Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Momaliche Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo
  • Jibu maswali yote.
  • Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
  1. UFAHAMU: ( Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
    Meli alipokivuka kizingiti cha lango la shule ya kitaifa ya Tungambele alikuwa na azma ya kusoma kwa bidii ili kuinukia kuwa kijana wa kutegemewa na jamii yake. Alikuwa kalelewa katika familia yenye pato wastani. Akasoma kwa juhudi za wazazi wake hadi darasa la nane alipokwangura alama za kumwezesha kujiunga na shule hii ya kifahari. Meli alijua kwamba alikuwa mwanagenzi, si katika masomo ya shule ya upili tu, bali pia katika maisha ya jijini ambamo shule hii ilipatikana. Kwa kweli hii ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kutia guu kwenye jiji hili ambalo habari zake akizisoma, ama katika magazeti machache yaliyowahi kufika kijijini, au kupitia somo la Elimujamii. Hata hivyo, Meli hakuwa mtu wa kuogopa au kunywea machoni mwa changamoto. Alijiambia kwamba kwa vyovyote vile atapambana na maisha haya mapya.

    Saa mbili kamili asubuhi ilimpata Meli kapiga foleni katika afisi ya kuwasajili wanafunzi wageni. Wasiwasi wa aina fulani ulianza kumnyemelea alipotazama hapa na pale bila kuona dalili ya mja yeyote aliyemfahamu. Alijihisi kama yule kuku mgeni ambaye mwalimu wake alishinda kuwaambia kuwa hakosi kamba mguuni. Hata hivyo aliupiga moyo wake konde na kujiambia kuwa kuja kwake hapa kulitokana na juhudi zake mwenyewe na katu hatauruhusu ugeni wa mazingira kuifisha ari yake ya masomo.

    Usajili ulikamilika, naye Meli na wenzake wakajitosa katika ushindani wa kimasomo jinsi waogeleaji wajitumbukizapo kidimbwini wakapiga mbizi, baadhi wakiambulia ushindi na wengine wakifedheheka kwa kushindwa. Meli na wenzake walibainikiwa kwamba wote walikuwa mabingwa kutoka majimbo na wilaya zao. Ilimbidi kila mmoja wao kujikakamua zaidi ili kuelea katika bahari hii ya ushindani. Muhula wa kwanza ulishuhudia kishindo cha Meli kubwagwa chini na majabali wenzake. Alijipata miongoni mwa wanafunzi kumi wa mwisho; au kama alivyozoea kuwatania wenzake katika shule ya msingi, “wanafunzi kumi bora kuanzia mwisho”! Hili lilimwatua moyo Meli na kumfanya kutahayari. Alifika kwao amejiinamia kama kondoo aliyeumia malishoni. Akawataka wazazi wake wambadilishie shule lakini wakakataa.

    Muhula wa pili na wa tatu mambo yalikuwa yaleyale. Meli akahisi kama askarijeshi aliyeshindwa kabisa kutambua mbinu za kuwavizia maadui. Akaona kwamba njia ya pekee ni kujiunga na wenzake kama yeye katika vitendo vya utundu kama vile kuvuruga masomo kwa kupiga kelele darasani, kupiga soga bwenini na hata kuvuta sigara. Mwanzoni alichukia vitendo hivi lakini alimeza mrututu akisema kwamba ndiyo njia ya pekee ya kujipurukusha na aibu. Wazazi wa Meli hawakusita kutambua mabadiliko katika hulka ya mwanao. Wakajaribu kumshika sikio nyumbani lakini akawa hasikii la mwadhini wala la  mteka maji msikitini. Wakawahusisha wataalamu wa ushauri nasaha ambao waliwaambia kuwa Meli hakuwa na tatizo lolote la kuyadumu masomo. Kile alichokosa ni kujiamini tu.

    Wazazi wa Meli waliona kuwa ni muhimu kuwahusisha walimu katika kutatua tatizo la mwanao. Mwanzo wa muhula wa pili uliwapata wazazi hawa afisini mwa naibu wa mwalimu mkuu. Mazungumzo kati ya wazazi, naibu wa mwalimu mkuu na mwalimu wa darasa la Meli yalidhihirisha kwamba walimu walikuwa wamemuasa Meli kuhusu kujiingiza katika makundi yasiyomfaidi lakini rai zao ziliingia katika masikio yaliyotiwa nta. Aliyopenda Zaidi Meli nishughuli zilizomtoa nje ya shule kama vile tamasha za mziki, ukariri wa mashairi na drama. Mazungumzo yalibainisha kwamba Meli alihitaji ushauri na uelekezaji Zaidi kutoka kwa mtaalamu wa nasaha pale shuleni.

    Meli alianza vikao na mtaalamu huyu ambaye pia alimpendekezea Meli ushauri zaidi kutoka kwa washauri marika. Hili lilimchangamsha zaidi Meli kwani aliwaona hawa kama wenzake waliojua changamoto zake. Juhudi za mtaalamu wa nasaha na washauri marika zilifua dafu. Mwisho wa kidato cha pili ulishuhudia mabadiliko makuu katika hulka na utendaji kimasomo wa Meli. Aliukata kabisa uhusiano wake na marafikiwaliompotosha na kuanza kuandamana na wanafunzi waliotia juhudi masomoni. Polepole alama zake ziliimarika. Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yalimweka kwenye safu ya wanafunzi bora zaidi nchini.           
    1. “Wanafunzi wawapo shuleni hukumbana na changamoto nyingi”. Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kurejelea hoja sita kutoka kwenye taarifa. .(alama 6)
    2. Eleza mchango wa washikadau mbalimbali katika kumsaidia Meli kupata ufanisi masomoni. (alama 4
    3. Bainisha mbinu tatu za lugha ambazo msimulizi anatumia katika kuwasilisha ujumbe wake katika kifungu. (alama 3)
    4.  
      1. Andika kisawe cha ‘kijipurukusha’ kwa mujibu wa taarifa (alama 1)                                                                                   
      2. Andika maana ya ‘kuwatania’ kulingana na taarifa. (alama 1)
  2. UFUPISHO  (Alama 15)
    Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali yafuatayo.


    Bei ghali ya  vyakula ni jambo linalowaathiri wakenya wengi kwa hivi sasa. Inasikitisha kupata kwamba bei ya unga wa ugali imepanda hadi sh. 200. Ni wazi kwamba familia nyingi nchini hukosa lishe lao kutokana na kufumka kwa bei ya bidhaa muhimu. Hata hivyo ibainike kwamba nchi isiyowakimu raia wake kwa chakula ni sawa ng”ombe aliyeshindwa kumnyonyesha ndama wake.

    Kwa muda mrefu, viongozi wamekuwa wakipambana na tatizo la ukosefu wa chakula. Msimu wa kiangazi unapobisha hodi, watu wengi hasa wale wahitaji hupukutika kutokana na mngato wa njaa. Japo serikali na wafadhili hutuma vyakula vya msaada kwa jamii zilizoathirika, chakula hiki huwa kama nguo ya kuazima, na bila shaka ya kuazima haikidhi haja.

    Mojawapo ya vyanzo vikuu vya uhaba wa chakula ni kiwango cha chini cha uzalishaji na uhifadhi wa chakula chenyewe. Zipo seheu nyingi ambazo ni kame nchini.sehemu hizi hukabiliwa na ukosefu wa maji kwani, ama mvua hainyeshi au inaponyesha haitoshelezi mahitaji ya mimea. Mimea mingi hujikaukia  ikiwa michanga na kudhihaki juhudi za wapanzi. Zipo sehemu katika nchi hii ambazo huenda kwa misimu hata mitano  bila kupata zao lolote kutoka mashambani. Hali ikiwa hivi makali ya uhitaji huzidi  na wakazi wa sehemu hizi hulazimika kuwa wategemezi kwa majirani na serikali. Wengine wanapokosa chakula kabisa huazimia kula visivyoliwa.Wanaamwa la mbwa baada ya kukosa la mama.

