Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa II Mock Examination 2021/2022

Share via Whatsapp

KISWAHILI LUGHA
Karatasi Ya 2

Maagizo

 • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili
 • Makosa ya sarufi na hijai yataadhibiwa

Maswali

 1. UFAHAMU (ALAMA 15)
  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuata.

  Ukame umetangazwa mara nyingi kuwa janga la kitaifa na serikali ya Kenya. Miaka nenda miaka rudi, Kenya imekumbwa na majanga mbali mbali. Linalosikitisha zaidi ni kwamba wakati wa msimu wa mvua mafuriko yanatokea katika maeneo mbali mbali ya nyanda za chini nchini. Mafuriko hayo yamesababisha vifo na uharibifu wa mali kwa kiwango kisichomithilika. Maji mengi yamekuwa yakisababisha mito na maziwa kuvunja kingo zake na watu wengi kufikwa na maafa. Cha hivi punde zaidi ni mto Tana uliovunja kingo zake na vilevile mafuriko katika kaunti ya Pokot Magharibi.

  Huku maji haya yakisababisha maafa. Wakenya wamekuwa wakiomba msaada misimu baada ya mingine. Miaka minane iliyopita, mama mmoja Kisumu alizua mdahalo mitandaoni kwa semi zake za "serikali tafadhali...saidia". Baada ya msimu wa mvua ni msimu kiangazi ambapo sasa habari za kusikitisha za vifo vya watu na mifugo hutokea kwa kutokea kwa ukame. Inaonekana Kenya imekosa mkakati maalum wa uhifadhi wa maji ili kusaidia wakati wa kiangazi.

  Kuna mambo mengi tu ya kulaumiwa kwa janga hili la ukame. Visa vya ufisadi vimeshuhudiwa nchini. Pesa zilizotengewa miradi mikubwa ya kuimarisha utoshelezaji wa vyakula zimefujwa na viongozi serikalini. Tazama mradi wa Galana Kulalu katika Puani ya Kenya. Ni mradi uliosifiwa kuimarisha uwezo wa Kenya wa kujilisha. Mabilioni ya fedha yalitengewa mradi huo. Hatima yake ni kukwama na kukosa kuwafaa Wakenya. Mingineyo ni miradi ujenzi wa mabwawa kama ya Kimwarer na Aror katika gatuzi la Elgeiyo Marakwet. Kama Kulalu, fedha zilitumika vibaya na hatimaye kukwamisha kuendelea kwake. Miradi hii ingejenga msingi ya unyunyiziaji wa maji na kuimarisha uwezo wa utoshelezaji wa vyakula. Visa vingi tu vya ufisadi vimesababisha maafa mengi kutokana na ukame. Mikono ya wanasiasa wengi ni mekundu kutokana na hali hii mbaya.

  Serikali na nchi fadhili zimekuwa zikiwapa Wakenya samaki badala ya kufunza kuvua. Huku kumezidisha viwango vya utegemezi nchini. Wakenya,badala ya kujifundisha kujistawisha katika utoajui wa lishe,wameishia kutegemea vyakula vya msaada. Ikumbukwe pia kwamba Kuna vipande vingi vikubwa vya ardhi visivyotumika. Vingine ni katika maeneo kame. Ikiwa miradi ya kutumia vipande hivi vya ardhi vingetumika kuendeleza ukulima. Hapa hatungelia ukame. Wakenya vilevile wamekuwa wakipanda mimea mmoja mmoja tu. Kutokeapo kiangazi wanashindwa kuwa na lishe ya kutosha. Wanapaswa kufundishwa kujihusishwa na mimea mingi ili kuwa na upana wa matumizi. Mimea mingine pia hushindwa kustahimili makali ya kiangazi kwa mrefu. Wakulima wanapaswa basi kuteua ile ambayo inaweza kustahimili hali hii.

  Uhifadhi wa vyakula unapaswa kuangaziwa upya. Bodi ya Kitaifa ya Uhifadhi wa Nafaka (NCPB) una uwezo mdogo wa kuhifadhi nafaka. Ili limesabisha Kenya kuendelea kuagiza nafaka kutoka nchi za nje kama Uhabeshi na Mexico wakati Wakenya wanavuna matani mengi ya mahindi na kuharibikia shambani wakati wa msimu wa mavuno. Wenye nacho vilevile wameteka nyara NCPB huku wakinunua mahindi mengi na kuuza pale na kuacha wakulima wakikadiria hasara ya kuharibika kwa nafaka shambani. Wala hai wamemeza usambazaji wa mbolea, mbegu na pembejeo nyingine za kilimo. Serikali inasambaza kwa bei iliyojaziwa ila huishia kuuza kwa wakula na kukosa kupunguza gharama ya uzalishaji. Hii inaishia kuwavunja moyo wakula. Wakulima wengine wametishia kung'oa mimea shambani kwa sababu ya tatizo kama hili.

