Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Lanjet Mock Exams 2021/2022

Share via Whatsapp

MAAGIZO KWA MTAHINIWA:

  • Karatasi hii ina sehemu tano: A, B, C, D na E.
  • Jibu maswali manne pekee. Kila swali lina alama ishirini.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Chagua maswali mengine yoyote matatu kutoka sehemu zilizosalia; B, C, D ama E.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Majibu yote yaandikwe kwa Kiswahili

SEHEMU YA A: FASIHI SIMULIZI

  1. Lazima
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali:
    Wanangu, mwanadamu lazima awe na malengo ya mambo anayohitaji kuyatekeleza siku za maisha yake duniani kabla ya maisha ya baada ya kifo. Ni lazima akumbuke kuwa si vyema akubali kufa kama kwamba hakuwahi kuishi duniani. Yaani, haifai kwa mtu yeyote kuondoka duniani na kuelekea peponi kuishi kwa starehe ama ahera kwa wale wanaokufa kabisa, bila kuacha lolote lenye mashiko duniani. Lazima kuhakikisha kwamba kuna bora, japo moja, ambalo waliosalia duniani watakukumbuka kwalo. Japo kiduchu tu. Ukiwa mwimbaji imba lau ubeti mmoja tu ukasikizwe wakati utakapokuwa umepumzika. Ukiwa kiongozi jenga daraja japo moja na kulizindua wewe. Mwili wako utakuwa umeondoka ila nafsi yako itasalia duniani kwa jina lako.

    Ukiwa na mkono wa kuandika andika japo ubeti mmoja wa shairi. Kumbusha watu kuhusu umuhimu wa maisha na kuwaeleza kutenda mema kabla hawajaisha. Andika hata aya tatu za hadithi. Jihusishe katika mashindano maarufu japo ujue kuwa wahariri wataiangalia kazi yako na kusema, “Uchafu mtupu! Huyu hana talanta. Ameharibu wakati wake tu katika shindano hili la jumuia nzima. Sisi tunasaka talanta! Huyu limbukeni anatuletea hapa ‘viswahili’ gani hivi visivyo na mkia wala kichwa hali mwenyewe si Mswahili? Potelea jalalani! Huenda hata wakati mwingine kazi yako isisomwe ila wewe andika tu. Andika tena na tena. Andika.Andika usihofu. Bora tu usife kama hukuwahi kuishi.Zingatieni wosia wangu huu wanangu.
    (Kutoka Riwaya: Hawakuziki Mama- Meja S. Bukachi)
    1. Tambua kipera hiki cha fasihi simulizi. (Alama 2)
    2. Fafanua vipengele kumi vya kimtindo ambavyo fanani ametumia katika uwasilishaji wake. (alama 10)
    3. Eleza umuhimu wa kipera hiki katika jamii. (alama 3)
    4. Wewe ni kati ya wanaopewa kipera hiki. Fafanua mambo matano ambayo wewe na wenzako mnaweza kufanya wakati wa kutolewa. (alama 5)

SEHEMU YA B
RIWAYA: CHOZI LA HERI
(Assumpta K. Matei)

Jibu swali la pili ama la tatu

  1.  
    1. “Ufyatuaji ovyo wa risasi umesababisha vifo vya wananchi wasio na hatia. Watetezi wa haki wanalilia kile wanachokiita Untimely death of innocent people, many of whom are youth. Kumbukeni kuwa hata mtu akiwa mhalifu, ana haki, ana haki ya kufikishwa mahakamani kabla hajapewa adhabu yoyote...”
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      2. Eleza aina mbili za taswira katika dondoo hili. (alama 2)
      3. Bainisha vipengele vingine vinne vya kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)
    2. Jadili umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya ya Chozi la Heri kwa kurejelea mazingira ya Shule ya Tangamano. (alama 10)
  2.  
    1. Changanua mtindo katika kifungu kifuatacho: (alama 10)
      Mkuu wa shule, walimu na wanafunzi wenzangu, suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Tumeona jinsi misitu ilivyovamiwa na viongozi wenye mate ya fisi. Nasikia baadhi ya vinara wa taasisi mbalimbali za umma wamewaacha wanyama kama mayatima kwa kuwapoka makazi yao. Maelfu ya maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda. Badala ya mibambakofi na na miti mingine inayosafisha hewa, michai imetwaa nafasi yake. Wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui wa mazingira! Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii sharti ijitosheleze kwa chakula.
    2. Kwa kurejelea kifungu hiki na sehemu zingine ambazo hazijanukuliwa katika, fafanua suala analojadili Lunga Kiriri kwa jamii. (alama 10)

SEHEMU YA C
TAMTHILIYA: KIGOGO
(Pauline Kea)

Jibu Swali la 4 au la 5

  1.  
    1. Jadili umuhimu wa mazungumzo kati ya Ashua na Majoka katika kujenga tamthiliya ya Kigogo. (alama 10)
    2. Jadili mchango wa wasomi katika hali ya maisha ya Wanasagamoyo. (alama 10)
  2. “La, la Mzee .... mbio za sakafuni zimefika ukingoni.Ikiwa umekataa kushindwa, mimi nimekubali.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Bainisha vipengele viwili vya kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)
    3. Jadili umuhimu wa mzungumzaji katika kuvijenga vipengele vifuatavyo vya tamthiliya hii.
      1. Ploti (alama 6)
      2. Maudhui (alama 6)

SEHEMU YA D: USHAIRI

Jibu swali 6 au 7

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali:

    TUNAPOSEMA

    Baba ya mtu ni baba, mama na baba wazazi
    Papa wa maji si baba, papa samaki wa pezi
    Papa hapa siyo haba, papa tulipo sahizi
    Tunaposema ni bapa, li wazi kama kiganja.

    Kura nitapiga kura, kura ya kuchaguana
    Kula kishampa kura, kula tumbo kujazana
    Gura kijiji taghura, gura kutoonekana
    Tunaposema ni guro, juwa hapo pamehamwa.

    Lia machozi we lia, lia yatoke machoni
    Lia chakula we lia, mwenzio njaa sioni
    Lia usikike lia, kwa sauti sikioni
    Tunaposema ya ria,manake kujishauwa.

    Lala chini sakafuni, lala usikuwe juu
    Lala ‘ngia singizini, ukapate ndoto kuu
    Lala na huko kazini, ukayaone makuu
    Tunaposema ya rara, simulizi meingia.

    Twapasa ‘fanya akiki, mtoto kuwekwa dua
    Akiki pete akiki, akiki kupendezea
    Akiki kwa mahandaki, akiki poromokea
    Tunaposema hakiki, manake ni kuchambua.

    Sharabu siyo sharabu, sharabu ina aibu
    Kishasharabu sharabu, utalewa kwa sharabu
    Kusharabu kwa sharabu, yaani kunywa sharabu
    Tunaposema sharafa, ni nywele kwenye mashavu.

    Ana ghali kali gari, gari analomiliki
    Kali kwa maana gari, lingine litamaniki
    Ghali bei yake gari, kwa peni linunuliki
    Na tunaposema kali, pia hukata kwa sana.

    Mambo husemwa kangaja, pole huenda yakija
    Nami nasema kangaja, samaki vumbaye yaja
    Wajua zile kangaja, nyasi nilizozitaja?
    Tunaposema kangaja, ni chenza zilizo dogo.
    (Kutoka: Meja S. Bukachi- Uketo wa Ushairi)

    Maswali
    1. Eleza maana nne za neno kangaja kama anavyoeleza mshairi. (alama 4)
    2. Eleza aina nne za taswira zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 4)
    3. Bainisha aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 4)
    4. Huku ukitoa mifano, onyesha aina mbili ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 2)
    5. Bainisha mbinu zifuatazo za kimtindo katika shairi hili: (alama 3)
      1. Takriri
      2. Methali
      3. Tanakuzi
    6. Eleza muundo wa ubeti wa nne. (alama 2)
  2. Soma mashairi yafuatayo kisha ujibu maswali:

    SHAIRI ‘A’

    Umekata mti mtima
    Umeangukia nyumba yako
    Umeziba mto hasira
    Nyumba yako sasa mafurikoni
    Na utahama
    Watoto wakukimbia

    Mbuzi kumkaribia chui
    Alijigeuza panya
    Akalia kulikuwa na pala
    Kichwani
    Mchawi kutaka sana kutisha
    Alijigeuza simba
    Akalia na risasi kichwani

    Jongoo kutaka sana kukimbia
    Aliomba miguu elfu
    Akaachwa na nyoka

    Hadija wapi sasa yatakwenda
    Bwanako kumpa sumu?
    Hadija umeshika nyoka kwa mkia
    Hadija umepitia nyuma ya punda

    SHAIRI ‘B’
    Piteni jamani, piteni haraka
    Nendeni, nendeni huko mwendako
    Mimi haraka, haraka sina
    Mzigo wangu, mzigo mzito mno
    Na chini sitaki kuweka

    Vijana kwa nini hampiti?
    Kwa nini mwanicheka kisogo?
    Mzigo niliobeba haupo.

    Lakini umenipinda mgongo na
    nendako
    Haya piteni! Piteni haraka! Heei!

    Mwafikiri mwaniacha nyuma!
    Njia ya maisha ni moja tu.
    Huko mwendako ndiko nilikotoka
    Na nilipofikia wengi wenu
    Hawatafika.

    Kula nimekula na sasa mwasema
    Niko nyuma ya wakati
    Lakini kama mungepita mbele
    Na uso wangu kutazama
    Ningewambia siri ya miaka
    Mingi.

    Maswali
    1. Haya ni mashairi ya aina gani ? Toa saabu. (alama 2)
    2. Washairi hawa wawili wanalalamika. Yafafanue malalamishi yao (alama 4)
    3. Onyesha jinsi kinaya kinavyojitokeza katika tungo hizi mbili. (alama4)
    4. Ni vipi Hadija :- (alama 2)
      1. Amekata mti mtima?
      2. Amepita nyuma ya Punda?
    5. Toa mifano miwili ya uhuru wa mshairi kwa kurejelea mashairi haya. (alama 4)
    6. Kwa kurejelea shairi ‘B’ eleza maana ya:- (alama 4)
      1. Mzigo
      2. Siri
      3. Kula nimekula
      4. Niko nyuma ya wakati

SEHEMU YA E: HADITHI FUPI
TUMBO LISILOSHIBA NA HDITHI NYINGINE
(Alifa Chokocho na Dumu Kayanda- Wahariri)

  1. Ali Mwalimu Rashid: Mkubwa
    1. “Unajua mimi nilikuwa sipo.Na kule vijana wangu wanaokujua walikuwa hawapo.Walipelekwa vijana wapya.Wale hawajui kitu. Na kuku mgeni usimtoe nje....”
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      2. Bainisha toni ya dondoo hili. (alama 2)
      3. Kwa hoja kumi kutoka katika hadithi hii, thibitisha jinsi wananchi walivyokuwa kama kuku wageni na wasiojua kitu. (alama 10)
    2. Bainisha vipengele vya kimtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 4)
      “Oya! Nani huyoo! Unga! Unga! Ebo! Mimi naweza kumtoa mtu mtu chango sasa hivi. Usituangalie bwana. Kwani tunakula kwa babako?Makande we!”
      “He! Anaumwa huyu?Isijekuwa kidume kimemshika huyu. Unajua tena ngiri! Haina sumile.”


MARKING SCHEME

SEHEMU YA A: FASIHI SIMULIZI

  1.  
    1. Tambua kipera hiki cha fasihi simulizi. (Alama 2)
      • Mawaidha- kuna matumizi ya lugha ya kushawishi na kushauri mtu kukabiliana na maisha.
        Moja kutaja, moja kueleza (1x2)
    2. Fafanua vipengele kumi vya kimtindo ambavyo fanani ametumia katika uwasilishaji wake. (alama 10)
      • Baba anazungumza moja kwa moja na wanawe.
      • Matumizi ya chuku- uchafu mtupu.
      • Tashihisi- potelea jalalani.
      • Methali- atakaye cha mvunguni sharti ainame.
      • Nahau- uchafu mtupu (isiyo na maana)
      • Urudiaji- Andika tena na tena. Andika. Andika usihofu.
      • Ritifaa- wahariri watasema, Potelea jalalani!
      • Tasfida- utakapokuwa umepumzika (utakapokuwa umekufa)
      • Kuigiza- Uchafu mtupu. Huyu hana talanta. Ameharibu wakati wake tu katika shindano hili la jumuia nzima. Sisi tunasaka talanta! Huyu limbukeni anatuletea hapa ‘viswahili’ gani hivi visivyo na mkia wala kichwa hali mwenyewe si Mswahili? Potelea jalalani!”
      • Nidaa/ Siyai- potelea jalalani! (10x1=10)
    3. Eleza umuhimu wa kipera hiki katika jamii. (alama 3)
      • Mawaidha hutoa mwongozo wa jinsi ya kukabiliana na matatizo au jinsi ya kutenda jambo.
      • Mawaidha huelimisha kwa kuwapa wanajamii maarifa ya kuendesha maisha.
      • Wanaopewa mawaidha hujifunza maadili kama vile adabu, heshima na kadhalika.
      • Mawaidha hutambulisha jamii kwani kila jamii huwa na aina yake ya mawaidha kulingana na thamani zake.
        Hoja zifafanuliwe (3x1=3)
    4. Wewe ni kati ya wanaopewa kipera hiki. Fafanua mambo matano ambayo wewe na wenzako mnaweza kufanya wakati wa kutolewa. (alama 5)
      • Kuuliza maswali.
      • Kutoa majibu kwa baadhi ya maswali ya anayetoa mawaidha.
      • Kusikiliza kwa makini.
      • Kuuliza maswali palipo na utata.
      • Kuonesha kukubaliana kwa ishara za uso.
        (5x1=5)

SEHEMU YA B
RIWAYA: CHOZI LA HERI
(Assumpta K. Matei)
Jibu swali la pili ama la tatu

  1.  
    1. “Ufyatuaji ovyo wa risasi umesababisha vifo vya wananchi wasio na hatia. Watetezi wa haki wanalilia kile wanachokiita Untimely death of innocent people, many of whom are youth. Kumbukeni kuwa hata mtu akiwa mhalifu, ana haki, ana haki ya kufikishwa mahakamani kabla hajapewa adhabu yoyote...”
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
        • Haya ni maneno ya Apondi katika mawazo ya Mwangeka. Mwangeka na mkewe Apondi wameketi kwenye behewa la nyumba yao. Mwangeka anakumbuka hotuba ya Aponddi kwa maafisa wa askari kuhusu jukumu la vikosi vya askari katika kudumisha usalama, amani na maridhiano nchini. Ni katika warsha hii ndipo Mwangeka alipokutana na Apondi na uchumba wao kuanza. (4x1=4)
      2. Eleza aina mbili za taswira katika dondoo hili. (alama 2)
        • Taswira masikizi/ ya kusikia- ufyatuaji wa risasi.
        • Taswira mwendo- kufikishwa mahakamani.
        • Taswira hisi/ ya kuhisi- hajapewa adhabu.
          (2x1=2) lazima mtahiniwa atoe mfano ili atunzwe alama 1
      3. Bainisha vipengele vingine vinne vya kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)
        • Hotuba- ya Apondi
        • Kuhamisha lugha/ msimbo- Untimely death of innocent people, many of whom are youth.
        • Takriri/ urudiaji- ana haki, ana haki ya kufikishwa mahakamani
        • Kinaya- Ufyatuaji ovyo wa risasi umesababisha vifo vya wananchi wasio na hatia
          (4x1=4) lazima mtahiniwa atoe mifano katika kifungu.
    2. Jadili umuhimu wa mandhari katika kuijenga riwaya ya Chozi la Heri kwa kurejelea mazingira ya Shule ya Tangamano. (alama 10)
      • Kuonyesha nafasi ya shule katika kuokoa maisha ya wanafunzi.
      • Kurejelea suala la ukiukaji wa haki za watoto.
      • Kuonyesha majanga yanayowapata watoto baada ya kifo cha wazazi. Umu anajipata shuleni baada ya kifo cha babake Lunga.
      • Kuonyesha athari za utengano wa wazazi kwa watoto. Umu anajipata shuleni Tangamano baada ya babake na mamake kutengana naye babake kuaga dunia,
      • Kuonyesha athari za vita vya kikabila kwa watoto. Kairu na jamaa wake wanalazimika kutoroka nyumbani baada ya vita.
      • Kuonyesha athari za wanajamii kwa ndoa za wanao na jinsi zinavyoathiri maisha ya kizazi cha baadaye.
      • Wazazi wa Mzee Kaizari waliingilia ndoa yake na kufanya mkewe kuondoka. Kifo cha mama kiliwaathiri sana Mwanaheri.
      • Kuonyesha umuhimu wa elimu katika kuleta mabadiliko katika jamii.
      • Kuonyesha nafasi waliyo nayo kina dada ya kuendeleza masomo yao hata baada ya kupitia hali ngumu kama vile ujauzito. Mtawa Pacha anamhakikishia Zohali kuwa angerejea shuleni baada ya kujifungua.
      • Kuonyesha baadhi ya matatizo wanayopitia wasichana wanapoambulia ujzauzito. Zohali alifanywa kijakazi wa kufua, kupiga deki, kupika na kadhalika baada ya kuambulia ujauzito.
      • Kuonyesha changamoto wanazopitia watoto wanaolelewa bila wazazi wao. Chandachema alilelewa na nyanya yake.
      • Kuonyesha jinsi baadhi ya wafanyakazi na walimu wanavyokiuka kaida za kikazi na kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi usiofaa na wanafunzi wao. Chandachema ni zao la Mwalimu Fumba kuhusiana kimapenzi na mwanafunzi wake.
      • Kuonyesha jinsi baadhi ya wazazi wanavyowatelekeza wanao kama alivyotelekezwa Chandachema.
        (10x1=10) hoja za mtahiniwa zifafanuliwe.
  2.  
    1. Changanua mtindo katika kifungu kifuatacho: (alama 10)
      Mkuu wa shule, walimu na wanafunzi wenzangu, suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Tumeona jinsi misitu ilivyovamiwa na viongozi wenye mate ya fisi. Nasikia baadhi ya vinara wa taasisi mbalimbali za umma wamewaacha wanyama kama mayatima kwa kuwapoka makazi yao. Maelfu ya maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda. Badala ya mibambakofi na miti mingine inayosafisha hewa, michai imetwaa nafasi yake. Wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui wa mazingira! Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii sharti ijitosheleze kwa chakula.
      • Hotuba- ya Lunga
      • Jazanda- viongozi wenye mate ya bafe (viongozi walafi)
      • Tashhihisi- wamewaacha wanyama kama mayatima.
      • Kinaya- maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda.
      • Nidaa/siyai- michai si adui wa mazingira!
      • Tashbihi- wamewaacha wanyama kama mayatima.
      • Taswira- tumeona jinsi misitu ilivyovamiwa.
      • Nahau- Mate ya fisi.
      • Kutumia usemi halisi.
      • Ukinzanzani- Wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui wa mazingira! Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii sharti ijitosheleze kwa chakula.
        (10 x 1=10)
    2. Kwa kurejelea kifungu hiki na sehemu zingine ambazo hazijanukuliwa katika kifungu, fafanua suala analojadili Lunga Kiriri kwa jamii. (alama 10
      Hotuba hii ilisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira. Anasisitiza kuwa:
      • Suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu.
      • Misitu ilikuwa imevamiwa na viongozi wenye mate ya fisi.
      • Baadhi ya vinara wa taasisi mbalimbali za umma wamewaacha wanyama kama mayatima kwa kuwapoka makazi yao.
      • Maelfu ya maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda.
      • Badala ya mibambakofi na miti mingine inayosafisha hewa, michai imetwaa nafasi yake.
      • Wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui ya mazingira!
      • Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii lazima ijitosheleze kwa chakula.
      • La kuhuzunisha ni kwamba hawa hawa wanaosema hivyo ndio wanaokita majengo ya kifahari katika sehemu ambazo zinastahili kutengewa upanzi wa chakula!
      • Wengine wamediriki kunyakua hata madhabahu kwenye Mlima wa Nasibu ili kujenga hoteli kubwa za kitalii.
      • Wazee wetu hata hawana mahali pa kuchomea kafara!
      • Tunakata miti bila kupanda mingine.
      • Hata mabustani ya maua tunashindwa kuyastawisha.
      • Tukiendelea kuharibu mazingira sehemu yetu itazidi kuwa jangwa.
        (zozote 10 x 1 = 10)

SEHEMU YA C
TAMTHILIYA: KIGOGO
Pauline Kea
Jibu Swali la 4 au la 5

  1.  
    1. Jadili umuhimu wa mazungumzo kati ya Ashua na Majoka katika kujenga tamthiliya ya Kigogo. (alama 10)
      • Kujenga sifa za wahusika- kupitia mazungumzo haya tunatambua ufuska wa Majoka.
      • Kufufua matukio ya awali- Majoka aliwahi kumchumbia Ashua akamkataa,
      • Kuonyesha suala la usaliti katika ndoa. Majoka anataka kujihusisha na mapenzi na Ashua wakati ana mke.
      • Kusisitiza umuhimu wa kuaminiana na kujiheshimu katika ndoa. Ashua anasisitiza kuwa ameolewa.
      • Kuonyesha jinsi viongozi wanavyotumia vibaya ofisi zao.
      • Kuonyesha jinsi baadhi ya viongozi wasivyothamini ndoa za wananchi. Majoka hajali kuvunika kwa ndoa ya Ashua.
      • Kuonyesha athari za ukosefu wa chakula kwa watoto.
      • Kuonyesha kuzinduka kwa wanawake katika kutetea haki zao.
      • Kuonyesha tatizo la ubinafsishaji wa uongozi. Babake Majoka alikuwa kiongozi wa awali.
      • Kuonyesha baadhi ya miradi duni ambayo viongozi wanashughulikia.
        (zozote 10 x 1 =10)
    2. Jadili mchango wa wasomi katika hali ya maisha ya Wanasagamoyo. (alama 10)
      • Wanachangia kuendeleza uchumi. Hata wanapokosa ajira, wanajiajiri. Sudi anachonga vinyago.
      • Wanapigania haki za wanyonge. Tunu na Sudi wakiwa chuoni walikuwa viongozi wa kupigania haki.
      • Wanawazindua Wanasagamoyo kuhusu umuhimu wa kuwa na uongozi unaozingatia misingi ya kidemokrasia.
      • Wanakosoa uongozi. Tunu anamkabili Majoka na kumwambia kuwa Wanasagamoyo wana haki ya kuishi.
      • Wanahimiza haja ya kuzingatia maadili ya kijamii. Ashua anakataa ushawishi wa Majoka.
      • Wanaboresha utendakazi katika taaluma zao. Walimu wanagoma ili kupata mazingira mazuri ya kufanyia kazi.
      • Wanatoa kielelezo cha uongozi ufaao. Tunu anasema kuwa wanahitaji uongozi unaofahamu matatizo yao.
      • Wanafunza kuhusu umuhimu wa familia na malezi. Sudi anamwambia Ashua awafikirie watoto wao.
      • Wanaimarisha itikadi za kijinsia zinazowaletea mabadiliko katika jamii. Tunu na Sudi wanashirikiana bila kujali kusemwa na watu.
      • Wanakosoa wanyonge wanaotumiwa kama vibaraka. Sudi anawatanabahisha kina Ngurumo kuhusu hali zao.
      • Baadhi yao wanaendeleza ubaguzi wa kijinsia. Ngurumo anasema hawezi kumpa Tunu kura yake.
      • Wanasisitiza umuhimu wa elimu na ustaarabu.
      • Baadhi wanakwamiza juhudi na kupigania haki.
        (zozote 10 x 1 = 10)
  2. “La, la Mzee .... mbio za sakafuni zimefika ukingoni. Ikiwa umekataa kushindwa, mimi nimekubali.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      Haya ni maneno ya Kenga. Anamwambia Majoka. Wapo kwenye lango kuu sokoni. Walinzi wa Majoka wamewashusha Tunu na Sudi. Majoka anamwamrisha Kingi awapige waandamanaji risasi anakataa. Majoka anamsisitizia Kenga kuwa hapendi waoga. Kenga anakiri kuwa amesalimu amri anajiunga na kundi la kina Tunu. (4 x1=4)
    2. Bainisha vipengele viwili vya kimtindo katika dondoo hili. (alama 4)
      • Urudiaji- La, la Mzee
      • Methali- mbio za sakafuni zimefika ukingoni.
      • Kinaya- Kenga anamsaliti Majoka.
        (zozote 2 x 2 =4)
        (Kutaja maelezo)
    3. Jadili umuhimu wa mzungumzaji katika kuvijenga vipengele vifuatavyo vya tamthiliya hii.
      1. Ploti (alama 6)
        • Kupitia kwake tunaelezewa kuhusu usuli wa Ngurumo kumvunja Tunu mguu.
        • Baadhi ya matukio katika maisha ya wahusika yanaangaziwa naye moja kwa moja. Anaenda katika karakana ya kina Sudi.
        • Kupitia kwake tunafafanuliwa kuhusu ila na hila za Majoka.
        • Anajenga mgogoro kati ya wanamabadiliko na wanaotaka hali ibakie hivyo. Kenga anasema kuwa amekubali kushindwa.
        • Matukio katika ofisi ya Majoka yanatusaidia kujua kuwa ndiye aliyepanga njama ya kumfunga Ashua jela.
        • Kuonyesha hatima ya mgogoro katika ya viongozi na wanyonge. Kuwa amekubali kushindwa.
        • Kuonyesha mustakabali wa Sagamoyo. Anaomba msamaha.
          (zozote 6 x 1 =6)
      2. Maudhui (alama 6)
        • Anaendeleza suala la ufisadi. Anapewa sehemu ya ardhi katika soko la Chapakazi.
        • Kuonesha ushauri mbaya. Anapanga njama ya Majoka kumnasa Ashua.
        • Kuonyesha ukosefu wa uwajibikaji. Anataka kumuhonga Sudi kwa mabaki ya keki.
        • Anaangamiza kizazi cha vijana. Anatumia vijana kama Chopi kufanikisha mauaji.
        • Anaonyesha matumizi mabaya ya cheo. Anatumia nafasi aliyopewa na Majoka kuendeleza mauaji na ushauri mbaya.
        • Anaonyesha haja ya maridhiano. Anakubali kushindwa na kujiunga na kundi la Tunu.
        • Kuangazia mabadiliko. Anakiri kuwa mbio zao za sakafuni zimefika ukingoni.
        • Anaendeleza maudhui ya tamaa na ubinafsi. Anajuhusisha na Majoka ili ajinufaishe.

SEHEMU YA D: USHAIRI
Jibu swali 6 au 7

  1.  
    1. Eleza maana nne za neno kangaja kama anavyoeleza mshairi. (alama 4)
      • Baadaye.
      • Samaki mwenye vumba kali.
      • Aina ya nyasi.
      • Chenza ndogo. (4x1=4)
    2. Eleza aina nne za taswira zinazojitokeza katika shairi hili. (alama 4)
      • Taswira masikizi/ ya kusikia- Tunaposema.
      • Taswira mwonjo/ ya kuonja- kula tumbo kujazana
      • Taswira uoni/ ya kuona- Lala chini sakafuni
      • Taswira hisi/ ya kuhisi- Lia usikike lia, kwa sauti sikioni.
      • Taswira mwendo- papa tulipo sahizi, Gura kijiji taghura.
      • Taswira mwonjo/ ya kuonja- Kishasharabu sharabu
        (zozote 4 x 1 =4)
        Mtahiniwa lazima atoe mfano.
    3. Bainisha aina mbili za urudiaji zilizotumiwa katika shairi hili (alama 4)
      • Urudiaji wa neno- tunaposema, gari
      • Urudiaji wa sentensi/ mstari/ kipande-
      • Urudiaji wa sauti- Papa hapa siyo haba
      • Urudiaji wa silabi- ni, bu n.k.
        (zozote 2 x 2 = 4)
    4. Huku ukitoa mifano, onyesha aina mbili ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 2)
      • Inkisari- vumbaye- vumba yake
      • Kufinyanga sarufi- ana ghali kali gari- ana gari ghali kali.
        (2x1=2)
        Mtahiniwa andike neno sahihi ili apate alama
    5. Bainisha mbinu zifuatazo za kimtindo katika shairi hili: (alama 3)
      1. Takriri- Akiki pete akiki n.k.
      2. Methali- Mambo kangaja huenda yakaja.
      3. Tanakuzi- Lala chini sakafuni, lala usikuwe juu.
        (3x1=3)
    6. Eleza muundo wa ubeti wa nne. (alama 2)
      • Una mishororo minne
      • Kila mshororo una vipande viwili.
      • Kila mshororo una mizani 16
      • Vina vya ndani ni –ni na vina vya nje ni –u.
        (4 x ½ =2)
  2.  
    1. Haya ni mashairi ya aina gani ? Toa saabu (alama 2)
      • Mashairi huru- Hayazingatii arudhi za beti, vina, mishororo, mizani na kibwagizo. (1x2=2)
        (kutaja 1, kueleza 1)
    2. Washairi hawa wawili wanalalamika. Yafafanue malalamishi yao (alama 4)
      • SHAIRI A – Anamlalamikia Hadija kwa kumuua mumewe kwa kumpa sumu.
      • SHAIRI B – Anawalalamikia vijana ambao wanamcheka eti amezeeka na kupitwa na wakati Wanamramba Kisogo (2x2=4)
    3. Onyesha jinsi kinaya kinavyojitokeza katika tungo hizi mbili (alama 4)
      • Katika SHAIRI ‘A’ - Hadija alidhani kumuua mumewe angepata suluhisho lakini badala yake amejiletea matatizo zaidi. Watu sasa wamemsuta kwa kitendo chake na watoto wanamsumbua. (2x2=4)
      • Katika SHAIRI ‘B’ – Mshairi anawakejeli vijana ambao wanamramba mzee kisogo bila kujua kwamba hawataki kupita.
    4. Ni vipi Hadija :- (alama 2)
      1. Amekata mti mtima ? Amemuua mumewe – Mti mkuu au kichwa cha nyumba.
      2. Amepita nyuma ya Punda- Anapata shida za kujitakia – matatizo yamefurika nyumbani kama mto (ukipita nyuma ya punda atakutega au kukupiga teke)
    5. Toa mifano miwili ya uhuru wa mshairi kwa kurejelea mashairi haya (alama 4)
      • Inkisari – Nendako – Niendako-
        Mwendako – Mnakoenda
        Bwanako – Bwana yako
      • Kufinyanga sarufi- haraka sina- sina haraka
    6. Kwa kurejelea shairi ‘B’ eleza maana ya:- (alama 4)
      1. Mzigo– uzee/umri
      2. Siri- Tajriba/ maarifa/ elimu ya maisha
      3. Kula nimekula- ameishi miaka mingi.
      4. Niko nyuma ya wakati- amebaki nyuma na usasa.

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
TUMBO LISILOSHIBA NA HDITHI NYINGINE
Alifa Chokocho na Dumu Kayanda
Ali Mwalimu Rashid: Mkubwa

  1.  
    1. “Unajua mimi nilikuwa sipo. Na kule vijana wangu wanaokujua walikuwa hawapo.Walipelekwa vijana wapya.Wale hawajui kitu. Na kuku mgeni usimtoe nje....”
      1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
        • Haya ni maneno ya Ng’weng’we wa Njagu. Anamweleza Mheshimiwa Mkubwa. Wako nyumabi kwa Ng’weng’we wa Njagu. Mkubwa amemtembelea Ng’weng’we usiku wa manane ili kujadili jinsi ya Mkumbukwa kutolewa mahabusu na Mkubwa kurejeshewa mzigo wake.
          (4x1=4)
      2. Bainisha toni ya dondoo hili. (alama 2)
        • Toni ya huruma/ huzuni- Ng’weng’we wa Njagu anamhurumia Mheshimiwa Mkubwa kwa yaliyompata. (1x2=2)
          (kutaja 1, kufafanua1)
      3. Kwa hoja kumi kutoka katika hadithi hii, thibitisha jinsi wananchi walivyokuwa kama kuku wageni na wasiojua kitu. (alama 10)
        • Bi. Kibwebwe anashirikiana na Mkumbukwa kuwashawishi Wanamchafukoge kumchagua Mkubwa kuwa kiongozi wao ambaye ni fisadi.
        • Bi kibwebwe na Mkumbukwa walishiriki katika kuwahonga watu ndiposa wakamchagua Mkubwa kuwa kiongozi wao.
        • Mkumbukwa anakubali kushirikiana na Mkubwa katika uuzaji wa dawa za kulevya. Aidha, anawahonga Wanamchafukoge ili wampigie Mkubwa kura.
        • Baada ya Mkumbukwa kushikwa, anageuza msimamo wake na kujiondoa kwenye biashara ya dawa za kulevya. Anawahurumia vijana waliofungwa jela.
        • Baadhi ya wananchi na viongozi wana tamaa. Mkubwa Haridhiki na pesa chache anazopata kutoka kwa biashara yake. Ana tamaa ya mali inayomfanya kuuza shamba la urithi wake na kuingilia siasa ili apate pesa rahisi.
        • Mkubwa anawauzia dawaya kulevya vijana wasiofahamu madhara ya dawa hizo za kulevya.
        • Wananchi waMchafukoge wanamchagua kiongozi (Mkubwa) bila kutathmini lengi lake la kujiingiza kwenye siasa.
        • Wananchi wana ndoto zisizotimilika na wengi wamejisahau kwa kutumia dawa za kulevya.
        • Wanaofungwa jela ni vijana maskini wasio na wa kuwatetea. Vigogo hawafungwi na wakitiwa ndani huachiliwa muda mfupi baadaye.
        • Wafungwa katika jela wanadhulumiwa na kuteswa na kuona kila kitu kama kifo. Kula kifo, malezi ni kifo, kukoga ni kifo, kufua kifo, kifo, kifo. Hawajui haki zao.
        • Viongozi serikalini hawakaguliwi wanapoingiza mizigo bandarini ama kwenye uwanja wa ndege. Wananchi wanyonge ndio wanaokaguliwa.
        • Mkumbukwa anaposhikwa, Mkubwa anatumia ushawishi wake na kuzungumza na Ng’weng’we wa Njagu (mkuu wa polisi) na mwishowe Mkumbukwa anaachiliwa. Anawaach vijana wasiojua chochote katika jela.
        • Aidha, Mkubwa anarudishiwa mzigo wake wa dawa za kulevya, ananedelee na biashara yake ya kuwadhuru wananchi.
          (zozote 10x1=10)
    2. Bainisha vipengele vya kimtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 4)
      “Oya! Nani huyoo! Unga! Unga! Ebo! Mimi naweza kumtoa mtu chango sasa hivi.Usituangalie bwana. Kwani tunakula kwa babako? Makande we!”
      “He! Anaumwa huyu? Isijekuwa kidume kimemshika huyu. Unajua tena ngiri! Haina sumile.”
      • Nidaa/ Siyai- Oya!
      • Urudiaji- Unga! Unga!
      • Balagha- Kwani tunakula kwa babako?
      • Matumizi ya usemi halisi.
        Zozote 4x1=4
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Lanjet Mock Exams 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest