Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Sunrise 2 Evaluation Mock Exams 2022

Share via Whatsapp
MAAGIZO 
 
  • Jibu maswali yote.
  1. UFAHAMU – (ALAMA 15)
    Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuatia.


    Takwimu za tafiti za umaskini kila mara huonyesha kuwa bara la Afrika ndilo bara maskini kabisa kote duniani. Takriban wakaazi kiasi cha asilimia themanini hawawezi kumudu kutumia dola moja kwa siku. Toka kaskazini hadi kusini. mashariki hadi magharibi mwa bara, makaazi ya vibanda yametamalaki. Wakaazi wengi hulala njaa kutokana na ukosefu wa chakula. Watu wa mitaani waliovaa mararuraru wamejaa katika miji ya bara hili. Swali ni: Je, kwa nini umaskini umeliganda bara la Afrika hivi mithili ya  kupe? Kwa nini bara huselelea katika lindi la uchochole?

    Ili kuelewa sababu za umaskini kuganda barani Afrika, yampasa mtu ima fa ima kurejelea historia ya bara hili. Kwa kipindi cha karne nyingi, Afrika ilidhibitiwa na walowezi pamoja na mabeberu. Wanawake ambao wangelistwawisha bara hili kiuchumi walitwaliwa kimabavu na kupelekwa, huku wamefungwa minyororo, kustawisha uchumi wa mabara mengine. Afrika ikaporwa nguvu ambayo ni rasilmali kuu katika ustawishaji wa uchumi. La kusikitisha ni kuwa Afrika haikufidiwa kutokana na wizi huu. Badala yake iliongezewa mizigo mingine.

    Baada ya kipindi cha biashara ya utumwa kumalizika, Afrika ilijipata katika janga jingine. Wakoloni wakaliingilia bara kwa pupa. Wakaligawanya katika koloni mbalimbali miongoni mwao. Wakaingiwa na wendawazimu kuiba malighafi ya bara hili. Wakaiba mashamba, madini, miti na chochote cha maana walichokipata. Badala ya malighafi haya kutumika kunawirisha bara la Afrika, yalitwaliwa kustawisha chumi za walikotoka wakoloni. Afrika ikaachwa kuzidi kudidimia katika lindi la umaskini.

    Wakoloni walipotoka barani Afrika na kuzipa dola nyingi za Afrika ‘uhuru’, waliacha mkururo wa madhila. Madhila haya hayangeikubalia Afrika kujikomboa kutoka katika biwi la uchochole. Tatizo la kwanza na kubwa zaidi ni wakoloni kugawanya na  kukatakata Afrika katika mataifa mengi. Mgawanyo huu ukawa haukufuata utaratibu wowote. Kwa sababu hii, watu wa nasaba moja wakawekwa katika nchi tofauti. Mathalani , watu wa nasaba ya Kisomali waligawanywa na kuwekwa chini ya nchi huru ya Somali, wengine chini ya dola la Uhabeshi, huku wengine wakiwa nchini Kenya na Jibuti. Watu kama hawa hawakutaka mpango huu. Waliokuwa Kenya na  Uhabeshi wakachukua silaha na kupigana ili warejeshwe chini ya himaya moja ya taifa huru la Somali. Watu kama hawa wakatumia muda mwingi  kupigana; muda ambao ungetumika kuinua Afrika kiuchumi. Mapigano haya ya wenyewe kwa wenyewe yamekithiri kote katika bara la Afrika.

    Halikadhalika, mkoloni hakufanya juhudi zozote za kuanzisha viwanda ambavyo vingenyanyua uchumi wa Afrika na kuwatoa Waafrika katika biwi la ufukara. Palipokuwa na ari yoyote ya kuanzisha kiwanda, kilipoanzishwa hakikusaidia Afrika kiuchumi. Vilikuwa viwanda vya kupunguza zigo la bidhaa na kuzifanya kuwa nyepesi ili zisafirishwe kwa ajili ya viwanda vya nchi walizotoka wakoloni.