  Kuna maeneo ambayo watu wamesema "si Kenya". Asili ya kauli kama hizi ni upungufu wa miundo msingi. Kule Kuna barabara mbovu ama hata kutokuwa na barabara kabisa. Kunapotokea kiangazi,hata usambazaji wa maji huwa ngumu. Usafirishaji wa vyakula kwa watu na mifugo ni mbaya. Taswira ambayo imekuwa ikichorwa ni ya ngamia,ng'ombe na hata punda waliokondeana na wengine waliogeuka kuwa mizoga. Hata mashirika ya kutoa misaada yanashindwa kuwafikia maskini Wakenya hao. Wengine wao wameshikilia itikadi za kale kama kufuga mifugo wengi ambapo patokeapo ukame hupoteza mamilioni ya pesa ukikadiri. Ni muhimu kuwaelimisha kubadili mwendo na kufuga wanyama wachache na kuanzisha mbinu zaidi ya moja ya ukulima. Hata hivyo, heri nusu shari kuliko shari kamili. Ni vyema hata kuchimba visima ili kutoa suluhu angalau kwa viwango kidogo vya kupata maji kuliko ndoto ya mabwawa ambayo imehama kutoka usiku mpaka kuwa ndoto ya mchana. Kenya haitalalamika kila wakati kuhusu ukame. Ni muhimu kujifunga kibwebwe kuukabili janga hili sugu. Tusipoziba ufa,tutajenga hukuta bila shaka.

  Maswali
  1. Ukirejelea kifungu fafanua njia mbili ambapo kinaya kimejitokeza waziwazi. (Alama 2)
  2. Eleza visababishi vinne vya ukame kama janga la taifa. (Alama 4)
  3. Fafanua athari zozote tatu za ukame nchini (Alam 3)
  4. Eleza mikakati minne inayoweza kuleta utoshelezaji wa vyakula nchini Kenya.(Alama 4)
  5.          
   1. Eleza maana ya kauli kuwa. “Mikono ya wanasiasa ni mekundu”. (Alama 1)
   2. Eleza maana ya" pembejeo " kama ilivyotumika katika utungo huu. (Alama 1)

 2. UFUPISHO (ALAMA 15)
  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali

  Kutokana na maendeleo ya teknolojia, dunia imejaa kila aina za maandishi, picha, michoro na kadhalika. Baadhi ya picha zinazopatikana katika vitabu, majarida, video na katika mitandao ya kijamii ni zile zinazoonyesha sehemu za siri za wanawake na hukusudiwa kuwasisimua wanaume kihisia. Picha hizi hupendwa sana na vijana; wavulana kwa wanume kwa ujumla. Si ajabu kuwakuta vijana katika mitandao wakitazama picha hzi kwa makini ajabu. Wengine hutumia pesa nyingi sana ili kununua video zilizojaa picha hizi chafu. Katika baadhi ya vyuo vikuu, tabia hii imekithiri. Utawapata wanafunzi wengi hasa wakati wa usiku wakitumia tarakilishi zao kutazama picha hizi na kuonyesha kuathiriwa moja kwa moja na wayatazamayo.

  Sinema hizi ni tatizo sugu katika jamii nan i lazima suluhisho la haraka litafutwe ili madhara yake yapunguzwe. Iwapo suluhisho halitapatikana basi kizazi hiki kitaangamia kutokona na athari za sinema hizi. Kulingana na utafiti uliofanywa na baadhi ya wataalamu wa kisaikolojia, sinema hizi huwa na madhara mengi kwa anayezitazama. Baadhi ya madhara haya ni kuwa picha hizi husababisha uraibu kwa mashabiki wazo. Hii ina maana kuwa wanaopenda kutazama picha hizi, mwishowe hujikuta wakinaswa na hamu kuu ya kutaka kuzitazama kila wakati. Hawawezi tena kujizuia. Iwapo watakosa kuzitazama hata kwa siku moja, wao hujihisi kana kwamba wanaumwa hadi watakapopata kitulizo-picha hizo. Uraibu huu ni ndwele kuu na lisilo na tiba. Wengine hujikuta kuwa wamepagawa na hawawezi tena kujizuia kihisia hadi watakapotazama kanda za sinema hizi chafu.

  Asilimia kubwa ya uhalifu wa kimapenzi hutokana na tabia ya kutazama picha hizi chafu. Jambo hili husababisha visa vingi vya ubakaji hasa wa watoto katika jamii. Ubakaji umekuwa ni tatizo kubwa katika nchi yetu. Kwa wakati mmoja jambo hili ovu lilimfanya Bi Njoki Ndung’u, akiwa mbunge maalum wakti huo, kupeleka mswada bungeni utakaohakikisha kuwa adhabu kali imetolewa kwa watakaopatikana na kosa la ubakaji. Hii ni kwa sababu ubakaji ni sawa na kumuua mtoto kwa sababu ni tendo la kinyama linalozamisha matumaini ya mtoto aliyebakwa katika kaburi la kuzimu. Ni juzi tu ambapo habari za kusikitisha za ubakaji ziliripotiwa wakati huu wa mgomo wa walimu ambapo wanaume wawili waliwanajisi wanafunzi watatu katika shule ya Manguo kule Limuru baada ya kutoka katika mashindano ya muziki wakiwa wamechelewa. Huenda wanaume hao ambao si walimu, waliathiriwa na sinema hizi.

  Ulawiti pia unasababishwa kwa kiasi kikubwa na tabia ya kutazama picha hizi chafu zinazohusu ngono. Ripoti za hivi punde zilionyesha kuwa mkoa wa Nyanza unaongoza katika tabia hii ya kusikitisha, ukifuatiwa na mkoa wa Pwani. Wanaume wengi hujiingiza katika uasherati na uzinzi kama njia moja ya kutekeleza waliyoyaona katika picha hizi za kuudhi. Wanapofanya hivyo, wao huhatarisha maisha ya wenzao kwa kujiingiza katika mtandao mkubwa wa kueneza magonjwa sugu ya zinaa kama vile ukimwi. Sinema hizi husababisha tabia ya kukera hasa miongoni mwa wavulana wetu ambapo wao hujaribu kujiridhisha kihisia na kimapenzi kwa kujiingiza katika kupiga pumyeto. Tabia hii ya kujisisimua ili kuhisi kana kwamba wanafanya mapenzi, in athari mbaya sana katika maisha yao ya baadaye.

  Picha hzi za ngono pia zinawadunisha wanawake kwa kaisi kikubwa sana. Zinawafanya kuonekana wakiwa watu duni na wasio na maana katika jamii. Wanaonekana sawa na wanyama kwa sababu wanyama hawana dhamiri inayowahukumu wanapofanya maovu. Wanyama hata hutembea ‘uchi’ lakini hawahukumiki. Sinema hizi zinatupa taswira ya mwanamke kuwa sawa na mnyama anayetembea uchi asiye na hisia zozote wala hana haya katika mambo yanayohusu usiri na sehemu za siri. Taswira hii ni mbaya kwa sababu mwanamke ni mwandamu aliye na hisia, heshima na anayeongozwa na sheria asilia kama mwandamu. Mwanamke ni kiumbe aliyeumbwa na Mungu na kupewa sifa za uungu katika maisha yake. Yeye si chombo wala si mnyama kama inavyoonyeshwa katika sinema hizi chafu za ngono.

  Dhuluma za kimapenzi zimesababisha kwa kaisi kikubwa na picha na sinema hizi za ngono zilizotapakaakatika mitandao na kwingineko. Ndoa nyingi siku hizi zinavunjika kiholela kwa sababu ya athari za sinema hizi. Taasisi ya ndoa imekosa umaarufu na staha yake kama ilivyokusudiwa na mwanzilishi wa ndoa, Maulana. Wanaume wengi wanapotazama sinema hizi, ambazo kwa kiwango kikubwa hufanywa na watu waliotamauka maishani au wanaotumia dawa za kulevya na kusisimua hisia zao, wanasahu uhalisia huo. Wafikapo katika ndoa zao wanatarajia kuwa wake zao watafanya tendo hilo la kimapenzi kwa kiwango sawa na kusisimua hisia kama wafanyavyo wale wa video au kanda. Jambo hili husababisha misukosuko katika ndoa. Wanawake wengine huamua kutalikiana. Talaka inapobisha, watoto wasio na hatia ndio huteseka na kuishi maisha ya kusonona.

  Ni wajibu wa kila mmoja wetu kupiga vita tatizo hili linalokumba jamii yetu. Wanaohusika na shughuli hizi za kuweka picha na sinema hizi katika mitandao, vitabuni, katika majarida, katika kanda na kwingineko lazima waangalie madhara ya sinema hizi kuliko kuangalia fedha wanazovuna katika biashara hii. Ni matumaini yetu kuwa mambo haya yataangaliwa kwa jicho la mwewe ili taasisiya ndoa iimarike zaidi na iwe mahali salama pa watoto wetu kufurahia wanapokua.

  1. Bila kupotosha maana fupisha aya za kwanza na mwisho kwa maneno yasiyozidi 70. (alama 7)
   Matayarisho
   Nakala Safi
  2. Eleza kwa kina madhara ya sinema chafu kwa maneno yasiyozidi 80. (Alama 8)
   Matayarisho
   Nakala Safi
 3. MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)
  1. Andika maneno yoyote yanayoanza kwa sauti zifuatazo: (al. 2)
   1. kitambaza na irabu ya chini 
   2. kizuiwa ghuna cha masine na kikwamizo hafifu cha koromeo 
   3. kiyeyusho cha midomo na irabu ya nyuma wastani
   4. kimadende na irabu ya mbele juu
  2. Tambua kiimbo: Askofu alimwomba radhi kakake kwa kumkosea heshima. (al.2)
  3. Andika maneno yaliyo na muundo ifuatayo. (al. 2)
   1. kiambishi cha umoja, mzizi, kiishio -o-
   2. kirejeshi, kiambishi cha mahali ………………………………………………………...
  4. Unganisha sentensi ifuatayo ili kuunda sentensi ya masharti:Wanasayansi watatabiri mapema. Wanasayansi watafaulu kuondoa majanga. (al. 2)
  5. Tunga sentensi kwa kutumia nomino kama kivumishi. (al.2)
  6. Andika sentensi inayoanza kwa kiima na kukamilika kwa kiarifu. (al. 2)
  7. Badilisha shamirisho kitondo kuwa shamirisho kipozi kwa kuandika sentensi upya: Mtoto wa Rosa amefundishwa virai kwa kutungiwa sentensi za virai. (al.2)
  8. Tunga sentensi yenye kirai nomino, kirai kitenzi na kirai kielezi. (al.3)
  9. Andika katika hali ya ukubwa: Kitabu ambacho kinauzwa kwenye duka hili kinavutia.(al.3)
  10. Kanusha: Mtoto hucheka sana akila. (al. 1)
  11. Akifisha: Jichunge akasema Musa msimamo wako unaweza kuwaathiri vibaya. (al. 2)
  12. Changanua kwa jedwali:Alichoka sana alipokuwa akifanya mazoezi uwanjani jana. (al. 4)
  13. Tunga sentensi mbili kudhihirisha maana mbalimbali za neno katia. (al. 4)
  14. Andika vinyume vya maneno yaliyopigiwa mstari: Msomi jasiri hujitahidi katika masomo yake. (al. 2)
  15. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo: Kila darasa likipunguza kiwango cha kelele idadi ya wanafunzi wanaofaulu itaongezeka. (al. 2)
  16. Tumia ‘ki’ katika sentensi kuonyesha: (al. 2)
   1. kitenzi kishirikishi
   2. masharti
  17. Onyesha uamilifu wa viambishi katika: Walilana (al. 2)
  18. Tofautisha aina mbili za mofimu. (al 1)

 4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
  Soma kifungu kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuatia.

