Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mathioya Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

Maswali

MAAGIZO

 • Jibu maswali manne pekee.
 • Swali la kwanza ni la lazima.
 • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki; yaani Tamthilia
 • Riwaya, Hadithi Fupi na Fasihi Simulizi.
 • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
 • Majibu yote lazima yaandikwa kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU YA A: SHAIRI
SWALI LA LAZIMA

 1. Soma shairi hili kisha ujibu maswali.
  Jicho, tavumiliaje, kwa hayo uyaonayo?
  Kicho, utasubirije, maonevu yapitayo
  Kwacho, lijalo na lije, nimechoka vumiliyo
  Naandika!

  Moyo, unao timbuko, maudhi tuyasikiayo
  Nayo, visa na mauko, wanyonge wayakutayo
  Kwayo, sina zuiliko, natoa niyahisiyo
  Naandika!

  Hawa, wanotulimiya, dhiki wavumiliayo
  Hawa, mamiya mamiya, na mali wazalishayo
  Hawa, ndo wanaoumiya, na maafa wakutayo
  Naandika!

  Hawa, sioni wengine, kwao liko angamiyo
  Hawa, uwapa unene, watukufu wenye nayo
  Hawa, bado ni wavune, kwa shida waikutayo
  Naandika!

  Bado, wawapo mabwana, wenye pupa na kamiyo
  Bado, tafauti sana, kwa pato na mengineyo
  Bado, tuling’owe shina, ulaji pia na choyo
  Naandika!

  Maswali
  1. Shairi hili laweza kuwekwa katika bahari zipi? Thibitisha kila jibu lako. (al 2)
  2. Eleza dhamira ya mshairi. (al 4)
  3. Onyesha mifano miwili ya uhuru wa kishairi jinsi ulivyotumika katika shairi. (al 2)
  4. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (al 3)
  5. Tambulisha kwa mifano mbinu zozote mbili za sanaa katika shairi. (al 2)
  6. Fafanua sifa nne za kiarudhi zilizotumika katika ubeti wa tano. (al 4)
  7. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumiwa katika shairi. (al 3)
   1. Zuiliko
   2. Wavune
   3. Wenye pupa na Kamiyo.

SEHEMU YA B: TAMTHILIA
Pauline Kea: Kigogo
Jibu swali la 2 au la 3

 1. “Ama kweli dunia gunia. Ilikumeza hindi bichi ikakuguguna, sasa inakutema guguta.”
  1. Fafanua muktadha wa dondoo hili. (al 4)
  2. Tambua tamathali mbili za usemi katika dondoo hili. (al 2)
  3. Eleza umuhimu wa mazingira waliyomo wahusika katika dondoo hili. (al 4)
  4. Wananchi katika tamthilia hii wamegugunwa na madhila kadhaa ya kisiasa. Dhibitisha. (al 10)
 2.     
  1. Juhudi za kujikomboa za jamii kutokana na matatizo yanayowakumba zinatingwa na changamoto si haba. Fafanua ukiegemea tamthilia ya Kigogo. (al 10)
  2. Kutokomaa na kutoadilika kwa viongozi ni kizingiti kikubwa cha maendeleo katika jamii ya Wanasagamoyo. Eleza kwa kutumia hoja kumi. (10)

SEHEMU YA C: RIWAYA
Assumpta Matei: Chozi La Heri
Jibu swali la 4 au la 5

 1.      
  1. “Vita vya baada ya uchaguzi vinasambaratisha na kukwaza maendeleo ya jamii”. Fafanua usemi huu ukuegemea riwaya ya Chozi La Heri. (al 10)
  2. Kwa kutumia hoja kumi, eleza nafasi ya vijana katika kuijenga jamii mpya ukirejelea riwaya ya Chozi la Heri. (al 10)
 2. “Hili ni pigo la tatu kutoka kwa walimwengu. Tofauti ni kwamba hili linauma na kudhalilisha zaidi…….”.
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (al 4)
  2. Ni mapigo yepi manne aliyoyapitia mrejelewa katika dondoo hili. (al 4)
  3. Eleza umuhimu wa mrejelewa kataka kujenga mtiririko wa vitushi katika riwaya ya Chozi la Heri. (al 12)

SEHEMU YA D: HADITHI FUPI
A.Chokochoko na D. Kayanda: Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine.
Jibu swali la 6 au la 7

 1. Eunice Kimaliro: Mtihani wa Maisha
  1. Changanua mtindo katika dondoo hili. (al 10)
   “Punde mwalimu mkuu ananyanyuka kitini na kulivuta karibu naye daftari jingine lililo mezani……Bodi ya usimamizi wa shule vilevile inajua hilo naye mmiliki wa shule anajua hilo pia. ...wanaodaiwa karo hawayaoni matokeo ya mtihani wao ng’o! Waliosema masomo si biashara wanaishi sayari nyingine! ……Anakitazama kidole cha mwalimu mkuu kikipiga masafa kwenye orodha ndefu ya majina. Kinatua kwenye jina lake. Kimya. …anamtupia kama mtu anavyomtupia mbwa mfupa…. Labda mwalimu mkuu kazidiwa na maumivu….
  2. Jamii imeekeza katika elimu. Fafanua ukijikita katika hadithi ya Mtihani wa Maisha. (al 10)
 2.    
  1. Maudhui ya ubadhirifu yamekita katika hadithi ya Shibe Inatumaliza. Jadili huku ukitoa mifano mwafaka. (al 10)
  2. “Ile haikuwa ziara ya muda mfupi. Pale nilipokwenda kulelewa, palikwa jahanamu kwangu.” Eleza ukweli wa usemi uliopigiwa mstari ukijikita katika hadithi ya Alifa Chokocho: Tulipokutana Tena. (al 10)

SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI

 1. Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali uliyopewa.

  Msichana wa sura nzuri
  Kitu gani kinakufanya usiolewe
  Elimu unayo ya kutosha
  Hata ng’ambo ukaenda ukarudi

  Msichana wa urembo kama wewe
  Uonyeshe mapenzi kwa vijana
  Ukionyesha majivuno kwa vijana
  Utazeeka ukiwa nyumbani kwenu

  Ooh baby, miaka yaenda mbio sana
  Na sura yako nayo ikichunjuka
  Ooh baby, miaka yaenda mbio sana
  Na sura yako nayo ikichuchuka

  Pengine tabia zako ndizo mbaya
  Awali kweli dada ulijivuna
  Kwanza mimi nilitaka nikuoe
  Ukaringa ati sina masomo

  Ooh baby, ona watoto wa nyuma yako
  Wameolewa wamekuwacha ukihangaika
  Ooh baby, ona watoto wa nyuma yako
  Wameolewa wamekuwacha ukihangaika

  Msichana wa sura nzuri
  Kitu gani kinakufanya usiolewe
  Elimu unayo ya kutosha
  Hata ng’ambo ukaenda ukarudi
  1.     
   1. Taja shughuli mbili za kijamii katika utungo huu. (al 2)
   2. Fafanua mbinu zozote mbili za kimtindo katika utungo huu huku ukitoa mifano mwafaka. (al 2)
   3. Eleza toni ya utungo huu. (al 2)
  2. Wewe kama mwasilishaji wa kazi ya fasihi simulizi, ni mbinu zipi ungetumia ili kufanikisha uwasilishaji wa utungo huu? (al 5)
  3. Taja changamoto nne zinazokumba kukua na kuendelea kwa fasihi simulizi. (al 5)
  4.  Ni sababu zipi zinaweza mfanya fanani kufaragua katika uwasilishaji wa hadithi? (al 4)

Mwongozo wa Kusahihisha

 1.      
  1. Tarbia - Lina mishororo minne katika kila ubeti
   Msuko - Kibwagizo kimefupishwa.
   Ukara- Vina vya nje vinatiririka katika beti zote ilhali vya ndani havitiririki.
   Ukawafi- Una vipande vitatu (ukwapi, utao na mwandamizi) katika mishiroro ya kwanza mitatu ya kila ubeti isipokuwa kibwagizo
   Kikwamba – Katika beti za 3-5 neno moja ndilo linaanza kila mshororo.
   Sakarani – Kuna bahari kadhaa katika shairi.
   2x1=2
  2. Kuwahimiza watu (hasa wanyonge ✓) wainuke na kupinga ✓maovu na maonevu wanayofanyiwa na matajiri wenye uwezo.
   4x1=4
  3. Inkisari km vumiliyo – kuvumilia nanaandika.
   Mazida kurefusha k.m. angamiyo, vumiliyo n.k.
   Tabdila k.m mamiya badala ya mamia .
   2x1=2
  4. Hawa wanaotulimia wanavumilia✓ dhiki
   Wao ni wengi ✓ na ndio huzalisha mali.
   Wao ndio wanaoumia✓ na kupata mateso / taabu
   Wanayokumbana nayo.Ninaandika / ninasema
   3x1=3
  5. Takriri – hawa, bado, mamiya.
   Balagha – uyaonaje?
   Taharuki – Naandika!
   Inkisari – Hawa, ndo
   Kinaya – Watukufu wenye nayo
   2x1=2
  6. Kuna mishororo minne
   Kuna vipande vitatu katika mishororo ya kwanza mitatu na kimoja katika kibwagizo
   Vina vinatiririka / vinafanana
   Mizani haitoshani kutika mishororo yote mine.
   Lina beti tano.
   Lina kibwagizo.
   4x1=4
   1. Cha kunizuia / kizuizi / kizingiti / uoga / hofu/ pingamizi
   2. Wachovu /dhaifu /hafifu
   3. Walio na tamaa kubwa / walafi/ mabwanyenye
    3x1=2
 2.     
  1. muktadha wa dondoo.
   • Msemaji- Majoka
   • Msemewa- Ashua
   • mahali- wakiwa ofisini.
   • Wakati- majoka anamsimanga Ashua kwa kukamtaa kumpenda na kujihusisha naye kimapenzi. Anasema sasa Ashua amezeeza ka kuparara kwa kuolewa na maskini.
    4x1=4
  2. Tamathali za usemi
   • Nahau-dunia gunia
   • Jazanda- hindi bichi…. Guguta.
    2x1=2
  3. Umuhimu wa mazingira( ofisi ya Majoka)
   • Mazingira haya yanaonyesha tofauti za kitabaka kiuongozi pale ambapo viongozi kama Majoka wanaishi maisha ya kifahari huku wanachi kama Ashua akikosa hata pesa za kuwalisha wanawe.
   • Mazingari haya yanadhihirisha uozo ulioko katika jamii kwani Majoka anataka kusinzi lakini Ashua anakataa.
   • Pia mazingira haya yanatuonyesha jinsi ambavyo viongozi wengine ni wabinafsi. Shule ya Majoka imejaa makabeji kutoka na wanafunzi kutumia dawa za kulevya.
   • Kupitia mazingira haya pia tunakuja kujua kuwa Ashua ni mzalendo kwani anakataa kazi katika shule ya Majoka na kuiita ya kihuni.
   • Pia mazingira haya yanaweka wazi shida wanazozipitia wanachi. Watoto wa Ashua walilala njaa.
   • Ulafi na tamaa ya viongozi pia umewekwa wazi katika haya mazingira. Majoka alifunga soko lililokuwa tegemeo la pekee la wananchi kwa madai ati ni chafu.
   • Ufisadi pia na matumizi mabaya ya vyombo vya dola umedhihirika katika mazingira haya. Ashua anasema kuwa kuku hawezi pata haki kama kipanga ndiye hakimu.
    4x1=4
  4. wananchi wamegugunwa na madhila ya kisiasa.
   • Jabali mpinzani wa Majoka anauliwa kwa kuupinga uongozi wake kwa kupangiwa ajali.
   • Ashua anatiwa gerezani ili kumshinikiza Sudi mpinzani wake Majoka kumchongea kinyago.
   • Tuna anapangiwa njama ya kuuliwa na kuumizwa vibaya karibu afe.
   • Wanasagamoyo wanafungiwa soko ambalo wanalitegemea.
   • Kandarasi zinapeanwa kwa mapendeleo. Asiya anapewa kandarasi ya uokaji keki kwa kujua na Husda mkewe Majoka.
   • Vijana wengi wanaaga dunia kwa kubugia pombe haramu iliyo hararishwa na uongozi wa Majoka.
   • Ukataji wa miti unaohararishwa na Majoka unasababisha ukame.
   • Watu wanaishi kwa hofu kwa kutishiwa kuhama na uongozi wa majoka.
   • Vijana watano wanauliwa wanapoandama kutokana na kupandishwa kwa bei ya chakula kiwandani.
   • Vyombo vya habari vinafungwa kiholela kwa kupeperusha habari zinazompinga Majoka. Yeye hataki upinzani.
   • Kiwanja cha soko la Chapakazi kimenyakuliwa na Majoka ili ajenge hoteli ya kibinafsi.
   • Sagamoyo hamna ajira kwa vijana waliohitimu. Kina Sudi wanasalia kuchonga vinyago kutokana na uhaba wa kazi.
   • Majoka ako na kikosi sugu cha kuwaadhibu wapinzani wake kikiongozwa na mshauri wake Kenga. Tunu anavamiwa.
   • Chopi anapangiwa njama ya kuuliwa kwa kujua siri nyingi za Majoka. Alikuwa askari mtiifu sana.
   • Kingi anafutwa kazi kwa kukataa kupiga risasi waandamanaji kinyume cha sheria.
   • Kadiria hoja zingine.
    10x1=10
 3.  
  1. juhudi za kujikomboa za Wanasagamoyo zinatingwa na changamoto nyingi.
   • Kuuliwa kwa viongozi wao-jabali aliuliwa kupitia ajali ya barabarani.
   • Kuvamiwa na kuumizwa kwa viongozi wapinzani-tunu anachapwa na kuumizwa mfupa wa muundi.
   • Vijana kuuliwa wakiandamana kutokana na bei za juu za chakula.
   • Kingi anafutwa kazi anapopinga amri ya kuwapiga watu risasi.
   • Ashua anatiwa ndani Sudi anapokataa kumchongea kinyago majoka na kuupinga uongozi wake.
   • Vijana wanawasaliti wenzao wanaopigania haki za jamii. Ngurumo anapinga mpango wa kuwaunganisha wanasagamoyo kupigania haki zao.
   • Vijana wanaopinga uongozi dhalimu wa majoka wanatupiwa vijikaratasi wahame Sagamoyo hata kama ndiko nyumbani kwao.
   • Kina Boza na Kombe wanaongwa na vijikeki ili waendelee kuwa vikaragosi wa uongozi wa Majoka.
   • Juhudi za kujikomboa na uongozi mmbaya wa majoka zinatingwa na mpango wa Majoka na watu wake wa kuwanunulia pombe ili wasione haja ya kufunguliwa kwa soko.
   • Wanasagamoyo wanalemazwa kwa kufungiwa soko ili waendelee kumwabudu Majoka na uongozi wake.
   • Kituo cha runinga ya mzalendo kinafungwa kwa kuwazindua wananchi kuhusu haki zao.
   • Majoka ametawala Nyanja zote za kiuchumi za jimbo na kuwalemaza wananchi kiuchumi ili wakose uwezo wa kumpinga. Ana kampuni, shule na mahoteli ilhali wananchi wengi ni maskini.
   • Majoka anatumia polisi vibaya. Maandamano yote yazimwa kwa vitoza machozi na risasi.
   • Majoka anaeneza propaganda za kuwapiganisha wanaharakati. Wavamizi wa Tunu waliotumwa na Majoka wanamwambia kuwa roho yake inawindwa na Sudi na Ashua kutokana na uhusiano wake na Sudi.
