Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Bondo Joint Mocks Exams 2022

Share via Whatsapp

Maswali

Maagizo

  • Andika jina lako, nambari ya usajili, mkondo, sahihi na tarehe katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
  • Jibu maswali manne pekee.
  • Swali la kwanza ni la lazima.
  • Maswali hayo mengine matatu yachaguliwe kutoka sehemu nne zilizobaki Riwaya, Tamthilia, Hadithi Fupi na Ushairi.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Maswali yote ni sharti yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: FASIHI SIMULIZI

  1. Lazima
    Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali
    Heri ujue mapema
    Nasaba yetu haina woga
    Woga haumei kwetu, humea kwa kina mamako.
    Tulichinja jogoo na fahali ili uwe mwanaume.

    Ah! Kisu cha ngariba ni kikali ajabu.
    Iwapo utatikisa kichwacho.
    Uhamie kwa wasiotahiri,
    Ama tukwite njeku.

    Mpwangu kumbuka hili,
    Wanaume wa mlango wetu
    Si waoga wa kisu
    Wao hukatwa mchana hadi usiku
    Wala hawalalamiki.

    Siku nilipokatwa
    Nilisimama tisti
    Nikacheka ngariba kwa tashtiti
    Halikunitoka chozi.

    Iwapo utapepesa kope
    Wasichana wa kwetu na wa mbali
    Wote watakucheka
    Ubaki ukinuna.

    Sembe umepokea
    Na supu ya makongoro ukabugia
    Sema unachotaka
    Usije kunitia aibu

    Maswali;
    1. Huu ni wimbo wa aina gani? Thibitisha (alama 2)
    2. Taja na uthibitishe shughuli zozote za kiuchumi za jamii ya wimbo huu (alama 4)
    3. Thibitisha nafsineni na nafsinenewa katika utungo huu. (alama 2)
    4. Mwimbaji wa wimbo huu ana taasubi ya kiume. Thibitisha kauli hii. (alama 2)
    5. Umepewa wajibu wa kutafiti michezo ya watoto katika jamii yako. Pendekeza mbinu ambazo jamii yako inaweza kutumia kuendeleza kipera hiki. (alama 6)
    6. Fafanua mbinu nne ambazo fanani anaweza kutumia kufanikisha uwasilishaji wa soga. (alama 4)

SEHEMU B: RIWAYA
Assumpta K. Matei: Chozi la Heri
Jibu swali la 2 au la 3

  1. Jadili mchango wa vijana katika hali ya maisha ya Wahafidhina wenzao ukirejelea riwaya Chozi la Heri. (alama 20)
  2. ‘Jahazi letu liligonga mwamba asubuhi moja nilipoamka na kupata kibarua juu ya meza ndogo iliyokuwa chumbani mwangu. Kibarua hicho kilikuwa kimehifadhiwa ndani ya bahasha ndogo nyeupe yenye picha ya moyo. Nilifungua barua kwa viganja vilivyokuwa vinatetemeka na kuyafikicha macho yangu ili kuona aliyekuwa ameiandika. Hata hivyo macho yalikataa kuona wakati huo. Woga huweza kumtia mtu upofu wa muda! Hatimaye moyo wa shauku uliyashurutisha macho kukisoma kile ambacho kilisomeka kama ujumbe wa mauti.’
    1. Changanua mbinu za kimtindo katika dondoo hili (alama 6)
    2. Fafanua umuhimu wa msemaji katika riwaya. (alama 4)
    3. Tathmini namna jahazi la wahusika mbalimbali lilivyogonga mwamba ukirejelea riwaya Chozi la Heri. (alama 10)

SEHEMU C: TAMTHILIA
Pauline Kea: Kigogo
Jibu swali la 4 au 5

  1.  “Si ni huku kugaragara kwako kama kuku anayetaka kutaga. Hiyo rununu haitulii mfukoni. Yakuuma?”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Fafanua vipengele vitatu vya kimtindo kwa mifano kutoka dondoo. (alama 6)
    3.  Thibitisha kuwa mhini na mhiniwa njia yao moja kulingana na tamthilia ya Kigogo. (alama 10)
  2.  
    1. Eleza dhima ya mandhari ya soko la Chapakazi katika ujenzi wa tamthilia. (alama 8)
    2. Jadili jinsi wahusika wanavyokuza maudhui katika tamthilia ya Kigogo. (alama 12)

SEHEMU D: HADITHI FUPI

A. Chokocho na D. Kayanda (Wah): Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine

Jibu swali la 6 au la 7
Euice Kimaliro: Mtihani wa Maisha

  1.  “Mahambe hawa kama mwalimu wao mkuu. Wadaku na wambea hawa. Chakumbimbi wenye tabia za kumbi kumbi. Kwa nini wananibughudhi hivi hawa?”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Taja vipengele vitatu vya kimtindo. (alama 3)
    3. Ni kwa vipi mzungumzaji anamchukulia mwalimu mkuu kama hambe. (alama 3)
    4. Taja na ufafanue sifa tatu za msemaji. (alama 3)
    5.  Eleza jinsi maisha ya msemaji yanavyoafiki anwani ya hadithi. (alama 7)
  2. ‘Pale nilipokwenda kulelewa, palikuwa jehanamu kwangu. Mara moja nikafahamu kwamba nilikuwa mtumwa wa nyumba hiyo.’
    1. Weka dondoo katika muktadha wake. (alama 4)
    2. Tambua mbinu za kimtindo zilizotumiwa. (alama 2)
    3. Kwa kurejelea matukio matatu ya mbinu rejeshi, jadili dhima yao katika hadithi Tulipokutana Tena. (alama 6)
    4. Eleza jinsi pale alipoishi msemaji palikuwa jehanamu kwake kwa kurejelea hadithi Tulipokutana Tena. (alama 8)

SEHEMU E: USHAIRI

  1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

    FUJO TUMBONI
    Siku moja, miongoni mwa wengi
    Virago vyetu migongoni
    Tulianza safari
    Kuhama janga la jangwa
    Kutafuta bonde la rutuba
    Na mvua nzitonzito
    Kulima kwa nyoyo imara
    Kuzima moto tumboni.

    Miaka imepita
    Na kupita
    Bali, tuzo kutoka ardhi
    Kwa wale ambao
    Wamekauka kama kuni
    Kutokana na nyimbo
    Za kuishi ardhi
    Ni moto tele tumboni

    Lo! Maisha haya!
    Ukweli mchungu!
    Hii ng`ambo tunayolimia
    Kwa kalamko zamisuli
    Siyo tuliyoona
    Kwa macho ya ndoto
    Tulipoanza safari
    Aka! Maisha haya!
    Maisha yanadondoka njama!
    Njama za malaika wa machozi
    Za kuiba matunda ya udongo
    Baada ya wakulima
    Kugofuka kama mahame
    Kutokana na makofi
    Ya jua
    Na mateke
    Ya njaa.

    MASWALI
    1. Eleza ujumbe wa shairi hili. (alama 4)
    2. Eleza maana ya kitamathali na kijuujuu ya mstari ‘Kuzima moto tumboni.’ (alama 2)
    3. Bainisha matumizi ya vipengele viuatavyo katika shairi.
      1. Mishororo mshata (alama 2)
      2. Usimulizi (alama 2)
    4. Thibitisha kuwa hili ni shairi huru. (alama 4)
    5. Eleza dhima ya aina mbili za urudiaji katika shairi hili. (alama 4)
    6. Eleza toni ya shairi hili. (alama 2)

Mwongozo wa Kusahihisha

  1.      
    1. Huu ni wimbo wa aina gani? Thibitisha (alama 2)
      • Wimbo wa tohara / nyisho – mpwake anatayarishiwa kukabiliana na kisu cha ngariba
      • Mwanafunzi lazima athibitishe
    2. Shughuli za kiuchumi (alama 2x1)
      1. Ufugaji / wafugaji – Anayeimbiwa wimbo alipozaliwa fahali alichinjwa.
      2. Ukulima / kilimo - sembe na supu
    3. Nani mwimbaji wa wimbo na anamwimbia nani? (alama 2x1)
      1. Mwimbaji – mjomba
      2.  Mwimbiwa – mpwa (mtoto wa dadake mwimbaji) 
    4. Mwimbaji wa wimbo huu ana taasubi ya kiume – Thibitisha kauli hii (alama 4x1)
      1. Anaona kuwa waoga ni akina mama
      2. Anasifu wanume wa mbari yao kuwa si waoga
      3. Akilia atachekwa na wasichana
      4. Anaambiwa kuwa ni “Ndume / mme” akabiliane na kisu
    5.  Mbinu za kuendeleza michezo ya watoto
      • Matumizi ya tamasha za muziki ya kitamaduni katika shule, vyuo na mashirika mbalimbali – katika ngazi ya kitaifa na kimataifa
      •  Kuirithisha jamii/ Kushirikisha fasihi simulizi katika sherehe za harusi, jandoni, mazishi na matambiko katika jamii mbalimbali
      • Kuimarisha na kusisitiza vipindi vya redio na runinga katika vituo vyetu stesheni zetu
      • Kuimarisha michezo ya kuigiza, mashairi, na nyimbo kupitia redio, runinga na shughuli nyingi za kitaifa
      • Kuimarisha utafiti wa Nyanja/vipera mbalimbali ya fasihi simulizi
      • Kufadhili utafiti wa michezo ya watoto
      • Kuandikwa vitabuni,
      • Tarakilishi na kanda za video kuhifadhi baadhi ya vipera vya fasihi simulizi
      •  Kufunzwa shuleni
      •  Kuweka sera za kuilinda
        (alama 6x1)
    6. mbinu za kufanikisha uwasilishaji wa soga.
      • Urudiaji
      • Uzungumzi nafsia
      • Uigizaji
      • Chuku
      • Taswira
      • Upenyezi / uchopekaji wa fanani
      • Tashhisi
      • Nidaa
      • Kuzungumza moja kwa moja
        Hoja nne za mwanzo 4x1= 4
  2. Mchango wa vijana katika hali ya maisha ya Wahafidhina
    1. Michango hasi
      • wauaji – mabarobaro kuwachoma moto wasafiri waliokuwa wakikimbilia usalama wakati wa vita vya baada ya uchaguzi.
      • wezi – wanavunja duka la Mzee Kaumu na kupora bidhaa zake.
      • wabakaji – mabarobaro waliwabaka mabinti wa Kaizari
      • wahuni - mabarobaro walimkata Subira mikato miwili ya sime, kumpiga kofi pia
      • vijana wanaikosesha nchi ya amani kwa kufanya maandamano. Inabidi Askari wa Fanya Fujo wakawakabili vikali. Vifo na majeraha yakatokea
      • wengine wanawapotosha wapiga kura wakongwe kuwapigia wagombea wasiowataka –
        “…alama ya X kwenye picha ya Kiboko…” (uk 23)
      • Kwa mujibu wa barobaro aliyevaa shati lenye maandishi ya Hitman mgongoni, wanahongwa kuwapigia viongozi fisadi kura. (uk 22)
      • Vijana kama Dick kuuza dawa za kulevya
      • Sauna kuwalangua wana wa waajiri wake kama vile wana wa Lunga – Dick na Umulkheri.
      • Wanaendeleza ukahaba – Pete kujiuza kwa majanadume, madanguro ya Bi. Kangara yana vijana wa kike
      • Utapeli – Sauna kuwauzia watu maji ya mto kama mineral water
    2. Michango chanya
      • Mhandisi Kombo kusimamia ujenzi wa nyumba ya Ridhaa ni ishara ya bidii kazini.
      • Kutunza mazingira – Lunga kuwa mwasisi wa Chama cha Watunza Mazingira Wasio na Mpaka.
      • Kuendeleza uzalendo – Mwangeka kuiwakilisha nchi yake katika udumishaji wa amani ughaibuni
      • Hazina kumsaidia Umulkheri kupata makazi katika makao yao ya vijana.
      • Hotuba ya Apondi
      • Neema kuokota mtoto
        (Zozote 10x2=20)
  3.  
    1. mbinu za kimtindo
      • Msemo/ nahau- jahazi kugonga mwamba yaani hatima mbaya/ kutofanikiwa.
      • Jazanda – jahazi letu ni maisha yetu au famili
      • Taswira oni – bahasha nyeupe na picha ya moy
      • Taswira mguso – viganja kutetemeka
      • Tashhisi – macho kukataa kuona, kushurutisha macho kukisoma
      • Taashira – ujumbe wa mauti
        alama 6 x1=6
    2. Umuhimu wa Mwanaheri
      Ni bintiye Kaizari na Subira, dadake Lime.
      • Ametumiwa kukuza talanta ya kughani mashairi mepesi
      • Anaendeleza maudhui ya elimu ambapo wanaendelea kusoma na wenzake kama Kairu nk
      • Ni kielelezo cha vijana waliokuwa wavumilivu – mateso kambini, machungu baada ya kuachwa na mama.
      • Ameonyesha maudhui ya ubakaji- Yeye na Lime walibakwa na mabarobaro kwao
      • Anadhihirisha ukiwa – barua inamtonesha kidonda rohoni alivyotorokewa na mama
      • Ametumiwa kuchimuza wahusika wengine kama Lime, Subira na mavyaa wake.
      • Maudhui ya ukabila baina ya Subira wa Bamwezi na mavyaa/ baba na wanakijii.
      • Ametumiwa kusukuma ploti ya hadithi. 4x1=4
    3. Mwanafunzi anatarajiwa kujadili shida walizopata wahusika mbalimbali riwayani.
      • Umu kuwapoteza wazazi wake na Sauna kuiba umbu wake
      • Masaibu ya Kairu, alivyosombwa na nduguze na wazazi hadi kambini, mamake pia kukosa samaki wa kuuza
      • Mwanaheri na Lime/ Kaizari kutorokewa na mama yao Subira.
      • Zohali kupata ujauzito na kufukuzwa shuleni.
      • Chandachema kulelewa na nyanyake, mamake kumtelekeza na kuishia shamba la chai.
      • Bi. Kimai kuletewa makahaba chumbani mwake na Tenge alipokuwa ameenda shambani, mbele ya wanawe na Chandachema.
      • Mateso ya Selume tangu msitu wa mamba, kisha hali ngumu ya kazi katika hospitali ya umma
      • Ridhaa kuchomewa nyumba yake na familia , nyumba zake tatu pia zinabomolewa.
      • Selume kubaguliwa katika ndoa
      • Neema na Mwangemi wanajitahidi kupata mtoto lakini hawafanikiwi na wanaishia kumpanga Mwaliko.
      • Kaizari anajitahidi kuzuia wahuni wasiwabake binti zake lakini wanamzidi nguvu na kuwabaka.
      • Lunga anajitahidi kumrithia na kumpendeza mkewe Naomi lakini hatimaye anamtoroka na kumwachia watoto
      • Kiriri anampinga Annette asiende ughaibuni lakini anampuuza na kuhamia huko.
      • Kiriri anawasihi wanawe warudi nyumbani lakini waliendelea kuishi ughaibuni hata baada ya kukamilisha masomo yao.
      • Ndoa ya Pete inapingwa na nyanyake.
      • Kipanga anataka kuambiwa babake halisi baada ya aliyemdhania kuwa babake kumkana lakini mamake hakumwambia.
      • Nyumba za mabwanyenye wa Tononoka zinabomolewa hata baada ya kutoa hongo ili zao zisibomolewe.
      • Dick anatishiwa na Buda kulangua dawa za kulevya lakini baadaye alijiondoa.
      • Naomi alimtoroka Lunga kwa sababu ya umaskini lakini anaishia kuteseka zaidi.
      • Amize Lucia wanajizatiti kupinga ndoa yake.
      • Wanaume kumtusi Mwekevu anapojitosa siasani ili kumvunja moyo lakini anavumilia mpaka anachaguliwa kuwa kiongozi wa Wahafidhina.
      • Pete anakunywa dawa ya kuua panya ili afe lakini anapelekwa katika kituo cha afya cha Mwanzo Mpya na kuendelea kuishi.
      • Pete anajaribu kuavya mimba ya mtoto wake wa pili na wa tatu.
        12x1
  4.   
    1. msemaji ni Kombe akiwaambia Boza na Sudi, wakiwa katika karakana wakichonga vinyago. Boza alikuwa akitematema mate na kushika rununu yake. Tabia iliyowaudhi.
      4x1= 4
    2.     
      • mbinu ya tabaini- si
      • taswira – kugaragara
      • tashbihi- kama kuku
      • balagha- yakuuma? Zozote 2x2= 4
    3.  
      • Tunu- Mwana harakati huyu alipigwa na kuvunjwa mguu. Mpango wa awali ulikuwa ni kumuua Hata hivyo alipona kwa bahati tu - Ngurumo
      • Ngurumo ananyongwa na chatu hata baadaye kuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa maasi katika uongozi wa Majoka. Kijana huyu anajitolea kufanya kila analoambiwa na utawala lakini anaangamizwa kwa sababu alijua siri nyingi za uongozi.
      • Chopi- Ni mlinzi wa Majoka ambaye anatakeleza maovu ya utawala kama vile mateso kwa Kenga ipasavyo. Hivyo katika mwendelezo uo huo Majoka na Kenga wanakubali kumuua Chopi ili asitoe siri zao.
      • Jabali – alikuwa mpinzani wa karibu sana wa Majoka. Alifanyiwa njama kauawa kwa kile kilichoonekana kuwa ajali ya barabarani.
      • Majoka alikuwa na kampuni kubwa barani sumu ya nyoka, alidhulumu wananchi mwishowe watu wanamwasi na kuhudhuria mkutano wa Tunu na kubaki na watu 10
      • Kenga mshauri mkuu wa Majoka alipanga njama ya kukutanisha Ashua na Husda wapigana ili kulazimisha Sudi kumchongea kinyago. Watu wanawatoroka.
      • Boza alijinadi kuwa mke wake na Husda ni marafiki hadi wakapata kandarasi ya kuoka keki. Baadaye Asiya anamalizwa.
      • Asiya aliyewafukuza Tunu na kundi lake kuwa wanamharibia wateja alirudi kuomba msamaha kwa Tunu ili amkinge.
      • Kingi akiwa mkuu wa polisi alitumiwa kuongeza vitoza machozi na risasi ili kutawanya waandamanaji. Mwishowe anahamia mrengo wa Tunu.
        6x2- 12
  5.   
    1. Dhima ya mandhari ya soko katika ujenzi wa tamthilia ya kigogo
      • Inatoa utangulizi wa wahusika. Katika mandhari ya soko tunawakuta wahusika Kombe, Boza na sudi
      • Inadokeza wakati wa matukio. Katika Onyesho la kwanza, tendo la kwanza uchongaji unafanyika asubuhi katika karakana la soko la Chapakazi.
      • Inakuza taswira kamili ya matukio. Kwa mfano, jinsi Boza anatematema mate na jinsi Kombe anavyosita kuchonga na kumwangalia kwa dharau wakiwa kwenye karakana ya uchongaji
      • Inakuza maudhui katika tamthilia. Kwa mfano, mandhari ya Soko lililochafuka linakuza maudhui ya Uongozi mbaya.
      • Yanakuza usuli wa matukio muhimu katika maisha ya wahusika. Pale sokoni, Kenga anaeleza usuli wa wafadhili wa miradi
      • Yanakuza sifa za wahusika. Tunu kukusanya watu kwenye lango kuu
        (zozote 4x2=8)
    2.    
      • Majoka ananyakua sehemu ya soko. Kenga kugawiwa kipande cha ardhi ya soko. Asiya kupewa kandarasi ya uoka keki kwa mapendeleo. Asiya kupewa kibali cha kuuza pombe haramu. Hawa wahusika wanakuza maudhui ya ufisadi.
      • Majoka kumdai Ashua kimapenzi ilhali ameoa. Ngurumo kushiriki kimapenzi na Asiya ili kupata kandarasi ya kuoka keki ya uhuru. Wanakuza maudhui ya uzinzi.
      • Uongozi mbaya – Majoka kutumia mbinu mbovu kuongoza Wanasagamoyo. Ametenda maovu mengi. Kwa mfano, kuwaua maadui wa kisiasa kama Jabali, kufunga soko n.k
      • Majoka kuwasaliti waliomchagua kuwafanyia kazi. Anafunga soko ambalo ndilo tegemeo lao. Asiya kumsaliti Boza kindoa, Ashua kumsaliti Sudi kindoa, Majoka kumsaliti Husda kindoa. Wanaendeleza maudhui ya usaliti.
      • Majoka anawaua mahasidi wa kisiasa kama jabali, Ngurumo na kuamuru Chopi kuuliwa kwa hivyo anakuza maudhui ya mauaji.
      • Ngurumo na wahuni wenzake wanamvunja Tunu muundi wa mguu. Wanajenga maudhui ya ukatili.
      • Ashua anakuza maudhui ya umaskini anapoenda kwa Majoka afisini kuomba msaada kwa ajili ya watoto wake lulala njaa.
      • Tunu ni mwanamke mkakamavu. Anatetea haki za Wanasagamoyo kwa hivyo kukuza maudhui ya nafasi ya mwanamke.
      • Majoka anawadharau wanawake. Anasema hana time ya wanawake akiwarejelea Husda na Ashua kwa hivyo kujenga maudhui ya ubabadume.
      • Tunu na Sudi kwa kushirikiana na Ashua, wanaendeleza harakati za ukombozi wa jimbon la Sagamoyo. Wanakuza maudhui ya mapinduzi.
      • Majoka kutawala Wanasagamoyo kimabavu. Hajaruhusu wafanyikazi kuwasilisha malalamishi yao kupitia maandamano. Anaendeleza maudhui ya udikteta. Anatishia kumfuta Kingi kazi kwa kutofuata amri yake
      • Maudhui ya tamaa yanaendelezwa na wahusika mbalimbali. Majoka anatamani Ashua kimapenzi. Anamtamani Ashua kimapenzi. Anatamani ardhi ya soko. Husda kummezea Chopi mate.
      • Majoka anaendeleza maudhui ya ukoloni mamboleo kwa kuiga ugeni. Anachanganya ndimi kwa Kiingereza – sina time.
      • Majoka anategemea mataifa ya ughaibuni kwa mkopo wa uchongaji wa kinyago. Anakuza maudhui ya utegemezi.
      • Ashua kuchuuza mandazi ili kuikimu familia yake, Sudi na wenzake kuchonga vinyago kama kitega uchumi kunakuza maudhui ya bidii kazini.
      • Dhima ya elimu inaibuka kupitia uwezo wa akina Sudi wa kutambua na kutetea haki. Waliyaanza wakiwa chuoni. Majoka naye anasambaratisha taasisi ya elimu kwa kuendeleza matumizi ya mihadarati katika shule yake.
      • Ukaragosi unaendelezwa na vitendo vya Boza na Ngurumo. Wanajipendekeza kwa Kenga na Majoka mtawalia.
      • Haki za wafanyakazi zinakuzwa na wafanyikazi wa kampuni ya Kajoka wasiolipiwa bima (babake Tunu).
  6.         
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili. Alama 4
      • Ni mawazo ya Samweli
      • Akiwa ametoka ofisini mwa mwalimu mkuu
      • Anakwepa wanafunzi waliotaka kujua matokeo yake ya mitihani
      • Alikuwa amefeli mtihani na hivyo kutamauka. 4x1=4
    2. mbinu za lugha
      • tashbiha – kama mwalimu wao
      • masimango- wambea, chakumbimbi
      • msemo- chakumbimbi
      • balagha – kwa nini…? 3x1
    3. Ni kwa vipi mzungumzaji anamchukulia mwalimu mkuu kama hambe 3x1
      • Mwalimu mkuu hakuwahi kumwamini Samweli hata siku moja kama anaweza kufaulu mtihani
      • Mwalimu mkuu hakumwamini Samweli aliposema amelipa ada mpaka alipohakikisha katika kijitabu/ kumbukumbu zake.
      • Anaonyesha dharau kwa Samweli kwa kumrushia karatasi kama mbwa, alimpuuza.
      • Hakumpa ushauri wowote iwapo angepata matokeo yake kuwa mabaya
      • Alimjibu kwa karaha na kumwita fidhuli, akamwuliza kuwa wengine wanalipa mawe au majani.
    4. Taja na ufafanue sifa tatu za msemaji. Alama 4x1
      • Ni msaliti-amelipiwa karo asome lakini badala ya kusoma anafanya mahoka na hivyo kufeli
      • Ni mwoga- anaonyesha kuogopa mbele ya mwalimu mkuu alipoenda kuchukua matokeo yake ya mtihani/anasitasita kuongea na kujibu maswali aliyoulizwa na mwalimu mkuu.
      • Ni mtiifu-alitii mamake alipomwambia waende nyumbani
      • Mwenye hasira-anakasirishwa na wanafunzi wengine walipotaka matokeo yake ya mtihani.
      • Ni msiri-hataki mtu yeyote ajue matokeo yake ya mtihani/alitaka kujiua kisiri
      • Ni mwongo-aliwadanganya wazazi wake kuwa hakupata matokeo kwa sababu hakuwa amekamilisha karo/alimdanganya ninake kuwa alikuwa mwerevu shuleni.
      • Ametamauka- alitaka kujiua kwa kujitosa majini alipofeli mtihani.
      • Ni mwenye maringo/kiburi-anajigamba kuwa mwalimu mkuu angeaibika kwa kuwa aliona amefaulu mtihani.
      • Mshirikina-anasema hakukutana nap aka mweusi alipokuwa anaenda kufanya mtihani hivyo hangefeli.
    5. Eleza jinsi maisha ya msemaji yanavyoafiki anwani ya hadithi. Alama 6x1
      • Samweli anasomea shule ambayo dadake Bilha na Mwajuma walisoma na kufaulu.Kwa vile ni mvulana anatarajia kufaulu lakini anafanya mahoka shuleni hadi anafeli.Kwa hivyo alifeli mtihani wa shule na wa Maisha kwa sababu hakuona matumaini mbele yake.
      • Samweli alimdanyanya mamake kuwa alikuwa mwerevu shuleni kumbe sivyo.Alitarajia kuendeleza uhusiano huu baada ya kufaulu mtihani lakini anafeli.Nina labda angemshuku, angejua ukweli kuwa mwanawe hakuwa mwerevu na hivyo akamfeli mamake na kufeli maishani.
      • Samweli aliwachunguza wanafunzi waliotoka ofisini ili kupima iwapo walipita au kufeli mtihani
      • Samweli anajiaminisha kuwa yeye ni mjanja na angeweza kumshangaza mwalimu.
      • Alifedheheshwa na alama za D zilizoorodheshwa na kumfanya kulewa lewa
      • Alidanganya nyumbani kuwa hakupata matokeo yake sababu ya salio la karo.
      • Babake alitarajia mwamawe wa kiume kufaulu. Kwa hivyo kusafiri kilomita 6
      • Samweli kutaka kujitosa majini ni kwa sababu ya kupoteza matumaini na kukolewa na mpitanjia. Alikuwa na maoni kuwa ili awe na maisha mazuri ilimlazimu apite mtihani na hivyo kufeli mtihani, ilimaanisha kuwa alifeli maishani.
      • Wazazi wa Samweli walitumia raslimali yao yote kwa kumlipia karo wakitarajia angewaokoa kutoka lindi la umaskini kama mtoto wa kiume.Anapofeli shuleni anafeli pia katika maisha na hivyo hangewaauni wazazi.
      • Baba Samweli anamletea Kamba ya kujinyonga kwa sababu ya kufeli shuleni kuonyesha kuwa pia katika maisha alikuwa amefeli na hakustahili kuishi.
      • Mamake anamshauri waende nyumbani kwani kufeli mtihani si kuanguka maishani.
        8x1= 8
  7.    
    1. Tulipokutana tena – Alifa Chokocho
      • Msemaji ni Bogoa Bakari
      • Kwa kina Sebu, Kazu na wake zao
      • Katika klabu ya Pogopogo.
      • Bogoa na Sebu rafiki yake wa zamani walipokutana baada ya miaka 40. 4x1
    2. mbinu
      • uashiriaji – pale
      • jazanda – jehanamu – masaibu 2x1=2
    3.       
      1. Sebu kurejelea jinsi alivyokuwa anapenda kucheza na Bogoa wakiwa watoto. Sebu alitoka katika familia inayojiweza ilhali Bogoa kutoka kwa ya kimaskini.
        Umuhimu
        1. Hapa mbinu rejeshi inaonyesha kuwa:
        2. Watoto hawajali tofauti za kitabaka zilizo baina yao. Sebu hakumbagua Bogoa.
        3. Inaibua maudhui ya umaskini, utabaka na dhuluma kwa watoto.
        4. Kuonyesha kuwa mchezo ni muhimu kwa watoto.
        5. Inaonyesha uketo wa uhusiano wa kirafiki baina ya Bogoa na sudi.
      2. Sebu kurejelea jinsi Bogoa aliletwa Zewa na babake ili alelewe nyumbani kwa Bi. Sinai.
        Umuhimu wake
        1. Inachimuza utepetevu wa wazazi ambao hutelekeza malezi ya wanao - Wazaziwe Bogoa kwa Bogoa
        2. Inaonyesha mateso ambayo watoto hupitia, kama vile dhiki ya kisaikolojia kwa vile wao kulazimishwa kuishi wasipopenda.
        3. Inajenga maudhui ya haki za watoto, malezi mabaya n.k
        4. Inakuza sifa za wahusika wengine. Kwa mfano, ukatili wa Bi. Sinai
      3. Bogoa anakumbuka walivyocheza michezo mbalimbali na akina Sebu kama vile kuvua makambare, walivyooga mtoni.
        Umuhimu wake
        1. Kuonyesha umuhimu wa mchezo kwa watoto.
        2. Inajenga sifa za Bi. Sinai. Ni katili. Alimchapa sana Bogoa alipochelewa kurudi nyumbani kutoka mchezoni.
        3. Inaonyesha hali ya watoto wanaoishi na wazazi walezi. Wanateswa.
        4. Inaonyesha dhiki za kisaikolojia wanayopitia watoto wanaolelewa na wazazi wasiowazaa.
        5. Inaonyesha kuwa walikuwa marafiki wa dhati.
    4. jehanamu
      1. Ulitima wa wazazi wa Bogoa – sabuni kuwa kitu cha anasa
      2. Ajira ya watoto – kuchoma maandazi na kuuza shuleni. Alimtuma kuuza mandazi shuleni wakati wenzake wakisoma.
      3. Kuuzwa na wazazi wake kwa familia ya Bi. Sinai kule jijini
      4. Kunyimwa nafasi ya kusoma kama mtoto. Alifunzwa na Sebu
      5. Kunyimwa nafasi ya kucheza na wenzake
      6. Ukiukaji wa haki ya kutibiwa. Alichomwa na mafuta ya maandazi
      7. Bi. Sinai kumchapa Bogoa vibaya anapoenda kucheza, kumchoma viganja, kumtisha kuwa atamng’oa ulimi.
      8. Watoto wa Bi. Sinai kuambiwa na mama yao kuwan watoto wa kimaskini hawapaswi kusoma bali ni wa kutumwa.
      9. Bogoa aliishii kwa hofu nyingi. Akatoroka.
        Zozote 8x1=8
  8. USHAIRI
    1. Eleza ujumbe wa shairi hili. (alama 4)
      1. Walianza safari ili kuhama janga la jangwa kutafuta bonde la rutuba.
      2. Walihama kutafuta mvua nzitonzito
      3. Walihama ili kupata pa kulima kwa nyoyo imara
      4. Walime ili pia kuzima moto tumboni
      5. Ardhi yenyewe imewageukia, inawadhuru.
      6. Ng’ambo wanayolima siyo waliyoazimia walipoanza safari.
      7. Malaika wa machozi (wenye uwezo mkubwa) wanafanya njama za kuiba matunda ya udongo.
      8. Wakulima wanakondeana kutokana na athari ya ukame.
        4x1=4
    2. Eleza maana ya kitamathali na kijuujuu ya mstari ‘Kuzima moto tumboni.’ (alama 2)
      1. Kumaliza njaa
    3. Bainisha matumizi ya vipengele viuatavyo katika shairi.
      • Mishororo mishata (alama 2)
        • Siku moja, miongoni mwa wengi
        • Virago vyetu migongoni
        • Bali, tuzo kutoka ardhi
        • Kwa wale ambao
        • Kutokana na nyimbo
        • Hii ng`ambo tunayolimia
        • Baada ya wakulima
          (Zozote 2x1=2)
      • Usimulizi (alama 2)
        • Nafsi neni anasimulia jinsi walivyopiga safari siku moja kutafuta maeneo yenye rotuba ili wayalime kwa ajili ya kujiondolea njaa.
        • Baadaye, kinyume kinatokea. Wenye uwezo wanawala jasho lao.
        • Wakulima kukondeana kutokana na athari za ukame na njaa.
          (Zozote 2x1=2)
    4. Thibitisha kuwa hili ni shairi huru. (alama 4)
      Halijafuata sheria/kanuni za utunzi wa mashairi ya kimapokeo. Kwa mfano:
      • Beti hazina idadi sare ya mishororo. Ubeti wa kwanza 8, wa mwisho 10
      • Mishororo haina idadi sawa ya vipande. Kwa mfano ubeti wa pili, mshororo wa tatu una vipande viwili vingine kimoja
      • Mishororo yake ina idadi tofauti ya mizani.
      • Beti zake hazina urari wa vina.
        (4x1=4)
    5. Eleza dhima ya aina mbili za urudiaji katika shairi hili. (alama 4)
      • urudiaji wa sauti – ‘i’ katika wengi, migongoni, safari
      • dhima: kujenga ridhimu/kulipa shairi mwonjo/kulipa shairi mdundo wa kimuziki
      • urudiaji wa silabi – imepita, kupita
      • dhima: kujenga ridhimu/kulipa shairi mwonjo/ mdundo wa kimuziki/ kuleta urari wa vina
      • urudiaji wa neno – nzitonzito, imepita, kupita
      • dhima:Kusisitiza wazo
    6. Eleza toni ya shairi hili. (alama 2)
      • Toni ya kukata tamaa – wakulima wametamauka kutokana na kutotimia kwa maazimio yao.
      • Huzuni – taswira ya wakulima walivyoteseka
      • Ya matumaini – walipoanza safari walitazamia kuzima njaa matumboni mwao.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Bondo Joint Mocks Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?