Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Maranda High Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

Maagizo

  • Jibu maswali manne pekee.
  • Sehemu zote ni lazima.
  • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
  • Maswali yote ni sharti yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.

SEHEMU A: USHAIRI

  1. Soma shairi hili kisha ujibu maswali.

    Mwanadamu mambo yake, kueleweka muhali
    Ubavuni umuweke, umtowe kule mbali
    Maskanini afike, umtindie fahali
    Utamu anufaike, sima, bada au wali
    Hatimaye ateuke, kwa viliwa vya samli
    Mwanadamu simuamini, afadhali nyama lumbwi.

    Mwanadamu umjenge, awe mwenye kutajika
    Mambo yake uyapange, ukawa wahangaika
    Uwashe wake muwenge, uhakikishe wawaka
    Nao mkono umuunge, vyake viwe vyaungika
    Dhorubani umkinge, asipate kudhurika
    Mara atakusahau, wema wako kafukia.

    Mwanadamu mpe cheo, kuwa akutumikie
    Amani yako umpeo, fanaka uirajue
    Kwake iwe kimbilio, wamini akukwamue
    Mwisho takuwa kilio, shika sikio ujue
    Ndio wake mwelekeo, yuauma avuvie
    Mwanadamu mgeuze, pande zote umtizame.

    Mwanadamu mfadhili, kwa kila lililo jema
    Pasiwe hata dalili, ya kwake kukosa wema
    Viteko siwe akali, kumbizo zikaterema
    Binadamu takudhili, dhili zako kuzitema
    Licha ya zote jamili, mwanadmu si muema
    Mwanadamu ni mtu, lakini nusu mnyama
    1. Onyesha kinaya cha mwanadamu anayezungumziwa. (alama 4)
    2. Fafanua toni ya shairi hili. (alama 2)
    3. Taja na ueleze bahari nne za shairi hili. (alama 4) 
    4. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2)
    5. Onyesha mbinu nne alizotumia malenga ili kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika shairi hili. (alama 4)
    6. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari. (alama 4)

SEHEMU B: FASIHI SIMULIZI

  1. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali

    Angole angole mwanangu
    Mwanangu nakuchombeza
    Nakuchombeza ulale
    Ulale ukiamka
    Nikupikie ubwabwa
    Na mchuzi wa papa
    Ukilia waniliza, wanikumbusha
    Ukiwa wa baba na mama

    Baba na mama watende
    Ilimu kunikatizia
    Ng’ombe, mbuzi kupokea
    Kunioza dumu kongwe
    Haliuki na halende
    Kazi kupiga matonge

    Likingia mvunguni
    Lavunjavunja vikombe
    Likilala kitandani
    Languruma kama gombe
    1. Bainisha kipera cha utungo huu. Thibitisha. (alama 2)
    2. Eleza ujumbe unaofumbwa katika wimbo huu. (alama 5)
    3. Tambua mbinu za kifani ambazo zimetumiwa kuwasilisha utungo huu. (alama 3)
    4. Bainisha shughuli mojamoja ya kijamii na ya kiuchumi ambazo huendelezwa katika jamii ya utungo huu. (alama 2)
    5. Unakusudia kukusanya data kuhusu kipera hiki. Eleza manufaa manne ya kutumia mahojiano. (alama 4)
    6. Kipera hiki kinazidi kufifia katika jamii yako. Fafanua njia nne ambazo jamii ya kisasa inaweza kutumia kukuza na kuendeleza kipera hiki. (alama 4)

SEHEMU C: RIWAYA
Assumpta K. Matei: Chozi la heri
Jibu swali la 3 au 4

  1. “Hili ni wingu la kupita na bila shaka wingu la kupita halipaswi kumtia mkulima matumaini. Tutapambana, sheria tunaijua.”
    1. Bainisha mitindo sita inayojitokeza katika dondoo hili. (alama 6)
    2. Bainisha mazaji inayojitokeza katika dondoo hili. (alama 2) 
    3. Kwa hoja kumi na mbili, onyesha namna jamii ya Chozi la Heri ni mfano wa jamii iliokosa ukomavu wa kisiasa. (alama 12)
  2. “Yote haya yamewezekana kutokana na mwongozo mlionipa nyinyi. Zaidi, utulivu nilioupata nilipoambulia familia hii ulinipa msukumo kila mara nilipokabiliwa na ndaro.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
    2. Eleza mchango wa mzungumzaji wa maneno haya katika kukuza ploti ya riwaya ya Chozi la Heri. (alama 5)
    3. “Familia ndicho kitovu cha ufanisi wa mtoto maishani.” Thibitisha kwa mujibu wa riwaya ya Chozi la Heri. (alama 11)

SEHEMU D: HADITHI FUPI
D. W. Lutomia na Phibiana Muthama: Mapambazuko ya Machweo na Hadithi Nyingine Jibu swali la 5 au 6


  1.        Nipe Nafasi – Mzamane Nhlapo
    1. Eleza tafsiri mbalimbali za kichwa cha hadithi hii, ‘Nipe Nafasi’ (alama 7)
      Pupa (F. M. Kagwa)
    2. Fafanua umuhimu wa mandhari ya Chenga-ways katika kujenga hadithi Pupa. (alama 5) Toba ya Kalia
      (Douglas Ogutu)
    3. “Ni kutokana na mchango wako kupitia twitter na facebook katika maswala mbalimbali ambapo iliamuliwa upewe fursa ya kuzungumza moja kwa moja na watazamaji wetu.”
      Eleza nafasi ya vijana kwa mujibu wa hadithi Toba ya Kalia. (alama 8)
  2.  
    1. “Wakati anaongea kwa simu, nikawa najifungua mkanda. Nikafaulu. Nikajaribu kufungua mlango. Duh! Ulikuwa ushatiwa loki. Sijui nilipata wapi nguvu za kupitia juu yake! Nikaponyoka pyu! Nikakimbia mguu niponye. Nilikimbia nisijue niendako. Nikakimbia. Sitaki kuangalia nyuma kwa kushtukia yaliyonikuta. Nilikata katikati ya misitu sijui nielekeako ila mbali na Romeo na pepo yake. Nimekaza mwendo huku nahema, pumzi si zangu! ”
      1. Fafanua aina za taswira zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 5)
      2. “Tamaa mbele mauti nyuma.” Jadili ukweli wa kauli hii kwa kurejelea hadithi: Nilitamani. (alama 7)
        Kifo cha Suluhu – Dominic Maina Oigo
    2. “Aliyaacha machozi yamtoke shibe yake kwani asingeweza kujizuia. Barua ile ilimfichulia siri si haba
      Thibitisha kauli iliyopigwa mstari ukirejelea hadithi Kifo cha Suluhu. (alama 8)

MARKING SCHEME

  1. USHAIRI
    1. Onyesha kinaya cha mwanadamu anayezungumziwa. (alama 4)
      • Mwanadamu analinganishwa na lumbwi kumaanisha kuwa anaweza kukugeuka baada ya kumsaidia.
      • Binadamu baada ya kuyapanga mambo yake umjenge hadi awe wa kutajika anakuja kukusahau na kufukia wema wako.
      • Mwanadamu hata ukampigania hadi akapata cheo kwa nia kuwa akusidie baadaye anakuja kukusababishia kilio.
      • Binadamu anakuja kusema dhili zako hata baada ya kumfadhili kwa kila jambo jema hadi akajaa vicheko.
    2. Fafanua toni ya shairi hili. (alama 2)
      • Toni ya huzuni - Mwisho takuwa kilio, shika sikio ujue.
      • Toni ya majuto – Mwanadamu simuamini, afadhali nyama lumbwi
      • Toni ya kukashifu - Mwanadamu ni mtu, lakini nusu mnyama
        (1 x 2= 2, kujata =1, maelezo/mfano = 1)
    3. Taja na ueleze bahari nne za shairi hili. (alama 4) 
      • Tasdisa/usita – kila ubeti una mishororo sita.
      • Kikwamba – neno mwanadamu lirudirudiwa mwanazoni mwa kila ubeti
      • Mathnawi – vipande viwili kila mshororo
      • Ukaraguni – vina vinabadilikabadilika.
      • Sabilia – shairi lina kiishio.
    4. Bainisha nafsineni katika shairi hili. (alama 2) 
      • Mshauri nasaha / kiathirika cha usaliti au kigeugeu – anashauri kuhusu tabia za binadamu. (1 x 2= 2) d
    5. Onyesha mbinu nne alizotumia malenga ili kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika shairi hili. (alama 4)
      • Inkisari - takuwa – utakuwa.
        Dhima - kupata urari wa mizani
      • Kuboronga sarufi
        • Mambo yake uyapange – uyapange mambo yake
        • Uwashe wake muwenge – uwashe mwenge wake
        • Nao mkono umuunge – nao umuunge mkono
        • wema wako kafukia – kafukia wema wako
        • Ndio wake mwelekeo – ndio mwelekeo wake
        • pande zote umtizame – umtizame pande zote.
          Dhima - kupata urari wa vina.
      • Tabdila - umtowe - umtoe
        • umtizame – umtazame.
          Dhima - kuleta mahadhi katika shairi / lugha ya kishairi.
      • Mazida
        • umuweke – umweke.
        • Muwenge – mwenge
        • Muema - mwema
          Dhima - kupata urari wa mizani
      • Lahaja
        • umtindie – umchinjie
        • viteko – vicheko.
          Dhima – kuleta upekee wa lugha ya kishairi.
      • Vikale
        • maskanini . makazi
        • akali – kidogo.
          Dhima – kuleta upekee wa lugha ya kishairi. 

          Kutaja na mfano- ½, dhima -½ (za kwanza 4 x 1 = al 4)
    6. Andika ubeti wa mwisho kwa lugha nathari. (alama 5)
      Mshairi anasema kuwa binadamu licha ya fadhili zote unazoweza kumpa hadi akawa anafurikwa na furaha bado atakusaliti na kusema mabaya kukuhusu. Anamlinganisha binadamu na mnyama.
  2. FASIHI SIMULIZI
    1. Bainisha kipera cha utungo huu. Thibitisha. (alama 2)
      • Bembelezi / bembea / pembejezi
      • Unawaliwaza na kuwabembeleza watoto walale auwanyamazewanapolia.
    2. Eleza ujumbe unaofumbwa katika wimbo huu. (alama 5)
      1. Kuhimiza uwajibikaji – nafsi neni kumpikia mwanawe ubwabwa
      2. Kueleza ugumu wa maisha / umaskini / ukilia wanikumbusha ukiwa wa baba na mama I
      3. Nafsi neni kukatiziwa elimu – ilimu kunikatizia
      4. Nafsineni kulazimishiwa ndoa – baba na mama kupokea ng’ombe na mbuzi 
      5. Kuwepo kwa vurugu – lavunjavunja vikombe
      6. Ukosefu wa usingizi – languruma kama gombe.
    3. Tambua mbinu za kifani ambazo zimetumiwa kuwasilisha utungo huu. (alama 3)
      1. Tashbihi–languruma kama gombe
      2. Takriri/uradidi–ulale,ukiwa,nakuchombeza,
      3. Taswira - Languruma kama gombe
      4. Kinaya – wazazi kumwachisha shule nasfuineni na kumwoza.
    4. Bainisha shughuli mojamoja ya kijamii na ya kiuchumi ambazo huendelezwa katika jamii ya utungo huu. (alama 2)
      • Kijamii – ndoa – kunioza dume kongwe
      • Kiuchumi–ufugaji ;languruma kama gombe
    5. Unakusudia kukusanya data kuhusu kipera hiki. Eleza manufaa manne ya kutumia mahojiano. (alama 4)
      • Kwa vile mtafiti anakabiliana namhojiwa ana kwa ana ni rahisi kupata habari za ana kwa ana na za kutegemeka.
      • Mbinu au sifa za uwasilishaji kama vile; Toni, utendaji, sauti, ishara za uso kubainika kwa mtafiti na hivyo kuimarisha kuelewa kwake.
      • Mtafiti anaweza kumfafanulia mhojiwa habari na kuweza kupata data inayoaminika
      • Mtafiti anaweza kubadilisha maswali au mtindo wa kuyauliza kulingana na kiwango cha elimu cha mhojiwa; lugha yake mhojiwa na mengine mengi
      • Mtafiti anaweza kutambua iwapo mhojiwa anatoa habari zisizo za kweli.
    6. Kipera hiki kinazidi kufifia katika jamii yako. Fafanua njia nne ambazo jamii ya kisasa inaweza kutumia kukuza na kuendeleza kipera hiki. (alama 4)
      1. Jamii inafundisha kipera katika taasisi mbalimbali za elimu kama vile shule ya msingi, vya upili na vyuo vikuu.
      2. Kuhimiza wataalamu kujihusisha na usomaji na utafiti wa kipera hiki.
      3. Kuhakikisha kuwa kipera hiki kimepewa nafasi inayostahili katika mfumo wa elimu. kwa mfano kinahusishwa katika tamasha za muziki na drama zinazohusisha taasisi mbalimbali za elimu
      4. Wanasarakasi wa kisasa wanaendeleza usanii wa kipera hiki.
      5. Jamii ya kisasa inatumia teknolojia ya habari na mawasiliano k.v Runinga, tarakilishi na redio kuendeleza utendaji wa kipera maathalan kuna vipindi mbalimbali vya watoto nidhazautangazaji
      6. Watafiti wa fasihi simulizi wanaendelea kukifanyia kipera utafiti, kuandika na kurekodi viperavya fasihisimulizi
      7. Kipera hiki kinaendelezwa katika jamii za kisasa.
  3. “Hili ni wingu la kupita na bila shaka wingu la kupita halipaswi kumtia mkulima matumaini. Tutapambana, sheria tunaijua.”
    1. Bainisha mitindo sita inayojitokeza katika dondoo hili. (alama 6)
      • Methali - wingu la kupita halipaswi kumtia mkulima matumaini.
      • Kinaya - kauli ya mpinzani wa Bi. Mwekevu kuwa “sheria tunaijua” ni kanaya kwani anasema anaijua sheria na wakati huohuo kushikilia msimamo kuwa mwanamke kuwa kiongozi wa nchi ni maonevu makubwa kwa mwanamume.
      • Jazanda- wingu la kupita – ni urahisi wa kumwondoa Bi. Mwekevu mamlakani
      • Sitiari - Hili ni wingu la kupita (Mwekevu kurejelewa kama wingu la kupita)
      • Taswira - Hili ni wingu la kupita
      • Litifati – ni unukuzi wa usemi wa mpinzani wa Mwekevu
      • Uhuishi – wingu la kupita
      • Kejeli / dhihaka – ni maneo ya kumdhihaki Mwekevu.
      • Takriri wingu la kupita llimerudiwarudiwa. Za kwanza 6 x 1 = 6
    2. Bainisha mazaji inayojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)
      • Mazaji ya dhihaka / hasira / chuki – maneno haya ni ya kuudhi watu.
    3. Kwa hoja kumi na mbili, onyesha namna jamii ya Chozi la Heri ni mfano wa jamii iliokosa ukomavu wa kisiasa. (alama 12)
      • Ubabedume katika siasa. Wafuasi wa mpinzani mwanamume wa Mwekevu wanashikilia msimamo kuwa mwanamke ni chombo duni na hawezi kushinda katika uchaguzi. Wanaandaa maandamano kupinga kuchaguliwa kwa Mwekevu.
      • Wananchi hawawateui viongozi kwa kuzingatia sera zao, bali wanachozingatia ni idadi ya misaada na riziki za bure. Kikongwe anataka kumteua Papa kwa kuwa aliwapa shilingi mia na unga.
      • Kutokubali matokeo ya kura. Mpinzani wa Mwekevu anakataa ushindi halali wa Mvekevu. Anawachochea wafuasi wake kwa nyimbo na kauli, wakaishia kuzua ghasia.
      • Wanasiasa wanatumia nafasi za kisiasa kama ngazi za kjitajirisha bali si kutoa huduma. Kiboko baada ya kuteuliwa amewasahau wapiga kura, si mwenzao tena.
      • Wanasiasa kutumia ghasia kusuluhisha tofauti za kisiasa badala ya kutumia njia za amani kama mahakama na mazungumzo. Mfano, Mwanzi.
      • Kuna siasa za kupakaziwa. Mrengo wa Mwanzi unamsingiziwa Mwekevu wizi wa kura anapomshida Mwanzi.
      • Kutoheshimu misimamo tofauti ya kisiasa. Selume wanatofautiana na mumewe kwa sababu ni mfuasi wa Mwekevu. Familia ya Kaizari inavamiwa kwa kuwa walimpigia Mwekevu kura.
      • Kueneza uhasama. Mpinzani wa Mwekevu anapokosa ukomavu wa kisiasa na kukubali kushindwa anapelekea kuzuka kwa vita vya baada ya uchaguzi.
      • Viongozi kulia machozi ya mamba kuonyesha jinsi wanavyowajali maskini. • Ufisadi katika upigaji kura. Vijana wanatumiwa kuwahadaa vikongwe ambao hawaelewi vizuri alama za wagombea wanaotaka kuwapigia kura.
      • Ukosefu wa elimu ya upigaji kura. Vikongwe hawaelewi vizuri alama za wagombea wanaotaka kuwapigia kura. Kikongwe mmoja anahadaawa na kuishia kumchagua Kiboko badala ya chaguo lake Papa.
      • Kutumia vijana vibaya. Vijana wanasukumizwa na wanasiasa katika vitendo vya ufisadi kama vile wizi wa kura katika vituo vya kupigia kura. Vijana hao huishia kuwahadaa vikongwe ambao hawaelewi vizuri alama za wagombea wanaotaka kuwapigia kura.
      • Vijana kupewa ahadi hewa na wanasiasa. Hizi zinakuwa kichocheo cha vijana kutafuta kila njia kuhakikisha viongozi wao wanaingia madarakani.
      • Vijana wanatumiwa na wanasiasa katika kushinikiza ushindi wao. Wanashawishiwa kushiriki katika maandamano ambapo wengi wao wanakufa kwa kupigwa risasi.
      • Viongozi kukaa tu majumbani baada ya kupiga kura badala ya kutoa mwito wa kudumisha amani wakati wa machafuko ya kisiasa.
      • Elimu ya kisiasa kutotathminiwa – Ridhaa anashangaa kwa nini mwalimu Meli anawafunza wanafunzi wake kina Tila kuhusu masuala ya siasa. Anaona ni kama anawachochea.
        Za kwanza 12x1 = 12
  4. “Yote haya yamewezekana kutokana na mwongozo mlionipa nyinyi. Zaidi, utulivu nilioupata nilipoambulia familia hii ulinipa msukumo kila mara nilipokabiliwa na ndaro.”
    1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
      • Msemaji ni Dick
      • Wasemewa ni walezi: Apondi, na Mwangeka.
      • Mahali ni hoteli ya Majaliwa
      • Anawashukuru kwa malezi mazuri.
    2. Eleza mchango wa mzungumzaji wa maneno haya katika kukuza ploti ya riwaya ya Chozi la Heri. (alama 5)
      • Kupitia Dick tunapata wahusika wengine kama Lemi na Tindi.
      • Kupitia Dick tunaonyeshwa mustakabali wa Wahafidhina. Anaachana na ulanguzi wa mihadarati na kuanzisha biashara.
      • Kupitia Dick tunaonyeshwa mgogoro kati ya mitandao ya uhalifu na uadilifu. Buda anamshinikiza kulangua mihadarati.
      • Anafanikisha maudhui kama vile ujasiriamali, mabadiliko, bidii na maadili.
      • Kupitia Dick tunaonyeshwa hatima ya mgogoro baina yao na mama yao. Wanafikiana kumsamehe na kuanza kumtafauta.
      • Kupitia Dick tunafichuliwa matukio fulani kama mitandao ya uhalifu inavyofanya kazi. Anauziwa Buda na Sauna.  5x1=5
    3. “Familia ndicho kitovu cha ufanisi wa mtoto maishani.” Thibitisha kwa mujibu wa riwaya ya Chozi la Heri. (alama 11)
      • Familia ya Ridhaa na Terry inayowalea watoto wao vizuri na kuwapa elimu.
      • Katika ndoa ya Mwangeka na Apondi wanawalea watoto wao vizuri kwa kuwapa elimu na mashauri. Dick na Umu wanashukuru kwa malezi yao.
      • Apondi anamshukuru Umu kwa malezi mazuri ya wadogo wake aghalabu anapokuwa mbali nao. Kutuliza hasira za Sophie.
      • Mwangemi na Neema walimpanga Mwaliko ambaye wamemlea vyema kwa kumpa elimu na kusoma hadi kitengo cha uzamili katika isimu na lugha.
      • Kangata alimuoa Ndarine na kubarikiwa na; Lunga Kiriri, Lucia Kiriri na Akelo Kiriri. Waliwalea vyema kwani waliweza kuwapa elimu iliyowasaidia.
      • Familia ya Mzee Mwimo Msubili inawadhibu Mwangemi na Mwangeka ili kuwarekebisha kitabia.
      • Mamake Kairu anamwendeleza kielimu.
      • Mamake Ridhaa anazungumza na mwalimu, Ridhaa anapobaguliwa shuleni hali iliyompelekea kupaa katika anga za elimu.
      • Maelekezo ya Ridhaa kwa Mwangeka kuhusu kuingia katika ndoa tena kunamfanya kuridhia ndoa tena na kumwoa Apondi.
      • Dick kupata wazazi Mwangeka ana Apondi waliweza kumpa ushauri uliomsaidia kibiashara.
      • Songoa anaelimishwa na Kiriri na hata kughuria Ngambo na kuwekeza huko. 
      • Mashirika ya kidini yanaungana pamoja kuwasaidia wakimbizi kwa kuwapa chakula katika kambi mbalimbali.
      • Mumewe Selume kushughulikia mahitaji ya mwanawe baada ya Selume kuondoka.
      • Lunga kuwalea wanawe baada ya Naomi kuondoka.
      • Neema kumtunza mpwake Cynthia baada ya wazazi wake kufariki kutokana na maradhi fulani.
      • Shule ya Tangamano iliwasaidia wanafunzi kama vile mwalimu Dhahabu anamwambia Umu arudi darasani anapoona amekumbwa na mawazo.
      • Mamake Kairu ni maskini kwamba kulipa karo ni jambo linalomtatiza ila anaongea na mwalimu mkuu wa Shule ya Tangamano kumruhusu mtoto wake asome akilipa kidogo kidogo.
      • Mwalimu Dhahabu anajishughulisha kuwatafutia mayatima na wanafunzi wake wasiokuwa na familia wazazi wa kuwapanga – Umu.
      • Nyanyake Chandachema
  5. SEHEMU D: HADITHI FUPI
    Nipe Nafasi – Mzamane Nhlapo
    1. Eleza tafsiri mbalimbali za kichwa cha hadithi hii, ‘Nipe Nafasi’ (alama 7)
      • Kuchukua nafasi ya kuboresha maisha yake. Kazili anapoona mumewe amemdhalilisha vya kutosha, anaamua kuondoka. Hajali kuomba ruhusa kama anavyotakiwa. 
      • Kuchukua hatua wanapoona waume zao hawawajibiki. Bi. Kazili anajisemea kuwa atarudi kufanya kazi kuwakimu, na siku hiyo lazima wale chajio.
      • Nafasi ya kuishi atakako. Kazili anawakumbusha wanaume kuwa yeye ni raia halali wa Lesotho kupitia kwa ndoa, na hakuna anayeweza kumlazimisha kurudi Swaziland, hata mumewe.
      • Kupinga maamuzi kuhusu maisha yake ambayo hajahusishwa kufanya. Mama Kazili anakana maamuzi ya wanaume kwenye kraal ambayo awali yanachukuliwa kuwa sheria isiyoweza kupingwa.
      • Wanawake kupewa nafasi na nyadhifa. Kazili anaeleza jinsi wanawake wanavyohiniwa nafasi na wadhifa katika jamii kwa kusingizia Biblia, kuwa mwanamke anafaa kuwa mnyenyekevu.
      • Nafasi ya kuheshimiwa. Kazili anapinga swala la mwanamke kuchukuliwa kama mtoto ambaye anafaa kuomba ruhusa kwa kila kitu kutoka kwa mumewe.
      • Nafasi ya ajira na kazi. Mwisho wa mwaka huo, Kaizili anafanya kazi ya ualimu bila ruhusa kutoka kwa yeyote, na wanawe wanapata chakula kila siku.
      • Kupatiwa nafasi ya usemi. Wanawake wa makamo wanakubaliana na rai ya Kazili, wanaona kuwa amaesema ukweli mchungu. Wako tayari kubadili mkondo huu wa dhuluma dhidi yao.
      • Kufanya maamuzi ya kibinafsi. Mama Kazili anawambia wanaume kwamba aliondoka bila kuomba ruhusa kwa mumewe kwa sababu alijua hangekubaliwa. Anawajuza kuwa hawezi kukaa tu kuwatazama wanawe wakihangaika kwa njaa.
      • Nafasi ya kusema ukweli. Wanaume wanahisi kwamba Kazili amewatusi, na kwamba lazima arudi kwao Swaziland kwa kuwakosea heshima. Hatarajiwi kusema ukweli.
        Pupa (F. M. Kagwa)
    2. Fafanua umuhimu wa mandhari ya Chenga-ways katika kujenga hadithi Pupa. (alama 5)
      • Kufichua mitandao ya uhalifu inavyofanya kazi / biashara haramu zinazoendeshwa katika jamii na madhara yake.. Ni danguro.
      • Kusawiri maudhui ya masaibu yanayoandama mtoto wa kike katika jamii.
      • Kuendeleza ploti. Baadhi ya matukio yanatokea katika mandhari haya. 
      • Kuwaibusha wahusika na sifa zao kama Mashaka.
      • Kuchimuza matabaka katika jamii. Kuna tabaka la wateja matajiri na wanyonge kina Mwakuona, Mashaka ambao ni bidhaa ya matajiri
        Toba ya Kalia (Douglas Ogutu)
    3. “Ni kutokana na mchango wako kupitia twitter na facebook katika maswala mbalimbali ambapo iliamuliwa upewe fursa ya kuzungumza moja kwa moja na watazamaji wetu.”
      Eleza nafasi ya vijana kwa mujibu wa hadithi Toba ya Kalia. (alama 8)
      • Kukuza vipaji. Jack na Siri wanashiriki katika shindano linaloandaliwa na wahandisi kutoka Uchina na kuibuka katika nafasi tatu za kwanza. Jack anaandaa kazi ya kupigiwa mfano na hata fomyula zake zinaingizwa kwenye vitabu, japo kwa jina la Siri
      • Kuendeleza lugha na utamaduni. Jack akiwa Uchina anaendeleza elimu ya lugha ya Kiswahili kwa wakazi wa huko, na anasema kwamba baadhi yao wanapata umilisi hata kuliko wazungumzaji wa nchi yake ya nyumbani.
      • Ujasiriamali. Jack anapokamilisha masomo yake ya shule ya upili kukosa karo anaanzisha biashara ya kuuza nguo.
      • Siri huwasiliana na wazazi wake kupitia skype, na Jack ndiye huwaunganishia mitambo kuhakikisha mawasiliano yanafaulu vizuri. Wanapatana naye vyema akiwa Uchina.
      • Urafiki wa dhati. Urafiki wake na Siri ni wa kipekee. Wanasaidiana sana, hata wanawafikiri kuwa ndugu. Hata kuhiniwa fursa yake na kupewa Siri hakuwatenganishi.
      • Usamehevu. Anawasamehe wote waliomkosea mwishoni.
      • Kukuza teknolojia kupitia kwake Jack , nafasi ya teknolojia na mawasiliano inabainika.
      • Kukuza uzalendo. Siri anakipigania Kiswahili na kukifunza Uchina.
      • Ushauri. Mwishoni mwa kipindi, Siri anawapa watazamaji wosia kuwa wasiwadhulumu mayatima na maskini
      • Siri na Jack wanawakilisha teknolojia ya mawasiliano na umuhimu wake katika kuunganisha jamii.
      • Watetezi imara wa haki na ukweli. Siri
      • Kukuza mahusiano ya kimataifa na umuhimu wake katika jamii unadhihirika. Siri
  6. Nilitamani (Phibiana Muthama)
    1. “Wakati anaongea kwa simu, nikawa najifungua mkanda. Nikafaulu. Nikajaribu kufungua mlango. Duh! Ulikuwa ushatiwa loki. Sijui nilipata wapi nguvu za kupitia juu yake! Nikaponyoka pyu! Nikakimbia mguu niponye. Nilikimbia nisijue niendako. Nikakimbia. Sitaki kuangalia nyuma kwa kushtukia yaliyonikuta. Nilikata katikati ya misitu sijui nielekeako ila mbali na Romeo na pepo yake. Nimekaza mwendo huku nahema, pumzi si zangu! ”
      1. Fafanua aina za taswira zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 5)
        • Taswira sikivu – Wakati anaongea kwa simu
        • Taswira mguso – nikawa najifungua mkanda / Nikajaribu kufungua mlango / Duh! Ulikuwa ushatiwa loki.
        • Tasira mwendo – Sijui nilipata wapi nguvu za kupitia juu yake! Nikaponyoka pyu! Nikakimbia mguu niponye. Nilikimbia nisijue niendako. Nikakimbia.
        • Taswira oni – Sitaki kuangalia nyuma kwa kushtukia yaliyonikuta. Nilikata katikati ya misitu sijui nielekeako ila mbali na Romeo na pepo yake.
        • Taswira hisi - Nimekaza mwendo huku nahema, pumzi si zangu!
      2. “Tamaa mbele mauti nyuma.” Jadili ukweli wa kauli hii kwa kurejelea hadithi: Nilitamani. (alama 7)
        • Tumaini, anaondoka kwao Kenya hadi nchi ya Wabongo kwa kutamani maisha mazuri.
        • Tumaini anatamani kuwa na milki na mali kama ya Nina. Anagundua kwamba alimwonea gere Nina.
        • Tumaini anapoishi na Nina anaanza kuwaonea wivu na kutamani kuwa na mume kama huwa Nina.
        • Tumaini anahama kwa Nina, kwa matumaini ya maisha mazuri bila mpangilio maalum: anaishia kuteseka zaidi.
        • Tumaini anapanda kutoka kiwango cha kutamani na kuanza kutaka. Anataka maisha mazuri, anataka mume wake waoane na kupata watoto wazuri.
        • Kwa tamaa yake, Tumaiini anamwona Romeo, kama mwanamume mtanashati aliyemwaza kwenye lile shairi lake. Nusra kumtoa kafara na analazimika kutoroka.
        • Matatizo ya kisaikolojia. Tumaiini anatamani kila kitu. Katika ushairi mawazoni, Tumaini anatamani kuwa na kasri afurahie, kazi ajikimu, na gari la kifahari. Anatamani maisha yawe mepesi na kumpa burudani.
        • Tuamini yuko katika ndoa ya kisaikolojia. Anatamani sana kupata mume mzuri amwoe, waishi maisha mazuri. Anajiona akiwa ameolewa, huku wamejaliwa watoto ambao wanawalea kwenye misingi ya kidini na kuwakuza vyema.
        • Unafiki wa kidini. Anapoona mambo yake yameenda kombo, anamgeukia Mungu na kumpa ahadi ya kumtumikia milele iwapo atamfungulia milango.
        • Ulaghai. Romeo anamhadaa Tumaini kwa kisingizio cha mahaba, lakini ukweli ni kwamba anataka kumtumia kwa matambiko yake.
        • Maamuzi mabaya. Tumaini anaamua kuondoka kwa Nina, japo hana pa kuishi. Ni ajabu kuwa anachoka kufadhiliwa hali hana hanani.
        • Maisha bandia. Tumaini anapopata hela kutoka kwa Nina, anaamua kwenda kudanganya moyo Coco Beach. Ananunua kaukau za mihogo na soda ya pepsi. Anavinjari kama mwenye vyake hali anateseka.
          Kifo cha Suluhu – Dominic Maina Oigo
    2. “Aliyaacha machozi yamtoke shibe yake kwani asingeweza kujizuia. Barua ile ilimfichulia siri si haba”
      Thibitisha kauli iliyopigwa mstari ukirejelea hadithi Kifo cha Suluhu. (alama 8)
      • Matatizo katika asasi ya ndoa. Suluhu anamsababishia mkewe uchungu kwa kutengana naye na hapati fursa ya kuzungumza naye.
      • Ukatili wa suluhu, ikiwemo kumwua mamake Abigael.
      • Usuli na Mabadiliko. Anamkumbusha kazi yake ya kuuza makaa ilivyofika hatima ya ghafla, kisha akatwaa ubunge kwa mbinu azijuazo.
      • Uumilivu wa Bi. Suluhu. Amevumilia kwa ajili ya watoto na kuwalea, na wa kwanza amekamilisha darasa la nane.
      • Uaminifu wa Bi. Suluhu. Anasisitiza jinsi anavyompenda mumewe, wala hajawahi kumwendea kinyume.
      • Bi. Suluhu anaonyesha thamani ya ndoa ya kuweka siri kwa kumhakikishia mumewe kuwa hajawahi wala hatatoa siri zake anazojua.
      • Ufisadi na kutowajibika. Suluhu haleti maendeleo kwa kuwa anawalipa wasichana wa vyuo vikuu na kula nao uroda. Pesa anamlipa Bwana Ngoma aliyefadhili siasa zake.
      • Ushauri. Anamuasa akome tabia zake kwa kuwa hali yake ni bayana.
      • Shukrani za Bi. Suluhu. Anamshukuru kwa mema aliyomtendea kabla ya kubadilika, na yale aliyotendea wazazi wake.
      • Athari za kutowajibika. Bi. Suluhu anamlaumu mumewe kwa kifo chake anachotarajia kutokana na kukosekana nyumbani na uzinzi, vinavyomletea msongo wa mawazo.
      • Utamaushi. Bi. Suluhu anakiona kifo kama suluhu.
      • Kufichua yaliyofichika. Barua hii inategua kitendawili cha kifo cha mamake Abigael aliyepatikana ameuawa.
      • Kuonyeha mustakabali wa jamii mpya. Abigael anajuta kuingilia ndoa ya Suluhu. Anaona kifo cha Suluhu hakitafaa lolote. Kifo kifaacho ni cha maovu na kupalilia utu. Anafanya uamuzi wa kutia bidii kujipa riziki na kumwachia Mungu wajibu wa hukumu.
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Maranda High Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?