mwaka 1962 ni pamoja na Tom Mboya, Jean Marie Seroney, Julius Kiano, Jomo Kenyatta, Masinde Muliro, Oginga Odinga, Ronald Ngala, Daniel Arap Moi na James Gichuru. Wengine ni Martin Shikuku, Dennis Akumu, Taita Towett, Abdilahi Nassir, Jeremiah Nyaga na John Keen.

  Katiba ni kitovu cha taifa. Baina ya mambo inayotekeleza ni kuweka utaratibu na kanuni za utawala, kwa mfano, utawala wa kimikoa na serikali za wilaya. Pamoja na haya, katiba hufafanua vyombo vikuu vya serikali ,mamlaka yavyo na mipaka yavyo ya kutenda. Vyombo hivi ni bunge, mahakama, urais, jeshi n.k. Hali kadhalika, katiba hupambanua haki za raia.

  Hii hudumisha demokrasia na huwawezesha wananchi kupata uhuru na haki za kimsingi. Katiba hukinga haki za kila raia, hasa kutokana na udhalimu wa wengi au wenye uwezo mkubwa. Zaidi ya yote, katiba huimarisha asasi za umma ili kudumisha uwajibikaji.

  Katiba huhalalishwa na watawaliwa. Hii hutokea wanaposhirikishwa katika uandishi wake. Kuanzia miaka ya themanini, raia walianza kudai katiba igeuzwe. Mwamko wa kutaka mageuzi ulianza kwa harakati za kubadilisha mfumo wa kisiasa kutoka ule wa chama kimoja hadi ule wa demokrasia ya vyama vingi. Haja ya mfumo mpya wa kisiasa ulilenga kuwashirikisha wananchi katika utawala na kuondoa uimla.

  Harakati zilitia fora miaka ya tisini. Mambo yaliyochochea hali hii ni mengi. Kwanza, katiba iliyokuwa imeandikwa na watu wachache ilikuwa imefanyiwa marekebisho mengi. Marekebisho haya yalimpa rais mamlaka mengi juu ya serikali kuu na vyombo tofauti vya serikali. Pili, viongozi na watu wenye uwezo na utajiri walipuuza katiba. Raia walihisi wanadhulumiwa. Walipinga hali ya wachache waliomzunguka rais kunufaika huku umma ukitengwa. Tatu, kutokana na uongozi uliokuweko wakati huo, wanawake, watoto na walemavu walidhulumiwa na kukosa uwakilishi ufaao.Hatimaye, pakawa na ongezeko la uharibifu wa mazingira, ufisadi na unyakuzi wa mali ya umma kama vile ardhi.

  Waliopigania katiba mpya walikuwa na haja ya katiba ambayo uandikaji wake ungewahusisha Wakenya wote. Mwanzoni, serikali ilipinga wito wa mabadiliko. Lakini mnamo mwaka 2001 iliunda Tume ya Marekebisho ya Katiba ili kutekeleza mahitaji ya wananchi. Tume hii iliwahamasisha na kuwashawishi raia kutoa maoni. Tume iliandaa vikao katika maeneo ya ubunge 210 ambapo wananchi walitoa mapendekezo kuhusu marekebisho ya katiba waliyotaka.

  Katika mapendekezo hayo raia walisisitiza mambo kadhaa. Jambo la kwanza ni utawala mwema na uwajibikaji wa viongozi na maafisa wa umma .Jambo lingine ni kulinda haki za binadamu zikiwemo za wanawake, watoto na walemavu. Raia walidai kanuni za usawa na ulinganifu. Aidha walitilia mkazo mahitaji ya msingi kama chakula, afya nzuri, makao, elimu, usalama, uchumi, na kadhalika.

  Msingi wa mapendekezo hayo yote ni kuwepo na amani ya kitaifa, umoja na uadilifu ili kulinda maslahi ya wananchi wote na taifa.

  Maswali :
  1. Eleza kilichosababisha kongamano la katiba la Lancaster (alama3)
  2. Taja mambo matatu yaliyotiliwa mkazo na raia katika maoni yao kuhusu katiba. (alama3)
  3. Eleza umuhimu wa katiba kwa mujibu wa taarifa. (alama3)
  4. Taja sababu zilizochangia ubadilishaji wa katiba. (alama3)
  5. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika taarifa. (alama3)
   1. Kitovu……………………………………………………………………………..................
   2. Harakati……………………………………………………………………………….........
   3. Hamasisha………………………………………………………………………………….
 2. MUHTASARI

  Soma taarifa ifatayo kwa makini kisha ujibu maswali yanayofuata.

  Nchi nyingi duniani zimetia saini mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu haki za watoto. Haki ni mambo mema ambayo watoto wanastahili kutendewa. Kwa kutia saini, nchi hizi zimetangaza kujitolea kwao kuzilinda na kuhahakikisha kuwa hakuna ukiukaji wake na kuwa watoto wote katika himaya zao wananufaika kutokana na haki hizi.

  Miongoni mwa haki hizi ni kuwa kila mtoto ana haki ya kuishi na kupata chakula cha kutosha na chenye viinilishe bora. Pili, kila mtoto ana haki ya kupata elimu. Elimu hii inafaa kutolewa bila ada na iwe inayofaa na inayopatikana kwa urahisi.Kisha kila mtoto ana haki ya kutopigwa na kutodunishwa kwa namna yoyote, iwe kitabaka, kirangi, kijinsia na vinginevyo. Mtoto ana haki pia kutolazimishwa kufanya kazi za kiutumwa, nzito na zakushurutishwa. Hali kadhalika, ana haki ya kuishi katika nyumba au makazi bora nasalama, kutunzwa na kulindwa dhidiya hali yoyote inayoweza kumhatarisha. Anatakiwa ashirikishwe katika kufanya maamuzi.Fauka ya haya, ana haki ya kupata huduma za afya,mahitaji maalum,michezo, upendo na habari. Isitoshe,anastahili kuheshimiwa kimawazo na kihisia. Haki hizi zinatakiwa kulindwa na kila mwanajamii, hivyo serikali za mataifa mengi zimeshirikisha haki hizi katika katiba za nchi zao na sheria zao.

  Walakini haki hizi bado zinakiukwa.Watoto wengi kote duniani bado wananyimwa haki zao. La kusikitisha na kukera ni kuwa wanaotarajiwa kuwa vigogo vya kuzilinda haki hizi, ndio wanaoongoza kuzikiuka. Kila siku tunasikia na kushuhudia visa vya watoto kupigwa, kunyimwa chakula, kufanyishwa kazi kipunda, kuteswa, kuishi katika mazingira hatari, na hata kuuawa. Kuna watoto wengi wanaolala nje, wengine hawapati chakula licha ya kuwa wanatakiwa kupata chenye lishe bora. Kwao kutarajiwa mlo awamu tatu kwa siku ni njozi kwani hata awamu moja ni adimu kupata.

  Watoto wengi katika mataifa yenye fujo na ghasia hutekwa na kutumikishwa vitani. Viongozi katika mataifa haya hawafanyi kitu ila kutazama tu wakati watoto wanaotakiwa kuwalinda wanageuzwa kuwa mibaba ya kuua na kuuana. Watoto hawa huvishwa magwanda ambayo miili yao minyonge haiwezi kuyahimili. Pia, huvalishwa mabuti ya kijeshi ambayo ni mizigo mizito ya kubeba mbali na bunduki zinazokaribia kuwazidi uzani wakati wanatakiwa kuwa wamelindwa majumbani, na shuleni na wazazi wao na serikali.

  Jukwaa la vijiji vya mataifa ya ulimwengu wa tatu limesheheni watoto wasioenda shule kwa sababu ya lindi la ufukara uliokithiri. Elimu ya bure inayogusiwa katika haki za watoto haipo. Wanaong’ang’ana iwepo ni kana kwamba ni waota ndotomchana. Jiulize watoto wangapi sasa hivi wamo majumbani bila kwenda shuleni kutokana na ukosefu wa karo? Wangapi wamo mitaani wakivuta na kunusa gundi huku wakiombaomba vishilingi?

  Hali ilivyo sasa hivi inadai kuwa mimi na wewe tufanye hima na kuungana mikono kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu haki za watoto. Twapasa kuhimiza serikali zetu kufanya kila ziwezavyo kuhakikisha kuwa watoto wote wamo shuleni. Nasi tushirikiane kutoa huduma kwa watoto na kukomesha dhuluma, mateso na dhiki kwao. Haitoshi kupeleka miswada mbungeni kuhusu haki za watoto na kuipitisha kuwa sheria. Twastahili kubadilisha misimamo yetu kuhusu haki hizi na kuzilinda kwa dhati bali si kwa chati.

  Maswali
  1. Fupisha aya mbili za kwanza. ( maneno 65-70) ( alama 8,utiririko 2 )

   Matayarisho

   Nakala safi

  2. Eleza ni vipi ukiukaji wa haki za watoto unaweza kuepukwa . ( maneno 30-35) (alama 4 , utiririko 1 )

   Matayarisho
   ……………………………………………………………………………………………………..
   ……………………………………………………………………………………………………..

   Nakala safi
   ……………………………………………………………………………………………………..
   ……………………………………………………………………………………………………..
 3. SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA (alama 40)
  1.  
   1. Sauti ni nini? (lama 1)
   2. Sauti gani ina sifa zifuatazo : (alama 1)
    Mbele, juu, tandazwa
  2.  
   1. Tunga sentensi moja kudhihirisha tofauti kimaana kati ya maneno yafuatayo : (alama 2)
    Tekeleza, telekeza
   2. Kwa kutolea mfano, eleza maana ya shadda. (alama 1)
  3.  
   1. Ainisha vielezi katika sentensi hii: (alama 2)
    Msichana yule aliongea kistadi kisha akaondoka kwa madaha.

   2. Tambua na ueleze aina za vitenzi katika sentensi : (alama 3)
    Mwalimu angali mgonjwa hata kama amekuwa akifunza darasani.

   3. Tunga sentensi kwa kutumia kihisishi cha kutakia heri. (alama 1)
  4. Akifisha sentensi ifuatayo: (alama 2)
   Lo mwalimu alimchapa vibaya hivyo, waziri aliuliza.
  5. Kanusha sentensi ifuatayo katika hali ya wingi . (alama 2)
   Mimi nikikosa nitakuja.

  6. Andika neno lenye muundo ufuatao. (alama 2)
   1. Kiambishi ngeli,wakati uliopita,mzizi,kauli tendwa,kauli tenda
   2. Kiambishi cha wingi,mzizi
  7. Tambua matumizi mawili ya kiambishi –li- na mawili ya kiambishi –ji- kama vilivyotumiwa katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
   Kijijiti kilichotumiwa kulipiga jitu kimevunjika.

  8. Andika sentensi ukitumia kauli iliyoko mabanoni. (alama 2)
   1. Hukumu (tendewa)
   2. la (tendeka)
  9. Kwa kutoa mifano, eleza miundo miwili ya nomino katika ngeli ya A-WA (alama 2)
  10. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya wingi (alama 2)
   Jipaka lile lilibebwa na jitoto lililosimama karibu na kilango
  11.  
   1. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mstari (alama 3)
    Huyu na yule walicheza mpira mbele ya nyumba

   2. Onyesha kijalizo katika sentensi ifuatayo (alama 1)
    Wambua ni mwanafunzi ……………………………………………………………………………

   3. Onyesha CH katika sentensi ifuatayo (alama 1)
    Tulitoka asubuhi na mapema……………………………………………………………………….
  12. Tumia neno fukia kutunga sentensi katika hali ya kinyume. (alama 2)
  13. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya udogo wingi. (alama 1)
   Kijana alichukua rununu yake.
  14. Unda nomino nyingine kutokana na nomino ifuatayo kisha uitungie sentensi. (alama 2)
   Mhadhara
  15. Tunga sentensi ukitumia neno kimya kama nomino na kielezi. (alama 2)
  16. Andika katika usemi halisi. (alama 3)
   Sista alisema kuwa angemwarifu endapo angemwona.
 4. ISIMUJAMII (alama 10)
  1. Eleza mitazamo minne kuhusu chimbuko la Kiswahili. (alama 4)
  2. Eleza sababu ambazo zimechangia kuenea kwa lugha ya Kiswahili nchini Kenya. (alama 6)

Huu ndio mwisho

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions with No Answers - Maseno Mock Exams 2020/2021.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest