Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Bungoma Diocese Mock Exams 2021/2022

Share via Whatsapp

INSTRUCTIONS TO CANDIDATES

 • Swali la kwanza ni la Lazima.
 • Maswali haya mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu zilizobaki.
 • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.

SEHEMU YA A

FASIHI SIMULIZI

 1. Lazima
  Tumia kifungu kifuatacho kujibu maswali yanayofuata
  1. Nyumbani mwetu mna papai lilioiva lakini siwezi kulichuma – ndugu wa kiume asimuoe nduguye wa kike.
   1. Bainisha kipera kinachorejelewa (Al 1).
   2. Andika shughuli moja ya Kijamii na moja ya Kiuchumi ambazo huendelezwa katika jamii ya utingo huu. (Al 2)
   3. Eleza dhima nne za kipera kinachorejelewa katika jamii yako. (Al 4)
   4. Wewe ni mwasilishaji wa kipera hiki jukwani. Eleza mambo matano ambayo utazingatia katika uwasilishaji wako. (Al 5)
  2. Fafanua majukumu yoyote manne ya nyimbo katika jamii. (Al 8)

SEHEMU B

TAMTHILIA

 1. Tathmini maudhui ya ndoa kwa mujibu wa tamthilia ya kigogo. (Al 20)
 2. “Asante ya punda kweli ni mateke, sikujua ungekuja kunihangaisha hivi”.
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Al 4)
  2. Kauli hii ina maana gani kwa mujibu wa muktadha huu (Al 2)
  3. Onyesha jinsi anayeambiwa maneno haya anavyoangaisha mzungumzaji. (Al 4)
  4. Jadili jinsi hali ya “Asante ya punda ni mateke” inawaafiki wanasagamoyo.(Al 8)

SEHEMU C

RIWAYA

 1. Eleza ufaafu wa anwani ya chozi la heri (Al 20)
 2. “uuuui! Uuuui! Jamani tusaidieni! Uuuui! Uuuui! Mzee kedi usituue, sisi tu majirani! Maskini wangu!”
  1. Elezea muktadha w dondoo hili.(Al 4)
  2. Fafanua tamathali ya usemi huu(Al 2)
  3. taja mambo yaliyofanyikia Ridhaa awali ya kuashiria mikasa. (Al 4)
  4. Kwa kurejelea riwaya ya chozi la heri jadili dhiki za wakimbizi.(Al 10)

SEHEMU D

HADITHI FUPI - TUMBO LISILOSHIBA

 1.  
  1. elezea misiba inayoikumba jamii ya, “shogake dada ana ndevu” ni ya kujitakia. Thibitisha (Al 10)
  2. Jadili madhila ya raia wanaoishi katika mitaa ya mabanda urirejelea hadithi ya ndoto ya mashaka. (Al 10)
 2. “Maswali ya sampuli hiyo yanafaa kuulizwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili (Al 4)
  2. Fafanua sifa tatu za msemaji wa dondoo hili (Al 6)
  3. Tadhmini namna maudhui ya utabaka yanavyojitokeza katika hadithi ambamo dondoo hili limetolewa (Al 10)

SEHEMU YA E

USHAIRI

 1. Soma shairi kisha ujibu maswali

  Ndugu ona mbwa yule, ambaye ananyekenya;
  Yaone mabuu yale, ambayo yamchezeya;
  Kuwa leo yuafile, mwili yanautaniya;
  Jana awile jasiri!

  Juzi shujaa awile, pasiwe kumfikiya;
  Kwenye makani yale, alipojisururiya;
  Leo kuwa yuafile, mainzi yamchekeya;
  Jana awile Jasiri!

  Mijino mikubwa ile, ambayo ‘mejitokeya;
  Yali kiwaliza wale, karibu walosogeya;
  Tena akibweka yule, waoga walijinyiga;
  Jana awile jasiri!

  Kamwe kuishi milele, kupe ukajinyonyeya;
  Walo chini yako wale, muhali unawaziya;
  Ameshindwa yule pale,sembuse wewe sikiya;
  Jana awile jasiri!

  Kama walo hai wale, yafaa kuzindukiya;
  Ni dunia maji male, muhimu kujiwaziya;
  Wazipunguze kelele, na kwingi kujishauya;
  Jana awile jasiri!
  1. Fafanua ujumbe wa shairi hili (Al 2)
  2. Eleza muundo wa shairi hili (Al 5)
  3. Eleza toni ya shairi hili (Al 2)
  4. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia (Al 3)
   1. Ruwaza ya mistari
   2. Ruwaza ya vipande
   3. Ruwaza ya mizani
  5. Eleza mbinu nne ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi (Al 4)
  6. Bainisha sifa mbili za anayezungumziwa katika shairi hili (Al 2)
  7. Eleza tamathali mbili za usemi zilizotumiwa katika shairi hili (Al 2)

   Au

 2. Soma shairi kisha ujibu maswali
  Nizike Ningali Hai!:
  Hassam Muchai

  Kipusa Binti Hamadi, siku n’takuwa kimba
  Nizikwe Kifudifudi, na yoyo kuyumbayumba
  Takuwa bure biladi, matozi ungayasomba
  Nizike ningali hai, n’kifa hutonizika

  Tena ningaumwa ungo, na mapumu kuugua
  Lioze ini na nyongo, na pua zisipumua
  Takuwa sina kinyongo, mradi nimeshatua
  Nizike ningali hai, n’kifa hutonizika

  Nizike sasa mwenzangu, nizike ningali hai
  Singojee kufa kwangu, uanze kurairai
  Kulilia kifo change, ni bure hakukufai
  Nizike ningali hai, n’kifa hutonizika

  Nikifa hutonizika, kimwana sanda nunua
  Manukato ya kupaka, na nguo za kuanua
  Nivishe sione shaka, Washindwe kupambanua
  Nizike ningali hai, n’kifa hutonizika

  Tena nikande misuli, nikande pande kwa pande
  Siate kiwiliwili, shingo, miguu ikande
  Umalizapo kiwiliwili, mwenzangu niende shonde
  Nizike ningali hai, n’kifa hutonizika
  1. Dhamira ya matunzi wa shairi hili ni gani? (Al 2)
  2. Bainisha nafsineni katika shairi hili (Al 2)
  3. Eleza toni ya shairi hili (Al 2)
  4. Changanua muundo wa shairi hili (Al 5)
  5. Fafanua maana ya kibwagizo cha shairi hili (Al 2)
  6. Eleza mbinu nne ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi (Al 4)
  7. Bainisha bahari ya shairi hili (Al 3)


MARKING SCHEME

 1.  
  1. Nyumbani mwetu mna papai lilioiva lakini siwezi kulichuma – ndugu wa kiume asimuoe nduguye wa kike.
   1. Bainisha kipera kinachorejelewa
    • Kitendawili
   2. Andika shughuli moja ya Kijamii na moja ya Kiuchumi ambazo huendelezwa katika jamii ya utingo huu
    • Kijamii – ndoa (kulichuma/ ndugu wa kiume asimuoe nguye wa kike).
    • Kiuchumi – kilimo – paipai lilioiva
   3. Eleza dhima nne za kipera kinachorejelewa katika jamii yako
    Umuhimu
    • Kuburudisha jioni baada ya kazi
    • Kukuza ubunifu wa kuvitunga kwa kulinganisha vitu katika mazingira ili kuviunda.
    • Kuimarisha uwezo wa kukumbuka.
    • Kukuza uwezo wa kufikiri kwani mfumbiwa huhitaji kufikiri sana ili kupata jibu.
    • Kuleta umoja na ushirikiano katika jamii kwa kuleta watu pamoja wakati vinategwa.
    • Kuimarisha ujuzi wa kujieleza kwa lugha.
    • Kupanua ujuzi wa mazingira wa mtoto.
    • Kuendeleza utamaduni wa jamii kama Nyumbani mwetu mna papai lilioiva lakini siwezi kulichuma – Ndugu wa Kiume asimuoe nduguye wa kike.
    • Kukejeli au kudharau tabia mbaya kama wazungu wawili wanachungulia dirishani – Makamasi
   4. Wewe ni mwasilishaji wa kipera hiki jukwani. Eleza mambo ambayo utazingatia katika uwasilishaji wako
    1. Kutumia fomyula/muundo maalum. Mifano
     Mtegaji : Kitendawili
     Mteguaji : Tega
    2. Kutumia ukakamavu wa kuweza kuzungumza hadharani.
    3. Kuwa na uelewa wa mazingira na masuala ibuka katika jamii ili kuweza kuwasilisha dhana zisizopatikana katika mazingira yake.
    4. Ufahamu mpana wa lugha ili aweze kuitumia kwa uhodari na kuwasilisha kwa wepesi.
    5. Kuwa mchangamfu na mcheshi ili kunasa makini ya hadhira na kuzuia isikinai.
    6. Ufahamu mpana wa utamaduni husika ili kuzuia kutumia maneno na ishara zinazoweza kuwaudhi au kupingana na Imani za hadhira.
    7. Kushirikisha hadhira kama vile kuimba, maswali ya balagha ili isikinai.
    8. Kudramatisha ili kuonyesha picha Fulani kama vile kuiga toni, sauti, na kiimbo kulingana na swala analowasilisha.
    9. Kutumia ishara za uso, mwili na miondoko kulingana na hali anayoigiza.
    10. Ufasaha wa lugha ili kuwasilisha mawazo kwa njia mwafaka na inayovutia.
    11. Kubadilisha toni na kiimbo kulingana na hali tofauti unazoigiza kama huzuni.
    12. Ufaraguzi/kubadilisha uwasilishaji papo hapo kutegemea hadhira na kutoa mifano inayofahamika kutoka katika mazingira ya hadhira.
  2. Fafanua majukumu yoyote manne ya nyimbo katika jamii. (Al 8)
   1. ni hifadhi za matukio muhimu ya kihistoria katika jamii
   2. hutumiwa kama nyenzo ya kupitisha utamaduni
   3. hutumiwa kama burudani
   4. huakisi umbuji wa tamaduni mbalimbali
   5. huhamasisha watu kutenda mambo mbalimbali
   6. huelimisha na kupitisha maarifa mbalimbali miongoni mwa wanajamii
   7. ni kiakisi cha fahari walio nayo wanaohusika katika utamaduni wao. Aina na maana za nyimbo
 2. Tathmini maudhui ya ndoa kwa mujibu wa tamthilia ya “Kigogo”
  1. Wanandoa wanasaidiana katika kuzikimu familia zao kwa kufanya kazi wote – kwa mfano, sudi na mkewe Ashua wafanya biashara katika soko la Chapakazi ili kujikimu kimaisha.
  2. Baadhi ya wanandoa wanapendana – Kwa mfano, Ashua anapompelekea mumewe sudi chai na mahamri sokoni, Sudi anasimama na kumkumbatia. Aidha sudi anamwita mkewe Ashua honey na sweetie, akiwa kwenye chumba cha wafungwa.
  3. Baadhi ya wanandoa si waaminifu – Kwa mfano, Asiya/mamapima anazini na Ngurumo ilhali ana mumewe, Boza. Isitoshe, hata Ngurumo ana mkewe. Hata Majoka anamwendea kinyume mkewe Husda kwa kutaka kuzini na Ashua.
  4. Baadhi ya ndoa hazina mapenzi ya kweli – kwa mfano, majoka anapozirai anazungumza na mkewe Husda na kumwambia kuwa hampendi kamwe na kumwambia kwamba ampendaye ni Ashua; mkewe sudi. Aidha Majoka anadai kwamba hata mkewe Husda hampendi/anachopenda ni mali zake.
  5. Ndoa inakabiliwa na tatizo la unafiki – Majoka anabainisha kwa husda anajifanya kuwa anampenda (Majoka) bali anachokipenda ni mali zake.
  6. Ndoa imekumbwa na tatizo la ujane – Bi. Hashima anabaki mjane baada ya kufiwa mumewe.
  7. Baadhi ya wanandoa wana tamaa ya mapenzi nje ya ndoa – Majoka anatamani Ashua, mkewe sudi, ilhali ana mkewe. Isitoshe, naye Husda anatamani Chopi kwa kumtazama kwa macho ya uchu ilhali ana mumewe, Majoka.
  8. Uchochezi ni chanzo ya kuvunjika kwa ndoa -. Ashua anamwomba mumewe, sudi talaka baada ya Majoka kumchochea dhidi yake, hali inayotishia kuvunjika kwa ndoa yao.
  9. Baadhi ya wanamume wanawadhulumu wake wao – kwa mfano, Husda anapozua rabsha ofisini baada ya kumkuta majoka na Ashua, Majoka anamwambia kuwa angeleta fujo angemchafua.
  10. Mwanaume ambaye ameoa na anatembea na mwanamke ambaye hajaolewa ni tishio la kuvunjika kwa ndoa, kwa mfano, Ashua anamtaka mumewe sudi kumpa talaka kwa sababu ya kutembea na Tunu mara kwa mara ilhali Tunu hajaolewa; hivyo kumshuku kuwa mpenziwe.
  11. Baadhi ya wanawake wanawataabisha wanaume kwa kutoridhika na wanachopewa na wanaume wao. Kwa mfano, Sudi anampa mkewe Ashua kila anachokiambua lakini Ashua haridhiki. Anataka Zaidi ya uwezo wa sudi hali ambayo imeleta mgogoro baina yao.
  12. Wanawake ni wasaliti katika ndoa – Ashua anamsaliti mumewe sudi kwa kumwambia kwamba amechoka kupendwa kimaskini ilhali anajua kwamba kipato cha sudi si kikubwa kwa sababu anafanya kazi duni ya kuchonga vinyago sokoni Chapakazi.
  13. Wanaume wanatoa ahadi za uwongo kwa wanawake wakati wa kuchumbiana – Kwa mfano, Sudi alimuahidi Ashua mengi kabla ya kumwoa lakini hakuyatimiza hali inayomchochea Ashua kutaka kuivunja ndoa yake.
  14. Baadhi ya wanandoa ni waaminifu – Kwa mfano, Ashua anakataa kufanya mapenzi na Majoka kwa kumwambia kuwa yeye ni mke wa mtu (sudi)
  15. Jukumu la mwanamke limedhiririka katika ndoa – kupika – Majoka amantaka mkewe Husda ampikie chapatti kwa kuku. Aidha, Ashua ampikia sudi chai na mahamri na kumpelekea kwenye karakana anakochongea vinyago.
  16. Wazazi wawatafutia wanao wa kiume mke wa kuoa – Kwa mfano, Majoka anamrai Tunu kukubali kuozwa kwa Ngao Junior, mwanawe Majoka lakini Tunu anakataa.
  17. Wanawake wanaochelewa kuolewa wanakejeliwa na wanajamii wenzao – Kwa mfano, walevi kule Mangweni wanamwimbia Tunu wimbo wa kumkejeli kwa kuchelewa kuolewa ilhali ana elimu ya kutosha.
  18. Jukumu la mwanamume katika ndoa ni kuikimu familia – Boza anamsuta Sudi kuwa jukumu la mwanamume si kukimbizana na waandamanaji bila kuikimu familia.
  19. Kuna ndoa za Lazima – Majoka akiwa amezirai anatetea jinsi alivyolazimishwa kumwoa Husda hali iliyomsababishia kulia usiku nzima. (UK. 75)
  20. Umaskini ni chanzo cha kuvunjika kwa ndoa. Kwa mfano , Ashua anamwitisha mumewe sudi talaka akidai kwamba amechokwa kupendwa kimaskini.
  21. Mapenzi ni wenzo muhimu katika kumchagua mwenzi wa ndoa. Kwa, mfano Majoka anapotaka Tunu aolewe na mwanawe Ngao Junior, Tunu anamwuliza iwapo anaona kuwa hawezi kusubiri akaolewa na mwanamume ampendaye.
  22. Ndoa imesawiriwa kama jambo, la Lazima kwa yeyote anayetaka kuwa kiongozi. Tunaambiwa kwamba Majoka alilazimishwa kumwoa Husda ili kutimiza wajibu wake katika jamii kama kiongozi
 3. “Asante ya punda kweli ni mateke, sikujua ungekuja kunihangaisha hivi…”
  1. Eleza muktadha dondoo hili
   1. Haya ni maneno ya majoka.
   2. Anamwambia Tunu
   3. Wamo ofisini mwa majoka
   4. Majoka anajuta kwa kugharamia masomo ya Tunua ambaye amekuja sasa kumhangaisha kwa kupinga utawala wake dhalimu
  2. Kauli hii ina maana gani kwa mujibu wa muktadha huu?
   • Majoka anajuta kwa kugharamia masomo ya Tunu ambaye sasa amekuja kumhangaisha kwa kupinga utawala wake.
  3. Onyesha jinsi anayeambiwa maneno haya anavyomhangaisha mzungumzaji
   1. Baada ya Majoka kufunga soko la chapakazi , Tunu anaongoza maandamano ya kupinga
   2. Baada ya Majoka kumuua jabali, kiongozi wa upinzani kwa ajali, Tunu anaaanza kupanga mikakati ya kuwaleta wachunguzi wa nje ili kuitathmini ajali hiyo upya, jambo linalomtia Majoka wasiwasi.
   3. Tunu anawaongoza raia kususia sherehe za kuadhimisha uhuru wa sagamoyo ambazo zingeongozwa na Majoka – Majoka anaishia kuaibika anapofika katika uwanja wa ikulu akiwa na wageni wake na kupata kwamba ni raia kumi tu waliokuwa wamekuja kuhudhuria sherehe hiyo.
   4. Baada ya kuwaongoza raia kususia sherehe za uhuru ambazo zingeongozwa na Majoka, Tunu anawahutubia raia na kuwachochea dhidi ya uongozi wa Majoka. Anawahimiza kumchagua kiongozi anayefahamu fika kadhia zao; njaa na kilio chao.
   5. Baada ya Majoka kubomoa vioski vilivyoko kwenye soko la chapakazi, Tunu anamwendea hadi ofisini mwake na kumhakikishia kwamba hatajenga hoteli yake mahali hapo.
   6. Baada ya Majoka kufunga soko na kufuja pesa za kusafisha soko hilo, Tunu anawahutubia waandishi wa habari na kumkashifu kwa matendo hayo.
   7. Asilimia sitini ya raia inataka kumpigia kura Tunu kutokana na juhudi zake za kuwatetea, jambo linalomtia Majoka tumbojoto.
  4. Jadili jinsi ambavyo hali ya “asante ya punda ni mateke” inawaafiki wasagamoyo
   1. Majoka anagharimia msomo ya Tunu ilhali Tunu anakuja kumhangaisha kwa kuupinga uongozi wake kwa sababu ya kuwadhulumu raia, kwa mfano, kufunga soko.
   2. Mumewe hashima anamfanyia Majoka kazi katika kampuni yake lakini anapokufa Majoka anataka kumnyima mkewe; Bi. Hashima fidia kwamba hawakuwa na bima.
   3. Kombe ni mfuasi sugu wa mrengo wa Majoka lakini serikali ya Majoka inasambaza vikaratasi ikiwataka watu kutoka katika kabila lake kuhama sagamoyo kwa madai kwamba si kwao.
   4. Chochote anachoambua sudi katika kazi yake huwa anamleta mkewe Ashua lakini Ashua haridhiki kwa sababu ya kutaka kuishi yasiyo yake. Anateta kuwa sudi hampi hata masurufu.
   5. Majoka anampa kenga kazi kw kumchagua kuwa mshauri wake mkuu lakini raia wanapoandamana kupinga kufungwa kwa soko, anaungana nao kumg’oa uongozini.
   6. Chopi anamtii Majoka kwa kufanya kila analomuagiza lakini anataka kumuua kwa kosa moja pekee – kutohakikisha kuwa Tunu amepigwa na kuuliwa jinsi alivyokuwa amemuagiza.
   7. Kuna vijana watano wanaomfanyia Majoka kazi katika Majoka and Majoka company lakini wanauliwa wanapoandamana kupinga kuongezwa kwa bei ya chakula kwenye kioski cha kampuni.
   8. Tunu anajitolea kuwatetea raia dhidi ya dhuluma za Majoka lakini raia wenzake kama Ngurumo wanakubali kutumiwa na Majoka kumvamia na kumuumiza – anaumizwa mfupa wa muundi.
   9. Walimu na wauguzi wanalitumikia jimbo la sagamoyo lakini serikali inawalipa mshahara duni, hali inayowasabibishia kugoma na kuandamana.
   10. Raia wanaimba nyimbo za kusifu utawala na babuye Majoka (Ngao) lakini Majoka anawadhulumu kwa kulifunga soko wanaolitegemea badala ya kuboresha maisha yao kwa maaana wanausifu uongozi wa familia yao.
   11. Sudi anadhihirisha mapenzi kwa mkewe, Ashua kwa kumwita baby, honey nan a sweetie lakini Ashua anataka talaka, hali inayotishia kuvunja ndoa yao.
   12. Boza na kombe wanakubali kumchongea Majoka kinvago cha babuye Ngao lakini Majoka analifunga sokoambapo wanachongea na kuuzia vinyago vyao, hivyo kuathiri biashara zao.
   13. Wafanyibiashara kama Ashua wanatii agizo la serikali la kutoa kodi lakini Majoka hawasafishii soko, hivyo kuishia kufanya biashara zao katika mazingira machafu licha ya kulipa kodi.
   14. Ngurumo ni mfuasi sugu wa Majoka lakini Ngurumo anapokufa Majoka hahudhurii maziko yake. Anatoa Maagizo kwamba azikwe juu ya wafu wengine kwa sababu maziara yalikuwa yamejaa.
   15. Sudi anawafungulia Boza na Kombe kiredio chake kwenye rununu yake wasikilize hukuwakichonga vinyago lakini sudi anapokizima, Boza anaanza kumtusi kwa kumwambia kwamba kirununu chake cha pesa nane kimsimtie kiburi.
   16. Wananchi wanawapeleka wanao katika shue ya Majoka and Majoka Academy , hivyo kumtajirisha Majoka kutokana na karo wanayolipa lakini wanafunzi hao wanaruhusiwa kutumia dawa za kulevya badala ya kusoma, hivyo kuishia kuanguka mtihani.
   17. Raia wanamchagua Majoka kuwa kiongozi wao lakini anawadhulumu kwa kuwaua baadhi yao na kulifungua soko wanalolitegemea.
   18. Boza anamruhusu Ngurumo kupika pombe haramu na mkewe, Mamapima lakini Ngurumo anamsaliti Boza kwa kuzini na mamapima.
 4. Eleza ufaafu wa anwani ya chozi la heri
  Chozi ni majimaji yanayotoka kwenye jicho la mtu kutokana na maumivu au furaha. Heri ni hali ya kuwa salama au nafuu au afadhali. Kwa hivyo, chozi la heri ni chozi la nafuu. Maana ya kijanda/kiistari ni maisha ya mhusika kubadilika kutoka hali mbaya hadi hali nzuri. Kwa mfano:
  1. Familia ya akina Ridhaa inateseka kutokana na udogo wa ardhi lakini hali inakuwa nzuri babake, mwimo msubili anapowahamishia katika eneo la msitu wa heri.
  2. Ridhaa anadhulumiwa shuleni na wanafunzi wenzake kwa kudhihakiwa na kusimangwa lakini mamake anapoenda huko na kusema na mwalimu hali hiyo inasitishwa
  3. Ridhaa anamsaidia Mzee kedi Kwa kuyadhamini masomo ya wapwaze wawili.
  4. Eneo la msitu wa heri lilikuwa kame lakini Ridhaa anawasaidia wenyeji wa eneo hilo kupata maji ya mabomba
  5. Mwekevu anapojitosa siasani anatusiwa na kutishwa na wanaume lakiniyupo raia mmoja anayejitokeza kumtetea akidai kwamba ni muhimu apewe nafasi.
  6. Licha ya mwekevu kukumbana na vizingiti kadhaa kama ile kutusiwa anapojitosa siasani anafanikiwa kuchaguliwa kama kiongozi wa taifa la wahafidhina
  7. Familia ya kaizari inapovamiwa na wahuni, jiraniye Tulia anajitokeza na kumsaidia kufunganya virago na kutorokea palipo salama.
  8. Kaizari anapovamiwa na mkewe Subira kukatwa kwa sime na wanawe, Lime na Mwanaheri kubakwa na kuamua kutoroka, jiraniye Tulia anajitolea kumlindia boma lake
  9. Familia ya kaizari inapovamiwa na kuamua kutoroka anafanikiwa kupata matwana inayomsaidia yeye pamoja na familia yake kutorokea mahali salama.
  10. Wakimbizi wanapoteseka kambini kutokana na ukosefu wa chakula, misikiti na makanisa yanayaweletea chakula
  11. Wakimbizi wanapoteseka kulala vibandani, shirika la makazi bora linajitolea kuwajengea makao bora
  12. Selume anapotaabika baada ya kutalikiwa na mumewe Mwanzi, anakutana na Ridhaa anayemsaidia kupata kazi ya uuguzi, hivyo kuweza kujikimu kimaisha
  13. Kuchomwa kwa familia ya Ridhaa kunamsababaisha kuugua shinikizo la damu lakini anasaidiwa kuudhibiti ugonjwa huu kutokana na huduma za ushauri na uekelezaji kutoka kwa wataalamu
  14. Lime na mwanaheri wanabakwa na wahuni na kukatwa lakini wanatibiwa na wauguzi waliotumwa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
  15. Subira anvamiwa na wahuni na kukatwa lakini anatibiwa na wauguzi waliotumwa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
  16. Ridhaa ana furaha kuktana na mwanawe Mwangeka aliyekuwa nje ya nchi, vita vya baada ya uchaguzi vilipozuka na kuwasababisha wanawe wengine pamoja na mkewe Terry kuangamia
  17. Usalama unazorota katika nchi ya wahafidhina , hivyo kuwasababisha kutaabika lakini jamii ya kimataifa inawasaidia kuwarejeshea amani
  18. Raia mmoja anakanyagwa na kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi lakini Ridhaa anamsaidia kwa kumfanyia upasuaji wa uti wa mgongo
  19. Kiriri anamsaidia kangata kuyadhamini masomo ya mabintiyee wawili
  20. Jamaa za Lucia zinakataa Lucia aziolewe kwenye ukoo wa waombwe lakini hali inakuwa njema kwake baabake Kangata anapopinga wazo hilo na kumkubalia kuolewa huko
  21. Kitoto kinatupwa na mamake kwenye biwi la taka lakini kinaokolewa na Neema na kupelekwa katika kituo cha benefactor
  22. Umu amekuwa akilia Kwa sababu ya kukosa wazazi wa kuishi nao nyumbani Kama wanafunzi wenzake shuleni Tangamano lakini hali inabadilika Apondi na Mwangeka wanapomchukua kama mwanao wa kupanga na kumlea Kwa upendo mpaka banguzi alilokuwa nalo moyoni likapona.
  23. Chandachema anataabika kwa kukosa mlezi lakini Tenge na Kimai wamechukua na kumlea pamoja na wanao
  24. Mwaliko anatekwa nyara nyumbani kwa Bi. Kangara lakini anaokolewa na polisi na kupelekwa katika kituo cha watoto cha Benefactor
  25. Mwangeka anafiwa mkewe Lily lakini hatimaye anaoa Apondi aliyemwondolea upweke.
 5. “uuuui! Uuuui! Jamani tusaidieni! Uuuui! Uuuui! Mzee kedi usituue, sisi tu majirani! Maskini wangu!”
  1. Elezea muktadha w dondoo hili.(Al 4)
   • Ni kumbukumbu ya Ridhaa akikumbuka kilio cha mkewe terry Ridhaa akiwa nje ya jumba lake liliochomeka, na hiki ni kilio cha mkewe wakati walipoangamia kwa mkasa wa moto huo.
  2. Fafanua tamathali ya usemi huu(Al 2)
   • tanakali ya sauti – uuuuwi! Uuuuwi!
  3. taja mambo yaliyofanyikia Ridhaa awali ya kuashiria mikasa.(Al 4)
   • Kupepesa kwa jicho lake la kulia kwa wiki mbili mtawalia
   • kuanguka sebuleni mwake bila kutu cha kumfanya ajikwae
   • mwili wake kuwa na mavune/uchovu ilhali hakuwa ameufanyia kazi ya kudhili
   • jeshi la kunguru lililotua juu ya paa la maktaba yake ya nyumbani
   • milio ya kereng’ende na bundi usiku kucha
  4. Kwa kurejelea riwaya ya chozi la heri jadili dhiki za wakimbizi
   • Wanaoishi mabandani – kama kaizari na familia yake
   • Uhaba wa chakula – kaizari anang’ang’ania uji na aliyekuwa waziri wa fedha/Ridhaa anakula mizizi mwitu
   • Wananyeshewa – lime na mwanaheri/hawana hata tambara la kujifunika
   • Kutoroka bila kujua waendako – kaizari na familia yake akiwa kwenye steji
   • dhiki za kisaikolojia – wakimbizi kama kaizari wanashuhudia uchomaji wa mabasi abiria wakiwa ndani yake walipokuwa wanatorokea maneno yenye amani na Usalama
   • magari wanayosafiria yanaishiwa mafuta – kwa mfano, kaizari na familia yake inawabidi kuingia msituni
   • kulala msituni tena njaa – kwa mfano, familia ya kaizari katika siku ya kwanza msituni
   • kukosa maji safi ya kunywa – akina kaizari wanakosa maji safi ya kunywa na wanaothubutu kunywa maji machafu ya mto wa mamba wanaugua homa ya matumbo na kuishi kufariki dunia
   • ukosefu wa misala – wanatumia vyoo vya kupeperusha, hivyo kusababisha kuzuka kwa kipindupindu
   • magonjwa – homa ya matumbo kutokana na matumizi ya vyoo vya kupeperusha
   • vifo vya watoto vinavyotokana na ukosefu wa chakula na magonjwa/watu wengine wanakufa kutokana na kunywa maji machafu ya mto wa mamba n.k
   • kuchomwa kwa familia – kedi ameiteketeza familia ya Ridhaa kwa sababu Ridhaa hakuwa mwenyeji wa msitu wa heri – uk.5
   • Ridhaa anachomewa mihindi yake kwa sababu hakuwa mwenyeji wa msitu wa heri – uk.4
   • Kuonwa kama wavuruga watulivu – Ridhaa anapohamia msitu wa heri pamoja na nduguze, watoto wa huko wanawaona kama waliokuja kuvuruga utulivu wao kwa sababu ya kutokuwa wenyeji wa msitu wa heri – uk.9
   • Kutengwa mchezoni – Ridhaa anatengwa na wanafunzi wenzake wanapocheza shuleni mchezo wa kavuta kwa sababu ya kuwa mwanafunzi mlowezi katika msitu wa heri uk.10
   • Kubandikwa majina. Wanafunzi shuleni wanamwita Ridhaa ‘mfuata mvua’ kwa sababu ya kuwa mwanafunzi mlowezi – uk. 10. Pia mavyaa wake Subira anamwita Subira ‘muki’ kwa sababu Subira anatoka anatoka katika jamii ya bamwezi; jamii tofauti na yake – uk. 94
   • Chuki za kikabila zinawasababishia wanafunzi kumchukia Ridhaa anapofaulu katika mitihani yake. Wanamwona kama aliyeenda katika mitihani yote – uk.10
   • Kusingiziwa wizi. Ridhaa anasingiziwa kuiba kalamu za wanafunzi wengine kwa sababu analowea Msitu wa heri – uk.10.subira pia anasingiziwa kuiba mayai ya kuku kwa sababu ya usuli wake. Yeye ni wa jamii ya bamwezi – uk.96
   • Dhiki za kisaikolojia. Unyanyapaa shuleni kutoka kwa wanafunzi wenyeji wa msitu wa heri unamsababishia Ridhaa kutoroka shuleni na kulia kwa kite na shake na kuapa kutorudi shuleni – 10
 6.  
  1. elezea misiba inayoikumba jamii ya, “shogake dada ana ndevu” ni ya kujitakia. Thibitisha
   1. mimba – safia anazini na kimwana na kuishia kupachikwa mimba
   2. kifo – safia anaenda kliniki kuavya mimba aliyopachikwa na kimwana – anaishia kufariki dunia
   3. masudi na bi. Hamida wanakosa kumlea mwanao safia ipasavyo – anaishia kupachikwa mimba na kufariki dunia anapojaribu kuiavya mimba hiyo
   4. bwana masudi na bi. Hamida wanakosa kumchunguza kimwana ili kumjua vizuri Zaidi – matokeo yanakuwa ni kuharibu mustakabali wa maisha ya mwanao safia – kimwana anampachika safia mimba inayoishia kuwa chanzo cha kifo chake
   5. upujufu wa maadili – habiba cheichei anashindwa kumlea mwanawe, mkadi ifaavyo – mkadi anaishia kuwa mwovu ajabu – tunaambiwa kwamba ayafanyayo hata shetani hayafanyi
   6. uzinifu – bi. Hamida anatumia muda wake kwenye vikao na Wanawake wengine kuwasengenya watoto wa wenzao badala ya kutumia muuda huo kumshauri na kumwelekeza mwanawe safia – matokeo yanakuwa ni safia kupotoka kimadili na kuanza kumleta mwanamume (kimwana) nyumbani kwao anayempachika mimba
   7. bi. Hamida na bwana masudi wanakosa uwajibikaji katika malezi kwa kumsifu mwanao safia badala ya kuzungumza naye na kumpa shauri ambao ungemsaidia kukabiliana na changamoto za maisha – safia anaishia kuwa mzinifu – anamleta kimwana nyumbani kwao na kuwandanganya wazazi wake kuwa wanasoma kumbe wanafanya mapenzi.
   8. Safia anakubali kufanya mapenzi na kimwana – anaishia kupachikwa mimba inayomsababisha kutapikatapika
   9. Badala ya bi. Hamida na bwana masudi kuhakikisha kwamba mwanao safia anasoma jinsi alivyowaambia, wanamhimiza ajifungie chumbani pamoja na kimwana ili lulua asiwasumbue hivyo kuwapa wakati mzuri wa kufanya mapenzi badala ya kusoma.
   10. Bwana masudi anampuuza mkewe, bi. Hamida anapomuuliza hali ya safia ya kutapikatapika kwa kumwambia kwamba asiwe na wasiwasi – mapuuza haya yanawafanya kutochukua hatua ya mapema na kusababisha kifo cha safia anapoenda kuiavya mimba.
  2. Jadili madhila ya raia wanaoishi katika mitaa ya mabanda ukirejelea hadithi ya ndoto ya mashaka
   1. vyumba vya kupanga – mashaka, waridi na watoto wake wanaoishi kwenye chumba cha kupanga ila kipato cha mashaka ni kidogo
   2. harufu – familia ya mashaka inaishi karibu na choo kinachohanikiza harufu kwenye chumba chao
   3. matumizi ya vyoo va karatasi – akina mashaka wanatumia vyoo vya karatasi kwa sababu ya ukosefu wa misala
   4. mazingira machafu – haja kubwa na ndogo zimepatikana mtaani tandale kwa sababu ya ukosefu wa misala
   5. kuvuja kwa paa – familia ya mashaka iliteseka msimu wa mvua kwa sababu paa ilimwaga michirizi ya maji kwenye chumba chao
   6. chumba kidogo – chumba ilimoishi familia ya mashaka hakukiwatosha. Watoto wa kiume wa mashaka walilala jikoni mwa jirani yao, chakupewa
   7. utegemezi – mashaka anamtegemea jiraniye chakupewa kumpa mahali ambapo watoto wake wa kiume walilala kwa sababu ya umaskini
   8. kufanya kazi duni – mashaka anafanya kazi duni ya ulinzi katika kampuni ya zuia wizi security (zws). Alilipwa mshahara duni kutokana na kazi hii.
   9. Kukosa vilalio – chumba cha mashaka hakikuwa na kitanda wala godoro. Waridi alilalia mayowe huku wanawe wa kike wakilalia mbacha
   10. Ukosefu wa samani – chumba cha mashaka hakikuwa na meza wala kiti.
   11. Watoto kutoenda shuleni – kila wakati mashaka alirudi kutoka kazini asubuhi, wanawe walicheza mbai n nyumba ishara kwamba hawakuwa wakienda shuleni kwa sababu ya umaskini
 7. ”Maswali ya sampuli hiyo yanafaa kuulizwa na wanafunzi wa kidato ch kwanza”
  1. Eleza miktadha ya dondoo hili
   • haya ni maneno ya dkt. Mabonga
   • anamwambia mwanafunzi wake
   • wamo darasani katika chuo kikuu cha kivukoni
   • anamwambia hivi baada ya kumuuliza swali kuhusu namna fasihi inavyoielekeza jamii
  2. Fafanua sifa tatu za msemaji wa dondoo hili
   msemaji ni dkt. Mabonga. Ana sifa zifuatazo:
   1. mshairi bora – anawahimiza wanafunzi chuoni kivukoni kujitegemea na kusuta ukupe
   2. Mwenye kiburi – anapoulizwa swali na mwanafunzi wake anamjibu kuwa maswali ya sampuli hiyo yalifaa kuulizwa wanafunzi wa kidato cha kwanza
   3. Mapujufu/mpyaro – anamwita mwanafunzi anayetaka kuuliza swali ‘Mama’
   4. Mwenye madharau – anamcheka mwanafunzi wake kicheko kikubwa kabla ya kumpa nafasi ya kuuliza swali
  3. Tathmini namna maudhui ya utabaka yanavyojitokeza katika hadithi ambamo dondoo hili limetolewa
   1. kazi – wazazi wa dennis ambao ni maskini wanawalimia matajiri mashamba yao ili kupata hela za kujikimu kimaisha
   2. utengano – tunaambiwa kwamba maskini na matajiri wametengana kama ardhi na mbingu chuoni – dennis ingawa wama chuoni kimoja na wafabya masomo pamoja
   3. mavazi – wnanafunzi kutoka familia za kitajiri hawavai vitenge kutoka mataifa ya afrika kama Ghana, na senegali kama wenzao. Wanavaa mavazi kutoka uingereza, ujerumani, marekani na ufaransa
   4. vifaa vya kielektroniki – wanafunzi kutoka familia za kitajiri wanamiliki simu za thamani, vipakatalishi na ipad huku wanafunzi maskini kama dennis machora wakiwa hawana hata vifaa kimojawapo. Wanasalia kuvimezea mate tu
   5. shule – wanafunzi kutoka tabala la juu wanasomea kwenye shule za mikoa na kitaifa huku wanaotoka katika tabaka la chini kama dennis wakisomea katika shule za vijijini
   6. ndoa – ni nadra mtu wa tabaka la chini na tabaka la juu kuoana – wazazi wake penina wanapinga ndoa ya penina na dennis kwa sababu ya dennis anatoka katika familia ya kimaskini huku wao wakiwa matajiri
   7. pesa za matumizi – wanafunzi kutoka familia za kitajiri wanatumiwa pesa nyingi za matumizi huku maskini wakitaabika. Kwa mfano, penina anatumiwa shilingi elfu tano kila wiki huku maskini dennis wakinywa uji bila sukari kwa kukosa pesa
   8. mahali pa kuishi – mtaa wa new Zealand wanakoishi wazazi wa penina ni mtaa wa watu wenye mapato ya kadri
   9. kukataa uchumba – wazazi wa penina wanamkataza penina kuchumbiwa na dennis kwa sababu ya dennis kuwa maskini huku kwao wakiwa matajiri
   10. tabaka la chini linakejeliwa. Wazazi wake dennis wanakejeliwa na kila mtu kwa sababu ya kuwa maskini
   11. magari – tabaka la juu linamiliki magari makubwa makubwa huku tabaka la chini kama dennis likiishia kubaki likitamani magari hayo kwa maana halina uwezo wa kuyanunua
   12. wanafunzi kutoka tabaka la juu wanataka kuacha masomo ambayo wanadai kuwa ni magumu ili kufanya kazi zinazomilikiwa na wazazi wao huku maskini kama dennis hawana la kufanya hata kama masomo hayo ni magumu. Kwa mfano, kuna mmoja anayetaka kuenda kuwa manamba katika magari ya babake.
   13. wanafunzi wa tabaka la chini wanaoishi maisha ya taabu chuoni huku wa tabaka la juu wakiishi maisha mazuri. Kwa mfano, dennis analalia shuka zilizochanika mbali na kuwa na shida ya kupata chakula huku matajiri kama penina wakitumiwa shilingi elfu tano kila wiki na wazazi wao
   14. wanafunzi wa tabaka la juu hawali Baadhi ya vyakula wanavyoichukulia kuwa duni huku maskini kama dennis wakivila. Kwa mfano, penina apoingia chumbani mwa dennis anashangaa kwa nini dennis anakunywa uji ishara kwamba yeye hanywi uji kwa sababu ni wa tabaka la juu
   15. utabaka ni chanzo cha mtu kujidunisha kwa mwingine. Dennis anayetoka katika tabaka la chini anaogopa kuwa mpenziwe penina anayetoka katika tabaka la juu hataki kuolewa na mwanamume asiye na kazi ya mshahara kubwa/mwanamume wa tabaka la chini, hivyo kuuvunja uchumba wao.
   16. watoto kutoka tabaka la juu wanajinaki kwa wenzao kuhusu kazi wanazozifanya wazazi wao. Kwa mfano, dennis anakumbuka shakila akajinaki kwamba mama yake ni mkurugenzi mkuu wa shirika la kuchapisha magazetini
   17. watu wa tabaka la juu wanaoishi jijjini huku maskini mashambani. Kwa mfano akina shakila wanaishi kijiijini kivukoni huku dennis akiishi mashambani.
 8.  
  1. Fafanua ujumbe wa shairi hili
   • Shairi linazungumzia jinsi walio na nguvu wasivyowazia walio chini yao na kuwahimiza watu kuzinduka na kupunguza kelele pamoja na kujishaua
  2. Eleza muundo wa shairi hili
   1. Lina beti 5
   2. Kila ubeti una mishororo minne
   3. Kila mshororo una vipande viwili isipokuwa kibwagizo chenye kipande moja.
   4. Lina kibwagizo – jana awile siri!
   5. Vina vya kati na vya nje vinatiririka isipokuwa ubeti wa kwanza, mshororo wa kwanza wenye kina tofauti
   6. Kila mshororo una mizani 16 isipokuwa ubeti wa pili, mshororo wa pili na ubeti wa tano, mshororo wa kwanza yenye mizani 15.
   7. Kibwagizo kimekamilika kwa alama hisi!
  3. Eleza toni ya shairi hili
   • Toni ya kushauri – nafsineni anawashauri watu kuzinduka na kupunguza kelele na hali ya kujishaua/kujisifu
  4. Ainisha shairi hili kwa kuzingatia:
   1. Ruwaza ya mistari
    • Tarbia – Kila ubeti una mishororo mine
   2. Mathnawi – Kila mshororo una vipande viwili isipokuwa kibwagizo chenye kipande kimoja
   3. Ruwaza ya mizani
    • Msuko – Kibwagizo kina mizani michache kuliko mishororo mingine
  5. Eleza mbinu nne ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi
   1. Tabdila
    • Yamchezeya – Yamchezea
    • Yanautaniya – Yautania n.k.
   2. Inkisari
    • ‘mejitokeya – imejitokea
    • Walosogoya – waliosogea
   3. Kikale – awile – alikuwa
   4. Kufinyanga sarufi – kwingi kujishauya – kwingi kujishaua
  6. Bainisha sifa mbili za anayezungumziwa katika shairi hil
   1. Mwenye vitisho – alipobweka/alipozungumza waoga walijinyia
   2. Mwenye ubinafsi – Hakuwawazia waliokuwa chini yake
  7. Eleza tamathali mbili za usemi zilizotumiwa katika shairi hili
   1. Jazanda – mbwa
   2. Taswira – mabuu yakimchezea mbwa
   3. Tashihisi- mainzi yamchekea
   4. Chuku – Tena akibweka yule, waoga walijinyinya
   5. Sitiari – ni dunia maji male
 9.  
  1. Dhamira ya mtunzi wa shairi hili ni gani?
   • Kuhimiza watu kutendea wenzao mema wakiwa wangali hai
  2. Bainisha nafsineni katika shairi hili
   • Kipusa Binti Hamadi – Kipusa Binti Hamadi, siku n’takuwa kimba
  3. Eleza toni ya shairi hili
   • Toni ya kushauri – Kipusa Binti Hamadi anatoa ushauri kwamba azikwe angali hai.
  4. Changanua muundo wa shairi hili
   1. Lina ubeti 5
   2. Kila ubeti una mishororo minne
   3. Kila mshororo una vipande viwili isipokuwa ubeti wa tano , mshororo wa pili wenye vipande vitatu
   4. Vina vya ndani na vya nje vinabadilika katika ubeti
   5. Lina kibwagizo – Nizike ningali hai, n’kifa hutonizika
   6. Kila mshororo una mizani 16
  5. Fafanua maana ya kibwagizo cha shairi hili
   • Nisaidie ningali hai kwa maana nikifa hutaweza kunisaidia
  6. Eleza mbinu nne amabazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi
   1. Kufinyanga sarufi
    • Matozi ungayasomba – ungayasomba matozi
    • na mapumu kuugua – na kuugua mapumu
    • sanda nunua – nunua sanda
   2. Lahaja
    • Matozi – machozi
    • siate – siache
   3. Tabdila
    • hutonizika – hutanizika
    • zisipumua – zisipumue
   4. Inkisar
    • takuwa – nitakuwa
    • singojee - usingojee
  7. Bainisha bahari ya shairi hili
   1. Tarbia – lina mshororo minnne katika kila ubeti
   2. Mathnawi – Kila mshororo una vipande viwili isipokuwa ubeti wa tano, mshororo wa pili wenye vipande vitatu.
   3. Ukaraguni – Vina vya kati na vya nje vinabadilika katika kila ubeti.

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Bungoma Diocese Mock Exams 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest