Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Lanjet Joint Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

MAAGIZO KWA MTAHINIWA:

  • Karatasi hii ina sehemu tano: A, B, C, D na E.
  • Jibu maswali manne pekee. Kila swali lina alama ishirini.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Chagua maswali mengine yoyote matatu kutoka sehemu zilizosalia; B, C, D ama E.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.

SEHEMU YA A
USHAIRI

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali:

    UMOJA WA MENDE            
    Wadogo tena wadudu, ila wajua kuvuna, wasikokupanda,
    Wakija utawabudu, kwa sura tunafanana, wanavyojipenda,
    Nyoyo zidunde dududu! Watabaki kujibana, waje kukuponda,
              Mende wanao umoja, waonapo pana lishe.

    Huja usiku usiku, waja wanapojilaza, wasionekane,
    Huwacha yao shauku, ila wanapeleleza, wasijulikane,
    Wametafuna mabuku, akili wamezijaza, nd’o tusiwaone,
               Mende wanao umoja, waonapo pana lishe.

    Wao ni kama mapanya, huuma kipulizia, kukutulizisha,
    Wanapenda kudanganya, huku mejinyamazia, kukupofuzisha,
    Usiwaone waminya, kwa kutukandamizia, kwani wanachosha,
                 Mende wanao umoja, waonapo pana lishe.

    Wao huja taratibu, kwa vipindi vya misimu, vijulikanavyo,
    Hurudi bila aibu, vitano vikishatimu, tuwapendezavyo,
    Wakatutia ububu, kutulisha na vya sumu, watuongozavyo,
                 Mende wanao umoja, waonapo pana lishe.

    Tumbo lake la kiriba, tayari limeshashiba, linamusokota,
    Lataka tena kushiba, wenye nyumba tuna tiba, tutamuokota,
    Wakishatupa kibaba, kina mama kwa wababa, si tunajitata,
                   Mende wanao umoja, waonapo pana lishe.

    Mwishowe tunafungua, apite akaingie, ndani kabatini,
    Humo mlimo murua, twataka atuchungie, vyetu vya thamani,
    Mwishowe anararua, ndani amejifungie, wamtakiani?
                    Mende wanao umoja, waonapo pana lishe.

    Hubeba na familia, wana na bibi za kwake, wale kwa pamoja,
    Nasi tukivumilia, kufikike kule kwake? Ng’o! sekunde moja,
    Hadi ije kufikia, kuosha kabati lake, hapa tu pamoja,
                    Mende wanao umoja, waonapo pana lishe.

    Kachukuwe yake dawa, mende tukawakatae, tukawafukuze,
    Tuseme tunazo mbawa, nd’o mende tuwakomee, siye tujikuze,
    Tuwang’atue machawa, tuseme tuondokee, tukawachukize,
                     Mende na wao umoja, tuje wapa redikadi.
    (Kutoka: Meja S. Bukachi – Diwani ya Kupe)

    MASWALI
    1. Tambua mende wanaorejelwa na mshairi. (Alama 1)
    2. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili. (Alama 1)
    3. Nani nafsi nenewa katika shairi hili? (Alama 1)
    4. Taja tamathali za lugha zilizotumika katika shairi hili. (Alama 2)
    5. Fafanua uhuru wa ushairi alioutumia malenga. (Alama 2) 
    6. Weka shairi hili katika bahari mbalimbali. (Alama 3)
    7. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (Alama 4)
    8. Tambua mambo manne anayolalamika nafsi neni kuhusu mende. (alama 4)
    9. Vifungu vifuatavyo vina maana gani katika shairi? (alama 2) 
      1. vitano vikishatimu
      2. Tuwang’atue machawa

SEHEMU YA B
RIWAYA: CHOZI LA HERI

(Assumpta K. Matei)
Jibu swali la Pili au la Tatu

  1. “Lakini itakuwaje historical injustice, nawe Ridhaa hapo ulipo sicho kitovu chako?”
    1. Eleza muktadha wa maneno haya. (Alama 4) 
    2. Tambua mbinu mbili za lugha zilizotumiwa katika dondoo hili. (Alama 4)
    3. Eleza umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya. (Alama 4)
    4. Ni mambo gani yaliyowakumba walioishi penye kitovu kisicho chao? (Alama 8)
      Au
  2.  
    1. “Jamii ya Chozi la Heri imeoza.” Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa mifano ya kutosha kutoka katika riwaya ya Chozi la Heri. (Alama 10)
    2. Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo:
      Lakini baba, sijasema tunataka kiongozi mwanamke. Sisi tunataka kiongozi yeyote, awe mwanamke au mwanamume, atakayeweza kulielekeza jahazi hili letu kwenye visiwa vya maendeleo. Pale tutakapoafikia Malengo ya Kimaendeleo ya Kimilenia.kiongozi ambaye ataendeleza juhudi za kukabiliana na wale maadui ambao wewe daima huniambia kuhusu: umaski, ujinga na magonjwa, (akisita kumtazama baba) uhaha wa nafasi za kazi na ufisadi. Je, huu sio uliokuwa muono wa waliopigania uhuru? Siyo ambayo viongozi waliochukua hatamu za uongozi kutoka kwa watu weupe waliyofanya juu chini kutekeleza?

SEHEMU YA C
TAMTHILIA: KIGOGO
(Pauline Kea)

  1. “Wewe nawe hukualikwa. Wataka kutia siasa tayari? Hamkosi kutia doa kila jambo zuri.” 
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Alama 4)
    2. Eleza vipengele viwili vya kimtindo alivyotumia msemaji kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. (Alama 2)
    3. Fafanua sifa nne za anayeambiwa maneno haya. (Alama 4)
    4. Fafanua jinsi mambo mazuri yalivyotiwa doa katika tamthiliya hii. (Alama 10) Au
  2. Jadili mbinu zifuatazo kama zilivyotumiwa na mwandishi wa tamthilia hii
    1. Majazi (Alama 10)
    2. Jazanda (Alama 10)

SEHEMU YA D
HADITHI FUPI: TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE

(Alifa Chokocho na Dumu Kayanda- Wahariri)
Jibu swali la sita ama la saba
Eunice Kimaliro- MTIHANI WAMAISHA

  1. “Lakini hajawahi kuniamini huyu hambe. Lakini mimi mwenyewe najiamini. Lazima mtu ajiamini. Au sio? Leo ndio siku yangu ya kuthibitisha ukweli wa mambo Leo mwalimu atajua kuwa mkataa biu hubiuka. ….”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Alama 4) 
    2. Bainisha mbinu nne za kimtindo katika dondoo hili. (Alama 4) 
    3. Bainisha toni ya dondoo hili. (Alama 2)
    4. Thibitisha ukweli wa kauli, “Leo ndio siku yangu ya kuthibitisha ukweli wa mambo,” kama alivyosema mzungumzaji. (Alama 12)
      Au
  2.  
    1. Salma Omar Hamad- SHIBE INATUMALIZA
      “Lakini nakwambia tena, kula kunatumaliza.”
      Onyesha jinsi kula kuliwamaliza wazungumzaji na wahusika wengine katika hadithi hii (Alama 10)
    2. Kenna Wasike- MAPENZI YA KIFAURONGO
      Jadili Suala la umaskini na athari zake kama ilivyo katika hadithi ya Mapenzi ya Kifaurongo (Alama 10)

SEHEMU YA E   
FASIHI SIMULIZI

  1. Soma utungo ufatao kisha ujibu maswali

    “Hapo zamani za kale, kale sana kabla ya ujio wa manabii Issa, Musa ama hata Yesu, walimwengu wote waliishi pamoja kama ndugu na dada. Hakukuwepo haya makabila tunayoyasikia yakitajwa kila siku. Hakukuwepo na utabaka. Hapakuwepo na maskini. Watu wote waliishi pamoja kama wafanyavyo wanyama wa familia moja. Hakukuwepo na tofauti na tamaa ya uongozi na kujitakia kwa wananchi. Ubinafsi.

    Mwanadamu alipogundua umoja aliopewa na Mungu wake, alianza kusoma mengi mno na kutaka kujua mengi kuhusu Mola. Alidhani kwamba Mungu aliishi mbinguni. Hivyo basi, wanadamu wote waliitana pamoja katika kamkunji; mkutano wa siri, waratibu jinsi wangeweza kumfikia mwenyezi Mungu. Mwisho wa kikao, walikubaliana kuwa waanze kujenga ukuta mkubwa ambao ungewawezesha kufika juu mbinguni na kuzungumza moja kwa moja na Mola Mkuu.

    Siku iliyofuatia waliingia katika kazi. Huyu alileta jiwe hili na huyu msumari huu. Kazi ilifanywa kwa kujitolea na jitihada kuu kila mmoja akiamini kuwa atakaye kilicho mvunguni ni sharti ainame. Aidha, mgaagaa na upwa hali wali mkavu. Ukuta wao ulipanda kwa kasi. Wazee wenye busara walijaribu kuwaonya wajenzi dhidi ya hatua hii yao ila wakashikilia msimamo wao wa kutaka kuonana na Muumba wa mbingu na ardhi ana kwa ana.

    Mungu alipoona kuwa mwanadamu amejawa na kiburi, aliwachanganya wajenzi kwa kuzichanganya lugha zao. Hili liliwanya kutoelewana kiasi kwamba fundi mmoja alipoomba aletewa bisibisi aliletewa nyundo. Hatimaye ukuta mzima ulianguka na kuwaangamiza wajenzi na waliosalia wakabaki kutoelewana lugha zao. Hii ndiyo sababu wanadamu wana lugha tofauti.”
    Kutoka: Meja S. Bukachi- Mola Mkuu (Riwaya)
    Maswali
    1. Tambua kipera hiki cha hadithi. (Alama 2) (
    2. Wewe ni mtafiti uliye nyanjani kwa uchunguzi zaidi kuhusu kipera hiki:
      1. Taja mbinu tatu utakazotumia katika utafiti wako. (Alama 3) 
      2. Upi umuhimu wa kukusanya na kuhifadi tungo kama hizi? (Alama 5). 
      3. Taja njia tano zinazotumiwa na jamii ya kisasa kuendeleza fasihi simulizi. (alama 5)


MARKING SCHEME

SEHEMU YA A
USHAIRI

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali:
    MASWALI
    1. Tambua mende wanaorejelwa na mshairi. (Alama 1)
      • Wanasiasa/ viongozi wa kisiasa
    2. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili. (Alama 1)
      • Kuonesha jinsi wanasiasa wanavyowalaghai wananchi kabla ya kuanza kuwanyonya. 
    3. Nani nafsi nenewa katika shairi hili? (Alama 1)
      • Wananchi/ raia
    4. Taja tamathali za lugha zilizotumika katika shairi hili. (Alama 2)
      • Jazanda- mende- wanasiasa.
      • Kinaya- mende huja kwa upole ila ni hatari.
      • Taswira- huja usiku usiku.
      • Tashbihi- wao ni kama mapanya.
      • Balagha- kufika kule kwake?                 (Zozote 2×1= 2)
        Mtahiniwa lazima atoe mfano katika shairi ndipo atuzwe alama kamili.
    5. Fafanua uhuru wa ushairi alioutumia malenga. (Alama 2)
      • Kufinyanga sarufi/ msimbo- yao shauku- shauku yao.
      • Inkisari- mejinyamazia- wamejinyamazia
      • Tabdila- kachukuwe- kachukue    (Zozote 2×1= 2)
        Mtahiniwa lazima atoe mfano katika shairi ndipo atuzwe alama kamili.
    6. Weka shairi hili katika bahari mbalimbali. (Alama 3)
      • Ukawafi- mishororo yake imegawika katika vipande vitatu isipokuwa mshororo wa nne. 
      • Ukaraguni- vina vyako vyote vinabadilikabadilika kutoka ubeti hadi mwingine.
      • Msuko- mshororo wa mwisho umefupishwa.     (Zozote 2×1= 2)
        (kutaja ½ kueleza ½ )
    7. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (Alama 4)
      Wao ni kama mapanya ambao huuma na kupuliza ili kukutuliza. Wanapenda kudanganya huku wamejinyamazia ili kukupofusha.
      Usiwaone wanaminya kwa kutukandamiza kwani wanachosha. Mende wana umoja waonapo pana lishe.

      (matahini ahakiki kazi ya mtahiniwa)
    8. Tambua mambo manne anayolalamika nafsi neni kuhusu mende. (alama 4)
      • Wanavuna wasikopanda.
      • Wanaponda watu.
      • Hawataki hila zao zionekane.
      • Huuma wakipulizia.
      • Wanapenda kudanganya.
      • Wanatukandamiza na kutuchosha.
      • Huwaonga wananchi.
      • Hujificha wapatapo kura.
      • Hurarua kila kitu bila kujali wananchi.    (Zozote 4×1= 4)
    9. Vifungu vifuatavyo vina maana gani katika shairi? (alama 2) 
      1. vitano vikishatimu- baada ya miaka mitano
      2. Tuwang’atue machawa - tuwaondoe uongzini

SEHEMU YA B
RIWAYA: CHOZI LA HERI
(Assumpta K. Matei)
Jibu swali la Pili au la Tatu

  1.  “Lakini itakuwaje historical injustice, nawe Ridhaa hapo ulipo sicho kitovu chako?”
    1. Eleza muktadha wa maneno haya. (Alama 4)
      • Haya ni mawazo ya Ridhaa. Ridhaa yupo katika lililokuwa jumba lake ambalo lilikuwa sasa limeteketezwa na Mzee Kedi na kuangamiza familia yake. Ridhaa anakumbuka mijadala mipana aliyokuwa na bintiye Annatila (Tila). Ridhaa anahuzunika jinsi Waafrika walivyofanyishwa kazi ngumu, wakiwamo watoto wadogo wasiokomaa. Anamuuliza Tila mawazoni kama hali hii ndiyo historical injustice, ila anajikumbusha kuwa naye hakuwa mzaliwa asilia wa eneo lile. (Hoja 4×1= 4)
    2. Tambua mbinu mbili za lugha zilizotumiwa katika dondoo hili. (Alama 4)
      • Uzungumzi nafsia- Ridhaa anakumbuka mjadala wake na Tila.
      • Kisengere nyuma/mbinu rejeshi- Ridhaa anakumbuka mjadala wake na Tila.
      • Balagha- hapo ulipo sicho kitovu chako?
      • Kuchanganya ndimi- lakini itakuwaje historical injustice.         (zozote 2×2= 4 - kutaja 1, kueleza 1)
    3. Eleza umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya. (Alama 4)
      Umuhimu wa Ridhaa
      • Anawakilisha watu walio na uwezo wa kukumbuka mambo muhimu yanayotokea maishani mwao.
      • Anaonyesha watu ambao wanaendelea kuwa na imani katika ushirikina na uhalisia wake katika jamii ya kisasa.
      • Anawakilisha watu walio na bidii katika shughuli za kuiauni jamii zao.
      • Anawakilisha watu wazalendo wanaoitetea jamii zao.
      • Ni kiwakilishi cha waathiriwa wa siasa za kikabila na athari zake kwa jamii.
      • Anaonyesha watu wenye moyo na imani walio tayari kuwasaidia watu na watoto wa wazazi wengine.
        (zozote 4×1= 4- lazima mtahiniwa ataje kuwa msemaji ni Ridhaa ndiposa apate alama za umuhimu)
    4. Ni mambo gani yaliyowakumba walioishi penye kitovu kisicho chao? (Alama 8) 
      • Walibaguliwa na wenzao- Ridhaa alibaguliwa shuleni.
      • Walifurushwa makwao- Ridhaa, Kaizari
      • Walivamiwa na kupigwa- Kaizari, mkewe na wanao.
      • Walilazimika kuwa wakimbizi.
      • Chakula kilikuwa adimu.
      • Kulikuwa na changamoto ya maji safi ya kunywa.
      • Kama wakimbizi, wengi walipata homa ya matumbo.
      • Wengine kuyapoteza maisha yao.
      • Wakimbizi walizidi kuongezeka nayo hali ya maisha ikazidi kuwa ngumu.
      • Idadi kubwa ya wakimbizi ilifanya kuwe na vyoo vya kupeperushwa.
      • Tishio la maenezi ya kipindupindu.
        (zozote 8×1= 8- mtahiniwa aeleze hoja zake kwa mifano ili atuzwe alama 1)
        Au
  2.  
    1. “Jamii ya Chozi la Heri imeoza.” Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa mifano ya kutosha kutoka katika riwaya ya Chozi la Heri. (Alama 10)
      • Jamii inaendeleza ubakaji. Genge la mabarobaro watano lilifululiza hadi walipokuwa maskini Lime na Mwanaheri na kuwabaka mbele ya baba yao (uk 25).
      • Kuna ulanguzi wa dawa za kulevya. Dick alipotoroshwa na Sauna alipelekwa kwa tajiri mmoja aliyemwingiza katika kusafirisha dawa za kulevya kutoka nchi moja hadi nyingine (uk 119- 120). 
      • Wanajamii wanaendeleza uporaji na wizi wa mali. Vijana wanawavamia watu, kuwaua na kupora katika maduka ya kihindi, kiarabu na ya waafrika wenzao.
      • Jamii inaendeleza ufuska/ ukahaba. Sauna aliiba watoto na kuwapeleka kwa mama mmoja aliyewatumia kwa biashara ya nipe nikupe (uk 84).
      • Biashara haramu inaendelezwa. Bi. Kangara alifanya biashara ya kuwauza watoto na vijana Safari yake ilipata mkondo mwingine baada ya polisi kupata fununu kuhusu njama ambazo yeye na Bi. Kangara walikuwa wakiendesha. Mabibi hawa walikuwa na mtandao ambao kazi yake ilikuwa kuwauza watoto na vijana (uk 84).
      • Kuna tatizo la mimba za mapema. Vijana wana mazoea ya kukumbatia mtafaruku wa kuhisia unaowapata na mara hujipata wameambulia ujauzito kama alivyofanya Zohali (uk 98).
      • Baadhi ya wanajamii wanaendeleza uavyaji mimba. Sauna alijaribu awezavyo kuavya mimba na mwishowe, baada ya kushindwa, anaamua kujiua.
      • Kukiuka maadili ya kikazi. Fumba (mwalimu) anakiuka maadili ya kazi na kujihusisha kwa mapenzi na mwanafunzi wake, Rehema, na hatimaye kumpachika ujauzito (uk 102).
      • Wazazi wanawabaka wana wao. Babake Sauna anafanya mapenzi na mwanawe kila apatapo nafasi, na mwishowe, Sauna anapata mimba.
      • Starehe na anasa kwa vijana. Vijana wa vyuo vikuu wameshindwa kutofautisha usiku na mchana. Tindi anasahau kumrejesha Lemi nyumbani kutokana na muziki (uk 121).
      • Wazazi wanakwepa malezi na kuwatupa wanao wakiwa wachanga. Neema anampeleka mtoto aliyemwokota kwa polisi (uk 162).
      • Vijana kuwaiga wazee. Mwangemi na mwangeka walikuwa na tabia mbovu ya kumuiga babu yao (uk 186).
        (zozote 10×1= 10- mtahiniwa ataje uozo na mfano kutoka katika riwaya)
    2. Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo:
      Lakini baba, sijasema tunataka kiongozi mwanamke. Sisi tunataka kiongozi yeyote, awe mwanamke au mwanamume, atakayeweza kulielekeza jahazi hili letu kwenye visiwa vya maendeleo. Pale tutakapoafikia Malengo ya Kimaendeleo ya Kimilenia. Kiongozi ambaye ataendeleza juhudi za kukabiliana na wale maadui ambao wewe daima huniambia kuhusu: umaski, ujinga na magonjwa, (akisita kumtazama baba)uhaha wa nafasi za kazi na ufisadi. Je, huu sio uliokuwa muono wa waliopigania uhuru? Siyo ambayo viongozi waliochukua hatamu za uongozi kutoka kwa watu weupe waliyofanya juu chini kutekeleza?
      • Dayalojia- baina ya Tila na Ridhaa.
      • Tanakuzi- mwanamume au mwanamke.
      • Jazanda- jahazi (nchi).
      • Istiari- visiwa vya maendeleo- maadu wa nchi.
      • Utohozi- Kimilenia (millennium).
      • Balagha- muono wa waliopigania uhuru?
      • Taswira- waliopigania uhuru, jahazi n.k.            (zozote 5×2= 10 –kutaja 1 maelezo 1)

SEHEMU YA C
TAMTHILIA: KIGOGO
(Pauline Kea)

  1. “Wewe nawe hukualikwa. Wataka kutia siasa tayari? Hamkosi kutia doa kila jambo zuri.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Alama 4)
      • Haya ni maneno ya Boza. Anamwambia Sudi. Wapo katika karakana yao sokoni. Ni baada ya kupata habari kupitia kwa redio ya simu ya Sudi kuwa wananchi watakuwa wakisherehekea mwezi mzima kuadhimisha miaka sitini ya uhuru. Komba anataka kujua watu watakula nini
        muda huu wote bila kazi. Sudi anajibu kwa kejeli kuwa wangekula mali walizochuma miaka sitini iliyopita. Boza anaona kuwa jibu hili ni la kutia doa mambo mazuri.   
        (4×1= 4)
    2. Eleza vipengele viwili vya kimtindo alivyotumia msemaji kufanikisha uwasilishaji wa ujumbe. (Alama 2)
      • Balagha- wataka kutia siasa tayari?
      • Kinaya- anaamini kuwa mwezi mzima wa sherehe bila kazi ni jambo bora.   (zozote 2×1= 2)
    3. Fafanua sifa nne za anayeambiwa maneno haya. (Alama 4)
      Sifa za Sudi
      • Ni mwenye msimamo thabiti. Anakataa katakata ushawishi wa Kenga anayemtaka amchongee Majoka kinyago cha babake, Ngao Marara. Anashikilia kuwa yeye anamchonga shujaa halisi wa Sagamoyo, Tunu (uk 10–12).
      • Ni mzalendo. Anajitolea kwa hali ili kuikomboa Sagamoyo kutoka kwa uongozi mbaya wa Majoka.
      • Mwenye mapenzi ya dhati. Anampenda sana mkewe Ashua. Anapopata habari za kushikwa kwake anaenda moja kwa moja hadi gerezani kumwona (uk 46).
      • Mshauri mwema. Anatumia muda wake mwingi kule karakarani kuwashauri Kombe na Boza kujaribu kuona ukweli wa uongozi mbaya wa Majoka.
      • Mwenye kuwajibika. Anawajibikia jamii yake. Anafanya kazi ngumu ya uchongaji wa vinyago ili aweze kuikimu jamii yake licha ya pato duni.
        (zozote 2×1= 2- mtahiniwa ataje kuwa mwambiwa ni Sudi)
    4. Fafanua jinsi mambo mazuri yalivyotiwa doa katika tamthiliya hii. (Alama 10) 
      • Maji machafu (uchafuzi wa mazingira) yalipita mtaroni na kueneza harufu mbaya kila mahali bila uongozi wa Sagamoyo kuliona hili kuwa tatizo (uk 2).
      • Soko la Chapakazi limebadilishwa na kufanywa uwanja wa kumwagia kemikali (uk 2). ⮚ Wafanyabiashara wanahangaishwa na  wanaosanya ushuru kwa kuwaitisha kitu kidogo na wengine kitu kikubwa (uk 2–3).
      • Serikali kutangaza mwezi mzima wa kusherehekea uhuru bila watu kufanya kazi ilhali haijali watakachokula watu (uk 4).
      • Serikali ya Sagamoyo haina mipango maridhawa ya kimaendeleo. Majoka anamiliki kampuni kubwa ya sumu ya nyoka badala ya miradi muhimu (uk 4).
      • Kuna ufisadi unaomfanya Asiya kupata kandarasi ya uokaji keki ya uhuru kwa kujuana na Husda bali si kwa kufuzu na kufaulu (uk 7).
      • Utawala wa Sagamoyo ni wa kimabavu. Kenga anamlazimisha Sudi amchongee Majoka kinyago cha Ngao licha ya kujua kuwa uongozi wa Majoka ni wa udhalimu (uk 9).
      • Kombe, mshiriki wa karibu wa Kenga anakiri kuwa mambo yameenda kombo Sagamoyo (uk 15). ⮚ Uongozi unafunga soko la Chapakazi. Soko hili ndilo kitegauchumi pekee kwa Wanasagamoyo (uk 25).
      • Kuna maandamano ya mara kwa mara na yasiyotatuliwa katika jimbo la Sagamoyo, wanachi wanapigania haki zao.
      • Majoka anawatumia polisi wake vibaya ili kujidumisha uongozini. Polisi wanawanyanyasa na kuwadhulumu wananchi bila Majoka kujali.
      • Sagamoyo kuna uongozi wa ubinafsi. Majoka anataka kuendeleza ubinafsishaji wa uongozi wa Sagamoyio kwa kumtangaza rasmi Ngao Junior kuwa mrithi wake (uk37).
      • Kuna unyakuzi wa mali ya umma. Majoka analifunga soko na kuinyakua sehemu hiyo ili ajenge hoteli ya kifahari (uk 45). (zozote 10×1= 10)
        Au
  2. Jadili mbinu zifuatazo kama zilivyotumiwa na mwandishi wa tamthiliya hii
    1. Majazi (Alama 10)
      Ni mbinu ya kuwapa wahusika (pamoja na kitu ama mahali) majina kulingana na tabia na sifa zao.
      • Majoka. Nyoka mkubwa ni joka. Wingi wake ni majoka. Nyoka ni mnyama atambaaye mwenye sumu kali aitumiayo kuwaangamiza wadudu na wanyama wengine ili awale. Majoka ana mbinu nyingi kama matumizi ya polisi (sumu yake) anaowatumia ili kuwapinga na kuwaangamiza wapinzani wa sera zake.
      • Tunu ni kitu ambacho ni adimu kupatikana na chenye kutumika kwa nadra. Mhusika Tunu anajitokeza kama mwanamke wa pekee anayezawadiwa kwa Wanasagamoyo ili kuwakomboa kutoka kwa uongozi mbaya wa Majoka.
      • Sudi ni bahati njema. Sagamoyo ina bahati kumpata Sudi anayeandamana na Tunu ili kupambana na jamii iliyojaa taasubi na ukandamizaji.
      • Kenga. Kumkenga mtu ni kumfanya kuamini jambo lisilo la kweli. Kenga anatumiwa na Majoka ili kuwalaghai watu na kuwafanya kukubaliana na sera duni za Majoka ili ajidumishe uongozini.
      • Husda. Kuhusudu ni kuwa na jicho la matamanio fulani. Husda anamhusudu Ashua kwa kisomo chake. Aidha anahusudu mali ya Majoka na kuolewa naye. Husda alimwangalia Chopi kwa macho yenye uchu.
      • Boza ni mtu mpumbavu. Mhusika Boza anaushabikia uongozi mbaya wa Majoka na amejawa na ubinafsi.
      • Siti ni jina la heshima kwa mwanamke. Siti anawasaidia Tunu na Sudi katika kuendeleza harakati za ukombozi.
      • Ngurumo ni sauti kubwa ya mvumo. Sauti hii huisha baadaye. Ngurumo anawatisha Tunu na Sudi huku akimshabikia Majoka. Baadaye anauawa na chatu wa Majoka.
      • Chopi ni kutembea kwa kuchechemea.Mhusika Chopi anatumwa ovyo na Majoka na kulemazwa na shughuli.
      • Pendo ni kuthamini kitu. Pendo anapendwa na kuthaminiwa na babake.
      • Kingi ni mfalme katika mchezo wa drafti (staranji). Kingi anakuwa mfalme katika ukombozi wa Sagamoyo kwa kukataa kuwaamrisha polisi kuwavamia wananchi.
      • Chapakazi. Kuchapa kazi ni kuifanya kwa bidii. Wanasagamoyo wanalipigania soko lao la Chapakazi wanakofanyia shughuli zao ili kupata mkate wao wa siku.
      • Sagamoyo. Kusaga ni kuvunjavunja. Kusaga moyo ni kuondoa matumaini na kuangamiza kabisa. Wanasagamoyo wanatamaushwa na uongozi mbaya wa Majoka anayewanyanyasa na kunyakua mali yao.
        (zozote 10×1=10- Mtahini atoe maelezo sahihi ndiposa atuzwe alama 1)
    2. Jazanda (Alama 10)
      Jazanda: Jazanda ni fumbo linalorejelea jambo fulani.
      • Anwani ya tamthilia, Kigogo, imetumiwa kijazanda kuonesha jinsi viongozi wanavyoyatumia mamlaka yao kwa kuwakandamiza wananchi wanapokuwa uongozini. Kigogo huyu ni Majoka anayaewaangamiza Wanasagamoyo.
      • Nyoka wa Majoka na sumu yake ni jazanda. Ni ishara ya mbinu hatari (sumu ya nyoka) ambazo anazitumia Majoka (nyoka) ili kuendeleza uongozi wake mbaya.
      • Damu imetumiwa kijazanda. Damu ni ishara ya mauaji na mateso waliyoyapitia Wanasagamoyo. Aidha, damu imetumika kama ishara ya ukombozi.
      • Ndoto ya Tunu akifukuzwa na Mzee Marara ili apate kumnyang'anya mkufu wake wa dhahabu ni ishara ya ulafi wa viongozi na namna wanavyowaangaisha watu wanyonge katika jamii (uk 55). ⮚ Ukali wa jua anaoulalamikia Majoka ni jazanda. Hii ni ishara ya nguvu za mabadiliko na upinzani ambao umeanza kumshinda Majoka kuhimili (uk 67).
        Tathmini ya Pamoja ya Lanjet Fasihi ya Kiswahili 102/3 8
      • Kuvunja mguu (uk 68) kama linavyotumiwa na Majoka na Kenga ni jazanda ya maangamizo na mauaji yanayotekelezwa na uongozi mbaya wa Majoka.
      • Kenga anasema kuwa anafikiri kuwa ni lazima Chopi aende safari (uk68). Hii ni safari ya kijazanda inayomaanisha kuwa Chopi aangamizwe.
      • Kazi ya chatu ni mauaji (uk 69). Chatu ni jazanda. Inaashiria mbinu na vyombo vya maangamizi avitumiavyo Majoka ili kuwanyamazisha wapinzani wake.
      • Ziwa la damu analoliona Majoka na sauti ya Jabali anayoisikia ni ishara ya maovu na mateso ya Wanasagamoyo aliowaangamiza. Sauti hii imerudi kuwakomboa waliosalia dhidi ya uongozi katili wa Majoka.
      • Marubani (uk 79) ni ishara ya viongozi. Majoka analalamika kuwa hawapendi marubani kwani ni malaghai asijue kwamba naye pia ni mmoja wa marubani hao walaghai.
      • Keki ya uhuru inayoliwa na wachache ni ishara ya rasililimali za nchi na jinsi zinavyowanufaisha wachache katika jamii.
      • Babu anamwambia Majoka kuwa kisima kimeingia paka na maji yake hayanyweki. Kisima ni jazanda ya jimbo la Sagamoyo naye paka kuingia kisimani ni ishara ya mambo kuwa mabaya.
        (zozote 10×1=10- Mtahini atoe maelezo sahihi ndiposa atuzwe alama 1)

SEHEMU YA D
HADITHI FUPI: TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE
(Alifa Chokocho na Dumu Kayanda- Wahariri)
Jibu swali la sita ama la saba
Eunice Kimaliro- MTIHANI WAMAISHA

  1. “Lakini hajawahi kuniamini huyu hambe. Lakini mimi mwenyewe najiamini. Lazima mtu ajiamini. Au sio? Leo ndio siku yangu ya kuthibitisha ukweli wa mambo. Leo mwalimu atajua kuwa mkataa biu hubiuka….” 
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Alama 4)
      • Haya ni maneno ya Samueli Matandiko. Anajiambia nafsini. Yupo katika mlango wa ofisi ya mwalimu mkuu. Amekuja ili kuchukua matokeo yake ya mtihani wa kitaifa. Anasema maneno haya kwani alijua kuwa mwalimu mkuu hakuamini uwezo wake masomoni.
        (zozote 4×1= 4)
    2. Bainisha mbinu nne za kimtindo katika dondoo hili. (Alama 4)
      • Uzungumzi nafsi- lakini hajawahi kuniamini huyu…
      • Balagha- au sio?
      • Kinaya- leo ndio siku yangu ya kuthibitisha ukweli wa mambo.
      • Methali- Mdharau biu hubiuka.
        (zozote 4×1=4)
    3. Bainisha toni ya dondoo hili. (Alama 2)
      • Toni ya tumaini- mimi mwenyewe najiamini
        (kutaja 1, maelezo 1)
    4. Thibitisha ukweli wa kauli, “Leo ndio siku yangu ya kuthibitisha ukweli wa mambo,” kama alivyosema mzungumzaji. (Alama 12)
      • Ukweli unathibitishwa kwa Samueli kufeli mtihani ilhali aliamini kuwa yeye ni hodari na atamshtua Mwalimu Mkuu. Anapata D na E kwenye kila somo.
      • Ukweli unathibitishwa kwa Samueli kudai kuwa anajua Mto Limpopo upo Misri na Mto Zambezi upo Tanzania ambayo inapakana kaskazini na Somalia.
      • Ukweli unathibitishwa Samueli anapodai eti anajua Kenya ilipata uhuru 1980. ⮚ Ukweli unathibitishwa kwa Samueli kusema kwamba mimea ya kijani ina kitu kiitwacho umbijani (uk 135). Haya yote ni uongo huku naye akidhani ni ukweli.
      • Samueli anashindwa kuwakabili wanafunzi wenzake na kujifungia chooni.
      • Ukweli unadhihirika babake Samueli anapoenda shuleni na kutambua kuwa Samueli alikuwa kafeli mtihani vibaya vibaya.
      • Samueli anamwepuka mpenziwe Nina baada ya kujua kuwa alikuwa amefeli katika mtihani. Anaogopa kuonwa zuzu.
        (zozote 6×2= 12)
        Au
  2.  
    1. Salma Omar Hamad- SHIBE INATUMALIZA
      “Lakini nakwambia tena, kula kunatumaliza.”
      Onesha jinsi kula kuliwamaliza wazungumzaji na wahusika wengine katika hadithi hii (Alama 10)
      • Mzee Mambo ni waziri kivuli wa wizara zote, hafanyi kazi maalumu kiasi kwamba haoni umuhimu wake. Hata hivyo, yeye hupakua mshahara (uk 37).
      • Viongozi wanatumia mali ya umma kufanikisha maslahi yao. Mzee Mambo anatumia magari ya serikali kubebea maji na kuwapeleka watoto kwenda kuogeshwa (uk 39).
      • Viongozi wanatumia pesa za umma kuandaa sherehe zisizo na maana. Mzee Mambo anasherehekea mwanawe kujiunga na chekechea na yule mdogo kumea vijino viwili (uk 38).
      • Viongozi wanakula bila kufanya kazi. Mzee Mambo anakiri kuwa kinachoangaliwa zaidi ni kwenda kazini bali si kufanya kazi (uk 37), aidha, katika sherehe hakupikwi, kunaliwa tu (uk 39).
      • Huku Sasa na Mbura wakijinufaisha, wanyonge wanahangaika kwa kukosa chakula. Kidogo walicho nacho kinachukuliwa na viongozi wanaokula wanyonge wakiteseka. Wamepuuzwa wanyonge. Viongozi wanakula tu. Wanadai kuwa wanakula vyao vya wenzao (uk 44). 
      • Viongozi kama Sasa na Mbura wanajinyakulia mali nyingi. Hawachukuliwi hatua yoyote bali wanaachwa kuendeleza uovu wao. Mbura anasisitiziwa kuwa aendelee kuwasasambura wananchi.
      • Uongozi wa kina Mambo haujali maumivu ya wananchi. Wanatumia falsafa potovu ya ‘kutojali lawama’ za wanyonge. Muziki anaousikiza Mzee Mambo unadhihirisha kuwa viongozi hawajali sheria.
      • Dj analipwa pesa nyingi kwa kuwatumbuiza watu.           (zozote 5×2)
    2. Kenna Wasike- MAPENZI YA KIFAURONGO
      Jadili Suala la umaskini na athari zake kama ilivyo katika hadithi ya Mapenzi ya Kifaurongo (Alam 10)
      • Chuoni, Dennis anakumbwa na tatizo kubwa la utabaka. Wanafunzi kutoka familia zenye nafasi walikuwa na simu za thamani, wengine walibeba vipakatalishi na iPad zao mikononi (uk 13) huku naye asiweze kupata hata chochote. Umaskini huu ulileta mpaka kati ya wanafunzi maskini na tajiri wasiweze kukaribiana.
      • Siku moja Dennis akiwa chumbani mwake baada ya kupika uji wa mahindi bila sukari kutokana na umaskini wake, Penina, binti yake Bw. Kitime, Katibu wa Kudumu katika Wizara ya Afya (uk 19) anabisha mlangoni pake.
      • Penina anamweleza kuwa lengo la kuja kwake ni kumtaka wawe wapenzi. Anamweleza hadharani kuwa kando na mapenzi ya wazazi, kuna mapenzi mengine anayoyakosa na anayataka kutoka kwake Dennis. Dennis anasita kujihusisha kwa mapenzi na msichana huyu wa kitajiri kwa kuhofu kutemwa tena; mapenzi ya kifaurongo.
      • Wanakuwa kwenye mapenzi. Mapenzi yao yanadumu kwa muda wa miaka miwili. Wanapomaliza chuo, wanahamia kwenye mtaa wa watu wa pato la wastani, Newzealand, licha ya kuwa hawajapata kazi. Wazazi wake Penina wanawalipia kodi.
      • Dennis anatafuta kazi kwa kila njia bila mafanikio. Anakosa kazi katika shirika la uchapishaji magazeti kwa kushindwa kujibu swali moja la kwanza.
      • Kukosa kazi kunamfanya Penina kumwamrisha asanye kila kilicho chake na aondoke. Akamfukuza na kumtaka aione nyumba yake paa. Haya yote yanatokana na hali mbaya ya umaskini wa Dennis.
        (zozote 5×2- Mtahini atathmini majibu ya watahiniwa)

SEHEMU YA E
FASIHI SIMULIZI

  1. Soma utungo ufatao kisha ujibu maswali
    Maswali
    1. Tambua kipera hiki cha hadithi. (Alama 2)
      • kisasili- inaeleza kuhusu chanzo cha lugha tofauti.
        (kutaja 1, kueleza 1)
    2. Wewe ni mtafiti uliye nyanjani kwa uchunguzi zaidi kuhusu kipera hiki:
      1. Taja mbinu tatu utakazotumia katika utafiti wako. (Alama 3)
        • Kusikiliza
        • Kushiriki
        • Kurekodi
        • Kutazama
        • Kutumia hojaji
        • Mahojiano
          (Zozote 3×1= 3)
      2. Upi umuhimu wa kukusanya na kuhifadi tungo kama hizi? (Alama 5). ⮚]]
        • Humpa mwanafunzi wa fasihi simulizi nafasi ya kutagusana na jamii iliyozaa fasihi husika.
        • Humpa mwanafunzi wa Fasihi Simulizi nafasi ya kushuhudia na kuathiriwa moja kwa moja na utendaji wa Fasihi Simulizi.
        • Husaidia kurekodi na kuhifadhi tamaduni za jamii.
        • Huiendeleza Fasihi Simulizi.
        • Husaidia kuziba pengo la utafiti lililopo.
        • Hutumiwa kama kiunzi cha uchanganuzi wa kiulinganishi wa Fasihi Simulizi za jamii mbalimbali.
        • Humwezesha mwanafunzi wa Fasihi Simulizi kupata maarifa ya fasihi.
        • Husaidia kurekebisha mawazo potovu kuhusu suala fulani.           (Zozote 5×1= 5)
      3. Taja njia tano zinazotumiwa na jamii ya kisasa kuendeleza fasihi simulizi. (alama 5)
        • Tamasha za muziki.
        • Sherehe za harusi, jando, mazishi na matambiko zipo.
        • Utegaji na uteguaji wa vitendawili kupitia redio na runinga.
        • Michezo ya kuigiza katika runinga, redio.
        • Tamasha za drama huendeleza utanzu wa maigizo. 
        • Sarakasi zinazofanywa na wasanii.
        • Ngoma za kienyeji kama Isukuti huchezwa katika hafla mbalimbali.
        • Watafiti wanaendeleza utafiti kuhusu Fasihi Simulizi.
        • Utambaji wa hadithi bado hufanyika.
          (Zozote 5×1= 5)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Lanjet Joint Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?