Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa II Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

Maswali

  1. UFAHAMU (ALAMA 15)
    Soma masimulizi yafuatayo kisha ujibu maswali yanayofuata.
                  Tuliongozana sote watatu hadi ofisi ya Hatubagui Publishers. Njiani Pam aliyenichukulia zawadi, alinichangamkia na kunizungumzia kama kurumbiza. Tim alijitia tabasamu bandia, lakini kainama kama kondoo. Haikosi alibeba mazito moyoni.
                  Meneja wa uchapishaji wa kampuni hiyo ya uchapishaji alikuwa mwanamme mmoja wa makamo, mwembamba, aliyevalia miwani. Alikuwa hana ubaguzi hasa. Alitupokea kwa mawili-matatu hata kabla ya kutujua sisi nani. Hakuwa na vikwazo vya kumwona. Nilipojitambulisha kwake alionyesha msisimko mkubwa.
                  “Umemlanda babako kweli kweli, hukumbakisha,” alimaka. “Hamjambo?”
                  “Mgonjwa, ndio maana amenituma kwako,” nikajibu. “Ataka ajue diwani yake itachapishwa lini? Mbona nyie wachapishaji mnakawia sana na miswada ya watu? Kama muswada ni mbaya hauchapishiki rejeshea mwenyewe haraka.”
                  “Lo! Hajapokea kifurushi chetu bado?” aliniuliza meneja.
                  “Kipi?”
                  “Diwani ya Mzee Sululu tuliichapisha miezi sita iliyopita. Tulimtumia nakala zake sita kwa njia ya posta.”
                  “Kweli?”
                  “Basi hajazipata bado?”
                  “Nimetoka nyumbani siku chache zilizopita na alikuwa bado hajapata chochote.”
                  “Basi wafanyikazi wa posta wamenyakua kifurushi hicho. Wengi wao ni kama paka waliowekwa kulinda kitoweo. Kawaida yao kudondoa mali za watu, na kuzichelewesha barua kufika.”
                  Meneja wa uchapishaji alinyanyuka kitini. Akafungua kabati alimotoa nakala sita za diwani ya babangu akazitia kwenye katoni ndogo na kunipa.
                  “Mpelekee Mzee nakala hizi,” akaniambia.
                  “Ahsante bwana,” nikamshukuru. “Amesubiri miaka zaidi ya kumi na kitu tangu kuwasilisha muswada wake. Hapana shaka kwamba atafurahi sana. Alikuwa anahofia kupatwa na kifo pasi kukiona kitabu chake kwenye chapa.”
                  “Na hii hapa nakala yako Bwana mdogo,” alinipa nakala moja ya kitabu hicho.
                  Kilikuwa na jalada ya binti mrembo na anwani Kero za Mkiwa. Nilishukuru, tukamuaga na kwenda zetu.
                  Hayawi hayawi huwa. Ndoto ya baba imetimia hatimaye. Furaha yangu kwa kukiona kitabu cha babangu mahabubu kimechapishwa ilihafifisha mengine yaliyonitendekea kutwa hiyo, mabaya na mazuri. Nilitafahari. Niliterema. Nilijitanua kifua. Hatubagui publishers sio kampuni uchwara ya uchapishaji. Ni miongoni mwa mashirika ya uchapishaji vitabu yenye kuheshimika sana nchini. Baba alikuwa kafaulu kutenda kilichowashinda hata baadhi ya wanachuo, licha ya kisomo chake haba. Ari na bidii yake havikwenda bure yao. Subira yake ilikuwa imevuta heri.
                  Nilikumbuka alivyojiendeleza mwenyewe kimasomo baada ya ya kuhitimu elimu ya ngumbaru. Nikafikia hitimisho kuwa nia ni nguzo muhimu katika maisha ya binadamu; humkokota mtu ikamfikisha kusikotarajiwa katu.
    (Kufa Kuzikana - Ken Walibora(2003) uk 51-53)
    Maswali
    1. Linganua hasia za marafiki za msimulizi walipokuwa njiani. (Alama 2)
    2. Meneja wa Hatubagui Publishers ni mtu mbaraza. Toa ushahidi kifunguni. (Alama 3)
    3. Kifungu hiki kinaonyesha hali kadha za kutamausha. Thibitisha. (Alama 3)
    4. Kwa kumrejelea Mzee Sululu, tetea kauli “…nia ni nguzo muhimu…humkokota mtu ikamfikisha…” (Alama 2)
    5. Tambua mbinu zozote tatu za lugha zilizotumika kifunguni. (Alama 3)
    6. Fafanua maana ya vifungu hivi kama vilivyotumika kwenye masimulizi. (Alama 2)
      1. Haikosi alibeba mazito moyoni
      2. Ni paka waliowekwa kulinda kitoweo

UFUPISHO (ALAMA 15)
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali
                Je, mtazamo hasi ni nini? Huwa na athari gani kwa binadamu? Mtazamo hasi ni kukata tamaa, kutamauka kuhusu hali, mtu au jambo fulani. Ni hisia ya kutotaka kushiriki wala kuhusishwa na jambo au hali fulani. Mtazamo huu ndio huwafanya wanafunzi kuchukia au hata kudunisha baadhi ya masomo na walimu wanaoyafundisha. Licha ya wengi kuwa na mtazamo huu, kwa kweli huwa hawatambui. Asilimia kubwa ya wanaotambua hutatizika kujikwamua kutoka katika hali hii.
                Inakadiriwa kwamba mtu wa wastani huwa na takribani mawazo elfu sitini ya kibinafsi kwa kila saa 24. Asilimia 95 ya fikra hizi huwa sawa na siku iliyotangulia na asilimia 80 ya fikra hizi zilizorudiwa huwa hasi. Isioshe, fikra hizi nyingi hutokea bila mtu mwenyewe kutambua na huwa ni mazoea. Hii ina maana kwamba watu wengi hawana ufahamu wa atahri za fikra hizi maishani mwao.
                Mitazamo hasi ina vyanzo na pia suluhu. Mwanzo kabisa ni imani potovu. Hiki ndicho chanzo cha mitazamo hasi. Kushikilia imani potovu kuhusu maisha pamoja na matukio fulani maishani hujenga mtazamo hasi. Unayaona maisha kwa macho ya imani zako na iwapo imani hizo ni potovu basi hutayathamini maisha yako. Ili kukabiliana na hali hii, sharti kwanza ubadili imani yako. Uamini kwamba mabadiliko yanaweza kutokea na uchukue hatua ya kuanzisha mabadiliko hayo maishani mwako. Unahitaji kuepuka fikra hasi zinazoambatana na maisha yako ya awali na kulithamini kila tukio maishani kama tukio huru; lisilo na uhusino na yaliyowahi kukutamausha.
                Kujikwamua kutoka katika imani duni unahitaji kuibuka na idadi kubwa ya imani chanya kuliko zilizo hasi kuhusu hali mahususi. Baada ya hilo, zikabili imani zako potovu moja baada ya nyingine huku ukijiuliza endapo imani hizo ni kweli na endapo zina mashiko. Tumia dakika tano hivi kila siku kushadidia fikra chanya inayokinzana na ile inayokudidimiza. Ukifanya hivi kwa takribani siku thelathini imani yako itaanza kuchukua mkondo unaofaa. Familia yako na rafiki unaoandamana nao huathiri pakubwa hisia zako. Wakiwa na mtazamo hasi huweza kukushawishi ukaanza kuhisi wanavyohisi na kuyaona mambo kwa mtazamo wao. Kukabiliana na hali wapaswa kudhibiti hisia zako.
                Tawala namna unavyohisi na kukabiliana na hali mbalimbali bila kuathiriwa na wandani hawa. Epuka wandani wa aina hii kadri inavyowezekana, ikiwezekana, jitenge nao ili ujifunze kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi yako binafsi bila kuathiriwa nao. Unapaswa kupunguza ushirika hata na jamaa zako wanaokuingiza katika hali ya kutamauka. Punguza muda wa kukaa nao hasa wanapogeukia mkondo huu wa kukukatiza tamaa.
                Mazingira hasi ni kizingiti kingine. Pengine huoni ukuruba baina ya maisha yako na mazingira unamokulia au unamokaa. Ukweli ni kwamba, huenda umedumu katika mazingira hayo na kuyaozoea hata ukafikiri huwezi kuyabadilisha. Kadri unavyohisi huna uwezo wa kuyabadilisha ndivyo unajizamisha zaidi katika mtazamo hasi. Ili kukabiliana na hali hii, unahitaji kuelewa kwamba fikra zako au za watangulizi wako ndizo zilikuingiza katika mazingira haya. Kwa hivyo, unapaswa kubadili mkondo wa fikra zako na kuanza kujaribu mazoezi ambayo umekuwa ukiyaona kama usiyoyaweza. Hatua kwa hatua utagundua panapo jitihada na uelekezi unaofaa kwamba mazoezi hayo yamekuwa mepesi na hivyo kukubakishia kuyabadilisha mazingira yako.
                Unapojikuta ukilalamika jinsi ulivyokerwa na hali fulani, hii ndiyo sababu ya kuwa na mtazamo hasi kuhusu hali hizo. Inaweza kukuwia vigumu kulikubali hili lakini kadiri utakavyolikubali mapema ndivyo utayaboresha maisha yako mapema. Kulalamika tu kutakudunisha katika hali zisizokuridhisha. Kwa hivyo ili uyabadilishe maisha yako, sharti ukome kulalamika tu kuanza kujikwamua toka kwenye hali hizo. Katika kufanikisha jambo lolote jema sharti viwepo vizingiti njiani. Mtendaji wa jambo lolote jema liwalo ana jukumu la kuibuka na mikakati mwafaka ya kuvikabili vizingiti hivi ili afanikishe ndoto yake. Hii huwa chanya. Kwa jinsi hii utayabadilisha maisha yako yawe ya kuridhisha zaidi na kuwa kielelezo kwa wengi waliotamaushwa na mitazamo hasi.

Maswali

  1. Fupisha aya ya kwanza na ya pili kwa maneno 60. (utiririko 1) (alama 5)
  2. Eleza namna ya kukabiliana na mitazamo hasi kwa maneno 80. (utiririko 1) (alama 8)

MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)

  1. Andika sauti zenye sifa zifuatazo: (alama 1)
    1.  irabu ya juu, viringe
    2. king’ong’o cha kaakaa gumu
  2.  
    1. Eleza maana ya sauti mwambatano. (alama 1)
    2. Andika sauti mwambatano zinayotamkwa katika midomo. (alama 1)
  3. Andika neno lenye mofimu zifuatazo: kikanushi cha nafsi ya kwanza umoja, kikanushi cha wakati uliopita, yambwa, mzizi, kauli tendea, kauli tenda.
  4. Onyesha aina za nomino katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
    Uadilifu wa wanafunzi hao uliwapendeza wakurugenzi wa Shule ya Tumaini.
  5. Tumia kielezi cha idadi kamili badala ya kile kilichopigwa mstari. (alama 1)
    Wazalendo huimba mara kwa mara.
  6. Andika katika wingi (alama 2)
    Mwanafunzi huyu alinunua uzi ambao nitautumia kushona.
  7. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo (alama 3)
    Ijapokuwa Sikitu aliwahonga Wanatomoko, alishindwa katika uchaguzi uliofanyika juzi.
  8. Eleza matumizi ya viambishi vilivyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo. (alama 3)
    Huyu ndiye mkimbiaji aliyekusifu uwanjani.
  9. Tumia kitenzi ‘la’ kama nomino katika sentensi. (alama 1)
  10. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mstari. (alama 3)
    Unga uliomwagika sakafuni umefagiliwa na Jerotich.
  11. Tofautisha maana: (alama 2)
    1. Ningepiga kura ningekuchagua.
    2. Ningalipiga kura ningalikuchagua.
  12. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya futa na vuta. (alama 2)
  13. Tunga sentensi mbili kubainisha maana mbili za neno: koo (alama 2)
  14. Andika katika msemo wa taarifa
    “Nitaenda mahakamani kesho kukushtaki kwa kuniibia ng’ombe wangu,” Yama alimwambia Birirei. (alama 3)
  15. Tunga sentensi kuonyesha matumizi ya vitenzi katika jinsi iliyo mabanoni. (alama 2)
    1. toa (kutendesha)
    2. cha (kutendeka)
  16. Huku ukitoa mifano mwafaka, eleza miundo ya majina katika ngeli ya Li-Ya. (alama 2)
  17. Kanusha (alama 1)
    Kucheza kwake kulimkasirisha Kapaloti.
  18. Sahihisha sentensi ifuatayo (alama 1)
    Furaha zao zilibainika walipokiona kiziwi akituzwa.
  19. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya udogo (alama 2)
    Miguu yake ilimuuma alipokuwa akibeba mlango huo.
  20. Unganisha sentensi zifuatazo ili kuunda sentensi changamano (alama 1)
    1. Mwangeka alifiwa na mkewe.
    2. Mwangeka alimuuoa Apondi.
  21. Andika sentensi ifuatayo kama ulivyoshauriwa. (alama 1)
    Mwanafunzi ambaye hana kitabu hataweza kusoma.
    Anza kwa: Kusoma…
  22. Bainisha silabi zinazowekwa shadda katika maneno yafuatayo (alama 1)
    1. angalia
    2. mwananchi
  23. Bainisha kiima na yambwa katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
    Huyu mzee alimnunulia Karori zawadi nyingi.

ISIMU-JAMII (ALAMA 10)

  1. Fafanua jinsi kanuni zifuatazo zinavyoathiri matumizi ya lugha katika jamii. (alama 4)
    1. Hali
    2. Uhusiano
    3. Lugha azijuazo mtu
    4. Jinsia
  2. Ukiwa shuleni ulipata nafasi ya kumsikiliza mtaalamu wa masuala ya vijana kuhusu maadili ya jamii.Ni mambo gani ambayo ungezingatia ili kuupata ujumbe wake barabara? (alama 6)

Mwongozo Wa Kusahihisha

  1. Ufahamu
    Maswali
    1. Linganua hisia za marafiki za msimulizi walipokuwa njiani. (Alama 2)
      • Pam alimchangamkia msimulizi.
      • Tim alijitia tabasamu bandia. (2×1)
    2. Meneja wa Hatubagui Publishers ni mtu mbaraza. Toa ushahidi kifunguni. (Alama 3)
      • Alikuwa hana ubaguzi
      • Aliwapokea kwa mawili-matatu hata kabla ya kuwajua.
      • Hakuweka vikwazo vya kumuona.
      • Alisisimka msimulizi alipojitambulisha. (3×1)
    3. Kifungu hiki kinaonyesha hali kadha za kutamausha. Thibitisha. (Alama 3)
      • Babake msimulizi alikuwa mgonjwa.
      • Kifurushi cha Mzee Sululu hakikumfikiakilipotumwa kwa posta.
      • Mzee Sululu kusubiri zaidi ya miaka kumi mswada wake kuchapishwa.
      • Wafanyikazi wa posta kuzidokoa mali za watu na kuzichelewesha barua.
        (3×1)
    4. Kwa kumrejelea Mzee Sululu, tetea kauli “…nia ni nguzo muhimu…humkokota mtu ikamfikisha…” (Alama 2)
      • Alifanikiwa kuchapisha kitabu.
      • Alijiendeleza kimasomo mwenyewe na kuhitimu. (2×1)
    5. Tambua mbinu zozote tatu za lugha zilizotumika kifunguni. (Alama 3)
      • Tashbihi - kunizungumzia kama kurumbiza
      • Msemo - alibeba mazito moyoni/ alitupokea kwa mawili matatu/ hayawi hayawi huwa
      • Jazanda - paka waliowekwa kulinda kitoweo
      • Tanakuzi - mabaya na mazuri
      • Uhaishaji - nia humkokota mtu ikamfikisha kusikotarajiwa
    6. Fafanua maana ya vifungu hivi kama vilivyotumika kwenye masimulizi. (Alama 2)
      • Haikosi alibeba mazito moyoni - Alikuwa na mambo fiche moyoni
      • Ni paka waliowekwa kulinda kitoweo - Ni watu waliovinyakua vitu walivyofaa kuvilinda
  2. Ufupisho
    1. Fupisha aya ya kwanza na ya pili kwa maneno 60. (alama 6)
      • Mtazamo hasi ni kukata tama / kutamauka kuhusu hali, mtu au jambo fulani.
      • Ni hisia ya kutotaka kushiriki wala kuhusishwa na jambo au hali fulani.
      • Huwafanya wanafunzi wengi kuchukia / kudunisha baadhi ya masomo na walimu wanaoyafundisha.
      • Wengi hawatambui / wanaotambua hutatizika kujikwamua kutoka katika hali hii.
      • Mtu wa wastani huwa na mawazo elfu sitini ya kibinafsi kwa saa 24. Asilimia 80 ya fikra hizi huwa hasi.
      • Fikra hizi hutokea bila mtu mwenyewe kutambaua na huwa ni mazoea / watu wengi hawana ufahamu wa athari za fikra hizi maishani mwao.
    2. Eleza namna ya kukabiliana na mitazamo hasi kwa maneno 80. (alama 9)
      • Kila mtu sharti abadili imani yake/ aamini kuwa mabadiliko yanaweza kutokea na achukue hataua za kuanzisha mabadiliko maishani mwake.
      • Aepuke fikra hasi zinazoambatana na maisha yake ya awali na kulithamini kila tukio maishani kama tukio huru (lisilo na uhusiano na yaliyowahi kukutamausha)
      • Kuibuka na idadi kubwa ya imani chanya kuliko zilizo hasi kuhusu hali mahususi.
      • Zikabili imani zako potovu moja baada ya nyingine ukitathmini endapo zina mashiko / shadidia fikra chanya inayokinzana na ile inayokudidimiza.
      • Dhibiti hisia zako / tawala namna unavyohisi na kukabiliana na hali mbalimbali bila kuathiriwa na wandani wako.
      • Epuka wandani wanaokuathiri / jitenge nao ili ujifunze kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi yako kibinafsi.
      • Punguza ushirika hata na jamaa zako wanaokuingiza katika hali ya kutamauka / punguza muda wa kukaa nao.
      • Unapaswa kubadili mkondo wa fikra zako na kuanza kujaribu mazoezi ambayo umekuwa ukiyaona kama usiyoweza / jitihada na uelekezi huyabadilisha mazingira yako.
      • Koma kulalamikia hali yako na kuanza kujikwamua toka kwenye hali hizo.
      • Mtendaji wa jambo lolote jema aibuke na mikakati mwafaka ya kuvikabili vizingiti ili afanikishe ndoto yake.
        (Zozote 8×1=08)
      • UTUZAJI
        KIsp2qa02B
        UTOZAJI
      • Hijai 6× ½h =3h
      • Sarufi 6 × ½ s=3s
      • Ziada – kila 10=1Z
  3. Matumizi ya lugha
    1. Andika sauti zenye sifa zifuatazo: (alama 1)
      1. irabu ya juu, viringe
        • /u/ 1/0
      2. king’ong’o cha kaakaa gumu
        • /ny/ 1/0
    2.  
      1. Eleza maana ya sauti mwambatano. (alama 1)
        • Sauti inayoundwa kwa mfuatano wa konsonanti mbili au zaidi na ambazo hutamkwa kama sauti moja. 1/0
      2. Andika sauti mwambatano zinazotamkwa katika midomo. (alama 1)
        • /mb/, /mp/, /bw/, /pw/, /mw/ 1/0
    3. Andika neno lenye mofimu zifuatazo: kikanushi cha nafsi ya kwanza umoja, kikanushi cha wakati uliopita, yambwa, mzizi, kauli tendea, kauli tenda.
      • Mf. Sikumpigia 1/0
    4. Onyesha aina za nomino katika sentensi ifuatayo: (alama 2)
      Uadilifu wa wanafunzi hao uliwapendeza wakurugenzi wa Shule ya Tumaini.
      • uadilifu – dhahania
      • wanafunzi – kawaida
      • wakurugenzi – kawaida
      • Shule ya Tumaini – pekee ½ x 4 = 2
    5. Tumia kielezi cha idadi kamili badala ya kile kilichopigwa mstari. (alama 1)
      Wazalendo huimba mara kwa mara.
      • mara tatu, mara mbili n.k. 1/0
      • k.m. Wazalendo huimba mara mbili.
    6. Andika katika wingi (alama 2)
      Mwanafunzi huyu alinunua uzi ambao nitautumia kushona.
      • Wanafunzi hawa walinunua nyuzi ambazo tutazitumia kushona. 2/0
    7. Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo (alama 3)
      Ijapokuwa Sikitu aliwahonga Wanatomoko, alishindwa katika uchaguzi uliofanyika juzi.
      • Ijapokuwa Sikitu aliwahonga Wanatomoko – tegemezi
      • alishindwa katika uchaguzi – huru
      • uliofanyika juzi- tegemezi 3x 1 = 3
    8. Eleza matumizi ya viambishi vilivyopigiwa mstari katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
      Huyu ndiye mkimbiaji aliyekusifu uwanjani.
      • ndi – kusisitiza
      • ji – kurejelea mtendaji
      • ku – mtendewa katika nafsi ya pili
      • ni – mahali ½ x 4 = 2
    9. Tumia kitenzi ‘la’ kama nomino katika sentensi. (alama 1)
      • chakula, mlo, kula, mlaji
      • mf. Chakula cha mtoto kimeiva. 1/0
    10. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya mstari. (alama 3)
      Unga uliomwagika sakafuni umefagiliwa na Jerotich.
      • S – KN(N +S)+ KT(T+H+N)
    11. Tofautisha maana: (alama 2)
      1. Ningepiga kura ningekuchagua.
        • Kuna uwezekano 1/0
      2. Ningalipiga kura ningalikuchagua.
        • Hakuna uwezekano 1/0
    12. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya futa na vuta. (alama 2)
      • Futa: toa kilichowekwa ndani ya kingine
      • Susia ama gomea kitu
      • Tumia vibaya miliki
      • Ondoa maji katika chombo
      • Kitu kizito
      • Filisi
      • Vuta: buruta kitu kwa nguvu
      • Shawishi
      • Kupeleka kitu kutoka taifa moja hadi jingine
        (mwanafunzi atunge sentensi moja kutofautisha maneno hayo) 2/0
    13. Tunga sentensi mbili kubainisha maana mbili za neno: koo (alama 2)
      • Koo: njia ya chakula shingoni
      • Ugonjwa unaoshika na kuathiri umio
      • Kuku, mbuzi, ng’ombe n.k. jike
        (Mwanafunzi atunge sentensi mbili zitakazobainisha maana mbili za neno koo.) 2 x 1 = 2)
    14. Andika katika msemo wa taarifa
      “Nitaenda mahakamani kesho kukushtaki kwa kuniibia ng’ombe wangu,” Yama alimwambia Birirei. (alama 3)
      • Yama alimwambia Birirei kuwa angeenda mahakamani siku iliyofuata kumshtaki kwa kumwibia ng’ombe wake. ½ x 6 = 3
    15. Tunga sentensi kuonyesha matumizi ya vitenzi katika jinsi iliyo mabanoni. (alama 2)
      1. toa (kutendesha)
        • Toza (atunge sentensi) 1/0
      2. cha (kutendeka)
        • chika - (atunge sentensi) 1/0
    16. Huku ukitoa mifano mwafaka, eleza miundo ya majina katika ngeli ya Li-Ya. (alama 2)
      • JI – MA: jitu – majitu
      • O – MA: dereva – madereva 2 x 1 = 2
    17. Kanusha (alama 1)
      Kucheza kwake kulimkasirisha Kapaloti.
      • Kutocheza kwake hakukumkasirisha Kapaloti. 1/0
    18. Sahihisha sentensi ifuatayo (alama 1)
      Furaha zao zilibainika walipokiona kiziwi akituzwa.
      • Furaha yao ilibainika alipomwona kiziwi akituzwa. 1/0
    19. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya udogo (alama 2)
      Miguu yake ilimuuma alipokuwa akibeba mlango huo.
      • Vijiguu vyake vilikiuma kilipokuwa kikibeba kilango hicho. 1/0
    20. Unganisha sentensi zifuatazo ili kuunda sentensi changamano (alama 1)
      1. Mwangeka alifiwa na mkewe.
      2. Mwangeka alimuuoa Apondi.
        • Mwangeka aliyefiwa na mkewe alimuuoa Apondi. 1/0
    21. Andika sentensi ifuatayo kama ulivyoshauriwa. (alama 1)
      Mwanafunzi ambaye hana kitabu hataweza kusoma.
      Anza kwa: Kusoma…
      • Kusoma hakutawezekana kwa mwanafunzi ambaye hana kitabu. 1/0
    22. Bainisha silabi zinazowekwa shadda katika maneno yafuatayo (alama 1)
      1. angalia
        • angalia
      2. mwananchi
        • Mwananchi ½ x 2 = 1
    23. Bainisha kiima na yambwa tendewa katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
      Huyu mzee alimnunulia Karori zawadi nyingi.
      • huyu mzee – kiima
      • yambwa tendewa – Karori 2 x 1 = 2
  4. ISIMUJAMII
    1.  
      1. Hali- Matumizi ya lugha hutegemea hali ya mtu. Kama vile, mtu akiwa mgonjwa, mlevi, mchangamfu, mwenye hasira n.k. Kwa mfano mlevi hutumia lugha legevu na yenye matusi. Mtu mgonjwa hutumia toni ya huruma na upole.
      2. Uhusiano- Lugha hubadilika kutegemea mahusiano ya wazungumzaji.kwa mfano, mtoto hutumia lugha ya heshima anapozungumza na mzazi wake ilhali anapozungumza na rafikize/wanahirimu atatumia lugha ya utani/mzaha.
      3. Lugha azijuazo mtu- Mtu aliye na ujuzi wa zaidi ya lugha moja, ana uwezo wa kuchanganya au hata kuhamisha ndimi anapozungumza.
      4. Jinsia- Lugha hubadilika kutegemea jinsia. Mazungunzo baina ya wanawake yatahusu mambo kama vile mapambo, mavazi,malezi n.k. Mazungumzo kati ya wanaume huenda yakahusu michezo, magari, siasa n.k. Wanawake hutumia msamiati wa heshima na adabu ilhali wanaume hutumia lugha kavu
        (4x1=4)
    2.          
      • Kuuliza maswali kuhusu yasiyoeleweka vyema
      • Kuandika mambo muhimu kwenye daftari.
      • Kusikiliza kwa makini.
      • Kuangaliana na hatibu uso kwa uso anapozungumza ili kupata kila ishara atakayoitumia.
      • Kujibu maswali iwapo atayauliza.
      • Kuketi/kusimama kwa namna itakayoniwezesha kuupata ujumbe bila kusinzia.
      • Kutulia / kuepuka maongezi na wenzangu ambayo yataninyima fursa ya kupata kila kitu kwenye hotuba yake.
        (Hoja 6x1=6)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Mokasa II Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?