Kiswahili Paper 2 Questions - Maranda Mocks 2021/2022 Exams

Share via Whatsapp

KISWAHILI (LUGHA)
Karatasi ya 2

Maagizo

  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  • Majibu yote sharti yaandikwe katika nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali. (f) Usitoe ukurasa wowote kutoka kwenye kijitabu hiki.

Maswali

  1. UFAHAMU (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    “Mabibi na mabwana, ndugu wapenzi, alianza Bi. Mkesha, “Huu ni mwaka wa tano tangu tufanye uchaguzi mkuu uliowapa vigoda wenzetu hawa. Katika kipindi hiki kumetokea mengi ya kujipigia kidari, pametokea pia mengi, mengi mabaya ya kuitia jamii ya Tungama izara. Tumejipa mkono wa tahania kwa uteuzi wetu mzuri. Vilevile tumejisuta kwa uteuzi usio wa kuridhisha.

    Ndugu wapenzi, sina haja ya kuwakumbusha yote ambayo tumepitia; mmeyashuhudia yote. Ila ninayotaka kusema ni kwamba malengo yetu ya kuwateua viongozi yamesalitiwa. Ndugu zangu, itakumbukwa kwamba watangulizi wetu walianza safari ya kurejesha utu wa Mwafrika wakiwa na nia thabiti ya kuwabwaga maadui watatu wa maendeleo. Je, mnawajua maadui hao? Ni ujinga, magonjwa na umaskini. Waanzilishi wa taifa hili, pamoja na viongozi waliowafuata walipigania huduma za bure za afya, na elimu ya bure na ya lazima kwa wote. Vijana wetu walijitoma ugani kuzamia lulu ya elimu; wakavidhihaki vitabu hadi kufikia kilelecha cha elimu. La kusikitisha ni kwamba elimu hii imekuwa laana kwao. Mnajua kisa na maana ya hali hii? Natija iliyotarajiwa haikupatikana. Na haya si mageni kwetu. Mnajua wapo vijana humu vijijini ambao wamepiga lami kwa miaka na mikaka bila kuambulia kazi za hadhi ambazo waliahidiwa huko vyuoni. Hatimaye hawa hawa wenye shahada mbili, na wengine hata tatu, ndio wanaokuwa matarishi wa wale ambao walichechemea masomoni. Vijana wengine, kwa kukosa hata huo utarishi, wameamua kuanzisha biashara rejareja ili kujikimu; wamekosa la mama, wanaamwa la mbwa. Sina haja ya kuwafafanulia kiini cha hali hii ya kutamausha.

    Ni dhahiri kwamba uthabiti wa taifa lolote lile hutegemea uthabiti wa uongozi, na uaminifu wa raia wake katika kuuwajibisha huo uongozi. Hata hivyo, inasikitisha kwamba wengi wetu tumejipoka uwezo wa kuuwajibisha uongozi kwa kuwa mawindo rahisi ya uzungukaji mbuyu. Huu ndio uwele ambao umeufisidi utu wetu na kutusahaulisha thamani za kitaifa. Hebu niambie ewe mama mwenzangu, kuna faida gani kuuza kura yako kwa kibaba cha unga na noti ya shilingi mia moja, ati kwa kuwa unaambiwa, ‘Ukinichagua nitahakikisha kwamba ile Affirmative Action imezingatiwa?’ Ipo haja gani kuchomwa na jua ukiwafuata hawa hawa viongozi, ukiwaimbia nyimbo za kuwatia raia kichaa cha shangwe ili kuwapembeja wawapigie kura? Je, faida kwako imekuwa gani? Hujangojea kwa kipindi chote hiki kusakafiwa kwa hiyo barabara uliyoahidiwa siku ulipouza kura yako? Na ile ahadi ya ‘mwenzetu’ ya kuwaajiri vijana wetu kwenye Jeshi la Wanamaji imetimia? Hatujashuhudia watu wa akraba moja wakisombwa kutoka humu kijijini kwenda kuchukua nyadhifa katika mashirika ya umma?”

    “Kweli waso haya wana mji wao, Bi. Mkesha amejikosha kweliweli,” Bi. Kuli alimwambia mwenzake Bi. Kengemeka kisha akaendelea.” Anatuambia yepi mageni ambayo masikio haya yangu yaliyokula chumvi ya miongo sita ushei ya miaka hayajasikia?”

    “Anasema tumpe nafasi ajitome kwenye uwanja wa majogoo,” akajibu Bi. Kengemeka, “Atakuwaje tofauti na hao wanaume?” Hata hao wanawake tumewahi kuwapa nafasi, wakatutenda zaidi ya wanaume. Usinikumbushe kura yangu niliyoipoteza kwa kumkweza Bi. Shali kwenye usukani. Siwezi kusahau namna ile ahadi ya maji ya mabomba na kuchimbwa kwa visima ilivyoishia kwenye kauli yake tu.”

    “Tumetendwa sote mwenzangu,” alisema Bi. Kuli, “Inasikitisha kwamba dau la masomo ya wanangu limeenda mrama huku nikimlilia huyo huyo Bi. Shali. Kila mara tunasikia kupitia vyombo vya habari kwamba serikali imeanzisha Hazina ya Eneobunge kuyafadhili masomo ya watoto kutoka familia maskini. Lengo kuu, nasikia, ni kuhakikisha kwamba asilimia kubwa ya watoto haipati fursa ya kujiunga na shule tu, bali pia inakamilisha masomo. ‘Hata hivyo, huu ni mwaka wa tatu tangu wanangu watatu waache masomo kutokana na ukosefu wa karo. Na usidhani ni karo ya shule ya kitaifa, la, hasha! Ni karo ya shule za kutwa ambapo niliwapeleka baada ya huyu huyu Bi. Shali kunitilia huku akinitolea huko kuhusiana na ufadhili wa masomo.”

    “Usinikumbushe yaliyomfika mwanangu Neema,” alisema Bi. Kengemeka huku akitwaa ukingo wa kanga yake kujipangusa machozi. “Mwana huyu alikaa nyumbani kwa muhula mzima,” akaendelea Bi. Kengemeka, “Dhiki ya kuwaona wenzake wakienda shuleni huku yeye anabaki nyumbani ikamfanya kuwa windo rahisi la mmoja wa hao wabunge, akaambulia uja uzito ambao hakuulalia wala kuuamkia. Mwenyewe mbunge ameshika hamsini zake kana kwamba hakufanya lolote. Mwanangu Jabali naye amehiari kuwa kibarua katika shamba la mbunge wa sasa. Mwenyewe anasema anataka kudunduiza pesa ili arudi shuleni kukamilisha mwaka wake wa mwisho. Na usidhani ni hao wangu tu waliofikwa na ya kuwafika. Tumewaona wana wa wenzetu tuliopiga foleni pamoja kuwateua hao hao wabunge, wakitumiwa kama masoko ya dawa za kulevya. Wengine wamegeuzwa walanguzi wa dawa hizi,” Bi. Kengemeka alikamilisha uzungumzi wake na kushusha pumzi kana kwamba ameutua mzigo mzito.

    Hata hotuba ya Bi. Mkesha ilipofikia ukingoni, Bi. Kuli alimwambia mwenzake, “Ninavyoona ni kwamba wanasiasa wote wamefınyangwa kutoka aina sawa ya udongo. Ikitokea kwamba tutampa huyu Bi. Mkesha kura, tumpe kwa kulazimika kikatiba kupiga kura; tusiwe na matarajio makuu. Inasikitisha kwamba vijana wetu waadilifu hawataki kujitia najisi kwa kuingilia siasa. Yule kijana wetu Angaza angekubali rai ya wazee kujitoma ukingoni tungemuunga mkono.

    1. “Malengo yetu ya kuwateua viongozi yamesalitiwa.” Thibitisha kauli hii kwa kurejelea hoja sita kutoka kwenye taarifa. (alama 6)
    2. Eleza mchango wa wanyonge katika hali ya uongozi nchini Tungama. (alama 3)
    3. Bainisha mbinu nne ambazo Bi. Mkesha anatumia kuishawishi hadhira yake. (alama 4)
    4.            
      1. Andika kisawe cha, ‘kuwapembeja’ kwa mujibu wa taarifa. (alama 1)
      2. Andika maana ya, ‘amejikosha’ kulingana na taarifa. (alama 1)
  2. UFUPISHO (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

    Hamadi alianza matumizi ya dawa za kulevya akiwa kidato cha tatu. Aliyemtanguliza kwa matumizi ya mihadarati ni ‘rafiki’ yake; waliyesakini naye kwenye bweni moja. Hapo awali, alikataa lakini hatimaye akaona kuwa lilikuwa wazo zuri kuzitumia. Hamadi alikuwa mvulana mwerevu; alifanya vyema katika mitihani yote na kuwafanya walimu wake kuterema. Matokeo yake yalianza kudorora alipoanza kutumia dawa za kulevya.

    Wakati wa Hamadi kujiunga na chuo kikuu ulipowadia, alikuwa mraibu wa dawa za kulevya tayari kiasi cha kuhitaji matibabu. Uraibu wake ulipokithiri, alianza kuwaibia wenzake ili apate hela za kununua dawa hizi. Kutokana na hali hii, masomo yalimwia vigumu; akawa anadorora kimasomo. Dawa hizi zilimwathiri kihasi kiasi cha kutohudhuria mihadhara. La kustaajabisha zaidi ni kuwa angekosa kufanya mitihani; si mijarabu si ya mwisho wa semesta. Hatimaye, wasimamizi wa chuo kikuu walisema kuwa uraibu wake ulikuwa umepita mipaka na hangeimudu elimu ya chuo kikuu; kwa hivyo, hakukubaliwa kuendelea na elimu ya chuo kikuu.

    Baada ya kufukuzwa chuoni, Hamadi alitamauka. Alijitenga na aila yake kwa muda: hakujua awaeleze vipi wazazi yaliyomsibu. Baada ya kuiondokea familia yake, hakufanikiwa kupata mtu wa kukidhi mahitaji yake ya kila siku kama ilivyokuwa kawaida yake alipoishi na wazazi wake. Alipokata tamaa, aliamua kwenda mtaani na kuwa ombaomba. Hatimaye aligeuka na kuwa mporaji na mwizi sugu madukani mwa watu katika mji wa Hatari. Siku zake arobaini zilipofika, Hamadi alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani.

    Hamadi aliachiliwa huru mwaka uliopita; ninapoandika taarifa hii, anajaribu kujitenga na uraibu wa dawa za kulevya. Yeye humwona mshauri wa waraibu wa dawa za kulevya mara mbili kila wiki. Aidha yeye hujaribu kutangamana na familia yake, marafiki na hata watu wa nasaba yake. Hapo awali, wazazi wake walikuwa wamekufa moyo kutokana na mienendo yake potovu, lakini sasa wamepata matumaini baada ya mwanao kutembelea kituo cha ushauri-nasaha. Wamekubali kuwa Hamadi ni mgonjwa anayeendelea kupokea matibabu. Wameipa hamnazo kauli kuwa Hamadi alijidunga mwiba wa kujitakia.

    Alipokuwa mraibu wa mihadarati, Hamadi alitengana na wazazi wake na kujihisi mpweke. Aliishi katika dunia yake. Aghalabu alikuwa mpyaro na mwenye rabsha. Sasa ni karimu na mwenye utu. Yeye huwasiliana na familia yake na hujaribu awezavyo kutangamana na marafiki zake. Ili kuweza kupata nafuu kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, Hamadi ameamua kufanya mambo matatu.

    Kwanza, ameamua kujiamini. Amekubali kuwa alikuwa mraibu wa dawa za kulevya na kwamba matumizi ya dawa za kulevya ni ya kihisia kama ilivyo hali nyingine yoyote inayohitaji matibabu. Amegundua kuwa hali ya kutokubali kuwa alikuwa mraibu wa dawa za kulevya ni sawa na kukataa kukabiliana na uhalisia. Ni kukataa ukweli, kumeza mrututu; na ni kama kupinga wanavyosema wajuao kuwa , ukweli unapodhihiri uongo hujitenga.

    Pili, ametambua kuwa pana haja ya kuwa na mwelekeo chanya kujihusu. Lazima ajione kama kiumbe mwenye maana, aliyehulukiwa na Maulana ili atekeleze wajibu wake ulimwenguni. Ameamua kujiona kama mmoja wa wanajamii muhimu; na kwamba jamii inahitaji mchango wake.

    Tatu, Hamadi amekata shauri kujihusisha na kazi yenye manufaa. Ameamua kutafuta ajira hata kuanzisha mradi utakaompa mtaji. Ikiwa hatafanikiwa kupata ajira, amepiga moyo konde kuanzisha ukuzaji wa nyanya na vitunguu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wazazi wake wana shamba kubwa kwao kitongojini. Hoja ni kuwa hafai kupiga zohali. Kwa mujibu wa maadili ya kijamii, ni vyema kufanya jambo moja au mawili yenye manufaa kuliko kukaa ovyo.

    Watu wengi katika jamii wamejifunza kumkubali na kumkaribisha kwa mikono miwili kama mtu aliyebadilisha mienendo yake potovu. Ukweli ni kuwa, uraibu wa dawa za kulevya ni hali ya kuhatarisha maisha lakini wahasiriwa wanaweza kubadilika na kuwa bora zaidi. Jamii ina jukumu la kumsaidia mraibu wa dawa za kulevya kubadilisha mienendo yake. Kuna yeyote anayejua Hamadi atakuwa mtu wa aina gani hapo kesho?

    1. Fupisha ujumbe wa aya tatu za mwanzo kwa maneno 85 (alama 7, 1 ya mtiririko)
      Matayarisho
      Jibu
    2. Bila kupoteza maana, eleza mawazo makuu yanayojitokeza katika aya sita za mwisho kwa maneno 100. (alama 8, 1 ya mtiririko)
      Matayarisho
      Jibu
  3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
    1. Andika maneno yenye miundo ifuatayo: (alama 2)
      1. nazali ya ufizi, mtuo ghuna wa kaakaa laini, irabu ya mbele wastani, kitambaza, irabu ya juu mbele
      2. kipasuo-kwamizo cha kaakaa gumu, irabu ya kati chini, irabu ya mbele juu
    2. Andika maneno yenye viambajengo vifuatavyo: (alama 2)
      1. nafsi ya pili umoja, wakati uliopo hali ya kuendelea, kirejeshi ngeli ya I-ZI wingi, mzizi, kiishio
      2. umoja (ngeli ya A-WA), mzizi, kiishio
    3. Fuata maagizo:
      1. Ziunganishe sentensi zifuatazo kuunda sentensi moja ikiwa katika hali ya kutendeshana. (alama 1)
        Nakusomesha
        Wanisomesha
      2. Unda sentensi moja changamano inayoanza kwa kiunganishi kutokana na sentensi hizi sahili. (alama 2)
        Ushairi huwavutia wengi.
        Ushairi huchukuliwa kuwa mgumu.
      3. Andika sentensi ifuatayo upya ukibadilisha vitenzi vilivyopigiwa mstari kuwa nomino na kivumishi mtawalia. (alama 2) Alizawidiwa kwa kupewa nazi iliyoharibika.
      4. Ainisha nomino katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
        Mamake ndiye aliyeandika ‘Darubini ya Sarufi’.
    4. Andika kinyume cha maneno yaliyopigiwa mstari . (alama 2)
      Mvua ikinya tutapanda mahindi.
    5. Bainisha vielezi vilivyotumika katika sentensi hii. (alama 2)
      Mwalimu anayevaa kinaijeria alituelezea kinagaubaga.
    6. Tunga sentensi ukitumia kihusishi cha a- unganifu kuibua dhana ya umilikaji katika ngeli ya LI-YA (umoja). (alama 2)
    7. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mstari. (alama 2)
      Babu, nyanya na shangazi walinunuliwa jozi za viatu na mnuna wangu.
    8. Andika katika umoja: (alama 2)
      Mashangingi hayo yalisimama kwenye barabara hizo na kuwafanya madereva wengine kuudhika.
    9. Kanusha kauli ifuatayo: (alama 2)
      Hivi ndivyo vitabu mnavyotaka.
    10. Tunga sentensi moja ambayo imetumia kishazi kitegemezi kirejeshi ambacho ni kiwakilishi. (alama 2)
    11. Eleza maana za sentensi zifuatazo ukizingatia kiakifishi (,) (alama 2)
      1. Hamadi, anasema atauza nyumba yake.
      2. Hamadi anasema, atauza nyumba yake.
    12. Igeuze sentensi ifuatayo iwe katika wingi. (alama 1)
      Nikimjengea ua huu, ataweza kupata ulinzi wa kutosha.
    13. Andika ukubwa wa: (alama 2)
      Mtoto alimuua nyoka mdogo kwa kumpiga kichwani.
    14. Andika sentensi ifuatayo katika usemi halisi. (alama 2)
      Safia alitaka kujua kutoka kwa mama yake kama wangeenda kuwatembelea wazazi wao siku hiyo.
    15. Ainisha sentensi hii kidhamira. (alama 1)
      Mlinzi akikuona ukirukia hapa atakuzuia.
    16. Bainisha vipengele ulivyopewa mabanoni katika sentensi zifuatazo:
      1. Huyu ndiye mwalimu wetu wa Kiswahili. (kijalizo) (alama 1)
      2. Baba yake amekatiwa mti wa mvule kwa shoka. (yambwa) (alama 2)
    17. Mohammed alifuzu mtihani huo vizuri kwa sababu alisoma kwa bidii. (alama 2) (Maliza kwa …mtihani huo vizuri)
    18. Mtu ambaye ameharibika kitabia kisha kuwaathiri watu wengine wanaohusiana naye huambiwa methali gani? (alama 1)
    19. Numbi ni kwa samaki ilhali ………………….kwa maua na …………………..kwa makaa. (alama 1)
  4. ISIMUJAMII (Alama 10)
    Wewe ni Rais wa Jamhuri ya Angaza. Umealikwa na Rais wa Jamhuri ya Nuru kuhudhuria sherehe ya Uhuru na kutoa hotuba kama Mgeni wa Heshima. Fafanua sifa kumi za lugha utakayotumia.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions - Maranda Mocks 2021/2022 Exams.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest