Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Joint Pre-Mock Exams 2021/2022

Share via Whatsapp

Instructions to candidates

 • Jibu maswali yote.
 • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili
 1. UFAHAMU
  Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali

  Ikolojia ni elimu ya kisayansi inayohusu uhusiano wa kimazingira kati ya vitu vyenye uhai (mimea na wanyama) na visivyokuwa na uhai (hali ya hewa na udongo.)Sayansi ya ikolojia ipo katika mfumo wa elimu ya mazingira. Mfumo huu umegawanyika katika sehemu mbili: mfumo wa mazingira ya nchi na mfumo wa mazingira ya majini (bahari, maziwa, mito na madimbwi)

  Viumbe wamejirekebisha kulingana na mazingira yao. Kwa mfano, samaki wana matamvua yenye uwezo na kusharabu hewa ndani ya maji. Ng’ombe wana mapafu ya kuvuta hewa katika nchi kavu. Sehemu za mvua ya kawaida zina mimea yenye majani makubwa ili iweze kuhifadhi maji nyakati za shida. Mimea ,wanyama,udongo na viathiri vingine vya hali ya hewa vinahusiana sana kimazingira. Mimea huota kutegemea hali ya nchi, umbo au sura ya ardhi na aina ya udongo.

  Hali ya nchi ni wastani wa hali ya jotoridi, wastani wa mvua, unyevunyevu hewani, upepo, msukumo na mwanga kwa muda wa miaka thelathini. Dunia imegawanyika katika kanda mbalimbali. Kila kanda ina mimea na wanyama wa aina yake kutegemea hali ya nchi. Ukanda wa istiwai una joto, mvua na unyevunyevu mwingi. Miti ya ukanda huu hufanya misitu minene, yenye miti mirefu. Miti hii ni mirefu kwa sababu ya msongamano unaofanya miti igombanie mwanga wa jua kwa kurefuka. Katika misitu hii, ipo mimea ya kangaga inayotambaa na kukwea miti mingine. Katika ukanda wa Savanna hali ya joto na mvua si kubwa kama katika ukanda wa istiwai. Kwa sababu hii, sehemu nyingi ni vichaka na nyika zenye uwezo wa kuota nyasi zisizohitaji mvua.

  Upepo una faida na hasara katika mazingira. Upepo husaidia kusukuma mawingu yaletayo mvua. Upepo unapozidi hudhuru mimea na wanyama kwa sababu hukausha maji ardhini, huvunja na kuharibu mimea, huleta vifo kwa wanyama na pengine kuharibu mazingira ya watu. Mimea katika mazingira hutegemea sana nuru ya jua ili kutengeneza chakula chake. Kiasi cha mwanga upatikanao mahali fulani huathiri mimea na wanyama wapatikanao katika mazingira yale.
  MASWALI
  1. Eleza dhamira ya mwandishi katika taarifa uliyoisoma (alama 2)
  2. Eleza maana ya Ikolojia (alama 2)
  3. Kwa nini wanyama huwa na sifa mbalimbali za kimaumbile? (alama 2)
  4. Ni kawa vipi Ukanda wa istiwai unatofautiana na ukanda wa Savanna? (alama 2)
  5. Ni kwa namna gani upepo unaweza kuwa na athari mbaya kwa mazingira? (alama 4)
  6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumika katika kifungu. (alama 3)
   1. Matamvua____________________________________________________________
   2. Kusharabu hewa________________________________________________________
   3. Istiwai________________________________________________________________
 2. UFUPISHO
  Dhuluma kwa wanawake sio matokeo ya siasa baada ya uhuru, bali ni matokeo ya hali iliyokuwepo tangu enzi za mababu zetu; kabla ya ukoloni. Kubaguliwa na kudhulumiwa kwa wanawake kisiasa kunaoana na kunyonywa kwake kijamii kunakoshuhudiwa siku nenda miaka rudi.

  Elimu ya jadi ilimwandaa mwanamke kuwa chombo kitiifu cha mwanamume. Mwanamke aliandaliwa katika unyago na katika mfumo mzima wa malezi kuwa chombo cha kutumikia mwanamume-kumstarehesha, kumfariji, kumlisha na kumzalia watoto. Mwanamke tangu jadi hakuruhusiwa kushiriki katika shughuli za kisiasa na utawala wala hakuna mtu aliyeamini kwamba mwanamke angeweza kushikilia wadhifa wowote wa uongozi.

  Demokrasia ya jadi naihusudu sana; ambapo wazee walikaa chini ya mbuyu na kuamua mambo ya jumuiya. Mahakama ya kijiji ilikuwa aghalabu ni ya wazee na ya wanaume pekee yao. Hakukuwa na mwanamke aliyeshirikishwa, hata kama alikuwa ajuza. Sifa waliyokuwa nayo wanawake ni ile ya usihiri na uganga. Mwanamke yeyote aliyezeeka alidhaniwa kuwa bingwa wa uchawi, ulozi na ushirikina. Kwa hivyo, wanawake ndio waliokuwa washirikina wakubwa, maana fursa ya kupata elimu pana zaidi hawakuwa nayo. Si ajabu kuwa mwanamke alipojitokeza na kusema jambo la busara, alipuuzwa na pengine kutukanwa hadharani.

  Kwa bahati nzuri, kumezuka mwamko uliotuingiza katika enzi mpya. Vita vya wanawake vya kujihami na kujiendeleza katika ulimwengu unaotawaliwa na wanaume vimetapakaa kote katika kila sehemu ya dunia. Wanawake wengi wamekiuka misingi na mizizi ya utamanduni na kung’oa asasi za kijamii na itikadi ambazo daima zimeendelea kumyanyasa na kumuumbua utu mwanamke tangu jadi. Watetezi wa haki za wanawake zamani walilaumu suala la serikali za mataifa mwaka hadi mwaka. Huku masuala ya wanawake ya kijamii, utu na utamaduni yakishangiliwa kupitishwa, watetezi wameeleza wasiwasi wao ikiwa kupitishwa kwa maazimio kutasaidia kuleta maendeleo ya haraka kwa wanawake kimataifa au katika nchi moja. Fauka ya hayo, baadhi ya wachunguzi wanaonelea kuwa maazimio mengi hayadokezi hatua za kufikiwa haki za wanawake.

  Maazimio mengine yanazungumzia juu ya kuondolewa kwa ubaguzi dhidi ya wanawake, kushiriki kwao katika uendelezaji wa amani ya kimataifa na ushirikiano wa kimataifa, majukumu yao katika jamii, mfumo wa Umoja wa Mataifa wa wanawake na kuimarisha hadhi ya wanawake katika sekretariati ya Umoja wa Mataifa miongoni mwa shughuli nyingine katika mkabala huu.

  Wanawake wameonyesha vipaji vyao katika nyanja mbalimbali za maisha; siasa, uchumi, utawala na kadhalika. Wanawake wamejikakamua na kudhihirisha kuwa wao pia wana jukumu muhimu la kutekeleza ili kuyaongoza maisha yao na ya watu wengi. Wadumishaji wa dhuluma za kijinsia hawana budi kusalimu amri na kuukubali ukweli huu, wapende wasipende. Mtazamo juu ya haki sawa unatokana na kukubaliwa na kuondolewa kwa aina zote za ubaya dhidi ya wanawake wanaojitolea mhanga kutetea hadhi yao pamoja na ya wanyonge wengine. Wao huonekana kama waasi, wapinga mila na watovu wa utii.
  MASWALI
  1. Bila kubadilisha maana asilia, fupisha aya tatu za kwanza. (Maneno 45-55) (Alama 6)
   Matayarisho ____________________________________________________________________________________________Jibu.
   ____________________________________________________________________________________________
  2. Kwa kurejelea aya tatu za mwisho, pambanua hoja muhimu zinazoguziwa na mwandishi. (Maneno 60-65) (Alama 9)
   Matayarisho
   ____________________________________________________________________________________________Jibu
   ____________________________________________________________________________________________
 3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
  1. Andika neno lenye sauti zifuatazo: (alama 1)
   Kipasuo hafifu cha midomo, irabu ya mbele wastani, kikwamizo sighuna cha ufizi, irabu ya kati chini. 
  2. Tunga sentensi moja moja yenye aina zifuatazo za vishazi: (alama 2)
   1. Cha nia
   2. Kitegemezi cha wakati
  3. Andika maana ya maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 2)
   Walisita kufanya kazi hiyo baada ya saa sita usiku.
  4. Tia shadda: (alama 2)
   1. pekee
   2. alinyongwa
  5. Huku ukitoa mfano, onyesha miundo mitatu ya maneno katika ngeli ya U-I (alama 3)
  6. Tunga sentensi yenye vijisehemu vifuatavyo vya sarufi: (alama 2)
   Kiambishi kiwakilishi cha kiima
   Kiambishi kiwakilishi cha wakati
   Yambwa
   Mzizi - dhiki
   Kauli ya kutendesha
   Kiishio
  7. Tumia neno dhahiri kama: (alama 3)
   1. Kitenzi____________________________________________________________
   2. Kivumishi_________________________________________________________
   3. Kielezi___________________________________________________________
  8. Huku ukitoa mifano, eleza miundo mitatu ya silabi za Kiswahili. (alama 3)
  9. Tofautisha mzizi na shina kwa mifano. (alama 2)
  10. Nyambua ziba katika kauli ya kutenduka kisha utungie sentensi. (alama 2)
  11. Bainisha hali zinazorejelewa katika sentensi hizi. (alama 3)
   1. Mwangeka hufika kituoni mapema._________________________________________
   2. Mgonjwa angetibiwa angepona.___________________________________________
   3. Umekuwa nanasi, kutagia mibani?__________________________________________
  12. Andika katika udogo wingi. (alama 2)
   Ugwe ulipitishwa juu ya ukuta uliomea uyoga na kufungiwa kwenye makuti.
  13. Onyesha kiarifu katika sentensi hii. (alama 1)
   Kilimia kimechomoka angani.
  14. Changanua kwa kielelezo cha mstari. (alama 3)
   Ndege aliruka angani ghafla.
  15. Ainisha Virai vinne katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
   Kicha cha funguo kilikuwa kimepotea jana nikicheza kandanda.
  16. Tunga sentensi kuonyesha matumizi mawili ya nukta mkato. (alama 2)
  17. Andika methali yenye maana sawa na jivu usilolilala usilipigie Jibwa. (alama 1)
  18. Andika upya sentensi ifuatayo ukianza kwa shamirisho kitondo. (alama 2)
   Kaizari amewakatia ng’ombe majani kwa muundu.
  19. Damka ni kwa rauka, wakati ni kwa_______________oa ni kwa taliki uza ni kwa_______ (alama 2)
 4. ISIMUJAMII (ALAMA 10)
  Tamu sana! Very sweet! Very nutritious! Onja ujionee! Nunua. Nunua leo. Usikose mummy. Mchukulie mtoto. Fifty na Fifty! Hamsa. Fifty. Bure kwa bure! Bei ya starehe! Burudika.
  1. Tambua sajili hii. _____________________________________________(alama 1)
  2. Eleza sifa tisa za sajili hii kwa kurejelea kifungu. (alama 9)


MARKING SCHEME

 1. UFAHAMU
  1. Eleza dhamira ya mwandishi katika taarifa uliyoisoma. (alama 2)
   • Kuelezea mfumo wa ikolojia na maisha yanayomzunguka binadamu.
  2. Eleza maana ya Ikolojia (alama 2)
   • Elimu ya sayansi inayohusu uhusiano wa kimazingira kati ya vitu vyenye uhai na visivyo na uhai.
  3. Kwa nini wanyama huwa na sifa mbalimbali za kimaumbile? (alama 2)
   • Ni kwa sababu wanaishi katika mazingira tofauti.
  4. Ni kawa vipi Ukanda wa istiwai unatofautiana na ukanda wa Savanna? (alama 2)
   • Ukanda wa Istiwai una joto,mvua,unyevu, miti yake ni minene ,ni mrefu, yenye msongamano na ipo miti aina ya kangaga.(alama1)
   • Ukanda wa savanna hali ya joto na mvua si kubwa kuna vichaka na nyika.(alama 1)
  5. Ni kwa namna gani upepo unaweza kuwa na athari Mbaya kwa mazingira? (alama 4)
   • Huharibu mazingira ya watu
   • Huweza kusababisha vifo kwa watu.
   • Hukausha maji ardhini.
   • Huvunja na kuharibu mimea. (Hoja 4=alama 4)
  6. Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumika katika kifungu. (alama 3)
   1. Matamvua;Viungo vya samaki vya kupumulia
   2. Kusharabu hewa;Kupata hewa
   3. Istiwai:Ikweta/duara ya kuizunguka dunia
 2. UFUPISHO
  MASWALI
  1. Bila kubadilisha maana asilia, fupisha aya tatu za kwanza. (Maneno 45-55) (Alama 6)
   • Dhuluma kwa kwa mwanamke ni hali ya tangu jadi.
   • Elimu ya jadi ilimwandaa kama chombo cha mume.
   • Taasubi ya kiume.
   • Mwanamke Kama msihiri na mgaga.
   • Kupuuzwa na kutukanwa hadharani.
   • Demokrasia ilimfungia nje. Alama 6
  2. Kwa kurejelea aya tatu za mwisho, pambanua hoja muhimu zinazoguziwa na mwandishi. (Maneno 60-65) alama 9
   Matokeo ya elimu ya kisasa .
   • Mwanamke wa enzi mpya.
   • Mwanamke kujiamini na kujiendeleza.
   • Vipaji katika nyanja mbalimbali.
   • Kikwazo cha itikadi na mila za kiasili.
   • Wadumishaji wa dhuluma wasalimu amri
   • Mwanamke anayeongoza maisha yake.
   • Hadhi ya mwanamke kukua. zozote 8
    MTIRIRIKO 1
    JUMLA –SARUFI- HIJAI- ZIADA
 3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
  1. Andika neno lenye sauti zifuatazo: (alama 1)
   • Kipasuo hafifu cha midomo, irabu ya mbele wastani, kikwamizo sighuna cha ufizi, irabu ya kati chini. Pesa
  2. Tunga sentensi moja moja yenye aina zifuatazo za vishazi: (alama 2)
   1. Cha nia
    • Ili kufaulu katika mradi huo, itakubidi ufanye bidii. (nia)
   2. Kitegemezi cha wakati
    • Tangu Mosi aondoke, hajarudi mpaka leo.
  3. Andika maana ya maneno yaliyopigiwa mstari. (alama 2)
   Walisita kufanya kazi hiyo baada ya saa sita usiku.
   • Sita-simama kutenda jambo baada ya kuonesha nia ya kutenda au baada ya kuanza.(al 1)
   • Sita-muda/tarakimu kati ya tano na saba.(al 1)
  4. Tia shadda: (alama 2)
   1. pe’kee
   2. ali’nyongwa
  5. Huku ukitoa mfano, onyesha miundo mitatu ya maneno katika ngeli ya U-I (alama 3)
   • M-MI:Mti-miti
   • MW-MI:Mwavuli-Miavuli
   • MU-MI:Muwa-Miwa
  6. Tunga sentensi yenye vijisehemu vifuatavyo vya sarufi: (alama 2)
   Kiambishi kiwakilishi cha kiima
   Kiambishi kiwakilishi cha wakati
   Yambwa
   Mzizi- dhiki
   Kauli ya kutendesha
   Kiishio
   Kinanidhikisha.
  7. Tumia neno dhahiri kama: (alama 3)
   1. Kitenzi: Dhihirisha nia yako.
   2. Kivumishi: Habari dhahiri ndio hizo.
   3. Kielezi: Nieleze dhahiri kiini cha habari hizo.
    (Kadiria jibu)
  8. Huku ukitoa mifano,eleza miundo mitatu ya silabi za Kiswahili. (alama 3)
   • Konsonanti moja pekee (K)
    Mtu, mbu,
   • Konsonanti, Konsonanti, irabu (KKI)
    Mbuzi, ndizi, mbizi, nguo
   • Konosonanti na Irabu (KI)
    Meza, kula, kalamu
   • Irabu pekee (I )
    Ingia, omba, imba
   • Konsonanti, Konsonanti , Konsonanti, Irabu (KKKI)
    Ngwena, skrubu, ndwele,
  9. Tofautisha mzizi na shina kwa mifano. (alama 2)
   • Mzizi ni umbo la msingi la neno . Haligawiki zaidi
   • Shina-sehemu ya neno inayokaa kiambishi tamati.
  10. Nyambua ziba katika kauli ya kutenduka kisha utungie sentensi. (alama 2)
   • Zibuka
    Mfereji wa majitaka umezibuka na taka zinapita mtaroni.
  11. Bainisha dhana zinazorejelewa katika sentensi hizi. (alama 3)
   1. Mwangeka hufika kituoni mapema.Mazoea
   2. Mgonjwa angetibiwa angepona. Hali ya masharti
   3. Umekuwa nanasi, kutagia mibani? Hali timilifu
  12. Andika katika udogo wingi. (alama 2)
   Ugwe ulipitishwa juu ya ukuta uliomea uyoga na kufungiwa kwenye makuti.
   • Vijugwe vilipitishwa juu ya vikuta vilivyomea vijoga na kufungiwa kwenye vikuti.
  13. Onyesha kiarifu katika sentensi hii. (alama 1)
   Kilimia kimechomoka angani.
  14. Changanua kwa kielelezo cha mstari. (alama 3)
   Ndege aliruka angani ghafla.
   S-KN(N)+KT(T+E+E) (S al 1,KN(N) al 1 KT(T+E+E)
  15. Ainisha Virai vinne katika sentensi ifuatayo. (alama 2)
   Kicha cha funguo kilikuwa kimepotea jana nikicheza kandanda.
   Kicha cha funguo-Kirai Nomino(RN)
   Cha funguo-Kirai husishi (RH)
   Kilikuwa kimepotea-Kirai Kitenzi(RT)
   Jana nikicheza-(Kirai Elezi(RE)
   Kandanda-Kirai Nomino(RN)
   Funguo-Kirai Nomino(RN)
   Cha funguo-Kirai vumishi(RV)

   (Zozote 4 *1/2 =alama 2)
  16. Tunga sentensi kuonyesha matumizi mawili ya nukta mkato. (alama 2)
   1. kugawa sentensi mbili zinazoweza kujisimamia bila ya viunganishi
    mfano:Wasichana walifuata maagizo waliyopewa; wafulana waliyagomea.
   2. kama kipumziko katika sentensi ndefu
    mfano:Alipochunguza ile hati aliyokabidhiwa na wale wafanya biashara aliona kuwa si nzuri; akaamua kujitenga nayo.
  17. Andika methali yenye maana sawa na jivu usilolilala usilipigie Jibwa .(alama 1)
   • Usiyoyala usiwawingie kuku.
  18. Andika upya sentensi ifuatayo ukianza kwa shamirisho kitondo. (alama 2)
   Kaizari amewakatia ng’ombe majani kwa muundu.
   • Ng’ombe wamekatiwa majani na Kaizari kwa muundu.
   • Damka ni kwa rauka, wakati ni kwa njeo oa ni kwa taliki uza ni kwa nunua (alama 2)
 4. ISIMUJAMII
  Tamu sana! Very sweet! Very nutritious! Onja ujionee! Nunua. Nunua leo. Usikose mummy. Mchukulie mtoto. Fifty na Fifty! Hamsa. Fifty. Bure kwa bure! Bei ya starehe! Burudika.
  1. Sajili ya biashara/ sokoni:Anasema nunua leo.(alama 1)
  2. Eleza sifa tisa za sajili hii kwa kurejelea kifungu. (alama 9
   1. Lugha ya kuvutia hutumiwa, bure kwa bure ili kuvutia wateja.
   2. Lugha shawishi mno hutumiwa, mfano bei ya starehe sana/ usikose mummy ili kuwavutia wanunuzi.
   3. Kuna matumizi ya takiriri nunua, nunua leo
   4. Kuchanganya ndimi, very sweet ili kuvutia wateja wengi.
   5. Huwa na ucheshi na porojo ili kuwavutia wateja. Mfano, bure kwa bure
   6. Lugha nyepesi hutumika ili kuwasilisha. Bei ya starehe
   7. Ubora wa bidhaa husisitizwa, ili kuwavutia wateja. Tamu sana
   8. Kuna upigaji chuku mwingi ili kuwavutia wateja. Mfano bure kwa bure. 
   9. Sentensi fupi fupi hutumika kurahisisha mawasiliano. Mfano nunua, nunua leo.
   10. Lugha ya mafumbo-fifty na fifty (ni mia)

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Joint Pre-Mock Exams 2021/2022.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest