Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kakamega Evaluation Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

MASWALI

 1. UFAHAMU (alama 15)
  Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali
  Wengi huchukia kutembea safari ndefu kwa kuogopa kuchoka.  Si ajabu kwamba njia za uchukuzi za kisasa kama vile boda boda zimekuwa maarufu sana hata kwa wanaofanya safari fupi. 
  Lakini wataalamu wa afya wanasema kuwa kwa kuepuka matembezi unajikosesha fursa ya kuimarisha uwezo wa ubongo  wako kukumbuka mambo. 
  Utafiti uliohusisha washiriki 120 ulithibitisha kuwa matembezi ya dakika arobaini pekee kwa siku yanatosha kuongeza uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu akilini, hata mtu anapozeeka. 
  Matembezi yaliongeza ukubwa wa eneo la ubongo ambalo huhusika katika uhifadhi wa habari na kumbukumbu katika  ubongo miongoni mwa walioshiriki. Utafiti huo uliofanywa kwa muda wa mwaka mmoja na matokeo yake kuchapishwa katika jarida moja la kisayansi yalionyesha kuwa mazoezi hayo yanaweza kukinga hata dhidi ya ugonjwa wa kusahau mambo maarufu kama ‘dementia.’ 
  Watafiti waliwagawanya washindi katika makundi mawili.  Waliokuwa kwenye kundi moja walitakiwa wawe wakitembea kwa muda wa dakika arobaini uwanjani mara tatu kwa wiki nao wengine walitarajiwa kufanya mazoezi ya kawaida tu, yasiyo makali ambayo yangechukua muda mfupi mfupi kama wa dakika tano au kumi tu. 
  Uchunguzi wa ubongo wao na matokeo ya mitihani ya uwezo wa kukumbuka ilifanywa  mwanzoni katikati na mwishoni mwa utafiti.  Utafiti ulionyesha kuwa ukubwa  wa eneo la ubongo linalotumika katika kukumbuka uliongezeka kwa asilimia mbili miongoni mwa watu waliozoea kufanya matembezi ya masafa marefu.  Eneo hilo la ubongo lilipungua kwa asilimia 1.4 katika wale waliofanya matembezi ya wastani, upungufu sawa na ule unaoshuhudiwa katika hali ya kawaida ya kuzeeka. 
  Makundi yote mawili yaliandikisha kuimarika katika mitihani ya uwezo wa kukumbuka, urefu wa kipindi cha mazoezi katika kundi lililofanya matembezi lilihusishwa na ongezeko la ukubwa wa sehemu hiyo ya ubongo. 
  Ingawa mtu hawezi kuzuia kupungua kwa sehemu ya ubongo ijulikanayo kitaaluma kama ‘hippocampus,’ kadiri mtu anavyozeeka.  Utafiti ulidhihirisha kuwa mazoezi ya muda mrefu yanaweza kuongeza ukubwa wake.  Mazoezi ya wastani yanaimarisha ubongo na kukinga mtu dhidi ya udhaifu wa ubongo unaotokana na kuzeeka.  Huu ni ushahidi mwingine unaonyesha kwamba mazoezi ya mara kwa mara na lishe bora hupunguza hatari ya maambukizi,uwezo wa kupoteza fikira na kumbukumbu uzeeni. Aidha,huimarisha uzingativu na umakinifu wa wahusika. Ni kwa mujibu wa matokeo ya tafiti kama hizi,waelekezi wenye ufahamu wanaoshughulikia vijana huhimiza vijana kukimbia au kutembea kwa kasi kutoka eneo moja au lingine wawapo shuleni.’Movement by Running’haiwi dhulma inayotendwa kinyume cha haki za vijana,bali inakusudiwa kuwafaidi wote.
  1. Eleza dhana ya wengi kuhusu matembezi.
  2. Ni thibitisho gani linaloonyesha kwamba matembezi hayathaminiwi?
  3. ‘Wasiotembea hujidhuru.’  Fafanua.
  4. Taja kiini cha ukosefu wa kumbukumbu ubongon
  5. Mazoezi huwa na mchango upi katika maisha ya binadamu.
  6. Eleza matokeo ya utafiti kwa makundi yote mawili
  7. Maneno haya yametumiwa kuleta maana gani kwenye kifungu?
   1. Utafiti
   2. Yaliandikisha
 2. UFUPISHO (alama 15) Mbooni west 2016
  Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.
