Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kangundo Subcounty Pre Mock Exams 2021/2022

Share via Whatsapp

MAAGIZO

  1. Jibu maswali yote
  2. Majibu yote yaandikwe katika nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali
  3. Majibu yote yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili

Kwa matumizi ya mtahini pekee

  1. UFAHAMU (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali
    Vijana waliombeba Naeku juu juu walipoingia uani mwa Mzee Laboyo walilakiwa kwa shangwe na vigelegele vilivyotoka vinywani mwa wanawake wachache waliokuwa pale. Bila shaka walialikwa makusudi ili kumlaki Naeku. Vijana hao walimteremsha Naeku ambaye alisesereka kutokana na uchovu mwingi. Ufyefye ulimvaa akajihisi kuwa mfungwa asiye na hatia. Huku michirizi ya machozi ikiwa ingali inabubujika toka machoni, wanawake hao walimwinua juu juu. Vicheko vya kusudi vilivyoandamana na riboribo za arusi vilipamba maskani ya Mzee Laboyo. Walimwingiza katika kijumba kilichokuwa mkabala na kasri la shaibu huyo na kushindika mlango.
    Kijumba kile hakikuwa na vitu vya haja. Mlikuwa na viti viwili vidogo, kitanda kimoja cha msonobari kilichotandikwa maridadi kabisa. Mito minne ya rangi ya hudhurungi ilitulia juu ya kitanda hicho kilichofarishiwa matandiko ya mahameli. Katikati ya chumba hicho, kulikuwa na kijimeza cha mviringo kilichotandikwa kitambaa cheupe. Juu yake kulikuwa na bilauri pamoja na chupa iliyojaa maji.
    Naeku aliketishwa kitandani baada ya kupakwa mafuta, huku akiwa bado anapigana nao ili kujiopoa. Kisha wanawake hao walitoka wakaukomelea mlango kwa nje, na kumwacha Naeku peke yake mle ndani.
    Naeku aliacha kulia na kuvuta fikra ili ajue namna ya kupatoroka mahali pale. Hapa ndipo picha za matukio yaliyoandama kutoroshwa kwake zilipomjia akilini. Naam, sasa alielewa fika kwa nini wazee fulani walikuwa wakija nyumbani kwao mara kwa mara, kuongea na wazazi wake. Alielewa kwa nini ng’ombe na mbuzi walikuwa wakiletwa kwao jioni jioni na watu asiowafahamu.
    Kila alipomuuliza mamake kuhusu mifugo hao, mama mtu alimjulisha kuwa waliletwa hapo kwa muda tu ili mwenyewe apate nafasi ya kujenga zizi kubwa zaidi la kuwasitiri. Naeku alipovuta fikra zaidi, lilimjia wazo jingine lililomshtua zaidi. Awali alimsikia mmoja wa wale vijana akitaja jina “shaibu”. Mamangu eee! Alikuwa ameletwa kuwa mke wa Mzee Laboyo mwenyewe!
    “Mimi niolewe na kikaramba yule! Labda niwe maiti,” Naeku alijisemea moyoni, “ Lazima nijinusuru kabla Mzee yule kuniharibia maisha,” aliwaza.
    Aliangaza angaza macho mle ndani na kuliona dirisha dogo lililofungwa kwa ndani. Hata hivyo, dirisha hili lilijengwa juu sana kiasi cha kwamba hata kama angekanyaga kiti ili kulifikia, ingekuwa kazi ya bure.
    Huko nje, aliwasikia watu wakijishughulisha na kadhia za jioni. Giza lilikuwa linanyemelea taratibu, na hivi punde kijiji chote kingezama gizani. Alimsikia mkewe Laboyo, Bi Mariamu, akiwabembeleza ng’ombe wake kuingia zizini, huku Hamadi akipiga miluzi ili kuwahimiza zaidi, Hadi kufikia wakati huu, hajamsikia wala kumwona Mzee Laboyo mwenyewe.
    Alipokuwa akiwazia la kufanya, mlango ulifunguliwa taratibu, akaingia mzee mfupi, mnene, menye ndevu nyeupe mithili ya theluji. Mara moja, Naeku alimtambua kuwa ndiye Mzee Laboyo mwenyewe, kwani alishapata kumwona mahali mara kadha. Shaibu huyu alimtupia Naeku macho huku tabasamu limepamba usoni.
    “Hujambo mpenzi?” Mzee Laboyo alimsalimu huku akimsogelea.
    Naeku alisimama ghafla na kumkabili, macho yakiwa yameiva kwa hasira.
    “Sina jambo nikiwa nalo n’takwambia,” alipasuka.
    “Aaah, wacha hasira kinda wangu, karibu nyu…” Lakini kabla Mzee huyo hajamaliza alilotaka kusema, Naeku alidakia, “Niondokee mie! Tangu lini jizee kama wewe umri wa babu yangu ukawa mpenzi wangu? Ulidhani ulipopeleka zizi zima la mifugo kwetu na kuwamwagia wazazi wangu mapesa chekwachekwa, ungenifanya nikupende? Nakwambia umekula huu babu, hunipati leo wala kesho!”
    Maneno ya Naeku yalimchoma Mzee Laboyo ambaye hakuzoea kujibiwa vile na mwanamke. Hasira zilianza kumnyemelea, zikapanda na kumsakama koo. Alifunua kinywa ili kutamka, lakini katu maneno hayakumtoka. Baada ya kupumua kwa nguvu aligugumia, “Ni………….nisubiri kidogo mpenzi………..naja hivi punde,,,,,,,tuyamalize usemayo.” Kisha alichomoka mbio na kuufunga mlango kwa nje.
    “Mawe! Labda tuyamalize nikiwa maiti! Katili mkubwa we!”
    Aliinuka pale alipoka na kuliendea lile dirisha. Aliliangalia kwa muda kisha akapanda juu ya kiti ili ajaribu kulifungua. Hakuweza kulifikia komeo ili afungue dirisha hilo.
    “Lazima nitoke humu kabla jizee lile kuingia humu tena,” alijipa moyo.
    Maswali
    1. Eleza namna mwanamke amenyanyaswa kwa mujibu wa kifungu hiki . (ala 4)
      …………………………………………………………………………………………….
    2. Naeku alipinga mila dhalimu katika jamii yake. Thibitisha kwa kurejelea kifungu hiki. (ala 3)
      ……………………………………………………………………………………………..
    3. “Hujambo mpenzi?” Eleza kinaya katika maneno haya kulingana na kifungu hiki. (ala 2)
      …………………………………………………………………………………………….
    4. Eleza taasubi ya kiume inayojitokeza katika aya ya kumi. (ala 2)
      …………………………………………………………………………………………….
    5. Vijana wanachangia kuendeleza desturi zilizopitwa na wakati. Eleza kwa kurejelea kifungu. (ala 1)
      …………………………………………………………………………………………….
    6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumika katika kifungu. (ala 3)
      1. alisesereka - ________________________________________________
      2. kuvuta fikra ________________________________________________
      3. nijinusuru __________________________________________________
  2. UFUPISHO (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali
    Miswada kadhaa imepitishwa ili kufanyia mageuzi sekta ya kilimo na kuboresha maslahi ya wakulima ambao wamehangaika kwa miaka mingi Waunda sheria wamejitokeza kuwatetea wakulima dhidi ya ushindani usio wa haki kutokana na wingi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa ya kigeni ambazo huuzwa kwa bei duni. Mabadiliko hayo yatafaidi maelfu ya wakulima ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilia kuhusu hasara wanayopata kutokana na kufurika kwa bidhaa kutoka nchi za kigeni, zinazouzwa kwa bei ya chini.
    Kuanzia samaki, mayai, sukari, vitunguu na kadhalika, masoko na maduka ya jumla nchini yamekuwa yakijazwa bidhaa zinazoagiziwa kutoka mataifa jirani na kuwaacha wakulima nchini wakiwa hoi. Uimarishaji wa kilimo utachangia kuunda nafasi za ajira na kuimarisha viwanda jambo litakalowafaa maelfu ya vijana ambao wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa ajira.
    Hii ni hatua muhimu ikizingatiwa ni mojawapo wa Ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru Kenyatta, kuhusu uongezaji thamani kwa bidhaa za kilimo. Japo juhudi hizo zinapaswa kupongezwa kwa kupatia kipaumbele maslahi ya raia, si jambo la kushangaza kwamba wabunge na wanasiasa wanaonekana ghafla kuanza kupatia kipaumbele maslahi ya raia.
    Hii ni kwa kuzingatia kuwa msimu wa kampeni unakaribia kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa 2022. Katika juhudi za kutaka kuvutia wapiga kura ili wapate kuchaguliwa tena, wanasiasa hujitahidi kwa kila hali ikiwemo kuungana na kupitisha sheria ambazo huwafaidi wananchi na wakati mwingine kuwaathiri.
    Hata hivyo, maamuzi hayo yanapofanywa kiholela kwa minajili tu ya kuvutia wapiga kura, baadhi ya sheria hizo huishia kuwaumiza wateja na uchumi na wananchi kwa jumla. Mfano mzuri ni kuhusu mswada wa Fedha 2021 ambao unahusu masuala mengi ya mwananchi wa kawaida kuanzia bidhaa kama vile pikipiki na shughuli za kilimo.
    Kwa kuidhinisha sheria kuhusu kutozwa ushuru wa asilimia 16 wa VAT ikiwemo ada nyinginezo dhidi ya bidhaa za kigeni zinazoagizwa nchini, ni wazi kwamba bei ya bidhaa hizo itapanda na raia wengi hawataweza kumudu.
    Isitoshe, hatua ya kuzuia ushindani kwa kufungia nje bidhaa za kigeni, pana tishio la wakulima na wenye viwanda nchini kulegeza kamba kuhusu viwango vya ubora na kuzalisha bidhaa duni. Hii ni kwa sababu wana hakika ya kupata soko bidhaa zao ziwe bora au vinginevyo hivyo, baadhi hawatajishughulisha mno na mwishowe, ni wateja tu watakaoumia kwa kukosa bidhaa bora. Ingawa juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo zinafanywa kwa nia njema, ni sharti kuwe na tahadhari zisije zikaleta madhara zaidi kuliko manufaa.
    1. Kwa maneno 85-90 fupisha aya ya kwanza tatu. (alama 7, 1, ya mtiririko).
      Nakala ghafi
      …………………………………………………………………………………………….
      …………………………………………………………………………………………….
      …………………………………………………………………………………………….
      Nakala safi
      …………………………………………………………………………………………….
      …………………………………………………………………………………………….
      …………………………………………………………………………………………….
    2. Eleza mambo muhimu yanayoibuka katika aya nne za mwisho. (maneno 90-95) (ala 6, 1 ya mtiririko)
      Nakala ghafi
      …………………………………………………………………………………………….
      …………………………………………………………………………………………….
      Nakala safi
  3. MATUMIZI YA LUGHA (alama 40)
    1.    
      1. Eleza maana ya sauti mwambatano. (ala 1)
        …………………………………………………………………………………………….
      2. Toa mfano wa sauti mwambatano inayotamkiwa midomoni. (ala 1)
        …………………………………………………………………………………………….
    2.    
      1. Andika neno lenye muundo ufuatao wa silabi. (ala 1)
        I + KKI + I
        …………………………………………………………………………………………….
      2. Andika neno lenye sauti zifuatazo:
        Voweli ya nyuma wastani, kikwamizo ghuna cha ufizi na voweli ya chini wastani. (ala 1)
        …………………………………………………………………………………………….
      3. Eleza tofauti kati ya sauti /t/ na /d/. (ala 1)
        …………………………………………………………………………………………….
    3. Andika upya kwa kufuata maagizo.
      1. Nyanya alijengewa nyumba maridadi na mjukuu wake. (Anza kwa kiima) (ala 2)
        …………………………………………………………………………………………….
      2. Tutamlipia mtoto ada kwa hundi. (Ainisha shamirisho) (ala 3)
        …………………………………………………………………………………………….
      3. Maji hayo yalinywewa na ngo’mbe wake. Andika katika hali ya kutenda) (ala 2)
        …………………………………………………………………………………………….
    4. Eleza matumizi mawili ya kila kiakifishi . (ala 4)
      1. kibainishi
        …………………………………………………………………………………………….
      2. mkwaju
        …………………………………………………………………………………………….
    5. Ainisha viambishi katika neno hili. (ala 2)
      1. mkobani
        …………………………………………………………………………………………….
    6. Andika katika ukubwa wingi. (ala 2)
      Kitanda hicho kilitumiwa na mtoto wake.
      …………………………………………………………………………………………….
    7. Eleza matumizi ya ji katika sentensi hii. (ala 2)
      Kijitoto hicho kilijing’oa mwiba chenyewe.
      …………………………………………………………………………………………….
    8. Bainisha vivumishi. (ala 2)
      Mwalimu mkulima alivuna maembe mengi.
      …………………………………………………………………………………………….
    9. Tunga sentensi kudhihirisha upatanisho wa ngeli wa nomino kukimbia. (ala 1)
      …………………………………………………………………………………………….
    10. Changanua sentensi kwa mtindo wa mchoro matawi. (ala 3)
      Walishangiliwa walipowasili.
      …………………………………………………………………………………………….
    11. Eleza matumizi ya na. (ala 2)
      Mama na mtoto wake walilakiwa na naibu wa rais.
      …………………………………………………………………………………………….
    12. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao wa KN na KT. (ala 2)
      KN(W) + KT(t + N)
      …………………………………………………………………………………………….
    13. Unda nomino mbili kutokana na kitenzi nena. (ala 1)
      …………………………………………………………………………………………….
    14. Jifya ni kwa figa, injika ni kwa __________________________________ na manati ni
      kwa _________________________________ (ala 2)
    15. Eleza maana ya msemo mkono wa birika. (ala 1)
    16. Ainisha vishazi katika sentensi hii. (ala 2)
      Meza aliyonunua ni maridadi sana.
      …………………………………………………………………………………………….
    17. Andika katika usemi wa taarifa. (ala 2)
      “Kula tunda hili ulimalize,” Amina alimwambia nyanya.
      …………………………………………………………………………………………….
  4. ISIMU JAMII (ala 10)
    “Chenga chenga, chenga tena, aaaa baas! Goal! Habari ndio hiyo ndugu yangu!
    1. Tambua sajili hii. (ala 2)
      …………………………………………………………………………………………….
    2. Huku ukitoa mifano, eleza sifa bainifu za sajili uliyotaja hapo juu. (ala 8)
      …………………………………………………………………………………………….


MWONGOZO WA KUSAHIHISHA

  1. UFAHAMU
    1.    
      1. Naeku anaozwa kwa mzee Laboyo ambaye ni mzee sana.
      2. Naeku anaozwa kwa lazima bila hiari yake.
      3. Naeku anadhalilishwa kwa kubebwa na vijana juu juu bila heshima yoyote.
      4. Naeku anafungiwa chumbani kwa nje kama mfungwa.
        4 x 1 = 4
    2.    
      1. Naeku anamkabili mzee Laboyo na kumkemea.
      2. Naeku anajaribu/anapanga namna atatoroka ili asiozwe kwa mzee Laboyo.
      3. Naeku anakataa kuozwa.
        3 x 1 = 3
    3. Mzee Laboyo anamwita Naeku mpenzi ilhali Naeku hamtaki ,hamjui na
      analazimishwa kuwa mke wake.
      1 x 2 = 2
    4.      
      1. Mzee Laboyo anakasirika anapozomewa na Naeku kwa sababu hakuzoea kujibiwa
        vile na mwanamke.
      2. Mzee Laboyo anatoka nje baada ya kujibiwa na Naeku.
        2 x 1 = 2
    5. Vijana walimbeba Naeku juu juu bila hiari yake na kumpeleka kwa mzee Laboyo ili
      akaozwe bila hiari yake.
      1 x 1 = 1
    6.    
      1. alisesereka - alipepesuka/alisesetuka/aliwayawaya. 1 x 1 = 1
      2. kuvuta fikira - kufikiria. 1 x 1 = 1
      3. nijinusuru - nujiokoe. 1 x 1 = 1
  2. UFUPISHO
    1.    
      1. Miswada imepitishwa ili kufanyia mageuzi kilimo na kuboresha maslahi ya Wakulima.
      2. Waunda sheria wanatetea wakulima dhidi ya ushindani wa bidhaa zinazoagizwa nje na huuzwa kwa bei duni.
      3. Mabadiliko yatawafaidi wanaolilia hasara wanayopata kwa kufurika kwa bidhaa zinazouzwa kwa bei ya chini.
      4. Masoko yamejazwa bidhaa za nje na kuwaacha wakulima wakiwa hoi.
      5. Uimarishaji utaunda nafasi za ajira na kuimarisha viwanda na kuwafaa vijana.
      6. Hii ni mojawapo ya ajenda nne kuu kuhusu uongezaji wa thamani kwa bidhaa za kilimo.
      7. Juhudi hizi zafaa kupongezwa.
      8. Hata hivyo si jambo la kushangazwa kwamba wabunge wanaonekana ghafla kuanza kupatia kipaumblele maslahi ya raia.
        7 x 1 = 7
    2.    
      1. Msimu wa kampeni unakaribia kuhusiana na uchaguzi mkuu wa 2022.
      2. Ili kuvutia wapiga kura, wanasiasa hupitisha sheria zinazowafaidi wananchi.
      3. Maamuzi yanapofanywa kiholela sheria huwaumiza wateja na uchumi.
      4. Kwa kuidhinisha sheria kuhusu kutozwa ushuru wa asilimia 16 wa V.A.T bei ya bidhaa itapanda na raia hawatamudu.
      5. Kuzuia ushindani kwa kufungia bidhaa za kigeni, wakulima na wenye viwanda watalegeza kamba kuhusu ubora na kuzalisha bidhaa duni.
      6. Wana hakika ya kupata soko.
      7. Hawatajishughulisha na wateja watakosa bidhaa bora.
      8. Juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo zinafanywa kwa nia njema lakini sharti kuwa na tahadhari zisilete madhara.
        6 x 1 = 6
        1
  3. SARUFI
    1.    
      1. Sauti mwambatano ni sauti zinazoundwa kwa konsonanti mbili au zaidi na kutam kwa kama sauti moja.
        1 x 1 = 1
      2. /mb/pw/mw/mbw/. 1 x 1 = 1
    2.    
      1. ingia/ondoa/ongea/endea/angua/ongoa/imbia/. 1 x 1 = 1
      2. oza. 1 x 1 = 1
      3. /t/ ni hafifu/sighuma ilhali /d/ ni ghuna/ nzito. 1 x 1 = 1
    3.    
      1. Mjukuu alimjengea nyanya nyumba maridadi. 1 x 2 = 2
      2. ada – kipozi. 3 x 1 - 3
        mtoto – kitondo
        hundi – ala.
      3. Ng’ombe wake aliyanywa maji hayo. 1 x 2 = 2
    4. Kibainishi
      1. Kuandika sauti ya king’ong’o.
      2. Kuonyesha sauti au nambari iliyodondoshwa.
      3. Kuonyesha shadda. 2 x 1 = 2
        Mkwaju
        1. Kuonyesha maneno yenye maana sawa.
        2. Kuleta dhana ya ama /au/.
        3. Kuandika tarehe.
        4. Kuandika nambari ya kumbukumbu.
        5. Kuandika anwani ya tovuti. 2 x 1 = 2
    5. M – awali
      Ni- tamati 2 x 1 = 2
    6. Matanda/majitanda hayo yalitumiwa na matoto/majitoto yao/yake.
      1 x 2 = 2
    7. Kijitoto
      Kuonyesha udogo/dharau/kudunisha. 1 x 1 = 2
      Kilijing’oa
      Kuonyesha kirejeshi cha mtenda/kujirejelea. 1 x 1 = 2
    8. mkulima - kivumishi cha nomino.
      mengi – kivumishi cha idadi. 2 x 1 = 2
    9. Kukimbia – ngeli ni ku-ku-liwe mwanzoni mwa sentensi. 1 x 1 = 1
    10. 2.png
          Walishangiliwa walipowasili 6 x ½ = 3
    11. Mama na mtoto – kiunganishi. 1 x 1 = 1
      na naibu - kihusishi/kihusishi cha mtenda. 1 x 1 = 1
    12. Yeye ni daktari/yeye alikuwa mwalimu. 1 x 2 = 2
    13. nena – neno/uneni/mneni/unenaji/kunena. 2 x ½ =1
    14. injika ni kwa teleka.
      manati ni kwa panda/fyata.
    15. mchoyo 1 x 1 = 1
    16. Meza aliyonunua - kishazi tegemezi.
      ni maridadi sana - kishazi huru. 2 x 1 = 2
    17. Amina alimwambia nyanya ale tunda hilo alimalize. 4 x ½ = 2
  4.      
    1. Sajili ya michezo. 1 x 2 = 2
    2.      
      1. Hutumia takriri.
      2. Ni lugha ya utohozi.
      3. Ni lugha ya kuchanganya ndimi/msimbo. 8 x 1 = 8
      4. Inavuruga sarufi.
      5. Ina msamiati tele.
      6. Ni lugha ya chuku.
      7. Ni lugha ya misimi.
      8. Hutumia sentensi fupi.
      9. Ni lugha ya lakabu.
      10. Ni lugha ya ishara
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Kangundo Subcounty Pre Mock Exams 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest