Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mincks Group of Schools Mock Examinations 2022

Share via Whatsapp

MAAGIZO

  1. Andika jina lako na nambari ya usajili kwenye nafasi ulizoachiwa hapo juu.
  2. Tia sahihi yako kisha uandike tarehe ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa.
  3. Jibu maswali MANNE pekee.
  4. Swali la KWANZA ni la LAZIMA.
  5. Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu zilizobakia.
  6. Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  7. Majibu yote ni lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

KWA MATUMIZI YA MTAHINI PEKEE

SWALI

UPEO

ALAMA

1.  USHAIRI

20

 

2.  

20

 

3.  

20

 

4.  

20

 

JUMLA

80

 

QUESTIONS

  1. LAZIMA

    Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

    Sahibu mwenda nyumbani, msalimu mke wangu
    Mwambie ni kifungoni, huku kwa wazungu
    Walonifunga katani, kutwaa uhuru wangu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Mwambie nawatamani, ninawahamu wanangu
    Hata niwapo njozini, huwaona tu wanangu
    Mavuno ya upeponi, ni sauti tu wanangu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Nina maradhi moyoni, niuhisio uchungu
    Ni mateso mtimani, wala si vyao virungu
    Nikiwaza kiamboni, huko makaoni kwangu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Mwambie anithamini, alitunze shamba langu
    Lisitolewe rubuni, kwa yeyote mlimwengu
    Kheri libaki porini, vimelea viwe chungu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Ukimuona hanani, hana chake wala changu
    Sahibu mpe auni, kirudi takupa fungu
    Wala usidai deni, kulitaka shamba langu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Sijui nikuamini, nikujuze siri yangu
    Au nawe u mhuni, japo huna tena pingu
    Nakwambia walakini, kam’manyishe mwenzangu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Kamwambe aole chini, chini ya ule mvungu
    Kuna shimo kibulani, na ndani mna kijungu
    Ya mumo humo mapeni, hiyo ndo akiba yangu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Asihofie katani, akumbuke yupo Mungu
    Nitatoka gerezani, nipumue kula ndengu
    Nitarudi na imani, japo yatande mawingu
    Ila asihofu sana, nitarudi siku moja

    Maswali

    1. “ila asihofu sana…”
      Fafanua kinyume kinachobainika katika dondoo hili kwa kumzingatia mtunzi wa shairi. (al. 6)
    2. Kwa kutoa mfano, eleza namna toni ya utunzi huu inakuza maudhui. (al. 2)
    3. Taja na ufafanue sifa zozote nne za mtunzi huyu. (al.4)
    4. Onyesha namna usambamba unajitokeza katika utunzi huu. (al. 2)
    5. Andika ubeti wa saba katika lugha nathari. (al. 2)
    6. Huku ukitoa mifano, eleza namna idhini ya kishairi ilivyotumika kukidhia mahitaji ya kiarudhi. (al. 2)
    7. Tambua nafsi neni na nafsi nenewa katika shairi. (al. 2) 

SEHEMU B: TAMTHILIA
P. Kea: Kigogo
Jibu swali la 2 au 3

2. Na wewe! Eeeh kidudumtu, hata haya huna. Umegeuka stesheni ya udaku. Tafuta kazi ufanye, umbeya hauna posho nyanya!

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili (al. 4)
  2. Eleza vipengele viwili vya kimtindo alivyotumia msemaji katika dondoo hili. (al. 2)
  3. Fafanua sifa sita za msemaji wa maneno haya. (al. 6)
  4. Jadili mambo yanayoyumbisha asasi ya ndoa kwa mujibu wa tamthlia hii. (al. 8)

3. “Hivyo vipembe vyao niwachie mimi profesa wa siasa. Michezo ya kitoto huchezwa kitoto. Hatutatumia mabomu kuulia mbu. Hawa ni wadogo. Usiichoshe akili bure. Dawa ninayo.

  1. Fafanua muktadha wa maneno haya. (al. 4)
  2. Huku ukitoa mifano kumi na sita, jadili dawa anayoirejelea msemaji. (al. 16)

SEHEMU C: RIWAYA
Assumpta Matei: Chozi la heri
Jibu swali la 4 au 5

4.

  1. Changanua mitindo katika dondoo lifuatalo. (al. 12)
    “Huyu binti ananikumbusha marehemu mke wangu, Lily. Ujasiri wake, ufasaha wa lugha, utundu wake, mwanya kwenye meno ya juu,” alijisemea Mwangeka huku akielekea alikokuwa Apondi kumpa mkono wa tahania.
    “Hongera kwa uwasilishaji mzuri. Naitwa Mwangeka….,” Mwangeka alisema kwa kigugumizi cha kujitia.
    “Vizuri kukujua,” alijibu Apondi bila kuzingatia aliyoyasema wala hisia za aliyetoa kauli ya awali. Baadaye, hata hivyo, Mwangeka alipata fursa ya kufahamiana zaidi na Apondi wakati wa chamcha.
  2. Jadili umuhimu wa Apondi katika kukuza riwaya ya Chozi la Heri. (al. 8)

5. “Nimeonja shubiri ya kuwa mtegemezi kihali na mali: lakini katika hayo yote, nimejifunza mengi.

  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (al. 4)
  2. Jadili nafasi ya vijana katika kuiendeleza na kuiumba jamii kwa mujibu wa riwaya Chozi la Heri. (al. 16)

SEHEMU D: HADITHI FUPI
WAH. A. Chokocho na D. Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine
Jibu swali la 6 au 7
6. A. Chokocho: Tulipokutana Tena
“Bwana we, huoni kwamba unaniumiza? Katafute mpira uupige shuti, mimi ni binadamu mwenzako.”

  1. Eleza muktadha wa sdondoo hili. (al. 4)
  2. Fafanua mbinu za kimtindo zinazobainika katika dondoo hili. (al. 4)
  3. Kwa kutoa mifano mwafaka, eleza vile mandhari ya “Hotel Rombeka” inavyokuza maudhui.(al. 4)
  4. Eleza namna haki za watoto zinavyokiukwa katika hadithi ya “Tulipokutana tena. (al. 8)

7.

  1. EUNICE K. Mtihani wa Maisha
    Jadili changamoto zinazokumba sekta ya elimu ukirejelea hadithi ya mtihani wa maisha. (al. 8)
  2. S. O. Hamad: Shibe Inatumaliza
    “Shangwe. Hoihoi. Nderemo. Vifijo ndio mchezo wao wakishapakua. Muziki laini wa taarabu unatumbuiza na ndani yake mna vijembe.”
    Kwa kurejelea hadithi hii, jadili ukweli wa maneno yaliyopigiwa mstari. (al. 12)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI
8. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
Hapo zamani, katika enzi za mababu zetu, wanyama wote waliishi jinsi sisi binadamu tunavyoishi. Waliweza kulima, kufunga, kuchota maji na hata kupika. Wanyama wote waliishi katika jamii tofauti tofauti kwenye vijiji. Vijiji kadha, kwa pamoja viliunda milki iliyotawaliwa na mnyama mmoja aliyechaguliwa na wanyama wengine kuwa mfalme wao. Kwa kawaida, mnyama aliyechanguliwa kuwa mfalme alikuwa na sifa za kipekee. Kama vile sungura alikuwa na werevu mwingi, Faru, Nyati na Ndovu walikuwa na nguvu za kupindukia . Simba , Chui au Duma walikuwa wakali sana.

Kulikuwa na milki mbili kubwa zaidi zilizopakana; Almasi iliyoongozwa na Simba na Dhahabu iliyoongozwa na Nyati. Milki hizi mbili zilitoshana kwa kila kitu – si ustawi wa kielimu, si wa kiuchumi, si wa miundomsingi. Wanyama wote katika milki hizi waliishi kwa mtagusano uliowawezesha kuishi kwa amani na umoja. Hili lilitiwa mbolea zaidi na kwamba viongozi wao walikuwa marafiki wa kufa kuzikana.

Hata hivyo, baada ya muda, Simba alianza kujiona kuwa alistahili eneo kubwa kuliko Nyati. Alianza kuota akiwa mfalme wa milki zote mbili. Katika ndoto zake alimwona Nyati akinyenyekea mbele yake. Alifikiri kuwa wadhifa wake ungekuwa wa juu zaidi kama angemiliki rasilmali za miliki zote mbili. Mawazo haya yalimfanya Simba kujaa chuki nyingi kila walipokutana na Nyati.

Kama wasemavyo wahenga, “Kikulacho ki nguoni mwako.” Simba alianza kumtembelea Nyati kuuliza ushauri wa jinsi wangeweza kuunda muungano wa milki zao. Nyati aliliona wazo la Simba kuwa nzuri lakini akampendekezea rafikiye kuwa wachukue muda kutafakari zaidi juu ya muungano huo. Wazo hili halikumfurahisha Simba kwani alimwona Nyati kama kizingiti kwenye ngazi yake ya madaraka. Hapo ndipo Simba alipoanza kupanga mikakati ya kumng’oa Nyati mamlakani.

Baada ta kuhakikisha kuwa mipango yake imekamilika, Simba aliamua kumvizia Nyati kumwangamiza. Hata hivyo, Nyati aliweza kuonywa na marafiki zake waliokuwa kwenye utawala wa Simba kabla ya Simba kumvamia. Alipofahamu mipango hasi ya Simba, Nyati pia aliamua kujihami ili kujikinga dhidi ya Simba. Pupa za Simba za kuongoza zilimfanya amvamie Nyati katika milki yake. Simba alikuwa amesahau kuwa mwenye pupa hadiriki kula tamu. Vita vikali kati ya milki hizi mbili vilizuka. Umoja uliokuwepo ukageuka utengano, uhusiano wao ulikuwa umeingia nyufa.

Nyati alikataa Abadan kumwachia Simba mamlaka kwa nguvu. Alihimiza kikosi chake kupigana kwa vyovyote vile ili kuhifadhi uhuru wao, jambo ambalo walilifanya kwa uwezo wao wote. Kama isemavyo, “Fahali wawili wapiganapo nyasi ndizo huumia.” Wengi waliumia wasiojua kiini cha vita hivi.

Vita vilidumu kwa muda mrefu. Kwa kawaida Nyati aliwapenda wanyama aliowaongoza kwa moyo wake wote. Kila usiku alifikiri jinsi ya kuvimaliza vita hivi ili kuepusha maafa zaidi katika milki yake. Hata hivyo, alipata na namna mbili tu za kulishughulikia jambo hili – aidha aendelee kupigana na kuwaangamiza wanyama wake wote au akubali wito wa Simba kung’atuka mamlakani. Aliamua kuwaita washauri wake kwenye makao makuu ya milki ili wajadili jinsi ya kunusuru milki yao. Washauri wake walionekana kugawanyika mara mbili. Kundi moja lilisistiza kuwa amani haiji ila kwa ncha ya upanga ilhali lingine liliona heri nusu shari kuliko shari kamili. Nyati aliwaza na kuwazua asijue la kufanya.

Hadithi yangu inaishia hapo.

Maswali

  1.                              
    1. Kwa kutoa mfano katika hadithi hii, eleza kwa nini ngano hii ni ya mtanziko. (al. 2)
    2. Fafanua mitindo yoyote mitano aliyotumia msimulizi kufanikisha usimulizi wake. (al. 5)
    3. Huku ukitoa sababu tano fafanua umuhimu wa kushirikisha hadhira katika usimulizi wa ngano kama hii. (al. 5)
  2. Onesha kwa mifano mine jinsi jamii huhifadhi kipera cha ngano sasa. (al. 4)
  3. Ni changamoto zipi zinazoweza kumkumba mtafiti akifanya utafiti wa ngano nyanjani. (al.4)

MWONGOZO WA KUSAHIHISHIA

  1.                              
    1. 'Kinyume katika dondoo : Ila asihofu sana: Sababu za kuhofu
      1. Amefungwa
      2. Anawakosa wanawe – anawaona njozini
      3. Ana maradhi
      4. Ana uchungu moyoni
      5. Huko gerezani anapigwa virungu
      6. Ana wasiwasi kuhusu shamba kutolewa rubuni
      7. Hamwamini anayetuma kwa mkewe
      8. Ana tumaini atarudi lakini hajui siku yenyewe
      9. Amenyimwa uhuru wake
        Zozote 6 x 1 =6
    2. Toni ya uchungu/huzuni/ - kunaonyesha hofu aliyonayo mtunzi kuonyesha wasiwasi wake.
      Kutaja toni x 1 kufafanua x 1 =2
    3. sifa za mtunzi
      1. Mwenye matumaini
      2. Ni mwajibikaji. Anajali familia/anajali hatima ya familia yake
      3. Mwenye mapenzi ya dhati – anaipenda familia yake
      4. Ana busara/hekima – ana akiba/ anatahadhari shamba lake lisije kupotea
      5. Ana mlahaka mzuri – ameunda urafiki na wenzake hadi anawatuma
      6. Ni mvumilivu – licha ya changamoto kifungoni hakati tama
      7. Mdadisi – anapekuapekua kama amwamini anayemtuma
      8. Mwenye kumbukizi – anakumbuka alikoficha pesa zake
      9. Ni mcha Mungu – anamshauri mkewe kuwa kuna Mungu
        4 x 1 =4
    4. Usambamba – urudiaji
      ubeti 2 ninawahamu wanangu
      huwaona tu wanangu
      ni sauti za wanangu x 2
    5. Mwambie mke wangu atazame mvunguni/ atapata shimo lililo na jumngu./ atapata ndani pesa ambazo nimehifadhi humo kama akiba/ asiwe na wasiwasi kwani ipo siku nirudi (1/2 x 4 = 2)
    6.                      
      1. Mkisari walonifunga – walionifunga – amefupisha ili apate wiano wa mizani
        - kam’manyishe – ukamumanyisha – kufupisha
        - ndo – ndiyo
      2. lahaja – aole – atazame – kupata uwiano wa mizani 2 x 1 =2
    7. Nafsi neni – mfungwa
      Nafsi nenewa – sahibu 2 x 1 =2
  2.                      
    1. Uk 27
      1. Husda
      2. Ashua
      3. Ofisini kwa Majoka
      4. Majoka amemfumanisha mkewe na Ashua kukazuka ugomvi 4 x 1 =4
    2. vipengele vya kimtindo
      1. nidaa/usiyani – Na wewe! Eeh!
      2. Kejeli/stihizai – kidudumtu
      3. Jazanda – stesheni ya udaku zozote 2 x 1 =2
    3. sifa za Husda (awe amemtaja)
      1. tamaa – anapenda mali
      2. mpenda anasa – anajifurahisha huko Majoka and Majoka Resort
      3. msinzi – anamtamani chopi kimapenzi
      4. Mpyaro – anamtukana Ashua
      5. wivu – hataki kumwona Majoka na mwanamke mwingine
      6. mwenye malalamiko – anadai Majoka haonekani kwake
      7. mwenye hasira – anampiga Ashua mbele ya Majoka
      8. Anamwajibikia Majoka anapozirai zozote 6 x 1 =6
    4. mambo yanayoathiri ndoa
      1. vifo – hashima ni mjane
      2. harakati za ukombozi – Sudi anasemwa kuwa mpenzi wa Tunu – Ashua halifurahii suala hili.
      3. Ukosefu wa kipato – unafanya Ashua kujipata mikononi mwa Majoka
      4. Hongo – Ngurumo analala na Asiya ili amsaidie kupata kandarasi ya kuoka keki
      5. uhaba wa chakula unafanya Ashua kumlaumu mmewe kuwa hajibidiishi
      6. Viongozi kama Majoka wanachonganisha wan ndoa. Zozote 4 x 2 =8
  3. Muktadha uk 35
    1. Maneno ya Majoka akimwambia Kenga /ofisini kwa Majoka/ wanapanga namna ya kuwakabili wapinzani wao – akina Tunu 4 x 1 =4
    2. Dawa inayorejelewa
      1. Mauaji – akina jabali
      2. Kupigwa – akina Tunu
      3. Kufunga soko ili wateseke
      4. Kuongeza bei ya vyakula
      5. Kuongeza kodi
      6. Kuwafumanisha kama vile Ashua na Husda
      7. Kuwatia kizuizini
      8. Kuwahinga – mabaki ya keki/vipande vya ardhi
      9. Kuwatisha – vijikaratasi
      10. Kuwatenganisha ili kuwatawala – akina Ngurumo ni wafuasi wake
      11. Kufunga vituo vya habari – runinga ya mzalendo
      12. Kuwapa likizo ya mwezi mzima kuadhimisha miaka sitini ya uhuru
      13. Kusambaratisha mikutano yao ya kisiasa
      14. Kuvunja maandamano yao
      15. Kutumia propaganda kama mtangazaji wa redio anavyofanya
      16. Kurithisha hatamu za uongozi – Ngao Juniour
      17. Kupujua thamani ya elimu – kuwadhalilisha waliosoma
      18. Kutoa vibali maalum kwa shughuli ambazo ni kinyume cha sheria – Asiya
      19. Kutotaka wafadhili kuendelea kutoa misaada
      20. Udanganyifu katika upigaji wa kura
      21. Kutumia asasi kama vile askari visivyo zozote 16 x 1 =16
  4.                          
    1. uchanganuzi wa mitindo
      1. Kisengere nyuma – ananikumbusha marehemu
      2. Ulinganishaji – analinganisha Lily na Apondi
      3. Uzungumzi nafsi – Mwangeka anajisemea
      4. Usimulizi – usimulizi wa Mwangeka
      5. Stihizai – Apondi hakuzingatia salamu
      6. Mazungumzo/dayolojia – kati ya Mwangeka na Apondi
      7. Msemo/nahau – kumpa mkono wa tahania
      8. Mdokezo – naitwa Mwangeka…
      9. Taswira – taswira ya kigugumizi cha kujitia
        Kutaja x 1 mfano x 1 zozote 6 x 2=12
    2. Umuhimu wa Apindi
      1. anakuza ploti/msuko – anaendeleza usimulizi kwa hotuba yake
      2. anachimuza sifa za wahusika kama Mwangeka/ Uzalendo wa Mandu
      3. Kuonyesha dhiki wanazozipitia wanawake wanaofiwa na waume wao/ulezi
      4. anakuza dhana ya kuwa mwanamke ana uwezo sawia na wanaume- anawadhibiti maaskari kwa hotuba na kauli zake kiasi
      5. Anaangazia dhuluma wanazofanyiwa raia na askari – kuua nzi kwa risasi
      6. Kiwakilishi cha mwanamke aliyejikomboa kimawazo….mtetezi wa haki
      7. Kiwakilishi cha mwanamke jasiri – shujaa haogopi chochote
      8. Anawakilisha wanawake wenye misimamo dhabiti – anampenda mmewe hata katika mauti.
      9. Anahimiza maridhiano na ndungu katika jamii.
      10. Kiwakilishi cha mwanamke msomi katika jamii
        Zozote 8 x 1 =8
  5.                              
    1.                           
      1. Haya ni maneno ya ridhaa
      2. Anamwamia Mwangeka
      3. Wamo katika ganjo la nyumba iliyochomwa
      4. Anamweleza dhiki ambazo amepitia tangu ghasia za baada ya kutawazwa kiongozi mpya.
        4 x 1 =4
    2. Mchango wa vijana katika ujenzi wa jamii mpya.
      Kujenga jamii mpya ni kurekeisha maovu yaliyokuwa yakitendeka katika jamii kwa kutenda mema/ kuyanyoosha yaliyoenda kombo. Baadhi ya hoja ni:
      1. Tila anataka jamii ambayo wananchi wanapata haki mahakamani. Anataka kusoma na kuwa jaji wa mahakama ya juu ili atatue kesi ambazo hazijasikizwa kwa miongo kadhaa, hivyo kuwapa mahabusu ambao wamekaa kwenye rumande muda mrefu haki yao – uk 45
      2. Tila anawahimiza wanajamii kumchagua kiongozi wa jinsia yoyote, awe mwanamke au mwanamume almradi alete maendeleo katika taifa. Hivi ndivyo anavyowaambia baba yake Ridhaa – uk 40
      3. Lucia – Kiriri anawatahadharisha wanajamii dhidi ya ukabila kwa kukubali kuolowa katika ukoo wa Waombwe amabo una uadui na ukoo wake wa Anyamvua – uk 66 – 67
      4. Umu anafunza umuhimu wa kuwasaidia wasiojiweza/maskini katika jamii. Anampa ombaombamjini karaha shilingi mia mbili licha ya mamake mzazi kukataa kuwasaidia. Apondi na Mwangeka pia wanahimiza jamii kuwasaidia wasiojiweza katika jamii. Wanawasaidia maskini waliomiminika kiamboni mwao kutoka sehemu mbalimbali za eneogatuzi lao. – uk 86
      5. Umu anawafunza vijana umuhimu wa kutumia pesa vizuri/ kutofuja pesa. Anatumia pesa alizodunduiza kutokana na masrufu aliyokuwa akipewa babake kumsaidia ombaomba mmoja mjini karaha – uk 86
      6. Rachael Apondi anaonya askari dhidi ya kutatua mizozo kwa makeke na bunduki. Anawaambia kwamba hilo ni jambo ambalo limepitwa na wakati – uk – 113
      7. Dick anawaonya vijana dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya kwa kuiacha biashara hiyo haramu na kufungua biashara halali ya kuuza vifaa vya simu/umeme – uk 123 – 124
      8. Daktari anahimiza jamii kuthamini haki za watoto kwa kukataa kumsaidia Pete kuavya mimba baada ya kumeza tembe – uk 151
      9. Dick pia anaifunza jamii umuhimu wa kuthamini elimu. Licha ya kukatiziwa masomo na Buda, anapojinasua kutoka mikononi mwake anarudi shuleni na kujiendeleza kimasomo – uk 124
      10. Kipanga anahimiza msamaha na maridhiano katika jamii. Licha ya kuwachukia na kuwatoroka wazazi wake baada ya aliyemdhania kuwa babake kumkana, anawasamehe wote hatimaye baada ya kunusurika kifo cha kangara. – uk 143
      11. Kipanga anaionya jamii dhidi ya unywaji wa pombe haramu kwa kubadilika na kuacha kuinywa baada ya kuwaua watu sabini. – uk 143
      12. Neema anahimiza jamii kuthamini haki za watoto kwa kumwokota motto aliyetupwa kwenye biwi la taka na kumpeleka kwenye kituo cha mayatima cha Benefactor – uk 161
      13. Dick anataka jamii ambayo vijana wanajitengemea kimaisha. Anafungua duka lka kuuza vifaa vya simu na kuwaajiri vijana wengine ili wapate riziki ya kujikimu. Uk 124/174
      14. Dick anahimiza wanajamii kusameheana- licha ya mama yao Naomi kuwatoroka walipohitaji malezi yake, anawahimiza nduguze Umu na Mwaliko kumsamehe akidai kwamba hakuna binadamau hata mmoja aliyekamilika. Uk 193
      15. Hazina anaionya jamii dhidi ya tabia ya utegemezi/kuombaomba – amekuwa akiombaomba jijini karaha lakini anakubali kuelimishwa na serikali na kusomea upishi na huduma za hotelini, hivyo kumwezesha kujikimu kimaisha baada ya kuajiriwa katika hoteli mojawapo jijini – uk 85/88
      16. Chandachema anaifunza jamii umuhimu wa bidii – licha ya kuwa motto mdogo, alijikakamua na kuchuma majanichai kwenye shirika la Tengenea asubuhi kabla ya kuenda shuleni na jioni baada ya kutoka shuleni ili kupata hela za kununua madaftari na sare za shule – uk 106
      17. Neema anaionyesha jamii umuhimu wa kuwatunza mayatima – anamchukua mpwawe Cynthia na kumlea baada ya wazazi wake wote kufariki dunia – uk 169
      18. Mwangeka na Mandu wanaonyesha jamii umuhimu wa kudumisha amani kwa kuenda katika mataifa ya nje kudumisha amani. Mwangeka alikuwa katika taifa la Mashariki ya kati – uk 5/115
      19. Mwangeka na Apondi wanaifunza jamii umuhimu wa kupanga uzazi – wanapanga kuwa na watoto wawili ili kuepuka kero la vinywa vingi vya kulisha. Uk 116
      20. Watu walikuwa na imani potofu kuwa uanajeshi ulitengewa tu watu wa viwango vya chini vya elimu lakini mwangeka anabadilisha imani hii kwa kujiunga na uanajeshi licha ya kuwa na shahada ya uhadisi kutoka chuo kikuu.
        Zozote 8 x 2 =16

A. CHokocho: Tulipokutana Tena
6.

  1. msemaji ni Sebu, akimwambia Kazu – akina kazu/ wakiwa hoteli ya Romeo. Sebu anarejelea uchawi wa akina kazu kwama ukalipiga pakacha teke, litalalamika. 1 x 4 =4
  2. mitindo
    1. swali la balagha – huchi kwamba unaniumiza?
    2. utohozi – shuti
    3. litifati – maneno ya pakacha yanasemwa na sebu
    4. uhuishi/tashihisi – pakacha lina uwezo wa kusema
      4 x 1 =4
  3. Maudhui ya anasa/raha/starehe/burudani
    Maudhui ya urafiki baina ya kazu na sebu
    Maudhui ya mapenzi kazu na mkewe /sebu na mkewe
    Maudhui ya ushirikiano /uchawi
    Maudhui ya kuwajibika – wanaamua kumtafuta Bogoa. 4 x 1 =4
  4. Ukiukaji wa haki za watoto
    1. Bogoa hataki kuenda kuishi na rafikiye babake mjini lakini babake anamlazimisha kumpeleka huko, hivyo kumtenga na familia ambayo hakutaka kutengana nayo kamwe.
    2. Bogoa anapokataa kutenganishwa na familia yake ili kuenda mjini na rafikiye babake, babake anatisha kumpiga kwa mkwaju iwapo hangekubali.
    3. Bi. Sinai hampeleki Bogoa shuleni. Anamfanyiza kazi tu. Anadai kuwa watoto wa kimaskini hawakustahiki kusoma; wanastahili kutumwa.
    4. Bi. Sinai anamtumkisha Bogoa, mtoto wa miaka tano. Anamfanyiza kazi kama vile kuchanja kuni, kufagia, kufua, kuteka maji kutoka kisimani na kuuza maandazi shuleni.
    5. Bogoa akiwa nyumbani kwa Bi. Sinai hakuwa na uhuru wa kucheza ila kwa kutoroka, Bi Sinai alipolala mchana baada ya kula.
    6. Bogoa alipochelewa kurudi nyumbani kutoka mchezoni, Bi. Sinai alimtafuta na alipompata alimpiga vibaya.
    7. Bi. Sinai hakumruhusu Bogoa kucheza na wanawe. Alicheza tu na watoto wa majirani kama vile Sebu.
    8. Bi Sinai alikuwa akimtusi na kumsimbulia Bogoa.
    9. Wazazi wake Bogoa walipomtembelea, Bi. Sinai alimzuia kuwa pamoja nao ili asiwaeleze dhiki alizokuwa akipitia mikononi mwake.
    10. Bogoa akiwa nyumbani kwa Bi. Sinai, alikuwa wa mwisho kula wakati kila mtu akiwa ashakula/alikula makombo ya watu waliyoacha baada ya kushiba.
    11. Bogoaalikula kwenye sufuria na vyungu wakati kila mtu katika familia ya Bi. Sinai alikula sahanini.
    12. B. Sinai alimtisha Bogoa kuwa angemkata ulimi iwapo angesema chochote kuhusu maisha ya familia yake – hivyo kumhofisha Bogoa kufichua siri kuhusu shida alizozipitia nyumbani kwake.
    13. Bogoa ambaye ni mtoto wa miaka mitano anaamshwa alfajiri kuchoma maandazi na kuenda kuyauza shuleni huku watu wazima kama Bi. Sinai wakiwa wamelala, hali inayomsababisha kusinzia akichoima maandazi.
    14. Bi. Sinai anamchoma Bogoa viganja vyake kwa kijinga baada ya kusinzia na kuacha maandazi kuungua.
      8 x 1 =8

7.

  1.                                
    1. matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yamesawiriwa kama daraja la kuwavusha wanafunzi hadi ufanisi na uluwa – Samueli alitegemea matokeo ya kidato cha nne kuwa daraja kati yake na ufanisi na uluwa.
    2. wanafunzi wanaiona shule kama jela. Baada ya kupokezwa matokeo ya mtihani, Samueli anafurahi na kumshukuru Mungu kuwa sasa hayupo kwenye jela iitwayo shule.
    3. matokeo ya kidato cha nne yanawasababishia wanafunzi woga. Wanafunzi waliokuwa wameenda kupokea matokeo yao ya kidato cha nne katika shule ya upili ya Busukalala walikuwa na hofu na misheshe nafsini mwao kwa kutofahamu iwapo walikuwa wamefaulu au wamefeli.
    4. elimu ina gharama – Baba Samueli anawauza ng’ombe ili kupata karo ya kumlipia Samueli.
    5. baadhi ya wanafunzi wamepujuka kimaadili – mfano, Samueli anamwita mwalimu wake mkuu hambe. Aidha anawaita wanafunzi wenzzake mahame, wadaku, wambea na chakubimbi
    6. baadhi ya wanafunzi hawang’amui wanayofundishwa. Kwa mfano, Samueli anasema kuwa mto Limpopo upo Misri na mto Zambezi upo Tanzania ilhali sivyo ilivyo
    7. wanafunzi wanaenda shuleni kwa miguu kila siku. Samueli alitembea kila siku kilomita sita kuelekea shuleni Busukalala.
    8. Kuanguka mttihani kunawatia wanafunzi wasiwasi. Baada ya kung’amua kwamba amefeli, Samueli anashindwa cha kuenda kuwaambia wazazi wake hasa babake.
    9. wazazi wanthamini elimu ya mtoto wa kiume kuliko ya mtoto wa kike – licha ya Bilha na Mwajuma kufaulu, baba yao aliwaona kuwa wanawake tu – fahari yake ya dhati ilikuwa katika kumwona mwanawe wa kiume Samueli – akifua dafu.
    10. wanafunzi wanakiuka mipaka ya uhusiano wao kwa kuanza kuhusiana kimapenzi kwa mfano, badala ya kuhusiana kimasomo, Nina na Samueli wanahusiana kimapenzi
    11. Wanafunzi wavulana wanatumia uongo ili kuwavutia wenzao wa kike. Kwa mfano, Samueli anamhadaa Nina kuwa yeye ni bingwa masomoni ili akubali kuwa mpenziwe.
    12. Kuanguka mtihani ni chanzo cha mwanafunzi kuwa mwongo- baada ya kufeli mtihani, Samueli anamhadaa babake kuwa mwalimu mkuu hakumpa matokeo ya mtihani
    13. Kufeli mtihani ni chanzo cha baadhi ya wanafunzi kujiua. Baada ya kufeli mtihani, Samueli anapanga kujiua. Anajitosa kwenye bwawa la maji ila anaokolewa na mpita njia.
      Zozote 8 x 1=8
  2. Shibe Inatumaliza
    1. sasa na mbura hawafanyi chochote cha kuwafaa maishani ila kusubiri kupewa.
    2. Mzee mambo ni waziri kivuli – hana wizara kamili lakini anapokea mshahara.
    3. viongozi/mawaziri hujiamulia kima cha mshahara wanachopokea.
    4. mzee mambo anapewa wadhifa ili kuongeza walaji
    5. Dini inatumiwa kuhalalisha haramu “Hadhaa min fadhil rabbi!”
    6. Viongozi wanabadiri fedha za umma – wanatumia kwa anasa- kusheherekea kuota kwa mtoto/mtoto kuingia shule ya chekechea.
    7. wanapofanya jambo linaloonekana la kifadhila wanajidai kwa mitandao/vyombo vya habari ili wajulikane kwa ufadhili wao.
    8. wanatumia magari ya umma /serikali kwa shughuli za kibinafsi.
    9. wanaandaa vyakula vya kila aina ilhali kama sasa na Mura huwa wenye njaa.
    10. shughuli kubwa katika sherehe ni kula bila kutoa mchango wa aina yoyote
    11. wanakula hawajali asili ya vyakula hivi
    12. walaji ni walafi, hula kupita kiasi
    13. Wakisha kula kazi yao huwa kulala – si kufanya kazi
    14. walaji hawavipendi vyakula vyao vya asili, wanashabikia mchele wa plastiki
    15. viongozi wanaibia umma la lawama haziwashtui kamwe
    16. dawa huibwa kutoka kwa mabohari ya serikali na kuuzwa katika maduka ya binafsi
    17. iongozi wanapata huduma za umeme, tiba bila kulipia ilhali maskini wanahangaika
    18. wanajiangamiza kwa kujiletea maradhi kama presha, bolisukari, saratani, vidondo vya tumbo, obesity.
    19. waliacha kufikiria kwa vile wanapata kila wanachokihitaji.
    20. watu wasio na elimu ndio viongozi
    21. mtu mmoja ana vyeo zaidi ilhali wengine hawana kazi zozote. 12 x 1 =12

8.

  1.                      
    1. mtanziko kwa vile hatimaye Nyati hakuweza kutoa uamuzi wa kuach vita au kuendelea na vita x 2
    2. minu tano za kimtindo
      1. Usimulizi
      2. Dayalojia
      3. Uhaishaji – wanyama kutenda kama binadamu
      4. Misemo – tia molea
      5. Chuku – kuwa na nguvu kupindukia
      6. Methali – kikulacho ki nguoni mwako
      7. Fonyula – hapo zamani
      8. Tabaini matumizi ya ‘si’
      9. Mninu rejeshi – hapo zamani 5 x 1=5
    3. umuhimu wa kushirikisha hadhira katika wasilisho
      1. Kuondosha ukinaifu
      2. Kulipa wasilisho uhai
      3. Huwapa kumbukizi ya matukio
      4. Huelewa funzo
      5. Watauliza maswali ili kueleweshwa
      6. Watajibu maswali ili kuonyesha uelewa wao
      7. Kuitikia huonyesha ukubalifu wao
      8. Kucheka kwao huonyesha kuburudika si haba
  2.                      
    1. kuandika vitabuni/ kuchapisha
    2. vinasa sauti/kurekodi
    3. filamu/ video
    4. Matandaoni/ mawinguni
    5. tarakilishi/vipatarakilishi/ vipakatalishi
    6. sidi/diski tepevu. Zozote 4 x 1=4
  3.                        
    1. gharama kuwa juu
    2. mtazamo hasi wa jamii
    3. kushukiwa kwamba mtafiti anawapeleleza
    4. wahojiwa kudai kulipwa
    5. mbinu nyingine kama hujaji huhitaji watu wanaojua kusoma na kuandika
    6. vikwazo vya kidini – fikiria kwamba matendo ya fasihi simulizi ni ya kishenzi
    7. kupotea na kufisidiwa kwa vifaa
    8. uchache wa wazee na wataalamu wa fasihi simulizi
    9. watawala kukataa kuoba idhini/ruhusa
    10. matatizo ya usafviri/matatgizo ya mawasiliano na uchukuzi
    11. hali mbaya ya anga
    12. kukosa wakati wa kutosha
    13. matatizo ya kibinafsi – mfano mtafiti kushindwa kuidhiiti hadhira.
    14. Ukosefu wa usalama
    15. Tatizo la tafsiri ya data
      Zozote 4 x 1 =4
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mincks Group of Schools Mock Examinations 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?