    Kwa kipindi cha muda ambao mkoloni amekuwa na maingiliano na wakaazi wa Afrika, amehakikisha kuwa mwafrika amekuwa mtegemezi wake. Malighafi ya Afrika yalipelekwa kutayarishiwa viwanda vya wakoloni. Kisha mwafrika alirudishiwa zikiwa bidhaa kamili za kutumiwa. Mwafrika akaonyeshwa kuwa chochote kilichotoka kwa wakoloni ni bora zaidi ya chake alichozalisha. Hii ikawa ni mbinu moja ya wakoloni kuwafukarisha Waafrika. Hata sasa, kilichotoka Ulaya, hata kama ni cha hali ya chini, huonekana bora zaidi kuliko alichozalisha Mwafrika

    Kwa upande mwingine, inadhihirika kuwa wakoloni hawajawahi kuondoka na kuwaachia Waafrika jukumu kamili la kuendesha uhuru wao kisiasa, kijamii na kiuchumi. Waliondoka kupita mlango mmoja na kurudi kwa wa pili. Mlango wa pili ukawa ni ukoloni  kuchukua sura nyingine, sura ya ukoloni mamboleo. Kupitia ukoloni huu, wakoloni hudhibiti uchumi na maendeleo ya Afrika kupitia asasi mbili walizozianzisha, yaani Benki Kuu ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani. Ili kupata mikopo ya maendeleo, asasi hizi hutoa masharti ambayo hukwamiza badala ya kuchangia kuleta maendeleo barani Afrika.

    Sasa hivi pana haja ya wana wa Afrika kufanya vikao vya dhurura ili kujadiliana kuhusu suluhisho la tatizo hili sugu la umaskini barani. Lazima wawahimize Waafrika wote kujikomboa kiakili na kung’amua kuwa maendeleo ya bara lazima yaongozwe na yadhibitiwe na Waafrika wenyewe. Wawahimize kuacha hulka za kukimbilia mataifa yaliyowafanya watumwa na kuwakalia kikoloni kwa misaada ya maendeleo. Misaada hii si ya dhati bali ni ya chati na hailengi kuondoa umaskini barani bali kuuendeleza.

    Pana haja pia Waafrika kuwa na miungano ya kiuchumi. Miungano hii husaidia katika uteteaji wa soko pamoja na bei za bidhaa zao ikilinganishwa na taifa moja kuyaendeleza mambo haya. Halikadhalika, Waafrika wanapaswa kutambua kile wanachotaka na kupanga mikakati ya kufikia mahitaji ya kimsingi kwa wananchi wake. Kwa mfano, uimarishaji wa mbinu msingi ambazo zitachangia kuimarisha uchumi wa mataifa wahitaji kuwa mstari wa mbele badala ya ununuzi wa magari na ndege za hadhi za kuwabebea viongozi.
    1. Ipe taarifa uliyoisoma anwani mwafaka. (alama 1)
    2. Kutamalaki kwa umaskini barani Afrika kunadhihirishwa na nini.   (alama 2)
    3. Onyesha jinsi ambavyo wakoloni wameendeleza umaskini barani Afrika. (alama 4)
    4. Thibitisha kwa kutoa hoja tatu, dhana ya kuwa “Waafrika wenyewe ndio wamechangia kuwepo kwa umaskini wa bara la Afrika.” (alama3)
    5. Umaskini barani Afrika unaweza kukabiliwa vipi kwa mujibu wa makala haya? (alama 3)
    6. Eleza msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika taarifa: (alama 2)
      1. kuselelea…………………………………………………………………………..………………
      2. mabeberu…………………………………………………………………………..………………
  2. UFUPISHO: (ALAMA 15)
    Soma kifungu kifuatacho kasha ujibu maswali.


    Katika ulimwengu huu tunaoishi wenye hekaheka nyingi, mwanadamu anaendeshwa na maisha mfano wa gurudumu la gari. Kwa watu wenye kufanya kazi katika mazingira ya ofisi ambapo wanaketi mchana kutwa, mazoezi ni muhimu sana. Baadhi ya watu huona fahari wapigapo tai na kuelekea au kutoka kazini kwa gari. Tabia hii ya mwanadamu inamsahaulisha kuwa mwili wake ulidhamiriwa kufanya mazoezi ya viungo kwa kutembea au kufanya kazi zenye kuhitaji misuli kuoashwa moto. Watu wengi hawana habari kuwa mazoezi yana faida tele kwao.

    Wataalamu wa sayansi wamebainisha kuwa watu wanaoidhiki miili yao kwa mazoezi ya mara kwa mara huishi zaidi kuliko wasiofanya mazoezi. Watu hawa huwa wamo katika hali nzuri ya afya na wenye nguvu kuliko wale ambao hawaishughulishi miili yao kwa mazoezi au kazi zinazohitaji utumiaji nguvu.

    Ni dhahiri kwamba mazoezi huchochea kuundwa kwa seli mpya za ubongo. Utafiti wa kisayansi umebainisha kuwa sehemu za ubongo zenye kusisimuliwa kwa mazoezi ndizo hutekeleza jukumu la kukumbuka na kujifunza. Bila mazoezi sehemu hizi zitashindwa kukumbuka au kujifunza maarifa mapya. Vile vile, imethibitishwa kwamba watu wanaoshiriki shughuli zenye kuwahitaji kutumia nguvu hutia fora katika mambo yanayowahitaji kukumbuka, kufanya maamuzi, pamoja na kusuluhisha matatizo.

    Hali kadhalika, mazoezi huimarisha siha ya binadamu. Mathalani, matatizo ya moyo yanaweza kukabiliwa kwa kufanya mazoezi ya viungo. Kufanya mazoezi mara kwa mara huufanya moyo kuwa imara na kuuwezesha kutekeleza jukumu lake ipasavyo. Ifahamike kwamba moyo wenye siha huweza kupiga kiasi kikubwa cha damu bila ya juhudi kubwa. Hili bila shaka litamkinga binadamu dhidi ya kulemewa na kazi.

    Isitoshe, kushiriki mazoezi au shughuli zenye kutumia nguvu mara kwa mara huuweka mwili katika hali nzuri ya kupambana na magonjwa. Utafiti wa kisayansi umeonyesha kuwa shughuli kiasi zinazomhitaji mtu kutumia nguvu, pamoja na upunguzaji wa uzito, na uzingatiaji wa lishe bora, huweza kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari kwa baina ya asilimia 50  na 60. Mazoezi hayapunguzi tu shinikizo la damu, bali pia hatari ya kupata kiharusi. Aidha, kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kuthibiti uzani wa mwili. Mtu anapokula kiasi cha chakula kinachozidi mahitaji yake ya kimwili huweza kujinenepea na kushindwa kutekeleza majukumu ya kimsingi. Mazoezi  husaidia kuzichoma kalori zisizohitajika mwilini. Hatua hii, licha ya kusaidia kupunguza uzani, huvisisimua viungo vya mwili. Matokeo ya haya ni utendakazi wa hali ya juu bila kuchoka. Vilevile mwili unaofanya mazoezi haudorori. Umbo la mtu anayefanya mazoezi hupendeza.

    Juu ya hayo, kufanya mazoezi mara kwa mara husaidia kujenga misuli yenye nguvu. Misuli inapokuwa na nguvu tunaweza kulifanya jambo kwa muda mrefu bila kuchoka. Mbali na misuli kuimarika, mazoezi na shughuli zinazohitaji utumiaji nguvu husukuma hewa na virutubisho kwenye viungo mahususi vya mwili na kuvisaidia kufanya kazi vyema zaidi.

    Hali kadhalika mazoezi husaidia kujenga mifupa. Kadri binadamu anavyoshiriki katika shughuli kama vile kuruka, ndivyo anavyoimarisha mifupa yake. Shughuli ya aina hii huipa mifupa uzito ambao unaiwezesha kukua na kujengeka ikiwa na nguvu. Mazoezi pia hukawiza kudhoofika kwa mifupa.

    Kunyooshanyoosha viungo nako huchangia kuufanya mwili kuwa imara na wenye kunyumbuka. Hali hii ya mwili hupunguza uwezekano wa kupata majeraha. Mwili usionyumbuka humfanya mtu ashindwe kutekeleza hata shughuli nyepesi zinazomhitaji kutumia nguvu. Si ibra kupata kwamba kuitekeleza shughuli ndogo tu humfanya mtu kupata maumivu.

    Utulivu wa akili nao huweza kupatikana kwa kufanya mazoezi. Imebainishwa kwamba kufanya mazoezi kwa angalau dakika thelathini kwa muda wa baina ya siku tatu na tano kwa wiki hupunguza kwa kiasi kikubwa, dalili za unyong’onyevu. Na je, wajua kwamba kufanya mazoezi husaidia kupata usingizi? Mazoezi ni mfano wa bembea inayokutuliza na kukupa usingizi.

    Mke ni nguo, mgomba kupaliliwa. Nao mwili wa binadamu, kama mgomba, unahitaji kushirikishwa katika mazoezi ili kuuwezesha kuwa na hamu ya kutenda kazi.

    Maswali
    1. Kwa kurejelea aya tano za kwanza, eleza matatizo ya kiafya yanayoweza kupatikana kwa kutofanya mazoezi. (maneno 100) (al.9, 1 ya mtiririko)
    2. Fupisha ujumbe wa aya tano za mwisho kwa maneno 80. (al. 6,1 ya mtiririko)
  3. MATUMIZI YA LUGHA   
    1. Tumia neno Kamene kama yambiwa katika sentensi. (alama 2)
    2. Taja misingi ya upangaji wa irabi za Kiswahili. (alama 3)
    3. Huku ukitoa mfano mmoja, eleza maana ya mofimu ya kimsamiati. (alama 2)
    4. Vitambue vijenzi vya kimsingi vya lugha ya Kiswahili. (alama 2)
    5.  
      1. Eleza maana ya kishazi. (alama 1)
      2. Tunga sentensi moja yenye kishazi tegemezi kinachovumisha. (alama 2)
    6. Badilisha kitenzi kisaidizi kilicho kwenye sentensi ifuatayo kiwe kishirikishi. (alama 2)
      Mvule alikuwa akilala bwenini.
    7. Taja majukumu ya vipengele vilivyopigwa kijistari. (alama 4)
      Nanyi nendeni haraka au muadhibiwe kinyama kwa utundu wenu.
    8. Andika sentensi ifuatayo katika ukubwa. (alama 2)
      Uteo alionunuliwa umezeeka sana. ................................................................................................................................................
    9. Tunga sentensi moja mwafaka kudhihirisha matumizi ya kiunganishi madhali. (alama2)
    10. Onyesha minyambuliko ya maneno yafuatayo katika kauli zilizotolewa mabanoni. (alama 2)
      1. ja (tendewa) …………………………………………………….……………………………………………………
      2. cha (tendeka) …………………………………………………………………………………………………………
    11. Katika sentensi moja, onyesha matumizi mawili ya kibainishi. (alama 2)
    12. Yakinishi (alama 2)
      Usipolipa usiingie ndani
    13. Neno ‘gofu’ linapatikana katika ngeli gani? (alama 1)
    14. Geuza sentensi ifuatayo iwe katika usemi halisi. (alama 2)
      Kassim alimwomba Hirshi aende mahali alipokuwa ili amtume.
    15. Changanua sentensi ifuatayo kwa kutumia kielelezo matawi. (alama 4)
      Japo Mutiso anasinzia darasani hajamaliza kazi yake.
    16. Iandike upya sentensi ifuatayo kwa kutumia visawe vya maneno yaliyo katika italiki. (alama 3)
      Mdarisi aliwashauri wanafunzi kuwa bidii huzaa ufanisi
    17. Unda kitenzi kutokana na kivumishi jasiri. (alama1)
    18. Andika maana ya nahau: kunjua jamvi (alama 1)
  4. ISIMU JAMII     
    Eleza hali ya lugha ya Kiswahili nchini Kenya baada ya uhuru (alama.10)


