Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Momaliche Pre Mock Exams 2023

Share via Whatsapp

SEHEMU YA  A

Swali la lazima

 1. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yafuatayo;

  Sinisumbue akili, nakusihie mwandani,
  Afiya yangu ni dhalili, muno nataka amani,
  Nawe umenikabili, nenende sipitalini,
  Sisi tokea azali, twenda zetu mizimuni,
  Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani!

  Mababu hawakujali, wajihisipo tabani,
  Tuna dawa za asili, hupati sipitalini,
  Kwa nguvu ya kirijali, mkuyati uamini,
  Kaafuri pia kali, na dawa ya ndwele fulani,
  Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani!

  Mtu akiwa halali, tumbo lina walakini,
  Dawa yake ni shubili, au zogo huauni,
  Zabadi pia zahali, kwa maradhi yako ndani,
  Au kwenda wasahili, wenyewe walo pangani,
  Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani!

  Mtu kwenda sipitali, ni kutojuwa yakini,
  Daktari kuona mwili, tanena kansa tumboni,
  Visu vitiwe makali, tayari kwa pirisheni,
  Ukatwe kama figili, tumbo nyangwe na maini,
  Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani!

  Japo maradhi dhalili, kuteguliwa tegoni,
  Yakifika sipitali, huwa hayana Kifani,
  Waambiwa damu kalili, ndugu msaidieni,
  Watu wakitamali, kumbe ndio buriani,
  Nifuateni sipitali, na dawa ziko nyumbani!

  Mizimu yakupa kweli, wakueleze undani,
  Maradhiyo ni ajali, yataka vitu dhamani,
  Ulete kuku wawili, wa manjano wa kijani,
  Matunda pia asali, vitu vya chanoni,
  Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani!

  Maswali
  1. Lipe shairi hili anwani mwafaka. (alama 2)
  2. Liweke shairi hili katika bahari mbili. (alama 2)
  3. Andika ubeti wa nne kwa lugha nathari. (alama 4)
  4. Kwa nini mshairi anakataa kwenda hospitali? (alama 2)
  5. Ni nani nafsi neni katika shairi hili? (alama 1)
  6. Tambua toni ya shairi hili. (alama 1)
  7. Eleza muundo wa ubeti wa pili. (alama 4)
  8. Eleza jinsi uhuru wa kishairi ulivyotumika katika shairi hili. (alama 2)
  9. Eleza maana ya msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika shairi. (alama 2)
   1. Pangani
   2. Nenende

SEHEMU YA B: HADITHI FUPI: MAPAMBAZUKO YA MACHWEO NA HADITHI NYINGINE.

 1. “Yu wapi kirukanjia wako? Wajua yuko wapi? Uliacha mbachao kwa msala upitao. Atakutunza nani, maana kwako fadhila za punda ni mashuzi!”
  1. Yaweke maneno haya katika muktadha wake. (alama 4)
  2. Taja mbinu mbili za lugha zilizotumika katika dondoo hili. (alama 2)
  3. Bainisha toni ya dondoo. (alama 1)
  4. Fafanua sifa zozote tatu za mzungumziwa. (alama 3)
  5. Kwa kurejelea hadithi “Fadhila za punda” onyesha ukweli wa kauli kuwa fadhila za punda ni mashuzi kwa mifano mwafaka. (alama 10)
   Au
 2. Huku ukirejelea hadithi zifuatazo tano jadili maudhui ya migogoro kwa kutoa mifano maridhawa. (alama 20)
  1. Fadhila za punda
  2. Msiba wa kujitakia
  3. Mapambazuko ya machweo
  4. Harubu ya maisha

SEHEMU YA C: RIWAYA YA CHOZI LA HERI

 1. “Kisa cha kaniki cha usiku wa manane kimetanda. Anayetazama anamwona mja aliyevaa koti kuukuu…..Anaimba huku ameshika chupa mkononi…..”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
  2. Tambua aina nne za taswira zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 4)
  3. Fafanua maudhui yanayochangiwa na mrejelewa huku ukirejelea riwaya.    (alama 2)
  4. Eleza sifa tatu za mrejelewa. (alama 3)
 2. Changanua kifungu kifuatacho.
  Mkuu wa shule, walimu na wanafunzi wenzangu, suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Tumeona jinsi misitu ilivyovamiwa na viongozi wenye mate ya fisi. Naskia baadhi ya vinara wa taasisi mbalimbali za umma wamewaacha wanyama kama mayatima kwa kupoka makazi yao. Maelfu ya maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda. Badala ya mibambakofi na miti mingine inayosafisha hewa, michai imetwaa nafasi yake. Wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui wa mazingira! Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii sharti ijitosheleze kwa chakula.
  1. Changanua mtindo katika kifungu kifuatacho. (alama 10)
  2. Mbali na maswala yanayojitokeza katika kifungu, eleza namna mwandishi alivyoshughulikia uharibifu wa mazingira katika riwaya ya chozi la heri.  (alama 6)
  3. Jadili mchango wa vijana katika kubomoa jamii katika riwaya ya chozi la heri.   (alama 4)

SEHEMU YA D: TAMTHILIA YA BEMBEA YA MAISHA

 1. “Mwanangu binadamu mchoyo kwa lake lakini mkarimu ajabu kwa la mwenziwe. Atakukarimu kwa la mwenziwe na atakupa nyongeza usiohitaji lakini lake atalizika katika giza la kina cha moyo wake. Ndiyo hulka yake mwana wa Adamu.”
  1. Eleza muktadha wa maneno haya. (alama 4)
  2. Jadili namna chanya msemaji na wenzake wa jinsia ya kike walivyosawiriwa katika tamthilia ya Bembea ya maisha. (alama 6)
  3. Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya msemaji na msemewa katika tamthilia ya Bembea ya Maisha (alama 10)
 2. Jadili maudhui yafuatayo kwa kutolea mifano maridhawa kama yanavyoshughulikiwa katika tamthilia ya Bembea ya maisha.
  1. Mabadiliko
  2. Migogoro
 3. SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI

  Dunia hii ina matatizo x2
  Watu wengi hawajajua
  Ni dunia yataabu
  Hata hivyo usijali.

  Karibu malaika karibu x2
  Mimi nikukaribishe
  Kwa mikono yote miwili
  Dunia mti mkavu.

  Usilie mtoto usilie x2
  Kwa kuiona dunia
  Iliyo na masumbuko
  Umebebwa miezi tisa.

  Maswali
  1. Huu ni wimbo wa aina gani? (alama 1)
  2. Eleza ujumbe wa wimbo huu. (alama 2)
  3. Eleza sifa za nyimbo za bembea . (alama 4)
  4. Taja tanzu kuu nne za fasihi simulizi. (alama 4)
  5. Unanuia kukusanya data za kipera kilicho hapo juu. Pendekeza njia tano utakazotumia. (alama 5)
  6. Eleza changamoto nne utakazokumbana nazo katika kukusanya data zako.    (alama 4)

MARKING SCHEME

 1. Maswali
  1. Lipe shairi hili anwani mwafaka.
   • Sipitali sendi, Nifwateni sipitali, Dawa ziko nyumbani . 1x2=2
  2. Liweke shairi hili katika bahari mbili.
   • Mtiririko – vina vya ukwapi na utao vinafanania.
   • Mathaawi – shairi lina vipande viwili. 1x2=2
  3. Andika ubeti wa nne kwa lugha nathari.
   • Mtu akienda hospitali ni kutojua vizuri. Kuwa daktari akiona mwili, atasema ni sratani ya tumbo. Atatia visu makali kujitayarisha kufanya upasuaji/paresheni, atakukata vyungo vya ndani. Kwa nini kwenda nyumbani na dawa ziko nyumbani. 4x1=4
  4. Kwa nini mshairi anakataa kwenda hospitali?
   • Tangu zamani wao huenda mizimuni.
   • Dawa za kiasili zipo.
   • Hapendi upasuaji.
   • Anafuata kielelezo cha mababu zetu. Zozote 3x1=3
  5. Ni nani nafsi neni katika shairi hili?
   • Mgonjwa/anayeugua 1x1=1
  6. Tambua toni ya shairi hili.
   • Huzuni/masikitiko/malalamiko 1x1=1
  7. Eleza muundo wa ubeti wa pili.
   • Mishororo minne.
   • Vipande viwili kila mshororo.
   • Mizani 16 kila mshororo.
   • Vina vya ndani ni –li na vya nje ni –ni. 4x1=4
  8. Eleza jinsi uhuru wa kishairi ulivyotumika katika shairi hili.
  9. Eleza maana ya msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika shairi. (alama 2)
   1. Pangani – palipona mizimu/mizimuni.
   2. Nenende – niende.

SEHEMU YA B: HADITHI FUPI: MAPAMBAZUKO YA MACHWEO NA HADITHI NYINGINE.

