KISWAHILI PAPER 2 - KCSE 2019 MOKASA PRE MOCK EXAMINATION

Share via Whatsapp
  1. UFAHAMU (Alama 15)

    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yanayofuata.

    Ustawi wa dola lolote lile hutegemea mseto wa nguvu, maarifa chipukizi, uchapuchapu wa barubaru, pamoja na maarifa, upevu, uvumilivu na tajriba ya wazee. Tunaweza kuumithilisha ufanisi wa nchi na jumba la ghorofa lililojengwa juu ya tegemezo: msingi huu ukiwa imara, ghorofa nyingi zaweza kuinuliwa. Nayo imara ya tegemezo hutegemea vyuma imara visivyotetereka na vifaa vinginevyo. Zaidi ya haya yote, mafundi wahusika kama vile wasanifu mjengo, wahandisi, mafundi bomba na wengineo sharti wawe na ujuzi tosha ili kufanikisha kazi inayohusika. Katika taswira hii, twaweza kuelewa ni kwa nini baadhi ya nchi zimestawi huku nyingine zikiitwa ulimwengu wa tatu. Shida za nchi hizo ni kutozistawisha taaluma ambazo ndizo msingi wa maendeleo, hivyo huwa na walakini katika utekelezaji. Matokeo yake ni kulimatia.               
                                                   
    Nchi nyingi humu barani mwetu zimekosa kustawi kutokana na kasoro nyingi tulizo nazo katika uimarishaji wa taaluma zetu. Sababu kuu ni kuwa, wengi wetu hukimbilia kutekeleza kazi mbalimbali hata bila ujuzi wowote kwa kazi hizo. Tabia kama hii inatokana na ukweli kuwa sisi hatujali kama tuna vipawa vya kufanya kazi fulani. Wengine huvunjwa moyo na waliowazingira kuwa vipawa vyao havifai. Hivyo, si ajabu kuona kijana aliye na kipawa fulani akikosa kukivuvia kwa sababu labda hata hatambui kuwa anacho. 
                                                    
    Wengi wa wakembe wetu hukosa kuvitambua vipawa vyao, hivyo kukosa kuendeleza utaalamu unaohusiana navyo kwa kukosekana kwa mtalaa wa kuvichochea katika mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu nchini Kenya kwa sasa unasisitiza wanafunzi kupita mtihani ili kuingia vyuoni. Hata hivyo, ni muhimu kuvikuza vipawa walivyo navyo vijana ili wavitumie katika siku za halafu. Vitambuliwe mapema shuleni bali si vyuoni. Kunao wanagenzi wengine ambao, licha ya kuvitambua vipawa vyao hawavifukutii kamwe, huvipuuza na kujisukuma katika taaluma ambazo hazikuwafaa kamwe. Kunao wanagenzi wengine ambao hutamani na kuingilia taaluma fulani, si kwa kuzipenda, bali kwa kuwa wandani wao wazishiriki. Hawajui kuwa kibaya chako si kizuri cha mwenzio. Huliona tanga la nguo wakalisahau la miyaa. Kuna wengine ambao huziandama taaluma fulani kwa kushurutishwa na wazazi au wadhamini wao. Nao vijana hukosa ukakamavu wa kujiamulia na kukubali shingo upande maamuzi hayo. Hata hivyo, kuna wale ambao hujitosa katika taaluma hizo bila kushurutishwa ili wapate hadhi. Matokeo ni kuwa kijana huzifanya kazi hizo kwa chati wala si kwa dhati. Wengine hujipenyeza kwa taaluma fulani eti kwa kuwa wamekosa nyingine. Si ajabu basi kutokana na ukosefu wa ajira kumwona mtaalamu wa mifugo akiwa mwalimu, mwalimu akiwa dereva na tabibu akiwa mkulima hali zaraa haimudu.       
                                                         
    Ili kupata suluhu katika jambo hili, sharti kila mmoja wetu ashiriki katika kuitambua, kuikuza, kuikomaza na kutumia taaluma ya kila kijana. Twaweza kuuiga mfano wa Wazungu wafanyavyo kwao. Wao hujitahidi kuvitambua vipawa vya watoto wangali wachanga hali ambayo huwasaidia kuzikuza taaluma zao baadaye. Naye kijana akishajua atakachofanya, afaa kufanya utafiti ili kufikia kina cha taaluma yake.

    Maswali
    1. Eleza sababu za watu kujishughulisha na taaluma zisizo zao.                             (alama 2)
    2. Eleza kikwazo cha ustawi wa nchi zinazoendelea.                                             (alama 1)
    3. Taja mambo manne yanayostawisha taifa.                                                          (alama 4)
    4. Taja mambo matano yanayokwamiza uendelezaji wa vipawa miongoni mwa vijana. (alama 5)
    5. Kuna tofauti gani kati ya Waafrika na Wazungu katika ukuzaji wa taaluma?      (alama 2)
    6. Eleza maana ya ‘Huliona tanga la nguo wakalisahau la miyaa’.                           (alama 1)
    7. Eleza maana ya vifungu vifuatavyo vilivyotumika katika ufahamu.                   (alama 2)
      1. kulimatia
      2. mtalaa
  1. MUHTASARI                                                                                                       (Alama 15)

    Tunapinga na kulaani vikali visa vya ugaidi vinavyoendelea kutetemesha usalama wa wananchi. Hivi ni vitendo vya kinyama vinavovyotekelezwa na watu waliokosa ubinadamu na utu kabisa. Inaghadhabisha kuona Wakenya wasio na makosa wakiteswa na kuuawa kinyama bila huruma na watu wasio na utu. Hatuogopi wala hatuna fedheha kuamba kuwa magaidi hawa wamelaaniwa na siku zao zimehesabiwa hapa duniani. Damu ya mwananchi asiye na makosa katu watailipia. Napinga vikali pale magaidi hawa wanapohusisha vitendo hivi kuwa vita vya kidini; vita hivi si vya kidini   kwani hakuna dini yoyote iliyo na imani ya kumuua kinyama binadamu asiye na makosa.

    Kando na tishio la ugaidi, Wakenya pia wanakabiliwa na hatari za ujambazi, mauaji, unajisi, ubakaji na maovu mengine. Katika juhudi za kudumisha usalama, polisi wana jukumu la kutumia kila mbinu kuhakikisha kuwa haki za kikatiba za Wakenya kuhusu kulindwa kwa maisha na mali yao zimedumishwa. Lakini cha kusikitisha ni kuwa, mbinu ambazo polisi wamekuwa wakitumia hasa ile ya kufanya misako inayoishia kuwanasa mamia ya raia wasio na habari kuhusu kinachoendelea, inawaongezea Wakenya mateso. Hali hii inawaacha kwenye hatari ya kunaswa na majambazi ama polisi.

    Matumizi ya mbinu hii ya misako yameishia kunasa raia wengi wasio na makosa.Wanaponaswa, hurundikwa kwenye seli usiku mzima ama siku kadha na hata kama wanaaachiliwa huwa tayari wameteseka. Huu ni ukiukaji wa haki za raia. Kadhalika, mbinu hii inaonekana kama hila ya polisi kutaka kuonyesha wanafanya kazi lakini sio mwafaka kwani wanapokuwa wakiwanasa raia mijini na mitaani, magaidi na majambazi wanaendelea na shughuli zao.

    Badala ya kusaka wakora kwa kubahatisha kwenye umati, polisi wanapaswa kubuni njia ambazo zitawapa mwelekeo mwafaka zaidi kuhusu wahalifu ili waweze kuwafuatilia. Ushirikiano baina yao na majasusi uwepo. Hii itawezesha polisi kupata habari muhimu kuhusu vitisho vya uhalifu. Maafisa wa usalama pia wanaweza kupata habari muhimu kutoka kwa raia.

    Maswali
    1. Ni nini maoni ya mwandishi kuhusu suala la ugaidi (alama 7,1 utiririko) (maneno 60-70)
    2. Kwa kutumia maneno yasiyozidi 50 fupisha aya mbili za mwisho. (alama 6, 1 utiririko)
  1. MATUMIZI YA LUGHA                                                                   (Alama 40)
    1.  
      1. Eleza jinsi kitamkwa /u/ kinavyozuiliwa                                                        (alama 2)
      2. Andika tofauti moja kati ya sauti hizi.                                                         (alama 1)
        /t/ na /d/
    2. Bainisha kiima na chagizo katika sentensi ifuatayo.                                        (alama 2)
      Mwanajamii yule alijibu maswali yote kwa makini.
    3.  
      1. Eleza maana ya vitenzi vishirikishi.                                                              (alama 1)
      2. Tunga sentensi moja moja kuonyesha aina mbili za vitenzi vishirikishi.   (alama 2)
    4. Yakinisha sentensi ifuatayo.                                                                             (alama 1)
      Mtoto hakufundishwa wala kupewa vitabu.  
    5.  
      1. Eleza maana ya silabi.                                                                                    (alama 1)
      2. Huku ukitoa mifano, eleza miundo miwili ya silabi za Kiswahili.           (alama 2)
    6. Ainisha viambishi katika sentensi hii kimuundo na kidhamira.                          (alama 3)
      Wataonana
      1. Kimuundo:
      2. Kidhamira          
    7. Tumia nomino yoyote katika ngeli ya KU-KU pamoja na kiashiria kisisitizi cha karibu kutunga sentensi.  (alama 1)
    8. Tunga sentensi moja katika wakati uliopita hali isiyodhihirika                            (alama 1)
    9. Tunga sentensi mbili ili kubainisha maana za neno: Jinsi                                     (alama 2)
    10. Huku ukitoa mifano, eleza matumizi mawili ya alama ya kinyota katika uakifishaji.    (alama 2)
    11. Eleza miundo mitatu ya vishazi tegemezi na kuitolea mifano mwafaka katika sentensi.                         (alama 3)
    12.  
      1. Eleza maana ya shamirisho kipozi.                                                                       (alama1)                                
      2. Benta alimlimia mamake shamba kwa trekta. Anza kwa yambiwa                       (alama1)
    13.  
      1. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao.
        S – KN (N/Wθ) + KT (Ts+T+RH+E)                                                                   (alama 2)
      2. Changanua kwa matawi sentensi ifuatayo:                                                           (alama 2)
        Kile chake kipya kinanipendeza mno.
    14. Eleza matumizi yoyote mawili ya kiambishi KU na kuyatolea mfano mmoja mmoja wa sentensi.      (alama 2)
    15. Tunga sentensi sahihi ukitumia kivumishi cha ki ya mfanano na kielezi cha namna kitumizi.                       (alama 2)
    16. Tunga sentensi ukitumia kitenzi cha silabi moja kinachomaanisha kuogopa katika kauli ya kutendeka.             (alama 2)
    17. Eleza maana ya:
      1. Papo kwa papo kamba hukata jiwe.                                                            (alama 1)
      2. Ua langu la waridi limechanuka.                                                                   (alama 1)
    18.  
      1. Tunasema baraza la wazee …………………cha kuni na ……………..…… ya nguo                                 (alama 1)
      2. Ajuza ni kwa mwanamke mzee na …………………ni kwa msichana mchanga ilhali shaibu ni kwa mwanamume mzee na ………………………ni kwa mvulana aliyebaleghe.   (alama 1)
  1. ISIMUJAMII (Alama10)
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.

    Niaje wasee! Midterm ilibamba lakini ilkua fupi sana, tumerudi books, huu ni mwaka wa mwisho tujikaze jo. Msifikirie hizo hepi zetu ni reality, kuchill ni jambo la maana jo! ama niaje bro…hustle ni real, bidii ndio itatuokoa
    1. Tambua sajili inayohusishwa na kifungu hiki                                                   (alama2)
    2. Eleza sifa zozote nne za kimtindo zinazojitokeza katika kifungu hiki.         (alama 4)
    3. Eleza sababu nne zinazosababisha matumizi ya lugha ya aina hii.              (alama 4)


MARKING SCHEME

  1. UFAHAMU (Alama 15)
    1. Eleza sababu za watu kujishughulisha na taaluma zisizo zao.             (alama 2)
      Kutojali kuwa wana vipawa vya kufanya kazi fulani.
      Kuvunja moyo na waliowazingira kuwa vipawa vyao havifai. (2×1=2)
    2. Eleza kikwazo cha ustawi wan chi zinazoendelea.                                 (alama 1)
      Kutozistawisha taaluma ambazo ndizo msingi wa maendeleo.
    3. Taja mambo matatu yanayostawisha taifa.                                              (alama 3)
      Maarifa chipukizi
      Uchapuchapu wa barubaru
      Maarifa         
      Uvumilivu
      Tajriba ya wazee                                                                 (Tatu za 3×1=3
    4. Taja mambo manne yanayokwamiza uendelezaji wa vipawa miongoni mwa vijana.                                                                                      (alama 4)
      Kukosekana kwa mtalaa wa kuvichochea
      Kuvipuuza na kujisukuma katika taaluma ambazo hazikuwafaa kamwe.
      Kuingilia taaluma fulani kwa sababu wandani wao wanashiriki.
      Kushurutishwa na wazazi wao.
      Kuingilia taaluma fulani kwa lengo la kupata hadhi.
      Kukosa taaluma nyingine.                 (Nne za kwanza 4×1=4)
    5. Kuna tofauti kati ya Waafrika na Wazungu katika ukuzaji wa taaluma? (alama 2)
      Wazungu hujitahidi kuvitambua vya watoto wangali wachanga hali hii ni kinyume Afrika. (2/0)
    6. Eleza maana ya ‘Huliona tanga la nguo wakasahau la miyaa’.               (alama 1)
      Hukimbilia taaluma za kifahariili kupata hadhi na kusahau taaluma za kimsingi zinazoafikiana na vipawa vyao.
    7. Eleza maana ya vifungu vifuatavyo vilivyotumika katika ufahamu.     (alama 2)
      1. kulimatia- kubaki nyuma/kuchelewa/kutaahiri.
      2. mtalaa –mpango wa utaratibu wa masomo                         (2×1=2)
  1. UFUPISHO                                                                                                  (Alama 15)
    1. Ni nini maoni ya mwandishi kuhusu suala la ugaidi? (alama 7, 1 utiririko)
      • Tunapinga na kulaani visa vya ugaidi
      • Ugaidi ni kitendo cha kinyama kinachotekelezwa na watu waliokosa ubinadamu.
      • Ugaidi hauna uhusiano na dini yoyote.
      • Polisi wanzembea katika kuzuia matendo ya kigaidi.
      • Polisi wabuni njia mbadala ya kukabiliana na ugaidi badala ya kunasa raia waio na hatia.
      • Wakenya wasio na makosa huteswa na kuuawa kinyama.
      • Magaidi watalipia matendo yao.
      • Wakenya wana haki ya kulindwa.
        (Hoja zozote 7×1=7, alama 1 ya utiririko)
    2. Kwa kutumia yasiyozidi 50, fupisha aya mbili za mwisho. (alama 6,1 ya utiririko)
      • Raia wasio na hatia hunaswa.
      • Hurundikwa kwenye seli na kuachiliwa huru kama wameteseka.
      • Huu ni ukiukaji wa haki za binadamu.
      • Hii ni hila ya polisi kujionyesha kuwa wanafanya kazi.
      • Magaidi huendeleza shughuli zao.
      • Polisi wanapaswa kubuni njia zitakazowapa mwelekeo mwafaka kuhusu wahalifu.
      • Ushirikiano baina yao na majasusi uwepo.
      • Maafisa wa usalama kupata habari muhimu kutoka kwa raia.
        (Hoja zozote 6×1=6, alama 1 ya utiririko)          
        Ondoa ½ alama kwa kila kosa la sarufi hadi makosa sita kila litokeapo kwa mara ya kwanza.
        Ondoa ½ alama kwa kila kosa la hijai hadi makosa sita kila litokeapo kwa mara ya kwanza.
  1. MATUMIZI YA LUGHA                                                                           (Alama 40)
    1.  
      1. Eleza jinsi kitamkwa /u/ kinavyozuliwa                                                        (alama 2)
        Ulimi huinuliwa juu huku ukijipinda nyuma
        Hutamkwa midomo ikiwa imeviringwa.         (2×1=2)
      2. Andika tofauti moja kati ya sauti hizi.                                                        (alama 1)
        /t/ na /d/                      
        /t/ ni sauti hafifu/sighuna na /d/ ni sauti ghuna         (alama 1/0)
      3. Bainisha kiima na chagizo katika sentensi ifuatayo.                                        (alama 2)
        Mwanajamii yule alijibu maswali yote kwa makini
        Kiima: mwanafunzi (yule), CH – kwa makini.   (2×1=2)
    2.  
      1. Eleza maana ya vitenzi vishirikishi.                                                              (alama 1)
        Vitenzi vinavyoonyesha tabia/ hali fulani iliyopo au isiyokuwepo kwa mtu/kitu.
        Hushirikisha vitu mbalimbali kihali, kitabia na kimazingira.   (1×1=1)
      2. Tunga sentensi moja moja kuonyesha aina mbili za vitenzi vishirikishi.   (alama 2)
        Yakinisha sentensi ifuatayo.                                                                              (alama 1)
        Mtoto hakufundishwa wala kupewa vitabu.   (2/0)
        Mtoto alifundishwa na akapewa vitabu.
    3.  Eleza maana ya silabi.                                                                                    (alama 2)
      Kipashio kinachotamkwa kwa pamoja kama fungu moja.
      Muungano wa sauti unaotamkwa kwa mpigo mmoja.
      Sehemu ya neno moja inayotamkika/ tamko moja katika neno.
      Pigo katika neno.     (2/0)
    4. Huku ukitoa mifano, eleza miundo miwili ya silabi za Kiswahili. (alama 2)
      I - oa
      K - mtu
      KI - bata
      KIK - daftari
      KKI - ndege
      KKKI - mbweha
      IK – alfajiri                                                                  (2×1=2)
    5. Ainisha viambishi katika sentensi hii kimuundo na kidhamira.      (alama 3)
      Wataonana
      1. Kimuundo: viambishi awali – wa-ta
        Viambishi tamati an-a     (2× ½ =1)
      2. Kidhamira
        wa- nafsi/ngeli
        ta- wakati/njeo
        an – kauli ya kutendana
        a –kauli ya kutenda                           (4× ½ =2)
    6. Tumia nomino yoyote katika ngeli ya KU-KU pamoja na kiashiria kisisitizi cha karibu kutunga sentensi.                                                                                                 (alama 1)
      k.m: Kuandika kuku huku kunapendeza sana. (upatanisho uwepo)   .     (1/0)
    7. Tunga sentensi moja katika wakati uliopita hali isiyodhihirika                             (alama 1)
      k.m: Maisha yalikuwa yamwendea vyema.   (1×1=2)
    8. Tunga sentensi mbili ili kubainisha maana za neno: Jinsi                                    (alama 2)
      Njia ya kutekeleza jambo. K.m: Nionyeshe jinsi ya kupika chai.
      Mwendo . k.m: Alishangiliwa kutokana na jinsi alivyocheza mpira.
      K.m: Watu wa namna/jinsi hii wanahitajika kufungwa.     (2×1=2)
    9. Huku ukitoa mifano, eleza matumizi ya alama ifuatayo ya uakifishaji. *
      Kuonyesha maendelezo mabaya. K.m:* Rara hapa.
      Kuonyesha ufafanuzi zaidi umetolewa chini. Km: uhandisi ni muhimu*
      Kusisitiza/ uzingativu wa jambo.                               (2×1=2)
    10. Eleza miundo mitatu ya vishazi tegemezi na kuitolea mifano mwafaka katika sentensi. (alama 3)

      Vinavyohusisha ‘O’ rejeshi
      Kilichopotea ni kile.
      Vinavyohusishwa kirejeshi amba-
      Mwanafunzi ambaye alisajiliwa amewasili.
      Vinavyohusisha ki ya masharti
      Ukinitembelea nitakutuza.
      Vinavyotokana na hali ya nge, ngali/ ngeli
      Ungesoma kwa bidii ungepita mtihani.
      Vinavyotokana na sentensi zinazoanza kwa viunganishi.
      Ingawa tulimpenda sana, Mola alimpenda zaidi.
      Vinavyohusisha hali ya Po
      Nivuapo au Ninapovua samaki wengi hutuzwa.
      (4×1=4) Ataje muundo na kueleza
    11.  
      1. Eleza maana ya shamirisho kipozi.                 (alama 1)                      
        Ni nomino inayotendwa.                                                                                                    
        Nomino inayopokea athari ya moja kwa moja kutoka kwa kitendo
      2. Benta alimlimia mamake shamba kwa trekta. Anza kwa yambiwa                       (alama1)
        Mamake alilimiwa shamba na Benta kwa trekta
    12.  
      1. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao.
        S – KN (N/Wθ) + KT(Ts+T+RH+E)                                                                   (alama 2)
        Atakuwa akitembea kando ya barabara jioni
        (Kadiria majibu mengine)     (2/0)
    13. Changanua kwa matawi sentensi ifuatayo:                                                          (alama 2)
      Kile chake kipya kinanipendeza mno.
    14. Eleza matumizi yoyote mawili ya kiambishi KU na kuyatolea mfano mmoja mmoja wa sentensi.                       (alama 2)
      Hutumiwa kama kiambishi cha awali cha vitenzi-jina.
      Kucheza kwa gwiji yule kulinivutia.}Hutumiwa kuonyesha shamirisho/ yambwa/ mtendewa.

      Mtendwa wa nafsi ya pili
      Alikupiga jana Au Walikupigia.

      Kiambishi cha mahali kusikodhihirika/ kwa jumla.
      Huku ndiko kule anakoishi.

      Kiambishi cha kuonyesha ukanushaji wa wakati uliopita,
      Hakufika jana alivyotarajiwa.

      Huambishwa kwenye vitenzi vya silabi moja katika kauli ya kutenda.
      Alikuja jana.

      Huambishwa mwanzoni mwa vitenzi vikuu katika sentensi yenye vitenzi sambamba.
      Yesu alikuja kutuokoa.
      (zozote tatu 3×1=3)
    15. Tunga sentensi sahihi ukitumia kivumishi cha ki ya mfanano na kielezi cha namna kitumizi.                   (alama 2)
      Nguo za kifalme hazivaliwi na watu wanaotembea kwa miguu.
      (kadiria majibu mengine) alama 2/0
    16. Tunga sentensi ukitumia kitenzi cha silabi moja kinachomaanisha kuogopa katika kauli ya kutendeka.           (alama 2)
      Mungu huchika katika maeneo mengi barani Afrika.                         Alama 1/0
    17. Eleza maana ya:
      1. Papo kwa papo kamba hukata jiwe.                                                             (alama 1)
        Ukifanya bidii, hata jambo liwe na changamoto zipi, hatimaye hutimilika. (1/0)
      2. Ua langu la waridi limechanuka.                                                            (alama 1)
        Mpenzi wangu amefurahi.                     (1/0)
    18.  
      1. Tunasema baraza la wazee ……………………… cha kuni na ………… ya nguo                            (alama 1)
        Kitita cha kuni
        Bahasha ya nguo   (2× ½ =1)
      2. Ajuza ni kwa mwanamke mzee na ………………ni kwa msichana mchanga ilhali shaibu ni kwa mwanamume mzee na ………ni kwa mvulana aliyebaleghe.       (alama 1)
        Kigoli/kigori kwa msichana (alama ½)
        Ghulamu/barobaro/rijali/shababi kwa mvulana aliyebaleghe. (alama ½)
  1. ISIMUJAMII (Alama10)
    Soma makala yafuatayo kasha ujibu maswali.

    Niaje wasee! Midterm ilibamba lakini ilkua fupi sana, tumerudi books, huu ni mwaka wa mwisho tujikaze jo. Msifikirie hizo hepi zetu ni reality, kuchill ni jambo la maana jo! ama niaje bro…hustle ni real, bidii ndio itatuokoa
    1. Tambua sajili inayohusishwa na kifungu hiki                                                (alama2)
      Sajili ya mtaani / Lugha ya vijana
    2. Eleza sifa zozote nne za kimtindo zinazojitokeza katika kifungu hiki.           (alama4)
      Matumizi ya takriri k.m jo                                                                                                                           
      Sentensi fupifupi k.m niaje wasee                                                                                                     
      Lugha hisishi k.m niaje wasee!                                                                                                       
      Kuchanganya msimbo k.m hizo hepi zetu ni reality
    3. Eleza sababu nne zinazosababisha matumizi ya lugha ya aina hii.                 (alama4)
      Ukosefu wa msamiati tosha                                                                                                   
      kuipa lugha ladha                                                                                                                     
      Kukubalika katika kikundi Fulani                                                                                         
      Kudumisha usiri / kuficha ujumbe Fulani
      Kufahamu lugha zaidi ya moja
Join our whatsapp group for latest updates

Download KISWAHILI PAPER 2 - KCSE 2019 MOKASA PRE MOCK EXAMINATION.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest