Kiswahili Paper 1 Questions and Answers - ACK Diocese Mumias Joint Evaluation Mock 2022

Share via Whatsapp

Maswali

MAAGIZO

Andika insha mbili.

  • Insha ya kwanza ni ya lazima.
  • Kisha chagua insha nyingine moja kati ya hizo tatu zilizosalia.
  • Kila insha isipungue maneno 400.
  • Kila insha ina alama 20.

 

  1. LAZIMA
    Andika hotuba utakayotoa katika mkutano wa vijana katika kaunti yako ukilalamika madhara ya pombe haramu huku ukipendekeza njia za kukabiliana nayo.
  2. Fafanua jinsi ambavyo Elimu huchangia kupata umoja wa kitaifa.
  3. Andika insha inayoambatana na methali;-
    • Mui huwa mwema;-
  4. Andika insha itakayo malizika kwa maneno;
    • “….Nilipogutuka nilikuwa nimezungukwa na aila yangu huku hali ya wasiwasi ikiwa imetanda.”

Mwongozo Wa Kusahihisha

Mwongozo wa Kusahihisha

  1. Utangulizi
    • Karatasi hii imedhamiria kutathmini uwezo wa mtahiniwa wa kuwasiliana na msomaji na kuwasilisha ujumbe kimaanddishi, akizingatia mada aliyopewa. Mawasiliano haya yategemea ukwasi wa lugha ya mtahiniwa, kwa mfano, kutunga sentensi sahihi zenye mtiririko mzuri kimawazo, lugha ya kuvutia na yenye mawazo asilia, ubunifu wa kiwango cha juu na hati nadhifu. Kwa kutegemea maagizo ya swali lenyewe na umahiri wa lugha, utahini lazima utilie mkazo mtindo, mada na uwezo wa mtahiniwa kufuata maagizo vilivyo. Mtahini sharti aisome insha yote huku akizingatia hoja, sarufi, hijai, msamiati na mtindo ili aweze kuikadiria kwa kurelea viwango mbalimbali vilivyopendekezwa. Viwango vyenyewe ni A, B, C na D kutegemea uwezo/umilisi wa mtahiniwa.
  2.   Viwango vya kutathminia
    Vielekezi hivi ndivyo vitakavyomwezesha mtahini kumweka mtahiniwa katika viwango mbalimbali vya kiutendaji.

    1. Kiwango cha D kwa jumla (Alama 01 – 05)
      • Insha haieleweki kwa vyovyote vile: uwezo wa mtahiniwa wa kutumia lugha ni hafifu sana, hivi kwamba lazima afikirie kile mtahiniwa anachojaribu kuwasilisha.
      • Mtahiniwa hana uwezo wa kutumia maneno ya Kiswahili kwa njia inayofaa.
      • Lugha ya mtahiniwa wa kiwango hiki ni hafifu mno, miundo ya sentensi ni mibovu kiasi kwamba insha inakosa muwala na mshikamano. Uakifishaji ni mbaya mno na insha ina makosa mengi mno ya sarufi na hijai.
      • Mtahiniwa anayejitungia swali na kulijibu huwa katika kiwango hiki.
      • Insha ya urefu wa robo ikadiriwe hapa.

        Ngazi mbalimbali za Kiwango cha D
        • D- (D ya chini) – Alama 01 – 02
          1. Insha haina mpangilio maalum na haieleweki kwa vyovyote vile.
          2. Mtahiniwa anajitungia swali tofauti na kulijibu.
          3. Mtahiniwa anaandika kwa lugha isiyo Kiswahili au kuchanganya ndimi.
          4. Mtahiniwa ananakili swali au maswali na kuyakariri.
          5. Mtahiniwa ananakili swali au kichwa tu.
        • D Wastani (Alama 03)
          1. Insha imekosa mtiririko wa mawazo.
          2. Mtahiniwa amepotoka kimaudhui.
          3. Mtahiniwa anatumia lugha hafifu mno.
          4. Insha ina makosa mengi ya kila aina.
        • D+ (D ya juu) – (Alama 04 -05
          1. Insha ya aina hii huwa na makosa mengi ya kila aina, lakini unaweza kutambua kile ambacho mtahiniwa anajaribu kuwasilisha.
          2. Hoja hazikuelezwa kikamilifu/mada haikukuzwa vilivyo.
          3. Mtahiniwa hana uhakika wa matumizi ya lugha/anajaribu kutumia lugha ila hana hakika na matumizi ya vipengele vya lugha anavyoteua.
          4. Mtahiniwa hujirudiarudia.
          5. Insha itakayozingatia sura lakini ikose maudhui ikadiriwe hapa.
    2. Kiwango cha C kwa jumla (Alama 06 – 10)
        • Mtahiniwa anajaribu kuishughulikia mada japo hakuikuza na kuiendeleza vilivyo.
        • Mtahiniwa anawasilisha ujumbe kwa njia isiyovutia/hana ubunifu wa kutosha.
        • Mtahiniwa anaakifisha sentensi vibaya.
        • Mtiririko wa mawazo unaanza kujitokeza japo kwa njia hafifu.
        • Insha ina makosa mengi ya sarufi, msamiati na tahajia (hijai).
        • Insha yenye urefu wa nusu ikadiriwe hapa.

          Ngazi mbalimbali za kiwango cha C
          • C- (C ya chini) – Alama 06 – 07
            1. Mtahiniwa ana shida ya kuwasilisha na kutiririsha mawazo yake.
            2. Mtahiniwa hana msamiati wa kutosha wala miundo ya sentensi ifaayo.
            3. Mtahiniwa anafanya makosa mengi ya sarufi, hijai na msamiati na insha yake haieleweki kwa urahisi.
          • C Wastani (Alama 08)
            1. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe lakini kwa njia hafifu.
            2. Dhana tofautitofauti hazijitokezi wazi.
            3. Mtahiniwa hana ubunifu wa kutosha.
            4. Mtiririko wa mawazo ni hafifu na hana ufundi wa lugha unaofaa.
            5. Amejajaribu kuishughulikia mada aliyopewa.
            6. Mtahiniwa ana shida ya unakifishaji.
            7. Mtahiniwa anafanya makosa mengi ya sarufi, ya hijai na ya msamiati lakini bado insha inaeleweka.
          • C+ (C ya juu) – Alama 09 – 10
            1. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe vizuri akizingatia mada lakini kwa njia isiyo na mvuto.
            2. Dhana tofautitofauti zimejitkeza japo kwa njia hafifu.
            3. Kuna mtiririko wa mawazo japo hana ufundi wa lugha unaofaa.
            4. Misemo na methali zimetumika kwa njia hafifu.
            5. Ana shida ya uakifishaji.
            6. Kuna makosa ya sarufi, ya msamiati na ya hijai yanayoathiri mtiririko wa mawazo.
    3. Kiwango cha B kwa jumla (Alama 11 – 15)
      • Katika kiwango hiki, mtahiniwa anaonyesha hali ya kuimudu lugha.
      • Mtahiniwa anatumia miundo tofautitofauti ya sentensi vizuri.
      • Mtahiniwa ana uwezo wa kutumia lugha kwa ufasaha.
      • Mada imekuzwa na kuendelezwa kikamilifu.
      • Insha ya urefu wa robo tatu ikadiriwe katika kiwango hiki.

        Ngazi mbalimbali za kiwango cha B.
        • B- (B ya chini) – Alama 11 – 12
          1. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe vizuri kwa kueleza hoja tofautitofauti Akizingatia mada.
          2. Mtahiniwa ana mtiririko mzuri wa mawazo.
          3. Mtahiniwa anatumia mifano michache ya msamiati unaovutia.
          4. Makosa yanadhihirika/kiasi.
        • B Wastani – Alama 13
          1. Mtahiniwa anadhihirisha hali ya kuimudu lugha.
          2. Mawazo ya mtahiniwa yanadhihirika akizingatia mada.
          3. Mtahiniwa anateua na kutumia mifano michache ya msamiati mwafaka.
          4. Sarufi yake ni nzuri.
          5. Makosa ni machache.
        • B+ (B ya juu) – Alama 14 – 15
          1. Mawazo ya mtahiniwa yanadhihirika na anajieleza waziwazi.
          2. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe kwa njia inayovutia na kwa urahisi akizingatia mada.
          3. Mtahiniwa ana mchanganyiko mzuri wa msamiati unaovutia.
          4. Sarufi yake ni nzuri.
          5. Uakifishaji wa sentensi zake ni mzuri.
          6. Makosa ni machache ya hapa na pale.
    4. Kiwango cha A kwa jumla – Alama 16 – 20
        • Mtahiniwa ana ubunifu wa mawazo (yenye uasilia) yanayodhihirika na kutiririka akizingatia mada.
        • Mtahiniwa anadhihirisha ujuzi wa lugha yenye mnato.
        • Ana uwezo wa kutumia tamathali za usemi ili kutoa hisia/hoja zake kwa njia bora na kwa urahisi.
        • Umbuji wake unadhihirisha ukomavu na ukakamavu wake kimawazo.
        • Insha ina urefu kamili na hoja tano au zaidi kamilifu ikadiriwe hapa.

          Ngazi mbalimbali za Kiwango cha A
          • A- (A ya chini) – Alama 16 – 17
            1. Mtahiniwa anadhihirisha ukomavu wa lugha.
            2. Mawazo ya mtahiniwa yanadhihirika na anaishughulikia mada.
            3. Ana mtiririko na muumano mzuri wa mawazo.
            4. Msamiati wake ni mzuri/mwafaka na unavutia.
            5. Sarufi yake ni nzuri.
            6. Anatumia miundo tofauti tofauti ya sentensi kiufundi.
            7. Makosa ni machache yasiyokusudiwa.
          • A Wastani- Alama 18
            1. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe vizuri kulingana na mada.
            2. Anajieleza kikamilifu akitumia lugha yenye mnato.
            3. Anatoa hoja zilizokomaa.
            4. Anatumia msamiati wa hali ya juu na unaovutia zaidi.
            5. Anatumia miundo tofautitofauti ya sentensi kiufundi.
            6. Makosa ni nadra kupatikana.
          • A+ (A ya juu) – Alama 19 – 20
            1. Mawazo yanadhihirika zaidi na mada imeshughulikiwa vilivyo.
            2. Anajieleza kikamifu akitumia lugha ya mnato zaidi.
            3. Hoja zake zimekomaa na zinashawishi
            4. Msamiati wake ni wa hali ya juu na unaovutia zaidi.
            5. Sarufi yake ni nzuri zaidi.
            6. Anatumia miundo tofautitofauti ya sentensi kifundi zaidi.
            7. Makosa yote kwa jumla hayazidi matano.
    5. Muhtasari wa Viwango mbalimbali
  3. Usahihishaji na Utuzaji kwa jumla
    • Ili kuikadiria insha ya mtahiniwa vyema bila kuongozwa na mtazamo – nafsi,
    • Mtahini sharti aisome insha yote akizingatia vipengele muhimu. Vipengele hivi ni maudhui, msamiati, mtindo, sarufi na hijai.

    •  Maudhui
      1. Maudhui ni hoja au mambo yanayozungumziwa, kuelezewa au kuhadithiwa kwa mujibu wa mada iliyoteuliwa.
      2. Maudhui ndio hasa uti wa mgongo wa insha yoyote ile.
      3. Ubunifu wa mtahiniwa hukisiwa kwa kutathmini uzito wa maudhui yake kulingana na mada teule.
    • Msamiati
      • Msamiati ni jumla ya maneno yatumiwayo katika lugha husika. Mtahiniwa anatarajiwa kutumia msamiati unaooana na mada teule. Kutegemea ukwasi wa lugha, mtahiniwa anatarajiwa kuikuza mada kwa kuifinyanga lugha kiufundi. Ni muhimu kuelewa kwambakutokana na maendeleo na ukuaji wa teknolojia na mawasiliano, maneno mapya yanaibuka kila kuchapo.
    • Mtindo na muundo
      • Mtindo unahusu mambo kama vile;-
      • Matumizi yafaayo ya lugha kama vile;- tamathali za usemi, kwa mfano, methali, misemo, sitiari na kadhalika;
      • Matumizi mwafaka ya msamiati unaohusiana na mada teule/matumizi ya sajili mwafaka.
      • Namna mtahiniwa/mwandishi anavyowaumba wahusika wake, kwa mfano kwa kuwapa majina ya majazi, kuwaua, na kadhalika;
      • Matumizi ya vipengele vya kimuundo kama vile mbinu rejeshi, udokezaji na sadfa.
      • Matumizi ya vipengele vya tanzu nyingine za kimandishi/ kifasihi/ kisanaa, kama vile kutumia barua katika insha ya masimulizi;
    • Muundo unahusu;-
      • Mpangilio wa kazi kiaya
      • Mtiririko na mshikamano wa mawazo kiaya na katika insha nzima
      • Hati nzuri na inayosomeka kwa urahisi
      • Kuandika herufi vizuri kwa mfano Jj, Pp, Uu, Ww na kadhalika.
      • Sura ya insha;
      • Mtahiniwa anayekosa kuzingatia sura inayostahilika aondolewe alama 4. (Sura) kwa jumla.
      • Unadhifu wa kazi ya mtahiniwa.
    • Sarufi
      • Sarufi ndio msingi wa lugha. Ufanisi wa mawasiliano hutegemea uwezo wa mtahiniwa wa kutunga sentensi sahihi zenye uwiano wa kisarufi. Mtahini ataonyesha makosa yoteya sarufi yaliyo katika insha anayosahihisha. Makosa ya sarufi huweza kutokea katika;
        1. Matumizi yasiyofaa ya alama za uakifishaji
        2. Kutumia herufi kubwa au ndogo mahali pasipofaa
        3. Matumizi yasiyofaa ya ngeli na viambishi, viunganishi, nyakati, hali, vihusishi na kadhalika.
        4. Mpangilio usiofaa wa maneno katika sentensi
        5. Mnyambuliko usiofaa wa vitenzi na nomino
        6. Kuacha neno linalohitajika au kuongeza neno lisilohitajika katika sentensi.
      • Matumizi yafuatayo ya herufi kubwa yazingatiwe;-
        1. Mwanzo wa sentensi/Mwanzo wa kauli/Usemi halisi
        2. Majina ya pekee;-
          1. Majina ya mahali, miji, nchi, mataifa na kadhalika
          2. Siku za juma, miezi n.k.
          3. Mashirika, masomo, vitabu. n.k.
          4. Makabila, lugha n.k.
          5. Jina la Mungu
          6. Majina ya kutambulisha hasa wanyama wa kufugwa, kwa mfano yale ya mbwa – Foksi, Jak, Popi, Simba, Tomi na mengineyo.
          7. Mwanzo wa kauli.
          8. usemi halisi
          9. Vidokezi
    • Makosa ya Hijai/Tahajia
      • Haya ni makosa ya maendelezo. Mtahini anashauriwa asahihishe huku akiyaonyesha yanapotokea kwa mara ya kwanza tu. Makosa ya tahajia huweza kutokea katika;-
        1. Kutenganisha neno kwa mfano ‘aliye kuwa’
        2. Kuunganisha maneno kwa mfano ‘kwasababu’
        3. Kukata silabi visivyo afikapo pambizoni kama vile ‘nga-o’
        4. Kuandika herufi isiyofaa kwa mfano ‘ngesa’ badala ya ‘ongeza’
        5. Kuacha herufi katika neno kwa mfano ‘aliyekuja’ badala ya ‘aliyekuja’
        6. Kuongeza herufi isiyohitajika kama vile ‘piya’ badala ya ‘pia’
        7. Kuacha alama inayotarajiwa katika herufi kama vile j i
        8. Kukosa kuandika kistari cha kuendelezea neno afikiapo pambizoni au kukiandika mahali pasipofaa
        9. Kuacha ritifaa au kuiandika mahali pasipofaa, kwa mfano ng’ombe, ngom,be, n’gombe, ngo’mbe n.k.
        10. Kuandika maneno kwa kifupi kama vile k.v., v.v., n.k. na kadhalika.Kuandika tarakimu kwa mfano 27-08-2010.
    • Alama za kusahihishia
      • ===Hupigwa chini ya sehemu ambapo kosa la sarufi limetokea kwa mara ya kwanza tu.
      • ___Hupigwa chini ya sehemu au neno ambapo kosa la hijai limetokeakwa mara ya kwanza tu.
      • ✔ Htumiwa kuonyesha hoja inapokamilikia pambizoni kushoto
      • ^ Hutumiwa kuonyesha kuachwa kwa neno/maneno
      • ✔ Hutumiwa kuonyesha msamiati bora. Alama hii hutiwa juu ya neno lenyewe
      • X Hutumiwa kuonyesha msamiati usiofaa. Alama hii hutiwa juu ya neno lenyewe
      • Maelezo mafupi yanahitajika kuhusu tuzo lililotolewa. Kila ukurasa uwe na alama ya chini katikati ili kuthibitisha kuwa mtahini ameupitia ukurasa huo.
    • Ukadiriaji wa Urefu wa Insha Zote
      • Maneno 9 katika kila msitari Ukurasa mmoja na nusu - 2
      • Maneno 8 katika kila msitari Ukurasa mmoja na robo tatu - 2 ¼
      • Maneno 7 katika kila msitari Kurasa mbili - 2 ½
      • Maneno 6 katika kila msitari Kurasa mbili na nusu - 3
      • Maneno 5 katika kila msitari Kurasa mbili na robo tatu - 3 ½
      • Maneno 4 katika kila msitari Kurasa tatu na robo tatu - 4 ½
      • Maneno 3 katika kila msitari Kurasa nne na nusu - 6
    • Kufikia maneno 174 Insha robo
      • Maneno 175 – 274 Insha nusu
      • Maneno 275 – 374 Insha robo tatu
      • Maneno 375 na kuendelea Insha kamili

SWALI LA KWANZA
HOTUBA

  1. Insha ya hotuba iwe na kichwa ambacho kinahusisha neno, “Hotuba.”
  2. Aya ya kwanza ni utangulizi. Ni ya utambulisho.
  3. Mwili wa insha uzingatie miongoni mwa mengine, madhara yafuatayo ya pombe haramu;
    • Vifo
    • Kufilisisha/umaskini
    • Kuharibu ndoa/familia
    • Watoto kukosa masomo
    • Vita/fujo
    • Ukiukaji sheria/uhalifu
    • Kulemaza/kuwa kipofu
  4. Zungumzia hoja saba hivi. Kila hoja ielezwe kikamilifu katika aya yake tofauti.

Njia za kukabiliana na pombe haramu

  • Upigaji marufuku wa pombe haramu: kupika na kuuza.
  • Kuweka sheria kudhibiti ugemaji na uuzaji wa pombe hizi haramu.
  • Kudhibiti wakati wa unywaji wa pombe.
  • Kutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa.
  • Kuhamasisha jamii kuhusu njia mbadala za burudani kama vile michezo.
  • Hitimisho
  • Nasaha ama ombi maalum kuhusu unywaji wa pombe litolewe.

SWALI LA PILI

Jinsi ambavyo Elimu huchangia kupata umoja wa kitaifa.
Hoja za kuunga mkono

  • Elimu humfanya mtu kuelewa jinsi ya kuishi na wengine katika taifa.
  • Shughuli kama michezo shuleni hukuza umoja miongoni mwa wanafunzi
  • Walimu wenyewe kutoka sehemu mbalimbali huleta umoja.
  • Masomo yanakuza upendo na umoja miongoni mwa wanafunzi.
  • Vyama vya amani na maridhiano shuleni hukuza umoja.
  • Taaluma kama vile Diplomasia na Mahusiano ya Kimataifa hufunza mbinu za kuleta umoja miongoni mwa wanajamii.
  • Ufunzaji wa tamaduni mbalimbali za wanajamii anuwai shuleni huleta uelewa wa kwa nini jamii Fulani huishi jinsi zilivyo.
  • Elimu huwafanya watu kuwa nna maazimio makubwa, hivyo hawawi na fikira za kuzua rabsha miongoni mwa makundi ya watu.

SWALI LA TATU

Insha ya Methali

Mui huwa mwema.

-Mui – Mbaya au mwovu

Utangulizi

  • Maana ni mtu aliye mbaya anaweza kubadilika na kuwa mzuri.

Matumizi

  • Husemwa hivi pale mtu aliyekuwa na tabia mbovu anapogeuka na kuwa mtu mwema.

Anaweza toa maana au afululize kisa moja kwa moja.
Mwili

  • Kisa kionyeshe mtu ambaye alikuwa mbaya kimatendo.
  • Baadaye, mtu huyo abadilike awe mwadilifu.
  • Kisa kijikite katika muktadha.
  • Lugha ya mnato itumike.

SWALI LA NNE

Insha ya Mdokezo

  • Kisa kioane kikamilifu na maneno yaliyotolewa.
  • Lazima maneno yaliyotolewa yawe ya mwisho katika insha yenyewe la sivyo mtahiniwa atachukuliwa kuwa amejitungia swali, basi kuishia kutuzwa alama za bakshishi pekee.
  • Nafsi husikia ni ya kwanza ‘mimi’ – umoja.
  • Ujumbe unafaa kudhihirisha huzuni.
  • Kisa kiishie katika hali ya wasiwasi. Mwanafunzi anayeweza kuzua taharuki mwisho wa insha atapata tuzo bora.
  • Insha isipungue maneno 400 kama yanavyoelekeza maelekezo.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 1 Questions and Answers - ACK Diocese Mumias Joint Evaluation Mock 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?