  Waziri Mkanga alisema kuwa vipakatalishi vitaboresha mafunzo na kuzidisha kasi ya wanafunzi kupata maarifa. Alikuwa akiwahutubia wakuu wa vitengo mbalimbali katika idara ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano. Alikariri kuwa watoto ambao ni wazito kuelewa wataweza kujifanyia udurusu nyumbani na hivyo kuwainua kielimu. Aidha, alisema kuwa mradi huu ulikuwa tunu ya kipekee kwa kizazi cha kesho. Alisema kuwa matumizi ya vipakatalishi ndiyo yatakayowaandaa vijana kwa ajili ya kufanikisha ruwaza ya 2030.
  1. Kifungu hiki kinatokea katika muktadha gani? (alama 1)
  2. Fafanua mbinu za uwasilishaji ambazo msemaji angetumia ili kufanikisha uwasilishaji. (alama4)
  3. Pendekeza mikakati yoyote tano inayoweza kuzingatiwa na washikadau mbalimbali ili kuimarisha Kiswahili nchini Kenya. (alama 5)

Mwongozo wa kusahihisha

 1. Ufahamu
  1. Kwa nini ukame ulitangazwa kuwa janga la kitaifa? (Alama 2)
   • Kwa sababu ukame ulikuwa umesababisha maafa ya kitaifa (vifo vya watu na wanyama).
    (2X1)

  2. Fafanua njia mbili ambapo kinaya kimejitokeza wazi wazi. (Alam 2)
   • Ni kinaya kwa mafuriko kusababisha maafa ilhali baada ya hapo kunatokea ukame/uhaba wa maji.
   • Ni kinaya kwa viongozi kuuza pembejeo zilizolipiwa na serikali.
   • Ni kinaya kwa viongozi kununua mahindi na kuuzia NCPB.
    (2×1)

  3. Jadili kauli kuwa "mikono ya wanasiasa ni mekundu". (Alama 1)
   • Kwa sababu walifuja fedha zilizotengewa ujenzi wa mabwawa.

  4. Eleza mikakati inayoweza kuleta utoshelezaji wa vyakula nchini Kenya. Alama 4)
   • Ujenzi wa mabwawa ya unyunyiziaji wa maji.
   • Wakenya kutumia vipande vya ardhi visivyotumika.
   • Wakenya kupanda mimea inayostahimili kiangazi.
   • Serikali kuimarisha uhifadhi wa nafaka baada ya mavuno/upanuzi wa NCPB.
   • Kuimarishwa kwa miundo msingi kama vile barabara ili kuimarisha usambazaji wa mbolea/mbegu au mavuno/maji.
   • Kuchimba kwa visima. (4X1)

  5. Eleza maana ya kauli ifuatayo kama ilivyotumika kifunguni "...si Kenya"(Alama 1)
   • Upungufu wa miundo msingi kama vile barabara katika maeneo haya. (1X1)

  6. Eleza maana ya" pembejeo " kama ilivyotumika katika utungo huu. (alama 1)
   • Ni vifaa vya ukulima kama vile mbolea na mbegu. (1X1)

 2.      
 3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
  1. Andika maneno yoyote yanayoanza kwa sauti zifuatazo: (al. 2)
   1. kitambaza na irabu ya chini /la/
   2. kizuiwa ghuna cha masine na kikwamizo hafifu cha koromeo /dh/
   3. kiyeyusho cha midomo na irabu ya nyuma wastani /wo/
   4. kimadende na irabu ya mbele juu /ri/

  2. Tambua kiimbo katika sentensi zifuatazo (al.2)
   Askofu Askofu alimwomba radhi kakake kwa kumkosea heshima.
    • taarifa

  3. Andika maneno yaliyo na muundo ifuatayo. (al. 2)
   1. kiambishi cha umoja, mzizi, kiishio -o- mnato
   2. kirejeshi, kiambishi cha mahali ambako/ambapo/ambako

  4. Unganisha sentensi zifuatazo ili kuunda sentensi ya masharti. (al. 2)
   Wanasayansi watatabiri mapema. Wanasayansi watafaulu kuondoa majanga.
   • Wanasayansi wakitabiri mapema watafaulu kuondoa majanga.

  5. Tunga sentensi kwa kutumia nomino kama kivumishi. (al.2)
   • Askari vijana waliwaachilia majambazi sugu.
  6. Andika sentensi inayoanza kwa kiima na kukamilika kwa kiarifu. (al. 2)
   • Yeye amefaulu kusoma gazeti baada ya wiki moja.

  7. Badilisha shamirisho kitondo kuwa shamirisho kipozi kwa kuandika sentensi upya. (al.2)
   Mtoto wa Rosa amefundishwa virai kwa kutungiwa sentensi za virai.
   • Rosa amefundishwa virai kwa kutungiwa sentensi za virai.

  8. Tunga sentensi yenye kirai nomino, kirai kitenzi na kirai kielezi. (al.3)
   • Juma ameandika kitabu cha mabepari vizuri sana.

  9. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa. (al.3)
   Kitabu ambacho kinauzwa kwenye duka hili kinavutia.
   • Jitabu/tabu ambalo linauzwa kwenye jiduka hili linavutia.

  10. Kanusha: Mtoto hucheka sana akila. (al. 1)
   • Motto hacheki sana akilia.

  11. Akifisha Jichunge akasema Musa msimamo wako unaweza kuwaathiri vibaya. (al. 2)
   • “ Jichunge !” Akasema Musa , “ msimamo wako unaweza kuwaathiri vibaya sana.”
  12. Changanua kwa kutumia jedwali. (al. 4)
   Alichoka sana alipokuwa akifanya mazoezi uwanjani jana.

       S    
   KN  KT       
   T E Ts T N E E
   Ø  Alichoka sana alipokuwa akifanya mazoezi​ uwanjani jana
  13. Tunga sentensi mbili kudhihirisha maana mbalimbali za neno katia. (al. 4)
   • Kaka alikatia dada kipande cha muwa tamu. (dhana ya kwa ‘niaba ya’)
   • Fundi alikatia kisu kipande cha nguo. (matumizi ya ala)

  14. Andika vinyume vya maneno yaliyopigiwa mstari. (al. 2)
   • Msomi jasiri hujitahidi katika masomo yake.
    Jasiri – mwoga hujitahidi – huzembea

  15. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo. (al. 2)
   • Kila darasa likipunguza kiwango cha kelele idadi ya wanafunzi wanaofaulu itaongezeka.
   • Kila darasa likipunguza kiwango cha kelele – kishazi kitegemezi
   • idadi ya wanafunzi wanaofaulu itaongezeka – kishazi huru

  16. Tumia ‘ki’ katika sentensi kuonyesha: (al. 2)
   • kitenzi kishirikishi - kitabu ki mezani
    masharti – mtoto akila vizuri afya yake huimarika

  17. Onyesha uamilifu wa viambishi katika: (al.2)
   Walilana
   • Wa- nafsi li- wakati uliopita an- kauli ya kutendana a- kiishio

  18. Tofautisha aina mbili za mofimu. (al 1)
   • Mofimu huru – ni mofimu iliyo na maana kamilifu
   • Mofimu tegemezi – ni mofimu ambayo hutegemea mofimu nyingine ili kuleta maana.

 4. Isimu Jamii
  1. Kikao cha wanataaluma – taaluma ya teknolojia ya habari na mawasiliano
  2.          
   1. Matumizi ya viziada lugha kama vile miondoko ya mwili, ishara za nyuso nk.
   2. Kurudia masuala muhimu kwa minajili ya kusisitiza.
   3. Matumizi ya toni mwafaka anaporejelea masuala mbalimbali. Toni ilingane na kinachorejelewa.
   4. Awashirikishe wahusika kwa kuwauliza maswali
   5. Matumizi ya lugha ya kushawishi ili matumizi ya vipakatalishi yakubalike.
   6. Matumizi ya tasfida pale inapohitajika.

  3. Pendekeza mikakati yoyote tano inayoweza kuzingatiwa na washikadau mbalimbali ili kuimarisha Kiswahili nchini Kenya. (alama 5)
   • Serikali ifanye juhudi kuwaajiri walimu zaidi wa Kiswahili.
   • Walimu wazingatie utaratibu ufaao wa kufundisha lugha ya Kiswahili.
   • Vyombo vya habari vitumie lugha sanifu ya Kiswahili katika vipindi vyao ili kukikuza Kiswahili.
   • Walimu wa Kiswahili wajibidiishe kuwa kielelezo chema katika kutumia Kiswahili.
   • Viongozi wahamizwe kutumia lugha sanifu katika mawasiliano yao na umma.
   • Shule ziwe na sera nzuri katika shule za kuhimiza matumizi sawa ya Kiswahili.
   • Wataalam waandike vitabu vya Kiswahili kwa wingi.
   • Watafiti wafanye utafiti wa kutosha katika nyanja ya sayansi na kuteknolojia ili kuwepo msamiati mwafaka.
   • Watafsiri watafsiri msamiati wa kitaaluma katika lugha ya Kiswahili.
   • Serikali itafsiri nakala zote rasmi kwa lugha ya Kiswahili – watu wakubaliwe kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zote rasmi za kiserikali kama vile kujaza fomu za kazi. nk.

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa II Mock Examination 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest