Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Sukellemo Joint Mock 2020/2021

Share via Whatsapp

MTIHANI WA PAMOJA WA SUKELLEMO
KISWAHILI
KARATASI YA 2
LUGHA
Muda: Saa 2 ½

MAAGIZO

  • Jibu maswali yote
  • Majibu yote yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili sanifu.
  1. SEHEMU A:UFAHAMU (ALAMA 15)
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali:

    Miaka mingi ya kutawaliwa na wakoloni iliwafanya wananchi wengi kupuuza umaarufu na uadilifu wa lugha ya Kiswahili kama lugha ya taifa kwa manufaa ya kuarifiana habari mbalimbali kwa ufasaha na kuelewana vyema.

    Wakoloni pia waliwashawishi wananchi waone, kwamba lugha ya Kiswahili ni kwa ajili ya watu wale wasiokuwa na elimu na kwa wale ambao hawajastaarabika. Kwa wale wenye ‘elimu ya wastaarabu,’ wakoloni waliwashawishi kuamini kwamba lugha ya kigeni, yaani Kiingereza, ndiyo hasa lugha inayofaa kwa kujieleza na kufahamishana habari.

    Kutokana na vikwazo hivi si ajabu kuona hadi hivi sasa, mwananchi halisi akijitwaza kwamba hawezi kujieleza kwa ufasaha au kumpasha mwenzie habari kwa ukamilifu mpaka atumie lugha ya Kiingereza. Hata katika maofisi mengi ya serikali, hadi hii leo, japo imeshapitishwa kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya taifa bado utawaona wananchi wengine wanapendelea kuzungumza Kiingereza wao kwa wao, ili wajulikane kwamba wana kisomo na wamestaarabika.

    Vikwazo vya namna hii vimewalemea wananchi vile vile kwa upande wa magazeti. Utaona mwananchi ambaye anafahamu Kiingereza kidogo sana, akijinunulia gazeti kubwa la Kiingereza na kuanza kuzurura nalo kutwa nzima bila kuambulia mengi ndani yake. Pia utawasikia wananchi wengi wakijidai kwamba hawataki kusoma magazeti ya Kiswahili kwa sababu inakuwa vigumu kwao kuelewa mambo yaliyomo kama vile ambavyo wangelielewa katika gazeti la Kiingereza.

    Mabeberu wameshagundua kwamba tunao upotovu wa aina hiyo, ndipo utaona mara nyingi wanawaletea wananchi magazeti mengi ya Kiingereza, mengine yakiwa na nia ya kuwapotosha wakijua kwamba watayasoma tu, mradi yameandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

    Mara nyingi taifa fulani la kibeberu likitaka tuchukiane na taifa jingine ambalo ni adui yake kisiasa au kiuchumi, taifa hilo la kibeberu linaandika habari za uchochezi kwenye magazeti yao kwa lugha ya Kiingereza, mambo kuhusu taifa lile adui yake (ambalo si adui yetu).

    Magazeti hayo huandikwa kwa lugha nadhifu ya Kiingereza na kuletewa wananchi hapa nchini. Maskini wananchi wengine waliotopea kwa kudhani Kiingereza ndicho lugha nzuri ya Kigazeti , wanayanunua mara moja na kuanza kuyasoma magazeti hayo, na pia kuwapa watoto wao wayasome. Matokeo yake ni kwamba, bila kujitambua, wanajikuta wanayafanya yale mabeberu waliyotarajia wayafanye, yaani wanaanza kuchukiana bure na taifa lile ambalo ni adui wa mabeberu hao, lakini si adui zetu. Madhumuni ya kuandika habari kwenye magazeti, ni kutaka kuwafahamisha wasomaji mambo yaliyotokea au yatakayotokea siku hata siku, kwa lugha inayofahamika na kueleweka kwa urahisi bila kumtatiza msomaji. Ikiwa basi ndiyo madhumuni, kuna haja gani kutumia lugha ya kigeni ili kuwaelezea wasomaji wako jambo wangaliweza kuelezwa kwa lugha yao wenyewe ambayo wanaielewa vyema.

    Mtu aelezeapo jambo kwa maandishi akitumia lugha yake mwenyewe anaielewa vyema na ambayo pia wasomaji wake wataielewa kwa ukamilifu. Kwa ujumla jambo ambalo mwandishi huyo ataliandika kwa lugha ambayo ni ya asili yake ambayo anaielewa vyema, halitamtatiza msomaji wake ambaye pia anaielewa vyema lugha hiyo.

    Maswali
    1. Eleza mbinu zinazotumiwa na wakoloni kuwafanya wananchi kuidunisha lugha ya Kiswahili (alama 3)
    2. Thibitisha kuwepo kwa ukoloni mamboleo katika habari uliyosoma (alama 4
    3. Eleza jinsi wabeberu wanaweza kuzua vurugu katika mataifa mbalimbali (alama 2)
    4. Taja sababu ambayo imewafanya wananchi wengi kupuuza lugha ya Kiswahili (alama 1)
    5. Wakoloni wana mtazamo gani kuhusu lugha ya Kiswahili? (alama 2)
    6. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika taarifa (alama 3)
      1. Uadilifu
      2. Akijitwaza
      3. Waliotopea

  2. SEHEMU B:UFUPISHO
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali:

    Mirundiko ya taka pamoja na utaratibu usiofaa wa uzoaji wake ni tisho kubwa kwa siha ya umma pamoja na mazingira. Hii ni kwa kuwa taka huwa na makaazi ya wadudu na wanyama waharibifu kama nzi, mbu, kombamwiko na panya ambao hueneza magonjwa na kuharibu vitu vyenye thamani. Maji taka nayo, pamoja na mifuko ya plastiki, huwa mastakimu ya wadudu na virusi vinavyoleta magonjwa mbalimbali. Mifuko ya plastiki ina madhara zaidi kwa kuwa huziba mitaro ya maji na kuzuia upitaji wa maji. Madhara hutokeza wakati mvua za gharika zinaponyesha. Maji hukosa njia yake ya kawaida ambayo huwa imezibwa na mifuko hii. Maji haya husababisha mafuriko ambayo huleta hasara ya mali na wakati mwingine ya uhai. Fauka ya haya, mifuko hii huwasakama tumboni wanyama sio wa nyumbani tu, bali wa porini na majini.

    Kwa sababu ya hatari zitokanazo na taka, pana haja kutafuta njia na teknolojia ya kuweza kukabiliana na taka ili kuyatunza mazingira na siha ya umma. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kuelimisha na kuhimiza umma kuwa na uangalifu katika matumizi ya bidhaa na rasilmali ili kupunguza uzalishaji wa taka. Matumizi ya bidhaa kwa njia ya ubadhilifu huwa chanzo cha uzalishaji wa taka kwa wingi. Kwa mfano maji ni rasilmali ambayo imeendelea kutumiwa kwa ubadhirifu na hiyo huzalisha maji taka kwa wingi. Rasilmali hii inaweza ikatumiwa kwa uangalifu. Kwa mfano badala ya kutumia bafu ya mnyunyu kuogea, mtu anaweza kutumia maji ya karai.

    Watu wengi huchukulia taka kuwa kitu kisicho na manufaa yoyote. Hawajui kuwa kwa kutumia teknolojia endelezi, taka nyingi zinaweza zikageuzwa na kuwa na manufaa mengi. Vijana wadogo sehemu za mashambani wanahitaji pongezi kwa kuwa na utambuzi huu. Wengi kwa kukosa hela za kununua mipira ya viwandani hutumia makaratasi na mifuko ya plastiki kutengeneza mipira wanayoitumia. Hii ni teknolojia endelezi ambapo taka hugeuzwa na kuwa na manufaa.

    Baadhi ya wananchi wenye ubunifu nao wameanzisha miradi ya kuzoa takataka kutoka majumbani mwa watu. Hutoza ada fulani ya uzoaji, kisha huzipeleka taka hizi kule zitakakobadilishwa ili ziwe na manufaa. Mifuko na mabaki ya plastiki kama vile matangi, mitungi, sapatu na champali. Taka hizi huwa malighafi ya kutengenezea bidhaa nyingine. Taka za chupa na chuma nazo huuzwa katika viwanda vinavyozigeuza kuwa na manufaa tena. Taka za karatasi hutumiwa kutengenezea bidhaa kama vitabu, katoni, shashi za chooni, magazeti na kadhalika.

    Taka zinaweza pia kugeuzwa kuwa zenye faida kwa kuzitumia kufanyia mboji. Ni muhimu kutambua kuwa si kila aina ya taka inaweza kutumiwa hapa. Taka zinazoweza kufanyiwa mboji ni zile ambazo huoza kwa haraka nazo ni kama vile mabaki ya vyakula, mboga na matunda. Kwa sadfa, hizi ndizo taka zinazozalishwa zaidi siku hizi na hasa sehemu za mjini na katika maeneo ya biashara kama mikahawa, hospitali n.k. Mtu akiwa na nafasi anaweza kuchimba shimo ambalo atafukia taka hizi ili kutengeneza mbolea. Hii ni njia isiyodhuru mazingira nayo ina manufaa kemkem. Kwanza, hugeuza taka ambayo inaweza kuwa hatari na kuifanya iwe yenye manufaa. Kwa hivyo, hutatua matatizo ya kiafya yanayoweza kutokana na mirundiko ya taka. Mchanga nao hufaidika kupata virutubishi. Mbolea kama hii inaweza ikatumika kukuzia mboga au maua katika bustani.

    Maji taka, hasa yanayotumiwa kuoshea vyombo, nayo yanaweza kutumika kunyunyizia mashamba madogo ya mboga au bustani za maua. Maji taka haya yanahitaji kutayarishiwa njia mahususi ya kuyaelekeza katika mashamba haya baada ya kutumiwa.

    Aghalabu watu wengi wana mazoea ya kuchoma taka. Ni kawaida kupata matanuri ya kuchomea taka katika baadhi ya mitaa, shule, hospitali na kadhalika badala ya kupoteza moto bure inawezekana pakawekwa birika kubwa au tangi la chuma ambalo litatumia moto huo kuchemshia maji ambayo yanaweza kutumiwa katika shughuli za nyumbani.

    Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa kuna baadhi ya taka ambazo ni hatari na huenda zisigeuzwe ili kutumika kwa njia yenye faida. Taka hizi ni kama vile mikebe au vifaa vingine vyenye kubeba sumu au dawa hatari. Ni bora kuzitupa dawa hizi katika mashimo marefu au vyoo vya mashimo.Kwa vyovyote vile, si jambo muhali kuwa watu popote wanapoishi kulinda siha yao pamoja na kutunza mazingira. Ulinzi na utunzaji huu huhitaji uangalifu mkubwa katika utupaji taka.

    Maswali
    1. Bila kupoteza maana iliyokusudiwa na mwandishi, fupisha aya ya kwanza na ya pili.(Maneno 70) (alama 7,1 ya mtiririko)
    2. Kwa kuzingatia aya ya 3,4,5,6 na 7 eleza mambo muhimu anayoshughulikia mwandishi ( maneno 100– 120) (alama 8,1 ya mtiririko)

  3. SEHEMU C: SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
    1. Andika neno moja lilo na mpangilio wa sauti zifuatazo: kikwamizo sighuna cha ufizi, irabu ya mbele wastani, nazali ya midomo na irabu ya nyuma wastani. (alama 2)
    2. Eleza miundo ya silabi katika neno: mbilikimo. (alama 2)
    3. Tunga sentensi ya neno moja iliyo na vipashio viifuatavyo vya kisarufi: kiima, kiambishi cha wakati ujao, shamirisho kitondo, mzizi, kauli tendea na kiishio. (alama 3)
    4. Tunga sentensi moja kudhihirisha matumizi mawili ya kiambishi i. (alama 2)
    5.  “Akisa! Akisa! Mbona huitiki! Njoo hapa upesi!” mama alimwamrisha. (alama 3)
      Andika kwa usemi wa taarifa:
    6. Waumini wa kweli humcha Maulana kila wakati. (alama 1)
      Anza: Maulana…
    7. Kanusha kwa udogo: Ndovu huyu alimdhuru nguruwe huyo mchafu. (alama 2)
    8. Andika kunyume: Shamsi alilewa kisha akaukomea mlango wake usiku. (alama 1)
    9. Tunga sentensi moja yenye kiwakilishi cha A-unganifu, kitenzi kishirikishi kipungufu na kijalizo. (alama 3)
    10. Ziunganishe sentensi zifuatazo kwa kiunganishi cha masharti. (alama 2)
      Wakulima watapata mazao mazuri. Wakulima watazingatia kilimo cha kisasa.
    11. Tumia neno ‘mpaka’ katika sentensi kama: (alama 3)
      1. Nomino
      2. Kihusishi
      3. Kiunganishi
    12. Bainisha aina za vishazi tegemezi katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
      Kipakatalishi kilichonunuliwa jana kitatumiwa inavyotakiwa na mwenyewe.
    13. Ichanganue sentensi ifuatayo kwa visanduku: (alama 3)
      Matandiko na Sisomi wataketi karibu na daraja.
    14. Jibu kulingana na maagizo:
      1. Kwetu kumenyesha mvua usiku kutwa na waongozi wakahairisha mikakati ya kuthibiti mmomonyoko wa udongo. (Sahihisha) (alama 2)
      2. Mwanariadha bora alipewa zawadi kisha akaandaliwa karamu katika ikulu. (Andika upya ukigeuza maneno yaliyopigiwa mstari kuwa vitenzi). (alama 2)
    15. Bainisha shamirisho na chagizo katika sentensi ifuatayo:
      Ajuza huyo alijengewa nyumba kwa matofali na mwanawe mara moja. (alama 2)
    16. Tunasema simile tunapoomba kupishwa, taib tunapo………… na ………… tunapotaka kitu kinusurike. (alama 2)
    17. Tunga sentensi moja yenye kirai elezi na kirai kihusishi. (alama 2)
    18. Jamala ni kwa hisani, kaba ni kwa …………………….. na ………………………….. ni kwa mziwanda. (alama 2)
    19. Iainishe sentensi ifuatayo kwa kuzingatia dhamira. (alama 1)
      Meza tembe mbili mara tatu kila siku.
  4. SEHEMU D: ISIMUJAMII (ALAMA 10)
    1. Fafanua dhana ya wingilugha. (alama 1)
    2. Eleza mambo manne yanayosababisha wingilugha. (alama 4)
    3. Fafanua sababu tano za watu kuhamisha na kuchanganya msimbo katika mawasiliano. (alama 5)

MARKING SCHEME

  1. SEHEMU A: UFAHAMU
    1. Eleza mbinu zinazotumiwa na wakoloni kuwafanya wananchi kuidunisha lugha ya Kiswahili (alama 3)
      • Mbinu zinazotumiwa na wakoloni kuwafanya wananchi kudunisha lugha ya Kiswahili.
      • Kuwashawishi wananchi waone kwamba lugha ya Kiswahili ni kwa ajili ya wale wasiokuwa na elimu wala kustaarabika
      • Wanawaletea wananchi magazeti mengi ya Kiingereza
      • Kuwashawishi kuamini kwamba lugha ya kigeni ndiyo inayofaa

    2. Thibitisha kuwepo kwa ukoloni mamboleo katika habari uliyosoma (alama 4)
      • Kuwepo kwa ukoloni mamboleo
      • Utamwona mwananchi halisi akijitwaza kwamba hawezi kujieleza kwa ufasaha mpaka atumie lugha ya Kiingereza
      • Katika maofisi ya serikali utawaona wananchi wengine wanapenda kuzungumza Kiingereza wao kwa wao
      • Utamwona mwananchi anayefahamu Kingereza kidogo akijinunulia gazeti kubwa la Kingereza na kuanza kuzurura nalo kutwa nzima bila kutambua mengi ndani yake
      • Utawasikia wengi wakidai kwamba hawataki kusoma magazeti ya Kiswahili kwa sababu ni vigumu kwao kuelewa

    3. Eleza jinsi wabeberu wanaweza kuzua vurugu katika mataifa mbalimbali (alama 2)
      • Jinsi wabeberu wanaweza kuzua vurugu
      • Taifa la Kibeberu kuandika habari za uchochezi kwenye magazeti yao kwa lugha ya Kiingereza.

    4. Taja sababu ambayo imewafanya wananchi wengi kupuuza lugha ya Kiswahili (alama
      • Sababu ya wananchi kupuuza lugha ya Kiswahili
      • Kutawaliwa kwa miaka mingi na wakoloni

    5. Wakoloni wana mtazamo gani kuhusu lugha ya Kiswahili? (alama 2)
      • Mtazamo wa wakoloni kuhusu lugha ya Kiswahili
      • Ni lugha ya watu wasiokuwa na elimu
      • Watu ambao hawajastaarabika

    6. Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumiwa katika taarifa (alama 3)
      1. Uadilifu - Umuhimu
      2. Akijitwaza - Kuwa na kiburi/akiringa akijitapa
      3. Waliotopea - waliobobea

  2. SEHEMU B. UFUPISHO
    1. Bila kupoteza maana iliyokusudiwa na mwandishi, fupisha aya ya kwanza na ya pili.(Maneno 70) (alama 7,1 ya mtiririko)
      • Mirundiko ya taka na utaratibu usiofaa wa uzoaji wake ni tisho kwa siha ya umma
      • Taka huwa makaazi ya wadudu na wanyama waharibifu.
      • Maji taka pamoja na mifuko ya plastiki huwa makao ya wadudu na virusi vinavyoleta magonjwa.
      • Wakati wa gharika, maji husababisha mafuriko kutokana na njia yake kuzibwa na mifuko hii
      • Njia mojawapo ya kuyatunza mazingira ni kuelimisha na kuhimiza umma kuwa na uangalifu katika matumizi ya bidhaa na kupunguza uzalishaji taka.

    2. Kwa kuzingatia aya ya 3,4,5,6 na 7 eleza mambo muhimu anayoshughulikia mwandishi ( maneno 100– 120) (alama 8,1 ya mtiririko)
      • Watu wengi hawajui kuwa kwa kutumia teknoloia endelezi, taka nyingi zinaweza kugeuzwa na kuwa na manufaa.
      • Mifuko na mabaki ya plastiki hupelekwakatika viwanda vinavyotengeneza bidhaa za plastiki
      • Taka za chupa na chuma nazo huuzwa katika viwanda vinavyozigeuza kuwa na manufaa
      • Taka zinazoweza kuoza zinaweza kutumiwa kutengeneza mbolea kwa kufukia mabaki ya vyakula, mboga na matunda ardhini
      • Njia hii haidhuru mazingira bali hutatua matatizo ya kiafya yanayoweza kutokana na mirundiko ya taka.
      • Pia hurutubisha udongo
      • Maji taka yanaweza kutayarishiwa njia mahsusi ya kuyaelekeza mashambani.
      • Badala ya kupoteza moto bure wakati wa kuchoma taka, taka hizi zinaweza kuchomewa ndani ya birika kubwa au tangi la chuma na moto huo ukatumiwa kuchemshia maji kwa matumizi ya nyumbani.
        SUKISWPP2

      • Ondoa makosa ya sarufi hadi alama 5 (makosa 10 x ½ alama)
      • Ondoa makosa ya hijai hadi alama 3 (makosa 6 x ½ alama)
  3. SEHEMU C:SARUFI NA MATUMIZI YA LUGHA 
    1. Andika neno moja lilo na mpangilio wa sauti zifuatazo: kikwamizo sighuna cha ufizi, irabu ya mbele wastani, nazali ya midomo na irabu ya nyuma wastani. (alama 2)
      • Sema
    2. Eleza miundo ya silabi katika neno: mbilikimo. (alama 2)
      • KKI+KI+KI+KI
    3. Tunga sentensi ya neno moja iliyo na vipashio viifuatavyo vya kisarufi: kiima, kiambishi cha wakati ujao, shamirisho kitondo, mzizi, kauli tendea na kiishio. (alama 3)
      • Atakusomea/watawachezea/utanipikia
    4. Tunga sentensi moja kudhihirisha matumizi mawili ya kiambishi i. (alama 2)
      Sukari iliyonunuliwa haipendezi.
      1. Kiambishi i ni kipatanishi ngeli ya I-I. Damu imemwagika.
      2. Kiambishi i hutumiwa kukanusha wakati uliopo: inapendeza – haipendezi.
      3. Kiambishi I kukanusha hali ya mazoea: Wao huimba – wao hawaimbi.
      4. Kiambishi I ni kipatanishi katika ngeli ya I-ZI umoja: Barabara imeundwa.

    5.  “Akisa! Akisa! Mbona huitiki! Njoo hapa upesi!” mama alimwamrisha. (alama 3)
      Andika kwa usemi wa taarifa:
      • Mama alimwita Akisa mara mbili na akashangaa (akastaajabu) ni kwa nini hakuitika kisha akamwamrisha aende pale (alipokuwa) upesi.

    6. Waumini wa kweli humcha Maulana kila wakati. (alama 1)
      Anza: Maulana…
      • Maulana huchiwa kila wakati na waumini wa kweli.

    7. Kanusha kwa udogo: Ndovu huyu alimdhuru nguruwe huyo mchafu. (alama 2)
      • Kidovu hiki hakikukidhuru kiguruwe hicho kichafu.
        Au
      • Kijidovu hiki hakikukidhuru kijidovu hicho kichafu.

    8. Andika kunyume: Shamsi alilewa kisha akaukomea mlango wake usiku. (alama 1)
      • Shamsi alileuka/alilevuka1/2 kisha akaukomoa1/2 mlango wake usiku.

    9. Tunga sentensi moja yenye kiwakilishi cha A-unganifu, kitenzi kishirikishi kipungufu na kijalizo. (alama 3)
      • Wa jirani ni mwongo
      • Ya kufulia si ghali.
      • La Ujerumani ndilo bora.

    10. Ziunganishe sentensi zifuatazo kwa kiunganishi cha masharti. (alama 2)
      Wakulima watapata mazao mazuri. Wakulima watazingatia kilimo cha kisasa.
      • Wakulima watapata mazao bora ikiwa/iwapo/endapo/kama watazingatia kilimo cha kisasa.
    11. Tumia neno ‘mpaka’ katika sentensi kama: (alama 3)
      1. Nomino -Huu ni mpaka wa Kenya na Uganda.
      2. Kihusishi - Nilimsubiri tangu asubuhi mpaka adhuhuri.
      3. Kiunganishi - Alisoma kwa bidii mpaka akafaulu.

    12. Bainisha aina za vishazi tegemezi katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
      Kipakatalishi kilichonunuliwa jana kitatumiwa inavyotakiwa na mwenyewe.
      • Kishazi tegemezi kirejeshi/kivumishi – kilichonunuliwa jana
      • Kishazi tegemezi kielezi cha namna – inavyotakiwa na mwenyewe

    13. Ichanganue sentensi ifuatayo kwa visanduku: (alama 3)
      Matandiko na Sisomi wataketi karibu na daraja.
          S  
       KN      KT
       N  U N   T   RH  
      H  N
       Matandiko  na  Sisomi  wataketi  karibu na daraja 
    14. Jibu kulingana na maagizo:
      1. Kwetu kumenyesha mvua usiku kutwa na waongozi wakahairisha mikakati ya kuthibiti mmomonyoko wa udongo. (Sahihisha) (alama 2)
        • Mvua imenyesha kwetu(1/2)usiku kucha(1/2) na viongozi wakaahirisha(1/2) mikakati ya kudhibiti(1/2) mmomonyoko wa udongo.

      2. Mwanariadha bora alipewa zawadi kisha akaandaliwa karamu katika ikulu. (Andika upya ukigeuza maneno yaliyopigiwa mstari kuwa vitenzi). (alama 2)
        • Mwanariadha bora alizawidiwa kisha akakirimiwa katika ikulu.

    15. Bainisha shamirisho na chagizo katika sentensi ifuatayo:
      Ajuza huyo alijengewa nyumba kwa matofali na mwanawe mara moja. (alama 2)
      • shamirisho kitondo – ajuza huyo
      • shamirisho kipozi – nyumba
      • shamirisho ala/tumizi – matofali

    16. Tunasema simile tunapoomba kupishwa, taib tunaporidhika/ridhia jambo na hamadi tunapotaka kitu kinusurike. (alama 2)

    17. Tunga sentensi moja yenye kirai elezi na kirai kihusishi. (alama 2)
      • Walikuja jana jioni (RE) baada ya kazi (RH).
      • Walisomea kivulini (RE) chini ya mwembe (RH).

    18. Jamala ni kwa hisani, kaba ni kwa bana/binya/gandamiza/ finya/fyanda na kitindamimba/mzuwanda ni kwa mziwanda. (alama 2)

    19. Iainishe sentensi ifuatayo kwa kuzingatia dhamira. (alama 1)
      Meza tembe mbili mara tatu kila siku.
      • Sentensi agizi

  4. SEHEMU D: ISIMU JAMII
    1. Fafanua dhana ya wingilugha. (alama 1)
      • Hali ya mtu au jamii kuwa na uwezo wa kuwasiliana kwa zaidi ya lugha mbili tofauti.
    2. Eleza mambo manne yanayosababisha wingilugha. (alama 4)
      • Michezo na utalii – watalii na wanamichezo huhamia na kuyazuru mataifa ambako lugha tofauti na zao huzungumzwa na kulazimika kujifundisha lugha hizo ili kufanikisha mawasiliano kati yao na wenyeji wao.
      • Elimu – mataifa huweka sera kuhusu lugha rasmi katika elimu, hali inayowalazimisha wanafunzi kujifundisha lugha zaidi ya mbili.
      • Vita na uhamiaji – hali hii huwashurutisha wakimbizi kujifundisha lugha inayosemwa ukimbizoni ili kufanikisha mawasiliano yao na ya wenyeji.
      • Dini – dini kama Uislamu na Ukatholiki huongozwa na linguafranka za Kiarabu na Kilati mtawalia, hali hii huwashurutisha haswa viongozi wake kujifundisha lugha hizi ili kufanikisha mahubiri na shughuli nyingine za kidini.
      • Shughili za kibiashara – hizi huwafanya watu kujifunza lugha za washitiri wao ili kuweza kuwasiliana nao.
      • Sanaa na burudani – hili huwapata sana wasanii wa muziki na filamu ambao hulazimika kujifundisha lugha fulani za kigeni ili kuweza kuigiza dhima fulani mahususi katika filamu. (4x1)

    3. Fafanua sababu tano za watu kuhamisha na kuchanganya msimbo katika mawasiliano. (alama 5)
      • Haja ya kuleta usiri au ufaraga katika mawasiliano yao.
      • Haja ya kujinasibisha/kujihusisha na kikundi fulani cha watu wanaotumia lugha Fulani.
      • Ukosefu wa tafsiri katika baadhi ya istilahi, misammiati au dhana.
      • Hali ya msemaji kukosa kujua au kusahau neno fulani katika lugha ya mawasiliano.
      • Kasumba kwamba lugha fulani ni duni katika muktadha fulani wa kimawasiliano.
      • Haja ya kujieleza kikamilifu na kueleweka miongoni mwa hadhira inayokwazwa kimawasiliano na lughha Fulani – msemaji aweza kuhamisha ndimi ili kufidia upungufu wa hadhira yake.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Sukellemo Joint Mock 2020/2021.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest