Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kijiset Revision Mock Exams 2022

Share via Whatsapp

Maswali

Maagizo

  • Andika jina lako na nambari yako katika nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali.
  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote yaandikwe katika nafasi ulizoachiwa katika kijitabu cha maswali.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

 

  1. UFAHAMU: (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
                 “Asante baba, asante mama,” akasema Bahati jioni moja baada ya chajio, “Sijui ilitokeaje kukawa na watu wanaothamini binadamu wenye mahitaji maalumu katika jamii hii. Sitawauliza mlichofanya kunikinga na hukumu ya ukoo ya kuniangamiza; hayo mtakuja kunihadithia siku moja. Ila nataka mjue kwamba kuishi na ulemavu wa aina yoyote ile kuna dhiki kuu. Niliyokabiliana nayo baada ya uamuzi wenu wa kunipeleka shuleni hayawezi kutoshea hata chapisho la kurasa elfu.Si kudhihakiwa na miale ya jua; ngozi yangu inashindwa kuuhimili ukali wake, si kutengwa na marika, si kulazimika kusoma hati za kawaida hadi pale serikali ilipoanzisha sera ya kuhakikisha kwamba matini zote za kiusomi zimeandikwa pia kwa hati ambazo zinaweza kusomwa na wenye changamoto kama yangu, si kubaguliwa kazini....”Bahati alitua, akawatazama wazazi wake kama anayetaka kuona taathira ya maneno yake kisha akaendalea.
                 “Msinione kama aliyekosa hisani, ila’ nataka niwaambie kwamba hata uamuzi wenu wa kunitafutia mlinzi kuandamana nami hadi shuleni ulinitia kwenye ngome zaidi.Nilijihisi kama niliyedhulumiwa zaidi katika kule kulindwa! Najua mlikuwa mnachelea kwamba ningekuwa windo rahisi kwa walanguzi wa binadamu ambao wanaamini kwamba viungo vyetu sisi ni dawa ya kutibia ndwele mbalimbali.Hata hivyo, katika kipindi chote hicho nilitamani kwamba mngenifunza mbinu za kujilinda mimi binafsi. Amini usiamini hata nilitamani kwamba ningetekwa nyara, nijadiliane na watesi wangu kuliko kupokwa nafasi ya kubuni mikakati ya kujihakikishia usalama”.
                 “Mwanangu Bahati,” alisema mume wangu, “binadamu hawi jagina kwa kuzifuata tamaduni za jamii yake bila kuzichunguza. :haidhuru kwamba ilichukua muda kuyangamua haya'. La muhimu ni kwamba umeweza kuishi kama ndugu zako”.
                 Nilimtazama mume wangu kwa macho yaliyokuwa yamepofushwa na dimbwi la machozi. Moyo uliituma akili yangu kurudi nyuma kule -e-e-e- kwenye miereka ya baada ya kuzaliwa kwa Bahati. Asubuhi hiyo ya kipupwe nilishika ujia ulioelekea kwenye msitu uliokuwa karibu na boma la Mzee Kedi, baba mkwe wangu; mgongoni nimeifungia mbeleko ambayo ilikisitiri kitoto changu. Nilitazama nyuma, nikaiona nyumba ambayo mimi na mume wangu tulikuwa tumechanga bia kuijenga.
                 “Haya yote nayaacha,” nilijiambia, “nayaacha na mengine mengi. Nawaacha mabinti wangu wawili, namwacha mume wangu, naiacha kazi yangu, nayaacha maisha yangu wala sijuti kwa kuyaacha haya yote. Sina cha kujutia kwani imebidi kuondoka. Jamii yangu imenitema; mimi na mwanangu.Haina nafasi ya mwanangu, kwa hivyo nami nimeamua kwamba haina nafasi yangu kwa vile imesema huu ni mzigo wangu. Ikiwa ukoo umeamua kuwa hatima ya mwanangu huyu ni kuwa kitoweo cha fisi, basi na tuwe sote karamu ya fisi” nilitamatisha kauli yangu kisha nikayarudisha nyuma tena mawazo yangu.
                 Nilikumbuka sauti ya muuguzi hospitalini siku ambayo nilijikopoa, “Pongezi Tamasha, Mungu amekutunukia kipusa”. Nilikifunua kitoto changu kilichokuwa kimefunikwa gubigubi, nikakitazama viguu, vikono, uso...kisha, ‘Mungu wangu!’ ikanitoka. “Dadangu, unastahili kumshukuru Mungu,” akasema muuguzi, “wapo wanawake, mimi mwenyewe nikiwemo, ambao hawajawahi kuambulia ujauzito, sikwambii hata kupoteza mimba.Huyu wako ni kiumbe kamili, kasoro yake i kwenye ngozi tu, na hii ni hali ambayo unaweza kukabiliana nayo. Hapa unionapo nimelazimika kumpa mume wangu talaka, mwenyewe alienda kortini akaiomba. Anadai kwamba hatusikilizani. Ila najua kiini cha haya yote ni kutoshika kizazi”.
                 Nilimtazama huyo muuguzi kana kwamba hajasema lolote. Nilimwona kama anayeuona mzigo wangu kuwa kanda la usufi. Huenda huyu muuguzi hakujua kwamba katika jamii yangu watoto wa aina hii ni kama pacha, huaminiwa kuwa nuksi kwa ukoo mzima, kwa hivyo hutupwa. Muuguzi huyu hakujua pia kwamba tayari nilikuwa na watoto wawili wa kike na huo tayari ulikuwa mzigo mkubwa kwangu kwani ilibidi kumhakikishia mavyaa kila mara kwamba hawa pia walikuwa watoto.
                 Moyo ulinipa kukumbuka jitimai iliyojiandika usoni mwa mume wangu asubuhi hiyo alipokuja hospitalini. Alikitazama kitoto chetu kana kwamba anaona mzuka. Alinyamaza kwa muda, akashusha pumzi, kisha akanishika kwenye bega na kuondoka kwenye wodi. Machozi yalivunja kingo zake huko yanakohifadhiwa, nikalia kama mfiwa, Mume wangu alirudi tena baada ya siku mbili; anakuja kunipeleka nyumbani.
                 “Mke wangu, naomba msamaha kwa kutokuja kuwatazama kwa siku mbili. Ilibidi nishauriane na ukoo kuhusu tanzia hii. Inavyoonekana ni kwamba msimamo wa baba na wazee wengine ni ule ule. Wanasema ukoo wa Baulanga haujawahi kupata mtoto wa aina hii, kwamba kumhifadhi mwana huyu kutakuwa kuupaka masizi ukoo. Wahenga hawatakubali tendo hili. Sijui nitakutetea vipi.Nimo kwenye njia panda,” mume wangu alikamilisha uzungumzi wake na kuelekea kwenye afisi ya mhasibu kukamilisha viviga vya kutuondoa hospitalini.
                 “Huna haja ya kuniitetea. Sijafanya kosa lolote. Nililofanya ni kujaliwa kiumbe ambaye anaonekana kuwa punguani kwa misingi ya jamii yako. Nitakilinda kitoto hiki hata kifoni,” nilimwambia mume wangu mawazoni.
    1. “Kufanikiwa kwa watu wenye mahitaji maalumu kunategemea jamii.” Thibitisha kwa kutoa hoja sita kutoka aya tatu za kwanza. (alama 6)
    2. Kwa kurejelea aya ya nne hadi ya saba, onyesha jinsi unyanyasaji wa kijinsia unavyoendelezwa katika jamii hii. (alama 3)
    3. “Msimulizi anahimiza. uwajibikaji.” Thibitisha kwa kutoa hoja nne kutoka aya tatu za ‘ mwisho. (alama 4)
    4.      
      1. Andika kisawe cha, ‘hisani’ kwa mujibu wa taarifa. (alama 1)
      2. Eleza maana ya, ‘kuupaka masizi’ kulingana na taarifa. (alama 1)

  2. UFUPISHO: (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
                 Wakenya walipoipitisha katiba mpya waliidhinisha mfumo wa ugatuzi.Katika mfumo huu, mamlaka ya serikali kuu katika uongozi, usimamizi na utumiaji wa rasilimali za nchi hupunguzwa.Kiasi fulani cha mamlaka hutwaliwa na maeneo ya ugatuzi.Suala hili halikuzingatiwa katika katiba ya awali ambapo mamlaka yote yalikuwa mikononi mwa serikali kuu. Kutokana na upana na wingi wa maeneo nchini, iliiwia vigumu serikali kuu kuhakikisha kwamba kulikuwa na usawa wa kimaendeleo katika sehemu zote nchini.
                 Kwa mujibu wa katiba mpya, serikali kuu haina budi kuyasaidia maeneo yote ya ugatuzi ili yaweze kujinyanyua kiuchumi na kuboresha hali za maisha za wakazi wake.Vilevile ni jukumu la kila eneo la ugatuzi kuweka mikakati madhubuti ili kuchunguza na kubainisha rasilimali zote katika maeneo husika.Hili litasaidia kuvumbua rasilimali ambazo zinaweza kuchangia katika ustawishaji wa maeneo haya.Maeneo haya pia yanatakiwa kutafuta mbinu zitakazofanikisha uzalishaji na utumiaji wa rasilimali hizi kwa njia endelevu.Mojawapo ya mbinu hizi ni uongezaji thamani katika rasilimali yoyote inayozalishwa kwenye eneo mahususi.
                 Maeneo mengi ya ugatuzi nchini humu yanategemea kilimo cha ufugaji kama mhimili wa uchumi.Licha ya kuwa nguzo, kilimo hiki hakijawahi kupigiwa darubini vizuri kwa lengo la kukiimarisha ili kiwanufaishe wenyeji kikamilifu.Aghalabu wafugaji wengi huandama mbinu za jadi za ufugaji ambazo haziwahakikishii ongezeko la mapato.Isitoshe, wafugaji hawa wanakabiliwa na tatizo katika soko la mifugo ambapo wengi hupunjwa na matapeli.Pamoja na haya, baadhi ya wakazi huuza mifugo nje ya nchi wakiwa wazimawazima bila kuwazia matokeo ya kitendo hiki.Si ajabu kuwaona ng'ombe , ngamia, mbuzi na kondoo wakipakiwa kwenye malori na kusafirishwa nje ya nchi.Ukweli ni kwamba jambo hili ni hatari sana, si kwa uchumi wa maeneo husika tu, bali pia kwa Kenya kwa jumla.Hii ni kwa kuwa walionunua mifugo wazimawazima wanaweza kuhiari kutowachinja na badala yake kuwatumia kama mbegu za kuzalisha mifugo wao.Hapa pana hatari ya maeneo haya kupoteza wateja kwani baada ya muda huenda wanaonunua mifugo wakajitosheleza na kukosa kuja kununua mifugo wengine.Hali ikiwa hivyo, maeneo yaliyotegemea soko hili huenda yakalipoteza taratibu, na bila shaka kupoteza natija inayotokana na soko lenyewe.
                 Ili kudhibiti hali hii, itakuwa bora ikiwa viwanda vya kuchinjia mifugo na kupakia nyama vitajengwa katika maeneo haya ya ugatuzi.Hili litawawezesha wakazi kuuza nyama badala ya kuuza mifugo wazimawazima.Fauka ya haya, maeneo haya yatajikinga dhidi ya kupoteza bidhaa zinazotokana na mifugo.Hizi ni kama vile ngozi, kwato na pembe ambazo bila shaka zina natija kuu.Ngozi kwa mfano, ni bidhaa muhimu sana katika sekta ya utengenezaji wa mavazi na mifuko.Viwanda vinavyotumia ngozi kama malighafi vikijengwa katika maeneo haya, wakazi wake watanufaika si haba.Mathalani, viwanda vya kutengenezea viatu, mishipi, mifuko na nguo vikianzishwa, wawekezaji watalazimika kuanzisha viwanda vingine vitegemezi.Kadhalika, ni dhahiri kwamba bidhaa zinazotokana na ngozi huhitaji kutiwa nakshi.Kuanzishwa kwa viwanda hivi basi kutazua haja ya kuanzishwa kwa viwanda vya kutengenezea rangi, pamoja na maduka ya kuuza bidhaa yenyewe.Isitoshe, gundi ya kugandisha bidhaa hizi itahitajika, hivyo kusababisha haja ya kuanzishwa kwa kiwanda cha gundi.Matokeo ya shughuli hizi zote ni kuzalishwa kwa nafasi anuwai za kazi kwa wakazi.Hili litakuwa na matokeo zaidi chanya, hususan kwa vijana.Badala ya kushiriki ulevi na burudani zinazowahatarisha, wataweza kujitafutia riziki katika viwanda hivi.
                 Juu ya hayo, mfumo wa ugatuzi utayawezesha maeneo husika kuongezea thamani utoaji wa huduma za kijamii na kiutawala kulingana na mahitaji ya maeneo haya.Ni muhimu hata hivyo kuzingatia kwamba kila eneo la ugatuzi una upekee wake,navyo vipaumbele hutofautiana kulingana na maeneo.Kuna yale ambayo yatasisitiza usalama, mengine ujenzi na uimarishaji wa miundomsingi kama vile barabara, vituo vya afya na hata taasisi za elimu.La muhimu ni wakazi wa maeneo husika kubainisha ni lipi litatekelezwa kwanza.
                 Kinga na kinga ndipo moto uwakapo.Kufanikiwa kwa mfumo wa ugatuzi kutategemea juhudi za kila mkazi wa eneo husika.Ni muhimu kila mkazi kujiona kuwa mmiliki wa eneo zima la ugatuzi na kuwajibika katika kuliendeleza kwa hali na mali.Uwajibikaji huu unajumuisha uteuzi wa viongozi wenye muono mzuri na ambao watawawezesha kuyafikia malengo yao ya kimaendeleo.aHakika, mustakabali na uwepo wa eneo la ugatuzi utakuwa zao la maamuzi ya wanaeneo.Vilevile ufanisi wa maeneo ya ugatuzi utakuwa msingi wa ufanisi wa taifa kwa jumla.
    1. Fupisha ujumbe wa aya tatu za mwanzo kwa maneno 85-90.(alama 8, 1 ya mtiririko)
      Matayarisho:
      Nakala safi.
    2. Kwa kutumia maneno 75-80, bainisha masuala ambayo mwandishi anaibua katika aya tatu za mwisho. (alama 7, 1 ya mtirin'ko)
      Matayarisho.
      Nakala safi.
  3. SARUFI
    1. Tunga neno lenye muundo ufuatao wa sauti
      1.    
        1. Kipasuo ghuna cha mdomo
        2. Irabu ya chini kati
        3. Kipasuo ghuna cha ufizi
        4. Irabu ya juu mbele (al .1 )
      2. Andika neno lenye muundo ufuatao wa silabi.
        K + KI + KKI
    2. Geuza kitenzi kilicho kwenye mabano kiwe katika hali ya kufanyana.
      1. Yohana na Jaheria (pokea) vijiti katika mazoezi ya mbio za mita mia moja. (al. 1 )
      2. Nguruwe (tafuna) walipohisi njaa. (al. 1 )
    3. Andika sentensi zifuatazo katika hali ya mazoea.
      1. Wanadrama wanaigiza mchezo wao. (Al. 1 )
      2. Wadudu wanapaa hewani. (Al. 1 )
    4. Andika sentensi moja moja kuonyesha matumizi ya alama zifuatazo za kuakifisha.
      1. Ritifaa (Al. 1 )
      2. Nukta mbili (Al. 1 )
    5. Andika katika msemo wa taarifa.
      Amina: Utangoja mimi nimalize au utaendelea kunipigia kelele?
      Makasi: Mradi uko kwangu utanyamaza. (Al. 3 )
    6. Andika na kueleza kila aina za nomino zilizotumika katika sentensi ifuatayo.
      Majura aliitwa kufika katika ofisi ya mwalimu mkuu kwa sababu ya ukora wake. (Al. 2 )
    7. Tunga sentensi moja moja kueleza vielezi vifuatavyo.
      1. Vya wakati (Al. 1 )
      2. Vya namna vikariri (Al. 1 )
    8. Andika na kubainisha viwakilishi mbalimbali katika sentensi hii.
      Mimi nilimpa yuyu huyu kitabu changu . (Al. 2 )
    9. Eleza tofauti ya maana kati ya sentensi zifuatazo.
      1. Mtoto amelia. (Al. 1 )
      2. Mtoto amelialia. (Al. 1 )
    10. Andika sentensi ifuatayo katika ukubwa wingi. (Al. 2 )
      Kiguo kilichovaliwa kilikibana kijiuno.
    11. Viambishi ngeli PA- KU - MU hutumiwa kuonyesha mahali patatu tofauti . Thibitisha. (Al. 3 )
    12. Andika sentensi ifuatayo katika kinyume.
      Mfalme alipanda mlimani polepole. (Al. 2 )
    13. Tunga sentensi zozote mbili kuonyesha maana tofauti za neno karibu. (Al. 2 )
    14. Tambulisha virai katika sentensi hii. (Al. 2 )
      Waliosomba changarawe wamelipwa.
    15. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao.
      KN (N + V + V ) + KT ( T + E )
    16. Changanua sentensi ifuatayo kwa njia ya jedwali .
      Ajabu! Nyumba zile nzuri zimebomolewa zote. (Al. 4 )
    17. Andika methali tatu tofauti zinazoafiki maneno haya.
      Usidharau mtu ambaye amekusaidia katika jambo huenda ukamhitaji baadaye. (Al. 3 )
  4. ISIMU JAMII (ALAMA 10)
    Bwana spika, ningependa wizara ya usafiri na miundo mbinu ieleze kwa nini ajali za barabarani zinazohusisha usafiri was imma zimeongezeka, na ni hatua gani zimechukuliwa kusitisha ajali huku ikijulikana kuwa kampuni fulani za usafiri zinavunja sheria maksuudi?Juma lililopita watu hamsini ( 50 ) walifariki katika ajali la basi lililokuwa limepata aboria 80 badala ya idadi rasmi ya 62. Ajabu ni kuwa gari hili lilikuwa limepita vizuizi kadhaa vya polisi.
    1. Bainisha muktadha wa dondoo hili. (Al. 2 )
    2. Fafanua sifa nane zinazotambulisha sajili hii. (Al. 8 )

Mwongozo Wa Kusahihisha

  1.  
    1. Bahati anapelekwa shuleni
      • Bahati anadhihakiwa na miale ya jua.
      • Bahati ana mlinzi.
      • Bahati na wengine kama yeye kusoma hati za kawaida.
      • Bahati anabaguliwa kazini.
      • Serikali kuhakikisha matini zimeandikwa kwa hati inayoweza kusomwa na walemavu.
      • Wazazi hawamfunzi Bahati mbinu za kujikinga.
      • Walanguzi kuhatarisha maisha ya watoto walemavu.
      • Ukoo kuamua kuangamiza watoto walemavu.
      • Bahati kudhihakiwa na marika.
      • Mama kuamua kumhifadhi Bahati.
    2. Kuamua kuondoka nyumbani na kuacha mali yake na mumewe.
      • Kuwa mzigo Kwa kuzaa punguani (zezeru).
      • Kulazimika kuacha nyumba aliyochangia kuijenga.
      • Laumiwa kwa kukosa mimba/mtoto.
      • Kutalikiwa
      • Kupelekwa kortini.
      • Kumsingizia muuguzi kuwa hawaelewani na mumewe.
    3. Mume kuenda kumuona mkewe hospitalini.
      • Mume kumshika mkewe begani.
      • Mume kuondoka hospitalini bila neno.
      • Mume kurudi hospitalini mara ya pili.
      • Mume kuomba mkewe msamaha.
      • Mume kutokuja hospitalini siku mbili.
      • Mume kushauriana na ukoo.
      • Ukoo kuamua kuangamiza mtoto mlemavu.
      • Mume kumjuza mkewe uamuzi wa ukoo.
      • Mume kulipa gharama ya hospitalini.
      • Make kuamua kumhifadhi mtoto wake.
      • Msimulizi anakashifu mtazamo wa jamii kuhusu watoto walemavu.
    4.    
      • Hisani - fadhila,wema ,shukrani, tajamela, jamala
      •  Paka masizi - haribu sifa , aibisha , fedhehesha , chafua , tia Soni
  2. Ufupisho
    1.  
      • Katiba mpya iliidhinisha mfumo wa ugatuzi ambao hupunguza mamlaka ya serikali kuu katika usimamizi wa rasilimali.
      • Eneo la ugatuzi hutwaa kiasi fulani cha mamlaka .
      • Ugatuzi utahakakikisha usawa wa kimaendeleo nchini kinyume na awali.
      • Serikali isaidie maeneo yote kujiimarisha.
      • Maeneo yaweke mikakati ya kutafiti na kubainisha rasilimali zilizomo.
      • Kuvumbua rasilimali mwafaka kutasaidia ustawi.
      • Wanamaeneo watafute mbinu za kuongezea thamani rasilimali.
      • Kilimo cha ufugaji ni nguzo ya maeneo mengi na kinahitaji kuimarishwa kwa kuandama mbinu za kisasa za uzalishaji.
      • Ipo haja ya wanaeneo kukabiliana na matatizo yanayohusiana na soko ili kukinga dhidi ya kupoteza wateja.
      • Ipo haja ya kujenga viwanda vya kuchinjia mifugo na kupakia nyama.
      • Baadhi ya wafugaji huhasirika kwa kuuza mifugo wazimawazima.
      • Wafugaji wengine hutapeliwa.
    2.  
      • Ujenzi wa viwanda vya kuchinjia na kupakia nyama utakinga dhidi ya kupoteza bidhaa zinazotokana na mifugo.
      • Kujenga viwanda hivi kunasababisha ujenzi wa viwanda tegemezi.
      • Hili litawezesha kuzalisha nafasi za kazi.
      • Kutakuwa na kuongezea thamani utoaji wa huduma za kijamii na kiutawala.
      • Kuzalisha nafasi za kazi kwa vijana kutasaidia kuwaadilisha vijana zaidi.
      • Kila eneo lina vipaumbele tofauti ;wakazi wabainishe kipaumbele chao.
      • Ugatuzi unahitaji ushirikiano. Kila mwanaeneo awajibikie maendeleo ya eneo.
      • Wanaeneo washiriki kuteua viongozi wenye muono mzuri.
      • Ufanisi katika maeneo ya ugatuzi utachangia katika ufanisi wa taifa kwa jumla.
  3. matumizi ya lugha
    1.       
      1. Bati
      2. Mlango, mkunga , mpenzi , mpango
        Kadhiria majibu ya mwanafunzi.
    2.  
      1. Yohana na Jaheria wanapokezana vijiti katika mazoezi ya mbio za mita mia moja.
      2. Nguruwe walitafunana walipohisi njaa.
    3.  
      1. Wanadarama huigiza mchezo wao.
      2. Wadudu hupaa hewani.
    4.  
      1. Mama amenunua ng'ombe.
      2. Amemletea vitu vifuatavyo: vitabu, kalamu na mkate.
        Kadhiria sentensi ya mwanafunzi.
    5. Amina alitaka kujua iwapo/kwamba/kuwa Makasi a✓nge✓m✓ngoja a✓malize au a✓nge✓endelea kum✓pigia kelele.✓ Naye Makasi akamjibu kuwa✓ mradi yuko✓ kwake✓ a✓nge✓nyamaza. ¼×12 (Al. 3)
    6.  
      • Majura - nomino ya pekee
      • Ofisi - ya kawaida
      • Mwalimu mkuu - ya kawaida
      • Ukora - dhahania
        (½×4) (Al. 2)
    7.   
      • Walienda shuleni Jumamosi/jana/juzi.
      • Walitembea pole pole.
    8.  
      • Mimi- kiwakilishi nafsi huru
      • Yuyu huyu - kiwakilishi kiashiria kisisitizi
        -nilimpa - nafsi tegemezi
        Changu - kimilikishi
        (½×4)
    9.   
      1. Kauli ya kutenda
      2. Kauli ya kutendatenda au kufanyafanya.
    10. Maguo yaliyoyavaliwa yaliyabana majiuno.
    11. Kiambishi PA- mahali panapodhihirika.
      Mfano, kwake ni hapa Malakisi.
      Kiambishi KU-mahali kusikodhihirika.
      Mfano, ameenda kule.
      Kiambishi MU- mahali ndani ya - mnamodhihirika
      Mfano, ameingia mle ndani.
      (3×1)
    12. Mfalme aliteremka/shuka mlimani.
    13. Nyumba yao ipo karibu na mto (ujirani ).
      Nilipobisha mlango, nyanya aliitikia karibu ( neno la kumwitikia anayebisha mlangoni).
      "Kwaheri!" Mama alimuaga mgeni kwa kusema , "Asante Kwa kututembelea, karibu tena!" (Kukaribishwa tena).
    14. Waliosomba changarawe - kirai nomino
      wamelipwa - kirai kitenzi/ tenzi
      (2×1)
    15. Mwanafunzi yule mrefu ameenda shuleni.
      Kadiria.
      Al.(2×1 )
    16.    
            S
          KN KT  
       I
       Ajabu! Nyumba  zile  nzuri  zimebomolewa  zote 
       
    17. Usitukane mkunga na uzazi ungalipo.
      Usitupe jongoo na mti wake.
    18. Jinsi ya kusahihisha matumizi ya lugha.
      • Ondoanusu( ½kwakilakosa la sarufi (s) litokeapokwamaraya kwanza kwakilakijesehemulakiniisipitenusuyaalamaalizopatakatikakijisehemuhicho.
      • Ondoanusualama( ½ ) kwakilakosa la tahajia (h) litokeapomaraya kwanza hadimakosasitakatikaswaliloateyaani ( 6 x ½ = 03)
  4. ISIMU JAMII
    1. Sajili ya bungeni (Al. 2)
    2.    
      • Sentensi fupi fupi .
      • Sentensi ndefu ndefu.
      • Lugha ya majibizano/ kudadisi / maswali na majibu.
      • Kunakili vifungu vya sheria.
      • Lugha ya tarakimu .
      • Matumizi ya msamiati maalum wa bungeni. Mfano, bwana spika, mbunge , waziri, sheria.
      • Lugha ya utohozi. Mfano, spika.
      • Matumizi ya misimu kama UDA, CDF , ODM?
      • Lugha ya adabu .Mfano, bwana spika.
        (Zozote nane, alama nane)
        Makosa
        S - 4×½
        h - 4×½
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kijiset Revision Mock Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?