    10x1=10
  2. kutokomaa kwa viongozi na kutoadilika ni kizingiti cha maendeleo ya jamii.
   • Ufisadi wa Majoka unafanya vijana wengi kupoteza maisha kutokana na unywaji wa pombe haramu aliyoihararisha.
   • Ulafi wa majoka unamsukuma kunyakua kiwanja cha soko la Chapakazi lililokuwa tegemeo la kiuchumi la wengi.
   • Kutokamaa kwa Majoka kunamfanya aamrishe kupigwa risasi kwa wananchi waliokuwa wakiandamana kutokana na kufungwa kwa soko.
   • Kutokomaa kwa Majoka kidemokrasia kunamfanya umwangamize mpinzani wake Jabali ili asipingwa na yeyote.
   • Ulafi wa majoka unafanya awauzie vijana dawa za kulevya shuleni hivyo kuwafanya kuwa mazuzu na makabeji.
   • Kutokana na kutokomaa kwa Majoka, anakosa kujua umuhimu wa miti kwa mazingira hivyo anafungulia biashara ya ukataji wa miti kiholela inayoathiri mazingira na ukulima kwa jumla..
   • Kutokomaa kwake pia kunamfanya akope mikopo kutoka nchi za nje ili kufadhili miradi isiyomuhimu. Wananchi watalipa madeni haya kwa miaka mia moja.
   • Kutoadilika kwa Majoka kunamfanya ampe Asiya kibali cha kuuza pombe hivyo kuwasukumiza vijana wengi katika ulevi na matumizi ya dawa za kulevya badala ya kujenga nchi.
   • Kandarasi sagamoyo zinapeanwa kwa mapendeleo kwa marafiki wa karibu wa uongozi wa Majoka. Asiya ndiye muokaji wa keki za uhuru jambo ambalo ni hatari kwa uchumi kwani ni ufisadi.
   • Elimu sagamoyo pamoja na mambo mengine kama umeme, maji safi na huduma za afya ni ndoto kwa Wanasagamoyo wengi. Hii ni kutokana na uongozi mbaya wa Majoka.
   • Uongozi katika serikali ya Majoka ni wa kinasaba. Mshauri wake mkuu ni binamu yake na ana mpango wa kumrithisha Ngao Junior uongozi wa jimbo.
   • Ukware na kutoadilika kwa Majoka kunaathiri ndoa yake na kumkosanisha na wananchi wengine kama Ashua anayetaka ampende kwa nguvu.
   • Wananchi Sagamoyo hawana haki ya kujitetea. Wanaondamana wakabiliwa vikali na polisi huku walimu na wauguzi wakiongezewa mishahara huku kodi ikizidishwa maradufu.
    10x1=10
 4. RIWAYA
  1. Vita vya baada ya uchaguzi vinatinga na kusambaratisha maendeleo.
   • Ridhaa anaipoteza familia yake kutokana na mkasa wa moto uliosababishwa na jirani yake Mzee Kedi kutokana na sababu za kikabila.
   • Vijana barabarani wanapoteza maisha wanapopigwa risasi wakiandamana na polisi.
   • Lime na Mwanaheri wanabakwa na vijana kutokana na sababu ya kikabila baada ya kuzuka kwa vita vya baada ya uchaguzi.
   • Watu wengi wanatoroka makwao wakikimbilia usalama baada ya vita vya baada ya uchaguzi. Ridhaa na Kaizari wanakimbilia usalama wao.
   • Jumba la kifahari la Ridha linachomwa na jirani yake Mzee Kedi.
   • Wananchi wanateseka kwa kukosa chakula na maji safi kwenye Msitu wa Mamba baada ya kutoka makwao vita vinapozuka.
   • Watu wengi wanapoteza maisha yao na mali zao. Kaizari anaacha kila kitu na kutoroka ili kuiokoa familia yake.
   • Vita vya baada ya uchaguzi vinapelekea uharibifu wa mali. Magari mengi na maduka yanachomwa na waandamanaji wanaopinga kutawazwa kwa Mwekevu kama kiongozi wa Wahafidhina.
   • Vita vya baada ya uchaguzi vinapelekea kuharibiwa kwa mazingira wahasiriwa wanapotafuta hifadhi katika msitu wa Mamba.
   • Ndoa zinasambaratika kutoka na vita hivi vya baada ya uchaguzi. Selume anaachwa na mumewe kutokana na msimamo wake wa kisiasa.
    10x1=10
  2. Nafasi ya vijana katika kuijenga jamaa mpya.
   • Chandachema unasoma kwa bidi ili kuwa mwanasheria aweze kuzitetea haki za watoto.
   • Dick anaachana na ulanguzi wa dawa za kulevya na kuanza biashara ya vyombo vya kielektroniki ili kujijenga kimaisha.
   • Mwangeka anaenda kudumisha Amani nchi za mbali ili waweze kujisitiri na kujikuza baada ya vita.
   • Pete anappojipata katika kituo cha afya cha Mwanzo Mpya, anaamua kuufikiria mkabala wa maisha yake upya baada ya kunusurika kifo.
   • Tuama anaamua kusaidia katika kupigana vita dhidi ya ukeketaji anaponusurika na marafiki wake kuaga wakikeketwa.
   • Umuheri anasoma na kuendelea kutia bidi akiwa na matumaini kuwa angeungana na ndugu zake waliotekwa nyara.
   • Baada ya Sauna kubakwa na babake mlezi, anaingia mjini na kuanza kufanya kazi tofauti tofauti ili kijikimu.
   • Hazina ananusuriwa na serikali kutoka kuranda mtaani anaamua kusoma na kuwa mhudumu wa makahawani. Anamsaidia Umu.
   • Apondi anawahutubia askari na mashirika mengi ya usalama umuhimu wa usalama na kutotumia nguvu kupita kiasi.
   • Mwangeka anaamua kuoa ili kuanza maisha yake upya baada ya familia yake kuangamia kutokana na mkasa wa moto.
   • Mwangemi na Neema wanaamua kupanga mtoto baada ya mtoto wao kufa. Wanapendana na hawangetaka ndoa yao usambaratishwe na ukosefu wa mtoto.
   • Dick anaamua kurudi shuleni ili kuweza kujitia makali kielimu na kufanya vizuri Zaidi katika uwanja wake wa kibiashara.
   • Kipanga anaamua kuacha ulevi na kurudi shuleni hata baada ya kukataliwa na babake mzazi.
   • Mwanaheri anatia bidii masomoni na kuahidi kumsaidia dadake Lime hata baada ya kuachwa na mamake Subira.
    10X1=10
 5.    
  1. Muktadha wa dondoo
   • Msemaji- mwandishi
   • Mrejelewa-Lunga Kiriri Kangata
   • Mahali- nyumbani kwa Lunga Mlima wa Simba
   • Wakati- hii ni baada ya Lunga kuacha na bibiye Naoma baada yao kufukarika wanapohamishwa kutoka Msitu wa Mamba.
    4x1=4
  2. Mapigo manne aliyopokea Lunga.
   • Anafutwa kazi katika shirika na nafaka la Fanaka baada ya kupinga uagizaji wa mahindi yenye majano.
   • Anaachwa na bibiye Naoni baada ya kufilisika akidai kuwa anaondoka kwenda kumsaidia kuikimu familia.
   • Anapoteza mali nyingi wanapohamishwa kutoka msitu wa Mamba alikokuwa mkulima hodari.
   • Baada ya kuachwa na mkewe Lunga anapatwa na kihoro cha upweke kinachosababisha kifo chake.
   • Kifo chake kinawaacha watoto wake mikononi mwa Kijakazi Sauna anayewateka nyara.
    4x1=4
  3. Umuhimu wa Lunga katika kujenga mtiririko wa vitushi(ploti)
   • Kupitia kwa Lunga tunaona jinsi mashirika ya kiserikali yamejaa ufisadi. Anatumiwa barua ya kufutwa kazi kwa kupinga uagizaji wa mahindi yenye sumu.
   • Pia lunga anatumika kuonyesha nafasi ya wazazi katika maisha ya watoto wao. Anapoaga dunia watoto wake wanatekwa nyara na mwingine Umu kuhangaika mno.
   • Kupitia kwa Lunga mbinu ya kutumia barua kama mbinu ya kimtindo inafanikiwa. Anatumiwa barua ya kufutwa kazi pamoja na ujumbe anaoachiwa na mkewe Naomi wa kumuacha.
   • Lunga anasaidia katika kukuza wahusika kama Naomi ambaye anaonekana mwenye tamaa ya mali.
   • Uhifadhi wa mazingira unatiliwa mkazo kupitia kwake Lunga. Akiwa shule alijulikana kama amri jeshi wa mazingira.
   • Kupitia kwake tuoana jinsi wanaume wanaumia baada ya kuachwa na mabibi zao. Anapatwa na kihoro na kuaga anapoachwa na Naomi.
   • Kupitia kwa Lunga sifa za wahusika kama Naomi zinadhirika kama mtu mbinafsi.
   • Lunga pia anawikilisha wananchi wanaoshiriki katika kuyaharibu mazingira ili kutimiza haja za kibinafsi. Anakata miti na kulima shamba kubwa katika msitu wa Mamba.
   • Lunga anaonyesha umuhimu wa elimu katika jamii. Anasoma na kuhitimu na hivyo kupata kazi kama meneja katika shirika na serikali la nafaka.
   • Lunga anawakilisha walezi wema. Anapoemewa na kuzidiwa na afya yake. Anawaacha watoto wake mikononi mwa Anti Sauna ili awatunze.
   • Kupitia kwa Lunga maudhui ya ndoa, malezi na kazi yanakuzwa.Anawakilisha vijana ambao wanalelewa katika umsikini lakini kutokana na bidii zao wanaweza kuboresha maisha yao. Lunga aliishi maisha ya kifahari pamoja na familia yake kabla ya kufutwa kazi.
    12x1=12
 6. HADITHI FUPI
  1. mtindo wa dondoo
   • Mdokezo-mezani…
   • Takriri-vilevile inajua…shule anajua
   • Utohozi-bodi
   • Tanakali za sauti-ng’o!
   • Nidaa-nyingine !
   • Taswira oni-anakitazama kidole
   • Taharuki-kinatua kwa jinalake. Kimya.
   • Tashbihi-anamtupia kama mtu…
   • Uzungumzi nafsi-labda mwalimu mkuu kazidiwa na maumivu..
   • Tashihisi-kidole kupiga masafa
    10x1=10
  2. jamii imekeza katika elimu
   • Babake samweli anampeleka shuleni ili aweze kuwafaa siku za usoni.
   • Mwalimu mkuu anadhibitisha kwanza kama mwanafunzi amelipa karo kabla ya kumpa matokeo. Elimu kwake ni biashara.
   • Bodi ya shule na mmiliki wa shule wanajua fika kuwa wanaosema elimu si biashara wanaishi sayari nyingine.
   • Kwake baba Samweli kuwafunzi binti wake si jambo la kujivunia kwani anaona kuwa wataolewa na kulepeleka ufanisi wa elimu yao kwa waume zao.
   • Samweli anatembea mwendo wa kilomita sita kwenda na kurudi shule ili kupata elimu na kuwasaidia wazazi wake.
   • Babake samweli anauza ng’ombe ili aweze kumpa mwanawe wa kiume wa pekee elimu.
    5x2=10
 7.   
  1. ubhadhirifu katika hadithi ya shibe inatumaliza.
   • Mzee mambo analipwa mshahara mnono kama mkuuwa wizara zote ilhali kila wizara ina waziri wake.
   • Sherehe kubwa za viongozi wa serikali zinatumia mali ya umma kwa manufaa yao wenyewe. Magari ya serikali yanatumika katika sherehe ya Mzee Mambo kuchotea maji na kusafirisha wageni.
   • Vyakula katika sherehe vinanunuliwa kwa pesa za umma. Pesa hizi zingetumika kuendeleza asasi za kijamii.
   • Ubadhirifu unadhihirishwa na DJ pale anapokeaa mabilioni ya pesa kwa kuwatumbuiza wageni katika sherehe.
   • Ubadhirifu unadhihirishwa na viongozi wa serikali wanaowachukua watu wao wa karibu na kuonelea wamefaidika kutokana na raslimali za wanajamii bila kutolea jasho.
   • Uuzaji wa dawa zilitolewa katika bohari la kitaifa katika duka la DJ ambayo ni biashara ya fedha ni ubadhirifu wa mali ya umma
   • Upeperushwaji wa habari za sherehe ya kibinafsi kwenye vituo vya habari vya serikali ni ubadhirifu wa mali ya umma.
   • Viongozi wa serikali kama vile Sasa na Mbura kujipakulia chakula kingi kupita kiasi katika sherehe ya Mzee Mambo ni ubadhirifu wa raslimali.
 8. FASIHI SIMULIZI
  1.            
   1. shughuli za kijamii
    • Elimu
    • Ndoa
     2X1=2
   2. mbinu za kimtindo
    • Kuchanganya ndimi-ooh baby
    • Taswira oni-sura nzuri
     2X1=2
   3. toni ya utungo
    • Toni ya huzuni-nafsi neni anahuzunika kwa kukataliwa na msichana mrembo.
    • Toni ya masimango-anamsimanga Yule msichana kwa sababu amezeeka kabla ya kuolewa. 2x1=2
  2. jinsi ya kufanikisha uwasilishaji wa fasihi simulizi
   • Kuvaa maleba panapohitajika.
   • Kubadilisha toni ipasavyo ili iwiane na matukio ya uwasilishaji wako.
   • Miondoko ya viungo vya mwili pia ni muhimu.
   • Kuihusisha hadhira pia njia nzuri ya kufanikisha uwasilishaji wa fasihi simulizi.
   • Kutumia ala husika hasa katika kipera cha ushairi simulizi.
   • Kuwasilishia kazi hii mahali panapofaa. Mfano, jukwaani.
   • Kuhakisha kwamba umezingia utamaduni wa jamii husika.
   • Pia ni vizuri kutilia maanani umri na kiwango cha elimu cha hadhira yako.
    5x1=5
  3. Changamoto zinazokumba kuendelea na kuenea kwa fasihi simulizi
   • Kukua na kuendelea sana kwa kazi ya kimaandishi.
   • ukosefu wa utafiti wa kutosha kuhusu fasihi simulizi.
   • Uchache wa wataalam wa kutosha wa kutafitia kazi ya fashihi simulizi.
   • maendelea ya kiteknolojia na sayansi yanayo athiri mtazama ya jamaa kuhusu fasihi simulizi.
   • Watu kuhamia mjini na kutangamana na watu wa jamii zingine tofauti kunafanya uhifadhi wa fasihi simulizi kuwa mgumu mno.
   • Mtaala wa elimu pia umepuuza lugha za kiasili ambazo ndizo nyenzo kuu ya kurithisha fasihi simulizi.
  4. Sababu za kufaragua
   • Fanani huenda akasahau na kubadilisha mtiririko wa hadithi
   • Anaweza kubadilisha ili kukidhi mahitaji ya hadhira yake k.v umri
   • Mabadiliko ya kiwakati pia yanaweza kumfanya afarague ili kuingiliana kiwakati na hadhira.
   • Kila fanani huwa na mtindo wake wa kuwasilisha.
   • Ubunifu wa fanani ili uwasilishaji wake uweze kuvutia zaidi
   • Mabadiliko ya falsafa ya vizazi na maingiliano katika jamii kusababisha kurithisha tu yale ambayo ni muhimu na kuacha mengine.
   • Kutoeleweka hivyo kuhifadhiwa vibaya.
    5x1=5

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Mathioya Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?