Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kassu Jet Joint Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

MAAGIZO

  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.


MASWALI

UFAHAMU
Majuto alihamia mjini Tija na kununua ardhi kubwa na kujenga jumba kubwa lenye vyumba mia moja vya kukodisha na kando yake akajenga jumba lake la kifahari la kuishi na familia yake. Aliipenda sana hali yake mpya. Aliipenda zaidi hewa safi ya utajiri mjini. Aliyapenda mno mandhari mapya. Familia yake ilitabasamu na kuifurahikia sana hali hii nzuri. Majumba yake ya kukodisha yalijaa watu. Kila mwisho wa mwezi alipata milioni moja kutoka kwenye vyumba vyake vya kukodisha. Jambo hili lilimweka katika nafasi nzuri ya kujilimbikizia mali.
Mji wa Tija ulijaa matajiri wenye hela nyingi. Majuto alitamani kuwa na mali zaidi. Alitamani kuwa kama mmoja wa mabwanyenye katika mji wa Tija. Alitamani kuwa kama Mzee Mwinyi ambaye alimiliki magari mengi ya kifahari. Mwinyi alikuwa bilionea. Kila siku Majuto aliwaambia wanawe na mkewe kuwa angetamani sana kuwa kama Mzee Mwinyi na hata kuupiku ukwasi wake. Wao walimhimiza tu na kumwombea utu, uhai na uzima ili azitimize ndoto zake. “Baba, ipo siku utakuwa kama yeye. Work smart na umwombe God. Katika Biblia tunaambiwa kuwa Anna aliomba sana na akapewa mtoi”, alisema Kiloo.
Kiloo alipenda sana kutembea mjini na kubugia pombe kwenye baa. Alipenda kujigamba sana mbele ya walevi wenzake. Aliwaeleza jinsi familia yake ilivyo tajiri na matarajio makubwa ya baba yake. Aliwadadavulia kuhusu nia nzuri ya baba yake kuwa bilionea na kumiliki vitu vya thamani kubwa. Walimsikiliza kwa umakini katika ulevi wao. Kumbe walevi huwa makini wakati mwingine!
Siku moja familia ya Majuto ilipata mgeni. Hawakuwa wamemwona mja huyu tangu kuhamia pale. Alikuwa amevalia suti ya samawati, shati jeupe na tai nyekundu. Alipendeza. “Jina langu ni Mweneza. Mimi ni nabii kutoka kijiji cha Mazingara. Roho wa Mungu amenielekeza hapa leo”, alisema. Baada kuupata staftahi Mwenezi aliomba kuzungumza na Majuto pembeni.
Majuto alimpeleka Mwenezi katika chumba kimojawapo kwenye kasri lake ili wawe na mazungumzo ya faragha. “Roho wa Mungu amenituma kwako Mzee Majuto. Naona unataka sana kuwa na mafanikio makubwa zaidi maishani. Unataka kuwa bilionea. Hilo linawezekana. Ni mapenzi ya Mola kila mtu kufanikiwa kwa kiwango cha juu kulingana na imani yake. Amini na Mungu atatenda. Hata Mzee Mwinyi mimi ndimi nilimsaidia mwaka jana. Sasa yeye ni bilionea. Roho wa Mungu alinituma kwake jinsi alivyonituma kwako hii leo. Zungumza na familia yako. Nitarejea baada ya siku mbili”, alisema Mwenezi. Machozi ya furaha yalimdondoka Majuto na kuulowesha uso wake. Aliiona hiyo kama nafasi bora ya kuwa bilionea.
Familia ya Majuto ilizipokea habari hizo kwa imani kwamba ndoto ya mkuu wa familia hatimaye ingetimia. Fikiri wewe, unatamani kuwa mkwasi wa wakwasi kisha upate njia rahisi na nyoofu ya kulitimiza lengo hilo. Bila shaka utajituma sana. Hata hivyo, Mawazo alikuwa na mawazo tofauti. “Huenda huyu nsi anataka kutupunja! Huenda ana lengo la kuiporomosha familia hii. Huenda ana habari akali kuihusu familia yetu. Huenda ametumwa kuja kuisambaratisha familia hii,” alijisemea.
Baada ya siku mbili Mwenezi alirejea. Uso wa Majuto ulidhihirisha waziwazi furaha aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake. Alimweleza Mwenezi kuwa familia yake ilikuwa imeridhia na wangependa kujua Mola alivyoagiza wafanye. “Uza majumba yako yote ya kukodisha, gari lako na jumba lako hili la kifahari. Baada ya hayo leta hela zote niziombee. Zitaongezeka mara mia moja”, alisema Mwenezi. Majuto alikubaliana na agizo hilo na kufanya yote aliyoelezwa. Alipata jumla ya milioni mia mbili baada ya kuwekua hela zote alizokuwa amehifadhi katika benki kutokana na kodi ya nyumba. Alijua moyoni na akilini kuwa hizi hela zingekuwa takribani bilioni ishirini baada ya kuombewa. Hatimaye angekuwa bilionea! Majuto alitafuta chumba cha kuishi siku hiyo ya siku pale mjini. Alilipa kodi ya mwezi mmoja katika chumba hicho kama alivyoagizwa na nabii wa Mungu.
Mzee Majuto alimpigia simu Mwenezi kwa furaha kuu na kumweleza kuwa amefanya yote jinsi alivyoagizwa. Nabii alimwambia aziweke pesa zote ndani ya karatasi nyeusi. Baadaye Majuto alimwelekeza nabii walipokuwa wamepanga chumba. Furaha ilijisawiri katika nyuso za wanafamilia. Kila mmoja akiwa na nia ya kuipokea hali yao mpya. Kulingana nao, walikuwa wameuona mkono wa Mungu usioonekana na wengi! “Leo ni leo, asemaye kesho ni mwongo. Walionikashifu watanisifu. Wataziramba nyayo zangu. Kumbe Mungu amekuwa akisikia kilio changu!” Alijisemea Majuto.
Mwenezi alifika katika eneo hilo bila kukawia. Alikuwa amebeba tangi kubwa la lita mia mbili na kumi. “Roho wa Mungu ameniamrisha nije na tangi hili ili nikimaliza kuziombea hela zako niziweke humu ndani. Utalifungua baada ya siku nne na uchukue mabilioni yako. Hata najua zitajaa na nyingine zimwagike humu ndani chumbani”, alisema Mwenezi bila kupepesa jicho. Majuto alikubali na kuahidi kuyafuata maagizo yote. “Fungeni macho tuombe. Yafumbeni kabisa ili Mola asikie sala zetu,” alisema. Baada ya maombi Mwenezi aliondoka na kurejea katika kijiji cha Mazingara.
Siku nne zilipoisha Mzee Majuto, mke wake na wanawe walijawa na furaha sana. “Leo mji mzima utanitambua. Nitanunua ardhi nyingine kubwa, magari mengi ya kifahari na ndege moja ya kuenda safari za mbali”, alisema Mzee Majuto. Aliwaongoza wenzake katika kuufungua ule mtungi wenye pesa. Walishangaa sana kupata kuwa ule mtungi ulikuwa na ile karatasi nyeusi waliyoiweka. Walidhani tu zilizomo ni hela walizoweka pekee. Waliifungua kwa wasiwasi mkubwa. Mioyo yao ilidunda kama ngoma. Akili ziliwaduru. Mawazo alikuwa na msongo wa mawazo. Ndani ya karatasi hiyo mlikuwa na vijikaratasi vidogo vya gazeti. Kijikaratasi kimoja kilikuwa kimeandikwa, AKILI NI MALI, kingine kikaandikwa, WEWE NI SAMAKI, MIMI NI BAHARI!
Mzee Majuto alisema kwa majuto,” Kumbe nimepunjwa! Eee Mungu wangu. Nionekanie Mola. Nilimwamini mtumishi wako.

Maswali

  1. Yape makala haya kichwa mwafaka. (alama 1)
  2. Ni jambo lipi ambalo Majuto alipania sana? (alama 1)
  3. Eleza ujumbe unaojitokeza katika kifungu hiki. (alama 3)
  4. Kwa nini Majuto alitaka kuwa bilionea? (alama 3)
  5. Taja na ufafanue mbinu tatu za lugha zilizotumiwa katika kifungu hiki. (alama 4)
  6. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika kifungu. (alama 3)
    1. kasri
    2. faragha
    3. akali
      UFUPISHO (ALAMA 15)
      Soma kifungu kifutacho kisha ujibu maswali yanayofuata
      Mataifa yanayoendelea yameathirika pakubwa na mabadiliko ya tabianchi. Hali hii imesababisha misimu mirefu ya kiangazi ambayo hatimaye yamesabisha ukame katika mataifa haya. Nchi nyingi pembeni mwa Afrika zenye maeneo kame yameitisha msaada wa dharura kwani jinamizi hili limesabisha maafa si haba. Taswira katika mataifa haya ni ya kutisha. Taarifa katika vyombo vya habari zimeonyesha mamia ya watu waliokufa kwa sababu ya ukosefu wa vyakula. Wengi wamekuwa watoto wachanga na wazee wasiojiweza. Watoto wamekuwa wakikumbwa na utapiamlo, kwani hata wakiambulia chakula hakitakuwa chenye madini mbalimbali yanayohiyajika mwilini. Utapigwa na butwaa vilevile unapoona watu waliokonda na kudhhofika kiafya. Huwa tayari wamefika mwisho na kupoteza matumaini huku wakichungulia kifo, yao imekuwa kusubiri misaada kutoka mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali.
      Maji katika nyakati kama hizi za kiangazi huwa nadra kupatikana. Watu wengi hulazimika kutembea kwa kilomita nyingi angalau kupata hata kiasi kidogo cha maji. Hata baada ya kubahatika, hupanga foleni ndefu kwani watu hutegemea sehemu moja kupata maji. Hii ni kwa sababu mito mingi hunyauka na hata visima ambavyo ni vichache pia hunyauka. Maji mengine yanayopatikana huwa machafu. Kwa kuwa wakaazi hawana hiari, huishia kunywa na kuyatumia maji haya nyumbani. Hatima yake ni magonjwa yanatokana na maji machafu. Magonjwa hayo ni vile kama kipindupindu, homa ya matumbo miongoni mwa mengine. Ikumbukwe kuwa, hali katika zahanati za vijijini ni duni. Kando na haya, zahanati ni chache na zilizotengana mithili ya ardhi na mbingu. Watu wengi huaga dunia katika harakati za kutafuta huduma za matibabu ama hata kwa kukosa huduma hizo kabisa. Maelfu ya mifugo pia wamekuwa wakifa nyakati za kiangazi. Hii ni kwa kukosa lishe na pia maji. Hasara hii inatokea huku wenyeji wakikosa chakula. Mifugo wanaosalia huwa wamekondeana kama wamiliki wao. Hata kuuza ni balaa. Hali hii imekuwa si hali kwa muda sasa. Ni muhimu jambo hili liangaziwe kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu.
      Baada ya miezi mingi ya kiangazi, mvua inazuka kwa fujo. Maeneo yaleyale yanaripoti mafuriko. Msaada wa kibinadamu unaanza kuitishwa tena. Vifo vya watu na mifugo vinaanza kushuhudiwa. Maji yaliyokuwa nadra sasa yanapatikana kwa wingi kupita kiasi. Je, serikali za nchi hizi zina mipango madhubuti? Kuitisha misaada nyakati zote mbili hushangaza. Ni muhimu kuzingatia ujenzi wa mabwawa. Huu utakusanya maji yote ambayo yangesabisha maafa na kuhifadhi kwa minajili ya kutumika nyakati za kiangazi. Isitoshe, maji yayo hayo yanaweza kunyunyiziwa mimea na hivyo kuchangia pakubwa katika uzalishaji wa vyakula. Bila shaka, vifo vinavyotokana na uhaba wa vyakula vitapunguzwa na hatimaye kuzikwa katika kaburi la sahau.
      Kuchimba visima vingi na kueneza nguvu za umeme pia kutaimarisha uwepo wa maji ya kunywesha mifugo na kutumika katika shughuli za nyumbani. Ni muhimu kumfundisha mtu kuvua samaki kuliko kumpa samaki kila wakati. Wananchi wafundishwe njia mwafaka za kuendeleza kilimo chenye kipato kikubwa. Huku kutawafanya kuzalisha kiwango kikubwa cha chakula. Kando na kuwafundisha ni kuwahimiza watu walio katika maeneo kame kupanda mimea inayoweza kustahimili angalau muda mrefu wa kiangazi ili isinyauke haraka. Serikali pia ziangazie upya bei ya pembejeo. Mbolea na mbegu zimekuwa bei ghali katika siku za hivi majuzi. Gharama hii imewavunja moyo wakulima wa maeneo ya nyanda za juu na yenye mashamba yenye uwezo wa kuzalisha vyakula vya kulisha maeneno mengine. Kwa sababu hii, kumekuwa hata na uhaba wa vyakula katika maghala ya serikali.
      Kichwa kibaya cha ufisadi hakijakosa kupata mgao wake wa lawama katika suala hili pana la ukame na mabadiliko ya tabianchi. Viongozi wenye ushawishi serikalini wameishia kufuja pesa zinazotengewa ujenzi wa mabwawa, upunguzaji wa bei ya pembejeo na hata usambazaji wazo. Ni lazima umma na serikali ijizatiti katika vita dhidi ya ufisadi ili kuweza kuukomesha. Serikali pia iweze kuimarisha miundo msingi katika maeneno mbalimbali kwani hali duni ya miundo msingi imechangia. Barabara duni zimezuia usambazaji wa pembejeo na mavuno mashambani huku watu wakikosa chakula kicho hicho baadaye.
      Ni lazima wafugaji wapate kuelewa kuwa mifugo wengi bila mipango ni hasara. Waweze kuwa na mifugo wanaoweza kuwashughulikia ili kupunguza hasara za vifo vyao wakati wa kiangazi. Wafugaji na serikali pia washirikiane kuanzisha au kuimarisha bima ya mifugo ili wafugaji wapate fidia wakati mgumu wa kiangazi na ukame. Kando na hilo, watafiti waimarisha mbegu ya mifugo wanaozaliwa kwani hili litaimarisha kipato chao. Kwa kweli, suala la madhara ya mabadiliko ya tabianchi linaweza kukabiliwa kwa kupanda miti mingi. Serikali na wananchi wapande miti katika mashamba ya serikali na ya watu binafsi. Wabinafsi wenye tabia ya kukata miti misituni ovyoovyo, hata katika chemichemi ya mito lazima wakomeshwe kwa kukabiliwa kisheria. Sheria zilizomo zitiwe shime ili kufanikisha vita hivi. Serikali, wananchi, mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, miungano ya kimaeneo, kibara na kimataifa ikivalia njuga mabadiliko ya tabianchi na madhara yake, tutakuwa na sababu ya kutabasamu.
      Maswali 
      1. Fupisha aya za kwanza kwa maneno 80-90. (Alama 6,1 utiririko)
      2. Eleza hatua za kukabiliana na madhara ya ukame na mabadiliko ya tabia nchi kwa maneno 100-110. (Alama 9,1 utiririko)

MATUMIZI YA LUGHA (ALAMA 40)

  1. Andika tofauti mojamoja kati ya sauti zifuatazo. (alama 2) 
    1.  /ny/ na /y/
    2.  /g/ na /gh/
  2. Kwa kupigia mstari, onyesha panapotokea shadda katika maneno haya. (alama 1)
    1. majaka
    2. paramamba
  3. Onyesha mofimu katika neno lifuatalo. (alama 2)
    awaye
  4. Tenganisha silabi katika maneno yafuatayo (alama 2)
    1. kinena
    2. masizi
  5. Tumia neno ‘zuri’ katika sentensi kama:
    1. kiwakilishi (alama 1)
    2. kivumishi (alama 1)
  6. Kutokana na mzizi ‘-baya’ unda: (alama 1)
    1. nomino
    2. kivumishi
  7. Ainisha virai katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
    Wale wengine wataenda Moyale kwa ndege.
  8. Andika kinyume cha sentensi hii kwa kuzingatia maneno yaliyopigiwa mstari (alama 1)
    Punde tu alipojibu swali hilo Tunai alitoka darasani.
  9. Andika katika wakati ujao hali ya kuendelea (alama 1)
    Neema alimlipia Asna karo.
  10. Andika miundo yoyote miwili ya nomino katika ngeli ya U-I (alama 2)
  11. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya udogo wingi (alama 2)
    Debe hilo litasafirishwa pamoja na nyundo hiyo.
  12. Ainisha vitenzi katika sentensi hizi:
    1. Paka alikuwa anamla panya. (alama 1)
    2. Simba alikuwa mtini. (alama 1)
  13. Andika katika usemi halisi. (alama 2)
    Mwenyekiti alisema kuwa wangetoa nyongeza ya mshahara mwaka ambao ungefuata.
  14. Tumia nomino ya jamii badala ya maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 1)
    Omanyala aliwaona waimbaji wengi sana.
  15. Jibu kulingana na maagizo:
    1. Mwalimu aliwashauri watahiniwa wajibidiishe masomoni.
      (Geuza maneno yaliyopigiwa mstari kuwa nomino) (alama 2)
    2. Naam, amepigwa sana. (Ainisha maneno yaliyopigiwa mstari) (alama 2)
    3. Wanafunzi wote walisoma maswali kwa makini. (Bainisha kiima na chagizo)
      (alama 2)
    4. Ingawa hakuanza vizuri, alimaliza vizuri. (Ainisha vishazi) (alama 2)
  16. Changanua sentensi ifuatayo kwa kielelezo cha jedwali (alama 4)
    Mkutano utakaofanyika wiki ijayo utahudhuriwa na wanajopo wengi sana.
  17. Bainisha shamirisho katika sentensi ifuatayo (alama 3)
    Nuru alimnywesha babu yake uji mtamu kwa kikombe
  18. Tunga sentensi kubainisha matumizi yafuatayo ya kiambishi ‘ki’ (alama 2)
    1. Kuonyesha namna tendo lilivyofanyika
    2. Kama kitenzi kishirikishi kipungufu
  19. Alama ya kitone hutumiwa mwishoni mwa sentensi. Tunga sentensi moja kuonyesha matumizi mengine ya alama ya kitone (alama 1)

ISIMUJAMII (alama 10)

  1. Eleza kaida zozote tatu za lugha (alama 3)
  2. “Hapana ni kifaduro!” Alibisha mwingine…Maana ninasikia kupumua kunamtatiza…anapumua kama mgonjwa wa kifua.
    1. Tambua sajili ya makala haya na uthibitishe (alama 1)
    2. Tambua mbinu tatu za kimtindo kifunguni. (alama 3)
    3. Tambua sifa ambazo zingetumika kwenye sajili hii. (alama 3)


MWONGOZO

UFAHAMU

MASWALI

  1. Yape Makala haya kichwa mwafaka. (alama 1)
    • Tamaa ya Majuto/Majuto/Majuto ni mjukuu
  2. Ni jambo lipi ambalo Majuto alipania sana? (alama 1)
    1. Majuto alitamani kuwa Tajiri Zaidi.
    2. Alipania kuwa na mali Kama mzee Mwinyi.
  3. Eleza ujumbe unaojitokeza katika kifungu hiki. (alama 3)
    1. Baadhi ya watu wanahadaika kutokana na tamaa ya mali na hivyo kupoteza mali nyingi.
    2. Watu kama vile Mwenezi wanatumia udanganyifu ili kujinufaisha na kujitumia jina la Mungu ili waaminiwe.
    3. Baadhi ya wahubiri wanatumia ujanja ili kujitajirisha.
  4. Kwa nini Majuto alitaka kuwa bilionea? (alama 3)
    Ili mji mzima umtambue
    1. Anunue ardhi nyingine kubwa.
    2. Anunue magari mengi ya kifahari.
    3. Anunue ndege moja ya Kwenda safari za mbali.
  5. Taja na ufafanue mbinu tatu za lugha zilizotumiwa katika kifungu hiki. (alama 4)
    1. nidaa-kumbe nimepunjwa!
    2. tashihisi -leo mji mzima utanitambua
    3. majazi-Mwinyi (Tajiri), Majuto-alijuta kwa kumwamini Mwenezi.
    4. methali -leo ni leo, asemaye kesho ni mwongo.
    5. kuchanganya ndimi-work smart na umwombe Mungu.
  6. Eleza maana ya maneno haya kama yalivyotumika katika kifungu. (alama 3)
    1. kasri -Jumba kubwa la kifahari.
    2. faragha- fiche, chemba
    3. akali- chache

MUHTASARI/UFUPISHO

  1. Fupisha aya za kwanza kwa maneno 90-100. (Alama 6,1utiririko) 
    1.  Mataifa yanayoendelea yameathirika pakubwa na mabadiliko ya tabianchi na madhara ukame.
    2. Nchi nyingi pembeni mwa Afrika zenye maeneo kame yameitisha msaada wa dharura.
    3. Mamia ya watu wamekufa kwa sababu ya ukosefu wa vyakula.
    4. Watu pia wamedhoofika kiafya kwa sababu ya uhaba wa vyakula.
    5. Kiangazi kimesababisha uhaba wa maji.
    6. Watu wanalazimika kutembea kilomita nyingi angalau kupata hata kiasi kidogo cha maji.
    7. Maji mengine yanayopatikana huwa machafu na hivyo kusababisha magonjwa.
    8. Watu wanaaga dunia kwa kukosa huduma za matibabu.
    9. Mifugo wengi hufa kwa kukosa maji na vyakula kwa sababu ya ukame.
  2.  Eleza hatua za kukabiliana na madhara ya ukame na mabadiliko ya tabianchi. (Alama 9,1 utiririko)
    NJIA YA KUKABILIANA YA MADHARA YA MABADILIKO YA TABIANCHI NA UKAME. 
    1. ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya unyunyiziaji wa maji
    2. uchimbaji wa visima
    3. kupunguza bei ya pembejeo na mbolea
    4. wananchi wafundishwe njia mwafaka za kuendeleza kilimo chenye kipato kikubwa cha chakula.
    5. wakulima wahimizwe kupanda mimea inayoweza kustahimili angalau muda mrefu wa kiangazi
    6. ufisadi ukabiliwe vikali
    7. lazima wafugaji wafuge mifugo wanaoweza kuwashughulikia ili kupunguza hasara
    8. wafugaji na serikali washirikiane kuanzisha au kuimarisha bima ya mifugo ili wafugaji wapate fidia wakati mgumu wa kiangazi.
    9. serikali na wananchi wapande miti katika mashamba ya serikali na ya watu binafsi.
    10. ukataji wa miti ukomeshwe kwa kuwachukulia hatua za kisheria wanaohusika.

MATUMIZI YA LUGHA (alama 40)

  1.  
    1. /ny/ ni king’ong’o ilhali /y/ ni kiyeyusho/nusu irabu (alama 1)
    2. /g/ ni kipasuo ilhali /gh/ ni kikwamizo. (alama 1)
  2.  
    1. ma-ja-ka (½)
    2. pa-ra-ma-mba (½)
  3. a-nafsi (½)
    w-mzizi(½)
    a-kiishio(½)
    ye-kirejeshi(½)
  4.  
    1. ki-ne-na (alama 1)
    2. ma-si-zi (alama 1)
  5.  
    1. Zuri limenunuliwa. (alama 1)
    2. Gari zuri limenunuliwa. (alama 1)
  6.  
    1. ubaya(½)
    2. mbaya/kibaya/vibaya/baya(½)
  7.  wale wengine- kirai nomino (alama 1)
    wataenda Moyale- kirai kitenzi (alama 1)
    kwa ndege- kirai kihusishi
    (mtahiniwa aandike virai vyovyote viwili, kila kimoja alama moja)
  8. punde tu alipouliza swali hilo Tunai aliingia darasani. (alama 1)
  9. Neema atakuwa anamlipia Asna karo. (alama 1)
    AU
    Neema atakuwa akimlipia Asna karo.
  10.  
    1. M-MI: mkoba-mikoba, mkate-mikate, mti-miti, mto-mito
    2. MW-MI: mwiba-miba, mwaka-miaka, mwezi-miezi
    3. MU-MI: muwa-miwa, muundi-miundi, muundo-miundo
    4. MO-MI: moyo-mioyo-moto-mioto
      Miundo yoyote miwili, kila muundo pamoja na mfano ni alama moja.
  11. Videbe hivyo vitasafirishwa pamoja na vijundo hivyo. (alama 2)
  12.  
    1. alikuwa-kitenzi kisaidizi(½)
      anamla- kitenzi kikuu(½)
    2. alikuwa-kitenzi kishirikishi kikamilifu (alama 1)
  13. “Tutatoa nyongeza ya mshahara mwaka ujao,” Mwenyekiti alisema. (alama 2)
  14. Omanyala aliona kikoa cha waimbaji. (alama 1)
  15.  
    1. Mwalimu aliwapa ushauri watahiniwa watie bidii masomoni. (alama 2)
    2. naam-kihisishi cha kuitikia (alama 1)
      sana-kielezi cha namna halisi (alama 1)
    3. kiima-wanafunzi wote (alama 1)
      chagizo-kwa makini (alama 1)
    4. kishazi huru-Alimaliza vizuri. (alama 1)
      kishazi kitegemezi- ingawa hakuanza vizuri (alama 1)
  16.   
    S
    KN KT
    N S T H N V E
    Mkutano Utakaofanyika wiki ijayo utahudhuriwa na wanajopo wengi sana
  17.  
    1. shamirisho kipozi-uji mtamu (alama 1)
    2. shamirisho kitondo-babu yake (alama 1)
    3. shamirisho ala-kikombe (alama 1)
  18.  
    1. Tetu alikula kifisi (alama 1)
    2. Kisu ki mezani. (alama 1)
  19. Sentensi ya mtahiniwa idhihirishe moja kati ya matumizi haya: (alama 1)
    1. kuandika maneno kwa kifupi- S.L.P (sanduku la posta)
    2. kuandika tarehe- 30.6.2023
    3. kutenganisha shilingi na senti- 200.50 (shilingi mia mbili na senti hamsini)
    4. kuonyesha nambari za desimali

ISIMU JAMII (alama 10)

  1. Eleza kaida tatu za Lugha. (alama 3)
    1. Cheo cha mtu-Madaraka ya mtu huchangia msamiati wa kutumia.Waajiri hutumia lugha ya kuamuru ilhali waajiriwa hutumia Lugha ya upole na adabu
    2. Umri-Vijana wana namna ya kutumia lugha inayojihusisha na mitindo mipya tofauti na wazee wanaotumia msamiati wenye hekima na ushauri.
    3. Uhusiano-Kuna mahusiano ya aina nyingi kwa mfano mtoto atatumia lugha kwa njia tofauti katika kuwasiliana na wazazi wake tofauti na vile atazungumza na watoto wa rika lake.
    4. Hali ya mtu-Mgonjwa atazungumza kwa upole wakati Melvin atazungumza kiholela bila kuchagua maneno
    5. Utabaka-Watu wa tabaka la juu wanapenda kuchagua maneno ya kifahari ilhali watu wa tabaka la chini hutumia maneno ya kawaida.
    6. Mazingira-Lugha hutegemea mazingira ya wazungumzaji kama vile mahakamani,nyumbani,sokoni,kanisani na kadhalika
    7. Jinsia-Unyenyekevu hujitokeza katika mazungumzo ya wanawake na ambayo ni tofauti na ya wanaume. Lugha ya wanaume huwa na fujo,kiburi na hali ya kutojali sana. Wanawake watajikita katika mapambo ilhali wanaume watajikita katika siasa na kandanda
      zozote 3×1=3
  2. "Hapana ni kifaduro!"Alibisha mwingine...Maana nikasikia kupumua kunamtatiza... anapumua kama mgonjwa wa kifua.
    1. Tambua sajili ya makala haya na udhibitishe (alama 1)
      • Sajili ya hospitalini-kupumua kunamtatiza anapumua kama mgonjwa wa kifua
        (ataje na athibitishe 1×1=1)
    2. Tambua mbinu za kimtindo kifunguni (alama 3)
      • nidaa-"Hapana ni kifaduro!"
      • mdokezo- Alibisha mwingine...
      • tashbihi-anapumua kama mgonjwa wa kifua
        3×1=3
    3. Tambua sifa ambazo zingetumika kwenye sajili hii (alama 3)
      • Lugha ya kudadisi-Daktari anapouliza maswali
      • Lugha ya upole na unyenyekevu-Mgonjwa
      • Utohozi hutumika
      • Lugha yenye huzuni na hofu
      • Hutumia sentensi fupi fupi Kwa urahisi wa maelewano
        zozote 3×1=
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kassu Jet Joint Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?