Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Moi Kabarak High School Mock 2020/2021

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote yaandikwe.
  • Majibu yote ni lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  1. UFAHAMU  (Alama 15)
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.
    Kama kawaida walevi wenzao walikuwa wameshatangulia. Ilikuwa marufuku kuuza vileo vyovyote vya kienyeji. Na ikiwa viliruhusiwa kuuzwa, basi ililazimu vitengenezwe viwandani, na viwanda vyenyewe mali ya wageni-unaona? Ama sivyo, basi mzalendo hakuwa na budi ila kunywa pombe ya chang'aa za kigeni- unaelewa? Hii ilitokana na hekima za watawala - na hekima za watawala hazina haya! Mama yangu ndivyo alivyoniambia siku moja alipokuwa amepagawa na pepo wake wa kifalsafa.

    Haya basi, kina yahe kama wao hawakupinga kunywa aina nyingi za pombe hizi ghali za kigeni, kilichowazuia kufanya hivyo hakikuwa kitu kingine bali ubaguzi tu- ambao ulitokana na sheria za kiuchumi. Hii ndiyo sababu iliyowafanya watu kama kina Mzee Matingasi kuwa wagema ili waweze kula vya walevi waliobaguliwa. Mangwe ya Mzee Matingasi kwa hivyo hayakuwa ya halali. Hakuwa na leseni ingawaje walevi hawakuacha kumiminika hapo. Kwa yeyote yule askari mpekuzi mja-wa-njaa , mlungula ulimkomesha. Mzee huyu aliweza kuhepa vikwazo vya sheria kwa ukarimu wake wa kumpa chupa mbili au tatu - au hata pesa taslimu, kwa askari kama huyu. Ni mbinu hii iliyomwezesha kila jioni kuwasha taa yake ya kibatali, kuitundika kiguzoni - kitendo ambacho kilipageuza hapo kwake kitaluni. Hii haikuwa taa ya kuangalia, bali ya kuvutia nondo. Wawili kati ya nondo hawa wakawa Dzombo na rafiki yake Jeuri.

    Walipofika walikuwa wameshatanguliwa na wenzao ambao walikuwa wameshawaka tayari. waliwakuta wamekaa kama mtu na nafasi yake ilivyomtuma. Lakini, kwa ujumla, walionekana wamekaa vikundi vikundi. Kwenye kila kikundi, yaonekana kulikuweko na wale walionong'ona ungedhani walikuwa hata wakiogopa kujisikia wenyewe wakizungumza na wapo wale waliopayuka ili waweze kusikizwa na yeyote mpita njia. Baada ya kuamkuana na walevi wenzao, waliagiza chupa zao nne za pombe ya mnazi na kujipachika gogoni. Huku wakikonga pombe taratibu, walisikia kwa kikundi kimoja mtu akisema kwa sauti ya juu:

    “Mwanamke! Hee, mimi siwezi kumnunulia mwanamke pombe"

    “Kwa nini?” Mwenzake akamuuliza.

    Kabla ya kujibu, kwanza akateuka, na huku akiwatupia macho ya dharau wateja wenzake wa kike, akasema, “Wote ni malaya tu.” Kisha akateuka“geee" huku akiyumbayumba kutoka shingoni.

    “Bila simile, ikasikika sauti ya kike ikimwambia, “Malaya ni mamako”

    “Mimi sijali," akajibu hata bila kuangalia hiyo sauti ilitokea wapi.

    "Mimi si mtoto wa mwanamke...mimi ni mwana wa mwanamume!" Alisema haya kwa madaha na midomo kuipindua juu, huku akiongezea, “Mimi si mtoto haramu nina baba - hachi ya mungu!"

    “Wajuaje?” Mwana-mama akawa bado anaye. Naye kwa sauti ya kutosadiki, akauliza, “Najuaje? Si baba alimwoa mamangu?” Alijichekelea huku akiwaangalia wenzake wa kiume na macho ya dharau yaliyokuwa kama yakiuliza: “Na huyu mwanamke ana kichaa nini?”

    “Basi tu, huko kumwoa?"

    "Aa! Si tena ali...aka...mmgh!" Alikohoa huku akionyesha tabasamu lililomng'arisha macho yake ya uchu. “Ulikuwako?" Huyu mwana-mama akauliza na kila mtu akaangua kicheko. Lakini naye mwana-mama hakutishika kwani aliendelea kumwambia: “Usiruke ama kumtolea macho mtu hapa. Wewe umetutusi kwa sababu unadhani wewe u mtoto wa babako, hu wa haramu. Na ni nani aliyekwambia hivyo? Mamako-ambaye ni mwanamke kama mimi, ama malaya kama ulivyotuita..."

    “ Ndiyo! Kwani utafanya nini?" Akamkatiza kwa ufidhuli huku akili yake sasa ikiwa na nia ya kumzaba makofi. “Sitakufanya kitu,” Mwana-mama akamwambia. Hata hivyo, akaongezea, “Kilicho wazi ni hiki: Kuwa una hakika kuwa mamako ni nani siku zote, lakini sivyo kuhusu baba zetu. Kikubwa ni kuheshimiana na kupendana tukijua kwamba hakuna asiye mzawa wa mwanamke.” Kumaliza kusema haya, mwana-mama alienda haja huku nyuma akiacha kimya kikiwazonga wateja wenzake. Naye yule cholemanga wa haya yote akawa hana lingine ila kukimbilia mboko yake... njia panda akawa amebwagwa na mboko ikawa kipengele cha kujinasulia.

    1. Ni kwa nini mzalendo hakuwa na budi ila kunywa pombe na chang'aa za kigeni?  (alama 2)
    2. Jamii ya msimulizi imezongwa na ukata. Thibitisha kwa mifano miwili. (alama 2)
    3. Huku ukitoa mifano, onyesha jinsi usaliti unavyojitokeza kwenye kisa hiki. (alama 2)
    4. Fafanua maana inayojitokeza kwenye kauli hii.   (alama 2)
      “Hii haikuwa taa ya kuangalia, bali ya kuvutia nondo"
    5. Kwa kutoa mifano mitatu kutoka kwenye kifungu, onyesha jinsi ulevi ulivyochangia unyanyasaji wa kijinsia.
      (alama 3)
    6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumiwa kwenye kifungu.  (alama 2)
      1. wakikonga....
      2. mboko...
  2. MUHTASARI  (Alama 15)
    Ni dhamira ya mwanafunzi yeyote kupata matokeo mazuri katika mtihani wa kitaifa punde tu anapojiunga na shule iwe ni ya sekondari au msingi.

    Matokeo hayo hutokea baada ya miaka minane katika shule za msingi na miaka minne katika shule za sekondari. Hata hivyo, punde tu matokeo yanapotangazwa, wengine hujipata wanyonge kwa kugundua kuwa wamefeli au wameambulia nunge kwa mtihani wao wa mwisho.

    Miongoni mwa mambo yanayosababisha hali kama hii ni mwelekeo mbaya wa wanafunzi katika baadhi ya masomo. Tunajua kweli kuwa palipo na ushindani lazima kuwe na mshindi na mshindwa. Iwapo ungemwuliza mtahiniwa akueleze jinsi anavyohisi baada ya kushindwa kwenye mtihani wa kitaifa, hatakuwa na la ziada ila kukueleza kuwa hajaridhishwa na matokeo. Wengine wao hata huvuka mipaka na kuyataja matokeo yao mabaya kusababishwa na vizingiti fulani au kuwakashifu walimu kwa kudai kuwa kulikuwa na hali ya kuonewa darasani. Unapochunguza zaidi, utakuta ya kuwa wanaodaiwa kuwa werevu ni walio stadi katika masomo ya sayansi yanayofikiriwa kuwa magumu.

    Wakati wanaofikiriwa kuwa werevu wanapofanya vyema katika mitihani yao, wale wanaokisiwa kuwa wajinga ambao wamefeli hujipata wakiomboleza kwa huzuni kwa muda mrefu. Swali la miaka mingi kuhusu elimu limekuwa ni kwa nini wanafunzi wote hawawezi wakafanya vyema na kufaulu katika mitihani ya kitaifa. Utafiti uliofanywa umebainisha wazi kwamba kunazo sababu kadhaa zinazochangia matokeo mabaya.

    Mojawapo ya sababu hizo, na ambayo ni muhimu sana ni ukosefu wa nidhamu shuleni. Mwanafunzi wa aina hii hajali anachoambiwa na walimu na aghalabu muda wake mwingi unapotelea katika adhabu.

    Wakati mwanafunzi anapokosa nidhamu iwe kwa wazazi au walimu wake, masomo yake huathirika. Matokeo yake katika mitihani hayatakuwa mazuri. Ni Lazima tabia ya mwanafunzi iambatane na matokeo yake. Sababu nyingine ni mshtuko unaowapata punde tu wanapoketi kwenye viti vyao kufanya mitihani ya kitaifa. Mtahiniwa anapojikuta katika hali hii, kuna uwezekano asifaulu katika masomo yake.

    Kuna uwezekano wa wanafunzi aliyefeli katika mtihani wa darasa la nane kufanya vyema katika shule ya upili na kupita mtihani wake wa kidato cha nne. Ilibainika pia kuwa wale waliofaulu katika mtihani wa darasa la nane hulegeza juhudi zao masomoni na huwa hawapati alama zinazoambatana na zile walizopata katika shule za msingi.

    Sababu nyingine ya kuwafanya wanafunzi kutofanya vyema katika mtihani ni kubaguliwa kwa wanafunzi hafifu na walimu na kukosa kushughulikiwa ipasavyo. Baadhi ya walimu jua kuwa wanafunzi fulani hawafanyi vyema katika masomo fulani, hawatumii muda wao mwingi kuwasukuma ili kuyaboresha matokeo. Badala yake huwashughulikia wanaoelewa haraka darasani.

    Kuna wanafunzi wengine wanaochukua muda mrefu kuelewa, si ya kwamba ni wajinga, la, ni katika somo moja tu. Ni wajibu wa mwalimu kuhakikisha mwanafunzi kama huyu anapata nafasi ya kuelewa anachofunzwa.

    Wanafunzi wengine hawafanyi vyema kwa sababu wazazi wao hawamudu kuwalipia karo kwa sababu ya umaskini, hawawezi hata kulipia masomo ya ziada kwa shule zinazosomesha wanafunzi wakati wa likizo.

    Kulingana na takwimu za elimu, muda wa kawaida hautoshi kukamilisha mtaala wa masomo ya mfumo wa 8-4-4, kwani ni mpana sana. Walimu wanaombwa kushughulikia mafunzo ya ziada.

    Maswali 
    1. Bila kubadilisha maana, fupisha aya tatu za mwanzo. Maneno (55 – 60) (Al. 7 Utiririko 1)
    2. Fafanua sababu zinazowafanya wanafunzi kutofaulu masomoni. Maneno ( 50-55) (Al. 6 Utiririko 1) 
  3. MATUMIZI YA LUGHA  (Alama 40)
    1. Andika kinyume cha sentensi hii.  (alama 2)
      Mama atazianika nguo jioni baada ya saa chache.
    2. Taja konsonanti ya kipua na midomo. (alama 1)
    3. Eleza maana ya mofimu.  (alama 1)
    4. Fafanua miundo yoyote miwili ya nomino katika ngeli ya U-ZI.  (alama 2)
    5. Taja misingi inayotumiwa katika upangaji wa irabu. (alama 3)
    6. Tumia neno mighairi kutungia sentensi sahihi.  (alama 2)
    7. Fafanua utata uliopo katika sentensi hii.  (alama 2)
      Mwaliko huo ulinishtua
    8. Katika sentensi, kitumie kishazi tegemezi ili kuvumisha nomino.   (alama 2)
    9. Tunga sentensi moja shurutishi. (alama 1)
    10. Kwa kutoa mfano, fafanua dhana ya silabi funge.   (alama 2)  
    11. Eleza matumizi ya viambishi vilivyopigiwa kistari.    (alama 2)
      Aliingia kisiri na kuchukua kijana chake. 
    12. Iandike upya sentensi hii kwa kutumia chagizo ya wakati.  (alama 1)
      Wanafunzi watasoma maktabani.
    13. Andika sentensi hii katika usemi wa taarifa.   (alama 3)
      " Maisha ya sasa ni magumu na sijui wakati kama huu mwaka ujao utakuwaje." Farida akasema.
    14. Tambulisha aina za vitenzi katika sentensi hii.     (alama 3)
      Panya yu mtegoni lakini anajaribu kujinasua.
    15. Itumie nomino ya kawaida na ile ya kitenzi jina katika sentensi moja sahihi. (alama 2)
    16. Ainisha virai    (alama 2)
      Yule mvuvi mwenye masharubu amewasili ufuoni sasa.
    17. landike sentensi hii katika ukubwa.          (alama 3)
      Ngoma ilipatikana karibu na shoka.
    18. Ichanganue sentensi hii kwa kielelezo cha mishale.   (alama 3)
      Lililimwa vizuri sana.
    19. Tambua aina za shamirisho katika sentensi hii.   (alama 3)
      Wafadhili wamewalipia mayatima karo kwa hundi.
  4. ISIMUJAMII   (Alama 10)
    1.  
      1. Eleza maana ya lugha rasmi.     (alama 2)
      2. Zitaje sifa zozote nne za lugha rasmi.     (alama 4)
    2. Fafanua nadharia zozote mbili zinazoeleza kuhusu chimbuko la lugha ya Kiswahili.  (alama 4)


Marking Scheme

 Ufahamu

  1. Watawala wageni waliharamisha utengenezaji wa pombe za kienyeji ila tu zile zilitengenezewa kwenye viwanda vyao (1x2=2)
  2.  
    1. Wazalendo walishindwa kununua pombe za kienyeji
    2. Mangwe ya Mzee Matingasi ilikuwa na taa ya kibatali.
    3. Pale magweni hapakuwa na viti ilibidi Dzombo na Maskini Jeuri waketi kwenye gogo
      (Hoja za kwanza 2x1=2)
  3.  
    1. Watawala kupiga marufuku pombe za kienyeji ilhali wao wanazitengeneza viwandani na kuziuza.
    2. Askari mpekuzi kuhongwa na Mzee Matingasi kwa pombe aliyotakiwa kuzuia uuzaji wake na hata kwa pesa taslimu.
    3. Mlevi mwanamume kumkana mamake anaposema yeye ni mwana wa mwanamume
    4. Mzee Matingasi kuendesha ugema kama njia ya kuwaibia walevi waliobaguliwa na sheria za kiuchumi.
      (Hoja 2x2=4)
  4. Ilikuwa ishara kuwa mangwe ya Mzee Matingasi yalikuwa wazi/ Ili kuwavutia wateja.
    (1x2=2)
  5.  
    1. Mlevi mwanamume kuwarejelea wateja wanawake kama malaya.
    2. Mlevi mwanamume kumkana mwanamke kwa kusema yeye ni mwana wa mwanamume.
    3. Mlevi mwanamume hakutaka mwanamke amjibize. Anasema, “Huyu ana kichaa"
    4. Mlevi mwanamume kumtazama mwanamke kwa macho ya uchu- anamwona kama chombo cha kutimizia ashiki yake ya kimwili.
    5. Mwanamume kumtazama mwanamke kwa macho ya dharau.
      (Hoja za kwanza 3x1=3)
  6.  
    1. wakikonga- wakinywa pombe/wakiondoa kiu yao kwa pombe/wakishiriki ulevi
    2. mboko- kifaa cha kunywea pombe.
      (Hoja 2x1=2)

Muhtasari
Swali la (a)

  • Ni madhumuni ya kila mwanafunzi kupata matokeo mazuri katika mtihani wa kitaifa.
  • Matokeo haya ni baada ya miaka minane katika shule za msingi na miaka mine katika shule za sekondari.
  • Punde matokeo yanapotangazwa, wengine hujikuta wamefeli
  • Yanayosababisha wafeli ni mwelekeo mbaya katika baadhi ya masomo.
  • Ukimuuliza aliyefeli anavyohisi atakueleza hajaridhishwa na matokeo hayo.
  • Atataja matokeo mabaya yamesababishwa na vizingiti fulani au kuwakashifu walimu kwa kuwaonea darasani.
  • Waliofeli huomboleza kwa huzuni muda mrefu.
  • Kwa nini wanafunzi hawawezi kufaulu kwenye mtihani wa kitaifa?
  • Kunazo sababu kadhaa zinazochangia matokeo mabaya
    (Hoja zozote 7x1=7 Ut. alama 1)

Swali la B

  • Ukosefu wa nidhamu shuleni na hivyo kupoteza muda mwingi katika adhabu.
  • Mshtuko unaowapata wanapoketi kufanya mtihani.
  • Kulegeza juhudi masomoni na kupata matokeo yasiyoambatana na ya darasa la nane.
  • Kubaguliwa kwa wanafunzi hafifu na walimu wao.
  • Wengine huchukua muda mrefu kuelewa.
  • Wazazi maskini ambao hawamudu kuwalipia karo na ada ya masomo ya ziada.
    (Hoja 6x1=6 Ut. alama 1)

Matumizi ya lugha

  1. Mama atazianua nguo asubuhi kabla ya saa nyingi. (½x4=2)
  2. /m/ (1x1=1)
  3. Kipashio kidogo cha lugha chenye maana na ambacho hakiwezi kutenganishwa zaidi bila ya kupoteza maana yake. (1x2=2)
  4.  
    1. U-O(ukucha – kucha)
    2. U-nd (udeve- ndevu) 
    3. W-ny-(wayo -nyayo)
    4. U- ny (unywele – nywele)
    5. U- nj (Ujia -njia)
    6. U - mb (ubao -mbao)
      (Mifano yoyote 2x1=2)
  5.  
    1. mahali kwenye ulimi
    2. mwinuko wa ulimi kinywani
    3. mkao wa midomo
      (3x1=3)
  6. Mwanafunzi alienda mjini mighairi ya ruhusa ya mwalimu. (sentensi ilete dhana ya bila ya/pasi na)
    (1x2=2)
  7.  
    1. Sauti iliyotokeza ilinipa wasiwasi.
    2. Mwito wa kunikaribisha mahali ulinishtua (Hoja 2x1=2)
  8. Kiti kilichovunjika tendeguu kitarekebishwa/ Kiti ambacho kilivunjika tendeguu kitarekebishwa. (Hoja 1x2=2)
  9. Ondoka haraka!/ Simameni mara moja! (1x1=1)
  10. Huwa ni silabi inayokamilika kwa konsonanti. Kab-la, Min-ta-ra-fu
    (kutoa maana alama 1, mfano alama 1)
  11. Kisiri - kielezi cha namna mfanano. Kijana- kuonyesha udogo (Hoja 2x1=2)
  12. Wanafunzi watasoma jioni/asubuhi/kesho. (1x1=1)
  13. Farida alisema kuwa maisha ya wakati huo yalikuwa magumu na hakujua wakati kama huo mwaka ambao ungefuata ungekuwaje. (vitahiniwa 6x½=3)
  14. yu- kishirikishi kipungufu
    anajaribu- kitenzi kisaidizi
    kujinasua- kitenzi kikuu (3x1=3)
  15. Kufaulu kwa wanafunzi kuliwaletea sifa nyingi. (2x1=2) (Tathmini majibu ya watahiniwa)
  16. yule mvuvi mwenye masharubu- kirai nomino
    mwenye masharubu- kirai kivumishi
    amewasili ufuoni sasa- kirai kitenzi
    ufuoni sasa- kirai kielezi (Aina zozote 2x1=2)
  17. Goma/jigoma lilipatikana karibu na jishoka. (vitahiniwa 3x1=3)
  18. S-KN + KT (1)
    KN-O (½)
    KT-T+KE (½)
    T- Lililimwa (½)
    KE-E + E (½)
    E- vizuri
    E- sana
  19. karo - kipozi
    mayatima - kitondo
    hundi- ala (Vitahiniwa 3x1=3)

Isimujamii

  1.  
    1. lugha rasmi- hii ni lugha inayotumiwa katika shughuli za mawasiliano yaliyo rasmi kama vile ofisini, katika shughuli za kiutawala, kisheria, kitaaluma n.k. (1x2=2)
    2. sifa za lugha rasmi
      • Huwa ni lugha sanifu
      • Ni lugha inayozingatia tasfida
      • Huwa ni lugha isiyo utani (urasmi hutawala)
      • Huvuka mipaka ya kitaifa katika matumizi yake
      • Msamiati wake hutegemea mazingira ya matumizi mfano katika sayansi, ofisini n.k.
      • Huwa na matumizi mengi ya lugha ya heshima.
        (hoja zozote 4x1=4)
  2.  
    1. Kiswahili ni lugha ya Kiarabu- wageni wa mwanzo wa pwani ya Afrika Mashariki walikuwa ni waarabu ambao waliwaoa wanawake wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki. Wazawa wa ndoa hii walizungumza lugha iliyokuwa na msamiati wa kiarabu na hivyo baadhi ya wachunguzi wa lugha wakahusisha asili ya Kiswahili na Uarabuni.
    2. Kiswahili ni lugha mseto- Kutokana na maingiliano ya wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki waliozungumza Kiswahili na wageni kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni, lugha ya wenyeji iliweza kukopa msamiati wa wageni hao mbalimbali na hivyo baadhi ya wachunguzi wa lugha wakadai kuwa Kiswahili ni lugha mseto. 
    3. Kiswahili ni lugha ya kibantu- Hii ndiyo nadharia inayoelekea kuwa ya ukweli. Hii ni kwa sababu uchunguzi wa kiisimu uliofanywa na baadhi ya wanisimu umethibitisha kuwa upo mshabaha mkubwa baina ya majina ya lugha ya Kiswahili na yale ya lugha nyingi za kibantu. Aidha utaratibu wa kupanga nomino katika makundi ya ngeli zake hufafana na ule unaotumiwa na lugha nyingi za kibantu.
      (Hoja zozote 2x2=4)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Moi Kabarak High School Mock 2020/2021.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest