Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sunrise 2 Evaluation Mock Exams 2022

Share via Whatsapp
Maagizo
  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la LAZIMA.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani: tamthilia, Riwaya, hadithi Fupi, shairi na Fasihi Simulizi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: RIWAYA (CHOZI LA HERI)
Jibu swali la 1 au 2

  1. “Kumbe hata mja akafanikiwa vipi kielimu na kitaaluma, maisha yake huwa ombwe bila mwana, awe wa kuzaa au wa kulea?”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
    2. Taja tamathali moja iliotumika katika dondoo (alama 1)
    3. Onyesha ukweli wa kauli hii ukirejelea wahusika wowote watano riwayani (alama 5)
    4. Fafanua umuhimu wa elimu katika jamii ukirejelea riwaya nzima. (alama 10)
  2. “Una bahati kupata mfadhili, mimi mzazi wangu wa pekee ni mama ambaye ni muuza samaki na baada ya ule mzozo… biashara imepigwa na mawimbi makali.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo (alama 4)
    2. Taja tamathali moja iliotumika katika dondoo (alama 1)
    3. Jadili jinsi mwandishi alivyoshughulikia maudhui ya ufadhili. (alama 6)
    4. Ukirejelea hadithi zozote tano riwayani, onyesha jinsi mwandishi alivyotumia mbinu ya hadithi ndani ya hadithi kujenga maudhui.(alama 10)

SEHEMU YA B - FASIHI SIMULIZI

  1. Niaje wazungu wanaweza kutunza vitu vikajaa kwenye friji.  Yani nimeweka soda mbili tu kwenye friji lakini haitulii hadi nizinywe.  Niko sebuleni nazunguka tu.  Najaribu kuwaza  vitu vingine lakini wapi akili inaniambia “My friend kunywa soda”.
    1. Taja na ueleze maana ya kipera hiki (alama 4)
    2. Utanzu wa kipera hiki huweza kuchukua nafasi muhimu katika fasihi simulizi.  Thibitisha kwa hoja zozote sita.               (alama 6)
    3. Ufanisi wa uwasilishaji wa utanzu huu unategemea fanani.  Tetea kauli hii.   (alama 4)
    4. Ni changamoto gani zinaweza kumkabili mwanafasihi nyanjani? (alama 4)
    5. Dokeza umuhimu wa kukusanya data nyanjani. (alama 4)

SEHEMU YA C - TAMTHILIA: KIGOGO na Pauline Kea

  1. “Udongo tungeliuwahi uli mbichi.  Limekuwa donda ndugu sasa.  Waliota ikakita na wakamea hata pembe.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.   (alama 4)
    2. Taja na kueleza tamathali moja ya usemi inayojitokeza kwenye dondoo hili.   (alama 2)
    3. Eleza sifa zozote nne za msemaji wa kauli hii.  (alama 4)
    4. Dondoo hili linadhihirisha jinsi baadhi ya Wanasagamoyo walivyoshiriki kuivunja jumuiya yao.  Fafanua.            (alama 10)
  2. “Wananchi katika mataifa ya Afrika wanakumbwa na tatizo la uongozi mbaya.”  Thibitisha ukweli wa kaui hii kwa mujibu wa Tamthilia .            (alama 20)

SEHEMU YA D HADITHI FUPI YA TUMBO LISILOSHIBA ( Swali la 6)
Robert Oduori: Kidege

  1.  
    1. Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo: alama 12
      ‘‘ Ndege akaamua kuwafunganisha ndoa. Ndiyo, ndoa hufunganishwa mbinguni. Kama mbingu ni huko juu, basi ndipo alipotua huyo Chiriku – ndege mdogo mwenye rangi ya kupendeza na mwenye nyimbo za peponi. Ukimlinganisha na tai, basi yeye ni kidege tu chenye madaraka madogo ya kuwafunganisha ndoa Joy na Achesa huko mbinguni juu ya mtu kulikotua. Kwa makini alidondosha kitone cha majimaji. Kikalenga kwenye pua, chwa! Achesa na Joy walishtuka. Wakatazama juu. Ndege akaruka. Mose alicheka sana pale alipokuwa. Waliokuwa wakilishana huba walitazamana. Wakabaki wanachekana, ama wanachekacheka ovyo tu.

      Wengi kamka hao walizoea bustani hii. Walizuru hasa baada ya shughuli nyingi za mchana kutwa. Shughuli za kujenga na  kubomoa. Kubomoa , hili hawalipendi baadhi ya binadamu ingawa wengine wanalipenda sana. Hata yule anayejua kwamba anabomoa atasema anajenga. Mimi nikubali hivyo. Au wewe waonaje?
      Ali Mwalimu Rashid: Mkubwa
    2. “… Basi niache nitafute pesa. Muhimu mniunge mkono…”
      Fafanua athari ya vitendo vya mzungumzaji wa maneno haya katika jamii (alama 8)

SEHEMU D:USHAIRI
Jibu swali 7 au 8

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

    Hizi bombo mwaanika, wa ndizini nashtuka,
    Peupe mwazianika, kwenye jua kukauka,
    Zingine zimeraruka, aibu zinatufika,
    Anikeni kwa kuficha, za ndani mkisafisha.

    Nako kule kwenye bafu, mwaziweka hizo chafu,
    Hilo nalo nakashifu, mkitoa nitasifu,
    Kuziweka maji chafu, hilo ndilo ninahofu,
    Anikeni kwa kuficha, za ndani mkisafisha.

    Kwenye meza wazileta, wana wenu wakipata,
    Wageni wakijateta, aibu haitatupata?
    Muondoeni utata, hizo zenu twazipata,
    Anikeni kwa kuficha, za ndani mkisafisha.

    Kwa heshima tudumuni, tufaapo za mwilini,
    Tamaduni jifunzeni, msiige uzunguni,
    Za bafuni zi jikoni, zi watoto makononi,
    Anikeni kwa kuficha, za ndani mkisafisha.

    Wino wangu kibindoni, nitatua tamatini,
    Za ndani ziwe za ndani,msonyeshe hadharani,
    Za bafuni si jikono, msiweke kabatini,
    Anikeni kwa kuficha, za ndani mkisafisha.
    MASWALI
    1. Pendekeza kichwa mwafaka katika shairi hili.    (alama 1)
    2. Eleza toni ya shairi hili.   (alama 1)
    3. Tambua nafsineni katika shairi. (alama 1)
    4. Jadili matumizi ya mitindo ifuatayo ya lugha katika shairi hili.
      1. Kinaya     (alama 2)
      2. Usambamba   (alama 2)
      3. Balagha          (alama 1)
    5. Onyesha kuwepo kwa uhuru ufuatao katika shairi.     (alama 3)
      1. Tabdila
      2. Kubananga sarufi
      3. Inkisari
    6. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha mjazo.              (alama 4)
    7. Eleza muundo wa shairi hili.                                      (alama 5)
  2. YALIMWAGIKA

    Lilianza kama wazo, nikawaza,
         Niwe na watoto,
    Si vikwazo, ghafla mama yao akapatikana,
        Kwa rutuba yake,
           Akavimba
          Kumbe ni mapacha,
              furaha!

         Majina walishapewa,
    Imani kudumu, watazaliwa,
           Tungo wakatungiwa,
             Amani na Imani,
        Baba yao ni malenga
            Anatayeita maneno.
             Maneno yanaitika.
                   Nikasubiri.
    Wazazi walitamani kupakata,
                  Amani na Imani
    Iwe yao burudani, siyo kama zamani
               Wachezee zuliani.
             Baba niwaweke kifuani
     Na migongoni bila susu, kwa mama yao
       Si mtoto hutizama kisogo cha ninake?
                 Tukangoja!
    Furaha kote nyumbani iliwatanda,
       Kuyaona makinda yao, kwa kitanda,
       Wadondokwe udende, wawapende!
    Mama anyonyeshe, kiwatazama machoni,
       Kuwagusa mashavuni, waliapo.
    Watulie Amani na Imani.

      Ukutani ni kiwimbo, baba alishawatungia,
    Kushotoni ni wa kike, kuumeni kijanadume
                 Watulie, Baba yao aliwazia
                   Wazo likaanza kupokwa.
                       Hospitali wakiwasili.

    Wiki zikajenga miezi
      Tamati ikajongea
    Kawanunulia mavazi
         Walifaa kuvaa
           Hawakuvaa!
    Vijulanga miezi saba, pukachaka!
       Kifo ni mwewe, kikaninyakulia.
              Amani na Imani.
                      Tunalia!
               Pema peponi wanetu!
    MASWALI
    1. Eleza jinsi usimulizi ulivyotumika kwenye shairi.   (alama 1)
    2. Eleza sifa tatu zinazoafiki shairi hili kuwa huru.      (alama 3)
    3. Shairi hili ni la tanzia. Thibitisha.                             (alama 1)
    4. Tambua mandhari ta tanzia.       (alama 1)
    5. Tambua nafsineni kwenye ubeti wa kwanza.     (alama 1)
    6. Eleza toni ya shairi.     (alama 2)
    7. Onyesha mifano miwili ya matumizi ya sadfa katika shairi.   (alama 3)
    8. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha tutumbi.     (alama 4)
    9. Eleza maana ya msamiati huu kulingana na shairi.   (alama 4)
      1. Vijulanga
      2. Susu
      3. Akavimba
      4. Kiwimbo


MARKING SCHEME

SEHEMU A: RIWAYA (CHOZI LA HERI)

  1.  
    1. Muktadha wa dondoo (alama 4)
      • Msemaji ni Mwangeka
      • Anajisemea kimoyomoyo ( uzungumzi nafsi)
      • Yeye na Neema wako katika afisi ya Annastacia katika kituo cha watoto cha Benefactor
      • Wamekwenda kumchukua mwanao wa kupanga (Mwaliko) baada ya kukosa kufanikiwa kuwa wan a mwana wa kuzaliwa. Wanamlea kwa tunu na kumsomesha hadi chuo kikuu.
    2. Tamathali moja (alama 1)
      • Istiara- maisha huwa ombwe
    3. Ukweli wa kauli (alama 5)
      1. Selume – amehitimu kuwa mkunga na kuajiriwa kama muuguzi katika hospitali kuu ya Tumaini na hatimaye katika kituo cha Afya cha Mwanzo Mpya.
        Maisha yake yanaonekana kuwa ombwe baada ya kutengana na mumewe ambaye anachukua binti yao Hajui kama atakutana na mwanawe Sara baada ya mumewe kuoa msichna wa kikwao
      2. Ridhaa- amehitimu katika taaluma ya udaktari na kufanikiwa maishani. Ni mkurugenzi, mfanyi biashara mkubwa na anamiliki hospitali ya Mwanzo Mpya
        Maisha yake yanaonekana kuwa ombwe anapopoteza mwanawe Dede na Tila baada ya jumba lake kuchomwa na mzee Kedi. Anapomkumbuka Tila anatokwa na machozi yanayolovya kifua chake.
      3. Mwangeka- amehitimu katika taaluma ya uhandisi, anajiunga na vikosi vya usalama na kupanda ngazi hadi juu.
        Maisha yake yanakuwa ombwe anapompoteza bintiye Becky katika mkasa wa moto, anabaki katika upweke mkuu. Anajuta kutofuata ushauri wa mkewe Lily. (uk62)
        Apondi anapoamua kumlea Umu, Mwangeka anamwona Umu kama Baraka kutoka kwa Mungu, fidia ya mwanawe aliyekufa. (uk 118)
      4. Neema na Mwangemi- Neema amehitimu katika taaluma ya uhasibu na ameajiriwa katika Hazina ya Kitaifa kama hasibu mwandamizi na Mwangemi ana shahada ya uzamili katika uuguzi. Miaka mitano katika ndoa bila mtoto inawahuzunisha, wanachekwa kuwa Neema hawezi kulea mimba.
        Maisha yao yanakuwa ombwe wanapompoteza mwanao Bahati kutokana na ugonjwa wa sickle-cell.
        Hatimaye wanaamua kupanga mtoto, wanajaliwa kupata Mwaliko (uk 159-167)
      5. Naomi- anamwacha Lunga na kwenda kutafuta riziki baada ya Lunga kupoteza kazi na mali yake.
        Hatimaye anajuta kuwatelekeza wanawe, anawatafuta kote na anapata habari kuwa Dick na Mwaliko waliibwa na Sauna anahuzunika.
    4. Umuhimu wa elimu  (alama 10)
      1. Chombo cha kueneza amani na upendo (uk 11)
        Mamake Ridhaa anamtuliza Ridhaa baada ya kusimangwa na wanafunzi wenzake shuleni na kumshauri kuwa ni vyema kujifunza kuishi na wenzake bila kujali tofauti za ukoo na nasaba. 
      2. Nyenzo ya kumfikisha binadamu kwenye kilele cha ufanisi (uk 11)
        Mwangeka, Ridhaa, Mwangemi, Lunga n.k wanafanikiwa maishani kutokana na elimu.
      3. Chanzo cha umilisi na stadi za kujitegemea (uk 21)
        Kijana mmoja wakati wa vurumai baada ya uchaguzi analalamikia uongozi duni unaohimiza elimu duni isiowasaidia vijana. Anasema elimu inafaa kuwafunza ujasiriamali ili waweze kujiajiri na kujitegemea.
      4. Nyenzo ya kuzindua jamii. (uk 38-39)
        Shuleni Tila wanafunzwa kuhusu mabadiliko, uwajibikaji wa mtu usipimwe kutokana na jinsia. Mwekevu anachaguliwa kama kiongozi baada ya jamii kuzinduliwa.
      5. Nyenzo ya kutoa maarifa ya kuendeleza jamii. (uk 67-68)
        Lunga anatumia elimu katika kilimo kuwaelimisha raia kuhusu mbinu bora za kilimo
      6. Nyenzo ya kuleta mabadiliko. (uk 97)
        Mwanaheri anajiunga na shule ya Tangamano kwa lengo la kuandama elimu ili aweze kuleta mabadiliko katika jamii.
      7. Nyenzo ya kuwaokoa vijana kutokana uovu. Uk88
        Hazina anaokolewa kutokana na kinamasi cha uvutaju gundi na matumizi ya mihadarati anapopelekwa shuleni katika mradi wa serikali.
      8. NJia ya kukabiliana na changamoto za maisha (uk 88)
        Hazina anapata kazi katika hoteli , wengi wao (watoto wa mtaani)ni maseremala, waashi na mafundi wa juakali baada ya kuelimishwa.
      9. Nyenzo ya kuondoa mwemeo wa mawazo/huzuni (uk92)
        Wasichana katika shule ya Tangamano wanatumia fursa hiyo kusimulia juu ya maisha yao na kuliwazana. Walimu pia wanawaliza wanafunzi wao na kuwapa matumaini..mf Mtawa Pacha anamliwaza Zohali.
      10. Chanzo cha kuboresha miundo msingi katika jamii
        Ridhaa anajenga kituo cha afya cha Mwanzo Mpya.
        Serikali inajenga makao ya watoto pamoja na shule ili kufadhili elimu.
      11. Kigezo cha kupima uwajibikaji
        Neema anakiokota kitoto barabarani kwani alielewa haki za watoto.
        Mwangeka anamshauri Dick kuacha ulanguzi wa dawa za kulevya na pia anakubali uamuzi wa Apondi kumlea Umu.
        Mwekevu anaikwamua jamii kwa miradi ya maji kinyume na wagombea wenza
         
  2.  
    1. Muktadha wa dondoo  (alama 4)
      • Msemaji ni Kairu
      • Anamwambia Umu
      • Bwenini, shule ya Tangamano pamoja na wanafunzi wengine; Zohali, Chandachema na Mwanaheri.
      • Baada ya Umu kusimulia hadithi yake na jinsi alivyopata ufadhili katika makao.
    2. Tamathali
      • Msemo - kupigwa na mawimbi makali - changamoto
    3. Maudhui ya ufadhili (alama 6)
      1. Shirika la Makai Bora lilijitolea kuwajengea wakimbizi nyumba bora.
      2. Misikiti na makanisa yalikusanya magunia ya vyakula kuwalisha wakimbizi. (CWA, Woman’s Guild, Mothers Union)
      3. Serikali inajenga makao ya watoto wa mtaani na kufadhili elimu yao. Mf Hazina (uk 88)
      4. Serikali inazindua hazina ya kufadhili masomo ya watoto (Idara ya Watoto). Mf Umu (uk 89)
      5. Kituo cha Wakfu wa Mama Paulina kinawafadhili watoto wa mtaani kama Zohali.
      6. Familia ya Bw. Tenge inamfadhili Chandachema kwa kukubali kuishi naye anapopata nafasi katika shule ya Msingi ya Kilimo (uk105)
      7. Shirika la kidini la Hakikisho la Haki na Utulivu lilimpeleka Chandachema katika makao ya Jeshi la Wajane (uk 107)
      8. Ridhaa anawasomesha wapwaze Mzee Kedi .
    4. Matumizi ya mbinu ya hadithi ndani ya hadithi kujenga maudhui. (alama 8)
      1. Hadithi ya Billy na Sally (uk 80)
        • mapenzi na ndoa -usaliti -utabaka
      2. Hadithi ya Lemi na Tindi (uk 121)
        • Anasa -ukatili/ mauaji
      3. Hadithi ya Pete (uk 146)
        • Ndoa (migogoro) -malezi duni -utamaduni ( tohara,ndoa za lazima)
        • taasubi ya kime -ajira duni -ukatili/uavyaji mimba
      4. Chandachema (uk 102)
        • elimu -tanzia/mauti -ukiukaji wa haki za watoto( malezi duni, ajira)
        • umaskini -ukware
      5. Hadithi ya Zohali (uk 98)
        • utabaka -elimu -malezi duni/kutowajibika/ ukiukaji wa haki za watoto
        • majuto -changamoto za vijana( mimba za mapema)
      6. Hadithi ya Mwanaheri (uk 93)
        • elimu -ndoa na changamoto zake
        • ukabila -majuto -mauti
      7. Kairu (uk 91)
        • tanzia -utamaduni -ukimbizi
        • umaskini -malezi duni

SEHEMU YA : B Fasihi simulizi 

  1. Niaje wazungu wanaweza kutunza  vitu vikajaa kwenye friji.  Yani nimeweka soda mbili tu kwenye frijilakini akili haitulii hadi nizinywe. Niko sebuleni nazungukz tu . Najaribu kuwaza vitu vingine lakini wapi akili inaniambia ‘’ My friend, kunywa soda”
    1. Taja na ueleze maana ya kipera hiki.                    AL 2
      • Kichekesho
      • Ni mchezo mfupi  ambao hupitisha ujumbe kwa njia au namna ya kuchekesha.
    2. Utanzu wa kipera hiki huweza kuchukua nafasi muhimu katika fasihi simulizi. Thibitisha kwa hoja zozote sita    AL 6
      • Huburudisha watazamaji na waigizaji wenyewe. Burudani hii mara nyingine hupumbaza.
      • Huhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii kama vile upashaji tohara, matambiko, majigambo, ngoma, miviga na michezo ya watoto hudumishwa kupitia maigizo
      • Ni kitambulisho cha jamii; kila jamii ina Sanaa ya maigizo ya jamii husika. Miviga na sherehe za arusi na mazishi hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
      • Hukuza umoja na ushirikiano wa watu wanapojumuika kushiriki katika maigizo. Hao hujitambulisha kama jamii moja.
      • Ni nyenzo za kupitisha maarifa na amali za jamii kupitia michezo ya jukwaani. Husawiri mtazamo wa jamii kuhusu masuala mbalimbali kama vile woga, wizi na usaliti.
      • Hukuza ubunifu madhalan watoto wanaposhiriki michezo ya watoto, hujifunza kubuni michezo wakiwa wachanga na pia Sanaa ya uigizaji.
      • Hukuza kipawa cha uongozi katika michezo, huweza kujifunza stadi za uongozi
      • Ni njia ya kuimarisha urafiki. Kwa vile mizaha na utani katika malumbano hukuza urafiki na uhusiano bora
      • Huongoza jamii kupambana na na mazingira wanamojipata. Kutegemea imani ya wanajamii,matambiko yanaweza kuondoa matatizo katika jamii kama vile njaa, ugonjwa na ukame kwa kuomba Mungu
      • Maigizo huelimisha kupitia maudhui na hulka za waigizaji na kushauri nafsi zao, kuiga au kukashifu hulka hizo.
    3. Ufanisi wa uwasilishaji wa utanzu huu unategenea fanani. Tetea kauli hii.   (Alama 4)
      • Huwa mchangamfu na mcheshi kwa hadhira yake ili kuwafanya wapendezwe na hadithi
      • Anafahamu utamaduni wa jamii yake.
      • Anaifahamu hadhira yake vizuri na kusimulia kulingana na mapendeleo yao. wasichana au wavulana? vijana au wazee?
      • Huwa na uwezo wa ufaraguni - uwezo wa kubadilisha sehemu fulani za sanaa bila kujifunga na muundo asilia.
      • Mwenye kumbukumbu nzuri - uwezo wa kukumbuka
      • Mwenye uwezo wa kuigiza kwa kutumia viungo vyake, uso (ishara-uso) na sauti(kiimbo)
      • Mwenye uwezo wa kujenga taharuki kwa kusita kidogo ili kuvuta nadhari ya hadhira yake.
      • Hushirikisha hadhira yake katika nyimbo n.k
      • Mtambaji hodari na mkwasi wa lugha.
    4. Ni changamoto gani zinaweza kumkabili  mwanafasihi nyanjani?( Alama 3)
      • Gharama ya utafiti-huenda gharama ikwa kubwa kiasi cha mtafiti kutoimudu. Baadhi ya mafanani au wahojiwa huenda wakadai walipwe kabla ya kutoa habari zozote.hivyo ikiwa mtafiti hana hela basi utafiti wake utakwamizwa.
      • Mtazamo hasi wa wanajamii kuhusu ujazaji wa hojaji huenda ukawafanya wengi wao kutojaza hojaji zao. Wanajamii wengine huweza kushuku kwamba mtafiti anawapeleleza na wakakataa kutoa habari.
      • Vizingiti vya kidini amabavyo hutokea pale ambapo baadhi ya wahojiwa wanaamini kwamba matendo ya fasihi simulizi k.v matambiko na uimbaji wa taarabu yanaenda kinyume na imani yao ya kidini.
      • Uchache wa wazee au wataalamu wa fasihi simulizi ,kukosekana kwa wazee wanaoweza kutamba ngano ama kueleza vipera vingine k.v vitendawili.
      • Matatizo ya mawasiliano na uchukuzi ikiwa mkusanyaji analazimika kwenda mbali kukusanya habari,hasa katika sehemu kame itakuwa vigumu iwapo hana gari.
      • Ukosefu wa usalama ,huenda mkusanyaji wa fasihi simulizi akavamiwa ,baadhi ya watu si wakarimu na huenda wakamshuku mtafiti na kuvamiwa.
    5. Dokeza umuhimu wa kukusanya data nyanjani.                                         (Alama 3)
      • Ukusanyaji husaidia kurekodi na kuhifadhi tamaduni za jamii mbalimbali kwa nia ya kuzipitisha kwa vizazi vijavyo.
      • Ukusanyaji huiendeleza fasihi simulizi kwa kurekodi vipera vya fasihi simulizi
      • Husaidia kuziba pengo la utafiti liliopo.
      • Ukusanyaji zaidi wa data za fasihi simulizi hutumiwa kama kiunzi cha uchunguzi wa kulinganisha fasihi simulizi za jamii mbalimbali.
      • Humwezesha mwanafunzi kupata maarifa au stadi za kufanya utafiti katika taalima nyingine za kijamii kama vile sosholojia.
      • Humpa mwanafunzi nafasi ya kushuhudia na kuathiriwa moja kwa moja na utendaji wa fasihi simulizi

SEHEMU YA : C TAMTHILIA : KIGOGO na Pauline Kea

  1.  “Udongo tungeliuwahi uli mbichi. Limekuwa donda ndugu sasa. Waliota mizizi ikakita na wakamea hata pembe.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili.        (alama 4)
      • Msemaji ni Kenga
      • Anamweleza Majoka
      • Walikuwa ofisini mwa Majoka
      • Walikuwa wakizungumzia jinsi ya kuwakomesha watetezi wa haki
      • Majoka anaahidi kuwanyamazisha anaposema dawa yao anayo.   (4x1=4)
    2. Taja na kueleza tamathali moja ya usemi inayojitokeza kwenye dondoo hili.      (alama 2)
      • Methali- udongo uwahi uli mbichi- kumaanisha wangewakomesha wapinzani walipoanza utetezi wao (kabla ya kupata nguvu zaidi)
      • Msemo- ndonda ndugu- kumaanisha tatizo ambalo haliishi (anarejelea jinsi kuna Tunu wanang’ang’ania kupigania haki za wanyonge)
      • Nahau- ota mizizi na mea pembe- nahau hizi zimetumiwa kuonyesha jinsi watetezi walivyo imara katika utetezi wao
        ( Ya kwanza 1x2=2) (kutambua ni alama 1, maelezoalama 1)
    3. Eleza sifa zozote nne za msemaji wa kauli hii.        (alama 4)
      • Mbabedume/mwenye taasubi ya kiume - anaamini mwanamke hawezi kuwa shujaa Sagamoyo. Anashangaa sana Sudi anapomwonyesha kinyago cha shujaa wa kike alichokuwa akichonga.
      • Mpyaro - anamtukana Tunu kuwa yeye ni hawara.
      • Dhalimu - yeye na Majoka wanapanga vifo vya watu. Mfano ni mauajiyaJabali. Anapanga kuwaumiza watu kwa kutumia wahuni.
      • Fisadi – anajaribu kumhonga sudi kwa zawadi nyingi kutoka kwa Majoka. Aidha anapokea kipande cha ardhi ya pale sokoni alichomegewa na Majoka.
      • Mshauri mbaya - amnamshauri Majoka vibaya hasa kuhusiana na kutumia nguvu zaidi dhidi ya waandamanaji. Aidha anazua mpango wa kumtia Ashua kizuizini ili kumlazimisha Sudi kumchongea Majoka kinyago cha Ngao.
      • Mwenye majuto - anapozinduka, anakiri makosa yake ya kuwanyanyasa raia na kujiunga na wanasagamoyo
      • Msaliti - anamwacha Majoka na kujiunga na wanasagamoyo anapoona raia wanakaribia kufanya mapinduzi
        (Hoja 4x1=4)
    4. Dondoo hili linadhihirisha jinsi baadhi ya Wanasagamoyo walivyoshiriki kuivunja jumuiya yao. Fafanua.       (alama 10)
      Jinsi Wanasagamoyo walivyoivunja jumuiya yao
      • Ngurumo na wahuni wenzake kumshambulia Tunu na kumjeruhi vibaya.
      • Ngurumo kumsaliti Boza kwa kuzini na mkewe.
      • Kenga kumpa Majoka ushauri mbaya. Mfano, kufunga soko na kulipa kisasi dhidi ya wapinzani.
      • Majoka kumiliki kiwanda kikubwa zaidi cha kuzalisha sumu ya nyoka (dawa za kulevya zinazowahasiri vijana vibaya)
      • Majoka kuidhinisha ukataji wa miti- matokeo yake ni ukame na ukosefu wa chakula.
      • Majoka kutoa kibali kwa Asiya  cha kutengeneza na kuuza pombe haramu inayowapofusha na kuwaua watu.
      • Majoka kuwafurusha wachuuzi sokoni. Ananyakua ardhi hiyo ili ajenge hoteli ya kibinafsi.
      • Majoka kuwapa wafanyakazi nyongeza ndogo ya mshahara huku akipandisha kodi
      • Uongozi wa Majoka kuwasaliti vijana kwa kutowapa ajira baada ya kufuzu mfano ni Tunu, Ashua na Sudi.
      • Viongozi kama Kenga kuwa na makundi haramu kama vile Kenga kuonekana akiwahutubia wahuni chini ya mbuyu.
      • Majoka kukopa pesa kutoka nje na badala ya kuendeleza maendeleo, anafuja pesa hizo kwa mradi wa kibinafsi wa uchongaji vinyago. Pesa hizo zitalipwa na umma kwa kipindi cha miaka mia moja.
      • Kampuni ya majoka kupandisha bei ya chakula kwenye kioski. Hii ni baada ya kulifunga soko.
      • Wizi wa kura- Majoka anazua mbinu za wizi wa kura kwa kuhofia ushindani na aendelee kusalia mamlakani.
      • Majoka kuwagawia wandani wake raslimali za umma. Mafano, Kenga anapewa kipande cha ardhi ya sokoni.
      • Ngurumo na walevi wenzake pale mangweni wanamdhalilisha Tunu. Anamweleza hawezi kumpigia kura, heri amchague paka kama si Majoka.
      • Majoka kuwatamani wanawake wengine licha ya kuwa na mke.
      • Majokma kuvitumia vyombo vya dola kudhulumu raia. Anawatumia polisi kuwaua vijana watano waliokuwa wanaandamana ili kupinga nyongeza ya bei ya chakula kwenye duka la kampuni.
      • Majoka kumchochea ashua dhidi ya mumewe Sudi- nia yake ni kuwatenganisha.
      • Majoka kupanga kukifunga kituo cha Runinga ya Mzalendo kinachowazindua wanasagamoyo kuzifahamu haki zao.
        (Hoja zozote 10x1=10)
  2. Tamthilia ya Kigogo
    1. Unyakuzi wa mali ya umma – Majoka anaamua kulifunga Soko la Chapakazi ili kujenga hoteli ya kifahari.
    2. Ubinafsi – Majoka anavibomoa vibanda vya Wanasagamoyo na kupanga kujenga hoteli yake ya kifahari.
    3. Utepetevu/ukosefu wa uwajibikaji – wananchi wanalipa kodi lakini wanakosa huduma kusafishiwa soko na huduma za maji taka.
    4. Vitisho – Majoka anatisha kumfuta Kingi kazi
    5. Viongozi wamekosa maadili ya kikazi – Majoka anamrai Ashua mkewe Sudi ili aendeleze ufuska naye.
    6. Kuwatesa wapinzani – Tunu na Sudi wanateswa lakini wanaendelea kupigania mageuzi
    7. Kuvunja sheria – Majoka anampa Mamapima kibali cha kuuza pombe haramu ambayo ni kinyume na katiba
    8. Wizi wa kura –Majoka anasema kuwa hata wasipompa kura atashinda
    9. Ubaguzi katika utoaji wa kandarasi  - kandarasi ya kuoka keki inatolewa kwa Asiya ambaye ni mke wa Boza
    10. Matumizi mabaya ya pesa za umma – pesa zinatumiwa katika shughuli za kuchonga vinyago
    11. Utawala wa kiimla na wa kutojali – Wanasagamoyo hawana usemi wowote; Majoka anasema kuwa atajenga hoteli watu wapende wasipende
    12. Mauaji ya kikatili – watu wasio na hatia wanauawa; Jabali
    13. Kuzwazulia watu wasio na hatia  - Ashua anazuiliwa na Majoka bila kosa lolote
    14. Wanasagamoyo wanakabiliwa na unyonyaji – bei ya chakula kwenye kioski cha kampuni imepanda maradufu tangu soko lilipofungwa
    15. Kuwanyima wanasagamoyo haki ya kaundamana – wanaharamisha maandamano
    16. Unasaba – Majoka anamwajiri Kenga ambaye ni binamuye kama mshauri wake mkuu
    17. Viongozi wanatumia nafasi zao kuwaangamiza vijana  - matumizi ya dawa za kulevya – wanfunzi katika shule ya Majoka Academy wadungana sumu ya nyoka
    18. Utapeli  - Kuwaongezea  walimu mshahara na wauguzi na kuongeza kodi
    19. Kurithisha uongozi – Majoka anapanga kutambulisha Ngao Junior kuwa kiongozi mpya mpya badala ya Wanasagamoyo kumchagua kiongozi wao
    20. Kuruhusu biashara ya ukataji wa miti -
    21. Matumizi mabaya ya vyombo vya dola – polisi wanatumiwa kuwatawanya waandamanaji

SEHEMU YA D  HADITHI FUPI

  1.  
    1. MBINU ZA KIMTINDO
      • Msemo – funganisha ndoa
      • Chuku – kama mbingu ni huko juu basi ndiko alikotua huyo chiriku
      • Ulinganishaji/ urejeleaji – ukimlinganisha na tai, basi yeye ni kidege tu
      • Stihizahi – yeye ni kidege tu
      • Tanakali ya sauti – chwa !
      • Nidaa – chwa !
      • Lakabu – Mose
      • Taswira oni – walitazamana
      • Tasfida – walilishana huba
      • Tanakuzi – kujenga / kubomoa
      • Takriri – kubomoa
      • Ukinzani wa kauli – hata yule anayejua kwamba anabomoa atasema anajenga
      • Kinaya - hata yule anayejua kwamba anabomoa atasema anajenga
      • Swali balagha – au wewe waonaje ?
    2. Athari ya vitendo vya mzungumzaji wa maneno haya na wenzake katika jamii     (alama 8)
      Mzungumzaji ni Mkubwa. Vitendo vyake vinajikita katika ulanguzi wa dawa za kulevya. Dawa hizi zinaiathiri jamii (vijana) kwa njia zifuatazo.
      • Huwafanya vijana kutojielewa.  Mkubwa akielekea pwani kununua pweza, aliwakuta vijana waliokuwa wamelaliana kutokana na kutumia unga. Walikuwa kama kuku na vifaranga walioona mwewe (uk 142).
      • Huwafanya vijana kupotoka kimaadili. Mmpjawapo wa vijana waliotumia unga anamtisha Mkubwa kwa upyoro wake. Anamuuliza kama wanakula kwake na kumuita ‘makande’.  Mkubwa anakupuka mbio.
      • Huwafanya vijana kuwa na hisia zisizo za kawaida. Kijana mmoja anamtusi Mkubwa na kumlaumu kwa kumwangusha na ndege. Anasema kuwa alikuwa anakata kona anaenda kwa Obama.
      • Tamaa ya mali inawafanya viongozi kuwaonga wapiga kura ili wachagulie, bila ya kujali kiwango chao cha elimu. Mkubwa anauza shamba ilia pate milioni kumi za kuwaonga wapiga kura.
      • Vijana wanaoshikwa baada ya kutumia dawa walizouziwa na wakubwa  wanateswa. Wakiwa ndani hawana haki. Kula ni kifo, malazi ni kifo,kukoga ni kifo, kufua ni kifo, kila kitu ni kifo.
      • Dawa hizi zinasababisha ubaguzi mkubwa katika jamii. Viongozi matajiri wanaachiuliwa kwa ulanguzi wa dawa huku vijana maskini wakiendelea kukaa ndani. Mkubwa anafanya mazungumzo na mkuu wa polizi, Ng’weng’we wa Njagu na kesho yake Mkumbukwa anaachiliwa.
      • Dawa za kuelvya huwafanya watu kuwehuka. Katika ndoto yake, Mkubwa anawaona vijana wachafu wakifanyiana vitendo vichafu. Anawaona watu wamehamaki hawana raha. Wizi umezidi mitaani. Miongoni mwa viajana wale ‘wala unga’ ni watoto wake wa kiume. Anatoka mbio. Kawa chizi.

SEHEMU E: USHAIRI  

  1.  
    1. Pendekeza kichwa mwafaka.
      • Aibu, Aibu kwetu
    2. Eleza toni ya shairi hili
      • Toni ya kukasifu/kushtumu/kukejeli mienendo ya kutojali.
      • Toni ya kughadhabika Kwa kutojali.
      • Toni ya kushauri kuhusu heshima na usiri.
    3. Tambua nafsineni wa shairi
      • Mhusika ambaye amepata aibu kutokana na mienendo ya watu kuanika mavazi ovyo ambayo anahisi ni vibaya.
    4. Jadili matumizi ya mitindo ifuatayo
      1. Kinaya
        • Ni kinaya kuwa angependa mavazi fulani yafichwe ilhali yamefichwa bafuni.
        • Ni kinaya kuwa anataka zikauke bila kuanika /ilhali zimefichwa.
        • Ni kinaya kuwa wageni wanaibika ilhali wenyewe huzitumia na huanika kwao
      2. Usambamba
        • Miundo sawa  ya mistari/mishororo-anikeni kwa kuficha,z ndani mkisafisha.
        • Urudiaji wa maneno –anika,kuficha.
        • Urudiaji wa silabi-ka(ubeti wa kwanza) fu(ubeti wa pil) ta (ubeti wa tatu)
      3. Balagha
        • Ubeti wa mwisho mshororo wa pili-aibu haitatupata?
    5. Onyesha kuwepo kwa uhuru ufuatao katika shairi
      1. Tabdila – muondoeni badala ya mwondoeni.
      2. Kubananga sarufi - anikeni kwa kuficha,za ndani mkisafisha. Badala ya mkisafisha za ndani mzianike kwa kuficha.
      3. Inkisari - tufaapo badala ya tunapofaa.
    6. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha ya mjazo/Nathari.
      • Mshairi anasema kuwa nguo za ndani zinazoanikwa ovyo/popote,watoto/wana huzipata na kutembea nazo hata mezani kwa wageni.Hili huleta aibu kubwa na hivyo hushauri watu waanike kwa tahadhari.
    7. Eleza muundo wa shairi hili
      • Shairi hili lina beti tano.
      • Kila ubeti una mishororo minne.
      • Shairi hili lina kibwagizo ambacho ni :anikeni kwa kuficha , za ndani mkisafisha.
      • Idadi ya mishororo inatoshana kaika kila mshororo;kumi na sita.
      • Kila mshororo una vipande viwili, ukwapi na utao.
      • Vina vyake vinatofautiana  kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
  2. YALIMWAGIKA
    1. Eleza jinsi usimulizi ulivyotumika kwenye  shairi.
      • Ushairi umesimulia safari kabla ya ndoa na katika ndoa.
    2. Eleza sifa tatu  zinazoafiki shairi hili kuwa shairi huru.
      • Idadi ya mishororo katika kila ubeti si sawa.
      • Idadi ya vipande katika kila mshororo si sawa.
      • Idadi ya mizani katika kila mshororo  inatofautiana.
      • Limechukua miundo mbali mbali lilivyoandikwa.
      • Shairi hili halina kibwagizo.
      • Vina vyake vinachanganywa/halina mtiririko wa vina.
      • Shairi hili lina alama nyingi za uakifishaji.
    3. Shairi hili ni tanzia
      • Kuna kifo cha mapacha waliotarajiwa kuzaliwa na walisuburiwa sana na wazazi zao.
    4. Tambua mandhari ya tanzia
      • Hospitalini ndiko walikofia mapacha.
    5. Tambua nafsineni kwenye ubeti wa kwanza
      • Baba / bwana mtarajiwa/mwanamume.
    6. Eleza toni ya  shairi.
      • Toni ya huzuni /majonzi kutokana na kifo cha mapacha Amani na Imani
    7. Onyesha mifano miwili ya matumizi ya sadfa  katika shairi.
      • Baba anawaza kuhusu watoto na kumpata mke papo hapo wa kuoa.
      • Msemaji anasema  akataka’ watoto’ na ghafla  ujauzito unakuwa wa mapacha.
      • Watoto wanapewa majina Imani na Amani na baadaye mimba kugundulika ni ya mapacha  kiume na kike.
    8. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha tutumbi.
      • Muda uliendelea kusonga wakisubiri watoto wao kuzaliwa.
      • Wakanunuliwa mavazi mbalimbali wakitarajiwa kuwapokea japo halikutimia.watoto wakafa  mimba ikiwa ya miezi saba  na kuombolezwa.
    9. Eleza maana ya misamiati ifuatayo.
      1. Vijulanga -Vitoto
      2. Susu-kitambaa cha kuzuia haja za mtoto.
      3. Akavimba-akawa mjamzito
      4. Kiwimbo.- wimbo mfupi
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Sunrise 2 Evaluation Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?