 1. “Yu wapi kirukanjia wako? Wajua yuko wapi? Uliacha mbachao kwa msala upitao. Atakutunza nani, maana kwako fadhila za punda ni mashuzi!”
  1. Yaweke maneno haya katika muktadha wake.
   • Ni maneno ya mamake Luka.
   • Anamwambia Luka.
   • Yumo katika hospitali (Luka).
   • Ni baada ya gavana Luka kuhusika kwa ajali na yule kirukanjia wake akakosa kuja kumwona baada ya kumsaliti Lilia alipokuwa gavana.   Zozote 4x1=4
  2. Taja mbinu mbili za lugha zilizotumika katika dondoo hili.
   • Methali – usiache mbachao kwa msala upitao.
   • Swali la balagha – yu wapi kirukanjia wako?
   • Takriri - …wapi…wapi
   • Nidaa - …mashuzi! 2x1=2
  3. Bainisha toni ya dondoo.
   • Huzuni, Majuto, uchungu.
   • Dhihaka,dharau 1x1=1
   • Umuhimu wa toni ni kuonyesha hisia za mzungumzaji.
  4. Fafanua sifa zozote tatu za mzungumziwa.
   • Mwenye bidii.
   • Ni laghai.
   •  Msaliti.
   •  Mzinzi.
   • Ni katili.
   •  Mnafiki.
   • Ni msomi.
   • Mwenye dharau. Zozote 3x1=3
  5. Kwa kurejelea hadithi “Fadhila za punda” onyesha ukweli wa kauli kuwa fadhila za punda ni mashuzi kwa mifano mwafaka.
   • Luka anaachiwa kanisa na pastor Lee Imani baadaye anauza kanisa ili awanie gavana.
   • Lilia anampenda Luka na anamshawishi babake akubali kuwabariki lakini Luka anamsaliti Lilia anapokuwa gavana kwa kumpiga makofi na teke la tumbo.
   • Luka anamsaliti pastor Lee baada ya kumkubali na kufadhili elimu, baadaye anakuwa na uhusiano na mtoto wake anayemtesa baadaye.
   • Luka anawasaliti waumini kwa kuuza kanisa na kuingia siasani.
   • Luka anamtendea uovu mkewe anapokosa kuandamana naye kwenye kampeni na kumtusi kuwa amenona kama nguruwe na kwamba wanawake ni wengi.
   • Luka anawasaliti wananchi waliomchagua kwa kutotimiza ahadi alizowatolea wakati wa kampeni.
   • Luka anamsaliti mkewe kwa kuwa na uhusiano ka kiruka njia.
   • Kirukanjia anamsaliti Luka kwa kukosa kumtembelea hospitalini baada ya kujulishwa na daktari huenda asiweze kutembea tena licha ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye.
   • Lilia anamsaliti babake kwa kuacha kazi ya meneja wa benki baada ya babake kumsomesha na kupata kazi ili awe akipokea wageni wa Luka.
   • Lilia anamsaliti babake kwa kushinikiza aolewe na Luka, ingawa babake hakutaka.
   • Lee anamsaliti Lilia kwa kumrithisha Luka Kanisa 10x1=10
    Au
 2. Huku ukirejelea hadithi zozote tano jadili maudhui ya migogoro kwa kutoa mifano maridhawa.
  1. Fadhila za punda
   • Lilia na Luka wana mgogoro unaosababisha vita k.m anapojitazama kwenye kioo anaona kovu shavuni na donda.
   • Mapenzi ya Lilia na Luka yanaleta mgogoro kati ya Lilia na babake-hapendi uhusiano ule.
   • Kuna mgogoro wa kinafsia kwa babake Lilia anayemshuku Luka kuwa na uhusiano na mwanawe Lilia.
   • Luka kumvamia mkewe na kumvuta nywele kumwelekeza kwenye chumba cha kulala, ambapo anampiga ngumi na mateke.
   • Luka anamtawisha Lilia na hata kumlazimisha kuandamana naye kwenye kampeni na hii inawafanya wakosane – Luka anamwambia wanawake ni wengi.
  2. Msiba wa kujitakia
   • Kati ya viongozi na raia ambao wako tayari kupigania haki zao-hawapewi huduma na viongozi.
   • Zuhura na Machoka-Zuhura angependa kumchagua kiongozi kwa misingi ya kikabila kinyume na Machoka.
   • Sugu Junior na Fumo Matata – Fumo anaona dai la serikali kwamba kuna maendeleo ni porojo tu.
   • Mgogoro kati ya tume ya uchaguzi na wananchi.
   • Mgogoro wa ushindi wa Sugu Junior dhidi ya Fumo matata.
   • Kati yam zee Sugu Senior na Zuzu Matata; ambapo mzee Sugu senior alitwaa uongozi baada ya kuondoka kwa wakoloni.
  3. Mapambazuko ya machweo
   • Mzee Makutwa kumtifulia mzee Makucha vumbi na kumdhihaki kuhusiana na kazi yake.
   • Bi Macheo anajikuta katika mgogoro na mumewe kwa vile hapendi jinsi mzee Makutwa anavyomfanyia stihizai mumewe.
   • Mzee Makucha anakuza mgogoro anapomwitia polisi mzee Makutwa kwa kuwahujumu vijana.
   • Mzee Makutwa ana mgogoro na sheria kwa vile anaendesha biashara haramu.
   • Migogoro kati ya vijana waliosoma na serikali kwa mfano Sai alidai kuwa vijana wanaachiwa kazi za hadhi ya chini.
   • Mzee Makutwa na polisi wakijaribu kumwingiza pangoni.
   • Mzee Makucha na shirika la reli-kukataa kumlipa pesa.
  4. Harubu ya maisha
   • Mama Mercy amtaka mumewe aeleze sababu ya kutofika ilhali motto anaelekea kulala. Mama Mercy analalamika kuwa mumewe hatimizi wajibu wake.
   • Familia ya Kikwai ina mgogoro na fundi wa nyumba hajalipwa kwa mwezi mzima.
   • Kikwai anagongana na Bosi kwa kuacha gari nyumbani kwa kukosa mafuta.
   • Nilakosi ana mgogoro wa mpangishaji wake kwa vile hajamlipa na mwezi unaenda kuisha.
   • Kikwai kutoleta chakula.
   • Kikwai kufika amechelewa.
   • Mercy kulalamikia njaa na upweke.

SEHEMU YA C: RIWAYA YA CHOZI LA HERI

 1. “Kiza cha kaniki cha usiku wa manane kimetanda. Anayetazama anamwona mja aliyevaa koti kuukuu…..Anaimba huku amewshika chupa mkononi…..”
  1. Eleza muktadha wa dondoo hili.
   • Maneno ya mwandishi/msimulizi.
   • Anamrejelea Bwana Shamsi.
   • Shamsi yu njiani akielekea kwake.(Kazikeni).
   • Ni usiku wa manane. Anapita akiimba kutokana na ulevi wake/machungu/jakamoyo yake. 4x1=4
  2. Tambua aina nne za taswira zinazojitokeza katika dondoo hili.
   • Taswira oni/mwono – anayetazama anamwona.
   • Taswira sikivu – anaimba.
   • Taswira mguso – ameshika chupa.
   • Taswira hisi – kiza kimetanda. 4x1=4
  3. Fafanua maudhui yanayochangiwa na mrejelewa huku ukurejelea riwaya.
   • Ulevi. Ameishi kusifu pombe yake.
   • Utabaka k.m anaishi kwenye mabanda kazikeni, majirani zake wanaishi mtaa wa Afueni.
   • Unyakuzi wa ardhi/dhuluma k.m shamba la babake lilitwaliwa na wenye nguvu.
   • Ufisadi/hila k.m mwenye nguvu aliyetwaa shamba la babake alikuja na hatimiliki bandia.
   • Elimu k.m babake alifanya kazi za sulubu ili kumlipia karo. Amefuzu chuo kikuu.
   • Ukosefu wa kazi k.m hata baada ya kufuzu hajapata kazi.
   • Mishahara duni k.m kibarua anachofanya kinamlipa mshahara wa kijungujiko.
   • Vifo/mauaji k.m babake Shamsi anakufa kwa njaa na ukosefu wa dawa hospitalini.
   • Umaskini k.m Shamsi anakula tu kibahati hana hakika kwamba mkewe amepata cha kupika.
   • Tanbihi: Mwanafunzi lazima apate mrejerelewa katika sehemu ya (a) ili apate sehemu ya (c). La sivyo apuuzwe katika sehemu ya (c).
  4. Eleza sifa tatu za mrejelewa
 2. Changanua kifungu kifuatacho.
  Mkuu wa shule, walimu na wanafunzi wenzangu, suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu. Tumeona jinsi misitu ilivyovamiwa na viongozi wenye mate ya fisi. Naskia baadhi ya vinara wa taasisi mbalimbali za umma wamewaacha wanyama kama mayatima kwa kupoka makazi yao. Maelfu ya maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda. Badala ya mibambakofi na miti mingine inayosafisha hewa, michai imetwaa nafasi yake. Wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui wa mazingira! Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii sharti ijitosheleze kwa chakula.
  1. Changanua mtindo katika kifungu kifuatacho.
   • Hotuba: ya Lunga
   • Jazanda: viongozi wenye mate ya fisi (viongozi walafi)
   • Tashhisisi: wamewaacha wanyama kama mayatima.
   • Kinaya: maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda.
   • Nidaa;siyahi: michai ni adui wa mazingira!
   • Tashbihi: wamewaacha wanyama kama mayatima.
   • Taswira: tumeona jinsi misitu lilivyovamiwa.
   • Nahau: mate ya fisi.
   • Kutumia usemi halisi.
   • Ukinzani: wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui wa mazingira! Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii sharti ijitosheleze kwa chakula.
   • Nidaa
   • Tashhisi-wanyama kubaki mayatima 10x1=10
  2. Mbali na maswala yanayojitokeza katika kifungu,eleza namna mwandishi alivyoshughulikia uharibifu wa mazingira katika riwaya ya chozi la heri. (alama 4)
   • Kuchomwa kwa magari-moshi.
   • Ukosefu wa vyoo.
   • Kujenga karibu na mito.
   • Kukata miti ili kujenga.
   • Mirundiko ya taka.
   • Lunga kukata miti.
   • Mzee Kedi kuteketeza shamba na nyumba ya Ridhaa
  3. Jadili mchango wa vijana katika kuharibu /kubomoa jamii katika riwaya ya chozi la heri.
   • Ulevi
   • Dawa za kulevya
   • Ubakaji
   • Mauaji
   • Uavyaji mimba
   • Kutumia mihadarati
 3. SEHEMU YA D: TAMTHILIA YA BEMBEA YA MAISHA
  “Mwanangu binadamu mchoyo kwa lake lakini mkarimu ajabu kwa la mwenziwe. Atakukarimu kwa la mwenziwe na atakupa nyongeza usiohitaji lakini lake atalizika katika giza la kina cha moyo wake. Ndiyo hulka yake mwana wa Adamu.”
  1. Eleza muktadha wa maneno haya.
   • Maneno ya Dina.
   • Anamwambia Kiwa.
   • Yuko nyumbani kwa Dina.
   • Dina alikuwa akimwambia Kiwa kuhusu yale magumu ambayo Sara ameyapitia katika maisha . 4x1=4
  2. Jadili namna chanya msemaji na wenzake wa jinsia ya kike walivyosawiriwa katika tamthilia ya Bembea ya Maisha.
   • Mwanamke ni karimu k.m Neema anatumia mshahara wake kulipia karo Asna na Salome.
   • Mwanamke ni mwenye bidii k.m Salome amesoma na kuhitimu first class.
   • Mwanamke ni mwajibikaji k.m Neema anamwendea mamake kijijini ili kumpeleka hospitali.
   • Ni mwenye utu k.m Dina anaenda kumsaidia Sara kwa upishi.
   • Mwanamke ni mtiifu k.m Bela anaitika anapoitwa na Sara na kuagizwa kuamka mapema.
   • Mwanamke ni mwenye busara k.m Sara anamshauri Neema kuwa maisha ya ndoa ni bembea. 6x1=6
  3. Fafanua umuhimu wa mazungumzo kati ya msemaji na msemewa katika tamthilia ya Bembea ya maisha
   • Yanachimuza maudhui ya uwajibikaji k.m Kiwa amekuja kumjulia hali mamake.
   • Yanadhihirisha sifa za Sara k.v uvumilivu k.m anapoitwa tasa anavumilia.
   • Yanaonyesha maudhui ya changamoto ya ndoa k.m Dina anasema Sara alikaa kwa muda kabla ya kujaliwa motto.
   • Yanaonyesha sifa za Neema wakati Kiwa anasema ana akili kama za simaku.
   • Yanachimuza maudhui ya umbea k.m wanajamii walimsema sana Sara.
   • Yanaendeleza ploti ya hadithi.
   • Yanaonyehsa Yona kama mwenye msimamo dhabiti.
   • Yanaonyehsa maudhui ya nafasi ya mwanamke. Ni mnyonge.
   • Yanaonyesha sifa za Dina kama mdadisi k.m anamuuliza mwanawe kwa nini amekonda.
   • Yanakuza maudhui ya mila na utamaduni k.m jamii inashinikiza Sara apate mtoto wa kiume wa kumrithi.
   • Yanachimuza falsafa ya mwandishi ya kupinga tamaduni zinazothamini mtoto wa kiume na kumdunisha wa kike.
   • Yanaonyesha mgogoro kati ya Yona na jamii huku ikimtaka azae mtoto wa kiume na kumrithi.
 4. Jadili maudhui yafuatayo kwa kutolea mifano maridhawa kama yanavyoshughulikiwa katika tamthilia ya Bembea ya maisha.
  1. Maudhui ya mabadiliko
   Ni hali ya kutoka katika hali moja hadi nyingine.
   • Yona alikuwa akiwanyoosha viboko wanafunzi lakini sheria ikabadilika kwamba siku huwezi kumnyoosha mtoto kwa kiboko.
   • Tofauti na hapo awali Yona ataka kuzitumia siku zake za uzee kumshughulikia mkewe.
   • Yona alikuwa mzuri lakini akageuka na kuwa mlevi.
   • Mtazamo kuhusu mtoto wa kike kutazamwa kama asiye na haki ya kurithi unabadilishwa na kizazi cha leo.
   • Zamani wasichana wakiozwa punde wanapobuleghe lakini ziku hizi wanaolewa wakitaka.
   • Zamani Yona hangepika lakini tunamwona akiandalia familia yake kiamsha kinywa – utamaduni kubadilika.
   • Uk. 72 Neema anabadilisha mtazamo wake kuhusu babake.
   • Bunju anabadilisha mtazamo wake wa kutomsaidia Neema katika matibabu ya Sara – sasa anasema atampiga Jeki.
   • Afya nzuri ya Sara kubadilika na kuwa duni.
   • Jamii inabadilika na kuiheshimu familia ya Yona – ambayo ilikuwa ikidharauliwa hapo mbeleni. Alama 10
  2. Maudhui ya migogoro
   • Kati ya kizazi cha jana na kizazi cha leo k.m katika ndoa.
   • Migogoro ya kitamaduni kati ya Asna na mamake – kuhusu babake kuchota maji kisimani.
   • Kitamaduni kati ya Asna na Sara. Sara anaamini kuwa msichana aolewe tu anapobaleghe.
   • Tamaduni- Bunju dhidi ya Neema, Asna na Bela. Bunju haamini wazazi kulala nyumbani kwa mkwe.
   • Migogoro kati ya Sara na Yona ambapo Yona anampiga Sara kwa kukosa mtoto wa kiume.
   • Kati ya Neema na Bunju kuhusu majukumu ya kifamilia-matibabu ya Sara.
   • Neema na Bunju wanavutana nani ampeleke Lemi Ziara.
   • Bunju anasema Neema anapenda kukana na kubishana, jambo ambalo litamfanya kuonekana mbwa kasoro.
   • Mgogoro kati ya jamii ya Yona na ile ya Sara baada ya Sara kutojaliwa na mtoto.
   • Mgogoro wa familia ya Yona na Sara unakuzwa na kuwa wa kijamii-inayomlaumu Yona kwa kukosa mtoto wa kiume.
 5. SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
  Dunia hii ina matatizo x2
  Watu wengi hawajajua
  Ni dunia yataabu
  Hata hivyo usijali.

  Karibu malaika karibu x2
  Mimi nikukaribishe
  Kwa mikono yote miwili
  Dunia mti mkavu.

  Usilie mtoto usilie x2
  Kwa kuiona dunia
  Iliyo na masumbuko
  Umebebwa miezi tisa.

  Maswali
  1. Huu ni wimbo wa aina gani?
   • Ni wimbo wa kuzaliwa kwa mtoto       alama 1
  2. Eleza ujumbe wa wimbo huu.
   • Msanii anamkaribisha vyema mtoto katika dunia yenye matatizo, taabu na masumbuko. Alama 2
  3. Eleza sifa za nyimbo za bembea.
   • Kumbembeleza watoto na kuwaonoga ili walale.
   • Kuwanyamazisha ili waache kulia.
   • Huakisi thamani za jamii.
   • Huakisi shughuli za kiuchumi za jamii.
   • Hutumiwa kama sifo kwa mtoto.
   • Hutakasa hisia za mwimbaji. Alama 4
  4. Taja tanzu kuu nne za fasihi simulizi.
   • Hadithi
   • Ushairi
   • Maigizo
   • Semi
   • Mazungumzo
  5. Njia za kukusanya data .
   • Kusikiliza
   • Kushiriki
   • Kurekodi
   • Kutumia hojaji
   • Mahojiano alama 5
  6. Changamoto
   • Ukosefu wa vifaa
   • Ukosefu wa fedha kv usafiri
   • Gharama ya utafiti
   • Mtazamo hasi wa jamii
   • Wahojiwa kudai walipwe alama 4
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Momaliche Pre Mock Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?