         Ukitaka kufaulu maishani lazima ujue kuwa una kazi kubwa sana inayokungoja. Baada ya kuikabili vilivyo kazi hiyo kwa kutumia Nyanja mbalimbali utayaimarisha maisha yako. Karibu kila mtu aliyestawi amepitia katika vikwazo vingi tena vya kutatiza kuliko vikwazo wanavyovipata vijana wa kisasa. Vijana wote wanatakiwa sasa wasugue bongo zao sawasawa watende mambo mengi mazuri kuliko yale wanayoyaona. Wasitosheke na yale yaliyotendwa na wazee wao. Kila kijana iwapo atakuwa na moyo kama huo nchi zote zitaendelea kwa kasi.
  Kwa kujisaidia katika kujiendeleza, yafuatayo yanafaa kuzingatiwa.Vijana wanatakiwa wawe watoto wenye kuelewana na wazazi wao ambao watawaelekeza vyema kitabia na wakiwa ni wazazi waelewa, watawapa watoto wao maelekezo na radhi ambavyo ni bora kuliko mali.Watoto wenyewe wajue wanataka nini, wawe na malengo katika maisha yao na wakazanie kupata kile wanachokitaka bila kukata tamaa,watie bidii katika kila wanalolifanya, wapende kusoma bila kulazimishwa kwani kusoma kwa kulazimishwa hakumpi mja amani. Kutaka kushurutishwa ili usome ni sawa na ng’ombe apelekwaye mtoni kunywa maji naye akifika mtoni akatae kuyanywa . Mtoto mwenyewe  anatakiwa ajitafutie na ajue kuwa hasara ni yake asipofanya bidii na ajiamshe kifikira.Mtoto huyu asiridhishwe na kupokea vitu vidogo vidogo, kamwe asiwe mwenye tamaa wala kutazamia kupewa zawadi kama peremende na hela kila saa. Lazima ajue kuwa kupewa au kutopewa ni mamoja.Aelewe hali yao, wazazi wakiwa na kitu cha kumpa aone kwamba ni sawa! wakiwa hawana pia aone kuwa ni sawa.Mtoto anatikiwa kuwa muelewa. Anatakiwa awe na ile fikira ya kujitafutia. Hata kama anatoka katika aila yenye utajiri azoee kutafuta ili ikiwezekana atajirike hata zaidi.Asitegemee cha ndugu kwani huenda akafa akiwa maskini. Kidogo chako ulichokitolea jasho ni bora kuliko kikubwa cha mwenzio.
  Vijana wanatakiwa kuwa na nidhamu ya kiwango cha juu popote walipo. Wawe ni watu wenye kujiamini. Wasikate tamaa eti kwa ajili masomo ni magumu bali wakazane kutafuta jinsi ya kuyarahisisha ili kuyaelewa,hatimaye, watayamudu na wafanikiwe maishani.Yafaa vijana waelewa kuwa hakuna kizuri kinachopatikana kwa urahisi, daima dawamu wakumbushwe kuwa ‘Mtaka cha mvunguni sharti ainame’. Lazima wadhurike wakitaka kufanikiwa.Aidha wakumbushwe umuhimu wa kuwaheshimu watu na wakati. Wasiwadharau walimu au  wenzao, wasipoteze wakati wao kusengenya. Wawapuuze wanaowanyanyasa,wasizingatie hata neno moja la kuwaudhi wanaloambiwa na watoto waovu. Vijana wawe tayari kukosolewa na kuomba msamaha wa makosa yao. Wanapaswa wawe ni watu wanaowaelewa wenzao na kuchukuliana vyema nao, wawathamini wengine kwa vile walivyo.Wasithamini vitu vya anasa kupita inavyostahili; kama maisha ya starehe au mavazi ya kitajiri. Watoto wengi wasio na chochote wanaopuuza mambo ya anasa ndio wanaofaulu pakubwa katika maisha. Wenye tamaa hawafaulu kwani huishia kuwa wezi kwa kuwa na hamu ya kujipatia vya ubwete, mwisho wakajipata gerezani. 
  1. Fupisha aya ya kwanza kwa maneno 40-45. (alama 5)
   Nakala ya majaribio
   Nakala safi
  2. Bila kupotosha ujumbe uliokusudiwa na mwandishi, fupisha aya mbili za mwisho.(maneno 45 – 50) ( alama 10)  
   Nakala ya majaribio
   Nakala safi
 3. MATUMIZI YA LUGHA (alama 40) 
  1. Andika sentensi mbili kuonyesha matumizi tofauti ya kihisishi.  (alama 2)
  2. Linganisha sifa za sauti hizi : (alama 2)
   1. /e/ na /o/
   2. /p/ na /k/   
   3. /m / na /gh/
   4. /s/ na /r/
  3. Weka  shadda katika neno walakini na ubainishe maana mbili tofauti
  4. Ainisha mofimu katika neno mliowafurahisha
  5. Andika sentensi zifuatazo upya kulingana na maagizo.  (alama 3)
   1. Mwanafunzi anayejikakamua  huwaacha wazaziwe wakitumaini.
    Badilisha maneno yaliyokolezwa kuwa nomino dhahania.
   2. Watumbuizaji wengi waliipamba sherehe siku hiyo.
    Anza kwa ‘Sherehe’
  6. Andika sentensi ukitumia nomino hizi na visistizi ulivyoelekezwa.(alama 2)
   1. Sukari (karibu)
   2. chandarua (wastani)
  7. Unganisha sentensi hizi kuunda moja ya masharti.(alama 1) Mkulima amepanda mbegu ifaayo.Mkulima  atavuna mazao mengi.
  8. Andika sentensi ifuatayo katika umoja. (alama 2)
   Marubani waliyakwepa mawingu yale vyombo vikapaa angani.
  9. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao. (alama 2)
   nomino, kishazi tegemezi, kielezi cha wakati, kitenzi, nomino, kivumishi
  10. Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao hali ya kuendelea.(alama 1)
   Watahiniwa wengi wanautazamia mtihani kwa hamu kubwa. 
  11. Unganisha kuwa sentensi moja  kwa kutumia neno ‘lau’ (alama 1)
   Askari  wamekuja kwa ajili ya Mashaka.
   Askari wangempata Mashaka wangemkamata. 
  12. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya wastani. (alama 2)
   Buzi lake limekata jikamba likaingia jishambani na kula maboga.
  13. Bainisha kiima, kipozi kitondo na ala katika utungo huu .(alama 2)
   Babu alinyweshwa uji na Andai kwa kikombe.
  14. Bainisha vishazi katika sentensi hii.(alama 2)
   Mwanariadha aliyeanguka akikaribia utepe alituzwa.
  15. Tunga sentensi yenye muundo huu :S –KN(N+V)+KT(T+KN(N+V)+E
  16. Andika maana mbili zinazojitokeza katika sentensi hii(alama 2)
   Salire alimkimbilia Roda.
  17. Akifisha.
   mwalimu mkuu aliuliza anita umechelewa kwa nini 
  18. Kanusha
   Aliwahutubia wanafunzi, na walimu.
  19. Tunga sentensi moja kubainisha maana mbili za neno : kanda(alama 2)
  20. Bainisha chagizo na kijalizo katika sentensi hii.(alama 2) 
   Umma ulimpokea Bi.Vitendo, mtetezi wa haki za raia, kwa furaha. 
  21. Eleza jinsi kiambishi ji kilivyotumiwa katika sentensi hii.
   Jina la jitu linalohusishwa na ukataji  wa miti katika msitu huo halitajwi. (alama 2) 
 4. ISIMUJAMII (alama 10)
  Umepewa nafasi kuwahutubia washika dau kuhusu jinsi ya kuthibiti ongezeko la vijana wanaofikishwa mahakamani kwa sababu anuai.
  1. Bainisha  sajili utakayotumia.(alama 1)
  2. Andika huku ukifafanua vipengele vinne vya kimtindo vitakavyothibiti uteuzi wa lugha katika sajili hii. (alama 4)
  3. Fafanua majukumu matano yaliyokabidhiwa Kamati ya Inter-Territorial  Language Committee iliyotarajiwa kusanifisha Kiswahili. (alama 5)


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

 1.    
  1. Matembezi huchosha / huchukiza  ( tuza   1) 
  2.    
   1. Ongezeko la njia za uchukuzi wa kisasa mfano boda boda. 
   2. Kutegemewa sana kwa uchukuzi wa kisasa.
   3. Wengi hawapendi kutembea. (tuza 2 x 1 = 2) 
  3. Kujikosesha fursa ya;
   1. kuimarisha bongo zao na 
   2. uwezo wao  wa kukumbuka mambo ( tuza 2 x 1 = 2) 
  4.      
   1. Kuzeeka ( tuza 1 x 1 = 1) 
   2. Kutofanya mazoezi kwa wingi . 
  5.      
   1. Kuongeza uhifadhi wa habari na kumbukumbu ubongoni. 
   2. Kukinga dhidi ya ugonjwa wa ‘dementia’    
   3. Kuimarika kwa ubongo
   4. Kulinda dhidi ya kuzeeka kwa haraka  (tuza 3 x 1 = 3 )
  6.         
   1. Kuimarika kwa uwezo wa kumbukumbu.
   2. Ongezeko kubwa lilihusishwa na kundi lililofanya matembezi kuliko lile lililofanya ya kawaida. (tuza 2 x 2=4)
  7. Utafiti – uchunguzi(tuza 2 x 1 = 2) 
   Yaliandikisha – Yalibainisha /Yalidhihirisha/Yalionyesha  
 2.      
  1. Fupisha aya ya kwanza kwa maneno 40 -45. (alama 5)
   Nakala ya majaribio
   Hoja
   • Ukitaka kufaulu maishani ufahamu kuna kibarau kigumu mbele yako.
   • Itakubidi kutumia nyenzo mbalimbali kuikabili kazi hiyo vilivyo na kuimarisha maisha yako.
   • Karibu watu wote waliofaulu au waliostawi maishani wamepitia vikwazo vingi.
   • Vijana waelewe kuwa wakiona vyaelea vimeundwa.
   • Vijana wanahimizwa kufanya kazi  kwa bidii zaidi kuliko wazee wao.
   • Wasitosheke na yale yaliyotendwa na wazee kwani moyo huo utaendeleza nchi.
    hoja (4 x 1=4) utiririko 1 jumla 5
  2.      
   1. Vijana waelewane na wazazi
   2. Wazazi wawape vijana maelekezo na radhi
   3. Watoto wawe na malengo maishani
   4. Wasikate tamaa
   5. Waelewe hali ya wazazi
   6. Wajitengemee wenyewe
   7. Wawe na nidhamu na kujiamini
   8. Waheshimu wazazi
   9. Wapuuze wanyanyasaji
   10. Wajifunze kuomba msamaha na kuheshimu wengine
   11. Wasipende anasa.
    hoja 9 x 1 = 9
    utiririko 1   jumla = 10
    Adhibu
    1. Ondoa nusu ( ½ ) alama kwa kila kosa la hijai hadi makosa sita( ½  x6=3)
    2. Ondoa nusu alama kwa kila kosa la sarufi hadi makosa sita ( ½  x6=3)
    3. Ondoa alama moja kwa maneno ya kwanza kumi ya ziada halafu ondoa nusu alama kwa kila    maneno matano ya ziada.
    4. Mwanafunzi atakayekosa kuandika kwa njia ya mtiririko atuzwe sufuri( 0)
 3.      
  1. Kitumiwe kuonyesha,furaha,huzuni,mshangao 
  2.    
   1. /e/ na /o/ 
    za katikati/wastani 
   2. /p/ na /k/ 
    vipasuo
   3. /m / na /gh/ 
    sighuna
   4. /s/ na /r/   
    za ufizi
  3. wa’lakini – ila/dosari/upungufu/udhaifu
   wala’kini- lakini
  4. m-kiambishi cha nafsi ya pili wingi, 
   li-wakati uliopita, ’O’rejeshi,
   wa-kiambishi cha nafsi ya tatu wingi (kitendwa/kipozi),
   furahi-mzizi, 
   sha-kauli ya kutendesha   
  5.      
   1. Mwanafunzi anayejikakamua  huwaacha wazaziwe wakitumaini.
    Badilisha maneno yaliyokolezwa kuwa nomino dhahania.
    Mwanafunzi mwenye ukakamavu huwaacha wazaziwe wakiwa na matumaini.
   2. Anza kwa kipozi
    Sherehe ilipambwa na watumbuizaji wengi siku hiyo.
  6.      
   1. Sukari (karibu)
    ii hii
   2. Chandarua (wastani)
    kicho hicho
  7. Mkulima amepanda mbegu ifaayo.Mkulima  atavuna mazao mengi.
   Mkulima akipanda mbegu ifaayo atavuna mazao mengi.
  8. Marubani waliyakwepa mawingu yale vyombo vikapaa angani.
   Rubani alilikwepa wingu lile,chombo kikapaa angani.
  9. nomino, kishazi tegemezi, kielezi cha wakati, kitenzi, nomino, kivumishi
   Mtoto  aliyepita hapa alifika nyumbani vizuri.
  10. Watahiniwa wengi wanautazamia mtihani kwa hamu kubwa. 
   Watahiniwa wengi watakuwa wakiutazamia mtihani kwa hamu kubwa.
  11. Askari  wamekuja kwa ajili ya Mashaka.
   Askari wangempata Mashaka wangemkamata. 
   Askari  wamekuja kwa ajili ya Mashaka lau wangempata wangemkamata.  Au
   Lau askari wangempata Mashaka waliyemjia wangemkamata.
  12. Buzi lake limekata jikamba likaingia jishambani na kula maboga.
   Mbuzi wake amekata kamba akaingia shambani na kula mboga.
  13. Babu alinyweshwa uji na Andai kwa kikombe.
   Kiima-Andai
   Kipozi-uji
   Kitondo-babu
   Ala-kikombe
  14. Mwanariadha aliyeanguka akikaribia utepe alituzwa.
   tegemezi-mwanariadha aliyeanguka akikaribia utepe
   huru-Mwanariadha alituzwa.
  15. Wanafunzi hawa wanapenda somo hili sana.
  16. Salire alimkimbilia Roda.
   Kwa niaba ya
   Kwenda aliko
  17. mwalimu mkuu aliuliza anita umechelewa kwa nini 
   Mwalimu Mkuu aliuliza , ‘  Anita, ulichelewa kwa nini ?’ 
  18. Aliwahutubia wanafunzi, na walimu.
   Hakuwahutubia wanafunzi wala walimu. .
  19.          
   1. Songa kwa mkono,sugua au binyabinya kwa mkono,
   2. fuko lililoshhonwa kwa chane za miyaa linalotumiwa kuwekewa vitu.
   3. kiingia porini-malipo yanayotolewa kwa mganga.mtu asiyeweza kuaminika ;laghai,ayari,
   4. mpotovu ;mbaya,hanithi,
   5. eneo kubwa la kijografia,
   6. makasia ya mikono wakati wa kuogelea.
   7. Kitu chenye utepe unaonasa sauti/picha na huweza kusikika/kuonekana kwa kuupiga utepe huo katika redio kaseti au video
  20. Umma ulimpokea Bi.Vitendo,mtetezi wa haki za raia,kwa furaha.
   Kijalizo-mtetezi wa haki za raia
   chagizo-kwa furaha
  21. Ji-katika ‘jina’- kiambishi ngeli ya LI-YA katika umoja
   Ji-katika ‘jitu’-ukubwa
   Ji-katika ‘ukataji’ –unominishaji wa vitenzi kurejelea anayetenda
 4. Umepewa nafasi kuwahutubia washika dau kuhusu jinsi ya kuthibiti ongezeko la idadi ya vijana wanaofikishwa mahakamani kwa sababu anuai.
  1. sheria/mahakamani/ kotini/ daawa
  2.         
   1. msamiati maalumu/ teule/wa kipekee- jela, rufani, hakimu,wakili, shahidi na kadhalika
   2. kuzingatia itifaki Mkuu wa usalama katika Kaunti hii,Manaibu wake,Walimu Wakuu,walimu
   3. lugha rasmi ya Kiswahili au Kiingereza
   4. kunukuu  vifungu vya sharia,sura ya sita ya sharia za nchi yetu…
   5. kuchanganya na kuhamisha msimbo, mfano,Take it from me, kijana atakayevunja sharia …
   6. sentensi ndefu ndefu ili kutoa maelezo.
   7. utohozi wa  msamiati,mfano,jaji.
   8. msamiati wa kukopa kutoka katika lugha nyinginezo kufidia upungufu wa kisayansi/kiteknolojia
   9. lugha sanifu
   10. lugha ya heshima kwa mfano, Mheshimiwa, Mshukiwa, Kiongozi wa Mastaka
   11. Lugha ya kuamuru
   12. Lugha yenye udadisi ili kushirikisha hadhira 
   13. Lugha hudhihirisha ukweli
   14. Lugha ya kushawishi 
   15. Lugha ya maagizo
   16. Lugha legevu inayoeleweka na wote
   17. Matumizi ya viziada lugha-ishara,kiimbo,miondoko na kadhalika.
  3.      
   1. Kusanifisha matumizi ya maandishi ya Kiswahili kote Afrika Mashariki 
   2. Kutunga kamusi za kutumia
   3. Kutafiti lahaja za Kiswahili
   4. Kuboresha vitabu vya shule na vingine vilivyokuwa tayari vimechapishwa.
   5. Kusoma na kuhakiki vitabu vilivyoshughulikiwa na kamati.
   6. Kufanya tafsiri ya vitabu vingine kwa lugha ya Kiswahili
   7. Kujibu maswali yanayohusu lugha ya Kiswahili na fasihi yake.
   8. Kuendeleza lugha moja kwa kuwepo maafikiano kamili katika mamlaka ya \Afrika Mashariki. 
   9. Kuleta ulinganifu wa matumizi ya maneno yaliyoko na maneno mapya kwa kusimamia uchapishaji. 
   10. Kuleta ulinganifu wa sarufi ya Kiswahili kwa kuchapishaaaaaa vitabu vifaavo vya kufundishia.
   11. Kuwatia moyo waandishi na kuwasaidia kuandika katika Kiswahili.
   12. Kuwasaidia wenyeji kuijua lugha ya Kiswahili.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kakamega Evaluation Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?