MARKING SCHEME

  1. UFAHAMU
    1. Anwani
      • Umaskini / umaskini barani Afrika (1)
    2.  
      • Takwimu kuonyesha kuwa wakaazi wengi wa Afrika hawawezi kuishi kwa dola moja kwa siku
      • Hali za maisha kote barani – makazi mavazi na chakula vinaashiria hali ya umaskini inayolikabili bara. (2)
    3.  
      • Kuporwa kwa nguvu za Afrika bila fidia katika kipindi cha biashara ya utumwa.
      • Nguvu hii ambayo ingetumika kustawisha bara la Afrika ilitwaliwa kwenda kustawisha chumi za mabara mengine.
      • Uporaji wa rasilmali na malighafi ya Afrika na kwenda kunufaisha mabara mengine.
      • Kutoanzisha viwanda ambavyo vingesaidia kustawisha uchumi wa Afrika.
      • Wakoloni walikatakata bara la Afrika katika dola ambazo hazina manufaa kiuchumi.
      • Watu wa nasaba moja kugawanywa na kuwekwa chini ya mataifa mbalimbali. Baadaye watu hawa kuzusha vita na kutumia muda mwingi ambao ungetumika kustawisha uchumi badala ya mapigano.
      • Mkoloni kuanzisha ukoloni mamboleo kupitia kwa asasi kama Benki Kuu ya dunia na Shirika la Fedha Duniani. Hizi zimechangia kuendeleza umaskini barani.
        (zozote 4 x 1 = 4)
    4.  
      • Wafrika kuwa wategemezi. Hununua vya watu wengine na kudharau walivyozalisha kwa hivyo bidhaa zao hukosa soko. Hili haliwezi kustawisha uchumi bali kuendeleza umaskini.
      • Waafrika kukosa kujikomboa kiakili na kujua kuwa maendeleo ya bara yanatakiwa kuanzishwa na kudhibitiwa na Waafrika wenyewe. Wao hukimbilia misaada ya maendeleo kwa njia ya mikopo kutoka kwa mataifa yaliyowafanya watumwa na kuwakalia kikoloni.
      • Waafrika kukosa utaratibu mwafaka wa uwekezaji. Badala ya kutumia walichonacho kuanzisha mbinu msingi ambazo zitachangia uimarishaji wa uchumi, wao hununua magari na ndege za kifahari ili kubeba viongozi. (zote  3 x 1 = 3)
    5.  
      • Waafrika kuelewa kuwa maendeleo ya bara lazima yaongozwe na kudhibitiwa na wao wenyewe.
      • Waafrika waache kuombaomba misaada kutoka kwa wakoloni waliowafanya watumwa na kupora malighafi.
      • Waafrika kuacha tabia ya  utegemezi. Wajue kuwa wanapodharau kilicho chao na walichozalisha wanaendeleza umaskini barani.
      • Waafrika kuunda muungano mmoja wa kiuchumi ambao utaweza kutafuta soko na kutetea bei za bidhaa kutoka Afrika. Hii itapunguza taifa moja kupunjwa kwani huwa halina nguvu ya kutetea haya.
      • Waafrika kupanga mambo yao kwa kubainisha mahitaji yao na kuyapa kipaumbele. Mambo ambayo yataendeleza kustawisha uchumi wa bara yawe katika mstari wa mbele. Rasilmali zitumike kugharamia haya badala ya kutumiwa kwa mambo yasiyokuwa na umuhimu kiuchumi.
      • Waafrika kuanzisha viwanda vitakavyotengeneza na kusindika bidhaa kikamilifu. Viwanda visiwe ni vya shughuli zinazohusisha kilimo tu bali shughuli mbali mbali.
    6.  
      1. Kuselelea – kuishi hivyo daima
      2. Mabeberu – wakoloni (alama 2
  2. UFUPISHO (Alama 15)
    1. Kwa kurejelea aya tano za kwanza, eleza matatizo ya kiafya yanayoweza kupatikana kwa kutofanya mazoezi (ala.8)
      • Hatari ya kufa mapema
      • Kukosa/ukosefu wa nguvu za kufanya kazi zinazohitaji nguvu
      • Bila mazoezi sehemu hizi zitashindwa kukumbuka/kusahau mambo kwa kutoundwa kwa seli mpya
      • Kushindwa kufanya maamuzi na kusuluhisha matatizo
      • Matatizo ya moyo k.v kushindwa kupiga damu ili kuisambaza mwilini
      • Mwili hushindwa kupambana na magonjwa k.v kisukari, shinikizo la damu na kiharusi
      • Hawezi kuthibiti uzani wa mwili/kujinenepea/kushindwa kuhoma kalori zisizohitajika.
      • Mwili huorora /hudhoofika /umbo la mtu halipendezi/kuharibika kwa umbo.     (Hoja zozote 8x1= alama 8)
    2. Fupisha ujumbe wa aya tano za mwisho kwa maneno 80
      • Mazoezi husaidia kujenga misuli inayowezesha kufanya kazi kwa muda mrefu bila kuchoka.
      • Husaidia kusukuma hewa yenye vurutubisho na kusaidia kufanya kazi vyema.
      • Husaidia kujenga mifupa.
      • Hukawiza kuchafuka kwa mifupa.
      • Huimarisha mwili na kuufanya kunyumbuka.
      • Huleta utulivu wa akili.
      • Hudhibiti unyong’onyevu/hupunguza dalili za unyong’onyevu.
      • Husaidia kupata usingizi.
      • Huwezesha mwili kuwa na hamu ya kutenda kazi.     Hoja zozote 5x1 = alama 5)
  3. MATUMIZI YA LUGHA
    1. Mwalimu anamsahihishia Kamene zoezi (1x2=2)
    2.  
      1. Mkao wa midomo
      2. Mahali katika ulimi
      3. Ulimi huwa wapi kinywani  (3x1=3)
    3. Ni mofimu ambayo hujisimamia na kuwa na maana kamilifu. Mfano baba, mama, sana, mno n.k. (Maana alama I  Mfano alama 1)
    4. Sauti, silabi, neno na sentensi (½x4= 2)
    5.  
      1. Ni tungo la kisarufi lenye muundo wa kiima na kiarifa na hupatika katika sentensi (1x1=1)
      2. Kitabu kilichonunuliwa dukani ni changu au Ng’ombe ambaye anaugua atatibiwa leo (1x2=2)
    6. Mvule alikuwa bwenini (1x2=2)
    7. Nanyi- ufupisho wa nafsi
      Nendeni- kuonyesha wingi
      Kinyama – kuunda kielezi cha namna mfanano
      Kwa – kuonyesha sababu (½x4 = 2)
    8. Teo lililonunuliwa limezeeka (½x4 = 2)
    9. Unaweza kwenda uwanjani sasa madhali umekamilisha kazi yako (1x2=2)
    10.  
      1. jiwa
      2. chika (2x1=2)
    11. Baba aliwanunua ng’ombe wawili mwaka ’10 (2x1=2)
    12. Ukilipa uingie ndani (2x1=2)
    13. LI- YA (1x1=1)
    14. “Hirshi, nakuomba uje hapa nilipo ili nikutume,” Kassim alisema. (1x2=2)
    15.  
      SwaPP22022SRAnso 
    16. Mwalimu/mdarisi/ustadhi aliwashauri wanafunzi kuwa juhudi huzaa fanaka/mafanikio (3x1=3)
    17. Jasirisha (1x1=1)
    18. Anza shughuli/ anza jambo (1x1=1)
  4. ISMU JAMII
    Hali ya lugha ya Kiswahili nchini Kenya baada ya uhuru
    1. Kiswahili kinafundisha  shuleni ;inatahiniwa kama somo la lazima katika shule za msingi  na sekiondari. Pia kinafundishwa katika vyuo vikuu
    2. Kinatumika katika utantgazaji katika vituo vya utangazaji
    3. Ni lugha rasmi
    4. Serikali inatumia sambamba na Kiingereza katika kusambazia hati za serikali
    5. Kinartumika kuendesha shughuli za kitawala katika vituo vya polisi , mahakamani n.k
    6. Kinatuika kaika shughukli za kidini
    7. Kina tumika katika shughuli za sanaa , maonyesho na muziki
    8. Wanasiasa waniona afadhali katika mikutano ya hadhara                                    (zozote 5x2 =10)
      Kuadhibu
      1. Ondoa  ½ alama kwa kosa la hijai(h) litakeapo kwa mara ya kwanza had ikufika makosa  4, yaani  alama 2  kwaswali la lazimna
      2. Ondoa  ½ alama kwa kosa la sarufi (S) litokeapo kwa mara ya kwanza hadi kufika makosaa 4, yani alama 2 kwa swalila lazima
 
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Sunrise 2 Evaluation Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?