    Hali kadhalika japo zipo sehemu zingine ambazo hazina tatizo la ukame, mbinu hasi za kilimo husababisha utoaji wa mavuno haba, hivyo kutojitosheleza kwa chakula. Bilas haka wanapopanda ovyo wanavuna ovyo. Kuna wakulima ambao hupalilia mmomonyoka wa udongo kwa kulima kando kando ya  mito, kupanda zao lile lile katika sehemu ile ile ya ardhi miaka nenda miaka rudi, na kutopanda mimea ambayo hukinga tabaka la juu la udongo dhidi ya kumomonyolewa na maji au upepo. Matokeo ya haya yanaweza kutabiriwa; udongo wenye rutuba huoshwa  na mashamba kutwaa utasa ambao huzidisha kuzalisha kwa chakula haba. Wakulima wengine hukaidi wito wa kupanda mimea ambayo hustahimili ukame kama vile mbaazi mihogo, mtama  na wimbi. Baadhi ya wakulima hufuga mifugo wengi ambao hushindwa kustahimili kiangazi. Si ajabu kupata kwamba katika baadhi ya maeneo mizoga ya ngombe na hata ngamia imezagaa kote tanuri la kiangazi linapofanya kazi yake.

    Sehemu zingine zimebarikiwa na ukwasi wa chakula. Hata hivyo baadhi ya wakazi wa sehemu hizi hawana mwao kuhusu umuhimu wa lishe bora. Wapo wanaodhani kuwa chakula ni chakula bora tumbo lipate haki. Hawa hula vyakula kama vile viazi, mahindi, na wengine nyama bila kujua wanahiyaji vyakula vyenye virutubisho muhimu, yani wanga, protini , vitamini na madini. Wapo wanaodhani kuwa protini pekee ni nyama. Hawa hula nyama mawio  na machweo, matokeo yakiwa kuambulia magonjwa kama vile shinikizo la damu.

    Katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa chakula, serikali kupitia wizara husika imeanzisha miradi ya kuhakikisha kuwa kuna uzalishaji wa chakula kwa kiwango cha kuridhisha. Serikali ya Ruto sasa imepunguza bei ya mbolea hadi sh 3500 ili kuwawezesha wakulima kupanda chakula kwa wingi. Visima na mabwawa ya maji pia vitachimbwa katika maeneo kame ili kunyunyuzia mashamba maji. Baadhi ya wakulima wameanza kupanda mimea ambayo inapevuka na kutoa mazao kwa haraka ipo mimea ya kuatika ambayo hutoa matunda baada ya muda mfupi, hivyo kusaidia kupunguza makali ya njaa. Wafugaji wengine wameanzisha miradi ya kufuga kuku wa kututumuliwa. Hawa hukuwa na kukomaa kwa muda mfupi na huweza kutoa nyama na mayai. Wafugaji wa kuku hawa huweza kuwauza kununua  aina nyingine ya chakula.

    Wakulima pia wanahimizwa kutumia njia za kisasa za kuzalisha na kuhifadhi chakula.chakula kinapohifadhiwa vyema, hata mvua isiponyesha raia huweza kujitegemea. Ikiwa maghala ya halmashauri za kuhifadhi chakula nchini hayahifadhi chakula mara nyingi hulazimika kuagiza chakula kutoka nje kiangazi kinapojiri. Aidha chakula kisipohifadhiwa vyemahuishia kuharibika na kuhasiri wanaokila ikawa msiba juu ya mwingine.

    Ni muhimu kufahamu kuwajukumu la kupambana na ukosefu wa chakula ni la kila raia. Hali ya kungojea kila mara kulishwa na serikali inatufanya kuwa  wategemezi Zaidi. Wadogo wadogo ambao huuza vyakula kwa bei ya chini sana mara tu wanapovitoa mashambani wanapaswa kujiasa dhidi ya mazoea haya na kujua kuwa akiba haiozi. Wanaoishi katika sehemu za vinamasi wasaidiwe kuzitunza sehemu hizi na kuzitumia kwa njia endelevu. Vijana wahimizwe wawaunge wazee mkono kushughulikia kilimo katika sehemu za mashambani badala ya kuhamia mijini kutafuta kazi za ajira ambazo ni haba.
    1. Fupisha ujumbe wa aya tano za kwanza kwa maneno 100.            (alama 9, 1 ya mtiririko)
      Matayarisho
      Jibu
    2. Kwa kurejelea aya tatu za mwisho, eleza njia sita za kukabiliana na uhaba wa chakula.  (maneno 85)                                                            (alama 6, 1 ya mtiririko)
      Matayarisho
      Jibu
  3. MATUMIZI YA LUGHA                                                                                     (ALAMA 40)
    1. Eleza maana ya kipashio kidogo cha lugha.                                                                  (alama 1)
    2. Andika maneno yenye sifa zifuatazo:                                                                            (alama 2)
      1. kikwaruzo ghuna cha ufizi, vokali ya chini-wastani, kizuiwa ghuna cha midomo, kiyeyusho  cha midomo, irabu ya chini-kati
      2. Kipua ghuna cha ufizi, kipasuo cha ufizi, irabua ya mbele-juu, nazali ghuna ya midomo, irabu ya nyuma-juu.
    3. Ainisha uamilifu wa kisarufi wa mofimu kwenye neno hili.                                         (alama 3)
      Lilimjisha
    4. Tunga sentensi moja kuonyesha matumizi mawili ya  “tu”.                                        (alama 2)
    5. Unda kitenzi kutokana na nomino toba kisha ukitungie sentensi.                                 (alama 2)
    6. Yakinisha kwa kutumia kiambishi cha masharti ya uwezekano kwa wingi.                  (alama 2)
      Usiposoma kwa bidii hutofaidika.
    7. Tumia nomino ya ngeli ya mahali dhahiri pamoja na kivumishi kirejeshi cha kati kwa sentensi.                    (alama 2)
    8. Andika kinyume cha sentensi hii.                                                                                   (alama 2)
      Mjomba alimtwika mwanawe mzigo akabana mlango.
    9. Bainisha kijalizo katika sentensi ifuatayo.                                                                      (alama 1)
      Tajiri huyo shupavu ana magari makubwa mno.
    10. Tunga sentensi kwa kutumia chagizo cha ulinganisho.                                                  (alama 2)
    11. Andika upya sentensi kwa wakati uliopita hali endelevu, kauli ya tendesheka.         (alama 2)
      Wenyeji wamewapokea wageni kwa taadhima.
    12. Tunga sentensi moja kuonyesha maana mbili za neno tema.                                        (alama 2)
    13. Ainisha aina ifuatayo ya sentensi kiutendakazi.                                                            (alama 1)
      Safari imekuwa ikitusumbua sana.
    14. Onyesha kiima na utambue muundo wake katika utungo huu.                                     (alama 2)
      Pesa zote zilihifadhiwa na mwekahazina shujaa.
    15. Tumia kishazi tegemezi kwenye sentensi kuonyesha vigezo vifuatavyo.                     (alama 2)
      1. Wakati
      2. Jinsi
    16. Changanua kwa kielelezo cha mistari.                                                                          (alama 4)
      Aliponijia kwa mkopo, nilikuwa nasali sebuleni.
    17. Andika upya kwa kuanza na yambwa tendwa.                                                               (alama 2)
      Mvua iliwanyea wanunuzi sokoni hivi majuzi.
    18. Tunga sentensi katika udogo ukitumia kihusishi cha uhusiano.                      (alama 2)
    19. Eleza matumizi ya kiambishi po katika sentensi.                                                           (alama 2)
      Achezapo anapofika sisi hushangilia.
    20. Twasema oyee tunapofurahia jambo………………………………..tunapotahadharisha na ………………  Tunapotoa himizo (alama 2)
  4. ISIMU JAMII (alama 10)
    Soma makala haya kisha ujibu maswali;

    Rafiki yako amezongwa na mambo magumu na anafikiria suluhu ni kujiua umepewa jukumu la kumshauri.Fafanua sifa kumi za lugha utakayotumia ili kufanikisha ujumbe wako.

MARKING SCHEME

  1. UFAHAMU
    1.  
      1. Meli kushindwa mtihanini na wanafunzi wenzake ingawa alikuwa na alama nyingi katika mtihani wa darasa la nane.
      2. Kutaniana. Meli alizoea kutania wenzake katika shule ya msingi waliokuwa wa mwisho katika mtihani.
      3. Kuatuliwa moyo/ kuvunjika moyo kwa Meli baada ya kufeli katika mtihani.
      4. Kutahayari baada ya kushindwa na wenzake katika mtihani.
      5. Kupiga kelele darasani ili kuvuruga masomo ya wenzake darasani.
      6. Kupiga soga bwenini
      7. Kuvuta sigara kwa wanafunzi kama Meli shuleni.
      8. Meli kupuuza ushauri wa wazazi wake awapo nyumbani.
      9. Kutojiamini katika masomo.
      10. Meli kujiingiza katika makundi yasiyomfaidi.                               
      11. Meli kupenda shughuli zinazowatoa nje ya shule kama tamasha za muziki, ukariri mashairi na drama baada masomo.                   (zozote 6x1=6)
    2.  
      1. Wazazi wa Meli walijaribu kumshika sikio / kumshauri akiwa nyumbani kuhusu masomo. Walishirikisha mtaalamu wa ushauri nasaha.
      2. Wataalamu wa ushauri nasaha walisema Meli alikosa kujiamini masomoni.
      3. Walimu walimuasa Meli dhidi ya kujiunga na makundi yasiyomfaidi
        • naibu wa mwalimu mkuu.
        • Mwalimu wa darasa la Meli
      4. Mtaalamu wa nasaha aliyemshauri Meli na kumpendekezea Meli ushauri wa washauri marika.
      5. Washauri marika – bidii zao zilimsaidia Meli kujiimarisha kimasomo alipojiepusha na marafiki waliompotosha.    (Zozote 4x1)
    3.  
      1. Masimulizi kuhusu maisha ya Meli shuleni
      2. Misemo – kutia guu/ kupiga foleni/ piga moyo konde/ lilimwatua moyo n.k
      3. Methali – kuku mgeni hakosi kamba mguuni / hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini.
      4. Urudiaji / takriri Meli na wenzake….
      5. Kinaya / kejeli “ wanafunzi kumi bora kuanzia mwisho”
      6. Tashbihi / tashbiha “… amejiinamia kama kondoo aliyeumia malishoni..”
      7. Taswira “Meli kufika nyumbani amejiinamia….”
      8. Sitiari ‘Majabali wa Meli – wale waliomshinda Meli mtihanini       (Zozote 3x1)
    4.  
      1. kujiepusha/ kujisahaulisha/ kujilinda/ kujiokoa (alama 1)
      2. kuwadhihaki/ kuwafanyia mzaha/ kuwakejeli/ kuwafyosa/ kuwafyoa.(alama 1)
  2. UFUPISHO   (AlAMA 15)
    1.  
      • Bei ghali ya vyakula ni jambo linalowaathiri wakenya wengi.
      • Familia nyingi nchini hukosa lishe.
      • Kwa muda mrefu, viongozi wamekuwa wakipambana na tatizo la uhaba wa chakula
      • Chakula kinachotumwa na serikali hakitoshi.
      • Kiwango cha chini cha uzalishaji na uhifadhi ndicho chanzo cha uhaba wa chakula.
      • Zipo sehemu nyingi nchini ambazo ni kame.
      • Wengine wanapokosa chakula kabisa huazimia kula visivyoliwa.
      • Mbinu hasi za kilimo husababisha utoaji wa mavuno haba.
      • Wakulima wengine hukaidi wito wa kupanda mimea inayostahimili ukame.
      • Baadhi ya wakazi hawana mwao kuhusu umuhimu wa lishe bora
      • Kupunguza bei ya mbolea hadi sh. 3500.
    2.  
      • Uchimbaji wa visima na mabwawa ya maji
      • Kupanda mimea inayopevuka na kutoa mazao haraka.
      • Kuanzisha miradi ya ufugaji wa kuku wa kututumuliwa.
      • Kutumia njia za kisasa za kuzalisha na kuhifadhi chakula.
      • Wakulima wajiasi dhidi ya kuuza vyakula kwa bei ya chini.
      • Wanaoishi sehemu za vinamasi wasaidiwe kutunza sehemu hizi.
      • Vijana wahimizwe kuwaunga wazee mkono kushughulikia kilimo mashambani.
  3. MATUMIZI YA LUGHA                             (ALAMA 40)
    1. Eleza maana ya kipashio kidogo cha lugha.                                                                   (alama 1)
      • Sauti ni kipashio kidogo cha lugha kinachoweza kutamkika.                              (alama 1/0)
    2. Andika maneno yenye sifa zifuatazo:                                                                            (alama 2)
      1. kikwaruzo ghuna cha ufizi, vokali ya chini-wastani, kizuiwa ghuna cha midomo, kiyeyusho    cha midomo, irabu ya chini-kati
        • zabwa                                                                                                                    (alama 1/0)
      2. Kipua ghuna cha ufizi, kipasuo cha ufizi, irabu ya mbele-juu, nazali ghuna ya midomo, irabu ya nyuma-juu.
        • ndimu                                                                                                                    (alama 1/0)
    3. Ainisha uamilifu wa kisarufi wa mofimu kwenye neno hili.                                       (alama 3)
      Lilimjisha
      • li-mofimu ya ngeli
      • li-mofimu ya wakati
      • m-mofimu ya mtendwa
      • j-mzizi
      • ish-mofimu ya kauli ya kutendesha
      • a-mofimu ya tamati/kiishio                                                                           (alama 1/26=3)
    4. Tunga sentensi moja kuonyesha matumizi mawili ya kiambishi 'tu'.                             (alama 2)
      • Kuonyesha nafsi ya kwanza wingi k.m Tulisoma
      • Kuleta dhana ya kudhibitisha k.m Alinipa kalamu moja tu
      • Kama kitenzi kishirikishi kipungufu k.m Sisi tu wazima
      • Kama yambwa k.m Alitubariki
        Mfano: Tulikuwa tu wazima kabla ya ugonjwa wa Korona.
        nafsi          t
        Tanbihi: Mtahiniwa atunge sentensi moja     
                                                       (alama 21=2)
    5. Unda kitenzi kutokana na nomino toba kisha ukitungie sentensi.                           (alama 2)
      Toba-Tubu
      Waumini wote walitubu dhambi zao.
      (alama 21=2)
    6. Yakinisha kwa kutumia kiambishi cha masharti ya uwezekano kwa wingi.             (alama 2)
      Usiposoma kwa bidii hutofaidika.
      • Mngesoma kwa bidii mngefaidika.                                                                     (alama 2/0
    7. Tumia nomino ya ngeli ya mahali dhahiri pamoja na kivumishi kirejeshi cha kati kwa sentensi.                        (alama 2)
      • Pahali panapopendeza panatufaa
        Kirejeshi cha kati  kijitokeze kwa kitenzi
        Tathmini majibu ya watahiniwa                                                                           (alama 2/0)
    8. Andika kinyume cha sentensi hii.                                                                                (alama 2)
      Mjomba alimtwika mwanawe mzigo akabana mlango.
      • Mjomba alimtua mwanawe mzigo akabanua mlango.(alama 21=2)
    9. Bainisha kijalizo katika sentensi ifuatayo.                                                                  (alama 1)
      Tajiri huyo shupavu ana magari makubwa mno.
      • Tajiri huyo shupavu ana magari makubwa mno.
                                                      Kijalizo                                                              (alama 1/0)
      • Kijalizo husaidia kukamilisha maana ya sentensi na huja baada ya vitenzi vishirikishi
    10. Tunga sentensi kwa kutumia chagizo cha ulinganisho.                                            (alama 2)
      Msichana mrembo alitembea kitausi.
      Chagizo cha ulinganisho ni sawa na kielezi cha ki ya mfanano
      Tathmini majibu ya watahiniwa   
                                                                         (alama 2/0)
    11. Andika upya sentensi kwa wakati uliopita hali endelevu, kauli tendesheka.               (alama 2)
      Wenyeji wamewapokea wageni kwa taadhima.
      • Wageni walikuwa wakipokezeka kwa taadhima na wenyeji.
        au
        Wageni walikuwa wanapokezeka kwa taadhima na wenyeji.                             (alama 2/0)
    12. Tunga sentensi moja kuonyesha maana mbili ya neno tema.                                       (alama 2)
      • Tema ni kutoa kitu kinywani mfano chakula, mate
      • Tema ni hali ya kukata kitu kama vile mti, mkono  kwa  mfano;
        Alitema mate alipokuwa akitema mti kwa shoka.
        Maana iwe dhahiri na iwe kwa sentensi moja.         
                                         (alama 21=2)
    13. Ainisha aina ifuatayo ya sentensi kiutendakazi.                                                       (alama 1)
      Safari imekuwa ikitusumbua sana
      • Sentensi ya taarifa/kauli                                                                                     (alama 1/0)
    14. Onyesha kiima na utambue muundo wake katika utungo huu.                                  (alama 2)
      Pesa zote zilihifadhiwa na mwekahazina shujaa.
      Mwekahazina shujaa- N+V
      Kiima
      Kiima huonyesha mtendaji                                                                          (alama 21=2)
    15. Tumia kishazi tegemezi kwenye sentensi kuonyesha vigezo vifuatavyo.                   (alama 2)
      1. Wakati
        • Nyumba ilipojengwa, tuliishi ndani. (PO ya wakati itumike)                     (alama 1/0)
      2. Jinsi
        • Mwalimu alitutembelea tulivyotarajia jana.
        • Watoto wote walituzwa tulivyoona shereheni.                                              (alama 1/0)
          Tathmini majibu ya watahiniwa
    16. Changanua kwa kielelezo cha mistari.                                                                      (alama 4)
      Aliponijia kwa mkopo, nilikuwa nasali sebuleni
      S-KN+KT
      KN-N/W+SwaMomaF42023PrMP2AnsP
      N/W- Ø
      SwaMomaF42023PrMP2AnsP-aliponijia kwa mkopo
      KT-Ts+T+E
      Ts-nilikuwa
      T-nasali
      E-sebuleni                                                                                                        (alama ½8=4)
    17. Andika upya kwa kuanza na yambwa tendwa.                                                           (alama 2)
      Mvua iliwanyea wanunuzi sokoni hivi majuzi.
      • Wanunuzi walinyewa na mvua sokoni hivi majuzi.                                           (alama 2/0)
    18. Tunga sentensi kwa udogo ukitumia kihusishi cha uhusiano.                   (alama 2)
      • Kijikalamu cha kijitoto kimepotea.
      • Kijumba cha kijimama kitabomolewa.
                Kihusishi cha uhusiano ni sawa na kihusishi cha a-unganifu        (alama 2/0)     
                                               
    19. Eleza matumizi ya kiambishi po katika sentensi.                                                         (alama 2)
      Achezapo anapofika sisi hushangilia.
      • achezapo-hali ya mazoea
      • anapofika-wakati maalum                                                                              (alama 21=2)
    20. Twasema oyee tunapofurahia jambo simile/hario tunapotahadharisha na harambee tunapotoa himizo.                     (alama 21=2)
  4. ISIMU JAMII(alama 10)
    Fafanua sifa za lugha utakayotumia ili kufanikisha mazungumuzo yako (alama 10)
    • Matumizi ya maswali ya balagha-ukijitoa uhai utanufaikaje?
    • Lugha ya ushawishi-maisha ni matamu
    • Kuchanganya msimbo/ndimi-ucommit suicide kwa nini?
    • Matumizi ya tasfida-kujitia kitanzi
    • Matumizi ya chuku-utaenda kwa shetani straight
    • Matumizi ya viziada lugha ili kusisitiza hoja’
    • Lugha ya ucheshi kama vile-mtu akihang anajiendea haja kubwa
    • Matumizi ya lugha yenye mdokezo-watu wataachwa na…
    • Matumizi yenye toni kali ya kuonya kamavile -nitakushtaki kwa polisi
    • Matumizi ya lugha dadisi -mbaona unataka kujitoa uhai
    • Matumiziya nyimbo-kumrai asijiue
    • Matumizi ya maombi-kumshawishi abadili nia
    • Matumizi ya kauli fupi-chagua Maisha.
    • Matumizi ya lugha nyepesi-hamna haja ya kujiua
      hoja zozote 10 x 1                                                                       
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Momaliche Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?